Monday, August 4, 2014

VAN GAAL KUWAPA "MAKAVU LIVE" WACHEZAJI ASIOWAHITAJI BAADA YA ZIARA YA MAREKANI.

MENEJA mpya wa klabu ya Manchester United, Luis van Gaal anatarajia kuwahabarisha wachezaji asiowahitaji uso kwa uso baada ya kumalizika kwa ziara yao ya Marekani ili kuwapa muda wa kutafuta vilabu vingine. Anderson, Nani, Javier Hernandez, Shinji Kagawa na Marouane Fellaini ni miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa ambao wako katika hatari ya kuondoka kabla ya dirisha la usajili majira ya kiangazi halijafungwa. Akihojiwa Van Gaal amesema atatoa maamuzi baada ya ziara hiyo kwasababu amewapa nafasi wachezaji wote kucheza na sasa anawafahamu kuliko ilipokuwa hapo mwanzo. Kocha huyo amesema amejaribu kumsoma kila mchezaji na anajua wapi anaowahitaji na wapi asiowahitaji hivyo atatoa uamuzi wa mwisho baada ya ziara hiyo ili kuwapa nafasi wanaoondoka kutafuta vilabu vingine vya kwenda. United inatarajiwa kuchuana na Liverpool katika mchezo wa fainali ya kirafiki ya michuano ya kimataifa itakayofanyika katika Uwanja wa Sun Life jijini Miami baadae leo.

REAL MADRID YAMNASA KIPA WA COSTA RICA.

KLABU ya Real Madrid imefanikiwa kumsajili golikipa wa kimataifa wa Costa Rica, Keylor Navas kwa mkataba wa miaka sita. Navas alikuwa nyota katika michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini Brazil mwezi uliopita kwa kuisaidia nchi yake kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anatua Santiago Bernabeu akitokea klabu ya Levante nayo ikiwa inashiriki La Liga. Inaaminika kuwa Madrid ambayo ni mabingwa wa Ulaya wametoa kitita cha paundi milioni 7.9 kwa ajili ya saini ya kipa huyo. Navas anatarajiwa kutambulishwa rasmi mbele ya mashabiki katika Uwanja wa Santiago Bernabeu kesho baada ya kufanyiwa vipimo vya afya. Golikipa huyo anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Madrid kiangazi hiki baada ya kuwasajili Toni Kroos kutoka klabu ya Bayern Munich na James Rodriguez kutoka Monaco.

VERMAELEN AKOMAA KUONDOKA ARSENAL.

BEKI mahiri wa klabu ya Arsenal, Thomas Vermaelen ameonyesha kutokuwa tayari kusaini mkataba mpta na klabu hiyo hivyo kumuweka katika nafasi ya kuondoka kiangazi hiki. Mkataba wa nahodha huyo wa Arsenal unatarajiwa kumalizika mwakani na klabu inaonyesha iko tayari kumpatia mkataba mwingine lakini mwenye hataki kuanza mazungumzo ya mkataba mpya. Kama Arsenal watashindwa kumuuza beki huyo katika kipindi cha usajili wa kiangazi, inamaanisha kuwa anaweza kufikia makubaliano ya mkataba a klabu nyingine kuanzia Januari. Arsenal wanaonekana kutotaka kumuuza nahodha wao huyo kiangazi hiki, lakini pia wanataka kuepuka uwezekano wa kukosa chochote kutoka kwake mwakani. Klabu za Barcelona, Manchester United na Napoli zote zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili beki huyo.

OBI MIKEL KUNG'ANG'ANIA CHELSEA.

KIUNGO wa kimataifa wa Nigeria, John Obi Mikael amesisitiza kuwa atabakia na kupambania nafasi yake katika kikosi cha timu ya Chelsea. Mikel alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Chelsea kufuatia ujio wa kiungo wa Serbia Nemanja Matic Januari mwaka huu. Kulikuwa na tetesi kuwa kiungo huyo angeondoka Stamford Bridge katika kipindi hiki cha usajili wa kiangazi lakini Mikel mwenye amekanusha vikali tetesi hizo. Akihojiwa Mikel amesema amekuwa na timu hiyo kwa miaka mingi kwani amekuja hapo akiwa na umri wa miaka 18 na sasa ameshafikisha 27. Nyota huyo ameendelea kudai kuwa kumekuwa na wakati na mzuri na pia wakati mbaya akiwa na wakongwe kama John Terry na Petr Cech na mara zote mambo yanapokwenda vibaya wamekuwa wakiungana pamoja kama timu na kujikwamua. Mikel amesema amekuwa akifanya mazoezi kwa nguvu kuhakikisha anarejesha makali yake ili aweze kupigania nafasi yake pindi msimu mpya wa ligi utakapoanza baadae mwezi huu.

MECHI ZA KUFUZU AFCON 2015: TANZANIA, KENYA OUT, UGANDA YATAKATA.

MECHI za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika zilizofanyika mwishoni mwa wiki zimekuwa na habari mbaya kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki baada ya Tanzania na Kenya kushindwa kusonga mbele wakati majirani zao Uganda wakifanikiwa kutinga hatua ya makundi. Kenya waliokuwa wamewakaribisha Lesotho walijikuta waking’olewa bila kutegemea baada ya kung’ang’aniwa sare ya bila ya kufungana katika mchezo uliochezwa jijini Nairobi, matokeo ambayo yalipelekea kutolewa kwa tofauti ya 1-0. Matokeo hayo yamepelekea Shirikisho la Soka nchini humo-KFF kufukuza benchi lote la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha mzaliwa wa Ubelgiji Adel Amrouche. Katika mchezo huo ambao Kenya walionyesha kuumudu vyema waliwatumia nyota wake wote akiwemo Victor Wanyama anayesakanata kabumbu katika klabu ya Southampton ya Uingereza na MacDonald Mariga anayecheza soka ya kulipwa nchini Italia. Lesotho sasa watacheza mechi zao za kufuzu katika kundi C wakiwa sambamba na timu za Angola, Burkina Faso na Gabon wakati Uganda wao watakuwa katika kundi E sambamba na timu za Ghana, Guinea na Togo. Msumbiji ambao wao waliiondosha Tanzania kwa jumla ya mabao 4-3 watakuwa katika kundi F sambamba na timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Jumla ya nchi 28 zinatarajiwa kushindana katika makundi saba kati ya Septemba, Octoba na Novemba ili kuamua nchi zitakazoungana na wenyeji Morocco kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika mwakani. Washindi wawili katika kila makundi ndio watakaofuzu kushiriki michuano hiyo.

WENGER ALALAMIKIA KUFURU YA FEDHA YA MAN CITY.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amehoji mpango uliotumika kumruhusu kiungo wa zamani wa Chelsea Frank Lampard kujiunga na Manchester City kwa mkopo kutoka timu ya New York City FC ambayo inamilikiwa na City. Mbali na Lampard kwenda Etihad Stadium, New York pia imempeleka kwa mkopo mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania David Villa katika timu ya Melbourne City ya Australia ambapo vilabu vyote vitatu vinamilikiwa na City. Wenger ambaye kikosi chake kitakwaana na City mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa Ngao ya Hisani anadhani kuwa mahusiano baina ya vilabu hivyo inaweza kuipa uwiano usiofaa mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Kauli hiyo Wenger imekuja baada ya kuhojiwa kuhusiana na uhamisho wa Lampard, ambapo amesema ameshangazwa lakini inavyoonekana vilabu hivyo vitakuwa vikiilisha Man City kwani amesikia kuwa wana mpango wa kununua vilabu vitano kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wenger amesema hafahamu vyema sheria zilivyo kwani kwasasa wachezaji wanaowasajili hawawezi kucheza mpaka mwakani hivyo wanawachukua halafu wanawapeleka kwa mkopo.

MICHUANO YA MADOLA YAMALIZIKA RASMI GLASGOW.

MASHINDANO ya Jumuiya ya Madola yamemalizika jana jijini Glasgow, Scotland huku mji huo ukimiminiwa sifa kem kem kwa kuandaa mashindano yaliyofana. Sifa hizo zilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Mashindano ya Jumuiya ya Madola Mike Hooper kwa kuandaa mashindano hayo. Baada ya siku 11 ya matukio mbali mbali ya michezo 17 hatimaye sherehe za ufungaji wa mashindano zilifanyika katika uwanja wa Hampden Park jana usiku huku wenyeji wa mashindano hayo Scotland wakimaliza wakiwa nafasi ya nne kwa kunyakua medali za dhahabu 19. Uingereza ndio wameibuka kidedea kwa mara ya kwanza tangu miaka 28 iliyopita kwa kunyakuwa medali 58 za dhahabu wakifuatiwa na Australia katika nafasi ya pili wakiwa na medali 49 za dhahabu na Canada wako katika nafasi ya tatu kwa kuchukua medali 32 za dhahabu. Kwa upande wa Afrika, nchi ya Afrika Kusini ndio imeongoza kwa kuwa katika nafasi ya saba baada ya kuchukua medali 13 za dhahabu, wakifuatiwa na Nigeria wenye medali 11 za dhahabu huku Kenya wakifuatia kwa karibu kwa kuchukua medali 10 za dhahabu. Katika mashindano hayo Tanzania ambayo iliwakilishwa na wanamichezo 39 hawakuambulia chochote hivyo kupelekea kurudi nyumbani wakiwa mikono mitupu.