MATHIEU Debuchy anatarajiwa kujiunga na Galatasaray katika muda wa siku chache zijazo baada ya Arsenal kukubali ofa ya mkopo kwa beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amecheza mechi 22 pekee toka ajiunge na Arsenal akitokea Newcastle United mwaka 2014 kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara na kupelekea nafasi yake katika kikosi cha kwanza kuchukuliwa na Hector Bellerin. Dubuchy kwasasa yuko na kikosi cha Arsenal kilichopo nchini Norway kwa ajili ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Viking FK na anatarajiwa kufanya uamuzi wa mustakabali wake baada ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya kumalizika. Nusu ya msimu uliopita, Debuchy aliutumia akiwa kwa mkopo katika klabu ya Bordeaux lakini alikosa michuano ya Ulaya baada kuumia wakati wa mchezo wa Ligue 1 dhidi ya Paris Saint-Germain Mei mwaka huu.
Friday, August 5, 2016
INFANTINO HURU BAADA YA UCHUNGUZI DHIDI YAKE KUKAMILIKA.
BARAZA la uchunguzi la Shirikisho la Soka Duniani-FIFA limekuta bila hatia ya kuvunja sheria za maadili ya shirikisho hilo, rais Gianni Infantino. Infantino alikuwa akichunguzwa kuona kama kuna uwezekano wa kuvunja sheria yeyote kwa safari alizofanya katika mwezi wake wa kwanza akiwa rais. Lakini baada ya uchunguzi uliochukua wiki kadhaa ambapo mashahidi na Infantino mwenyewe walihojiwa, baraza limeona rais huyo mwenye umri wa miaka 46 hana kesi ya kujibu. Kufuatia uamuzi huo rais na watendaji wengine wa shirikisho hilo wataendelea na shughuli zao kama kawaida kwa ajili ya maendeleo ya soka.
CITY YAPANGWA NA STEAUA MCHUJO WA LIGI YA MABINGWA ULAYA.
KLABU ya Manchester City chini ya meneja wake mpya Pep Guardiola inakabiliwa na safari ya kwenda Romania kukabiliana na Steaua Bucharest katika mzunguko wa mwisho kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mchezo wa mkondo wa kwanza City watacheza ugenini Agosti 16 mwaka huu kabla ya kurudiana Agosti 24 katika Uwanja wa Etihad. Katika mechi zingine FC Porto ya Ureno wao watapepetana na AS Roma, wakati Villarreal ya Hispania wakicheza AS Monaco ya Ufaransa. Kwingineko Young Boys ya Uswisi wao wanatarajiwa kucheza na Borussia Monchengladbach ya Ujerumani huku Ajax Amstederdam ya Uholanzi wao wakipepetana na Rostov ya Urusi ambao wanshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.
Thursday, August 4, 2016
ZIDANE AMVUTIA PUMZI RONALDO.
MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema hatakuwa na haraka ya kumrejesha uwanjani Cristiano Ronaldo kipindi ambacho amekuwa akiuguzi majeruhi ya goti aliyopata wakati akiitumikia Ureno katika michuano ya Ulaya. Ronaldo aliumia goti katika mchezo wa fainali ambao Ureno walishinda bao 1-0 katika muda wa nyongeza dhidi ya Ufaransa katika michuano hiyo mwezi uliopita na Madrid mpaka sasa hawajapata tarehe ya kurejea kwa nyota huyo. Akiulizwa kuhusu Ronaldo mara baada ya mchezo wao wa kirafiki walioshinda bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich, Zidane amesema kwasasa Ronaldo bado ni majeruhi hivyo hawana haraka ya kumrejesha mpaka hapo atakapopona vyema. Ronaldo ambaye alifunga mabao 51 katika mechi 48 za mashindano yote alizocheza msimu uliopita, yuko likizo nchini Marekani na anatarajiwa kukosa mchezo wa Super Cup ya Ulaya dhidi ya Sevilla utakaofanyika Agosti 9 mwaka huu. Nyota huyo pia anahofiwa kuukosa mchezo wa ufunguzi wa La Liga ambapo Madrid watafungua dimba na Real Sociedad Agosti 21.
MSHAMBULIAJI WA BORDEAUX AKATIKA SIKIO.
MSHAMBULIAJI wa Bordeaux, Jeremy Menez amefanyiwa upasuaji baada ya kipande cha sikio lake la kulia kukatika katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Fc Lorient jana. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ambaye amejiunga na Bordeaux akitokea AC Milan siku tatu zilizopita, alipata majeruhi hayo kufuatia kugongana kwa bahati mbaya na kiungo wa Lorient Didier Ndong dakika ya 15 ya mchezo. Katika taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo, Jeremy anadaiwa kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kushona sikio lake. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa muda wa Jeremy kurejea uwanjani utategemea jinsi sikio lake litakavyopona. Bordeaux ambao walimaliza katika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligue 1 msimu uliopita, wanatarajia kuanza kampeni zao kwa kupepetana na St Etienne Agosti 13 mwaka huu.
USAJILI WA SAKHO KWENDA WEST BROM WAKWAMA.
UHAMISHO wa mshambuliaji wa West Ham United Diafra Sakho kwenda West Bromwich Albion ka kitita cha paundi milioni 15 unadaiwa kusitishwa baada ya mchezaji huyo kufanyiwa vipimo vya afya huko The Hawthorns. Inaaminika kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Senegeal hakushindwa vipimo vya afya lakini inadaiwa asingekuwa fiti kwa ajili ya mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu. Sakho mwenye umri wa miaka 26, amefunga mabao 15 katika mechi 44 za ligi alizoichezea West Ham katika kipindi cha miaka miwili iliyopita lakini amekuakisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Ujio wake West Brom ulizua tetesi kuwa klabu hiyo inaweza kumuuza mshambuliaji wake Saido Berahino mwenye umri wa miaka 23 ambaye amekuwa akiwindwa na klabu za Crystal Palace na Stoke City.
CITY WATUPA NDOANO KWA CHIPUKIZI WA COLOMBIA.
KLABU ya Manchester City inadaiwa kukaribia kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia Marlos Moreno. City wanatarajiwa kuilipa klabu ya Atletico Nacional ya Colombia kiasi cha paundi milioni 4.75 kwa ajili ya chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 19. Hata hivyo, City wanatarajia kumpeleka kwa mkopo mchezaji huyo katika klabu ya Deportivo La Coruna. Moreno atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Pep Guardiola wiki hii kufuatia ujio wa Leroy Sane kutoka Schalke na Gabriel Jesus kutoka Palmeiras.
Subscribe to:
Posts (Atom)






