Friday, April 7, 2017

COLE AFANYIWA UPASUAJI KUPANDIKIZA FIGO.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester United, Andrew Cole amefanyiwa upasuaji kupandikiza figo. Nguli huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye aliwahi kuzichezea Newcastle United na Blackburn Rovers alipata matatizo ya figo baada ya kupata vurusi vya airborne mwaka 2015. Msemaji wa klabu ya United amesema upasuaji huo ni sehemu ya matibabu ya maradhi hayo yanayomsumbua nguli huyo. Msemaji huyo aliendelea kudai kuwa Cole kwasasa atachukua likizo ya muda katika kibarua chake kama balozi wa klabu hiyo. Akiwa Old Trafford, Cole alifunga mabao 121 katika mechi 275, nab ado anaendelea kuwa mchezo wa tatu mwenye mabao mengine zaidi kwenye Ligi Kuu akiwa mabao 187.

WAAMUZI MCHEZO WA YANGA NA MC ALGERS.

MCHEZO wa kimataifa wa Raundi ya Pili kati ya Young Africans ya Dar es Salaam, Tanzania na Mouloudia Club D’Alger ya Algeria unatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi Aprili 8, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambako utachezeshwa na waaamuzi kutoka Rwanda. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), waamuzi hao ni Louis Hakizimana ambaye atakuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Theogene Ndagijimana akiwa mshika kibendera wa mstari wa kulia na Jean Bosco Niyitegeka ambaye atakuwa mshika kibendera mstari wa kushoto. Mwamuzi wa akiba ambaye pia atakuwa anatokea Rwanda ni Ruzindana Nsoro wakati Kamishna wa mchezo atakuwa Ata Elmanan Hassan Osama kutoka Sudan. Waamuzi hao pamoja na Kamishna wa mchezo wamefikia Hoteli ya Urban Rose iliyoko Mtaa wa Jamhuri, katikati ya jiji la Dar es Salaam, Tanzania. Wapinzani wa Young Africans ambao ni Alger waliingia ujana usiku saa 3.30 kutoka Algeria kwa ndege maalumu ya kukodi na kufikia Hoteli ya Holiday Inn. Kwa mujibu wa kanuni, leo Ijumaa Aprili 7, mwaka huu saa 10.00 jioni watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezo huo muhimu kwa Young Africans kusonga mbele kama ilivyotokea msimu uliopita kwa kuifunga Sagrada Esperanca ya Angola na kutinga hatua ya makundi, viingilio vimepangwa kuwa Sh 30,000 kwa VIP ‘A’; Sh 20,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ wakati mzungunguko itakuwa ni Sh 3,000. Akizungumzia mchezo huo, Kocha msaidizi wa Young Africans, Juma Mwambusi alisema: “Wachezaji wa Yanga wako na morali wa hali juu na kikubwa tunawaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hii kwa sababu ni klabu pekee iliyobaki ikiiwakilisha nchi.”

MECHI ZA WIKIENDI LIGI KUU TANZANIA BARA.

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo sita. Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, Jumamosi Aprili 8, mwaka huu Mbeya City itashindana na Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji ya Songea itaialika African Lyon ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma. Mechi nyingine kwa siku ya Jumamosi Aprili 8, mwaka huu itakuwa ni kati ya Kagera Sugar na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera wakati wakati siku ya Jumapili Aprili 09, mwaka huu Stand United itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga. Ligi inatarajiwa kuendelea Jumatatu Aprili 10, mwaka huu kwa michezo miwili ambako Simba itakuwa mgeni wa Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ilihali Mtibwa Sugar itaialika Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro. 

Thursday, April 6, 2017

"NIPO FITI" - LEWANDOWSKI AWATOA HOFU MASHABIKI WA BAYERN.

MSHAMBULIAJI nyota wa Bayern Munich, Roberto Lewandowski amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kufuatia majeruhi aliyopata wakati wa mazoezi. Mapema leo Lewandowski alipigwa picha akiwa mazoezini ameshikilia msuli wa paja kwa hisia za maumivu hivyo kuzua wasiwasi kama atakuwepo kwenye mchezo muhimu wa Jumamosi hii wa Bundesliga dhidi ya Borussia Dortmund. Baadhi ya vyombo vya habari nchini Ujerumani vilikuwa vimeripoti kuwa Lewandowski amechanika msuli wa paja na anaweza kukaa kwa muda nje ya uwanja. Hata hivyo, nyota huyo aliibuka na kukanusha taarifa hizo zilizozagaa huku akiwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa anasikia vyema na yuko fiti. Bayern mbali na kukabiliwa na mchezo dhidi ya Dortmund kwenye Bundesliga Jumamosi hii, pia wanakabiliwa na mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid wiki ijayo.

TANZANIA YAKWEA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imepanda kwa nafasi 22 katika viwango vipya vya ubora duniani vinavyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kila mwezi. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa nafasi ya 157 lakini katika viwango vipya vilivyotolewa mapema leo vinaonyesha kupanda mpaka nafasi ya 135 duniani na 39 Afrika na kufanya kujisogeza mpaka nafasi ya nne wakiipita Burundi kwa nchi za Afrika Mashariki. Uganda bado wanaendelea kuongoza kwa Afrika Mashiriki wakiwa nafasi ya 15 kwa Afrika na 72 duniani wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 16 Afrika na 78 duniani wakati Rwanda wako nafasi ya 33 Afrika na 117 duniani na Burundi wao wapo nafasi ya 41 Afrika na 141 duniani. Kwa upande wa Afrika Misri wameendelea kuwa vinara wakipanda nafasi moja zaidi hadi nafasi ya 19, wakifuatiwa na Senegal walioko nafasi ya 30 kufuatia kuteleza kwa nafasi mbili huku mabingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Cameroon nao wakiteleza nafasi moja mpaka nafasi ya 33 duniani. Kwenye orodha za jumla Brazil wamekwea kileleni wakiiondoa Argentina iliyoanguka kwa nafasi moja mpaka ya pili, wa tatu ni mabingwa wa Dunia Ujerumani wakifuatiwa na mabingwa wa Amerika Kusini Chile na Colombia ndio wanahitimisha tano bora.

DORTMUND YAMLIMA FAINI AUBAMEYANG.

KLABU ya Borussia Dortmund imemlima faini Pierre-Emerick Aubameyang kufuatia kushangilia huku akiwa amevaa kinyago kwenye sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Schalke Jumamosi iliyopita. Aubameyang mwenye umri wa miaka 27 alifunga bao la kuongoza kwenye mchezo huo na kuanza kushangilia huku akiwa amevaa kinyago ambacho baadae iligundulika kuwa sehemu ya kampeni ya Nike ambao wanamdhamini. Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Aubameyang ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuwatangaza wadhamini wake hao wakati akiichezea Dortmund ambao wanadhaminiwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma. Katika taarifa yake Dortmund wamedai kuwa walifanya mazungumzo na Aubameyang baada ya mchezo wa Juzi ambao walishinda mabao 3-0 dhidi ya Humburg huku nyota huyo wa kimataifa wa Gabon akifunga bao moja na kusaidia lingine.

BROOS KUENDELEA KUBAKI CAMEROON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Hugo Broos amesisitiza anataka kuendelea kubaki na kibarua chake ikiwa imepita wiki moja baada ya kudai anafikiria kuhusu mustakabali wake. Kocha huyo raia wa Ubelgiji alitishia kujiuzulu kufuatia matatizo ya kiongozi na fedha lakini baada ya kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo amebadili uamuzi wake. Broos pia amekanusha tetesi kuwa aliomba kibarua cha kwenda kuinoa timu ya taifa ya Ghana maarufu kama Black Stars, ambao wamemteua Kwesi Appiah kushika nafasi hiyo. Broos mwenye umri wa miaka 64 amesema hataki kuondoka Cameroon kwnai kama angetaka kuondoka angeshafanya hivyo kitambo.