Tuesday, January 5, 2016

GOLIKIPA WA ZAMANI WA NEWCASTLE AZIKWA.

WACHEZAJI wenzake kadhaa wametoa heshima zao za mwisho kwa golikipa wa zamani wa Newcastle United na timu ya taifa ya Jamhuri ya Czech Pavel Srnicek katika mazishi yake jijini Ostrava jana. Wachezaji hao wa zamani wa Newcastle Steve Howey na Steve Harper walihudhuria mazishi hayo sambamba na wachezaji wenzake wa timu ya taifa akiwemo Ludek Miklosko na nguli wa Juventus Pavel Nedved. Srnicek alifariki Desemba 29 mwaka jana akiwa na umri wa miaka 47, siku tisa baada ya kuugua ugonjwa wa moyo. Golikipa huyo alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Newcastle katika kipindi cha kuanzia mwaka 1991 mpaka 1998 alichoichezea timu hiyo.

Friday, January 1, 2016

WAKALA WA POGBA AWAKATA MAINI BARCELONA.

WAKALA wa Paul Pogba amekanusha tetesi kuwa Barcelona ndio wenye nafasi ya kumsajili kiungo wa huyo wa kimataifa wa Ufaransa na Juventus mwishoni mwa msimu huu. Pogba amekuwa mmoja kati ya wachezaji wanaowindwa zaidi duniani toka alivyojiunga na Juventus kwa uhamisho huru akitokea Manchester United majira ya kiangazi mwaka 2012. Nyota huyo amefanikiwa kushinda mataji matatu ya Serie A akiwa na Juventus na kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita. Juventus bado ina mkataba na Pogba unaomalizika mwaka 2019 lakini ofa kutoka katika klabu kubwa zinaweza kutolewa katika kipindi cha kiangazi kwa mujibu wa wakala wake Mino Raiola. Raiola amesema anafahamu klabu kubwa zitakuja kujaribu kumsajili Pogba majira ya kiangazi lakini wenye nafasi kubwa mpaka sasa Juventus wenyewe na hizo klabu zingine zinazotajwa.

NILIWAHI KUJA CITY - DE BRUYNE.

KIUNGO wa Manchester City, Kevin De Bruyne amekiri kuwa angeweza kubakia Ujerumani kwa msimu mwingine zaidi kama mpenzi wake asingekuwa akitegemea kujifungua. De Bruyne mwenye umri wa miaka 24, alihamia City akitokea Wolfsburg kwa kitita cha paundi milioni 54 majira ya kiangazi mwaka jana ambapo tayari ameshafunga mabao matano na kusaidia mengine nane katika mechi 15 za Ligi Kuu alizocheza. Lakini nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji sasa amebainisha kuwa angeweza kuendelea kubakia Ujerumani kama sio masuala binafsi. Akihojiwa De Bruyne amesema kuzaliwa kwa mwanaye ni jambo kubwa kufanyika katika maisha yake na ndio lilichangia kwa kiasi kikubwa kuhama mapema kuliko alivyotegemea. De Bruyne aliendelea kudai kuwa kama lisingekuwa suala hilo angeendelea kubakia Wolfsburg walau kwa msimu mwingine zaidi.

PETR CECH APANIA KUENDELEZA REKODI YAKE YA KUMZUIA MESSI.

GOLIKIPA wa Arsenal, Petr Cech amekiri kupania kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa na nyota wa Barcelona Lionel Messi. Wawili hao wamekutana mara kadhaa wakati Cech akiwa Chelsea ambapo katika mechi nane walizokutana Messi hajafanikiwa hata mara moja kumfunga golikipa huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech. Nyota hao wanatarajiwa kukutana tena wakati Arsenal watakapovaana na Barcelona katika hatua ya timu 16 bora za michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi ujao. Akihojiwa Cech amesema ni jambo kubwa kwakuwa sio makipa wengi ambao wamewahi kucheza na Messi katika mechi nane na hajawafunga. Golikipa huyo aliendelea kudai kuwa kama Messi akifanikiwa kufunga halafu bado wakafuzu itakuwa sio muhimu sana kwani wanahitaji wao ni kusonga mbele.

WENGER AIPA NAFASI UINGEREZA MICHUANO YA EURO 2016.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema timu ya taifa ya Uingereza ina ubora wa kunyakuwa taji la michuano ya Ulaya mwaka huu. Uingereza imewahi kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mara mbili na robo fainali mara mbili katika historia yao. Wenger amesema Uingereza haitakuwa inapigiwa chapuo kushinda michuano hiyo itakayofanyika nchini Ufaransa lakini wana vipaji vinavyoweza kuwashangaza wengi. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Uingereza ina wachezaji wengi wadogo wenye vipaji hivyo haitashangaza sana kama wakifanya vyema katika michuano hiyo pamoja na kutotegemewa na watu wengi.

VAN GAAL AWAAMBIA UNITED WASITEGEMEE MIUJIZA.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amesema hakuna miujiza ya kuimarisha hali ya klabu hiyo zaidi ya wahusika wote kuongeza bidii. United wamecheza mechi nane bila kushinda hata moja, sita zikiwa Ligi Kuu hivyo kuwafanya kuporomoka mpaka nafasi ya sita katika msimamo. Mbali na kushuka katika msimamo pia wameng’olewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuangukia katika michuano ya Europa League. Akihojiwa Van Gaal amesema hakuna miujiza, jambo muhimu wanaloweza kufanya ni kuangalia walipokosea na kuona jinsi gani wanaweza kuboresha kama timu ili waweze kupata matokeo wanayohitaji.

RUFANI YA BILITY YAKATALIWA.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Liberia, Musa Bility ameshindwa rufani yake ya kupinga kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. FIFA ilimuengua Bility Novemba 12 mwaka jana katika kinyang’anyiro hicho kwa madai kuwa hakukidhi baadhi ya vigezo vya kuwa mgombea. Bility aliipinga adhabu hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS akitegemea jina lake kurejeshwa tena. Hata hivyo, CAS katika taarifa yake jana walitupilia mbali rufani hiyo na Bility amesema anasubiri sababu haswa za kukataliwa kwa rufani yake ili aweze kuangalia hatua zaidi za kuchukua.