Tuesday, November 19, 2013

TAJIRI WA LIVERPOOL AMTUMIA NDEGE BINAFSI SUAREZ ILI AWAHI MECHI DHIDI YA EVERTON.

MMILIKI wa klabu ya Liverpool John W Henry ametoa ndege yake binafsi kwa ajili ya kuharakisha ujio Luis Suarez kabla ya mchezo dhidi ya mahasimu wao Everton Jumamosi. Kwasasa Suarez yuko nchini Uruguay katika akiitumikia timu yake ya taifa katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya mtoano kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani dhidi ya Jordan unaotarajiwa kuchezwa kesho. 
Kwa upande mwingine unaweza sema Uruguay wameshafuzu michuano hiyo kwani katika mechi ya mkondo wa kwanza waliibugiza Jordan kwa maba 5-0. Liverpool inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Everton Jumamosi mchana katika Uwanja wa Goodison Park na ili kuhakikisha mshambuliaji anapata muda wa kupumzika wa kutosha, Henry ameamua kumtumia usafiri huo binafsi ili kumuwahisha.

AMNESTY INTERNATIONAL YAIKALIA KOONI QATAR.

KAMATI ya maandalizi ya michuano ya Kombe Dunia itakayofanyika nchini Qatar 2022, imedai kufanya mazungumzo na shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International. Hatua hiyo imekuja kufuatia shirika hilo kudai kuwa kampuni za ujenzi za nchi hiyo zinawanyanyasa wafanyakazi wa kigeni. Kamati hiyo imedai kuwa itashughulikia suala hilo ili kuhakikisha wafanyakazi hao wanapata haki yao bila ya kunyanyaswa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Kamati iliendelea kudai kuwa kampuni za ujenzi itabidi kukubaliana na sheria mpya za ustawi wa wafanyakazi watakazoweka kwasababu wanatambua mchango wa Amnesty.

BECKHAM, LEBRON JAMES KUANZISHA TIMU YA SOKA MIAMI.

MCHEZAJI nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani LeBron James amethibitisha kuwa yuko katika mazungumzo na David Beckham kwa ajili ya mipango ya baadae ya kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Marekani-MLS kutoka Miami. Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, ambaye aliweka kipengele cha kuwa na uwezo wa kununua timu katika mkkataba wake wakati aliposaini klabu ya Los Angeles Galaxy mwaka 2007, tayari ameshakutana na viongozi wa MLS Octoba kuangalia uwezekano wa kuanzisha timu huko Florida. 
James, ambaye anamiliki hisa katika klabu ya Liverpool amethibitisha kuzungumza na Beckham kuhusu uwezekano wa kuirejesha MLS katika mji wa Miami na ana uhakika mpango wao huo utakuwa na mafanikio. James amesema Beckham amekuwa rafiki yake kwa miaka kadhaa iliyopita na pia anadhani itakuwa ni jambo zuri jiji hilo kuwa na timu yake ya soka. Mara ya mwisho jiji la Miami kuwa na timu MLS ilikuwa mwaka 2002 wakati timu Miami Fusion iliposhushwa daraja baada ya misimu minne pekee.

DESCHAMPS HAPASWI KULAUMIWA KAMA UFARANSA IKISHINDWA KUFUZU - PLATINI.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini anaamini kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps hatalaumiwa kama nchi hiyo ikishindwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Brazil mwakani. Ufaransa ina kibarua kigumu katika mchezo wao wa mkondo wa pili hatua ya mtoano utakaochezwa baadae leo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ukraine wiki iliyopita, lakini Platini amesisitiza kuwa ni jukumu la wachezaji kupambana kuhakikisha wanapata nafasi ya kwenda Brazil. Platini amesema siku zote amekuwa akiwaunga mkono makocha wa Ufaransa hivyo kwa maono yake hadhani kama kocha anapaswa kuwajibishwa kama nchi hiyo ikishindwa kufuzu kwani ni jukumu la wachezaji kuhakikisha wanageuza matokeo ya wiki iliyopita ili waweze kufuzu. Deschamps alikuwepo katika kikosi cha Ufaransa enzi hizo akiwa mchezaji wakati waliposhindwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 baada ya kupoteza mechi zake za mwisho dhidi ya Israel na Bulgaria.

FABREGAS AANZA MAZOEZI.

KLABU ya Barcelona imesema kuwa kiungo wake mahiri Cesc Fabregas amerejea tena mazoezini huku akiendelea kupona maumivu ya mguu yanayomkabili. Fabregas aliumia kisigino cha mguu wake wa kulia katika ushindi wa mabao 4-1 waliopata dhidi ya Real Betis Novemba 10 na kusababisha kuondolewa katika kikosi cha Hispania kilichokuwa kikijiwinda na mechi za kimataifa za kirafiki dhidi ya Equatorial Guinea na Afrika Kusini. Mbali na Fabregas nyota wengine walio majeruhi Gerard Pique na Jordi Alba wameendelea kufanya mazoezi mbali na wachezaji wenzao wakati nao wakiendelea kupona taratibu. Mabingwa hao wa La Liga ambao hawajafungwa mpaka sasa wataikaribisha Granada Jumamosi huku wakiongoza La Liga kwa tofauti ya alama tatu mbele ya Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 13.

RAGE ANG'OLEWA SIMBA, WAMO PIA JULIO NA KIBADEN.

KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Simba, imemsimamisha mwenyekiti wake Ismail Aden Rage kwa madai ya kukiuka miiko ya uongozi pamoja na katiba ya klabu hiyo. Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Rage kuwasainisha mkataba wachezaji wawili kutoka Zanzibar Ally Badru na Awadh Juma aliyekuwa anacheza Mtibwa. Taarifa ya awali inadai kuwa Rage amekuwa hajishughulishi kwa karibu na timu hiyo lakini pia amekuwa akikiiuka baadhi ya mambo ndani ya katiba na ndio maana kamati ya utendaji imepata nguvu ya kumsimamisha kwenye kikao walichokaa jana. Maamuzi juu ya hatma ya Rage yatatolewa katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Desemba mosi mwaka huu. Mbali na Rage lakini pia kamati hiyo ilivunja benchi lote la ufundi la timu hiyo lililokuwa likiongozwa na kocha mkuu Abdalah Kibaden na msadizi wake Jamhuri Kihwelu maarufu kama Julio. Nafasi ya Kibaden sasa itashikiliwa na kocha wa zamani wa Gor Mahia, Zdravko Logarusic ambaye ni raia wa Croatia ambaye atakuwa akisaidiwa na aliyekuwa kocha wa kikosi B cha klabu hiyo Seleman Matola. Kocha huyo anatarajiwa kutua nchini Desemba mosi na moja kwa moja kuanza maandalizi ya msimu ujao siku inayofuata.

Monday, November 18, 2013

HAYE ASHAURIWA KUSTAAFU MASUMBWI BAADA YA KUFANYIWA UPASUAJI.

BINGWA wa dunia wa zamani wa ngumi za uzito wa juu, David Haye ameshauriwa kustaafu mchezo huo baada ya kufanyiwa uapsuaji mkubwa wa bega. Haye mwenye umri wa miaka 33 raia wa Uingereza alifanyiwa upasuaji huo uliochukua saa tano katika bega lake la kulia huko nchini Ujerumani Alhamisi iliyopita. Bondia huyo ambaye alifuta pambano lake na Tyson Fury lililokuwa lifanyike Februari mwakani, amesema amekuwa akiokea ushauri kutoka kwa wadau wa mchezo huo kwamba wakati wake wa kustaafu umefika. Kama akiamua kustaafu itakuwa ni mara ya pili kwa Haye baada ya kufanya hivyo Octoba mwaka 2011 miezi mitatu baada ya kupoteza mkanda wake wa WBA kwa Wladimir Klitscho wa Ukraine katika pambano lilofanyika Ujerumani.