Tuesday, January 21, 2014

ANELKA AKABILIWA NA ADHABU KUTOKA FA.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya West Bromwich, Nicolas Anelka atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa mechi tano kama akipatikana na hatia na Shirikisho la Soka nchibni Uingereza, FA kwa kuonyesha ishara ya quenelle. Anelka alionyesha ishara hiyo ambayo inadaiwa kutumika salamu ya wafuasi wa Nazi, wakati alipofunga bao dhidi ya West Ham United Desemba 28 mwaka jana. Wadhamini wa West Brom kampuni ya Zoopla wamepanga kukatisha udhamini wao na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu kutokana na ishara hiyo aliyoonyesha Anelka. Katibu wa mashabiki wa klabu hiyo, Alan Cleverley amesema kama Anelka akikutwa na hatia ya kufanya kitendo hicho cha kibaguzi atakuwa anastahili adhabu yoyote atakayopewa kwasababu vitendo hivyo haviruhusiwi katika soka.

CAMEROON KUJENGA VIWANJA VIPYA KWA AJILI YA AFCON 2019.

WAZIRI wa michezo wa Cameroon, Adoum Garoua ametangaza ujenzi wa viwanja viwili vipya kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019 ambapo nchi hiyo inategemea kuwa mwenyeji baada ya kutuma maombi ya kuandaa michuano hiyo Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF. Kampuni moja ya China imepewa tenda ya kuandaa michoro ya viwanja viwili ambao utajumuisha mmoja wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 katika wilaya ya Olembe katika mji mkuu wa nchi hiyo Yaounde. Waziri huyo amesema viwanja vilivyopo jijini Yaounde, Douala na Garoua vitafanyiwa ukarabati ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kufanyia marekebisho miundo mbinu ya michezo. Cameroon imewahi kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika mara moja pekee mwaka 1972 ambapo Congo walinyakuwa taji hilo.

RIBERY AMCHANA RONALDO KUWA HAKUSTAHILI BALLON D'OR.

NYOTA wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery ameponda tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2013 na kudai kuwa mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo hakuistahili kushinda tuzo hiyo kwasababu hajashinda taji lolote mwaka uliopita. Katika tuzo hizo Ribery alijikuta katika nafasi ya tatu nyuma ya Ronaldo na Lionel Messi wa Barcelona na kueleza tuzo za mtu mmoja mmoja sio vitu anavipa kipaumbele sana. Hata hivyo Ribery amesema anadhani alistahili tuzo hiyo kufuatia mafanikio makubwa aliyiopata akiwa na Bayern mwaka jana. Ribery amesema alishinda kila kitu akiwa na Bayern na pia peke yake ambapo kwa upande mwingine Ronaldo hakushinda kitu chochote ndio anadhani alistahili zaidi tuzo hiyo kuliko Ronaldo. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliendelea kudai kuwa ilikuwa ni wazi Ronaldo angeshinda kwasababu muda wa kupiga kura uliongezwa kwa wiki mbili suala ambalo halijawahi kutokea kabla hivyo ulikuwa ni uamuzi wa siasa zaidi kuliko soka.

Monday, January 20, 2014

VIDIC AKIRI KUWA MAN UNITED MBIO ZA UBINGWA NDIO BASI TENA.

BEKI mahiri wa klabu ya Manchester United, Nemanja Vidic amekiri kuwa timu hiyo tayari imetoka katika mbio za ubingwa za ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Chelsea. Kipigo hicho cha United katika Uwanja wa Stamford Bridge kinakuwa cha saba msimu huu na kuwaacha wakiwa nyuma ya vinara wa ligi Arsenal kwa alama 14. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Vidic alikiri kuwa kwasasa wako mbali sana na wanatakiwa kuhamishia nguvu zao katika kutafuta nafasi ya tatu au ya nne kwenye msimamo ili waweze kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Beki aliongeza kuwa sio jambo rahisi kushindana kujua kuwa wameshindwa kutetea taji lao katika kipindi hiki lakini hawana jinsi kwani bado kuna mashindano mengine ya kushindania kama Kombe la Ligi na Ligi ya Mabingwa.

ARSENAL YAMNYATIA VUCINIC WA JUVENTUS.

KLABU ya Arsenal inatarajia kuanza mazungumzo na wakala wa mshambuliaji wa Juventus Mirko Vucinic leo ikiwa ni mipango ya kocha Arsene Wenger kujaribu kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. Wenger anataka kumchukua nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 kwa mkpo wa miezi mitano lakini Juventus wanataka kumuuza kabisa ili watumie fedha hizo kuimarisha sehemu nyingine katika kikosi chao. Wakala wa mchezahuyo wa kimataifa wa Montenegro, Alessandro Lucci anatarajiwa kwenda jijini London kuzungumza na Arsenal katika siku hizo chache za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili. Hata hivyo Arsenal wanaonekana hawana haraka kuhusiana na uhamisho huo ambapo Wenger yuko tayari kusubiria mpaka masaa ya mwishoni kabla ya dirisha hilo kufungwa. Timu hiyo kwasasa imebakiwa na mechi mbili pekee kwa mwezi huu, ambapo wanakabiliwa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Coventry City na mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Southampton.

VAN GAAL AKIRI TOTTENHAM KUMTAKA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal amethibitisha kuwa klabu ya Tottenham Hotspurs walimfuata baada ya kumtimua Andres Villas-Boas. Van Gaal mwenye umri wa miaka 62 sambamba na Guus Hiddink na Fabio Capello wote walitafutwa na Spurs kabla kocha wa muda Tim Sherwood hatapewa kibarua cha kuwa kocha kamili wa timu hiyo. Akihojiwa kocha huyo amesema kila mtu anajua hivyo anakiri kuwa ni kweli Spurs walimtafuta lakini hakupenda kufanya kazi kwa wakati mmoja. Van Gaal aliendelea kudai kuwa tatizo la kazi za ukocha ni kuwa wakati una muda mara nyingi nafasi huwa hazipo lakini wakati una kazi ndio nafasi nyingi za kufundisha zinatokea. Pia kocha huyo amekiri kutamani kufundisha soka katika Ligi Kuu nchini Uingereza lakini hilo litakuwa baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Dunia.

CHAN 2014: WENYEJI BAFANA BAFANA WAAGA MASHINDANO.

TIMU ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles wamewafungisha virago wenyeji Afrika Kusini au Bafana Bafana kwa kuitandika kwa mabao 3-1 katika mchezo wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani uliochezwa jijini Cape Town. Ushindi huo umewafanya Nigeria kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi A wakiwa na alama sita nyuma ya Mali ambao wamemaliza kama vinara wa kundi hilo. Kocha wa Bafana Bafana Gordon Igesund amekiri kuwa kikosi chake kimefungwa kihalali na Nigeria na kuongeza kuwa hawana la kujitetea kutokana na hilo. Hata hivyo kocha huyo alipuuza suala la kujiuzulu na kudai kuwa ataendelea kukifundisha kikosi hicho mpaka mkataba utakapomaliza Juni mwaka huu. Michuano hiyo inaendelea tena leo jioni katka kundi B ambapo Burkina Faso itachuana na Zimbabwe huku Morocco wakicheza na Uganda, timu zote zina nafasi ya kusonga mbele kama zikifanikiwa kushinda mechi zao.