MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte amesisitiza kuwa Manchester United bado wako katika mbio za ubingwa pamoja na kuwazidi kwa alama 14. United tayari wameshacheza mechi 15 mfululizo bila kufungwa katika Ligi Kuu lakini bado wameendelea kubakia nafasi ya sita katika msimamo wkiwa alama mbili nyuma ya Arsenal waliopo nafasi ya nne. Akizungumza na wanahabari, Conte amesema kuna timu sita imara na zinaweza kupigana kushinda taji. Conte aliendelea kudai kuwa United bado wana nafasi ya kutwaa ubingwa pamoja na pengo kubwa la alama lililopo kati yao.

Friday, February 10, 2017
MKHITARYAN AMSHUKURU KLOPP.
KIUNGO wa Manchester United, Henrikh Mkhitaryan amemshukuru Jurgen Klopp kwa ushauri uliomsaidia kupita mwanzo mgumu alipotua Old Trafford. Klopp alikuwa akimpa ushauri mchezaji huyo kwenye kipindi kigumu wakati walipokuwa katika klabu ya Borussia Dortmund mwaka 2013. Mapema msimu huu, Mkhitaryan hakucheza mechi yeyote ya ligi kwa wiki 10 na alikumbuka ushauri aliokuwa akipatiwa na Klopp. Akizungumza na wana habari, nyota huyo alimshukuru Klopp kwa kumsaidia kwa kiasi kikubwa kisoka na hata ushauri. Nyota huyo wa kimataifa wa Armenia alifanya kazi na Klopp kwa misimu miwili Ujerumani kabla ya meneja huyo hajajiuzulu na baadae kutua Liverpool Octoba mwaka 2015.
DELLE ALLI, KOCHA WA SWANSEA WATWAA TUZO YA MWEZI.
KIUNGO wa Tottenham Hotspurs, Dele Alli amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari akimshinda mchezaji mwenzake wa timu hiyo Harry Kane. Alli na Kane kila mmoja amefunga mabao matano katika mechi za ligi Januari na kuisaidia Spurs kutofungwa katika mechi tano wakishinda mechi dhidi ya Watford, Chelsea na West Bromwich Albion huku wakitoa sare na Manchester City na Sunderland. Beki wa kulia wa Everton Seamus Coleman naye pia alikuwepo katika kinyang’anyiro hicho kufuatia kuisaidia timu yake kutofungwa katika mechi tatu za ligi walizocheza Januari. Kwa upande mwingine meneja mpya wa Swansea City Paul Clement yeye ametwaa tuzo ya kocha bora wa mwezi baada ya kushinda mechi tatu kati ya nne alizosimamia mwezi uliopita. Clement aliteuliwa kuchukua kibarua hicho Januari 3 na kuisaidia kuichapa Crystal Palace mabao 2-1 katika siku yake ya kwanza kazini kabla ya kuja kufungwa na Arsenal mabao 4-0 na baadae kkushinda tena mechi dhidi ya Liverpool na Southampton.
CARROLL AMSHINDA GIROUD BAO BORA LA MWEZI.
MSHAMBULIAJI nyota wa Crystal Palace, Andy Carroll amefanikiwa kutwaa tuzo ya bao bora la mwezi akimshinda nyota wa Arsenal, Olivier Giroud katika kinyang’anyiro hicho. Januari mosi Giroud alifanikiwa kufunga bao murua lililopewa jina la Scorpion kick katika mchezo dhidi ya Palace hatua ambayo ilidhaniwa ndio linaweza kuwa bao la mwezi. Hata hivyo, Palace ilifanikiwa kujibu mapigo kwa bao safi la Carroll alilofunga katika dakika ya 79 ya mchezo dhidi ya West Ham United katika Uwanja wa London Januari 14. Akizungumza na wanahabari Carroll amefurahi kushinda tuzo hiyo haswa ikizingatiwa kuwepo kwa mabao mengine mazuri yaliyofungwa mwezi uliopita.
MARADONA AKUBALI KUWA BALOZI WA FIFA.
NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona amethibitisha kukubali kuwa balozi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na kueleza furaha yake ya kujiunga na shirikisho hilo safi na linalofanya shughuli zake kwa uwazi. Maradona mwenye umri wa miaka 56 ambaye amewahi kutwaa Kombe la Dunia akiwa na Argentina mwaka 1986, alikuwa mpinzani mkubwa wa rais wa zamani Sepp Blatter aliyeondoka kufuatia kashfa kubwa ya ufisadi iliyolikumba shirikisho hilo mwaka 2015. Maradona alituma picha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook akiwa pamoja na rais wa sasa Gianni Infantino, na kusema sasa atatimiza ndoto yake aliyokuwa kwa kipindi kirefu. Maradoma amesema sasa anaweza kutimiza ndoto yake ya kufanya kazi kwa usafi na uwazi na FIFA sambamba na watu ambao wanaolipenda soka na kuwashukuru wote waliomuunga mkono katika changamoto hiyo mpya.
MOURINHO ALITAKA KUMPELEKA WILLIAN MAN U.
WINGA wa Chelsea, Willian amebainisha kuwa Manchester United ilitaka kumsajili katika kipindi cha majira ya kiangazi. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil amekuwa hana nafasi ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza msimu huu, huku akibadilishana na Pedro mara kwa mara. Willian mwenye umri wa miaka 28 alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Chelsea kilichotwaa taji chini ya Jose Mourinho miaka miwili iliyopita. Willian amekiri kuwepo kwa maombi kutoka United na kufafanua kuwa ni kwasababu Jose Mourinho yuko kule.
SUAREZ KUKOSA FAINALI YA KOMBE LA MFALME.
MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Luis Suarez anatarajiwa kukosa mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme Mei 27 baada ya kushindwa rufani kupinga kadi ya pili ya njano aliyopewa katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid Jumanne iliyopita. Shirikisho la Soka la Hispania-RFEF limetoa adhabu ya kumfungia mechi mbili Suarez kutokana na tukio lake baada ya kutolewa nje katika dakika za mwisho katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Baada ya rufani hiyo kukataliwa, Barcelona wamesema sasa watakwenda mbali zaidi kwenye kamati ya rufani ya RFEF ili kujaribu tena kuipinga kadi hiyo. Suarez alisema baada ya mchezo kuwa uamuzi wa kadi hiyo ulikuwa wa kuchekesha na kuitaka klabu kukata rufani jambo ambalo meneja Luis Enrique alifanya.
Subscribe to:
Posts (Atom)