BAADA ya Yanga kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho sasa klabu hiyo ina uhakika wa kuingiza kiasi cha dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000 au zaidi kulingana na hatua watakayoishia. Yanga ambayo imekuwa timu pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kutinga hatua hiyo sasa inasubiri upangaji wa makundi ambao unatarajiwa kufanyika Jumanne Mei 24 mwaka huu. Katika hatua hii kutakuwa na timu nane ambapo mbali na Yanga lakini pia watakuwepo Etoile du Sahel ya Tunisia, TP Mazembe ya Congo DRC, Mo Bejaia ya Algeria, Madeama ya Ghana, Kawkab Marrakech ya Morocco, Al Ahly Tripoli ya Libya na Fus Rabat ya Morocco. Makundi yatakuwa mawili yenye timu nne nne ambapo mshindi wa kwanza na wa pili kutoka katika kila kundi ndio atakuwa amesonga mbele katika hatua nusu fainali. Bingwa wa michuano hii atajivunia kitita cha dola 625,000 sawa na shilingi 1,366,250,000 huku mshindi wa pili katika fainali akikunja kitita cha dola 432,000 sawa na shilingi 944,352,000. Mshindi wa pili na wa tatu kutoka katika makundi kila mmoja atapata dola 239,000 sawa na shilingi 522,454,000 na wa nne atakunja dola 150,000 sawa na shilingi 327,900,000.
Thursday, May 19, 2016
KLOPP AKUBALI LAWAMA.
MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amekubali kutupia lawama kufuatia kipigo cha mabao 3-1 walichopata kutoka kwa Sevilla katika mchezo wa fainali ya Europa League na kudai kuwa watarejea wakiwa imara zaidi. Liverpool walianza vyema mchezo huo kwa kuongoza lakini walijikuta wakipoteana katika kipindi cha pili na kuipa mwanya Sevilla kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo. Kipigo hicho pia kinamaanisha Liverpool hawatashiriki michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao. Akihojiwa Klopp ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Liverpool Octoba mwaka jana, amesema kikosi chake kilicho kwa asilimia 50 mpaka 60 ya kiwango chao cha kawaida na wanatakiwa kukubaliana na hilo. Klopp aliongeza kuwa anawajibika kwa kikosi chake kucheza kwa kiwango hicho na kuahidi kuwa watatumia kama mfano ili wakirejea wawe imara zaidi.
MABINGWA LEICESTER KUONGEZA WATATU KIANGAZI.
MAKAMU mwenyekiti wa Leicester City, Aiyawatt Srivaddhanaprabha amedai klabu hiyo inatarajia kusajili wachezaji watatu au wanne katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi ili waweze kujiimarisha kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ubingwa Ligi Kuu uliwafanya Leicester kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu uja ikiwa ni mara yao ya kwanza. Leicester pia watashiriki michuano ya Kombe la Kimataifa litakalofanyika kipindi hiki cha kiangazi na wanatajia kupambana na bingwa wa Kombe la FA katika mchezo wa Ngao Hisani. Akizungumza wakiwa nchini Bangkok walipokwenda kwa ziara makamu mwenyekiti huyo amesema wanafurahia kikosi walichonacho hivi sasa lakini msimu ujao wana mashindano mengi zaidi hivyo inabidi waongeze baadhi ya wachezaji ili kujiimarisha.
RONALDO, RODRIGUEZ KUIKOSA OLIMPIKI.
NYOTA wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na James Rodriquez wanatarajiwa kuikosa michuano ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu nchini Brazil. Ronaldo nahodha wa Ureno na Rodriguez anayeiwakilisha Colombia wote hawatarajiwi kuteuliwa katika vikosi vitakavyotumika kwa ajili ya michuano hiyo kwasababu ya ushiriki wao katika michuano ya Euro 2016 na baadae Copa America. Kocha wa kikosi cha Olimpiki cha Ureno Rui Jorge amesema pamoja na kwamba hajafanya maamuzi ya wachezaji gani waliozidi umri wa miaka 23 atakaowatumia katika michuano hiyo lakini hadhani kama Ronaldo atakuwa mmoja wapo. Kwa upande wa Rodriquez, rais wa Chama cha Soka cha Colombia, Ramon Jesurun amesema tayari nyota huyo ameshafanya maamuzi kuwa atacheza Copa America badala ya Olimpiki.
MKATABA MPYA WA NIKE WAIPA JEURI BARCELONA YA KUWAONGEZA MKATABA NEYMAR NA BUSQUETS.
KLABU ya Barcelona inadaiwa kuwa tayari imeanza kuweka sawa mipango yao ya baadae baada ya kutwaa taji lao la sita la La Liga katika kipindi cha miaka nane Jumamosi iliyopita. Utawala wa soka wa Barcelona nchini Hispania unaonekana hautaweza kuisha katika siku za karibuni kwani tayari wanadaiwa kufikia makubaliano ya mikataba mipya kwa nyota wake Neymar na Sergio Busquets pamoja na wadhamini wao kampuni ya vifaa vya michezo ya Marekani, Nike. Neymar anadaiwa kufikia makubaliano ya awali ya nyongeza ya mkataba ambao utadumu mpaka mwaka 2021 na kufanya nyongeza ya kuvunja mkataba huo kuongezeka mpaka kufikia dola milioni 213. Barcelona wana matumaini mkataba huo mpya Neymar atausaini kabla ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya mabingwa wa Europa League Sevilla. Kiungo Busquets pia anatarajiwa kusaini mkataba mpya ambao utamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika orodha ya klabu hiyo. Yote hayo yanatarajiwa kuweza kufanikishwa kutokana na mkataba mpya watakaosaini na Nike ambao unakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 112 kwa mwaka ukiwa unazidi ule wa Manchester United waliosaini na kampuni ya Adidas ya Ujerumani.
TORRES ADAI HANA SHIDA NA EURO.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania, Fernando Torres amedai kuachwa kwake katika kikosi cha nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 hakujamzuia kujiandaa kwa kila kitu kwa ajili ya kuiongoza Atletico Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Torres ambaye hajaitumikia Hispania toka Kombe la Dunia mwaka 2014, amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu huku mabao ake yakiisaidia klabu yake kumaliza katika nafasi ya tatu katika msimamo wa La Liga. Mbali na kuisaidia Atletico katika La Liga lakini pia ameisaidia kutinga hatua ya fainali ambapo sasa watakwaana na majirani zao Real Madrid Mei 28 mwaka huu katika Uwanja wa San Siro jijini Milan. Pamoja na kufunga mabao 12 msimu huu, Torres mwenye umri wa miaka 32 hakuchaguliwa katika kikosi cha awali cha kocha Vicente Del Bosque kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 itakayofanyika huko Ufaransa mapema mwezi ujao. Akihojiwa Torres amesema hajali sana kuhusu Euro kwani ana mchezo mkubwa wa maisha yake atakaocheza hivi karibuni.
OFISA WA EL MERREIKH ACHUNGUZWA NA CAF KUFUATIA MADAI YA KUMPIGA MWAMUZI.
SHIRIKISHO la Soka la Afrika-CAF linamfanyia uchunguzi ofisa wa klabu ya Al Merreikh ya Sudan, Hatim Mohamed Ahmed baada ya kunaswa akimpiga mwamuzi Eric Otogo-Castane wa Gabon usoni. Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 84 ya mchezo wa jana wa Kombe la Shirikisho kati ya Merreikh na Kawkab Marrakech ya Morocco. CAF inalifanyia uchunguzi kwa karibu tukio hilo huku wakisubiri ripoti ya waamuzi. Kawkab walishinda mchezo huo kwa mabao 2-0 ambayo yote yalifungwa kwa njia ya panati na kuwafanya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.
Subscribe to:
Posts (Atom)






