Monday, August 3, 2015

MAMBO YA FEDHA: RONALDO AMNUNULIA WAKALA WAKE KISIWA KAMA ZAWADI YAKE YA HARUSI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amempa wakala wake Jorge Mendes kisiwa cha Greek kama zawadi katika harusi yake. Kisiwa hicho hakikutajwa jina lake lakini taarifa zinadai kuwa thamani yake inaweza kuwa zaidi ya euro milioni tatu. Taarifa kutoka nchini Hispania zinadai kuwa Ronaldo inavifahamu vyema visiwa vya Greek kwani amekuwa akivitumia mara kwa mara kwa mapumziko yake. Mendes alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi Sandra nchini Ureno Jumapili iliyopita huku Sir Alex Ferguson akiwa miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria harusi hiyo. Miongoni mwa watu wengine mashuhuri waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na rais wa Real Madrid, Florentino Perez, rais wa benfica Luis Filipe Vieira na mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abramovic.

RAKITIC AIKINGIA KIFUA BARCELONA PAMOJA NA VIPIGO VITATU MFULULIZO.

KIUNGO wa Barcelona, Ivan Rakitic amepuuza matokeo mabaya wanayopata katika mechi za kirafiki za kujiandaa na msimu mpya akidai kuwa timu hiyo itapata matokeo mazuri pale watakapoyahitaji. Mabao mawili yaliyofungwa na Federico Bernardeschi yalitosha kuipa ushindi Fiorentina wa mabao 2-1 dhidi ya Barcelona jana hivyo kumaanisha kuwa sasa wamepoteza michezo mitatu mfululizo. Rakitic ambaye alitengeneza nafasi ya bao la kufutia machozi lililofungwa na Luis Suarez katika mchezo huo, bado ana imani kuwa watarejea katika kiwango chao karibuni. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 amesema siku zote timu inataka kushinda na kwa ujumla walicheza vyema lakini matokeo hayakuwa mazuri kwao. Rakitic aliendelea kudai kuwa pamoja na matokeo hayo hana shaka wanaweza kurejesha wimbi lao la ushindi pindi watakapoanza kucheza mechi za mashindano. Jumatano hii Barcelona ina kibarua kingine na klabu ya AS Roma kabla ya Agosti 11 mwaka huu kuanza rasmi mechi za mashindano kwa kucheza na Sevilla katika mchezo wa Super Cup wa Ulaya ambao hukutanisha bingwa wa Ligi ya Mabingwa na Europa League.

RAFAEL KUTIMKIA LYON.

RAIS wa klabu ya Lyon, Jean-Michel Aulas amedai kuwa timu hiyo inajipanga kukamilisha uhamisho wa beki wa kulia wa Manchester United Rafael. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 25, alichezeshwa mara 11 pekee chini ya meneja Louis van Gaal msimu uliopita na hakujumuishwa katika kikosi cha United kilichofanya ziara nchini Marekani mwezi uliopita. Rafael sasa amesafiri kuelekea nchini Ufaransa ili kukamilisha uhamisho wake Lyon na Aulas alithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter. Julai mwaka huu wakala wa Rafael alidai kuwa United ilikuwa tayari kumtoa beki huyo kwa klabu ya Benfica ili waweze kumnasa Nicolas Gaitan..

BERLUSCONI AKUBALI KUIUZA AC MILAN.

WAZIRI mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi amesaini makubaliano ya mauzo ya awali ya hisa asilimia 48 za klabu ya AC Milan kwa kundi linaloongozwa na mfanyabiashara wa Thailand Bee Taechaubol. Msemaji wa kampuni ya Fininvest inayomilikiwa na Berlusoni amesema mpaka ifikapo Septemba 30 mwaka huu hisa hizo zitakuwa zimehamishwa sambamba na malipo ya euro milioni 480. Klabu ya AC Milan inamilikiwa na Fininvest, kampuni inayomilikiwa na familia ya Berlusconi ambayo pia inamiliki kituo cha luninga cha Mediaset na kampuni ya uchapishaji ya Mondadori. Msemaji huyo amesema dili hilo limesainiwa na Fininvest na Taechaubol na kuthibitishwa na Berlusconi mwenyewe. Naye mfanyabiashara huyo wa Thailand alithibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram. Milan ambao ni mabingwa mara saba wa Ulaya, wamepoteza mng’aro wao katika miaka ya karibuni na kufanikiwa kushinda taji la mwisho la Serie A mwaka 2011. Klabu hiyo pia kwasasa inakabiliwa na madeni yanayofikia euro milioni 250 na mwaka jana wamepata hasara ya euro milioni 91.

MALINZI AMSHUKURU TENGA.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amemshukuru Rais wa CECAFA, Leodgar Tenga kwa kuipa Tanzania uenyeji wa mashindano ya Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) iliyomalizika jana kwa klabu ya Azam FC kutawazwa Mabingwa wapya wa michuano hiyo. Aidha Malinzi ameishukuru Kamati ya Ndani ya Uendeshaji ya Michuano hiyo (LOC) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa na kuhakikisha michuano hiyo inafanyika na kumalizika katika hali ya usalama na amani. Malinzi pia amewapongeza wapenzi, washabiki na wadau wa soka nchini waliojitokeza kushuhudia michezo ya michuano hiyo na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ndani nan je ya uwanja kipindi chote cha michuano. Rais Malinzi ameipongeza klabu ya Azam FC kwa kutwaa Ubingwa Kagame, kwa kutwaa ubingwa huo imeweza kuweka historia ya kutwaa Ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake na pia kuwa klabu iliyocheza michuano hiyo na kuwa Bingwa bila kuruhusu nyavu zake kutikisika. Pia Malinzi amewashukuru waandishi wa habari/vyombo vya habari kwa sapoti yao wakati wa michuano hiyo. Shukrani hizo pia zimepelekwa kwa klabu za Yanga SC, KMKM kwa kushiriki mashindano hayo.

WENGER AANZA KUTAMBA BAADA YA KUIBANJUA CHELSEA.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini wachezaji wake wamefanikiwa kuvuka kikwazo kikubwa cha kiakili kwa kuifunga Chelsea katika mchezo wa Ngao ya Hisani jana. Arsenal walikuwa hawajawahi kuifunga Chelsea chini ya Jose Mourinho katika mechi 13 walizokutakana kabla ya mchezo wa jana. Lakini bao la Alex Oxlade-Chamberlain lilitosha kuipa ushindi Arsenal wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Wembley. Akihojiwa Wenger amesema ilikuwa muhimu kwa kikosi chake kukiondoa kikwazo hicho mbele yao hivyo ana imani ari ya ushindi itakuwa imeongezeka kuelekea katika msimu mpya.

SAFARI YA MESSI GABON YAZIDI KUZUA MAZITO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Barcelona, Lionel Messi ameshutumiwa na Shirika la Haki za Binadamu, ambao wamemtuhumu kuungana na wakandamizaji katika ziara yake ya Gabon hivi karibuni. Messi alipigwa picha akiwa na rais wa Gabon Ali Bongo ambaye anatajwa kama diktekta, baada ya kusaidia kuweka jiwe la msingi katika uwanja mpya utakaotumika kwa ajili ya fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017. Mbali na kuweka jiwe hilo la msingi, Messi alitembelea kituo cha afya kinachoendeshwa na serikali ya nchi hiyo pamoja na mgahawa unaomilikiwa na familia ya Bongo. Wakati serikali ya Gabon ikikanusha taarifa kuwa Messi alilipwa mamilioni ya fedha kwenda nchini humo mwezi uliopita, sasa nay eye mwenyewe amekuwa akikosolewa vikali kwa kuonekana hadharani akiunga mkono utawala wa Bongo. Rais huyo amekuwa akituhumiwa na masuala ya ufisadi huko nyuma pamoja na kukiuka haki za binadamu ikiwemo kuzia uchunguzi wa mauaji ya watoto yanayodaiwa kuelendelea nchini humo.