Monday, January 9, 2017

NANI KUIBUKA MBABE?

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo anapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani katika sherehe zitakazofanyika baadae leo jijini Zurich. Nyota huyo wa Real Madrid alimshinda hasimu wake Lionel Messi na kushinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya nne mwezi uliopita. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilimaliza mkataba wake na jarida la France Football kwa tuzo ya Ballon d’Or mwaka jana. Nyota wa Barcelona Messi na mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann nao pia wamo katika kinyang’anyiro hicho. Mbali na tuzo hiyo lakini pia atapatikana mchezaji bora wa mwaka duniani kwa upande wa wanawake na kocha bora kwa upande wa wanaume na wanawake.

KLOPP ATETEA UAMUZI WAKE WA KUPANGA YOSO.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amekingia kifua uamuzi wa kikosi alichokichagua kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la FA waliotoka sare ya bila kufungana na klabu ya daraja la pili ya Plymouth. Liverpool sasa wanakabiliwa na safari ya kwenda Devon kwa ajili ya mchezo mwingine wa marudiano huku wakikabiliwa na mechi sita mwezi huu. Klabu hiyo pia inakabiliwa na mchezo wa mikondo miwili wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Southampton pamoja na mechi za Ligi Kuu dhidi ya Manchester United, Swansea City na Chelsea. Hata hivyo alipohojiwa kuhusiana na kikosi alichotumia, Klopp amesema hadhani kama alifanya makosa kuchagu kikosi hicho.

Friday, January 6, 2017

MOURINHO AUNGA MKONO MPANGO WA RAIS WA FIFA.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho ameunga mkono mapendekezo ya kuongeza timu kufikia 48 katika Kombe la Dunia akiamini kuwa wachezaji watalindwa vyema. Rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ana matumaini mpango wake kuwa na makundi 16 yenye timu tatu kuanzia michuano ya mwaka 2026 utapitishwa wakati wa kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo wiki ijayo. Muungano wa Vilabu Ulaya ambao United pia ni mjumbe wake, tayari wameshaonyesha kutounga mkono pendekezo hilo lakini Mourinho yeye anaunga mkono. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Mourinho amesema anaunga mkono kwasababu ana uhakika FIFA itazingatia maslahi ya wachezaji kwa kutowachezesha mechi nyingi zaidi kuliko sasa.

UNITED YAANZA MAZUNGUMZO YA KUMUWANIA GRIEZMANN.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kuanza mazungumzo ya kumuwania Antoine Griezmann na wanatarajia kumpa ya mshahara wa paundi 220,000 kwa wiki ili kumshawishi kutua Old Trafford. Taarifa zinadai kuwa United tayari wameanza mazungumzo na wawakilishi wa nyota huyo wa Atletico Madrid na wameahidi mshahara wake utafikia ule anaolipwa Paul Pogba katika klabu hiyo. Griezmann ameshawahi akikaririwa akieleza jinsi anavyoihusudu United na Mourinho katika mahojiano yake huko nyuma. Kama wakifikia makubaliano hayo United inadaiwa italazimika kutoa kitita cha paundi milioni 86 ili kutengua kitenzi katika mkataba wa mshambuliaji huyo.

UGANDA WAITOA KIMASOMASO AFRIKA MASHARIKI TUZO ZA AFRIKA.

KIPA wa timu ya taifa ya Uganda, Denis Onyango ameweka historia kwa kuwa kipa wa kwanza kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka anayecheza soka ndani ya Afrika katika sherehe zilizofanyika jijini Abuja, Nigeria jana usiku. Onyango mwenye umri wa miaka 31 alitwaa tuzo hiyo kufuatia kufanya vyema mwaka 2016 akiisaidia klabu yake ya Mamelodi Sundowns kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na timu yake ya taifa ya Uganda. 
Katika tuzo hiyo ya Onyango pia Uganda ilitutoa kimasomaso nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kuteuliwa kuwa timu bora ya mwaka baada ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Kabla ya Onyango tuzo hiyo ilikuwa ikishikiliwa na nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta ambapo aliitwaa wakati akiwa na klabu ya TP Mazembe kabla ya kwenda kucheza Genk ya Ubelgiji kiangazi mwaka jana. Wengine waliotawala tuzo hizo jana ni Riyad Mahrez wa Algeria aliyetwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika akiwashinda Sadio Mane wa Senegal na mshindi wa mwaka jana Pierre-Emerick Aubameyang.

GUARDIOLA ANA HAMU YA KUONA MSISIMKO WA KOMBE LA FA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema ana hamu kubwa ya kusimamia mchezo wake wa kwanza wa michuano ya Kombe la FA wakati kikosi chake kitakapovaana na West Ham United katika mchezo wa mzunguko wa tatu. City wanatarajiwa kukwaana na West Ham katika Uwanja wa London baadae leo. Akihojiwa Guardiola amesema michuano hiyo ni muhimu kwasababu timu za chini zinaweza kuzifunga timu kubwa ndio maana inakuwa na msisimko. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa ana hamu kubwa na mchezo huo lakini utazikutanisha timu zote za Ligi Kuu hivyo utakuwa mgumu.

OBI MIKEL AONDOKA CHELSEA KWENDA CHINA.

KIUNGO John Mikel Obi ametangaza kuondoka Chelsea rasmi na kwenda kujiunga na klabu ya Tianjin TEDA inayoshiriki Ligi Kuu ya China. Nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria mwenye umri wa miaka 29, ameichezea Chelsea mechi 372 toka ajiunge nao mwaka 2006. Katika barua yake kwenda kwa mashabiki, Obi Mikel amesema imekuwa ni heshima kubwa kwake kuichezea klabu hiyo lakini anadhani wakati umefika wa kwenda kutafuta changamoto nyingine. Obi Mikel amefanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu, manne ya Kombe la FA moja na Europa League na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Obi Mikel anakuwa mchezaji wa pili wa Chelsea kutimkia China katika wiki za karibuni baada ya Oscar aliyehamia Shanghai SIPG.