Saturday, September 21, 2013

ANCELOTTI ALINIBAKISHA MADRID.

WINGA mahiri wa klabu ya Real Madrid, Angel Di Maria amebainisha kuwa aliamua kubakia klabuni hapo baada ya kujadiliana mustakabali wake na muargentina mwenzake anayecheza klabu ya Paris Saint-Germain Ezequiel Lavezzi na kocha wake carlo Ancelotti. Kulikuwa na tetesi kuwa winga huyo alikuwa akitaka kuondoka Santiago Bernabeu mapema katika kipindi cha usajili wa majira wa kiangazi lakini alichagua kubakia pamoja na ugumu wa kupata namba katika kikosi cha Madrid kilichosheheni nyota kibao. Di Maria amesema aliamua kubakia pamoja na kujua aina ya wachezaji ambao wangekuja klabuni hapo kwasababu anajiamini kwa kipaji alichokuwa nacho. Nyota huyo anasema mbali na kuzungumza na Lavezzi lakini pia alizungumza na Ancelotti na alimuhakikishia kuwa mchezaji atakayekuwa bora ndio atakayempanga katika kikosi chake cha kwanza.

Thursday, September 19, 2013

WORLD CUP 2022: WAJUMBE WA UEFA WAUNGA MKONO MICHUANO HIYO KUCHEZWA MAJIRA YA BARIDI.

WAJUMBE kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa Shirikisho la Soka barani Ulaya wameunga mkono mpango wa kuhamisha michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kuchezwa katika majira ya baridi baada ya kukubaliana kwamba haitawezekana michuano hiyo kuchezwa katika majira ya kiangazi kama ilivyo kawaida. Makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Duiani-FIFA Jim Boyce alithibitisha kuwa jambo walilokubaliana katika mkutano huo ni kwamba Kombe la Dunia nchini Qatar haliwezi kuchezwa katika majira ya kiangazi. Hata hivyo Boyce aliongeza kuwa kila mtu amekubaliana na hilo lakini ni tarehe halisi ya kuhamisha michuano hiyo ndio hawajafikia maamuzi yake. Suala la michuano hiyo kuandaliwa majira ya kiangazi nchini Qatar limekuwa likizua mjadala mkubwa kutokana na joto kali katika kipindi hicho linaloweza kufikia nyuzi joto 50. Kamati ya Utendaji ya FIFA inatarajiwa kukutana Octoba 3 mwaka huu huko jijini Zurich, Switzerland ili kujadili mapendekezo ya kuhamisha michuano hiyo katika majira ya baridi.


SUAREZ YUPO FITI - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amesema mshambuliaji nyota wa timu hiyo Luis Suarez yuko tayari kurejea katika kikosi cha kwanza baada ya wiki kadhaa za kufanya mazoezi na maandalizi mazuri. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay atamaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi 10 kwa kumuuma beki wa Chelsea Branislav Ivanovic April mwaka huu, katika mchezo dhidi ya Southampton Jumamosi. Hiyo itakuwa habari njema kwa Rogders kumtumia nyota huyo katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Manchester United Jumatano ijayo. Lakini meneja huyo alipuuza habari hizo na kudai kuwa hana uhakika kama atamtumia Suarez katika kikosi chake cha kwanza kwenye mchezo huo pamoja na kwamba anajua amefanya mazoezi ya kutosha wakati akiitumikia adhabu yake.

CESAR AVUNJIKA KIDOLE MAZOEZINI.

KLABU ya Queens Park Rangers-QPR imetangaza kuwa golikipa wake Julio Cesar atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita mpaka nane kutokana na majeraha. Cesar alifanyiwa upasuaji baada ya kuvunjika kidole chake cha mkono wa kushito wakati wa mazoezi Jumanne. Golikipa huyo alitegemewa kuondoka QPR mara baada ya klabu hiyo kushuka daraja masimu uliopita lakini ilishindikana kutokana na kukosa ofa aliyohitaji kutoka timu zingine. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ndio golikipa chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ambacho kinanolewa na Luis Felipe Scolari na kuna uwezekano mkubwa wa kukosa mechi za kimataifa za kirafiki dhidi ya Korea Kusini na Zambia mwezi ujao.

WACHEZAJI WAMEKOSA UKOMAVU - MOURINHO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekiri kikosi chake kinakosa ukomavu baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa FC Basel katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya uliofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge. Katika mchezo huo wenyeji Chelsea ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Oscar muda mchache kabla ya mapumziko lakini Basel walinikiwa kubadilisha matokeo katika kipindi cha pili kwa mabao yaliyofungwa na Mohamed Salah na Marco Streller. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Mourinho amesema anafikiri kikosi chake kimekosa ukomavu wa kutosha ili kupambana na shinikizo lolote linalotokea katika mechi. Mourinho amesema watakwenda nyumbani wakiwa na huzuni kutokana na kipigo hicho lakini wataamka na kuufanyia kazi udhaifu wao ili kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao nyingine.

MBABE WA MOHAMMAD ALI AFARIKI DUNIA.

BINGWA wa zamani wa ngumi za uzito wa juu, Ken Norton wa Marekani ambaye alimtandika Mohammad Ali amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Norton ambaye afya yake ilianza kuyumba baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi na kupooza sehemu kubwa ya mwili wake, amefariki dunia akiwa katika kliniki moja iliyopo jijini Las Vegas, Nevada. Bondia huyo alimvunja Ali taya katika pambano lao walilocheza kwa mara ya kwanza jijini San Diego, California mwaka 1973 ambapo alishinda pambano hilo. Katika pambano lao la mwisho lililofanyika Septemba mwaka 1976 katika Uwanja wa Yankee uliopo jijini New York, Ali alishinda kwa ushindi mwembamba na kurejesha taji lake la uzito wa juu. Norton alianza kucheza ngumi wakati akiwa mwajiriwa wa jeshi la wanamaji nchini Marekani na muda mfupi baadae aliacha shughuli za jeshi na kuingia katika ulimwengu wa ngumi za kulipwa mwaka 1967. Bondia huyo alishinda taji lake la kwanza la uzito wa juu mwaka 1977, na baada ya kustaafu alijishughulisha na mambo ya utangazaji na pia kushirikishwa katika sinema kadhaa.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MIL 58/- ZAPATIKANA MECHI YA SIMBA, MGAMBO
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mgambo Shooting Stars iliyochezwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 58,365,000. Watazamaji 10,241 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 23 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 6-0. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 13,839,327.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,903,135.59. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,036,946.16, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 4,222,167.70, Kamati ya Ligi sh. 4,222,167.70, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,111,083.85 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,641,954.10.



MIKATABA YA MAKOCHA VPL, FDL YATAKIWA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa siku 14 kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na za Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) kuwasilisha mikataba ya makocha wao. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Septemba 12 mwaka huu imebaini klabu nyingi hazijawasilisha mikataba ya mabenchi yao ya ufundi, kitu ambacho ni matakwa ya kikanuni. Siku hizo 14 zimetolewa kuanzia Septemba 17 mwaka huu. Kwa klabu ambazo zitashindwa kuwasilisha mikataba hiyo na vielelezo vingine ndani ya mudau huo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.