KUSUASUA kwa klabu za Arsenal na Barcelona katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kumepelekea kuporomoka katika viwango vya vilabu vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA. Arsenal mpaka sasa hawajapata alama yeyote katika michuano hiyo baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Dinamo Zabreb na Olympiakos na matokeo yake wameporomoka mpaka nafasi ya 10 nyyuma ya Paris Saint-Germain na Juventus. Barcelona kwa upande wao walifanikiwa kushinda mchezo wao wa pili dhidi ya Bayer Leverkusen lakini sare ya bao 1-1 waliyopata katika mchezo wa kwanza dhidi ya AS Roma imefanya kupokwa nafasi ya kwanza na Bayern Munich ambao wameshinda mechi zao zote mbili. Tano bora katika orodha hiyo ukiacha Bayern na Barcelona katika nafasi ya kwanza na pili, Real Madrid ndio wanaofuatia katika nafasi ya tatu huku Chelsea na Atletico Madrid wakishika nafasi ya nne na tano.
Thursday, October 1, 2015
VAN GAAL ALALAMIKIA MECHI NYINGI KWA KIKOSI CHAKE.
MENEJA wa Manchester United Louis van Gaal amesema kikosi chake kinataabika baada ya kucheza mechi sita ndani ya siku 18, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 waliopata dhidi ya Wolfsburg jana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao mkwaju wa penati la Juan Mata katika kipindi cha kwanza na lile la Chris Smalling katika dakika ya 53 yalitosha kuipa United ushindi wao kwanza katika kundi B. Vinara hao wa Ligi Kuu ambao watakwaana na Arsenal Jumapili hii, walilazimika kujilinda zaidi wakati Wolfsburg waliopokuwa wamecharuka wakitaka kusawazisha. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Van Gaal amesema wachezaji wengi wamechoka kwasababu ya mechi nyingine walizocheza kwa kipindi kifupi. United walipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya PSV Eindhoven lakini ushindi dhidi ya Wolfsburg unamaanisha timu zote zinalingana kwa alam tatu kila moja baada ya mechi mbili.
PELLEGRINI ADAI CITY HAWAKUSTAHILI USHINDI.
MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema kikosi cha hakikustahili ushindi wa dakika za mwisho walipata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach jana. Sergio Aguero aliifungia City bao la penati lililoipa ushindi wa mabao 2-1, huku Joe Hart naye akokoa penati kabla ya wapinzani wao hao hawajapata bao la kuongoza katika kipindi cha pili. Akihojiwa mara bada ya mchezo huo, Pellegrini amesema City ambao walipoteza mchezo wao kwanza dhidi ya Juventus, walikuwa na bahati kushinda mchezo huo. City wametandikwa katika mechi tatu kati ya nne walizocheza za mashindano yote, ikiwemo michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspurs na West Ham United. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa katika michezo dhidi ya Juventus na West Ham hawakustahili kupoteza lakini leo wameshinda ingawa haikutakiwa kuwa hivyo.
RONALDO AFIKIA REKODI YA MABAO YA RAUL.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefanikiwa kufikia rekodi ya mabao ya Raul kwa Real Madrid na kuongeza idadi ya mabao toka aanze kusakata kabumbu kufikia 501 baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Malmo jana. Mabao mawili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, sasa yanamfanya kufikia rekodi iliyowekwa na Raul katika klabu hiyo ya mabao 323. Akihojiwa Ronaldo amesema ni jambo kubwa kufikia rekodi hiyo na anafurahi kwenda nchini Sweden na kufunga pamoja na Malmo kuonyesha mchezo mgumu. Pamoja na mchezo huo kuwa mgumu, Ronaldo amesema anashukuru wameshinda na kupata alama tatu muhimu. Ushindi huo unaifanya Madrid kushinda mechi zake mbili za kundi A walichocheza mpaka hivi sasa baada ya kuichap mabao 4-0 Skakhtar Donetsk katika mchezo wa kwanza ambao Ronaldo alipiga hat-trick.
MASCHERANO KUPANDA KIZIMBANI OCTOBA 29.
MAHAKAMA nchini Hispania imedai kuwa kiungo wa Barcelona Javier Mascherano anatarajiwa kupanda kizimbani Octoba 29 mwaka huu kujibu tuhuma za ukwepaji kodi. Jaji wa mahakama wa jiji la Barcelona alikiri kuletewa kesi na waendesha mashitaka ambao wanamtuhumu nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 31 kutumia kampuni za kigeni kuficha mapato yake halisi yanayotokana na haki ya kutumia picha zake. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa katika kitongoji cha Gava eneo ambao Mascherano ndilo analoishi. Waendesha mashitaka wanamtuhumu kiungo huyo wa zamani wa West Ham United na Liverpool kushindwa kuweka wazi zaidi ya euro milioni 1.5 alizopata mwaka 2011 na 2012 kutokana na haki za matangazo alizotoa kwa kampuni anazomiliki Ureno na Marekani.
MOURINHO AKWEPA KITANZI CHA FA.
MENEJA wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho hataadhibiwa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA, baada ya kuthibitika hakutumia lugha mbaya dhidi ya aliyekuwa daktari wa timu Eva Carneiro. FA ilipitia mikanda ya video iliyohusika na tukio hilo la Mourinho na Carneiro ambapo ilionekana kama alitumia lugha chafu kwa daktari huyo. Carneiro aliingia uwanjani kumtibu mshambuliaji Eden Hazard wakati wa dakika za lala salama kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Swansea, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2. Mara baada ya mchezo na na Swansea, daktari huyo aliondolewa kuihudumia kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Carneiro amebwaga manyanga kuwepo Chelsea licha ya kutakiwa kurudi kazini na sasa yuko mbioni kusaka sheria katika mamlaka husika.
KOCHA GUINEA-BISSAU ALIMWA ADHABU KWA KUMTUKANA MWAMUZI.
KOCHA wa timu ya taifa ya Guinea-Bissau, Paulo Torres amefungiwa kusimama katika benchi la ufundi katika mechi zilizobakia za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 kwa kosa la kumtukana mwamuzi. Shirikisho la Soka la Afrika-CAF lilimpata na hatia Torres ya kutumia lugha ya kuudhi na matusi kwa mamuzi aliyechezesha mechi yao dhidi ya Zambia ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana. Torres atakosa mechi ya nyumbani na ya ugenini dhidi ya Kenya Machi mwakani na kisha mechi dhidi ya Congo na Zambia. Sare hiyo ya Guinea-Bissau iliwaacha wakishika mkia katka Kundi E wakiwa wameambulia alama moja. Hata hivyo adhabu hiyo hiyo ya CAF haitaathiri mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2018 na Torres yuko huru kuongoza timu hiyo dhidi ya Liberia kwenye mzunguko wa kwanza.
Subscribe to:
Posts (Atom)






