Wednesday, February 5, 2014

CAF YAMUWEKEA NGUMU CHUJI, KUWAKOSA WACOMORO.

SHIRIKISHO la Soka Afrika,CAF limeikumbusha klabu ya Yanga kutomtumia kiungo wao Athumani Iddi ‘Chuji’ katika mchezo wake wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Komorozine ya Comoro, kwa kuwa bado anatumikia adhabu ya kadi nyekundu. Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto amewaambia Waandishi wa Habari leo kuwa CAF iliwaandikia barua kuwakumbusha kwamba, Chuji alipewa kadi nyekundu mara ya mwisho klabu hiyo ilipocheza michuano ya Afrika mwaka juzi katika mechi dhidi ya Zamalek. Kwa sababu hiyo, Yanga haitamtumia Chuji siku hiyo hadi hapo atakapomaliza adhabu yake. Aidha, Kizuguto pia amesema kwamba hawatamtumia mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi japokuwa CAF imempa leseni ya kucheza michuano hiyo mwaka huu, hadi hapo Shirikisho la Soka Tanzania,TFF litakapotoa baraka zake. Yanga wanarejea kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika na watafungua dimba nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi na Komorozine ya Comoro katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

FA YAKATAA RUFANI CARROLL.

MSHAMBULIAJI wa West Ham United, Andy Carroll ameshindwa rufani yake ya kadi nyekundu aliyopewa katika mchezo dhidi ya Swansea Jumamosi iliyopita baada ya Chama cha Soka cha Uingereza, FA kuitupilia mbali. Carroll mwenye umri wa miaka 25 alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kugongana na beki wa Swansea Chico Flores katika mchezo huo ambao West Ham waliibuka kidedea kwa kushinda mabao 2-0. Mshambuliaji huyo sasa atakosa mechi tatu za Ligi Kuu ambazo timu yake itacheza na Aston Villa, Norwich na Southampton. Kwa mujibu wa taarifa kutoka FA, West Ham wameshindwa kuwasilisha ushahidi kuwa mwamuzi Howard Webb aliyechezesha mchezo huo alifanya makosa kumtoa Carroll baada ya mkono wa nyota huyo kumpiga usoni Flores.

MATA ATAKUJA KUWA NGULI MAN UNITED.

WINGA mkongwe wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs ametonya kuwa kiungo mahiri aliyesajili kwa ada iliyovunja rekodi Juan Mata atakuja kuwa nguli hapo Old Traford. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alijiunga na United kwa ada paundi milioni 37.1 Januari mwaka huu na amecheza mechi mbili kwa mabingwa hao watetezi huku zote akitoa pasi za mwisho zilizozaa mabao. Kocha-mchezaji Giggs ambaye amecheza mechi 959 akiwa na United amesema hana shaka kuwa Mata atacheza kwa mafanikio akiwa hapo na hana kuja kuwa nyota wa kukumbukwa huko mbele. Giggs amesema hataki kumbebesha mzigo mkubwa nyota huyo lakini haoni kwanini kwasababu anafikiri kuwepo United kutamsaidia na pia kwa timu yake ya taifa ya Hispania. Giggs aliendelea kudai kuwa ujio wa Mata kutoka Chelsea pia utaongeza ari kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo ambao msimu wamekuwa wakisononeka kutokana na kutofanya vizuri.

NYOTA WA ZAMANI WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA.

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Zambia, Dennis Lota amefariki dunia jana jijini Johannesburg akiwa na umri wa miaka 40, baada ya kuugua kwa muda mfupi. Lota ambaye alikuwa akifanya kazi kama kocha msaidizi wa klabu ya Moroka Swallows ya Afrika Kusini alijulikana sana kwa umahiri wake wa ufungaji wakati akicheza katika timu ya Orlando Pirates ambako alicheza mechi zaidi ya 100 katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2002. Afrika Kusini ilikuwa kama nyumbani kwao baada ya kutumia muda wake wa uchezaji soka akiwa huko katika vilabu vya Witbank Aces, FC AK, Mpulanga Black Aces na Amazulu huku akicheza kwa kipindi kifupi pia katika vilabu vya FC Sion ya Switzerland na Esperance ya Tunisia. Lota pia aliitumikia timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo huku akiwemo katika kikosi hicho kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1996,1998,2000 na 2002. Aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa Moroka Swallows Machi mwaka 2011 ikiwa ni miaka michache baada ya kutundika daruga. Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF Issa Hayatou alituma salamu zake za rambirambi kwa familia, Chama cha Soka cha Zambia sambamba na Moroka Swallows na kueleza kusikitishwa na kifo cha nyota huyo.

BLANC AFARIJIKA PSG KUINGIA FAINALI YA KOMBE LA LIGI.

MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain,PSG ya Ufaransa, Laurent Blanc amepata ahueni baada ya wachezaji wake kufanikiwa kukwepa kwenda katika muda wa nyongeza katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Nantes. Katika mchezo huo kulikuwa na kila dalili ya kuongezwa kwa dakika 30 wakati Olivier Vigneau alipoisawazishiwa Nantes bao baada ya PSG kuongoza kwa kipindi kirefu kwa bao la Zlatan Ibrahimovic. Lakini alikuwa Msweden huyo huyo aliyefunga bao la ushindi katika dakika za mwisho na kuiwezesha PSG kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara yao ya tano. Blanc amesema katika kipindi cha kwanza Nantes waliamua kutocheza na kutumia muda mwingi wakizuia lakini walibadilika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha hivyo kufanya mchezo kuwa mgumu zaidi. Kocha huyo alikiri wachezaji wake kuonyesha kuchoka kidogo lakini anashukuru kwa kukwepa kucheza muda wa nyongeza. PSG sasa watakutana na mshindi kati ya Olympique Lyon au Troyes katika mchezo wa fainali.

SIMEONE AIHOFIA MADRID.

MENEJA wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone anaamini kuwa kikosi chake kitapambana na timu ngumu ya Real Madrid tofauti na ile waliyoifunga mapema msimu huu. Atletico waliwachabanga mahasimu wao hao wanaotoka jiji moja kwa bao 1-0 katika mchezo wa La Liga uliochezwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu huku Diego Costa akifunga bao hilo pekee. Hata hivyo, Simeone anafikiri kuwa itakuwa ni makosa kufikiria kuwa watakutana na Madrid waliyoifunga kipindi cha nyuma katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe a Mfalme utakaochezwa leo usiku. Simeone amesema kipindi kile cha mwanzoni mwa msimu Madrid ndio kwanza walikuwa wakijipanga baada ya kupata kocha mpya Carlo Ancelotti lakini hivi wamebadilika na tofauti kabisa. Lakini hata hivyo Simeone amesema anachukulia hiyo kama changamoto na atafanya kila analoweza kuhakikisha anashinda tena mchezo huo.

Tuesday, February 4, 2014

HATMA YA RONALDO KUJULIKANA KESHO.

KLABU ya Real Madrid inatarajiwa kujua hatma ya Cristiano Ronaldo ataongezewa adhabu na Shirikisho la Soka la Hispania, RFEF hapo kesho kufuatiwa nahodha huyo wa kimataifa wa Ureno kutolewa kwa kadi nyekundi Jumapili. RFEF ilitangaza kuwa itakutana ili kujadili adhabu anayostahili Ronaldo Februari 5, siku ambayo Madrid wanakutana na mahasimu wao Atletico Madrid katika mchezo wa Kombe la Mfalme. Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Manchester United alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia kumpiga konzi Carlos Gurpegui wa Athletico Bilbao katika mchezo wa La Liga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mfumo wa nidhamu wa RFEF, adhabu inaweza kupanda kutoka kufungiwa mechi moja hadi tatu kulingana na kosa lenyewe na ushahidi uliokuwepo. Ronaldo ambaye pia anafikisha miaka 29 hapo kesho amefunga mabao 32 katika mechi 30 alizoichezea Madrid msimu huu.