Wednesday, January 21, 2015

WALCOTT ADAI SAFU YA USHAMBULIAJI YA ARSENAL YA SASA INATISHA KULIKO ILE KINA HENRY NA BERGKAMP MWAKA 2006.

WINGA mahiri wa kimataifa wa Uingereza Theo Walcott amedai kuwa safu ya sasa ya ushambuliaji ya Arsenal ni bora kuliko ile ya mwaka 2006. Walcott alijiunga na Arsenal mwaka huo na kucheza sambamba na baadhi ya wachezaji waliokuwepo katika kikosi ambacho kilimaliza msimu bila kufungwa mwaka 2003-2004 akiwemo Thierry Henry na Dennis Bergkamp. Lakini Walcott ambaye alitokea Southampton kabla ya kujiunga na Arsenal amesema safu ya ushambuliaji ya sasa yenye kuwajumuisha Alexis Sanchez, Olivier Giroud, Danny Welbeck na Alex Axlade-Chamberlain ndio imara zaidi. Walcott amesema kikosi cha sasa ndio bora ila wanatakiwa kuthibitisha ubora wao kwa matokeo watakayopata.

ASTON VILLA YAMKOMALIA BENTEKE.

MENEJA wa klabu ya Aston Villa, Paul Lambert amedai kuwa hawatakubali ofa yeyote kwa mshambuliaji wao Christian Benteke ili waweze kuimarisha safu yao ya ushambuliaji. Villa wako katika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa alama tatu juu ya mstari wa kushka daraja huku wakiwa wamefunga mabao 11 katika mechi 22 walizocheza. Kutoka hali ilivyo Lambert amesema hawezi kukubali kumuuza Benteke katika kipindi cha usajili wa Januari kwnai wanahitaji nguvu ili waweze kupambana na balaa la kushuka daraja. Lambert aliendelea kudai kuwa hana shaka kwamba mmliki wa Villa Randy Lerner atauelewa uamuzi wake huo kwa manufaa ya klabu. Benteke amefunga mabao mawili katika mechi 13 za Ligi Kuu alizocheza msimu huu.

BILIONEA WA CHINA AWEKEZA ATLETICO.

BILIONEA Wang Jianlin kutoka China amenunua hisa ya asilimia 20 katika klabu ya Atletico Madrid kwa kiasi cha paundi milioni 34 huku akijipanga kuongeza zaidi hisa zake katika siku za usoni. Bilionea huyo ambaye anamiliki kampuni kubwa ya Dalian Wanda anatajwa kama mmoja matajiri wakubwa wa China akiwa nyuma ya bilionea wa Alibaba Jack Ma. Kampuni hiyo itakuwa ya kwanza kutoka China kuwekeza katika klabu kubwa barani Ulaya. Wang amesema uwezkezaji huo utatoa nafasi kwa wachezaji wanaochipukia kutoka China kupelekwa Ulaya na Wanda na kusajiliwa na vilabu vikubwa. Wang pia aliendelea kudai kuwa uwekezaji huo utaimariisha soka la nchi hiyo na kupunguza pengo lililokuwepo na mataifa mengine duniani. Mabilionea kadhaa kutoka Asia wamepata muamko wa kuwekeza katika vilabu mbalimbali barani Ulaya akiwemo bilionea kutoka Malaysia Vincent Tan anayemiliki klabu ya Cardiff City. Wengine ni bilionea anayemiliki shirika la ndege la AirAsia Tony Fernandez ambaye ni mwenyekiti wa klabu ya Queens park Rangers na bilionea wa Singapore Peter Lim ambaye anamiliki hisa katika klabu ya Valencia.

ARSENAL YAMSAJILI RASMI KINDA WA LEGIA.

KLABU ya Arsenal imethibitisha kumsajili kiungo chipukizi Krystian Bielik kutoka klabu ya Legia Warsawa ya Ukraine kwa kitita cha paundi milioni 2.4. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 17 ambaye alifanyiwa vipimo vya afya wiki iliyopita alisajiliwa na Legia akitokea klabu ya Lech Poznan ya Poland Julai mwaka jana akiwa amecheza mechi sita katika mshindano yote msimu huu. Bielik ambaye amewahi kukichezea kikosi cha timu ya taifa ya Poland kwa vijana chini ya umri wa miaka 16, ana uwezo wa kucheza nafasi zote kama kiungo mkabaji au nafasi ya beki wa kati. Kuna taarifa kuwa Bielik anaweza kuingizwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal moja kwa moja kutokana na uwezo mkubwa alionao.

Tuesday, January 20, 2015

TETESI ZA USAJILI ULAYA: UNITED KUMUACHIA DE GEA KWA KITITA CHA PAUNDI MILIONI 50, HUMMELS AZIZODOA UNITED, LIVER NA CHELSEA.

KATIKA habari za tetesi za usajili barani Ulaya ni pamoja na klabu ya Manchester United imemthaminisha kwa paundi milioni 50 golikipa wake David de Gea mwenye umri wa miaka 24 ambaye anawindwa na Real Madrid. Beki wa kimataifa wa Ujerumani Mats Hummels mwenye umri wa miaka 26 amezinyong’onyesha klabu za Manchester United, Liverpool na Chelsea kwa kudai kuwa anataka kuendelea kubakia Borussia Dortmund. Nyota wa kimataifa wa New Zealand na klabu ya West Ham United Winston Reid mwenye umri wa miaka 26 ameipasha klabu hiyo kuwa hatasaini mkataba mpya kwani anataka kujiunga na Arsenal. Klabu ya Wolfburg ya Ujerumani iko tayari kutoa kitita cha paundi milioni 23 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Andre Schurrle mwenye umri wa miaka 24 lakini Chelsea wenyewe wanataka paundi milioni 30. Kiungo wa Arsenal Francis Coquelin mwenye umri wa miaka 23 anatarajiwa kupewa mkataba mpya na klabu hiyo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa toka arejeshwe kutoka Charlton Athletic alipokwenda kwa mkopo. Naye kiungo wa Manchester United Darren Fletcher mwenye umri wa miaka 30, anahusishwa na taarifa za kwenda Valencia kutokana na kushindwa kupata namba katika kikosi cha Louis van Gaal lakini anaweza kuamua kubakia Ligi Kuu kutokana an kutakiwa na klabu ya West Ham United.

ZIDANE AMPASHA POGBA KUWA WACHEZAJI BORA WOTE LAZIMA WAPITIE MADRID.

NGULI wa soka wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane amesema wachezaji bora siku zote kujiunga na Real Madrid baada ya kuhojiwa kuhusu nia yao ya kutaka kumsajili nyota Juventus Paul Pogba. Mkurugenzi wa Juventus Giuseppe Marotta amekiri Jana kuwa klabu hiyo inaweza kushindwa kumzuia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21 kwasababu ya mshahara anaoahidiwa na vilabu tajiri barani Ulaya. Marotta pia amebainisha kuwa meneja wa Madrid Carlo Ancelotti tayari ameshamfuata kuhusiana na suala la kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa. Zidane ambaye kwasasa anakinoa kikosi B cha Madrid amesema hajawahi kujaribu kumshawishi Pogba kujiunga na timu hiyo kwani hafahamiani naye kwa karibu. Lakini Zidane aliendelea kudai kuwa siku zote wachezaji bora lazima waende Real Madrid.

CARRAGHER AWASHUSHUA WACHEZAJI WA ARSENAL.

BEKI wa zamani wa klabu ya Liverpool, Jamie Carragher amewakosoa wachezaji wa Arsenal kwa kushangilia kwao baada ya kuichapa Manchester City kwa mabao 2-0 katika Uwanja wa Etihad Jumapili iliyopita. Mabao yaliyofungwa na Santi Cazorla na Olivier Giroud yalitosha kuwapa Arsenal ushindi dhidi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kikiwa ni kipigo cha kwanza katika mechi 12 walizocheza. Baada ya mchezo huo Aaron Ramsey na Alex Oxlade-Chamberlain wote walituma picha zikiwaonyesha wakishangilia katika mitandao ya kijamii jambo ambalo halijamfurahisha Carragher. Carragher amesema haikatazwi kushangilia lakini sio timu nzima kama walivyofanya wakati hakuna taji lolote waliloshinda mpaka sasa hivyo anadhani wanapaswa kuacha. Carragher pia alishangazwa na aina ya mchezo uliotumiwa na meneja Arsene Wenger katika mchezo huo kwani alikuwa akizuia zaidi jambo ambalo sio kawaida yake kwani amezoea mchezo wa wazi.