Sunday, November 3, 2013

UZEMBE WASABABISHA PELLEGRINI KUMPIGA CHINI JOE HART.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amesema golikipa namba moja wa timu hiyo Joe Hart anahitaji muda wa kupumzika baada ya kumuacha katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Norwich City. Hali hiyo imekuja kufuatia Hart mwenye umri wa miaka 26 kufanya makosa ya kizembe katika mechi za karibuni alizocheza hivyo kuigharimu timu hiyo. Akihojiwa Pellegrini na mtandao wa timu hiyo amesema jukumu lake ni kuangalia kila wiki mchezaji gani ni bora kwa ajili ya kucheza. Kocha aliendelea kudai kuwa Hart anahitaji mapumziko na yataweza kumsadia kwasababu amecheza katika kila mechi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita na kila mchezaji hupitia kipindi kibaya. Amesema anachotakiwa kufanya Hart hivi sasa ni kujituma kwa bidii ili aweze kurejea katika kiwango chake na atakuwa pamoja nae katika kipindi chote.

VIPIGO MFULULIZO VYAMFUKUZISHA KAZI RAVANELLI.

KLABU ya Ajaccio imemtimua kocha wake Fabrizio Ravanelli baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 nyumbani kutoka kwa Velenciennes katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1. Ravanelli ambaye ni nyota wa zamani wa kimataifa wa Italia alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo Juni mwaka jana lakini ameshindwa kufanya vyema toka kuanza kwa msimu huu hatua ambao imepelekea timu hiyo kushika nafasi ya pili kutoka mikiani katika msimamo wa Ligue 1. Mara baada ya mchezo huo Ravanelli alitangaza kuondoka na kudai kuwa mchezo huo waliopoteza ulikuwa wa mwisho kwake baada ya rais wa klabu hiyo Alain Orsoni kumtimua. Katika taarifa yake Orsoni amedai kuwa alikuwa hana njia nyingine zaidi ya kumtimua kocha huyo baada ya timu kupokea vipigo vinne mfululizo.

VIJANA WAMEONYESHA UJASIRI - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekipongeza kikosi chake kwa kuonyesha ujasiri katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool jana. Arsenal ilitinga katika mchezo huo huku wakiwa wamepoteza mechi zao mbili za nyumbani moja ikiwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund na nyingine ya Kombe la Ligi dhidi ya Chelsea. Akihojiwa Wenger amesema ni muhimu kubadilika na kuwashawishi watu kwamba mnaweza kushinda mechi kubwa kama hiyo. Wenger aliendelea kudai kuwa kushinda mechi kubwa kama hiyo katika kiwango bora kama walivyocheza jana ni suala la umuhimu zaidi. Kocha huyo amesema safu yake ya ulinzi ilicheza kwa nidhamu kubwa na kuwanyamazisha nyota wa Liverpool kama Daniel Surridge, Luis Suarez, Steven Gerrard na Philipe Coutinho hivyo mabeki wanne waliocheza jana wanastahili pongezi. Arsenal itasafiri kuifuata Borussia Dortmund Jumatano ijayo na kufuatiwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Manchester United katika Uwanja wa Old Traford mwishoni mwa wiki ijayo.

WILSHERE, GIBBS HATARINI KUIKOSA DORTMUND.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa wachezaji wake Jack Wilshere na Kieran Gibbs wako katika hatihati ya kukosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund Jumatano. Wilshere ameendelea kusumbuliwa na tatizo lake la kipindi kirefu la kifundo cha mguu lilosababisha kukosa mchezo dhidi ya Liverpool wakati Gibbs yeye alitolewa katika dakika ya 78 baada ya kuumia kwenye kigimbi. Wenger amebakia katika kiza juu ya mstakabali wa wachezaji hao majeruhi na kukiri kuwa hana uhakika kama watakuwa fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Dortmund utakaofanyika huko Ujerumani. Arsenal imeongeza pengo la alama kileleni kufikia tano baada ya kuichapa Liverpool na Wenger ameonyesha kufurahishwa na kikosi chake kufuatia vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Dortmund na Chelsea.

BAYERN MUNICH YAFIKIA REKODI YA KUTOFUNGWA MECHI 36 ZA LIGI ILIYOWEKWA NA HUMBURG .

KLABU ya Bayern Munich jana ilipambana baada ya kuwa nyuma kwa bao moja katika mchezo dhidi ya Hoffenheim na kufanikiwa kushinda mabao 2-1 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Bundesliga huku wakifikia rekodi ya kucheza mechi 36 za ligi bila kufungwa. Katika mchezo huo wenyeji Hoffenheim walifanikiwa kufunga bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa kinda Niklas Sule lakini Bayern walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika tano baadae kupitia kwa Mario Mandzuki na kupelekea timu kwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu. Bao la pili la Bayern lilifungwa na Thomas Muller aliyemalizia pasi maridadi ya Franck Ribery na kuifanya timu hiyo kukaa kileleni kwa tofauti moja ya alama na Borussia Dortmund wanaoshika nafasi ya pili. Bayern haijapoteza mchezo wa ligi toka walipofungwa mabao 2-1 na Bayer Liverkusen Octoba mwaka jana na kama wakifanikiwa kushinda mchezo dhidi ya Augsburg mwishoni mwa wiki ijayo watakuwa wameipita rekodi hiyo iliyowekwa na Humburg miaka 30 iliyopita.

UKAME WA MABAO HAUMSUMBUI MESSI.

KOCHA wa Barcelona, Gerardo Martino amesema mshambuliaji nyota wa timu hiyo Lionel Messi hana wasiwasi pamoja na kushindwa kufunga katika mechi za mechi za La Liga zilizopita. Alexis Sanchez alifunga bao pekee wakati Barcelona walipowafunga mahasimu wao wanaotoka mji mmoja Espanyol kwa bao 1-0 Ijumaa iliyopita na kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa mechi 12 za ligi toka kuanza kwa msimu. Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Messi toka Agosti mwaka 2011 kutofunga bao katika mechi nne za ligi. Martino amesema nyota huyo hana tatizo lolote pamoja na kushindwa kufunga na haoni kwanini watu wanafanya kitu hicho kuwa cha ajabu. Messi amefunga mabao 223 katika mechi 217 za ligi toka aanze kuitumikia Barcelona.

MOURINHO AWAPONDA WACHEZAJI WAKE BAADA YA KIPIGO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekikosoa kikosi chake kufuatia kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Newcastle jana na kuongeza hakustahili chochote kutoka katika mchezo huo. Kama Chelsea ingepata ushindi katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Saint James Park wangeweza kukaa kileleni kwa muda lakini badala yake wamebakia katika nafasi ya pili mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa wamefungana alama 20 na Liverpool. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Mourinho amesema hakupenda kabisa mchezo waliocheza na walistahili kushindwa katika mchezo huo. Mourinho amesema walikuwa na nafasi nzuri za kufunga na kusawazisha lakini Newcastle walikuwa kimchezo zaidi kuliko wao ndio maana walistahili.