Saturday, October 5, 2013

NADAL ATINGA FAINALI CHINA OPEN.

MCHEZAJI tenisi nyota wa Hispania Rafael Nadal amejiweka katika nafasi nzuri ya kurejea kileleni katika orodha za ubora duniani baada ya kutinga fainali ya michuano ya wazi ya China. Nadal mwenye umri wa miaka 27 alikuwa akiongoza kwa alama 4-2 katika seti ya kwanza wakati Tomas Berdych wa Czech alipojitoa kutokana na majeraha ya mgongo. Akihojiwa Nadal ambayeni bingwa wa michuano wazi ya Ufaransa na Marekani amesema mwaka huu umekuwa mzuri kwake na anashukuru kwa mafanikio aliyopata. Nadal alirejea katika ulingo wa tenisi Februari mwaka huu baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miezi saba kutokana na majeraha.

Friday, October 4, 2013

WENGER ACHUKIZWA NA WILSHERE KUVUTA SIGARA.

MENEJA wa klabu ya Arsenal ameonyeshwa kuchukizwa Jack Wilshere baada ya kiungo huyo kupigwa picha akiwa anavuta sigara nje ya klabu moja ya usiku jijini London. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza alipigwa picha akiwa na sigara mdomoni wakati akishangilia ushindi wa timu yake iliyopata kutoka kwa Napoli na Wenger amemuonya juu ya tabia yake hiyo. Wenger amesema hakubaliani kabisa na tabia za namna hiyo, hivyo atamtafuta na kuzungumza naye kuhusiana na suala hilo. Kocha huyo Mfaransa aliendelea kudai kuwa unapokuwa mchezaji unatakiwa kuwa mfano na hutakiwi kufanya vitu vinavyoweza kuharibu afya na wadhifa wako.

MOYES ASISITIZA KUWA MTU SAHIHI KWA UNITED PAMOJA NA KUANZA VIBAYA.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes amesisitiza kuwa ni mtu sahihi kwa kazi ya kuinoa timu hiyo pamoja na kuanza vibaya msimu huu. United ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Uingereza, wamepoteza mechi zao tatu kati ya sita walizocheza msimu huu chini ya Moyes na kwasasa wanashika nafasi ya 12 wakiwa wamejikusanyia alama saba. Lakini Moyes ambaye alichukua mikoba ya Sir Alex Ferguson aliyeifundusha klabu hiyo kwa miaka 26, ana imani na uwezo wake pamoja na kikosi alichonacho kukwea na kurejea tena kileleni mwa msimamo wa ligi. Moyes amesema ana uhakika United walichagua mtu sahihi kwa kazi hiyo na Ferguson alikuwa sehemu ya mchakato huo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa msimu bado ni mrefu na hana shaka kikosi chake kitarejesha makali yake katika miezi michache ijayo hivyo kusahau magumu yote ambayo wanapitia hivi sasa.

SAGNA NJE WIKI TATU.


MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema beki mahiri wa kulia wa timu hiyo, Bacary Sagna atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu kutokana na majeraha ya msuli wa nyuma ya paja yanayomsumbua. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa alipata majeraha hayo Jumanne wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Napoli ambao Arsenal ilishinda kwa mabao 2-0. Sagna anatarajiwa kukosa mechi za ligi dhidi ya West Bromwich Albion Jumapili hii na Norwch City itakayochezwa Octoba 19 pamoja na mechi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Finland Octoba 15. Mbali na mechi hizo Sagna pia ataukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal Na Borrusia Dortmund Octoba 22 mwaka huu.

Thursday, October 3, 2013

MJADALA WA QATAR 2022 KUCHUKUA NAFASI KUBWA MKUTANO WA FIFA ZURICH.

RAIS wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Sepp Blatter anakabiliwa na upinzani kuhusu mpango wake wa kubadilisha michuano ya Kombe la Dunia 2022 itakayofanyika nchini Qatar kuchezwa katika majira ya baridi. Mapema mwezi Agosti Blatter amesema anataka kuhamisha michuano hiyo ili kuepuka joto kali linaloweza kufikia nyuzi joto 40 katika majira ya kiangazi. Hata hivyo wajumbe watatu wa kamati ya utendaji ya FIFA wamedai kuwa watapingana na maamuzi yoyote ya haraka yatakayofanyika kuhamisha michuano hiyo. Naye rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini amesema itakuwa ni suala lisilowezekana kupigia kura suala hilo wakati watakapokutana kulijadili baadae leo. Mkutano huo wa siku mbili utakaofanyika jijini Zurich, Switzerland utahudhuriwa na wajumbe wapatao 28.

GABON YATAKA KUANDAA MICHUANO YA MATAIFA YA AFRIKA 2019.

GABON imetangaza jana kutuma maombi ya kuomba kuandaa michuano ya 32 ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019 na kuthibisha tuhuma zilizokuwa zimezagaa kwa kipindi kirefu. Kwa mujibu wa Wizara ya Michezo ya nchi hiyo maombi hayo yalitumwa Septemba 30 wakidai kuwa tayari nchi hiyo ina miundo mbinu ya kutosha iliyotumika kwa ajili ya michuano hiyo mwaka 2012 ambayo iliandaliwa kwa pamoja na Equatorial Guinea. Hata hivyo Gabon watapata upinzani mkali kutoka kwa Algeria, Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao nao tayari wameshatuma maombi yao. Katika taarifa yake wizara hiyo ilitamba kuwa nafasi kubwa ya kulishawishi Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kutokana na mafanikio waliyopata kwenye michuano ya 2012.

NADAL MBIONI KUMPIKU DJOKOVIC KATIKA ORODHA ZA UBORA.

MCHEZA tenisi nyota wa Hispania, Rafael Nadal amepiga hatua nyingine kusogelea nafasi ya kwanza katika orodha za ubora wa mchezo huo duniani baada ya kupambana na kushinda dhidi ya Philipp Kohlschereiber katika michuano ya wazi ya China. Nadal mwenye umri wa miaka 27 alishinda kwa alama 6-4 7-6 na kutinga robo fainali ya michuano hiyo ambapo sasa atakwaana na Fabio Fognini wa Italia. Nadal atachukua nafasi ya kwanza inayoshikiliwa na Novak Djokovic kama akitinga fainali ya michuano hiyo au Mserbia huyo akishindwa kushinda taji hilo. Kwa upande wa wanawake Agnieszka Radwanska anashika namba tatu, Li Na anayeshika namba nne na Petra Kvitova anayeshika namba tisa wote walishinda mechi zao na kusonga mbele katika michuano hiyo inayofanyika jijini Beijing.