Tuesday, July 31, 2012

RAMIREZ AITWA TENA BRAZIL.

KIUNGO wa kimataiafa wa Brazil, Ramirez ameitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kinachonolewa na kocha Mano Menezes kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Sweden ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Ramires mwenye umi wa miaka 25 amekuwa tegemeo katika klabu yake ya Chelsea ambayo aliiwezesha kushinda taji la FA pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita lakini hakujumuishwa katika kikosi cha Brazil toka alipoitwa katika michuano ya Copa Amerika 2011. Lakini Menezes ameamua kumjumuisha kiungo huyo ambayo atacheza pamoja na wachezaji wenzake ambao wanacheza klabu moja David Luis na Oscar. Katika kikosi hicho kocha huyo amewaita wachezaji walewale waliopo katika kikosi cha Olimpiki na kuongeza wengine kidogo ambao wataziba nafasi za wale ambao watapumzika baada ya olimpiki. Mchezo wa kirafiki hidi ya Sweden unatarajiwa kuchezwa Agosti 15 mwaka huu.

ALMUNIA ATIMKIA WATFORD.

Emmanuel Almunia.
KLABU ya Arsenal imesema kuwakipa wake wa zamani Manuel Almunia amejiunga na klabu ya Watford inayoshiriki ligi daraja pili nchini Uingereza. Almunia ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja anakuwa mmoja kati ya wachezaji wapya saba waliosajiliwa na Watford ambayo inanolewa na kocha Gianfranco Zola. Taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu ya Arsenal ilithibitisha kuwa ni kweli klabu hiyo imemwachia Almunia kwenda Watford kwa mkataba wa mwaka mmoja. Almunia amecheza michezo 175 akiwa na klabu ya Arsenal ukiwemo mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006 dhidi ya Barcelona ambao aliingia kama mchezaji wa akiba lakini alipoteza namba katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo kwa Wojciech Szczesny ambaye ni raia wa Poland. Watford ambayo katika siku za karibuni ilinunuliwa na familia ya Pozzo ambao pia wanamiliki klabu ya Udinese inayoshiriki Ligi Kuu nchini Italia na Granada ya Hispania, pia imewasajili Fitz Hall, Almen Abdi, Matej Vydra na Steve Leo Beleck.

MORGANELLA ATIMULIWA KAMBINI.

Michel Morganella.
BEKI wa kimataifa wa Switzerland, Michel Morganella ameondolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 inayoshiriki michuano ya Olimpiki jijini London baada ya kutuma ujumbe wa kibaguzi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwenda kwa mchezaji wa Korea Kusini. Viongozi wa timu hiyo walimuondoa mchezaji huyo katika kikosi hicho baada ya kutuma ujumbe huo kufuatia kufungwa na Korea Kusini kwa mabao 2-1 Jumapili iliyopita. Mkuu wa msafara wa nchi hiyo kwenye michuano ya olimpiki Gian Gilli amesema kuwa beki huyo ametuma ujumbe ambao unadhalilisha kwa watu wa Korea Kusini pamoja na timu yao ya taifa hivyo baada ya kupata ushauri kutoka kwa Chama Cha Soka cha Switzerland wakaamua kumuondoa kikosini mchezaji huyo. Mchezaji huyo alikubali maamuzi yaliyochukuliwa na kuomba radhi kutokana na tabia aliyoionyesha ingawa alijitetea kuwa zilikuwa ni hasira baada ya kupoteza mchezo dhidi ya timu hiyo.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MECHI YA NGORONGORO HEROES YAINGIZA MIL 12/-
Mechi ya kwanza ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Nigeria (Flying Eagles) iliyochezwa juzi (Julai 29 mwaka huu) imeingiza sh. 12,901,000. Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 3,377 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 2,697 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 15,000 kwa VIP A iliyoingiza watazamaji 21. Mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 1,967,949.15, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, gharama za waamuzi na kamishna wa mechi hiyo sh. 760,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000. Malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 714,610.17, asilimia 10 ya uwanja sh. 357,305.08, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 178,652.54 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 2,322,483.05. Mechi ya marudiano ya michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Agosti 12 mwaka mjini Ilorin, Jimbo la Kwara, Nigeria.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SIREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 28 mwaka huu. Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SIREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Singida. TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya SIREFA chini ya uenyekiti wa Baltazar Kimario ambaye amechaguliwa kwa mara ya kwanza. Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Singida kwa kuzingatia katiba ya SIREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake. Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya SIREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF. Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Singida ni Baltazar Kimario (Mwenyekiti), Hussein Mwamba (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Gabriel Mwanga (Mhazini), Hamisi Kitila (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Omari Salum (Mwakilishi wa Klabu TFF), Yagi Kiaratu na Dafi Dafi (wajumbe wa Kamati ya Utendaji). Nafasi za Makamu Mwenyekiti, Mhazini Msaidizi na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji zitajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye.

MICHELSEN AITA 22 KAMBI YA COCA-COLA
Kocha wa timu za Taifa za vijana za Tanzania, Jakob Michelsen ameita wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya Coca-Cola itakayofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini. Baadaye watachujwa na kubaki 16 ambao ndiyo watakaokwenda kwenye michuano ya Afrika Kusini. Wachezaji waliochaguliwa wametokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani kuanzia Juni 24- Julai 2 mwaka huu. Wachezaji walioitwa ni Abdulrahman Mandawanga (Dodoma), Abraham Mohamed (Mjini Magharibi), Ayoub Alfan (Dodoma), Bakari Masoud (Tanga), Daniel Justin (Dodoma), Denis Dionis (Ilala), Edward Songo (Ruvuma), Fikiri Bakari (Tanga), Hassan Kabunda (Temeke), Joseph Chidyalo (Dodoma), Mutalemwa Katunzi (Morogoro) na Mwarami Maundu (Lindi). Wengine ni Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Omari Saleh (Singida), Rajab Rajab (Mwanza), Said Said (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma), Tumaini Baraka (Kilimanjaro) na William John (Ruvuma). Pia Michelsen ameongeza wachezaji saba kwenye kikosi cha Serengeti Boys ambacho Septemba mwaka huu kitacheza na Kenya kuwania tiketi ya fainali za vijana wenye umri chini ya miaka 17 za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Wachezaji walioongezwa kwenye kikosi hicho ambao pia wametoka kwenye Copa Coca-Cola ni Abdallah Baker (Mjini Magharibi), Abdallah Kheri (Mjini Magharibi), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Hassan Mganga (Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni) na Mzamiru Said (Morogoro).

OLIMPIKI 2012: YE SHIWEN AKANA KUTUMIA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU.

Ye Shiwen.
MUOGELEAJI kutoka China aliyeshinda medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki, Ye Shiwen amekanusha taarifa kuwa alikuwa ametumia madawa ya kuongeza nguvu katika mashindano hayo. Kocha wa timu ya waogeleaji kutoka Marekani awali alikaririwa akisema kuwa Shiwen ambaye alivunja rekodi katika mashindano ya uogeleaji ya mita 400 alikuwa ametumia kitu cha ziada kutokana na kasi aliyoionyesha katika mzunguko wa mwisho uliopelekea kuvunja rekodi hiyo. Kwa upande mwingine polisi jijini London walimkamata kijana mmoja kutokana na tuhuma za kutuma ujumbe wa kuudhi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii twitter kwenda kwa mpiga mbizi wa Uingereza Tom Daley. Kikosi cha timu taifa ya Uingereza kinatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza baadae leo kuwania medali katika michezo ya canoeing, sarakasi, kupiga mbizi, na kukimbiza farasi.

Monday, July 30, 2012

FIRST LADY MICHELLE OBAMA HUGS ENTIRE U.S. BASKETBALL TEAM AFTER WIN OVER FRANCE.







HISPANIA WAAGA MAPEMA MICHUANO YA OLIMPIKI.

TIMU ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 ya Hispania imeenguliwa mapema katika michuano ya Olimpiki inayofanyika jijini London baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Honduras ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kufuatia kile walichopata kutoka kwa Japan kwa idadi kama hiyo ya mabao. Honduras ambao walishinda bao la mapema kupitia kwa mshambuliaji wake Jerry Bengtson wamefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali pamoja na Japan ambao waliwafunga Morocco bao 1-0 katika kundi D. Katika michezo ya kundi C Brazil ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kuifunga Belarus mabao 3-1 wakati Misri ilitoa sare ya bao 1-1 na New Zealand hivyo itabidi washinde mchezo wao wa mwisho dhidi ya Belarus ili waweze kusonga mbele. Mexico ilifanikiwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Gabon katika kundi B wakati Korea Kusini walifanikiwa kushinda mabao 2-1 hivyo kupelekea timu hizo kuwa na alama sawa katika kundi hilo.

HAMILTON AIBUKA KINARA WA MBIO ZA LANGALANGA ZA HUNGARY GRAND PRIX.

DEREVA wa magari yaendayo kasi ya Langalanga kutoka timu ya McLaren, Lewis Hamilton amefanikiwa kushinda mbio za Hungary Grand Prix jana. Hamilton ambaye ni raia wa Uingereza alimaliza mbio hizo kwa kasi zaidi ya wenzake ambao aliwaacha kwa sekunde 0.413 na kufuatiwa na dereva wa timu ya Lotus, Romain Grosjean aliyeshika nafasi ya pili katika mbio hizo. Sebastian Vettel wa timu ya Red Bull alimaliza katika nafasi ya tatu akifutiwa na Jenson Button ambaye ni muingereza kutoka timu ya McLaren pia alimaliza katika nafasi ya nne. Wengine ni Kimi Raikkonen aliyemaliza katika nafasi ya tano akifuatiwa na Fernando Alonso wa timu ya Ferrari katika nafasi ya sita wakati mkali mwingine wa mbio hizo Mark Webber alimaliza katika ya 11. Magari ya Ferrari ambayo yalitamba kipindi cha mvua katika michuano ya Ujerumani katika mbio hizo za majira ya kiangazi yameshindwa na kusababisha kupunguza pengo la alama ambazo Alonso alikuwa akiongoza katika orodha ya madereva bora duniani.

WILSHERE KUREJEA UWANJANI OCTOBA.

Jack Wilshere.
MENEJA wa klabu ya Arsenal Arsenal Wenger amesema kuwa kiungo nyota wa klabu hiyo Jack Wilshere hata kuwa sehemu ya kikosi chake katika michezo ya mwanzo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kutokana na majeraha yanamsumbua. Wilshere ambaye ana miaka 20 alishindwa kucheza msimu uliopita kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti aliofanyiwa Mei mwaka jana. Wenger ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kukamilisha ziara ya bara la Asia jijini Hong Kong amesema kuwa anatarajia mchezaji huyo kurejea dimbani mwezi Octoba. Wakati akiuguza goti lake Wilshere alilitonesha tena wakati akifanya mazoezi ili arejee uwanjani na hivyo kumfanya mchezaji kukosa michuano ya Ulaya iliyomalizika Julai mosi mwaka huu ambapo anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi Agosti na akitarajia kurejea uwanjani Octoba.

Arsenal vs Kitchee FC 2-2 Pre Season Hong Kong

Sunday, July 29, 2012

WAKIDADA WA CAMEROON WAPIGWA TATU NA UINGEREZA KATIKA OLIMPIKI.






Chelsea vs AC Milan 0-1 All Goals & Highlights 28/07/2012

SHEVCHENKO AAMUA KUKIMBILIA KWENYE SIASA.

Andriy Shevchenko.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea Andriy Shevchenko ametangaza kustaafu kucheza soka rasmi ili aweze kujishughulisha na nmasuala ya siasa. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ukraine mwenye miaka 35 alithibisha taarifa hizo ambazo zilitolewa katika mtandao wa klabu ya Dynamo Kiev ambayo alikuwa akicheza. Shevchenko amecheza mechi 111 kwa nchi yake ambapo mara ya mwisho ilikuwa katika michuano ya Ulaya iliyomalizika mapema mwezi huu ambapo Ukraine ilifungwa bao 1-0 na Uingereza. Mshambuliaji huyo aliibukia katika klabu ya Dynamo mwaka 1994 na baadae kuhamia klabu ya AC Milan mwaka 1999 ambapo alifanikiwa kushinda taji la Ligi ya mabingwa ya Ulaya mwaka 2003 na klabu hiyo huku yeye akiwa ndio nyota wa mchezo baada ya kushinda penati ya mwisho. Akiwa na miaka 29 Shevchenko alihamia katika klabu ya Chelsea ambayo ilikuwa ikifundishwa na Jose Mourinho mwaka 2006 kwa ada paundi milioni 30 lakini hakupata mafanikio katika misimu miwili aliyochezea klabu hiyo na kuamua kurejea AC Milan ambapo nako hakukaa sana kabla ya kuamua kurejea Dynamo mwaka 2009. Shevchenko amefunga mabao 48 na kurekodi ya mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika timu ya taifa ya nchi hiyo huku akikiongoza kikosi cha nchi hiyo kilichofika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 na pia aliwahi kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya mwaka 2004.

FEDERER, SERENA WAANZA VYEMA OLIMPIKI.

Roger Federer.
WACHEZA tenisi nyota Roger Federer na Serena Williams wameanza vyema kampeni zao za kuhakikisha wanaondoka na medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki baada ya kushinda michezo yao ya kwanza. Federer kutoka Switzerland ambaye anashikilia namba moja katika orodha za ubora za mchezo huo duniani kwa upande wa wanaume alifanikiwa kumfunga Alejandro Falla kutoka Colombia kwa 6-3 5-7 6-3. Kwa upande wa wanawake Williams ambaye anashika nafasi ya nne katika orodha za ubora alifanikiwa kumfunga kirahisi Jelena Jankovic kutoka Serbia kwa 6-3 6-1 na kufanikiwa kutinga raundi ya pili. Kim Clijsters kutoka Ubelgiji ambaye amepanga kustaafu mchezo huo mwishoni mwa mwaka huu alifanikiwa kumfunga Roberta Vinci kutoka Italia kwa 6-1 6-4 ambapo sasa anatarajiwa kukutana na Carla Suarez wa Hispania katika mzunguko wa pili wakati Serena atakutana na Urszula Radwanska wa Poland. Federer atacheza na Julien Benneteau kutoka Ufaransa ambaye alimfunga kwa seti tano katika michuano ya Wembledon iliyopita.

YE SHIWEN AWEKA REKODI YA DUNIA OLIMPIKI.

Ye Shiwen.
MUOGELEAJI Ye Shiwen kutoka China amevunja rekodi ya dunia ya mita 400 katika mchezo huo na kunyakuwa medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki inayoendelea jijini London, Uingereza. Shiwen mwenye miaka 16 aliweka rekodi hiyo akitumia muda bora wa dakika 4:28:43 mbele ya bingwa wa dunia kutoka Marekani Elizabeth Beisel na Li Xuanxu ambaye pia anatoka China. Muogeleaji huyo alivunja rekodi ya muda wa dakika 4:29:45 ambayo ilikuwa imewekwa na Stephanie Rice kutoka Australia katika michuano ya olimpiki iliyofanyika Beijing mwaka 2008. Muogeleaji kutoka Uingereza Hannah Miley ambaye alishinda medali ya fedha katika mashindano ya dunia mwaka jana na kutegemewa kufanya vizuri katika mashindano hayo alishindwa kutamba baada ya kumaliza katika nafasi ya tano. Mara baada ya mashindano hayo Miley aliomba radhi mashabiki wake ambao walitarajia atafanya vizuri ambapo kwasasa amesema anahamishia nguvu zake katika mbio za kuogelea za mita 200 kuhakikisha anafanya vyema.

SPURS YAKUBALI KUMUUZA MODRIC KWA PAUNDI MILIONI 36.

KLABU ya Tottenham Hotspurs imekubali kumuuza kiungo wake Luka Modric kwa ada ya paundi milioni 36 kwenda klabu ya Real Madrid ya Hispania. Kiungo huyo wa kimataifa wa Croatia tayari alishasema kuwa atajiunga na Madrid lakini alikuwa akisubiria klabu hizo kufikia makubaliano. Modric kidogo apoteze nafasi yake ya kwenda Madrid baada ya kukataa kusafiri na Spurs katika ziara huko nchini Marekani lakini viongozi wa Madrid walimlazimisha kuomba msamaha na kwenda kwenye ziara hiyo. Mkataba huo utamaliza utata wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye alianza kushinikiza kuondoka kwenda Chelsea mwaka uliopita lakini alikataliwa na klabu yake hiyo.

Friday, July 27, 2012

BOLT YUKO FITI KUTETEA TAJI LAKE.

Usain Bolt.
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt amekiri kuwa maumivu ambayo yalikuwa yakimsumbua yaliathiri kiwango chake kwa kiasi fulani. Bolt amesema kuwa maumivu hayo ya mgongo kwasasa yamepona na yuko tayari kutetea taji lake wakati atakapopeperusha bendera ya nchi yake katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo baadae leo. Nyota huyo ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya sekunde 9.58 katika mbio za mita 100 alishindwa kutamba mbele ya mjamaica mwenzake Yohan Blake katika mbio za majaribio zilizofanyika jijini Kingston na baadae kukosa mbio za Diamond League zilizofanyika jijini Monaco. Akihojiwa Bolt amesema kuwa katika mbio hizo alikuwa yuko sawa lakini hakuwa katika kiwango chake ambacho amekizoea lakini anashukuru baada ya mapumziko na mazoezi aliyokuwa akifanya anaamini anaweza kutete taji lake kwenye michuano hiyo. Bolt pia alishukuru kwa kupewa heshima ya kubeba bendera ya nchi yake katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo ambayo inatarajiwa kufanyika baadae usiku.