Tuesday, September 23, 2014

WALCOTT KUREJEA UWANJANI OCTOBA.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uingereza, Theo Walcott anatarajiwa kurejea uwanjani tena uwanjani kuitumikia timu yake ya Arsenal Octoba baada ya kukaa nje kwa miezi 10 kutokana na majeruhi goti. Walcott anatarajiwa kurejea baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa ambapo Uingereza itacheza na San Marino Octoba 9 na Estonia siku tatu baadae. Walcott mwenye umri wa miaka 25 aliumia goti lake la kushoto wakati wa mchezo wa Kombe la FA mzunguko wa tatu dhidi ya Tottenham Hotspurs Januari mwaka huu. Majeruhi hayo yalipeleka kukosa michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Brazil. Kama akifanikiwa kurejea uwanjani mwezi ujao, anaweza kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kitakachoachuana na Slovenia katika mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya Novemba 15.

MECHI ZA LIGI KUU UGANDA KUSIMAMA KWA DAKIKA KWA HESHIMA YA MCHEZAJI ALIYEAGA DUNIA AKITIZAMA MECHI CITY NA CHELSEA.

VILABU vinavyoshiriki Ligi Kuu nchini Uganda vinatarajia kusimama kwa dakika moja na kuvaa vitambaa vyeusi kabla ya kuanza kwa mechi zao wiki hii kwa heshima beki wa timu ya Simba Fahad Musana aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita. Musana mwenye umri wa miaka 24 alifariki dunia Jumapili wakati akitizama mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza kati ya Manchester City na Chelsea timu ambayo ni anaishabikia. Taarifa zinadai kuwa Musana ambaye alizikwa leo nyumbani kwake katika wilaya ya Iganga alifariki kwa shinikizo baada ya timu yake ya Chelsea kufungwa bao la kusawazisha dakika za mwisho wakati wengine wanadai alikuwa ameshafariki wakati Frank Lampard akiisawazishia City. Jambo lingine linalohusishwa na kifo cha mchezaji huyo ni katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Entebe uliochezwa Jumamosi iliyopita ambapo Musana aligongwa kichwani.

FIFA KUANZISHA MPANGO MPYA KUWALINDA ZAIDI WACHEZAJI.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA linatarajia kuwasilisha pendekezo katika kamati ya utendaji la kuangalia mbinu mpya za kukabiliana na majeraha ya kichwa. Kiongozi wa kamati ya tiba ya FIFA, Michel D’Hooghe aliandaa mpango huo mapema mwezi huu. Mpango huo unampa nafasi mwamuzi kusimamisha mchezo kwa dakika tatu ili daktari wa timu aweze kufanya tathmini yake uwanjani huku pia akipewa rungu la kuamua kama mchezaji anaweza kuendelea kucheza. Mapendekezo hayo yanafanana na taratibu mpya za Ligi Kuu zilizotolewa mwanzoni mwa msimu huu na ambazo pia ziliwasilishwa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA Septemba 18 mwaka huu. Kama mapendekezo hayo yakipitishwa na FIFA na UEFA, yataanza kufanya kazi kuanzia Octoba na kujumuishwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League pamoja na mechi za kimataifa.

SINA SHAKA NA GERRARD - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers amesisitiza kuwa hana mashaka na Steven Gerrard baada ya kupoteza michezo mitatu kati ya mitano ya Ligi Kuu waliyocheza msimu huu. Gerrard ambaye ni nahodha wa Liverpool alikuwa akihaha huku na kule katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya West ham United ili kuona uwezekano kama anaweza kubadilisha matokeo. Hata hivyo mambo hayakwenda kama walivyotarajia kwani mwisho wa mchezo walijikuta wamechapwa mabao 3-1 na timu hiyo. Rodgers amekaa kumshuhia lawama nahodha wake huyo kwa kudai kuwa kikosi kizima hakucheza vizuri katika mchezo huo waliopoteza. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Gerrard bado ana mchango mkubwa sana kwa timu hiyo.

MAN UNITED INAHITAJI KUTUMIA PAUNDI MILIONI 100 ZAIDI ILI WAWEZE KUSHINDA TAJI LA LIGI KUU - NEVILLE.

BEKI wa zamani wa Manchester United, Phil Neville amedai kuwa klabu hiyo inahitaji kutumia tena kitita cha paundi milioni 100 kwa ajili ya kununua wachezaji kabla ya kuanza kushindania taji la Ligi Kuu nchini Uingereza. United ilitandikwa kwa mabao 5-3 na Leicester City Jumamosi iliyopita lakini Neville amesema hakushangazwa na matokeo hayo. Neville mwenye umri wa miaka 37 amesema anajua kuwa United wametumia kitita cha paundi 150 katika usajili uliopita lakini anafikiri vipindi vingine viwili vya usajili ambavyo watahitajika kutumia kiasi kama hicho cha pesa kabla ya kuanza kufikiria kushionda taji. Meneja mpya wa United Louis van Gaal alitumia kitita cha paundi milioni 150 kuwasajili viungo Angel Di Maria, Ander Herrera na Daley Blind pamoja na mabeki Marcos Rojo na Luke Shaw wakati Mshambuliaji Radamel Falcao yeye alichukuliwa kw amkopo wa paundi milioni sita. Neville amesema United kwasasa wanapaswa kuangalia uwezekano wa kupata beki mzuri wa kati sambamba na kiungo mkabaji au mchezaji anayeweza kucheza nafasi ya kiungo wa kati. Tyler Blackett mwenye umri wa miaka 20 ndio amekuwa akicheza nafasi ya beki wa kati katika mechi tano za Ligi Kuu za United msimu huu lakini alionekana kuzidiwa na kasi ya Leicester na kutolewa nje.

HUWEZI KUMFANANISHA GOTZE NA RIBERY - BECKERNBAUER.

RAIS wa heshima wa klabu ya Bayern Munich, Franz Beckenbauer amesisitiza kuwa Mario Gotze hawezi kufananishwa na Franck Ribery kwakuwa ni wachezaji wa aina ya tofauti. Nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alihamishwa nafasi yake na kocha Pep Guardiola kutoka kati kwenda wingi ya pembeni mara kadhaa wakati Ribery alipokuwa kijiuguza. Hata hivyo, Beckernbauer haoni kama Gotze ni mchezaji muafaka kuziba nafasi ya Ribery. Nguli huyo wa soka wa zamani amesema huwezi kumuiga mtu kama Ribery kutokana na aina yake ya uchezaji ya kutanua uwanjani ili kuwavuta mabeki wa upinzani. Beckernbauer aliendelea kudai kuwa Gotze yuko tofauti na anadhani anafaa kwa mbinu za Guardiola kwani anapenda kucheza kitimu zaidi kwa kutoa pasi za haraka ila inabidi aongeze bidii kukuza kiwango chake. Gotze mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao mawili katika mechi saba za mashindano yote alizocheza za Bayern msimu huu.

KOUYATE NJE WIKI SITA.

KIUNGO wa klabu ya West Ham United, Cheikhou Kouyate atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita baada ya kupata majeruhi ya nyonga. Kouyate aliumia wakati wa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Liverpool ambapo walishinda ka mabao 3-1. Kiungo huyo huenda akakosa michezo mitano ya ligi kuu ya England iliyo mbele yao ukiwemo ule wa dhidi ya Manchester United utakaopigwa Septemba 27 mwaka huu. Kouyate alihamia West Ham akitokea Anderlect kwa kitita cha paundi milioni saba Julai na toka ametua hapo ameonyesha kiwango cha hali ya juu.