Thursday, April 6, 2017
CONTE SASA AUONA UBINGWA UKIKARIBIA.
MENEJA wa Chelsea Antonio Conte amesema kikosi chake kimepiga hatua kubwa kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 2-1 waliopata dhidi ya Manchester City jana kwenye Uwanja wa Stamford Bridge. Eden Hazard alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza huku Sergio Aguero akifunga la kusawazisha la City, wakati Chelsea wakirejesha makali yao ya ushindi kufuatia kipigo cha mabao 2-1 walichopata nyumbani kutoka kwa Crystal Palace. Ushindi huo unaifanya Chelsea kuendelea kujiimarisha kileleni kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Tottenham Hotspurs wanaoshikilia nafasi ya pili huku kukiwa kumebaki mechi nane msimu kumalizika. Akizungumza na wanahabari, Conte amesema ushindi huo ni hatua kubwa dhidi ya timu kubwa. Conte aliendelea kudai kuwa kushinda mchezo mgumu baada ya kutoka kufungwa sio jambo jepesi na anashukuru wachezaji wake wameonyesha ubora wao.
OZIL AMFURAHISHA WENGER.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema Mesut Ozil amefanikiwa kusahau kuondolewa kwao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa amehamishia nguvu zake katika Ligi Kuu. Kauli hiyo ya Wenger imekuja kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-0 waliopata dhidi ya West Ham United jana na kuwapandisha mpaka nafasi ya tano kutoka ile ya sita. Katika miezi ya karibuni Ozil alionekana kuwa chini ya kiwango lakini jana alionyesha kiwango kikubwa kwa kufunga bao moja na kutengeneza linguine katika ushindi wa pili wa Arsenal kati ya mechi saba za ligi zilizopita. Akizungumza na wanahabari, Wenger amesema anadhani Ozil amerejea kwenye ubora wake kwani anamfahamu vyema. Wenger aliendelea kudai kuwa anadhani kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kulimuathiri kwa kiasi kikubwa na ilimchukua muda kusahau.
Wednesday, April 5, 2017
AS ROMA YAMUWANIA MANCINI.
KLABU ya AS Roma imeripotiwa kufanya mawasiliano na Roberto Mancini kuhusu kuchukua nafasi ya Luciano Spalletti, huku akikubali kupunguza kiwango cha mshahara anachohitaji. Kwasasa kocha huyo anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu na amekataa kujadili mustabali wake wa baadae. Hatua hiyo imezusha tetesi kuwa Spalletti ataondoka mwishoni mwa msimu huu huku klabu hiyo ikidaiwa kuhaha kutafuta mbadala wake. Taarifa kutoka nchini Italia zinadai kuwa Roma wamezungumza na Mancini ambaye yuko tayari kushusha kiwango cha mshahara wake chini ya euro milioni 4.5 alizokuwa akichukua alipokuwa Inter Milan.
WATATU WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA UPANGAJI MATOKEO.
POLISI nchini Hispania imekamata watu wengine watatu wakiwemo wachezaji wawili kuhusiana na uchunguzi wa upangaji wa matokeo wa klabu ya CD Eldense. Wachunguzi tayari wanamshikilia kocha wa klabu hiyo ya daraja la tatu Filippo Vito di Pierro na Mkurugenzi Mkuu Nobile Capuani. Kukamatwa huko kumekuja kufuatia Eldense kuchapw amabao 12-0 mwishoni mwa wiki iliyopita na Barcelona B huku klabu hiyo ikichapwa mabao matano baada ya dakika 15 huku mpaka mapumziko wakitandikwa mabao 8-0. Shirikisho la Soka la Hispania-RFEF ilitangaza kufungua kesi dhidi ya Eldense kwa suala la upangwaji matokeo.
CHAPECOENSE WAICHAPA ATLETICO NACIONAL.
KLABU ya Chapecoense imefanikiwa kuifunga Atletico Nacional kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Supercup ya Amerika Kusini uliofanyika jana. Mchezo huo ulitoa kumbukumbu ya wachezaji waliokufa katika ajali ya ndege kabla ya timu hiyo haijacheza mchezo wa fainali ya Copa Sudamericana Novemba mwaka jana. Mchezo huo ni wa kwanza kati ya timu hizo toka wachezaji wote kasoro watatu kwenye timu hiyo ya Brazil na viongozi wao kufariki kwenye ajali ya ndege wakati wakikaribia Medellin mwaka jana. Watu sita pekee kati ya 77 waliokuwepo kwenye ndege ndio waliopona kwenye ajali hiyo. Kabla ya mchezo huo wa jana timu zote pamoja na mashabiki walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka wote waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo. Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo unatarajiwa kufanyika Mei 10 mwaka huu.
SIJALI WANAONIKOSOA - MESSI.
MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amesisitiza kuwa hafuatilii wale wote wanaokosoa kiwango chake akiwa na timu ya taifa ya Argentina. Messi amekuwa na msimu mzuri Camp Nou lakini ameshindwa kupeleka mafanikio hayo kwenye timu ya taifa. Nyota huyo alitwaa medali ya dhahabu mwaka 2008 lakini walijikuta wakishindwa kwenye fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 pamoja na fainali mbili za Copa America mwaka 2015 na 2016. Akizungumza na wanahabari, Messi amesema huwa hajali sana wanaomkosoa kwani anafahamu kitu gani kinaendelea. Messi aliendelea kudai kuwa anafahamu kuwa watu siku zote wanataka washinde na kuleta mataji nyumbani.
Subscribe to:
Posts (Atom)



