Tuesday, October 2, 2012
MESSI HASTAHILI KUSHINDA TUZO YA BALLON D'OR - IBRAHIMOVIC.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Sweden na klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Zlatan Ibrahimovic amesema kuwa hadhani kama nyota wa Barcelona Lionel Messi anastahili kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia maarufu kama Ballon d’Or kwa mwaka huu. Ibrahimovic anafikiri kuwa nyota huyo wa kimataifa kutoka Argentina alikuwa na msimu mzuri binafsi lakini kaongeza kuwa hakuweza kushinda taji lolote linaloweza kumfanya atunukiwe tuzo ya mchezaji bora wa dunia. Nyota huyo aliendelea kusema kuwa Messi tayari ameshinda tuzo hiyo mara tatu na kama ikiendelea hivyo itakuwa vigumu kwa mchezaji mwingine kushinda tuzo hiyo ndiyo maana anadhani muda wa mchezaji mwingine kushinda tuzo hiyo umefika. Mapema wiki hii Messi aliweka wazi kuwa hatilii maanani suala la yeye kushinda tuzo bali anachofikiria ni jinsi ya kuisaidia klabu ya yake kushinda mataji zaidi.
MOURINHO APANGA KUREJEA UINGEREZA.
MENEJA wa klabu ya Real Madrid ya Hispania, Jose Mourinho amesema kuwa atarejea Uingereza pindi mkataba wake na klabu hiyo utakapomalizika lakini amesisitiza kuwa ana furaha kuwepo Madrid. Wakati mkataba wa Mourinho ambaye pia amewahi kuinoa Chelsea unaisha mwaka 2016 anafikiri kuwa mkataba mwingine baada ya huo utakuwa katika timu ya Ligi kuu nchini Uingereza. Akihojiwa na kituo cha luninga cha nchini Marekani cha CNN, Mourinho amesema kuwa yeye huwa anapenda kuwa muwazi na kwasababu nyingi alizonazo ataelekea Uingereza baada ya mkataba wake Madrid kumalizika. Mourinho alijiunga Madrid akitokea Inter Milan mwaka 2010 baada kuiwezesha klabu hiyo ya Italia kunyakuwa taji lake la tatu la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
SERENA, VENUS KUZURU NIGERIA.
WANADADA nyota wa kimataifa wa mchezo wa tenisi kutoka Marekani, Serena na Venus Williams wanatarajiwa kufanya ziara barani Afrika katika jiji la Lagos, Nigeria kuanzia Octoba 30 mpaka Novemba 2 mwaka huu. Ziara ya nyota hao ambao ni ndugu ni sehemu ya kampeni ya mpango wa uwezeshwaji kwa wanawake nchini humo mpango ambao tayari umefanikiwa na kuungwa mkono kimataifa. Kama wanavyofanya Marekani na sehemu zingine duniani wakati watakapokuwa Lagos nyota hao wanatarajiwa kuvutia, kuhamasisha na kutoa ushauru kwa mapama katika chakula cha jioni, kliniki na mechi za maonyesha ambazo zitakuwa zimeandaliwa kwa ajili ya ziara wanadada hao. Ziara ya wanadada hao inatarajiwa kuongeza chachu juu ya jukumu ushiriki wa wanawake katika kuhimiza, kuhamasisha na kutoa mitizamo yao katika maendeleo barani Afrika. Pia hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa wanadada hao kuchuana wenyewe kwa wenyewe katika tenisi kwenye ardhi ya Afrika.
NCHI TANO ZATUMA MAOMBI KUSHIRIKI CHALENJI.
NCHI tano wakiwemo mabingwa wa soka Afrika, Zambia zimetuma maombi ya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji ambayo inaandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. Mbali ya Zambia nchi nyingine ambazo zimetuma maombi hayo ni pamoja na Cameroon, Malawi, Zimbabwe na Ivory Coast ambapo kwa mwaka huu michuano hiyo imepangwa kufanyika jijini Kampala, Uganda kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 8. Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alithibisha kutumwa kwa maombi hayo lakini amesema kuwa uamuzi utatolewa katika kikao cha bodi watakachokutana baada ya mechi za mzunguko wa mwisho wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013. Katika michuano ya mwaka jana iliyofanyika jijini Dar es Salaam, nchi za Malawi na Zimbabwe ndio zilikuwa timu ngeni katika ukanda huu zilizopewa mwaliko na CECAFA. Musonye aliomba nchi wanachama wa CECAFA kuthibitisha ushiriki wao wa michuano hiyo mpaka ifikapo Octoba 8 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya ratiba kamili kupangwa Novemba 8 mwaka huu jijini Kampala.
Monday, October 1, 2012
CHELSEA YAENDA SWEDEN KUSAKA USHINDI WA KWANZA CHAMPIONS LEAGUE.
MABINGWA wa soka barani Ulaya Chelsea ya Uingereza imesafiri kuelekea nchini Sweden kuifuata timu ya Nordsjaelland katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Meneja wa Chelsea Roberto di Matteo aakuwa akisaka ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kutoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Juventus katika mchezo wa kwanza wa kundi E uliochezwa katika Uwanja wa Stamford Bridge wiki mbili zilizopita. Mbali na mchezo huo pia kutakuwepo na michezo mingine ambapo Juventus nao wataikaribisha Shaktar Donetsk, Spartak Moscow watakuwa wenyeji wa Celtic, Valencia watapambana na Lille huku Benfica wakiwakaribisha mabingwa wa zamani wa michuano hiyo Barcelona. Michezo mingine ya kesho Galatasaray itakuwa mwenyeji wa Braga, huku BATE wakiwakaribisha Bayern Munich wakati CFR Cluj nao watawakaribisha Manchester United.
NYAMILANDU ANUSURIKA KATIKA AJALI.
RAIS wa Chama cha Soka nchini Malawi-FAW, Walter Nyamilandu amenusurika katika ajali mbaya ya gari ambayo imewaua mchumba wake mtarajiwa Maria Inglis na shangazi yake ajali ambayo ilitokea Juzi. Nyamilandu ambaye alitibiwa na kuruhusiwa katika hospitali ya wilaya ya Balaka nchini humo alikuwa akiendesha gari aina na Nissan Pathfinder akitokea Blantyre kuelekea Lilongwe. Ajali hiyo ilimkuta katika eneo la Phalula ambapo gari hilo lilipinduka ambapo taarifa za kwanza za polisi zinasema kuwa alikuwa akijaribu kulikwepa roli ambalo inaonekana lilikuwa limekosa mwelekeo. Katika ajali hiyo watoto wawili wa Nyamilandu nao pia walitoka salama, ambapo sasa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kugundua haswa chanzo cha ajali hiyo ambaya.
ETO'O AREJEA KUIOKOA CAMEROON.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o amerejea rasmi katika katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo. Eto’o ambaye katika kipindi cha karibuni alitangaza kupumzika kuitumikia Cameroon alithibitisha kubatilisha uamuzi wake huo hivyo hiyo inamaanisha kuwa mchezaji ambaye ndiye anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani kwasasa atakuwepo katika mchezo wa kufuzu mataifa ya Afrika dhidi ya Cape Verde mchezo ambao utapigwa jijini Younde Octoba 14 mwaka huu. Mcheaji ambaye amewahi kunyakuwa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara nne amesema kuwa katika kipindi cha karibuni amekuwa akipokea wageni ambao ni maofisa wa soka nchini kwake kuzungumzia masuala ya soka la nchi hiyo hususani mustakabali wa timu ya taifa. Eto’o amesema mbali na viongozi hao wa soka lakini pia rais wan chi hiyo na Waziri Mkuu nao pia walimfuata kuzungumzia suala hilo na kupelekea kubadilisha mawazo na kurejea katika kikosi hicho ili kujaribu kunusuru soka la nchi ambalo katika kipindi cha karibuni limekuwa kama halina muelekeo. Kocha mpya wa kikosi hicho Jean Paul Akono aliweka wazi toka akipewa kibarua hicho kuwa lazima awajumuishe Eto’o na beki wa kushoto wa timu ya Tottenham Hotspurs Benoit Assou Ekotto katika kikosi chake ambapo kitakuwa kikisaka ushindi baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0.
Subscribe to:
Posts (Atom)






