Tuesday, April 1, 2014

COSTA HATARINI KUIKOSA BERCELONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Costa kuna hati hati ya kukosa mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Barcelona baada ya kuwahi kuondoka mazoezini jana. Kocha wa Atletico Diego Simeone amedai kuwa itakuwa ni jambo gumu kwa Costa kucheza katika mchezo huo wa leo baada ya kufanya mazoezi kwa dakika 10 pekee na kuondoka kutokana na maumivu. Costa amekuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Simeone akiwa amefunga mabao 32 katika mashindano yote msimu huu, yakiwemo mabao sita katika mechi tano zilizopita. Simeone amesema madaktari watamfanyia uchunguzi kama atakuwa fiti lakini hadhani kama atamjumuisha katika kikosi chake.

MOYES AMTAHADHARISHA MWAMUZI JUU YA ROBBEN.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes amemtaka mwamuzi Carlos Carballo wa Hispania kutoa maamuzi sahihi katika mchezo dhidi ya Bayern Munich baada ya Wajerumani hao kulalamikiwa kwa kupenda kujirusha. United itaikabili Bayern Katika Uwanja wa Old Trafford baadae leo katika mchezo wa wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bayern ambao wanafundishwa na Pep Guardiola wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo lakini wamekuwa wakilalamikiwa baada ya kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kumtuhumu Arjen Robben kwa kwa tabia kupenda kujirusha. Akihojiwa kabla ya mchezo huo Moyes amesema wanaamini waamuzi watafanya maamuzi sahihi na suala la kujirusha ni moja ya vitu vigumu kwa mwamuzi kutoa uamuzi sahihi.

ALVES AWASHANGAA WANAOILALAMIKIA BARCELONA KUBEBWA.

BEKI wa klabu ya Barcelona, Dani Alves amedhihaki jinsi timu hiyo isivyopewa nafasi kwasasa na kudai kuwa wakishinda mechi mwamuzi lazima alaumiwe na wakifungwa watu wanadai ufalme wao umekwisha. Mwezi uliopita Barcelona waliteleza na watu kudhani kuwa mbio zao za kutetea ubingwa wa La Liga zilizkuwa zimekwisha lakini walifanikiwa kubadilika na kurejea katika mbio hizo kwa ushindi dhidi ya Real Madrid na Espanyol. Hata hivyo mechi zote mbili walizoshinda zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na maamuzi yaliyotolewa na waamuzi baada ya mechi na Alves anafikiri kuwa hakuna uwezekano tena wa Barcelona kushinda bila kulalamikiwa. Alves amesema tuhuma kwa waamuzi zimekuwa zikiwapa ari kwasababu ni kawaida kwa ushindi wao kuelezewa hivyo ndio maana wamezoea hivi sasa. Barcelona leo itaikaribisha Atletico Madrid katika mchezo wa mkondo wa kwanza war obo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaofanyika katika Uwanja wa Camp Nou.

SIKUPEWA OFA KUINOA UNITED NA FERGUSON - GUARDIOLA.

MENEJA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola ametania kuwa pengine alipewa ofa ya kuinoa Manchester United lakini hana uhakika kutokana na kutofahamu lugha ya kiingereza sawasawa. Mwaka uliopita, kocha huyo wa zamani wa Barcelona ambaye alikaa kwa muda bila kufanya kazi, alikaririwa kutaka kufundisha soka Uingereza. Kocha huyo raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 43 alichukua mikoba ya kuinoa Bayern majira ya kiangazi mwaka jana, lakini alitania pengine Sir Alex Ferguson alimpa ofa ya kuchukua nafasi yake Old Trafford. Guardiola alikutana na Ferguson jijini New York wakati yuko katika likizo yake ya miezi 12 baada ya kuondoka Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2011-2012. Kocha amesema alialikwa na kocha huyo nguli katika mgahawa wa gharama kwa ajili ya chakula cha usiku na alikuwa mpole lakini katika mazungumzo yao kuna sehemu alikuwa hamwelewi kutokana na kutojua lugha ya kiingereza sawasawa.

VURUGU ZAPELEKEA VIONGOZI WA SOKA KUJIUZULU URUGUAY.

BODI nzima ya uongozi wa Chama cha Soka nchini Uruguay imelazimika kujiuzulu kufuatia mgogoro juu ya vurugu zinazotokea katika mechi za soka. Bodi hiyo imedai kuchukua uamuzi huo ili kupisha watu wengine wenye mawazo tofauti kuongoza chama hicho. Wiki iliyopita rais Jose Mujica aliondoa ulinzi wa polisi katika viwanja vya timu za Penarol na Nacional, ambazo ndio zenye mashabiki wengi nchini humo kufuatia vurugu zilizozuka baada ya mechi. Jumatano iliyopita mashabiki wa Nacional walipambana na polisi baada ya timu yao kufungwa huku polisi kadhaa wakiumizwa na mashabiki hao katika mji mkuu wa Montevideo. Pamoja na kukosekana kwa usalama kufuatiwa polisi kuondolewa, chama hicho kiliamuru timu kuendelea kucheza mechi zao za ligi kama kawaida ingawa umoja wa wachezaji ulikataa.

BAYERN YAMNG'ANG'ANIA KROOS.

MWENYEKITI wa klabu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge amesisitiza kuwa Toni Kroos hatajiunga na Manchester United msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 hajasaini mkataba mpya huku ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika Juni mwaka 2015 na David Moyes alipigwa picha akiwa sambamba na wakala wa mchezaji huyo katika safari yake nchini Ujerumani aliyofanya Januari mwaka huu. Mapema mwezi uliopita Kroos alikataa kuondoa uwezekano wa kwenda United lakini Bayern sasa wameweka wazi kuwa kiungo huyo hataruhusiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu. Rummenigge alikaririwa akidai kuwa ana uhakika wa Kroos kuendelea kuvaa jezi ya Bayern kwa kipindi kirefu kijacho.

DURBAN, EDMONTON ZATUMA RASMI MAOMBI YA KUANDAA JUMUIYA YA MADOLA 2022.

MIJI ya Durban na Edmonton amethibitisha rasmi nia yao ya kuandaa michuano ya 22 ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022. Afrika Kusini haijawahi kuandaa michuano hiyo toka ianzishwe, wakati Mji wa Edmonton uliopo nchini Canada wenyewe waliwahi kuandaa mwaka 1978. Rais wa Shirikisho la Michuano ya Jumuiya ya Madola-CGF, Tunku Imran amesema nia iliyoonyeshwa na miji hiyo ni dalili chanya za kukua kwa michuano hiyo. Michuano ya 20 ya Jumuiya ya Madola inatarajiwa kufanyika jijini Glasgow Julai mwaka huu huku ile mwaka 2018 ikitarajiwa kufanyika katika Pwani ya Dhahabu huko Australia.