Tuesday, July 23, 2013
GUARDIOLA USO KWA USO NA BARCELONA.
MENEJA mpya wa klabu ya Bayerm Munich, Pep Guardiola anatarajiwa kukutana na timu yake ya zamani ya Barcelona katika mchezo wa kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi barani Ulaya. Barcelona walitua jijini Munich bila kuwa na kocha wao mkuu baada ya Tito Vilanova kujiuzulu wadhifa wake Ijumaa iliyopita kwa matatizo ya kiafya huku klabu hiyo ikiwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya. Msadizi wa Vilanova Jordi Roura ndiye atachukua mikoba yake kwa muda katika mchezo huo wa kirafiki utakaofanyika Allianz Arena. Guardiola alichukua mikoba rasmi ya kuinoa Bayern mapema mwezi uliopita baada ya kuchukua mapumziko ya mwaka mzima toka alipoondoka Barcelona katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana.
FIFA YAITOLEA KITANZI CAMEROON.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza kuondoa adhabu ya kuifungia Cameroon kushiriki mechi za kimataifa baada ya kuundwa kamati ya muda itakayoongozwa na Joseph Owona. Kwa maana hiyo klabu ya Coton Sport sasa inaweza kucheza na Sewe katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwishoni mwa wiki hii huku pia timu ya taifa ya Cameroon nayo ikichuana na Cameroon katika mechi za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN. FIFA ilifikia hatua ya kulifungia Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot baada ya kutokea mganganyiko katika uchaguzi wake ambao ulimrudisha madarakani Mohamed Iya ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi mahakamani ya matumizi mabaya ya fedha wakati akiwa kiongozi wa kampuni moja ya katani nchini humo. Katika barua iliyotumwa na FIFA katika mtandao wake imedai kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kuundwa kwa kamati hiyo itakayoliongoza shirikisho hilo kwa muda mpaka hapo utakapofanyika uchaguzi mwingine.
NFF YAWAFUNGIA MAISHA WACHEZAJI NA VIONGOZI.
SHIRIKISHO la Soka nchini Nigeria-NFF limewafungia maisha wachezaji na viongozi wote walioshiriki katika mechi mbili za mtoano kwa ajili ya kupanda daraja. Katika mechi hizo klabu ya Plateau United Feeders waliifunga Akurba FC kwa mabao 79-0 wakati timu ya Police Machine FC wenyewe waliigaragaza Bubayaro FC kwa mabao 67-0. Mbali na adhabu hizo kwa wachezaji na viongozi vilabu navyo vimefungiwa miaka 10 huku kamati ya NFF iliyokuwa ikichunguza tukio hilo imependekeza waamuzi nao wafungiwe maisha kujishughulisha na mambo ya michezo. Plateau United Feeders na Police Machine zilikwenda kwenye mechi zikiwa na alama sawa huku kila timu ikitaka kupanda daraja ambapo mabao 72 ya Feeders yalifungwa katika kipindi cha pili wakati Police Machine nao walifunga mabao 61 baada ya kipindi cha mapumziko. Matokeo hayo yalizua gumzo kubwa na kupelekea NFF kuanza uchunguzi haraka huku Shirikisho la Soka Duniani-FIFA nalo likifuatilia tukio hilo kujua hatma yake.
Monday, July 22, 2013
KUONDOKA KWA VILANOVA PIGO KWA BARCA - PUYOL.
NAHODHA wa klabu ya Barcelona, Carles Puyol ameeleza uamuzi wa Tito Vilanova kuachia ngazi kuinoa klabu hiyo kuwa ni pigo kubwa. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 alitangaza kuachia ngazi wiki iliyopita ili zweze kuendelea na matibabu yake ya saratani baada ya kuiongoza Barcelona kunyakuwa taji la La Liga katika msimu wa 2012-2013. Puyol amekiri kuwa habari ya kujizulu kwa Vilanova imekuja kwa mshituko lakini ameahidi kuonyesha kiwango cha hali ya juu msimu ujao ikiwa kama sehemu ya kumshukuru kocha huyo. Beki huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akisumbuliwa na majeruhi amedai kuwa wakati Vilanova akiwaaga aliwaomba kujituma kwa bidii katika msimu mpya uliopo mbele yao na watafanya hivyo kwa heshima yake.
MOYES AMKOMALIA FABREGAS.
MENEJA wa klabu ya Manchester United David Moyes amethibitisha kuwa klabu hiyo imetuma ofa nyingine kwa ajili ya kujaribu kumsajili Cesc Fabregas na kuonya kuwa bado hajakata tamaa na kiungo huyo wa Barcelona. Akihojiwa na waandishi wa habari katika Uwanja wa Nissan jijini Yokohama, Japan, Moyes amesema ofisa mkuu wa klabu hiyo Ed Woodward bado anafanya mawasiliano na Barcelona kuhusiana na Fabregas baada ya kutuma ofa ya pili inayokadiriwa kufikia paundi milioni 30 ambayo itakuwa rekodi mpya ya klabu kwenye usajili. Moyes alidai kuwa ingawa wana wachezaji kadhaa ambao wako katika mipango yao kama usajili wa Fabregas ukishindikana lakini kwasasa bado hawajakata tamaa ya kupata saini ya nyota huyo. United kwasasa wako katika ziara yao ya tatu jijini Tokyo ambapo tayari nyota wake Shinji Kagawa, Ashley Young na Chris Smalling wameshaungana na wenzake baada ya kupona majeraha yao.
MOURINHO AMTAKA MOYES KUACHANA NA NDOTO ZA KUMREJESHA RONALDO OLD TRAFORD.
FROOME BINGWA WA MICHUANO YA TOURE DE FRANCE.
MSHINDANO ya baiskeli yajulikanayo kama Tour de France yamefikia tamati jana kwa Chris Froome wa Uingereza kutawadhwa bingwa mpya wa mashindano ambayo ni ya 100 toka kuanzishwa kwake. Akishinda taji hilo kwa zaidi ya dakika nne, Froome alishikana mikono na na wenzake wa timu ya Sky wakati akikatisha katika msitari wa ushindi jijini Paris, Ufaransa. Huo unakuwa ushindi wa pili kwa Uingereza kwenye michuano hiyo baada ya mwendesha baiskeli Sir Bradley Wiggins ambaye naye anatoka katika timu ya Sky kushinda michuano hiyo mwaka jana. Mashindano yalishirikisha waendesha baiskeli kutoka nchi mbalimbali ambapo waliendesha baiskeli kwa kilometa 3,200 katika miji mbalimbali ya ya Ufaransa katika kipindi cha wiki mbili cha mashindano hayo.
Subscribe to:
Posts (Atom)






