Thursday, November 20, 2014

KOCHA WA TOGO AKUBALIA KUSHINDWA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Togo, Tchakala Tchanile amekiri kuwa timu yake walifungwa na timu bora baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Ghana katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani. Kiwango cha chini kilichoonyeshwa na Togo katika mchezo huo uliofanyika huko Tamale mji uliopo kaskazini wa Ghana ulipelekea kuipa nafasi Black Stars kujikatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo. Tchanile alikipongeza kikosi cha Ghana kwa mchezo mzuri na kuonyesha nia ya kupambana kuanzia mwanzo wa mchezo mpaka mwisho. Kocha huyo amesema Ghana walionekana toka mwanzo kuwa wanataka kushinda katika mchezo huo na anadhani wachezaji wote 11 uwanjani walifanya juhudi kuhakikisha wanashinda. Kwa matokeo hayo Togo imeshindwa kufuzu michuano hiyo itakayofanyika mwakani huko Guinea ya Ikweta.

ALIYEJITANGAZA SHOGA NBA ASTAAFU.

MCHEZAJI wa kwanza aliyejitangaza kuwa shoga katika Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani Jason Collins ametangaza kustaafu rasmi mchezo huo. Collins mwenye umri wa miaka 35 alijitangaza kuwa ni shoga wakati akiichezea timu ya Brooklyn Nets msimu uliopita. Nyota huyo ambaye hakujumuishwa katika kikosi cha msimu huu amesema mwili wake umeshafikia hatua ya mwisho ndio maana ameamua kuchukua hatua hiyo ngumu. Kabla ya kustaafu Collins amecheza NBA kwa kipindi cha miaka 13 kabla ya kujitangaza shoga Aprili mwaka jana. Collins amesema anadhani kwasasa atabakia mshabiki wa mchezo huo ambao amekuwa akiupenda katika maisha yake.

SWANSEA YAMUONGEZA MKATABA WA MWAKA MMOJA BONY.

KLABU ya Swansea City imetangaza kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast Wilfried Bony. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 sasa ataendelea kusalia Swansea mpaka mwaka 2018. Bony amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka Swansea huku vilabu vya Liverpool, Arsenal na Tottenham Hotspurs zikitajwa kutaka kumsajiali. Meneja wa Swansea Garry Monk amesema amefurahishwa kumbakisha nyota huyo kwani amekuwa sehemu muhimu katika kikosi chake hicho. Bony ambaye aliiongoza Ivory Coast katika michuano ya Kombe la Dunia June mwaka huu, amefunga mabao 25 akiwa na Swansea msimu uliopita huku akifunga mengine manne katika mechi 11 msimu huu.

NYOTA WA NBA AFUNGIWA MECHI 24 KWA KUMPIGA MPENZI WAKE.

MCHEZAJI nyota wa mpira wa kikapu wa timu ya Charlotte Hornets Jeffery Taylor amefungiwa kucheza mechi 24 bila kulipwa baada ya kukutwa na hatia ya kudhalilisha. Kwa mujibu wa taarifa za polisi Taylor alionekana akimbamiza rafiki wake wa kike ukutani na kumpiga mkononi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 tayari ameshakosa michezo 11 kutokea kuanza kwa msimu lakini alikuwa akilipwa hivyo sasa ataendelea kukosa mshahara mpaka atakapomaliza adhabu yake. Kamishna wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani-NBA, Adam Silver amesema matukio kama hayo yanatia doa ligi hiyo.

ALIYEFICHUA SIRI KUHUSU QATAR KUTOA HONGO AHOFIA MAISHA YAKE.

ALIYEFICHUA siri kuhusu tuhuma za rushwa kutolewa na Qatar ili kuiwezesha nchi hiyo kushinda nafasi ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 ameiambia BBC kuwa anaishi kwa hofu kutokana na hatua yake hiyo. Mwaka 2011, Phaedra al-Majid alidai kuwa maafisa wa Qatar walijitolea kuwalipa maafisa watatu wa vyama vya soka barani Afrika kiasi cha dola milioni moja na nusu ili kuiunga mkono Qatar kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa duniani. Baadaye Bi Phaedra al-Majid aliondoa tuhuma hizo, lakini sasa anasema alilazimishwa kubadili kauli yake. Amesema ameingia katika hali ya kutojitambua na kuona anaonewa kila wakati, hofu na vitisho na kudai atajiona atajiona mkosaji maisha yake yote. Kamati ya Qatar ya uandaaji wa mihuano hiyo imesema ushahidi wa Phaedra al-Majid ulitiliwa mashaka na timu ya uchunguzi ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, na kwamba tuhuma zote zilichunguzwa na kutupiliwa mbali.

Tuesday, November 18, 2014

KOCHA URENO ABAINISHA KUMPIGIA KURA RONALDO BALLON D'OR.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ureno Fernando Santos amedokeza kuwa Cristiano Ronaldo ndio mwenye nafasi ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or na kukiri kuwa amempigia kura nahodha wake huyo badala ya Lionel Messi. Ureno ina alama sita katika mechi zao tatu za kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 walizocheza mpaka sasa baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Armenia Ijumaa iliyopita huku wakikabiliwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Argentina baadae leo. Mchezo huo ni nafasi nyingine kuona Ronaldo akichuana na hasimu wake Messi ambapo safari hii watavaana katika Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester. Akihojiwa Santos alikiri kumpigia kura Ronaldo kwani anadhani msimu huu ndiye mchezaji bora wa dunia lakini pia hakuacha kusifia na ubora wa Messi.

AFCON QUALIFIER 2015:KUFA AU KUPONA KWA VIGOGO VYA AFRIKA KESHO.

MABINGWA watetezi Nigeria kesho wataongoza timu kongwe wakiwemo mabingwa mara nne Ghana na Ivory Coast katika mechi za mwisho za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon itakayofanyika Guinea ya Ikweta. Nigeria ambao walifufua matumaini yao ya kufuzu mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuichapa Congo Brazzaville sasa wanakabiliwa na kibarua cha kuhakikisha watawafunga vinara katika kundi A Afrika Kusini katika mchezo utakaofanyika katika uwanja mpya wa Akwa Ibom huko Uyo ili kujihakikishia nafasi hiyo. Afrika Kusini ambao walikuwa mabingwa wa Afcon mwaka 1996 hawajafungwa katika mechi zao tano walizocheza lakini watakwenda Uyo huku wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kushinda mara moja katika mechi 10 walizocheza na Nigeria. Congo ambao mara ya mwisho walicheza michuano hiyo miaka 14 iliyopita wanategemea sana huruma ya Afrika Kusini kwa kushinda mchezo wao dhidi ya Nigeria huku wao wakitakiwa kushinda mchezo wao dhidi ya Sudan. Ghana wanaojulikana kama Black Stars pamoja na kufungwa bao 1-0 na Uganda Jumamosi iliyopita lakini bado wanaendelea kuongoza kundi E wakiwa na alama nane na watahitaji sare yeyote katika mchezo wao dhidi ya Togo kesho ili waweze kufuzu. Kundi hilo bado liko wazi kwani Guinea na Uganda ambao wote wana lama saba bado nao wana nafasi ya kufuzu kama wakifanya vyema katika michezo yao mwisho. Katika kundi D vita vikali vimebakia kati ya Ivory Coast na DR Congo ambao watagombea nafasi ya kufuzu moja kwa moja. Ivory Coast ambao wana alama tisa tofauti ya alama tatu na DRC, watahitaji walau sare nyumbani dhidi ya Cameroon kesho ili waweze kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele. Katika kundi B Mali, Malawi na Ethiopia watakuwa wakigombea nafasi moja iliyobakia ya kufuzu baada ya Algeria kuwa tayari wameshachukua nafasin ya kwanza.