Sunday, December 20, 2015

PIGO ARSENAL, WELBECK MPAKA FEBRUARI.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema mshambuliaji wake Danny Welbeck hatarejea uwanjani hivi karibuni kufuatia upasuaji wake wa goti kusogeza mbele tena. Welbeck amekuwa nje ya uwanja toka Aprili mwaka huu na Wenger anadhani nyota huyo ataweza kurejea uwanjani tena Februari mwaka huu. Mara ya mwisho Wenger alidai kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 25 angeweza kurejea uwanjani Septemba kabla ya kusogeza mbele mpaka Christmas. Hata hivyo akihojiwa leo, Wenger amesema bado Welbeck hataweza kurejea uwanjani hivi karibuni na hilo ni pigo kubwa kwao kwani wanashindwa kuwapa muda wa kupumzika wachezaji wengine.

Friday, December 18, 2015

RONALDO AANZA KUWAZA MAISHA BAADA YA SOKA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo tayari ameshaanza kuangazia maisha yake baada ya soka kufuatia kubainisha mpango wake wa kuwekeza zaidi ya dola milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa hoteli za kifahari zitakazokuwa na jina lake CR7 nchini kwake Ureno, Madrid na New York. Akihojiwa Ronaldo amesema wachezaji wengi wa soka wanamaliza kucheza wakiwa hawajui kitu gani wanataka kufanya lakini kwake hilo ni tofauti kwani anataka kuendelea kulilinda jina lake. Ronaldo ambaye ni mshindi wa tuzo tatu za Ballon d’Or ataungana na kampuni inayomiliki hoteli za Pestana ambayo kama ilivyo yeye mmiliki wake pia anatoka Madeira. Nyota huyo amesema akiwa na umri wa miaka 30 sasa ana machaguo mengi na anafurahia kwasababu ana watu wengi wanaomuunga mkono. Ronaldo aliendelea kudai kuwa anataka jina lake kuendelea kuwa bora katika kitu chochote atakachofanya baada ya kuacha soka.

GUUS HIDDINK ANUKIA CHELSEA.

KLABU ya Chelsea inadaiwa kuanza mazungumzo na Guu Hiddink ili aweze kuwa kocha ajaye baada ya Jose Mourinho kutimuliwa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 69 raia wa Uhoanzi kwasasa yuko jijini London akifanya mazungumzo na maofisa wa klabu hiyo. Hiddink ambaye ameshawahi kuinoa Chelsea, bado hajasaini mkataba lakini ndio anatarajiwa kuja kuwa kocha wa muda wakati wakiendelea kutafuta mbadala wa kudumu. Chelsea kwasasa inashikilia nafasi ya 16 katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa alama moja juu ya eneo la kushuka daraja. Mourinho alitimuliwa jana ikiwa imepita miezi saba toka aiongoze klabu hiyo kunyakuwa taji la Ligi Kuu.

ROONEY KUREJEA TENA UWANJANI.

NAHODHA wa Manchester United Wayne Rooney anaweza kurejea tena uwanjani kesho katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Norwich City. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye kama akicheza mchezo huo atakuwa ametimiza mechi 500 akiwa mchezaji wa United, alikosa michezo mitatu iliyopita kwasababu ya majeruhi ya kifundo cha mguu. Meneja wa United Louis van Gaal amebainisha kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza amekuwa akifanya mazoezi wiki yote hii. Van Gaal mwenye umri wa miaka 64 amesema anaweza kucheza lakini inabidi kusubiri na kuona kama itawezekana.

BENZEMA AMEKOSEA - DESCHAMPS.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps amesema Karim Benzema alifanya makosa juu ya sakata la mkanda wa ngono na hataweza kuitumikia nchi hiyo katika michuano ya Euro 2016 mpaka jina lake litakaposafishwa. Mshambuliaji huyo wa Real Madrid anakabiliwa na makosa ya jinai baada ya kutuhumiwa kuhusika katika sakata hilo ambalo linamhusu mhchezaji mwenzake Mathieu Valbuena. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo Deschamps amesema kwasasa ni jambo lisilowezekana kwa nyota huyo kuitumikia timu ya taifa mpaka pale jina lake litakapotakasika. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Benzema hajakubaliana na hali ilivyo ndio anadhani amefanya makosa.

DEL BOSQUE KUIACHA HISPANIA BAADA YA EURO 2016.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque anategemea kuachia nafasi yake hiyo baada ya michuano ya Euro 2016. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 ameliongoza taifa hilo kunyakuwa mataji mawili ya Ulaya pamoja na Kombe la Dunia. Del Bosque ambaye amewahi kuinoa Madrid amesisitiza michuano hiyo itakayofanyika nchini Ufaransa inaweza kuwa ya mwisho kwake na ana matumaini ya kuondoka kwa mafanikio. Akihojiwa kocha huyo amesema kama kila kitu kikienda kama anavyotegemea baada ya michuano hiyo ataachia kibarua chake hicho.

RAIS WA MADRID AMKANA MOURINHO.

RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez amedai klabu hiyo haina mpango wa kumrejesha Jose Mourinho. Mourinho mwenye umri wa miaka 52, alishinda taji la La Liga na Kombe la Mfalme katika kipindi chake alipokuwa Bernabeu mwaka 2010 mpaka 2013 lakini jana alitimuliwa na Chelsea. Meneja wa Madrid Rafa Benitez yuko chini ya shinikizo kufuatia matokeo yasiyoridhisha msimu huu kikiwemo kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa mahasimu wao Barcelona. Akihojiwa Perez amesema hakuna anayejua mambo yajayo lakini kwasasa Mourinho hawezi kurejea Madrid.