Tuesday, December 3, 2013

BURKINA FASO YAPINGA UAMUZI WA FIFA.

SHIRIKISHO la Soka la Burkina Faso-FBF limekata rufani dhidi ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ambao ulitupilia mbali malalamiko yao dhidi ya Algeria kuhusu mechi zao za mtoano za kufuzu Kombe la Dunia 2014. Mwenyekiti wa FBF Sita Sangare aliwaambia waandishi wa habari jijini Ouagadougou kuwa wamenyang’anywa tiketi yao ya kwenda katika michuano hiyo nchini Brazil, wakimtuhumu mwamuzi kwa kuwanyima nafasi hiyo. Sangare amesema kwa tukio la mchezo wa Novemba 19 uliochezwa huko Blida FBF inaweza kudai kuwa nafasi yao ya kwenda Brazil iliporwa kutokana na maamuzi mabovu ya mwamuzi. Sangare aliendeleaa kulalama kuwa bao la Charles Kabore lililokataliwa na muda wa nyongeza uliowekwa bila sababu yoyote ni mfano tosha wa maamuzi mabovu yaliyotokea katika mchezo huo. Wiki iliyopita FIFA ilitupilia mbali malalamiko ya Burkina Faso na kuithibitisha Algeria katika michuano hiyo lakini sasa itabidi ipitie tena rufani hiyo na kutoa uamuzi wake wa mwisho Desemba 5 kabla ya upangwaji wa ratiba Ijumaa hii.

Monday, December 2, 2013

KUIONA TANZANITE BUKU.

WASHABIKI watakaoshuhudia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini watalipa kiingilio cha sh. 1,000. Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Kiingilio cha sh. 1,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na orange. Viingilio vingine kwa mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa sh. 10,000. Tanzanite chini ya Kocha Rogasian Kaijage inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na ule wa Taifa kujiandaa kwa mechi hiyo. Kambi ya Tanzanite hivi sasa imehamia Msimbazi Hotel kutoka Ruvu mkoani Pwani.

MBABE WA TP MAZEMBE AJIUZULU.

NAHODHA wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Ruud Krol amejiuzulu nafasi ya ukocha katika timu ya CS Sfaxien ikiwa zimepita siku chache baada ya kuiwezesha klabu hiyo ya Tunisia kushinda michuano ya Kombe la Shirikisho. Kuondoka kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 kunakuja kufuatia kuifundisha timu hiyo kwa miezi 12 yenye mafanikio baada ya kuiwezesha kunyakuwa taji la ligi kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka nane na baadae kuisambaratisha TP Mazembe kwa jumla ya mabao 3-2 katika fainali za mikondo miwili za Kombe la Shirikisho. Krol pia alifanya kazi kama kocha wa muda wa timu ya taifa ya Tunisia wakati ilipocheza mechi mbili za hatua ya mtoano kufuzu Kombe la Dunia ambapo walifungwa kwa jumla ya mabao 4-1. Krol ambaye alikuwa beki enzi enzi zake aliiongoza Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia 1978 ambapo walifungwa mabao 3-1 na wenyeji Argentina katika mchezo wa fainali.


RATIBA YA KOMBE LA DUNIA 2014 KUPANGWA IJUMAA HII.

MACHO na masikio ya mamilioni ya mashabiki wa soka Ijumaa hii yatahamia katika kiota cha Costa do Sauipe kilichopo katika jimbo la Bahia nchini Brazil kushuhudia upangwaji ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limetenga kiasi cha dola milioni nane kwa ajili ya shughuli hiyo itakayoonyeshwa dunia nzima kwa dakika 90 huku ikishirikisha nyota wa soka wa Brazil pamoja na muziki utakaowapa ladha mashabiki. Baadhi ya nyota wa zamani katika soka wakiwemo Pele, Zinedine Zidane na Lothar Matthaeus watakuwepo kusaidia uapngwaji ratiba hiyo wakati maofisa 5,000, waandishi wa habari na wageni waalikwa watakuwa wakishuhudia tukio hilo muhimu. Brazil imesubiri kwa miaka 64 kuandaa michuano hiyo baada ya kushindwa kunyakuwa kombe hilo mwaka 1950 katika mchezo wa fainali dhidi ya majirani zao Uruguay katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro.

KOMPANY KUIVAA WEST BROM.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini anaamini kuwa nahodha wake Vincent Kompany atakuwa fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya West Bromwich utakafanyika Jumatano. Kompany amekuwa nje ya uwanja toka apate majeraha ya msuli katika mchezo dhidi ya Everton uliochezwa Octoba 5 mwaka huu. Pamoja na kufanya vizuri mechi za nyumbani, City wamekuwa wakihangaika katika mechi za ugenini za ugenini na kushinda mechi moja pekee toka msimu huu umeanza hivyo ujio wa beki huyo unaweza kuwa ahueni kwa Pellegrini. Akihojiwa Pellegrini amesema anadhani Kompany anatakuwepo katika mchezo wa ugenini Jumatano. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa mchezo huo ni muhimu kwao kushinda kama wanahitaji kuendelea kuwa katika mbio za kugombea taji la ligi.

LAHM AANZA MAZOEZI MEPESI.

KOCHA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola amepokea habari njema baada ya nahodha wake Philipp Lahm kuanza mazoezi binafsi. Lahm alipata majeruhi ya msuli wiki iliyopita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya CSKA Moscow na kumfanya kukosa mchezo wa mwishoni mwa wiki dhidi ya Eintracht Braunschweig. Beki huyo wa kati ambaye msimu huu amekuwa akicheza katika nafasi ya kiungo hatarajiwi kuwemo katika mchezo wa katikati ya wiki dhidi ya Augsburg lakini anaweza kuwemo katika kikosi kitakachopambana na Werder Bremen Jumamosi ijayo. Bayern kwasasa wanaongoza Ligi Kuu nchini ujerumani wakiwa na alama 38 katika michezo 14 waliyocheza wakiwazidi Bayer Leverkusen wanaoshika nafasi ya pili kwa alama nne.

BASI LA PSG LASHAMBULIWA KWA MAWE.

MABASI yaliyokuwa yamebeba wachezaji wa timu za Paris Saint-Germain, PSG na Lyon yameshambuliwa kwa mawe kabla ya mchezo wa Ligue 1 baina ya timu hizo katika Uwanja wa Parc des Princes jijini Paris jana. PSG walithibitisha taarifa hizo za basi lao kushambuliwa wa mawe na kuvunjwa vioo wakati wakielekea uwanjani huku pia basi Lyon nalo linadaiwa kukutwa na tukio kama hilo. Nyota wa PSG akiwemo Zlatan Ibrahimovic, Thiago Silva na Edson Cavani wanasadikiwa kuwa walikuwemo katika basi hilo lakini hawakupata majeraha yoyote kwasababu walikuwepo katika kikosi kilichoshinda mabao 4-0 dhidi ya Lyon. Baadhi ya luninga za Ufaransa zilionyesha basi hilo jinsi basi hilo lilivyoathirika.