Tuesday, October 18, 2016

MAN CITY YAINGIZA FAIDA KWA MSIMU WA PILI MFULULIZO.

KLABU ya Manchester City imetangaza rekodi mpya ya mapato yao kufikia paundi milioni 391.8, huku wakitengeneza faida kwa mwaka wa pili mfululizo. Vinara hao wa Ligi Kuu walitoa taarifa yao ya mwaka wa fedha wakionyesha kutengeneza faida ya paundi milioni 20.5 kwa msimu wa 2015-2016. Mwaka jana, City walitangaza mapato yao ya kwanza toka Sheikh Mansour alipochukua umiliki wa klabu hiyo mwaka 2008 na kuanza kuwekeza katika kikosi cha kwanza. Klabu hiyo ilitangaza hasara ya paundi milioni 197.5 msimu wa 2010-2011 ikiwa ni hasara kubwa kuwahi kupata klabu za Uingereza na kufuatia na hasara zingine za paundi milioni 97.9 msimu wa 2011-2012, paundi milioni 51.6 msimu wa 2012-2013 kabla ya hatimaye kutangaza ongezeko ya paundi milioni 11 msimu uliopita. Mapato ya paundi milioni 391.8 ya City ni ongezeko la asilimia 11 kulinganisha ya yale ya paundi milioni 351.8 waliyopata mwaka jana. Mapato hayo yamechangiwa kwa kiasi kubwa na upanuzi wa Uwanja wa Etihad ambao kwasasa unabeba mashabiki 55,000 na pia uwekezaji wa asilimia 13 wa kampuni mama ya China Media Capital Holdings.

MOURINHO AIPONDA LIVERPOOL KUFUATIA SARE.

MENEJA wa Manchester United, Jose Mourinho amesema Liverpool sio timu ya kwanza ya ajabu kama inavyoripotiwa na vyombo vya habari, baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana jana. Katika mchezo huo wa Anfield uliokuwa na nafasi chache, wenyeji Liverpool walionyesha kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa kufuatia wapianzani wao muda mwingi kucheza kwa kujihami. Akihojiwa Mourinho amesema jambo la muhimu ni kuwa wamepata alama moja ambayo imewazuia wapinzani wao kupata alama tatu. Kwa upande wa meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, yeye ameonyesha kutofurahishwa na kikosi chake kwani walikuwa wakitaka kucheza haraka na kupoteza umakini katika pasi zao. Matokeo hayo ynaiacha Liverpool katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama saba huku United wakiwa nyuma yao kwa tofauti ya alama tatu kwenye nafasi ya saba.

MISRI SASA MASHABIKI RUKSA VIWANJANI.

CHAMA cha Soka cha Misri-EFA kimetangaza kuwa kitaruhusu mashabiki 50,000 kuhudhuria mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Misri na Ghana utakaofanyika jijini Alexandria. Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Novemba 13 katika Uwanja wa Borg El Arab. Kuzuiwa kwa mashabiki katika mechi nchini humo kuliwekwa toka mwaka 2012 wakati mashabiki 72 wa Al Ahly walipokufa kufuatia vurugu zilizotokea huko Port Said. EFA pia imetangaza kuwa mashabiki 40,000 wataruhusiwa kwnda kuangalia mchezo wa fainali ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itafanyika jijini Alexadria. Katika mchezo huo Zamalek watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini Jumapili hii.

KICHUYA MCHEZAJI BORA WA MWEZI.

MSHAMBULIAJI Shiza Kichuya wa Simba SC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa Septemba msimu wa 2016/2017. Kichuya aliwashinda nyota wengine wa VPL akiwemo Adam Kingwande wa Stand United na Omari Mponda wa Ndanda FC. Mchezaji aliisadia timu yake kwa mwezi huo kupata pointi zote 12 katika mechi nne ilizocheza, matokeo ambayo yameifanya Simba iendelee kuongoza Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16. Pia alifunga mabao matatu katika mechi mbili kati ya nne ilizocheza timu yake. Kwa kushinda tuzo hizo ya mwezi, Kichuya atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

Monday, October 17, 2016

KUFA NA KUPONA ANFIELD LEO.

MACHO na masikio ya wapenzi wa soka duniani baadae leo watakuwa luningani kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu ambao utazikutanisa timu mahasimu Liverpool dhidi ya Manchester United. Mchezo huo utakaofanyika Anfield unakutanisha timu hizo zenye uhasimu wa kipindi kirefu nchini Uingereza ambapo klabu hizo kwa pamoja wametwaa jumla ya mataji 87, Liverpool 44 na United mataji 43. Liverpool inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika kiwango kizuri kwa kushinda mechi zake zote nne zilizopita za ligi huku United wao wakiwa tayari wameshapoteza mechi mbili msimu huu na wako nyuma ya vinata Manchester City kwa alama tano. Hata hivyo, rekodi ya United wakikutana na Liverpool iko juu ambapo wameshinda mechi nne za ligi zilizowakutanisha huku mara ya mwisho ikiwa ni Januari mwaka huu wakati waliposhinda bao 1-0. Liverpool mara ya mwisho kuishinda United katika Uwanja wa Anfield ilikuwa katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Europa League msimu uliopita ambapo walishinda mabao 2-0.

NEYMAR KUSAINI MKATABA MPYA IJUMAA.

KLABU ya Barcelona imethibitisha kuwa mshambuliaji wake nyota Neymar anatarajia kusaini mkataba mpya Ijumaa hii. Barcelona walitangaza taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ataisaini mkataba mpya ambao utamuweka klabuni hapo mpaka mwaka 2021. Neymar amekuwa akihusishwa na tetesi kuwindwa vilabu kadhaa ikiwemo Paris Saint-Germain lakini sasa mshambuliaji huyo anajipanga kusaini mkataba mpya wa muda mrefu Camp Nou. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa katika kiwango bora msimu huu akiwa amefunga mabao manne katika mechi sita za La Liga alizocheza. Neymar alijiunga na Barcelona akitokea Santos mwaka 2013 na ameshinda mataji mawili ya la Liga na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

DROGBA AGOMA KUCHEZA.

MENEJA wa klabu ya Montreal Impact, Mauro Biello amedai kuwa nyota wao Didier Drogba aligoma kucheza baada ya kuambiwa kuwa hataweza kuanza katika mchezo dhidi ya Toronto. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea mwenye umri wa miaka 38, hakuonekana kabisa katika Uwanja wa Saputo ambapo Impact walipata sare ya mabao 2-2 na kupenya kwenye hatua ya mtoano ya Ligi Kuu ya Soka ya Marekani-MLS. Mapema klabu hiyo ilitoa taarifa kuwa Drogba alienguliwa katika kikosi kufuatia kusumbuliwa na majeruhi ya mgongo. Lakini baada ya mchezo huo, Biello amesema Drogba hakuwepo kwasababu hakutaka kuanzia katika benchi kwenye mchezo huo. Drogba ambaye aliondoka Chelsea Julai mwaka 2015, amekuwa akitumika kama mchezaji wa akiba mara mbili katika mechi nne zilizopita za Impact.