Friday, February 1, 2013

MUSTAKABALI WA KAKA MASHAKANI.

MUSTAKABALI wa kiungo wa kimataifa wa Brazil na klabu ya Real Madrid, Kaka unaonekana kuwa mashakani baada ya uhamisho wake katika kipindi cha dirisha dogo la usajili kushindikana huku kocha wake Jose Mourinho akimuondoa katika kikosi chake cha kwanza. Kaka mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mwaka 2007 ambaye aliigharimu Madrid kiasi cha euro milioni 65 wakati aliponunuliwa akitokea Ac Milan mwaka 2009 hatakuwepo hata kwenye benchi la wachezaji wa akiba wakati wa mechi ya La Liga dhidi ya Granada baadae leo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwemo katika benchi ya wachezaji wa akiba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mfalme waliotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Barcelona Jumatano iliyopita lakini hakupata nafasi ya kuingia. Mambo yamekuwa hayamuendei vyema mchezaji huyo toka Mourinho atue klabuni hapo akiwa ameanza mara 11 pekee katika mechi za La Liga, mara mbili katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na maa moja katika Kombe la Ligi. Kulikuwa na tetesi kuwa nyota huyo angeweza kurejea katika klabu yake ya zamani ya Milan lakini muda wa kufungwa kwa dirisha hilo hakuna makubaliano yoyote yaliyofikia huku kikubwa kilichokwamisha mpango kikiwa ni mshahara mkubwa wa mchezaji huyo anaoupokea.

BALOTELLI APONDA MAISHA YA UINGEREZA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Italia mwenye vituko vingi, Mario Balotelli amesema anajisikia faraja kuondokana na vyombo vya habari, kuendesha, hali ya hewa pamoja na vyakula vya Uingereza wakati akisaini rasmi kuiwakilisha klabu ya Ac Milan ya Italia. Balotelli ambaye wakati akiwa Uingereza amekuwa akipata adhabu za mara kwa mara kutokana na aina ya uendeshaji wake, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuichezea Milan ilikuwa ni ndoto alizokuwa nazo siku nyingi na amefurahi kuwepo hapo. Nyota huyo mwenye miaka 22 amesema amefurahi kurejea karibu na familia na marafiki zake baada ya kuiacha klabu yake ya Manchester City ambayo amekuwa akiingia mizozo ya mara kwa mara na kocha wake Roberto Mancini. Balotelli ambaye amesajiliwa na Milan kwa ada ya euro milioni 20 amesema kuna baadhi ya mambo atakayokumbuka wakati alipokuwa mojawapo ni wakati wa kwenda mazoezini huko Carrington akiwa na wachezaji wenzake pamoja na kocha.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KUONA TAIFA STARS, CAMEROON 5,000/-
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya FIFA Date kati ya Taifa Stars na Cameroon itakayochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani. Viti vya bluu ni sh. 7,000 wakati viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000. Kwa viti vya VIP viingilio ni kama ifuatavyo; VIP C sh. 15,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohia/Samora, kituo cha mafuta OilCom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.

FECAFOOT YATAJA NYOTA WAKE 21, ETO’O NDANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon (FECAFOOT) limetaja msafara wake wa watu 36 wakiwemo wachezaji 21 wa timu yao ya Taifa Indomitable Lions) wakiongozwa na nahodha Samuel Et’oo Fils kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano. Kiongozi wa msafara wa timu hiyo itakayoanza kuingia nchini keshokutwa (Februari 3 mwaka huu) ni Mwakilishi wa Serikali ya Cameroon, Dieudone Wassi. Naibu kiongozi wa msafara wa Cameroon itakayofikia hoteli ya New Africa ni Makamu wa Rais wa FECAFOOT, John Ndeh. Mbali ya Et’oo, wachezaji wengine waliomo kwenye msafara huo ni Charles Itandje, Benoit Assou Ekoto, Jehu Rustand Youthe (Union Douala), Fabrice Olinga Essono, Allam Nyam, Bouba Aminou, Benoit Angwa, Herve Tchami, Henri Bedimo, Nicolas Nkoulou, Jean Makoun, Jean Kana Biyick, Joel Matip, Vincent Aboubakar, Alexandre Song, landre Nguemo, Pierre Wome, Jean Nyontcha, Achille Emana na Charles Eloundou. Wengine ni Andre Nguidljol Nlend (Mkurugenzi wa Utawala FECAFOOT), Jean Paul Akono (Kocha Mkuu), Martin Ndtouungou Mpile (Kocha Msaidizi), Jacque Songo’O (Kocha wa makipa), Dk. Baoubakary Sidiki (Daktari wa Timu) na Emmanuel Francis Ambane (Psychologist). Pia wapo Tchonkontey Monkam (Fitness Trainer), Rigobert Song (Meneja wa Timu), Aoudou Mvotoung (Team Security), Fouda pascal Linus (Ofisa Habari FECAFOOT), Boubakar Ndou (Meneja Vifaa), Daniel Tcheuffa Tecky (Physiotherapist), Elias Kalaguem (Physiotherapist) na Justin Addo (Wakala wa Mechi). Wakati huo huo, kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kitaingia kambini kesho jioni (Februari 2 mwaka huu) kwenye hoteli ya Tansoma.

YANGA, MTIBWA SUGAR KAZI KWELIKWELI
Yanga na Mtibwa Sugar zinapambana kesho (Februari 2 mwaka huu) katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa sasa. Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa. Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

VILLA SQUAD, MORO UNITED UWANJANI FDL
Villa Squad na Moro United zinaumana kesho (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza mzunguko wa lala salama. Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa. Mechi nyingine ya Kundi B itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kundi C ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora). Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

TUZO YA MWANAMICHEZO BORA KUTOLEWA APRIL 27 - TASWA.

Haji Manara, Mwenyekiti Kamati ya Tuzo TASWA.
TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania wa mwaka 2012 zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zitafanyika Aprili 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kamati inayoratibu tuzo hiyo ilifanya kikao chake cha kwanza Jumanne wiki hii, ambapo wajumbe wa kamati hiyo walikubaliana mambo mbalimbali ya kimsingi kuhakikisha tuzo zinakuwa na mvuto kama ilivyokuwa miaka iliyopita na pengine ziwe bora zaidi. Kutokana na hali hiyo vyama vyote vya michezo vilivyosajiliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambavyo vipo hai na vinaendesha mashindano vitaandikiwa barua kwa ajili ya kutoa mependekezo yao ya wanamichezo waliofanya vizuri kwa mwaka jana upande wa michezo yao na yawasilishwe kabla ya Februari 28, mwaka huu. Tunaomba ieleweke kuwa vyama vitatoa mapendekezo na hivi sasa Kamati ya Tuzo inafanya mazungumzo na kampuni mbalimbali zinazohusika na mambo ya mawasiliano ili kuona namna zitakavyoshirikiana na wadau katika kuchambua majina hayo, ambapo kila chama kimetakiwa kiwasilishe majina matano ya wanamichezo wao kwa kila jinsia kama ni mchezo unaochezwa na jinsia mbili, lakini kama ni mchezo wa jinsia moja watatakiwa kuwasilisha majina matano ya jinsia husika tu. Yapo marekebisho kadhaa yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya tuzo kutoka 36 za mwaka jana hadi kufikia 42 mwaka huu na idadi inaweza kuongezeka ama kupungua kulingana na sifa za wanamichezo ambazo vyama vitaleta. Tunaomba wadau watupe ushirikiano wa kutosha katika jambo hili ili kuzifanya tuzo ziwe bora na kuhakikisha kila anayestahili kupata tuzo anazawadiwa kwa kuthamini kile alichokifanya, ambapo ukumbi utakapofanyika tuzo hizo utatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilisha baadhi ya mambo. Idadi ya michezo itakayopewa tuzo pamoja na aina nyingine ya tuzo zitakazotolewa ikiwemo Tuzo ya Heshima tutaendelea kujulishana kadri siku zitakavyokuwa zinasonga mbele. Washindi wa kila tuzo ndiyo mmojawapo ataibuka kuwa Mwanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2012. Dhamira ya kamati yangu ni kutaka kuhakikisha kuwa TASWA haikukosea kututeua na tutaleta wanammichezo sahihi na hatimaye kumpata yule bora ambaye ataungana na wengine waliopata kutwaa tuzo hiyo miaka ya nyuma. Wanamichezo ambao wamepata kutwaa Tuzo ya Mwanamichezo Bora Mwaka wa Tanzania ni Samson Ramadhan (2006), Martin Sulle (2007) na Mary Naali (2008) wote wakiwa wanariadha, wakati mwaka 2009 alikuwa Mwanaidi Hassan na mwaka 2010 alikuwa pia Mwanaidi Hassan ambaye ni mcheza netiboli na mwaka 2011 alikuwa mwanasoka Shomari Kapombe.

LANGALANGA 2013: FERRARI YAZINDUA GARI JIPYA.

TIMU ya Ferrari imezindua gari lake jipya litakalotumika kwa mwaka huu 2013 ili kujaribu kumaliza ukame wa vikombe latika mashindano ya Langalanga. Gari hilo aina ya F138 lilizinduliwa na kiongozi wa timu hiyo Stefano Domenicali akidai kuwa madhumuni makubwa ya kutumia gari ya aina ni kuweka historia ya kuvutia katika mashindano ya mwaka huu baada ya ukame wa miaka mingi. Mara ya mwisho Ferrari kushinda taji katika michuano hiyo ilikuwa ni mwaka 2008 wakati huo ikiendeshwa na dereva Kimi Raikkoen. Domenicali amedai kuwa wataanza msimu wa mwaka huu kiushindani zaidi katika mbio zitafanyika jijini Melbopurne, Australia tofauti na mbio za msimu uliopita ambapo walianza vibaya. Mwaka jana walilikosa taji hilo na kukamata nafasi ya pili baada ya Sebastian Vettel timu ya Red Bull kufanikiwa kushinda taji hilo kwa tofauti ya alama tatu pekee mbele ya Fernando Alonso ambaye amehamia timu ya Marcedes mwaka huu. 

GIBBS NJE WIKI SITA.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa beki wake wa kushoto Kieran Gibbs atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita kutokana na majeraha yanayomsumbua. Gibbs mwenye umri wa miaka 23 alilazimika kutoka katika kipindi cha kwanza baada ya kuumia paja wakati wa mchezo dhidi ya Liverpool ambao walitoka sare ya mabao 2-2. Wenger alithibitisha kuumia kwa nyota huyo baada ya kupata taarifa ya uchunguzi wake kutoka madaktari na sasa antegemea kumtumia Andre Santos kuziba nafasi hiyo. Pamoja na kumsajili beki mwingine wa nafasi hiyo Nacho Monreal kutoka klabu ya Malaga ya Hispania Wenger alionyesha bado kuwa na imani na Santos ambaye katika mchezo dhidi ya Liverpool alicheza chini ya kiwango. Wenger alimtetea santos akidai bado yuko katika kiwangi kizuri pamoja na makosa aliyofanya katika mchezo uliopita na kusema baadhi ya lawama anazotupia na mashabiki hastahili.

KOCHA WA CAPE VERDE ATAMBA KUNYAKUWA AFCON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Cape Verde, Lucio Antunes ametabiri kikosi chake kiyakuwa taji la michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon inayofanyika nchini Afrika Kusini mwaka huu. Cape Verde itaikabili Ghana katika mchezo wa Robo Fainali utakaochezwa katika Uwanja wa Port Elizabeth Jumamosi na kocha huyo anaamini kuwa kikosi chake kimeonyesha kiwango bora baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi A nyuma ya wenyeji Afrika Kusini kwa tofauti ya bao moja. Anmtunes amesema michuano ya mwaka huu inatofauti kubwa na michuano iliyopita na kuamini kuwa kikosi chake kinajiamini zaidi na kiko imara hivyo wana nafasi ya kusonga mbele mpaka katika hatua ya fainali ya michuano hiyo. Kocha huyo anasema bidii ndio silaha pekee itakayowawezesha kuwashangaza watu kwa kunyakuwa taji hilo kama walivyofanya Zambia mwaka jana.