Monday, February 18, 2013

TUKIKUBALI KUFUNGWA SAN SIRO TUMENG'OKA - BOJAN.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Barcelona, Bojan Krkic anaamini kuwa kufungwa kwa klabu yake ya sasa ya AC Milan katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutakuwa kumefifisha matumaini yao ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Nyota huyo alielezea umuhimu wa Milan kuepuka kufungwa katika mchezo wa kesho usiku ambao wataikaribisha Barcelona katika uwanja wao wa nyumbani wa San Siro. Bojan amesema watakuwa wakicheza na timu bora duniani lakini wanashukuru kwakuwa wenyewe watakuwa na mashabiki watakaokuwa nyuma yao ambapo wanachotakiwa kufanya ni kupata angalau sare ili kuweka matumaini yao hai kwa mchezo wa marudiano. Bajan mwenye umri wa miaka 22 aliondoka Barcelona mwaka 2011 na kubainisha kuwa bado anawasiliana na wachezaji wenzake wa zamani ambao walimsaidia kwa namna moja au nyingine kufikia hapo alipo.

CITY WAANZA MBIO ZA KUMGOMBEA NEYMAR.

KLABU ya Manchester City yenye nguvu kubwa kifedha katika Ligi Kuu nchini Uingereza wamepiga hatua yao ya kwanza katika mbio za kumuwania mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Brazil, Neymar. Maofisa wa ngazi za juu wa klabu hiyo Ferran Soriano na Txiki Begiristain wametajwa kuanza mazungumzo ya awali na familia pamoja na mwakilishi wa nyota huyo katika Uwanja wa Wembley wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya Uingereza na Brazil uliochezwa Februari 6 mwaka huu. Ofisa Mkuu Soriano na Begiristain ambaye ni mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo walikuwa wageni waalikwa wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA katika mchezo huo. Katika mchezo huo ambao Neymar hakung’ara sana baada ya Uingereza kushinda kwa mabao 2-1 maofisa hao walionekana wakijongea karibu na mahali familia ya Neymar ilipokuwa imekaa huku mara kwa mara wakiwa katika mazungumzo na baba wa nyota huyo.

MTANIKUMBUKA NIKIONDOKA - WENGER

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amewaonya mashabiki wa klabu hiyo wanaomponda kwamba watamkumbuka wakati akiwa ameondoka. Akizungumza kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich Wenger alitetea rekodi yake toka aanze kuinoa klabu hiyo na kuwahakikishia kuwa lazima watamkumbuka wakati ataoondoka. Wenger alidai kuwa amekuwa akifundisha soka kwa kipindi cha miaka 30 na miaka 16 kati ya hiyo amefanya kazi Uingereza hivyo anastahili heshima kutokana na mafanikio mengi ambayo ameipa Arsenal katika kipindi chote. Katika kipindi cha karibuni Wenger amekataa kazi ya Kuzinoa timu za taifa za Uingereza, Ufaransa pamoja na klabu za Bayern Munich, Real Madrid na Paris Saint-Germain ambazo zote zilikuwa zikimuwania kutaka huduma yake. Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wameonyesha kuishiwa na imani na kocha huyo baada ya miaka nane kupita bila ya kushinda taji lolote huku mara ya mwisho kufanya hivyo ikiwa ni mwaka 2005 waliponyakuwa Kombe la FA.

Sunday, February 17, 2013

ALVES ASIFU KIWANGO CHA MESSI.

BEKI wa klabu ya Barcelona, Dani Alves amesifu kiwango cha mshabuliaji nyota wa klabu hyo Lionel Messi kwa kudai kuwa hufanya kazi yao kuwa rahisi pindi awapo uwanjani. Alves alijiunga katika orodha ya watu wengi waliosifia kiwango cha nyota huyo wa kimataifa wa Argentina baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-1 waliopata ugenini dhidi ya Granada. Messi alifunga bao lake la 300 na 301 kwa klabu hiyo baada ya kuwa nyuma kwa bao lililofungwa katika kipindi cha kwanza na kufanikiwa kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Alves amesema kucheza na Messi kwenye timu moja kunafanya mambo yawe rahisi zaidi kutokana na kiwango cha hali ya juu alichonacho nyota huyo hivyo kufanya matokeo kuwa mazuri baada ya dakika 90. Messi amefikisha mabao 37 katika ligi msimu huu huku wakitofautiana kwa alama 15 na Atletico Madrid ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo. 

VILANOVA YUKO KATIKA HALI NZURI - ZUBIZARRETA.

MKURUGENZI wa Michezo wa klabu ya Barcelona, Andoni Zubizarreta amesema kuwa meneja wa klabu hiyo Tito Vilanova yuko katika hali nzuri toka lianza matibabu yake huko jijini New York, Marekani. Zubizarreta alibainisha kuwa matibabu ya mionzi ili kutibu kansa ya koo inayomkabili Vilanova yanaendelea vyema na hivi karibuni anaweza kurejea kuendelea na kibarua chake kama kawaida. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 alichukua kibarua cha kukinoa kikosi cha Barcelona katika kipindi ca majira ya kiangazi lakini kabla ya nusu ya msimu aligundulika kuwa na kansa ya tezi ambayo hivi anapatiwa matibabu yake huko New York. Zubizarreta amesema kocha huyo kwasasa amerejea katika hali yake ya kawaida baada ya mionzi huku akitizama soka katika luninga kila Barcelona inapokuwa uwanjani na anashukuru watu wote wanaomuombe katika kipindi hiki kigumu.

SABC YAJITETEA KUONYESHA KIPINDI CHA STEENKAMP.

TELEVISHENI ya SABC ya nchini Afrika Kusini imetetea uamuzi wake wa kuonyesha kipindi kilichorekodia na Reeva Steenkamp, rafiki wa kike wa mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius ambaye anatuhumiwa kumuua mwanadada huyo. Muandaaji wa kipindi hicho, Samantha Moon aliliambia shirika la habari a BBC kuwa uamuzi wa kuonyesha kipindi hicho ulikuja baada ya kushauriana na familia ya mwanadada huyo ambaye aliwahi kuwa mwanamitindo. Kipindi hicho kiitwacho Tropika Island Treasure kilirekodiwa nchini Jamaica ambapo watu kadhaa hushindanishwa kugombea zawadi ya dola 113,500. Kwa upande mwingine mjomba wa Pistorius amesema jana kuwa mwanariadha huyo ambaye aliweka historia mwaka jana kwa kushiriki katika olimpiki ya watu wa kawaida pamoja na ile ya walemavu bado yuko katika mshituko na masikitiko makubwa kutokana na tukio hilo.

KENYA YAJIPANGA KUOMBA KUANDAA AFCON 2019.

KENYA inajipanga kuwa nchi ya tatu kwa upande wa Afrika Mashariki baada ya Sudan na Ethiopia kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2019. Shirikisho la Soka la Kenya-FKF limedokeza kuwa watatumia michuano ya Afrika ya Vijana watakayoandaa mwaka 2017 kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani humu. Katika taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo ilidai kuwa FKF kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana na Michezo nchini humo wanajipanga ili kutuma maombi ya kuandaa michuano ya Afcon 2019 pamoja na ile ya vijana itakayofanyika mwaka 2017. Taarifa hiyo ilidai kuwa serikali kwa kupitia wizara hiyo tayari imetoa ruhusa kwa FKF kuomba kuandaa michuano hiyo na sasa wanakabiliwa na upinzani kwa Algeria, Nigeria, Liberia, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC ambao nao wote wameomba kuandaa michuano ya kipindi hicho.