Monday, February 3, 2014

GUARDIOLA AKISIFU KIKOSI CHAKE KWA KUCHEZA KWA KIWANGO BORA DHIDI YA FRANKFURT.

MENEJA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola anafikiri kuwa ushindi wa mabao 5-0 iliyopata timu yake dhidi ya Eintracht Frankfurt katika mchezo wa Bundesliga ndio waliocheza kwa kiwango cha juu kabisa msimu huu.Mabao yaliyofunga na Mario Gotze na Franck Ribery yaliisaidia Bayern kuongoza kwa mabao mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya Arjen Robben, Dante na Mario Mandzukic kuongeza mengine katika kipindi cha pili. Akihojiwa Guardiola amesema wamecheza katika kiwango bora kabisa kuliko mechi yoyote msimu huu na ameridhishwa kutokana na hatua hiyo kubwa waliyopiga. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa katika mchezo huo walifanikiwa kumiliki mpira katika vipindi vyote viwili na kufanikiwa kuwaweka washambuliaji wao katika maeneo ya hatari. Bayern kwasasa wanaongoza katika msimamo Bundesliga wakiwa ana alama 13 zaidi ya Bayer Leverkusen wanaoshika nafasi ya pili.

NEYMAR AMTETEA BABA YAKE KUHUSU SAKATA LA UHAMISHO WAKE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar amemtetea baba yake kuhusiana na sakata la uhamisho wake kutoka Santos kwenda Barcelona. Kampuni ya N&N ambayo inamilikiwa na wazazi wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 ilipokea kiasi cha euro milioni 10 mwaka 2011 ili kuhakikisha kuwa Neymar haondoki Santos kwenda katika klabu yoyote ila Barcelona. Malipo hayo ni sehemu ya euro milioni 40 ambazo Barcelona ililipa kwa ujumla ili kuhakikisha wanapewa nafasi ya kwanza kama ukifanyika uhamisho wowote. Neymar alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba hawezi kunyamaza kimya na kuacha watu waseme vibaya kuhusu familia yake wakati hawajafanya lolote baya. Nyota huyo amesema alikaa kimya kipindi kirefu kwasababu baba yake alimwambia afanye hivyo nay eye anashughulikia tatizo hilo lakini ameshindwa baada ya kuona tuhuma dhidi ya familia yake zinazidi. Kwasasa yuko benchi akikiuguza kifundo cha mguu.

TFF YAADHIMISHA MIAKA 50 FIFA.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaadhimisha miaka 50 tangu lipate uanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (TFF) kwa shughuli mbalimbili ikiwemo michezo na makongamano. Kamati maalumu itaundwa kwa ajili ya kupanga na kuratibu shughuli hiyo ambayo TFF imepanga kuadhimisha nchini nzima kwa kutumia wanachama wake. TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) ilijiunga na FIFA Oktoba 8, 1964.



PAMBANO LA YANGA, MBEYA CITY LAINGIZA MIL 175
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Yanga na Mbeya City lililofanyika jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 175,285,000. Watazamaji 30,411 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Yanga ndiyo iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0. Mgawanyo wa mapato ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 26,738,389.83, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,919,200 wakati kila klabu ilipata sh. 42,960,086.50. Uwanja sh. 21,844,111.53, gharama za mechi sh. 13,106,466.92, Bodi ya Ligi sh. 13,106,466.92, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 6,553,233.46 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 5,096,959.36. Nayo mechi ya Simba na Oljoro JKT iliyochezwa Februari 1 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 47,705,000 ambapo kila timu imepata sh. 11,254,122 kutokana na watazamaji 8,267. Mgawanyo mwingine katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Simba kushinda mabao 4-0 ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 7,277,033.90 na gharama za kuchapa tiketi sh. 2,278,400. Uwanja sh. 5,722,434.92, gharama za mechi sh. 3,433,460.95, Bodi ya Ligi sh. 3,433,460.95, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,716,730.47 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,335,234.81.



TFF YAPATA HATI YA KIWANJA TANGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepata hati ya kiwanja chake kilichopo eneo la Mnyanjani katika Jiji la Tanga. Hati hiyo ya miaka 99 ya kiwanja hicho namba 75 Block D chenye ukubwa wa ekari 7.6 ilikabidhiwa kwa TFF, Januari 13 mwaka huu. Kiwanja hicho kitaendelezwa kwa matumizi mbalimbali, kubwa ikiwa ni uwanja wa mpira wa miguu.

Sunday, February 2, 2014

DRAXLER ATUHUMU UONGOZI WA SCHALKE KUMNYIMA KWENDA ARSENAL.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Schalke, Julian Draxler ameishutumu timu yake hiyo kwa kuzuia uhamisho wake kwenda Arsenal katika dirisha dogo la usajili lililofungwa juzi. Maofisa wa Arsenal walisafiri kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya kujadili ofa ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 lakini walishindwa kufikia dau la paundi milioni 37.2 walizotaka Schalke. Draxler amesema anajua kuna vilabu vingi vimekuwa vikimhitaji katika kipindi cha Januari na anajisikia vyema ingawa mtendaji mkuu wa klabu hiyo Horst Heldt alikataa ofa hizo bila kumshirikisha. Heldt akihojiwa kuhusiana na hilo amesema ni kweli walipata ofa nyingi kwa ajili ya nyota huyo lakini walishindwa kumuuza kwasababu ya kukosa mbadala wake.

MAN CITY WANA UDHAIFU KATIKA MECHI ZA UGENINI - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa kiwango cha Manchester City katika mechi za ugenini kinaweza kuwagharimu pamoja na kupewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji la Ligi Kuu nchini Uingereza. Kauli ya Wenger imekuja kufuatia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Southampton ambaye imewafanya kuteleza mpaka nafasi ya pili katika msimamo na kupitwa na City walioifunga Tottenham Hotspurs kwa mabao 5-1 katika Uwanja wa White Hart Lane. Lakini kocha huyo amesisitiza kuwa kikosi chake kinaweza kurejea kileleni kwa kudai kuwa City bado wanakabiliwa na ratiba ngumu zikiwemo mechi za ugenini dhidi ya Manchester United, Liverpool na Everton. Wenger amesema hakuna shaka kwamba City ndio timu bora kwasasa na hapingi uwezo wao pamoja na wachezaji bora walionao lakini wana udhaifu katika mechi za ugenini kwasababu mpaka sasa wameshapoteza mechi nne.

PAMOJA NA KUANDAMWA NA SARE SEEDORF ADAI MILAN INAIMARIKA.

MENEJA wa klabu ya AC Milan, Clerence Seedorf amedai kuwa klabu hiyo inaendelea kuimarika pamoja na kupata sare ya kufungana mabao 1-1 na Torino katika mchezo wa Serie A uliofanyika jana. Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa San Siro wageni Torino ndio walioanza kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Ciro Immobile lakini wenyeji walirudisha bao hilo katika kipindi cha pili kupitia kwa Adil Rami. Sare hiyo inaonekana kumfurahisha Seedorf ambaye anadai kuwa wachezaji wake wameanza kuzoea mfumo anaofundisha. Seedorf amesema ni jambo jema kuona kikosi chake kikianza kuelewana taratibu na kudai kuwa ni dalili nzuri za kufanya vyema huko mbele. Sare hiyo imeiacha Milan katika nafasi ya tisa ya Serie A, wakiwa wanajikongoja toka alipotimuliwa kocha Massimiliano Allegri Januari mwaka huu.

LIBYA MABINGWA WAPYA CHANA.

TIMU ya taifa ya Libya wametawadhwa mabingwa wapya wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN baada ya kuifunga Ghana kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Cape Town nchini Afrika Kusini. Libya walinyakuwa taji lao hilo la kwanza la kihistoria kwa kuigaragaza Ghana kwa penati 4-3 baada ya mchezo huo kumalizika bila ya kufungana mpaka katika muda wa nyongeza. Hiyo inakuwa mechi ya tatu kwa Libya kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kuziengua Gabon na Zimbabwe katika hatua ya robo fainali na nusu fainali. Kwa wa mechi ya kutafuta mshindi wa tatu Nigeria walifanikiwa kuibuka kidedea baada ya kuifunga Zimbabwe kwa bao 1-0.