![]() |
| Makao Makuu, FIFA |
Tuesday, March 6, 2012
BLATTER NAE AOMBA RADHI SERIKALI YA BRAZIL.
GAMBIA YAONYWA NA FIFA.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limeionya nchi ya Gambia baada ya serikali ya nchi hiyo kutengua uongozi wa soka kufuatia timu hiyo kufungwa katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Katika taarifa yake FIFA imesema kuwa haitafanya kazi na uongozi mpya ambao umewekwa na Wizara ya Vijana na Michezo ya nchi hiyo. FIFA imewataka viongozi walioenguliwa na wizara hiyo kuwasilisha maelezo yao ifikapo Alhamisi kabla ya kuamua kupeleka suala hilo katika Kamati ya Dharura ya FIFA ambayo inasimamiwa na rais wa Shirikisho hilo Sepp Blatter. Jopo linaloongozwa na Blatter lina uwezo wa kuifungia nchi kushiriki katika mashindano yoyote duniani kama serikali husika itaonekana kuingilia masuala ya uongozi wa michezo. Wizara ya Vijana na Michezo ya nchi hiyo iliwatimua viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo-GFA Ijumaa iliyopita baada ya timu ya taifa kufungwa na Algeria kwa mabao 2-1 katika mchezo ambao timu hiyo ilikuwa nyumbani.
ARSENAL YAFA KIUME.
TIMU ya AC Milan imefanikiwa kutinga hatua robo fainali ya michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya pamoja na kufungwa na Arsenal katika mchezo wa pili wa michuano hiyo kwa mabao 3-0. Katika mchezo wa kwanza AC Milan wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani wa San Siro walifanikiwa kuwafunga Arsenal mabao 4-0 hivyo kufanikiwa kuingia katika hatua hiyo kwa idadi ya mabao 4-3. Mabao ya Arsenal katika mchezo huo yalifungwa katika kipindi cha kwanza na Laurent Koscielny kwa kichwa, Tomas Rosicky akitumia vyema makosa ya mabeki wa Milan na Robin van Persie aliyefunga bao la tatu kwa nia ya penati baada ya mshambuliaji Alex Oxlade-Chamberlain kuangushwa katika eneo la hatari. Mchezo mwingine uliochezwa jana ulishuhudia Benfica wakisonga mbele baada ya kufanikiwa kuwafunga Zenit St Petersburg kwa mabao 2-0 na kuifanya timu hiyo kuingia robo fainali kwa idadi ya mabao 4-3. Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo ambapo mabingwa watetezi wa michuano hiyo Barcelona watajitupa uwanjani kupambana na Bayer Leverkusen katika Uwanja Camp Nou ambapo katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Ujerumani Barcelona walishinda mabao 3-1. Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Apoel Nicosla ambao wataikaribisha Lyon ambao katika mchezo wa kwanza walifanikiwa kushinda bao 1-0.
VALCKE AOMBA RADHI SERIKALI YA BRAZIL KWA KAULI YAKE.
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Jerome Valcke ameiomba msamaha Brazil Jumatatu baada ya serikali ya nchi hiyo kulifahamisha shirikisho hilo kuwa ahwahitaji kufanya kazi na katibu huyo kufuatia kauli yake kuhusu maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Katika taarifa yake aliyoituma kwa Waziri wa Michezo wa Brazil Aldo Rebelo, Valcke amesema kauli yake ambayo ilitafsiriwa kutoka lugha ya kifaransa kwenda kireno imekuwa na maneno makali zaidi ya alivyosema. Msamaha huo umekuja baada ya Brazil kuandika barua iliyosainiwa na Rebelo kwenda kwa rais wa FIFA Sepp Blatter kuwa nchi hiyo haihitaji kufanya kazi na Valcke. Valcke aliomba msamaha kwa Rebelo na wengine wote ambao kwa namna moja au nyingine walichukizwa na kauli yake lakini alijitetea kuwa maneno hayo yamekuwa makali zaidi yalipotafsiriwa kwa kireno kuliko yale halisi aliyozungumza kwa kifaransa.
WENGER KUTUMIA WASHAMBULIAJI WENGI ZAIDI KUIKABILI AC MILAN.
MENEJA wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger anaweza kubadilisha mfumo wakati timu hiyo itapoikaribisha AC Milan katika mchezo wa michuano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya leo jioni. Timu hiyo italazimika kuifunga Milan si ya mabao manne au zaidi ili waweze kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika uwanja San Siro nchini Italia. Kocha huyo amesema anakabiliwa na upungufu mkubwa katika safu ya kiungo baada wengine kuwa majeruhi kitendo ambacho kitamlazimisha kutumia washambuliaji wengi zaidi katika mchezo huo. Kocha huyo aliongeza kuwa kwasasa ana viungo wawili ambao ni Alex Song na Tomas Rosicky lakini ana washambuliaji sita ambao atawatumia ambao ni Oxlade-Chamberlain, Marouane Chamakh, Chu-Young Park, Robin van Persie, Gervinho na Theo Walcott kitendo ambacho kitakuwa ni hatari kwa timu hiyo lakini amesema hana jinsi.
BERLUSCONI BADO AMMEZEA MATE RONALDO.
RAIS wa klabu ya AC Milan ya Italia Silvio Berlusconi amekiri kuwa ana nia ya kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo kama bei ya kuuzwa mchezaji huyo itakuwa ya kuridhisha. Berlusconi ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo amekuwa akimfuatilia mashambuliaji huyo na hii sio mara ya kwanza kudai kuwa atamkaribisha mreno huyo katika Uwanja wa San Siro kwa mikono miwili. Kauli ya Berlusconi imekuja wakati akihojiwa na luninga moja nchini kwake ambapo pia mbali na kumkubali Ronaldo kutua klabuni kwake aliondoa mawazo ya kuwasajili mshambuliaji wa Arsenal Robin van Persie na Carlos Tevez wa Manchester City mwishoni mwa msimu huu. Kiongozi huyo wa Italia wa zamani ambaye ana umri wa miaka 75 sasa pia alimsifia mshambuliaji wa klabu hiyo Zlatan Ibrahimovic na kudai kuwa anaamini mshambuliaji huyo anafaa kushindania tuzo ya mchezaji bora wa dunia.
FIFA KUSOGEZA MBELE MECHI ZA KIRAFIKI ZA KIMATAIFA.
SHIRIKISHO la Soka duniani-FIFA linataka kuondoa michezo ya kimataifa ya kirafiki ambayo huchezwa Februari na Agosti kitendo ambacho kinaonekana ni kama kuziridhisha klabu za Ulaya. FIFA tayari imeshatangaza mapendekezo ya kalenda hiyo kwa mwaka 2015-2018 ingawa mpaka sasa hakuna tarehe maalumu iliyotajwa kwa ajili ya michezo hiyo. Kalenda iliyopendekezwa itazihitaji timu za taifa kucheza michezo miwili kila moja mwezi Machi, Septemba, Octoba na Novemba ukiongeza na June katika miaka ambayo haigawanyiki. Kama kalenda hiyo ikipitishwa bara la Amerika Kaskazini, Kati pamoja na nchi za Caribbean zinaweza kulazimika kufanya mabadiliko ya michezo yao ya kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2018.
Subscribe to:
Posts (Atom)






