Friday, March 7, 2014

BILIONEA WA KLABU YA BIRMINGHAM AHUKUMIWA JELA MIAKA SITA.

MMILIKI wa klabu ya Birmingham City Carson Yeung amehukumiwa jela miaka sita na mahakama ya Hong Kong baada ya kukutwa na hatia ya kutakatisha fedha chafu. Yeung mwenye umri wa miaka 54 alihukumiwa Jumatatu kwa makosa matano yanayohusu paundi milioni 55 zilizopitia katika akaunti yake kati ya mwaka 2001 hadi 2007. Bilionea huyo alishitakiwa mwaka 2011 ikiwa ni miaka miwili toka ainunue Birmingham. Yeung ambaye ni mtengeneza mitindo ya nywele ameai kuwa amejipatia utajiri wake kupitia biashara ya hisa, kukodisha majumba, saluni za kutengeneza nywele na kamari.

WILSHERE HATI HATI KOMBE LA DUNIA.

KIUNGO wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Arsenal, Jack Wilshere yuko katika hatihati ya kukosa michuano ya Kombe la Dunia kufuatia ya klabu yake kuwa majeraha ya mguu yanayomkabili yanaweza kumuweka nje kwa zaidi ya wiki tisa. Mguu wa kiungo huyo unatarajiwa kupona kwa muda wa wiki sita na klabu yake inategemea inategemea kwamba anaweza kurejea rasmi baada ya wiki tatu au zaidi. Majeruhi hayo yatamfanya Wilshere kukosekana katika kikosi cha Arsenal mpaka wiki ya pili ya mwezi Mei mwaka huu hivyo kukosa mbio za timu kujaribu kukata kiu ya miaka tisa ya kukosa mataji. Kiungo alipata majeraha hayo baada ya kukwatuliwa na beki wa Denmark Daniel Agger katika mchezo wa kirafiki baina ya timu hizo uliochezwa katika Uwanja wa Wembley ambapo Uingereza ilishinda kwa bao 1-0.

Thursday, March 6, 2014

RONALDO AIPIKU REKODI YA PAULETA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo amefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mshambuliaji mwenye mabao mengi zaidi kwa timu ya taifa ya nchi hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1 waliopata dhidi ya Cameroon jana. Ronaldo hivi amefikisha mabao 49 kwa Ureno, mawili zaidi ya aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo Pauleta. Akihojiwa kuhusu rekodi hiyo, Ronaldo amesema hajali sana kuhusu mambo ya kuvunja rekodi kwasababu ni mambo ambayo huja yenyewe kama ukifanya kazi kwa bidii. Katika mchezo huo Ronaldo alifunga mabao yake katika dakika 21 na lingine katika dakika ya 83 huku mengine yakifunga na Raul Meireles dakika ya 65, Fabio Coentrao dakika ya 67 na Edinho dakika ya 77.

AL AHLY YAHAHA KUTAFUTA UWANJA.

KLABU ya Al Ahly ya Misri bado inahaha kutafuta uwanja watakaoutumia kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa barani Afrila dhidi ya Yanga huku zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya mchezo. Vurugu za mashabiki wao katika mechi ya hivi karibuni imepelekea mamlaka ya nchi hiyo kuifungia timu hiyo kucheza mechi zake katika mji mkuu wa Cairo. Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo hivi sasa wanahaha kujaribu kuomba kutumia uwanja uliopo katika mji wa Alexandria kwa ajili ya mchezo huo lakini muda unaonekana kutokuwa upande kutokana na kubaki siku chache. Mashabiki wa Al Ahly waliwaumiza askari 25 mwezi uliopita wakati wa mchezo wa Super Cup walioshinda dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia katika Uwanja wa Taifa uliopo jijini Cairo. Mamlaka nchini humo inasita kuruhusu mechi yoyote kuchezwa na mashabiki baada ya tukio hilo na kuna uwezekano mchezo huo wa Jumapili ukachezwa bila uwepo wa mashabiki. Al Ahly ilitandikwa bao 1-0 na Yanga katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa michuano hiyo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

AWEKA REKODI YA KUFUNGIWA MECHI NYINGI ZAIDI HUKO VIETNAM.

BEKI wa kimataifa wa Vietnam Tran Dinh Dong amepewa adhabu iliyovunja rekodi ya kufungiwa mechi 28 na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kwa kumvunja mguu mchezaji mwenzake kwenye mchezo wa ligi. Dong anayecheza katika timu ya Song Lam Nghe An pia alipigwa faini ya dola 950 kwa kumkwatua na kumvunja Hung Vuong An Giang ambaye anacheza timu ya Nguyen Anh Hung. Dong ambaye hategemewi kurejea uwanjani mwaka huu amesema atakata rufani kupinga adhabu ambayo pia imehusisha kumlipia gharama za matibabu mchezaji aliyemvunja. Naye kocha wa timu ya Dong, Nguyen Huu Thang amesema shirikisho hilo halikutenda haki kwani inaonekana wametoa adhabu hiyo kwa msukumo kutoka kwa watu.

WACHEZAJI WA MADRID MABISHOO - MOURINHO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amewaponda wachezaji wa Real Madrid kuwa anadhani wanajali zaidi muonekano wao kwa watu kuliko kushinda mataji. Mourinho aliondoka Madrid kwenda Chelsea mwaka jana baada ya kukaa Santiago Bernabeu kwa miaka mitatu na kudai alikuwa hafurahishwi na tabia zilizokuwa zikionyeshwa na wachezaji wakati akiwa huko. Kocha huyo amesema mara nyingi wachezaji wa Madrid walikuwa wakijipanga mbele ya kioo kabla ya mchezo wakati mwamuzi akiwasubiria koridoni lakini anadhani ndivyo jamii ya sasa ilivyo kwamba vijana wanajali zaidi mambo hayo. Mourinho amesema ameanza kazi ya ukocha mwaka 2000 na anadhani kipindi cha nyuma wachezaji walikuwa wakipigana kutengeneza fedha wakati wakicheza soka na kuwa matajiri baada ya kuachana na mchezo huo. Lakini hivi sasa watu wanaowazunguka ndio wanajaribu kuwafanya matajiri kabla hata hawajaanza kucheza soka.

Wednesday, March 5, 2014

BARCELONA KUMFANYA MESSI KUWA MCHEZAJI ANAYELIPWA ZAIDI DUNIANI MWISHONI MWA MSIMU.

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amebainisha kuwa Lionel Messi atasaini na kuboresha mkataba mpya mwishoni mwa msimu huu ambao utamfanya kuwa mchezaji anayelipwa vizuri duniani. Klabu hiyo katika siku za karibuni ilidai kuwa inataka kumtunza nyota huyo wa kimataifa wa Argentina kwa ubora wake na sasa wameweka wazi nia yao ya kutaka kumfanya mchezaji huyo amalizie soka lake hapo. Bartomeu amesema nia ya klabu hiyo ni kutaka kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi duniani na majira ya kiangazi jambo hilo litakamilika. Rais huyo amesema kuwa hawana mpango wa kumuuza nyota huyo wako naye na ni mategemeo yao atastaafu soka akiwa Camp Nou.