Tuesday, November 20, 2012

BECKHAM KUIKACHA GALAXY MWISHONI MWA MSIMU.

Nahodha wa zamani wa Uingereza, DAVID BECKHAM anatarajiwa kuondoka katika klabu ya Los Angeles Galaxy mwezi ujao baada miaka sita kucheza katika Ligi Kuu nchini Marekani maarufu kama Major League. Nyota huyo amepanga kuikacha klabu hiyo baada ya msimu wa ligi hiyo kumalizika Desemba 1 mwaka huu. Katika taarifa yake BECKHAM mwenye umri wa miaka 37 amesema kuwa anahitaji changamoto nyingine kabla ya kuamua rasmi kustaafu soka. Klabu ya Melbourne Heart ya Australia imedai kuwa ipo katika mazungumzo na nyota huyo ili wamsajili kwa ajili ya mechi 10 nyota huyo pamoja na mwenyewe kudai kuwa hana mpango wa kucheza soka katika Ligi Kuu ya nchini humo maarufu kama A League. BECKHAM alianza kucheza soka katika klabu ya Manchester United ambapo akiwa hapo alifanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uingereza mara sita pamoja na taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutua Real Madrid mwaka 2003 na baadae Marekani mwaka 2007.

KESI YA PARK KUSIKILIZWA LEO.

Kesi ya mchezaji soka wa kimataifa wa Korea Kusini ambaye aliyeleta msuguano wa kidiplomasia na Japan baada ya kupeperusha bango lenye maandishi ya kisiasa katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika London, Uingereza inatarajiwa kusikilizwa tena na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Kamati hiyo ambayo itaamua kama mchezaji huyo aitwaye PARK JONG-WOO atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kutokana na kitendo chake hicho alichokifanya mwishoni mwa mchezo wa kugombea nafasi ya tatu dhidi ya Japan, imekuwa ikishindwa kutoa uamuzi wakati ilipokutana Octoba kusikiliza kesi hiyo. Msemaji wa FIFA amesema kuwa hata kama uamuzi utafikiwa hii leo hautatangazwa kwa siku kadhaa mpaka ripoti kamili iweze kuandikwa na kutafsiriwa kabla ya kutolewa kwa wandishi wa habari. Kiungo huyo alishika bango lenye ujumbe ambao unaokumbushia tofauti za mipaka kati Korea Kusini na Japan wakati akishangilia ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya mahasimu wao hao. PARK alizuiwa kuhudhuria sherehe za kukabidhiwa medali ya shaba waliyopata lakini Chama cha Soka cha Korea-KFA mwezi uliopita kilitoa taarifa kuwa wametumiwa ujumbe kupitia kamati ya nchi iliyoandaa michuano ya olimpiki ikithibitisha kuwa mchezaji huyo atapokea medali yake.

Monday, November 19, 2012

CHAMPIONS LEAGUE...

MATUMAINI ya klabu ya Juventus kusonga mbele katika hatua ya timu 16 bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inaweza kuamuliwa katika mchezo dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Chelsea baadae leo. Baada ya miaka kadhaa kupita bila kushiriki michuano hiyo Juventus wanaojulikana kwa jina la utani la bibi kizee wa Turin ambao wamewahi kushinda taji la michuano hiyo mara mbili walijihakikishia nafasi ya kushiriki tena michuano hiyo baada ya kunyakuwa taji lao la 28 la Ligi Kuu nchini Italia. Lakini kampeni zao katika michuano hiyo ya Ulaya imekuwa ikisuasua baada ya kutoa sare michezo mitatu na kufanikiwa kushinda mmoja dhidi ya Nordsjaelland wiki iliyopita katika kundi H na kujiweka katika mahali pagumu kusonga mbele. Baadhi ya michezo mingine ya mihuano hiyo itakayochezwa leo ni pamoja na Spartak Moscow itaikaribisha Barcelona, BATE itacheza na Lille, Bayern Munich watakuwa wageni wa Valencia, Benfica itaikaribisha Celtic wakati Manchester United nao watakuwa wageni wa Galatasaray.

TOURE AONGOZA KWA KULIPWA FEDHA NYINGI AFRIKA.

KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure ametajwa kama mwanamichezo kutoka Afrika anayelipwa fedha nyingi zaidi katika orodha ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani iliyotolewa na gazeti la Forbes hivi karibuni. Toure mwenye umri wa miaka 29 anashika namba 73 katika orodha ya wachezaji wanaolipwa zaidi duniani akiwa sambamba na mchezaji wa mpira wa kikapu kutoka Marekani Tim Duncan ambao wote kwa pamoja wanakusanya kiasi cha dola milioni 19.1 kwa mwaka. Kiungo huyo ambaye anacheza katika klabu ya Manchester City na mcheza gofu Ernie Els kutoka Afrika Kusini ndio waafrika pekee katika orodha hiyo ya wanamichezo 100 wanaolipwa zaidi iliyotolewa na gazeti hilo. Toure ambaye ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 2011 ana mkataba wa miaka mitano na City unaomuwezesha kukusanya kiasi cha dola milioni 16.6 ukijumlisha na dola milioni 2.5 kwa ajili ya matangazo unapata dola milioni 19.1 anazokusanya kwa mwaka. Katika orodha hizo inaongozwa na bondia kutoka Marekani Floyd Mayweather akikusanya kiasi cha dola milioni 85 akifuatiwa na bondia mwingine kutoka Philippines Manny Pacquiao anayekusanya kiasi cha dola milioni 62. Wanamichezo wengine na kiasi wanachokusanya ni pamoja na Tiger Woods dola milioni 54.9, LeBron James dola milioni 53, Roger Federer dola milioni 52.7, Kobe Bryant dola milioni 52.3, Phil Mickelson dola milioni 47.8. Wengine ni David Beckham dola milioni 46, Cristiano Ronaldo dola milioni 42.5 na Peyton Manning dola milioni 42.4 anayefunga orodha ya wanamichezo 10 bora wanaolipwa zaidi duniani.

DJOLIBA, LEOPARDS ZATOKA SARE YA MABAO 2-2 KATIKA FAINALI YA KWANZA YA KOMBE LA SHIRIKISHO.

TIMU ya Djoliba ya Mali imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya AC Leopards ya Congo katika fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa jijini Bamako jana usiku. Wageni Leopards ndio walikuwa wa kwanza kuona lango la wenyeji wao dakika ya 21 kupitia kwa mchezaji Rochel Fernand kabla ya Alou Bagayoko kuisawazishia Djoliba kwa penati dakika 10 baadae na kunyanyua matuamaini ya mashabiki wengi waliojitkeza kuishangilia timu yao katika Uwanja wa 26 Mars. Kipindi cha pili wenyeji walionyesha juhudi za kutafuta ushindi kwa kushambulia lango la wapinzani kasi na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 73 baada ya beki wa Djoliba kuifungia bao la kuongoza na kuwafanya mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kulipuka kwa furaha. Zikiwa zimebakia dakika tano kabla ya mpira kumalizika Heritier Ngouelou wa Leopards aliwanyamazisha mashabiki waliokuwa wakijua wameshinda mchezo huo kwa kufunga bao la kusawazisha. Matokeo hayo yatakuwa sio mazuri kwa Djoliba ambao wiki ijayo watasafiri kuelekea jijini Dolisie kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Leopards, mchezo ambao utaamua bingwa wa Kombe la Shirikisho kwa mwaka huu.

HAMILTON ASHINDA MBIO ZA GRAND PRIX ZA MAREKANI.

DEREVA nyoya wa Langalanga, Lewis Hamilton wa timu ya McLaren amefanikiwa kushinda mbio za Marekani za Grand Prix baada ya kufanikiwa kumpita katika dakika mwisho Sebastian Vettel wa timu ya Red Bull. Katika mashindano hayo Hamilton alionekana kumfukuza kwa karibu Vettel toka mwanzo na baadae kufanikiwa kumpita ikiwa imebakia mizunguko 14. Nafasi ya tatu katika mashindano hayo ilishikwa na Fernando Alonso wa timu ya Ferrari hivyo kufanya mbio za ubingwa mwaka huu kuwa wazi kwa kubakisha alama 13 nyuma ya kinara Vettel. Mashindano ya mwisho yatakayofanyika nchini Brazil mwishoni mwa wiki ijayo ndio yatakayoamua bingwa wa dunia kwa msimu huu.

NYOTA WA ZAMANI WA UNITED AFARIKI DUNIA.

NYOTA wa zamani wa klabu ya Manchester United ambaye ni mmoja wa wachezaji waliopona katika ajali ya ndege iliyotokea jijini Munich, Ujerumani mwaka 1958, Kenny Morgans amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73. Katika taarifa iliyotumwa katika tovuti ya United imebainisha kuwa Morgans alikimbizwa hospitali Jumamosi baada ya kuugua ghafla na baadae kufariki dunia katika hospitalini. Nyota huyo ambaye alikuwa winga alianza rasmi kucheza katika kikosi cha kwanza cha United katika mchezo dhidi ya Leicester City Desemba mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 18. Morgans aliumia wakati ndege iliyokuwa imepakia wachezaji wa United wakitokea jijini Belgrade kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Ulaya wakati walipopata ajali hiyo baada ya kujaza mafuta jijini Munich na kuua watu 23 kati ya 44 waliokuwepo katika ndege hiyo. Katika ajali hiyo Morgans alipatikana baadaye joni akiwa amebanwa kwenye viti vya ndege hiyo na waandishi wawili wa Ujerumani na baadae alifanikiwa kupona na kurejea tena uwanjani kabla ya kuhama Old Traford mwaka 1961 kwenda Swansea City.