Friday, September 16, 2016

KLOPP ATAMBIA WASHAMBULIAJI ALIONAO.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema isingewezekana kuimarisha safu yake ya ushambuliaji katika kipindi cha usajili wa kiangazi kwakuwa kulikuwa hakuna mshambuliaji ambaye alikuwa bora zaidi ya wale alionao. Liverpool imefunga mabao 50 katika Ligi Kuu mwaka huu zaidi ya timu yeyote na kuongezeka kwa Sadio Mane aliyetoka Southampton kwa kitita cha paundi milioni 30 Juni kumeimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo zaidi ya ilivyokuwa awali. Vijana wa Klopp wamefunga mabao manne katika mchezo dhidi ya Arsenal na mabingwa Leicester City mpaka sasa msimu huu na Klopp ameisifu safu yake ya ushambuliaji kwa uwezo mkubwa walioonyesha. Akihojiwa Klopp amesema kiangazi watu wengi walikuwa wakitaka asajili washambuliaji zaidi lakini ukweli ni kuwa hakupata mshambuliaji ambaye alikuwa bora zaidi ya wale aliokuwa nao.

AGUERO KUONGEZA MKATABA MAN CITY.

MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Sergio Aguero anadaiwa kukubali kuongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi ambao utamuweka katika klabu hiyi mpaka mwaka 2020. Aguero mwenye umri wa miaka 28, amewahi kusema atajiunga tena na klabu yake ya kwanza ya Independiente pindi atakapomaliza mkataba wake mwaka 2019. Hata hivyo, nyota huyo wa kimataifa wa Argentina sasa anaonekana ataendelea kubakia Etihad kwa mwaka mmoja zaidi. Aguero ameanza msimu huu kwa kiwango cha juu, akiwa amefunga mabao tisa katika mechi tano zikiwemo hat-trick katika mechi mbili za michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa Aguero amesema anategemea kufunga mabao zaidi chini ya meneja mpya Pep Guardiola kwani ni meneja anayefurahia aina ya mchezo wake. Aguero alijiunga na City akitokea Atletico Madrid mwaka 2011 kwa kitita cha paundi milioni 38 na ameshafunga mabao 145 katika mechi 213 alizoichezea City.

SIMEONE ATHIBITISHA KUPUNGUZIWA MKATABA.

MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone amethibitisha kuwa mkataba wake na klabu hiyo ya La Liga ulipunguzwa kwa miaka miwili kiangazi mwaka jana, lakini amesisitiza kuwa hakuna chochote kilichobadilika. Taarifa zilibainisha mapema wiki hii kuwa, baada ya mazungumzo kufuatia Atletico kupoteza fainali ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi cha miaka mitatu, Simeone alikubaliana na wamiliki wa klabu hiyo kwa mkataba wake sasa kuishia Juni mwaka 2018. Akihojiwa kufuatia kuvuja kwa taarifa hizo, Simeone alikiri kuwa ni kweli suala hilo lilitokea lakini hakuna lililobadilika kwani anafurahia mahali alipo. Meneja huyo amesema haoni kama kuna tatizo kwenye hilo suala kwani katika kipindi cha miaka miwili anaweza kusaini mkataba mwingine mpya kama wamiliki wakiwa bado wanahitaji huduma yake.

SOUARE WA PALACE KUKAA NJE KWA MIEZI SITA BAADA YA AJALI.

MENEJA wa Crystal Palace, Alan Pardew amedai kuwa beki wa Crystal Palace, Pape Souare anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita baada ya baada ya kuvunjika mfupa wa paja katika ajali ya gari aliyopata. Nyota huyo wa kimaaifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 26, alikimbizwa hospitali kwa helikopta baada ya ajali hiyo aliyopata Jumapili iliyopita jijini London. Majeruhi pia yanamaanisha atakosa michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika Januari mwakani. Akihojiwa Pardew amesema beki huyo hayupo katika wakati mzuri lakini watu wote wako pamoja naye wakimuunga mkono katika kipindi hiki kigumu. Souare anategemewa kuachiwa kutoka Hospitali Jumamosi hii.

BAADA YA KICHAPO, MOURINHO KURUDIA KIKOSI CHAKE CHA KAWAIDA J'PILI.



MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema atapanga kikosi chake cha kawaida katika mchezo wao dhidi ya Watford Jumapili hii baada ya kufungwa katika mchezo wa Europa League dhidi ya Feyenoord. Mourinho alifanya mabadiliko nane katika kikosi chake alichokitumia jana na kupelekea kutandikwa bao 1-0 na timu hiyo ya Uholanzi. Nahodha Wayne Rooney, Antonio Valencia na Luke Shaw wote waliachwa nyumbani wapumzike kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili wa Ligi ya Kuu. Akihojiwa Mourinho amesema sasa atarejea katika kikosi chake cha kawaida bila mabadiliko makubwa sana. Kipigo hicho kinakuwa cha nne mfululizi kwa United kupata ugenini katika michuano ya Ulaya na kimekuja siku tano baada ya kutandikwa mabao 2-1 na Manchester City.

Thursday, September 15, 2016

TANZANIA YAPOROMOKA VIWANGO FIFA.

TANZANIA imeporomoka kwa nafasi nane mpaka kufikia nafasi ya 132 katika viwango vya ubora vipya vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA leo. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 123 lakini mwezi huu imeshuka na kushika nafasi hiyo huku kwa upande wa Afrika nako ikishuka mpaka nafasi ya 42 na kuzidiwa na Burundi inayoshika nafasi ya 129 duniani na 40 Afrika. Nchi inayoongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki ni Uganda waliopo nafasi ya 65 duniani na 15 Afrika wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 91 duniani na 23 Afrika na Rwanda ndio wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa katika nafasi ya 107 duniani na 33 Afrika. Kwa upande wa Afrika orodha hiyo sasa inaongozwa na Ivory Coast waliopanda kwa nafasi mbili mpaka nafasi ya 34, wakifuatiwa na Algeria waliopo nafasi ya 35 baada ya kuporomoka kwa nafasi tatu. Wengine ni Senegal waliop nafasi ya 39, Tunisia nafasi ya 42, Ghana wapo nafasi ya 43 baada ya kushuka kwa nafasi nane huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC wakiwa nafasi ya 51 baada ya kupanda kwa nafasi tano. Kwa upande wa orodha za jumla, Argentina bado wameendelea kukaa kileleni wakifuatiwa na Ubelgiji katika nafasi ya pili, Ujerumani nafasi ya tatu, Colombia nafasi ya nne, huku mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia Brazil nao wakirejea katika tano bora.

GENK YA SAMATTA KUTUPA KARATA YAO YA KWANZA EUROPA LEAGUE.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta baadae leo anatarajiwa kuingoza klabu yake ya Genk ya Ubelgiji katika mechi yao ya kwanza ya makundi ya michuano ya Europa League. Katika mchezo huo wa kundi F ambao unatarajiwa kutizamwa na wapenzi wengi wa soka nchini, Genk watakuwa ugenini katika Uwanja wa Allianz kuchuana na Rapid Vienna ya Australia. Akihojiwa huko nyuma kuhusiana na kundi walilopo katika michuano hiyo, Samatta amesema ni kundi gumu tofauti na wengi wanavyodhani kwani timu zilizopo zina uzoefu mkubwa na michuano hiyo. Toka Samatta ametua Genk akitokea TP Mazembe ya DR Congo mwaka jana amekuwa akiimarika ambapo mpaka sasa amefunga mabao nane katika mechi 24 za mashindano yote.