KLABU ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC imeshapiga hatua moja kufikia fainali ya Kombe la Shirikisho wakati watakapoikaribisha timu ya Stade Malien ya Mali mwishoni mwa wiki hii. Timu hizo mbili zinatarajiwa kukwaana katika mchezo wa nusu fainali ya mkondo wa pili jijini Lubumbashi kesho huku Mazembe wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-1 waliyopata katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa jijini Bamako Octoba 6. Kocha wa Mazembe Patrice Carteron amesema nusu ya kazi tayari wameshafanya lakini bado hawatawadharau wapinzania wao katika mchezo huo. Hata hivyo kuna wingu kubwa limetanda katika mchezo huo kwa Mazembe ambapo hakuna uhakika kama viungo Rainford Kalaba na Nathan Sinkala pamoja na beki Stopilla Sunzu watacheza katika mechi hiyo. Utata huo umekuja kufuatia Shirikisho la Soka la Zambia kutuma malalamiko yao Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa Mazembe kuwakatalia wachezaji kutimiza majukumu yao ya kimataifa.
Friday, October 18, 2013
OZIL, SAGNA NA CAZORLA WAKO POA - WENGER.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa nyotwa wake Mesut Ozil, Bacary Sagna na Santi Cazorla wote wako fiti kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Norwich City. Kulikuwa na wasiwasi wa nyota hao kukosekana baada ya Ozil kutolewa nje kwa maumivu katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia kati ya Ujerumani na Sweden wakati Sagna na Cazorla wenye walikuwa majeruhi kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa. Lakini Wenger aliwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kudai kuwa nyota hao pamoja na kikosi kizima cha timu hiyo wako fiti tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi. Cazorla ambaye alikuwa majeruhi kwa muda alianza kufanya mazoezi rasmi na timu hiyo wakati wa mapumziko wa mechi za kimataifa.
DROGBA ATUNUKIWA TUZO YA GOLDEN FOOT.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba ametunukiwa tuzo ya Golden Foot jijini Monaco, Ufaransa. Drogba mwenye umri wa miaka 35 ambaye anakipiga katika klabu ya Galatasaray ya Uturuki alipokea tuzo hiyo kutoka kwa Mwana wa Mfalme wa Monaco tuzo ambayo hutunukiwa wachezaji wenye umri wa miaka 28 na zaidi ambao bado wanacheza. Nyota huyo pia anakuwa mchezaji wa pili aliyecheza katika Ligi Kuu nchini Uingereza kutunukiwa tuzo hiyo baada ya Ryan Giggs wa Manchester United. Drogba anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kupata tuzo hiyo ambayo mwaka uliopita ilikuwa ikishikiliwa na mshambuliaji nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain Zlatan Ibrahimovic.
Thursday, October 17, 2013
SABA BORA KATIKA ORODHA ZA FIFA KUONGOZA DROO ZA UPANGAJI RATIBA YA KOMBE LA DUNIA BRAZIL.
SWITZERLAND itakuwa mojawapo ya nchi nane zitakazoongoza droo ya ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 itakayofanyika Desemba mwaka huu baada ya kukwea mpaka nafasi ya saba katika orodha za ubora dunia zilizotangazwa leo. Hispania, Argentina, Ujerumani, Colombia, Ubelgiji na wenyeji Brazil nao pia wataongoza droo hiyo wakiungana na Uruguay kama wakifanikiwa kuwafunga Jordan katika mechi za mikondo miwili za mtoano mwezi ujao. Kama Uruguay ikishindwa kufuzu michuano hiyo, Uholanzi ambao wanashika nafasi ya nane katika orodha hizo sambamba na Italia itachukua nafasi hiyo. Katika kanuni za Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Brazil ukijumlisha na timu saba zilizopo katika orodha za juu za shirikisho hilo ndio zitaongoza droo ya upangaji ratiba ya michuano hiyo.
TANZANIA YAENDELEA KUSUASUA VIWANGO FIFA.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetoa orodha mpya ya viwango vya ubora kwa mwezi huu huku Tanzania ikizidi kudidimia kwa kuporomoka kwa nafasi mbili. Katika orodha hizo Tanzania imeshuka mpaka katika nafasi ya 129 kutoka nafasi ya 127 waliyokuwepo mwezi uliopita. Kwa upande wa Afrika Ivory Coast wameendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya 17 katika orodha hizo duniani wakifuatiwa na Ghana ambao wanashika nafasi ya 23 huku Algeria nao wakiwa katika nafasi ya 32. Mabingwa wa Afrika Nigeria wanashika nafasi ya nne kwa kushika nafasi ya 33 na tano bora kwa upande wa Afrika inafungwa na Mali walioko katika nafasi ya 41. Mabingwa wa dunia Hispania wameendelea kubaki katika nafasi ya kwanza kwenye orodha hizo wakifuatiwa na Ujerumani waliopanda mpaka nafasi ya pili na kuiondoa Argentina iliyopo katika nafasi ya tatu. Nafasi ya nne katika orodha hizo inashikiliwa na Colombia ambao wamepanda kwa nafasi moja kulinganisha na walipokuwa mwezi uliopita huku Ubelgiji wakifunga tano ya orodha hizo.
ABOUTRIKA KUTUNDIKA DARUGA.
MKONGWE Mohamed Aboutrika anayechezea klabu ya Al Ahly ya Misri anatarajia kutundika daruga mwaka huu. Kwa mujibu wa luninga ya Al-Ahly ,Aboutrika mwenye miaka 34 atastaafu baada ya Al Ahly kukamilisha kibarua chake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika watakapochuana na Coton Sport ya Cameroon Jumapili ijayo katika mechi ya mkondo wa pili. Kama Al Ahly watafuzu watakutana na Esperance ya Tunisia au Orlando Pirates ya South Africa kwenye hatua ya fainali ya mikondo miwili itakayochezwa November mwaka huu. Mkongwe huyo ni mmoja wa wachezaji bora Africa ambaye hakuwahi kucheza Ulaya ambapo alikuwepo katika kikosa cha timu ya taifa ya Misri kilichogaragazwa na Ghana kwa mabao 6-1 katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kushiriki KOmbe la Dunia 2014.
WAZIRI WA MICHEZO BRAZIL KUJIUZULU.
WAZIRI wa michezo wa Brazil, Aldo Rebelo anatarajiwa kujiuzulu Desemba mwaka huu ikiwa imebaki miezi sita kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia ambayo imeandaliwa na nchi hiyo. Rebelo amesema atajiuzulu nafasi hiyo ili aje mtu mpya baada ya kukabidhi viwanja 12 ambavyo vitatumika kwa ajili ya michuano hiyo, vinavyotarajiwa kukamilika Desemba. Mwaka uliopita Rebelo aliingia katika mzozo wa kidiplomasia na kugoma kuonana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Jerome Valcke baada ya katibu huyo kuponda maandalizi ya nchi hiyo na kudai kuwa wanahitaji msaada. Rebelo amesema sababu kubwa ya kujiuzulu ni kwa ajili ya kujiandaa ili aweze kuogombea kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Octoba mwakani.
Subscribe to:
Posts (Atom)






