Thursday, October 3, 2013

INIESTA ATAKA KUZEEKEA BARCELONA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Barcelona, Andres Iniesta ameonyesha nia yake ya kumalizia soka lake akiwa na klabu hiyo na kumaliza utata uliozagaa kuwa hataweza kuongeza mkataba wake. Tetesi za kuondoka kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ziliibuka baada ya tuhuma kuwa alikataa kuongeza mkataba na klabu hiyo. Hata hivyo Iniesta ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2015 amesema ana ndoto za kumalizia soka lake hapo hivyo hana shaka kwamba ataongeza mkataba wake wakati utakapofika. Iniesta amesema amekuwepo Barcelona toka akiwa na umri wa miaka 12 na ndoto zake ni kustaafu soka akiwa hapo.

GIGGS AMPIKU RAUL KWA KUCHEZA MECHI NYINGI CHAMPIONS LEAGUE.

MSHAMBULIAJI mkongwe wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs ameweka rekodi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati timu yake ilipong’ang’aniwa sare ya bao 1-1 na Shakhtar Donetski katika mchezo wa kundi A. Giggs mwenye umri wa miaka 39 aliingia uwanjani katika dakika ya 66 akichukua nafasi ya Marouane Fellaini na kufikisha jumla ya mechi 145 katika michuano hiyo zikiwemo za kufuzu na kumpita mshambuliaji nyota wa zamani wa Hispania Raul. Meneja wa United David Moyes alimpongeza Giggs kwa rekodi hiyo lakini kwa upande mwingine alisononeshwa na matokeo waliyopata baada ya timu yake kuongoza karibu dakika zote za mchezo. Katika mchezo huo United walimkosa Wayne Rooney lakini Robin van Persie alirejea uwanjani na kuipa timu yake bao la kuongoza katika dakika ya 18 kabla ya Shakhtar hawajasawazisha zikiwa zimebaki dakika 14 mpira kumalizika. Baadhi ya matokeo ya mechi zilizochezwa jana ni pamoja na Manchester City walishindwa kutamba mbele ya Bayern Munich kwa kufunguwa mabao 3-1, Bayer Leverkusen waliifunga Real Sociedad kwa mabao 2-1, Paris Saint Germain walishinda mabao 3-0 dhidi ya Benfica. Nyingine ni Juventus iling’ang’aniwa sare ya mabao 2-2 na Galatasaray, Anderlecht walishindwa kutamba mbele ya Olympiacos kwa kufungwa mabao 3-0 na Real Madrid walipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya FC Copenhagen.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

WARUNDI KUCHEZESHA WANAWAKE U20 KOMBE LA DUNIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20 Kanda ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji. Waamuzi hao watakaochezesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Oktoba 26 na 27 mwaka huu wataongozwa na Ines Niyonsara. Atasaidiwa na Jacqueline Ndimurukundo na Axelle Shikana. Irene Namiburu kutoka Uganda ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mezani wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Evelyn Awuor wa Kenya. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Maputo kati ya Novemba 9 na 10 mwaka huu, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar. Fainali hizo za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani nchini Canada, ambapo Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa wasichana. Timu ya Tanzania tayari imepiga kambi mkoani Pwani ikiwa chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage. Wachezaji walioko kambini ni Amina Ally, Amina Ramadhan, Amisa Athuman, Anastazia Anthony, Anna Hebron, Belina Julius, Donisia Daniel, Esther Mayala, Fatuma Issa, Gerwa Lugomba, Happiness Lazoni, Harriet Edward, Hellen Maduka, Irene Ndibalema, Jane Cloud, Khadija Hiza na Latifa Salum. Wengine ni Maimuna Hamis, Mwanaidi Khamis, Najiati Abbas, Neema Paul, Niwael Khalfan, Rehema Abdul, Sabahi Hashim, Sada Ramadhan, Shamimo Hamis, Shelder Boniface, Stumai Abdallah, Tatu Idd, Therese Yona, Violet Nicholas, Vumilia Maarifa, Yulitha Kimbuya na Zena Said.


WATATU KUSHIRIKI KOZI YA FUTURO ADDIS ABABA
Watanzania watatu ni miongoni mwa washiriki 30 walioteuliwa kuhudhuria kozi ya wakufunzi ya waamuzi ya FUTURO III itakayofanyika Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Oktoba 5 hadi 10 mwaka huu. Leslie Leonard Liunda, Abdi Soud Mohamed na Israel Nkongo Mujuni ndiyo watakaoshiriki katika kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Kozi hiyo pia itakuwa na washiriki kutoka nchi nyingine tisa za Afrika. Nchi hizo ni Gambia, Ghana, Kenya, Liberia, Nigeria, Seychelles, Sierra Leone, Somalia na Uganda.

Wednesday, October 2, 2013

BARKER KUTETEA UBINGWA WAKE WA IBF DHIDI YA STURM.

BONDIA Darren Barker wa Uingereza anatarajiwa kupigana kwa mara ya kwanza kutetea taji lake la IBF uzito wa kati dhidi ya Felix Sturm wa Ujerumani Desemba 7 mwaka huu. Barker mwenye umri wa miaka 31 alishinda taji hilo kwa alama dhidi ya Daniel Geale wa Australia katika pambano lilifanyika Atlantic City Agosti mwaka huu. Akihojiwa kuhusiana na pambano hilo promota wa Barker aitwaye Eddie Hearn amesema kuna makubaliano ya kuwepo pambano la marudiano jijini London kama bondia wake akitandikwa katika pambano hilo. Sturm ambaye alidundwa na Geale Septemba mwaka jana ana rekodi ya kushinda mapambano 38 ambapo 17 kati ya hayo alishinda kwa knockout, kupigwa matatu na sare mapambano mawili. Kwa upande wa Barker yeye ameshinda mapambano 26 kati ya 27 akiwa chini promota wake Hearn.

ZAWADI ZAONGEZWA MICHUANO YA WAZI YA AUSTRALIA.

WARATIBU wa michuano ya wazi ya Australia wameongeza zawadi kwa washindi wa michuano hiyo kwa asilimia 10 mpaka kufikia dola milioni 33 kwa mwaka 2014. Mwaka jana zawadi za jumla katika michuano hiyo zilifikia dola milioni 30 ambapo bingwa kwa upande wa wanaume Novak Djokovic na wanawake Victoria Azarenka kila mmoja alipokea hundi ya dola milioni 2.43. Hatua ya kuongeza zawadi katika michuano hiyo mikubwa kabisa ambayo hufanyika jijini Melbourne Januari ya kila mwaka ilifikiwa baada ya baadhi ya wachezaji kulaumu mgao kiduchu kulingana na hadhi yake. Mkurugenzi wa michuano hiyo Craig Tiley amesema wachezaji wameshataarifiwa kuhusiana na mabadiliko hayo na wote wameonyesha kukubaliana nao.

BOLT KUSHIRIKI MBIO ZA HISANI ARGENTINA.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt anatarajiwa kushiriki mbio za mita 100 za maonyesho zitakazofanyika jijini Buenos Aires, Argentina Desemba mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchi hiyo Bolt ambaye anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 100, atashiriki katika mbio zitakazofanyika Desemba 7 au 13. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo mratibu wa mbio hizo za hisani, Guillermo Marin alithibitisha ujio wa Bolt na kudai kuwa nyota huyo atakuja na wanariadha wengine watatu kutoka Jamaica. Marin pia amesema mbali na kufanyika kwa mbio hizo kutakuwa na mchezo wa tenisi wa hisani ambao utawahusisha wanadada wawili ndugu kutoka Marekani Venus na Serena Williams.

TORRES KUFANYIWA UCHUNGUZI.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Chelsea, Fernando Torres anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa mguu wake ambao aliumia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Steaua Bucherest iliyochezwa jana. Meneja wa Chelsea, Jose Mourinho amesema kuwa mchezaji huyo hatakuwa fiti kwa ajili ya kwenda kuitumikia timu ya taifa ya Hispania wiki ijayo lakini ana matumaini tatizo lililompata sio kubwa sana. Mourinho aliendelea kudai kuwa madaktari wa timu hiyo wana uhakika majeruhi aliyopata sio makubwa sana kama aliyopata Marco van Ginkel ya kukaa nje ya uwanja miezi sita. Torres mwenye umri wa miaka 29 tayari hayumo katika kikosi cha timu hiyo kitakachopambana na Norwich City Jumapili kufuatia kutolewa nje kwa kadi mbili za njano kwenye mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs mwishoni mwa wiki iliyopita.