Friday, August 8, 2014

DONOVAN ATANGAZA KUSTAAFU MWISHONI MWA MSIMU WA MLS.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Marekani, Landon Donovan ametangaza kustaafu soka mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Soka ya Marekani-MLS. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 32 ndiye mfungaji anayeoongoza kwa mabao katika timu yake ya taifa akiwa amefunga mabao 57 katika mechi 156. Donovan aliwahi kuitumikia Everton kwa kuichezea mechi 22 na kufunga mabao mawili alisajiliwa mara mbili kwa mkopo. Nyota huyo anayecheza timu ya Los Angeles Galaxy aliuambia mtandao wa klabu hiyo kuwa baada ya kufikiri na kupata ushauri kutoka kwa watu wake wa karibu ameamua kuwa mwaka huu ndio utakakuwa wa mwisho kwake. Donovan ameshiriki katika fainali tatu za Kombe la Dunia akiwa na Marekani na pia amekuwa akiitwa katika kikosi cha wachezaji nyota wa MLS mara sita. Msimu wa MLS unatarajiwa kumalizika Octoba mwaka huu.

NASTAHILI KUPEWA NAFASI NYINGINE KAMA DUNGA - MARADONA.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona amependekeza kuwa anastahili kupewa nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya nchi yake kwa mara nyingine hususani baada ya Brazil kuteua Dunga. Dunga ambaye ni kiungo wa zamani wa Brazil, ambaye aliiongoza nchi hiyo akiwa kocha katika Kombe la Dunia mwaka 2010 alipewa tena mikoba ya kufundisha akichukua nafasi ya Luis Felipe Scolari. Maradona ambaye naye alikuwa akiinoa Argentina katika michuano hiyo mwaka 2010 nchini Afrika Kusini amedai kuwa anastahili nafasi kama hiyo aliyopewa Dunga na Brazil. Akihojiwa Maradona amesema kwasasa timu ya taifa ya Argentina haina kocha na yeye aliwahi kuitumikia kama mchezaji hivyo kama Brazil wamemrudisha Dunga haoni kwanini Argentina nao wamuite yeye. Hata hivyo Maradona amesema ana furaha na shughuli zake anazofanya nchini Dubai hivyo hana haja ya kumpigia mtu magoti ili aweze kupata kibarua hicho. Aliyekuwa kocha wa Argentina Alejandro Sabella aliamua kuachia ngazi baada ya kipigo walichopata katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani na sasa kocha wa zamani wa Barcelona Gerardo Martino ndiye anayepewa nafasi ya kuchukua nafasi hiyo.

LIGI YA MABINGWA AFRIKA YAFIKIA PATAMU WIKIENDI HII.

KLABU kongwe nchini Tunisia, CS Sfaxien inamatarajia makubwa ya kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika wakati watakapokuwa wageni wa timu ya Ahly Benghazi ya Libya katika mchezo wa mkondo wa pili wa kundi B utakaochezwa baadae leo. Kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na kocha Philippe Troussier kitajitupa uwanjani huku kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Ahly Benghazi kwa mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa jijini Tunis Mei mwaka huu. Kwasasa Sfaxien wanashikilia nafasi ya pili katika kundi lao nyumba ya E.S Setif na ushindi wowote leo utakuwa umewavusha moja kwa moja katika hatua ya nusu fainali. Mechi nyingine katika kundi B itakayochezwa kesho timu ya Setif kutoka Algeria watawakaribisha Esperance ya Tunisia wakati Jumapili kutakuwa na mechi za kundi A ambapo TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC itachuana na Al Hilal ya Sudan wakati Zamalek ya Misri wataikaribisha AS Vita nayo ya DRC.


LIGI KUU UINGEREZA KUTAMBULISHA SHERIA MPYA.

LIGI Kuu nchini Uingereza inatarajia kutambulisha sheria mpya za jinsi kushughulikia majeruhi ya kichwani toka kuanza kwa msimu wa 2014-2015. Mchezaji anayepata jeraha la kichwa sasa anatakiwa kutolewa uwanjani na daktari wa klabu lazima aamue kama mchezaji anaweza kuendelea na benchi la ufundi. Msimu uliopita Tottenham walishambuliwa kwa kumruhusu golikipa Hugo Lloris kuendelea kucheza baada ya kuzimia katika mchezo dhidi ya Evrton uliomalizika kwa sare ya bila kufungana. Baada ya Lloris kupatiwa matibabu na kuzinduka meneja wa wakati huo Andre Villas Boas alimrudisha uwanjani kumalizia mchezo huo hatua ambayo ililalamikiwa vikali na wataalamu wa magonjwa ya kichwa na ubongo kuwa inaweza kuhatarisha uhai wa mhusika. Baadhi ya wadau akiwemo kocha wa klabu ya Leicester City iliyopanda Ligi Kuu msimu huu wanaamini mabadiliko hayo yatakuwa msaada mkubwa kwa wachezaji.

AZAM, KMKM KUTUPA KARATA ZAO KAGAME LEO.

MICHUANO ya Kombe la Kagame inayoandaliwa na Baraza la Michezo la Afrika Mashariki na Kati-CECAFA inatarajiwa kuanza kutimua vumbi baadae leo jijini Kigali, Rwanda. Jumla timu 14 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo ambayo itafikia kilele chake Agosti 24 huku mechi 34 zilitarajiwa kuchezwa katika viwanja viwili vya Amahoro na Nyamirambo. Wawakilishi wa Tanzania Bara Azam FC watatupa karata yao ya kwanza dhidi ya wenyeji Rayon Sport katika mchezo wa ufunguzi wa kundi A, mchezo ambao utatanguliwa na ule wa wawakilishi wa Zanzibar KMKM watakaomenyana na Atlabara ya Sudan Kusini. Azam itarudi tena uwanjani, Agosti 10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Adamma ya Ethiopia Agosti 16. Azam imechukua nafasi ya Yanga SC iliyoenguliwa na CECAFA kwa kushindwa kuthibitisha kupeleka kikosi cha kwanza.

Tuesday, August 5, 2014

YANGA YAENGULIWA CECAFA, NAFASI YAO YACHUKULIWA NA AZAM.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania-TFF limeiteua klabu ya Azam kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano hiyo baada ya waandaaji wake, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati-CECAFA kuamua kuindoa Yanga iliyokuwa icheze awali. CECAFA imesema baada ya majadiliano na Yanga kupitia TFF, klabu hiyo ilipewa muda hadi jana iwe imetekeleza matakwa ya kikanuni ili iruhusiwe kushiriki michuano hiyo lakini haikufanya hivyo. Yanga iliwasilisha orodha ya wachezaji wengi wa kikosi cha pili kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, jambo ambalo limekatawaliwa na CECAFA kwa vile linakwenda kinyume na kanuni za michuano hiyo. Azam FC ambayo ilishika nafasi ya pili- nyuma ya Yanga katika ligi iliyopita msimu wa 2012/2013 imekubali kushiriki michuano hiyo na inatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Kigali. Msafara wa Azam FC katika michuano hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.

NEYMAR, MESSI WAREJEA BARCELONA BAADA YA LIKIZO ZA KOMBE LA DUNIA.

NYOTA wa klabu ya Barcelona Neymar na Lionel Messi wamerejea mazoezini leo baada ya likizo ndefu ya Kombe la Dunia wakiwa sambamba na Javier Mascherano na Dani Alves. Hatua ya fainali iliyofikiwa na Argentina katika michuano hiyo imesaidiwa kwa kiasi kikubwa na Messi na Mascherano wakati Alves alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kilichimaliza katika nafasi ya nne na sasa kocha mpya Luis Enrique anaweza kuwajumuisha wachezaji hao katika maandalizi ya msimu mpya. Neymar ambaye aliumia mgongo katika mchezo war obo fainali dhidi ya Colombia yeye amerejea lakini hataweza kujiunga na wenzake wakati akiendelea kupona badala yake atakuwa akifanya mazoezi peke yake. Mechi za kirafiki za Barcelona walizocheza mpaka sasa zimekuwa za kusuasua ambapo wameambulia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Recreativo Huelva na sare ya bao 1-1 baada ya wiki tatu za mazoezi. Hata hivyo bado wanakabiliwa na mechi zingine za kujipima nguvu dhidi ya Napoli, HJK na Leon kabla ya kucheza mechi yao ya ufunguzi wa La Liga dhidi ya Elche Agosti 24 mwaka huu.