KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania, Xavi ametangaza kustaafu soka la kimataifa akiwa na umri wa miaka 34. Mchezaji huyo wa Barcelona ameiwakilisha nchi yake kwa rekodi ya mechi 133 na kuisaidia kushinda Kombe la Dunia mwaka 2010, na michuano ya Ulaya mwaka 2008 na 2012. Xavi aliwaambia waandishi wa habari kuwa anajivunia kwa miaka yote aliyoiwakilisha nchi yake kwani wamefanya mengi mazuri. Nyota huyo aliongeza kuwa kwasasa hana miaka 20 tena lakini bado ana morali kama mtoto mdogo. Xavi pia alikuwa mmoja ya wachezaji wa Hispania walioshindwa kuvuka hatua ya mzunguko wa kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Brazil mwaka huu.
Tuesday, August 5, 2014
KOCHA MWANAMAMA WA TIMU YA WANAUME YA CLERMONT APIGWA MECHI YAKE YA KWANZA.
MWANAMAMA Corinne Diacre anayeinoa klabu ya Clermont Foot ya Ufaransa amepoteza mchezo wake wa kwanza akiwa kocha wa timu hiyo kwa kufungwa mabao 2-1 na timu ya Brest. Mechi hiyo ya Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa ilishuhudia kwa mara ya kwanza mwanamke akiisimamia timu ya wanaume kama kocha katika ligi ya Ulaya. Clermont ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Souleymane Sawadogo katika kipindi cha kwanza kabla ya wapinzania kufunga mabao mawili na kuibuka washindi katika kipindi cha pili. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Diacre amesema kufungwa siku zote sio jambo zuri lakini hana chaka kwamba timu yake itafanya vyema msimu huu. Kocha alisherekea miaka 40 ya kuzaliwa kwake jana na alipokea shahada la maua na busu katika shavu kutoka kwa kocha mwenzake wa timu pinzani ya Brest, Alex Dupont kabla ya kuanza kwa mchezo huo. Diacre alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo Juni mwaka huu akichukua nafasi ya mwanamke mwenzake Helena Costa ambaye alijiuzulu kabla ya kucheza mechi hata moja akiituhumu Clermont kwa kushindwa kumheshimu.
EBOLA YALETA BALAA KATIKA SOKA SIERRA LEONE.
CHAMA cha Soka nchini Sierra Leone kimesimamisha shughuli zote za mchezo wa soka nchini humo kutokana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa Ebola. Uamuzi hu umefikiwa baada ya rais wa nchi hiyo, Ernest Bai Koroma wiki iliyopita kutangaza hali ya hatari kiafya katika nchi hiyo. Taarifa hiyo ya hali ya hatari inatarajiwa kudumu kwa miezi mitatu na kuhatarisha nafasi ya timu ya taifa ya nchi hiyo kushiriki hatua ya makundi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco. Sierra Leone walitarajiwa kucheza ugenini dhidi ya Ivory Coast Septemba 5 au 6 kabla ya kuikaribisha nyumbani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC Septemba 10 mwaka huu. Ofisa mmoja wa shirikisho hilo Abu Bakarr Kamara alikaririwa akidai kuwa wanamategemeo Ebola itaweza kudhibitiwa kabla ya mchezo wao dhidi ya RDC na kuweza kucheza katika uwanja wao nyumbani jijini Freetown lakini kama ikishindikana itabidi watafute uwanja huru kwa ajili ya mchezo huo. Sierra Leone ilifuka katika hatua ya makundi ya kufuzu baada ya Shelisheli kujitoa katika mchezo wao wa pili kwa ushauri wa wizara yao ya afya.
FIFA YAMLIMA ADHABU KOCHA WA ZAMANI WA UGIRIKI.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limemfungia mechi nane za kimataifa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ugiriki Fernando Santos baada ya kutolewa nje mwishoni mwa mchezo wa Kombe la Dunia dhidi ya Costa Rica. Katika taarifa yake FIFA imedai kuwa Santos ambaye alitolewa nje mwishoni mwa dakika za nyongeza katika mchezo wa hatua ya mtoano Juni 29 mwaka huu, alikutwa na hatia ya kumzonga mwamuzi. Katika mchezo huo Costa Rica walishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati na kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 aliacha kuifundisha Ugiriki baada ya michuano hiyo iliyomalizika nchini Brazil. Santos ambaye amekuwa akiinoa Ugiriki kwa miaka minne anatarajiw akuitumikia adhabu hiyo wakati atakapata nafasi ya kuinoa timu nyingine ya taifa. FIFA pia imesema kamati yake ya nidhamu imemfungia mechi sita za kimataifa mwalimu wa viungo wa timu ya taifa ya Italia Aldo Esposito baada ya kutolewa nje wakati nchi hiyo ilipotandikwa bao 1-0 na Uruguay katika hatua ya makundi.
GOURCUFF KOCHA MPYA ALGERIA.
KOCHA Mfaransa Christian Gourcuff ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Algeria akichukua nafasi ya Vahid Halilhodzic. Shirikisho la Soka la Algeria lilithibitisha taarifa hiyo huku jukumu la kwanza alilopewa ni kuhakikisha nchi hiyo inafanikiwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani na 2017 pamoja na michuano ya Kombe la Dunia 2018. Kocha huyo wa zamani wa klabu ya Lorient mwenye umri wa miaka 59 pia atafundisha timu A iliyotengenezwa maalumu kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani. Kocha huyo atafanya kazi sambamba na nahodha wa zamani wa Alegria Yazid Mansouri ambaye alicheza chini yake katika timu ya Lorient na sasa ametajwa kama meneja mkuu wan chi hiyo. Halilhodzic ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yugoslavia alichukua mikoba ya kuinoa Algeria mwaka 2011 lakii alikataa kusaini mkataba mpya pamoja na kuivusha nchi hiyo katika hatua ya mtoano kwenye michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Brazil.
VAN GAAL AITAMBIA LIVERPOOL MAREKANI.
KLABU ya Manchester United, imemaliza ziara yao nchini Marekani wakiwa hawajafungwa mchezo hata mmoja baada ya kuwatandika mahasimu wao Ligi Kuu Liverpool kwa mabao 3-1. Mkongwe Steven Gerrard ndio aliyetangulia kuipa Liverpool bao la kuongoza kwa penati lakini Wayne Rooney, Juan Mata na Jesse Lingard walihakikisha wanafunga na kuihakikishia timu yao ushindi. Zaidi ya mashabiki 50,000 walihudhuria mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Sun Life unaotumiwa na timu ya NFL ya Miami Dolphins. Akihojiwa meneja mpya wa United Louis van Gaal amesema ulikuwa mchezo mzuri kwa mashabiki wa Marekani na pia mashabiki wa nyumbani kwakuwa wameifunga Liverpool.
Monday, August 4, 2014
MAKUNDI YA KUFUZU AFCON 2015.
Kundi A: Nigeria, South Africa, Sudan, Rwanda
Kundi B: Mali, Algeria, Ethiopia, Malawi
Kundi C: Burkina Faso, Angola, Gabon, Lesotho
Kundi D: Ivory Coast, Cameroon, DR Congo, Sierra Leone
Kundi E: Ghana, Togo, Guinea, Uganda
Kundi F: Zambia, Cape Verde, Niger, Mozambique
Kundi G: Tunisia, Egypt, Senegal, Botswana
Kundi B: Mali, Algeria, Ethiopia, Malawi
Kundi C: Burkina Faso, Angola, Gabon, Lesotho
Kundi D: Ivory Coast, Cameroon, DR Congo, Sierra Leone
Kundi E: Ghana, Togo, Guinea, Uganda
Kundi F: Zambia, Cape Verde, Niger, Mozambique
Kundi G: Tunisia, Egypt, Senegal, Botswana
Subscribe to:
Posts (Atom)






