Wednesday, October 2, 2013

WENGER AMPA TANO OZIL.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amempongeza kiungo mahiri Mesut Ozil kwa kiwango alichokionyesha na kufunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Napoli ya Italia. Katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ozil alifunga bao la kuongoza katika dakika ya nane ya mchezo kabla ya kutengeneza bao lingine lililofungwa na Oliver Giroud dakika saba baadae. Wenger ambaye kikosi chake kimeshinda michezo 10 mfululizo mpaka sasa alifurahishwa na kiwango cha nyota wake walichokionyesha katika mchezo huo huku akimsifu Ozil kwa kuonyesha thamani yake. Wenger amesema nyota huyo ameongeza ari katika kikosi chake na kuwafanya wachezaji wenzake kujiamini zaidi kitu ambacho ni kizuri.

Tuesday, October 1, 2013

NILIKUWA NAHOFU SUAREZ KUONDOKA - GERRARD.

NAHODHA wa klabu ya Liverpool, Steven Gerrard amesema alikuwa na hofu mshambuliaji nyota wa timu hiyo Luis Suarez angeondoka katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi. Suarez mwenye umri wa miaka 26 aliomba kuondoka Anfield na alikuwa akihusishwa kwenda katika vilabu vya Arsenal na Real Madrid. Gerrard amesema timu inapokuwa na mchezaji mzuri kama Suarez ni wazi kuwa vilabu mbalimbali vitakuwa vikimuwinda ndio maana alikuwa na hofu ya nyota huyo kuondoka. Suarez alirejea uwanjani katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Manchester United baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kufungiwa mechi 10 kwa kumuuma mkono Branislav Ivanovic.

BENCHI LAMSUMBUA GOTZE.

MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Mario Gotze amekiri kuwa anazidi kuchanganyikiwa kuhusiana na suala la kukaa nje ya uwanja na ana hamu kubwa ya kurejea tena katika kiwango chake. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umriwa miaka 21 amecheza mechi tatu pekee akiwa na Bayern toka ajiunge nao akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya euro milioni 37 na amekuwa nje ya uwanja toka Agosti baada ya kupata majeruhi katika mchezo Supercup dhidi ya Chelsea. Gotze amesema sio jambo rahisi kuendelea kuvumilia kwasababu kila mchezaji anapenda kucheza kila dakika na kila mchezo. Nyota aliendelea kusema kuwa hilo haliwezi kumkatisha tamaa kwasababu atapambana kuhakikisha anakuwa na namba ya kudumu katika kikosi hicho kinachonolewa na Pep Guardiola.

KAGAWA AKIRI KUSHUKA KIWANGO.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Manchester United, Shinji Kagawa amebainisha kuwa anatakiwa kuimarisha kiwango chake la sivyo atashindwa kudumu katika timu hiyo yenye maskani yake Old Traford. Nyota huyo wa kimataifa wa Japan alifanikiwa kuanza katika kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya West Bromwich Albion Jumamosi iliyopita lakini alitolewa katika kipindi cha mapumziko. Kagawa amepangwa mara nne pekee katika kikosi cha Moyes msimu huu na amekiri kwamba anatakiwa kujiimarisha kama anataka kubakia hapo. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 amesema anajua bado ana safari ndefu ya kuhakikisha anakuwa na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza lakini haweza kukata tama kuhakikisha anafikia malengo yake.

DERBY COUNTY YAMNASA MACCLAREN.

KLABU ya Derby County imemtaja kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Steve McClaren kuwa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miaka miwili. McClaren anachukua mikoba ya Nigel Clough ambaye alitimuliwa Jumamosi iliyopita baada ya timu hiyo kupata kipigo kutoka kwa Nottingham Forest. Akihojiwa kuhusiana na hilo ofisa mkuu wa Derby Sam Rush amesema walifikia uamuzi wa kumpa kibarua McClaren kutokana na uzoefu wake na wana imani kuwa atawapeleka mbali. Hata hivyo pamoja na uteuzi huo MacClaren kwenye miaka 52 hatakuwepo katika benchi la ufundi katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Ipswich utakaochezwa leo badala yake atakuwepo meneja wa muda Darren Wassall.

LENNON MENO NJE.

MENEJA wa klabu ya Celtic ya Scotland, Neil Lennon ameonyesha kutofurahishwa sana na kukosekana kwa Lionel Messi katika kikosi cha Barcelona ambacho watacheza nacho baadae jijini Glasgow. Messi ambaye anashikilia taji la mchezaji bora wa dunia atakosa mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kundi H kutokana na majeruhi ya msuli yanayomsumbua. Akihojiwa kuhusiana na mechi hiyo Lennon amesema kwa maoni yake kukosekana kwa Messi ni habari njema kwao lakini kwa upande mwingine inasikitisha kwasababu huwa ni vyema kuwaona wachezaji bora wa dunia wakicheza jijini Glasgow. Messi alikuwepo katika kikosi cha Barcelona kilichofungwa katika Uwanja wa Celtic Park katika hatua ya makundi msimu uliopita lakini hii itakuwa ni mara ya kwanza Neymar kucheza dhidi ya mabigwa hao wa Scotland.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

RUFANI KAMATI YA MAADILI MWISHO OKT 2
Wakati walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakiwa wameshapokea uamuzi dhidi yao kwa maandishi, mwisho wa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili ni kesho (Oktoba 2 mwaka huu). Walalamikiwa wote saba waliohudhuriwa mashauli dhidi yao; Kamwanga Tambwe, Nazarius Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih Dauda na Wilfred Kidao wamepokea uamuzi wa Kamati hiyo inayoongozwa na Jessie Mnguto. Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili, kwa ambao hawakuridhika na uamuzi huo wanatakiwa kukata rufani Kamati ya Rufani ya Maadili inayoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika kesho. Rufani ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni. Kwa mujibu wa Kanuni ya 74 (1) na (2) ya Kanuni za Maadili, rufani zikionesha sababu za kufanya hivyo zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku tatu kwa njia ya posta (registered post or dispatch or courier service) kwa Sekretarieti. Vilevile inatakiwa rufani inatakiwa kuambatanishwa risiti ya malipo ya ada ya rufani. Ada ya rufani ni sh. milioni moja.



MECHI ZA YANGA, SIMBA ZAINGIZA MIL 182/-
Mechi za Yanga na Simba za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zilizochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam zimeingiza jumla ya sh. 182,103,000. Yanga katika mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 imeingiza sh. 94,202,000. Watazamaji 16,492 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 22,630,921.58. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000, na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,369,796.61. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,507,248.26, tiketi sh. 3,117,215, gharama za mechi sh. 6,904,348.96, Kamati ya Ligi sh. 6,904,348.96, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,452,174.48 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,685,024.59. Nayo Simba ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 87,901,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 41 walikuwa 15,780. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 21,051,025.92 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 13,408,627.12. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 10,703,911.48, tiketi sh. 3,132,963, gharama za mechi sh. 6,422,346.89, Kamati ya Ligi sh. 6,422,346.89, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,211,173.44, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,248,789.67 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 1,248,789.67. Wakati huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya Mbeya City na Coastal Union iliyochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya imeingiza sh. 16,959,000 huku kila klabu ikipata sh. 4,035,229. Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 2,586,966, uwanja sh. 2,051,811.57, tiketi sh. 696,290, gharama za mechi sh. 1,231,086, Kamati ya Ligi sh. 1,231,086, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 615,543, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) sh. 478,756.



MICHUANO YA CHALENJI KUANZA NOV 27
Michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inafanyika Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu. Nchi wanachama ambazo zinataka kushiriki zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa Sekretarieti ya CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu. Wanachama wa CECAFA ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zanzibar. Michuano hiyo itatanguliwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA utakaofanyika Novemba 26 mwaka huu ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya uchaguzi. Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Wajumbe wanaomaliza muda wao ni Sahilu Gebremarian wa Ethiopia ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CECAFA, Abdigaani Saed Arab (Somalia), Tariq Atta (Sudan) na Raoul Gisanura (Rwanda). Majina ya wagombea yanatakiwa kuwa yamewasilishwa katika Sekretarieti ya CECAFA kabla ya Oktoba 20 mwaka huu, na yakiwa yamethibitishwa na vyama vyao vya mpira wa miguu.



SUALA LA PAPIC, YANGA LASUBIRI UAMUZI WA FIFA
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limewasilisha rasmi suala la madai ya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Kostadin Papic dhidi ya klabu hiyo katika Kamati ya Hadhi ya Wachezaji. FIFA imesema imepeleka rasmi suala hilo katika kamati yake hiyo baada ya kupokea vielelezo vya Papic anayedai kuidai Yanga dola 10,000 za Marekani pamoja na vile vya Yanga inayodai kumlipa kocha huyo fedha zote alizokuwa akiidai klabu hiyo. Kwa taratibu za FIFA, hivi sasa haitapokea vielelezo vingine kutoka pande hizo mbili, na badala yake Kamati hiyo inayoongozwa na Theo Zwanziger kutoka Ujerumani itafanya uamuzi na kuziarifu pande husika. Zwanziger kitaaluma ni mwanasheria. Papic aliyeinoa Yanga kwa vipindi viwili tofauti aliwasilisha malalamiko yake FIFA akidai hadi mkataba wake unamalizika klabu hiyo ilikuwa haijamlipa dola 10,000 za Marekani.



LIPULI, MAJIMAJI KUUMANA WAMBI FDL
Mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Lipuli ya Iringa na Majimaji ya Songea sasa itachezwa kesho (Oktoba 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Wambi uliopo Mafinga badala ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa. Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora kwa ajili ya shughuli za mbio za Mwenge. Mechi nyingine ya FDL kesho itakuwa kati ya Tessema FC ya Dar es Salaam na Ndanda FC ya Mtwara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.