
Sunday, January 15, 2012
YANGA YAIFUNGA SOFAPAKA.
Mabingwa wa Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga wameendeleza ushindi katika michezo ya kirafiki, baada ya kuwafunga Sofapaka ya Kenya jana katika uwanja wa Taifa. Katika mchezo wa leo uliochezwa katika uwanja wa Taifa, Yanga wamewachapa Sofapaka toka Kenya goli 2-1 katika mchezo wa kujipima ubavu, ambapo Yanga waliutumia mchezo kwa ajili ya maandalizi wa ligi kuu ya Vodacom na michuano ya klabu bingwa Afrika. Yanga walianza kuandika goli la kwanza kupitia kwa mchezaji bora wa Uganda kwa mwaka 2011, Hamis Kiiza katika dakika ya 29 kabla ya kurejea tena nyavuni katika dakika ya 60. Goli la Sofapaka lilifungwa na Thomas Wanyama katika dakika ya 88. Leo katika uwanja wa Taifa Mnyama Simba atacheza na mabingwa wa Kenya Tusker saa kumi jioni.
CECAFA KAGAME CUP YAREJEA TENA DAR ES SALAAM.
UDHAMINI mnono unaopatikana Tanzania umelifanya Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuamua kurudisha Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam tena mwaka huu. Michuano hiyo ya Kagame iliyofanyika mwaka jana na kushuhudia Yanga ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga Simba katika fainali huku umeme ukikatika Uwanja wa Taifa, mwaka huu yalipangwa kufanyika Rwanda. Akizungumza na gazeti la The New Times la Rwanda, Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema wameamua kurudisha mashindano hayo Tanzania kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana. Pamoja na mafanikio ya mashindano hayo, Cecafa pia kuna jambo moja la muhimu la kupatikana kwa wadhamini Tanzania ambao wameshapata siku moja iliyopita. Taarifa hiyo inalifanya jiji la Dar es Salaam kuwa mwenyeji kwa mara ya pili mfululizo kwa Kombe la Kagame kama ilivyokuwa kwa Kombe la Chalenji lililofanyika mwaka jana na kushudia Uganda 'Cranes' wakitwaa ubingwa huo kwa kuichapa Rwanda. Zanzibar na Sudan pia walikuwa wakipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa kwa klabu Afrika Mashariki na Kati, lakini tatizo la fedha limewakosesha nafasi hiyo. Fainali ya mwaka jana ya Kombe la Kagame, ilizikutanisha timu zote za Tanzania, Simba na Yanga na kushuhudia kocha Sam Timbe akipata taji lake la nne la Kombe la Kagame baada ya kufanya hivyo akiwa na SC Villa (2005), Polisi (2006), Atraco (2009) na Yanga (2011).
CANNAVARO ATIMKIA INDIA.
NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa la Italia iliyonyakuwa Kombe la Dunia mwaka 2006 Fabio Cannavaro ameamua kuvaa tena daruga baada ya kustaafu na kuelekea nchini India. Cannavaro ambae aliisaidia timu yake Iitalia kunyakuwa kombe hilo akiwa kama beki atakuwa sehemu ya michuano itayoshirikisha timu sita huko nchini India mashindano ambayo yameandaliwa na Chama cha Soka cha nchi hiyo wakishirikiana na kampuni ya CMG. Beki huyo atakuwa na majina mengine maarufu katika ulimwengu wa soka wakiwemo Robbie Fowler na John Barnes wa Uingereza, Mfaransa Robert Pires, Hernan Crespo na Juan Pablo Sorin wa Argentina, Fernando Morientes wa Hispania na Jay Jay Okocha wa Nigeria ni mojawapo ya sura mpya zitakazoonekana katika Ligi Kuu nchini India. Katika mtandao wa kijamii wa Twitter Cannavaro amesema kuwa ameamua kurejea uwanjani tena akiwa na klabu ya West Bengal ya nchini India lakini hakueleza ni kwa kipindi gani ataichezea klabu hiyo.
BERLUSCONI AMKUMBATIA MKWEWE PATO.
MMILIKI wa klabu ya AC Milan Silvio Berlusconi amesema ameamua kumbakisha mshambuliaji wa klabu hiyo Alexandre Pato kuliko kumuuza katika klabu ya Paris Saint-German ya Ufaransa kwa ada iliyoripotiwa kuwa kiasi cha euro milioni 35. Pato alitoa taarifa rasmi Alhamisi iliyopita kuhusu mustakabali wake wa baadae na mabingwa hao wa Serie A uamuzi huo unaonekana utasimamisha mbio za klabu hiyo za kumnyakuwa mshambuliaji wa Manchester City Carlos tevez. Katika taarifa aliyoitoa Berluscon Jumamosi amesema kuwa makubaliano ya kumuuza Pato hayakumridhisha kiufundi wala kiuchumi na anaamini maamuzi aliyochukua ni sahihi kwa klabu hiyo. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil alijunga na klabu hiyo mwaka 2007 na sasa anatoka binti wa Berlusconi aitwaye Barbara.
WENGER ADAI DIRISHA DOGO LA USAJILI LINAWAPA WACHEZAJI KIBURI.
MENEJA wa Arsenal Arsene Wenger anaamini kuwa usajili katika kipindi cha dirisha dogo unatakiwa ufutwe kwa kuwa unawapa nguvu wachezaji ambao wanakuwa hawana furaha katika timu zao. Wenger aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa kwa mawazo yake dirisha dogo la usajili liondelewe na badala yake liachwe wazi kwa mwaka wote au kulifunga kwa mwaka mzima. Meneja huyo aliongeza kuwa kila mtu anakaa roho juu inapofika kipindi cha Novemba mpaka Januari halafu na wachezaji nao wanapata mawazo tofauti kwamba kama wasipocheza basi wanaweza kuondoka ikifika Januari hiyo inawapunguzia kujituma. Wenger amesema ukiwa kama mchezaji hata kama hujapangwa kucheza lakini unatakiwa kujituma kwa klabu husika katika maisha yako yote na kupigania nafasi yako katika kikosi cha kwanza.
Saturday, January 14, 2012
AVB AFURAHISHWA NA UJIO WA ESSIEN.
KIUNGO wa timu ya Chelsea jana alicheza mchezo wake wa kwanza wakati timu yake iliposhinda mchezo dhidi ya Sunderland kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya siku 273 za kuuguza majeraha. Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amesema wakati akihojiwa na waandishi wa habari kabla ya mchezo huo kuwa anawapongeza madaktari waliokuwa wakimuuguza mchezaji huyo kwani kurejea kwake uwanjani mwezi mmoja kabla ni jambo la kushangaza. Kiungo huyo wa Kimataifa wa Ghana aliingia katika dakika ya 73 akichukua nafasi ya Frank Lampard na kwa muda mfupi alioingia alibadilisha mchezo juhudi ambazo zilizaa matunda dakika chache baadae. Essien mwenye umri wa miaka 29 aliumia mwanzoni mwa msimu wa ligi majeraha ambayo yamemuweka nje ya dimba kwa muda miezi sita na hatakuwa sehemu ya kikosi cha Ghana kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya makubaliano kwamba lazima apone kabisa ili atumike katika majukumu ya kimataifa.
Subscribe to:
Posts (Atom)