Tuesday, April 30, 2013

FERGUSON AKIRI MAPAMBANO MAKALI KATIKA USAJILI KIANGAZI.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson amekiri atakuwa katika mapambano makubwa na mahasimu wake Manchester City na Chelsea mara dirisha la usajili majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Pamoja na kutwaa taji la Ligi Kuu nchini Uingereza, Ferguson tayari ameanza kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao na anatatarajia kusajili wachezaji nyota kadhaa. Ferguson atawaongeza nyota hao atakaowasajili katika majira ya kiangazi na kuwaunganisha na kikosi chake cha sasa ambacho kimesheheni wachezaji vijana kwa ajili ya kutetea taji lake la ligi na kujaribu kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kocha huyo amesema ni lazima aongeze nguvu katika kikosi chake ili waongeze nguvu damu change alizonazo kwani wachezaji wenye umri mkubwa alionao tayari soka lao linelekea ukingoni hivyoni muhimu kufanya mabadiliko.

UNITED WAPEWA MWAMUZI WAO MECHI DHIDI YA CHELSEA.

MWAMUZI Howard Webb ameteuliwa kuchezesha mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kati ya Manchester United na Chelsea utakaochezwa katika Uwanja wa Old Traford Jumapili. Webb mwenye umri wa miaka 41 ambaye alichezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2010 sio mgeni katika kuchezesha mechi zenye utata baina ya vilabu hivyo vikubwa ambavyo vyote vimekuwa vikilalamikia baadhi ya maamuzi yanayotolewa naye. Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Ryan Babel aliwahi kutuma picha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akimuonyesha Webb ametinga jezi ya United kufuatia kufingwa na timu hiyo bao 1-0 Januari mwaka 2011 huku akiandika ujumbe mkali wa kumponda. Hatua hiyo ilipelekea Babel kuwa mchezaji wa kwanza kuadhibiwa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa matumizi mabaya ya mtandao wa kijamii. Webb pia alishakwaruzana na meneja wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho kufuatia kukataliwa kwa bao la Salomon Kalou katika mchezo dhidi ya Blackburn Rovers mwaka 2007 ambapo Mourinho alimtaka mwamuzi huyo kuomba radhi kwa kosa alilofanya. United wameshinda mechi 13 na kupoteza moja tu katika mechi 15 za ligi kuu ambazo Webb amechezesha Old Traford.

MWAMUZI AFUNGIWA MAISHA URUSI KWA KUSHAMBULIA.

MWAMUZI msaidizi wa ligi ya soka nchini Urusi amefungiwa maisha jana kufuatia kumshambulia mchezaji wa miaka 18. Mwamuzi huyo Musa Kadyrov alimshambulia beki wa timu ya Amkar Perm, Ilya Krichmar mara baada ya kupulizwa filimbi ya kumaliza mchezo kati ya timu hiyo na wenyeji Terek katika mji wa Grozny, Chechnya. Krichmar amesema mara baada ya mwamuzi wa kati kupuliza filimbi ya mwisho alianza kutembea kuelekea katika benchi lao la ufundi ndipo ghafla mwamuzi huyo alipokuja nyuma yake na kumsukuma kisha kuanza kumpiga mateke. Mchezaji anaendelea kusema muda mfupi baadae wachezaji wa timu mwenyeji nao walivamia eneo hilo na kuanza kumshambulia kabla ya wachezaji wenzake hawajafika na kumuokoa asiendelee kupata kichapo zaidi. Wadau wa masuala ya michezo huko Chechnya wameungana kuponda kitendo kilichofanywa na Kadyrov na kudai kuwa adhabu ya kufungiwa maisha kwa mamuzi huyo haikutosha kutokana na kitendo cha aibu alichofanya.

HAVELANGE ATAJWA KULA MLUNGULA, BLATTER ASAFISHWA.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Joao Havelange wa Brazil ambaye aliiongoza shirikisho hilo kwa zaidi ya miongo miwili, amejiuzulu wadhifa wake wa rais wa heshima aliopewa baada ya kutajwa kupokea mlungula. Taarifa iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na kamati ya maadili ya FIFA kuhusiana na sakata la wabia wao wa masoko-ISL ambapo Havelange ametajwa pamoja wajumbe wawili wa zamani wa kamati ya utendaji Ricardo Teixeira na Nicolas Leoz kupokea rushwa. Mwenyekiti wa tume hiyo maalumu uliyotolewa kusimamia sakata hilo Hans-Joachim Eckert pia alimtaja rais wa sasa wa FIFA Sepp Blatter kwamba alikuwa mzito kushughulikia suala hilo lakini akasema kwamba hajavunja sheria zozote za maadili ya shirikisho hilo. Pamoja na ripoti hiyo kusafisha Blatter ambaye kipindi wakati Havelange akiwa madarakani yeye alikuwa katibu mkuu wa FIFA wadau wengi wa soka bado wanaona rais huyo naye alihusika kwa namna moja au nyingine kutokana na nafasi aliyonayo.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 25 
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea katika raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi. Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini. Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa. Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo. Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha. 

MTANZANIA APEWA ITC KUCHEZA MSUMBIJI 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Yusuf Kunasa kucheza nchini Msumbiji. Shirikisho la Mpira wa Miguu cha Msumbiji (FMF) lilituma maombi TFF kumuombea hati hiyo Kunasa anayekwenda kujiunga na timu ya Estrela Vermelha da Beira inayocheza Ligi Kuu nchini humo. Kunasa ambaye msimu huu hakuwa na timu (free agent) amejiunga na timu hiyo akiwa mchezaji wa ridhaa (amateur). Zaidi ya wachezaji kumi kutoka Tanzania hivi sasa wanacheza katika klabu mbalimbali nchini Msumbiji. 



MECHI YA SIMBA, POLISI MOROGORO YAINGIZA MIL 18/-
Mechi namba 163 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Morogoro imeingiza sh. 18,014,000. Watazamaji 3,145 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,564,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,747,898.31. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 2,841 na kuingiza sh. 14,205,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 36 na kuingiza sh. 720,000. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,812,331.75, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,087,399.05, Kamati ya Ligi sh. 1,087,399.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 543,699.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 422,877.41.

Monday, April 29, 2013

RONALDO AKANUSHA KULALA NA 'MISS BUMBUM'.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo amekanusha vikali tuhuma za kumsaliti rafiki yake wa kike Irina Shayk kwa kutembea na mwanamitindo wa Brazil Andressa Urach ambaye anajulikana pia kwa jina ya ‘Miss BumBum’. Urach alikaririwa na gazeti la The Sun akidai kuwa alilala na nyota huyo wa Madrid katika hoteli ya Villa Magna saa 48 kabla ya mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund lakini nyota huyo amesisitiza kuwa hakuna ukweli katika hilo. Ronaldo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter akilalamikia kitendo cha mwanamitindo huyo kutaka kumchafua kwa kile kilichoandikwa katika gazeti hilo. Ronaldo aliendelea kuandika kuwa ni kweli alifikia katika hoteli hiyo Aprili 22 kwa ajili ya mahojiano lakini mengine yote yaliyozungumza baada ya hapo ni uongo na uzushi mtupu.

JAY Z ASHUHUDIA ARSENAL IKITOA SARE EMIRATES.

MWIMBAJI wa kundi la Coldplay la Uingereza na rapa machachari wa Marekani Jay Z walionekana kuwa kivutio kikubwa katika mchezo kati ya Arsenal na Manchester United uliochezwa katika Uwanja wa Emirates ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Wawili hao walionekana katika jukwaa maalumu wakishukuhudia mtanange huo na kuonyesha mapenzi makubwa kwa Arsenal. Miaka mitatu iliyopita Jay Z alikaririwa akisema kuwa anataka kuwekeza mahela yake katika klabu hiyo ingawa alikiri kutokuwa na uzoefu wa kutosha katika sekta hiyo. Jay Z ambaye alikuwa akivutiwa na nyota wa zamani wa Arsenal Thierry Henry bado amesisitiza nia yake ya kuwekeza Arsenal akidai kuwa atakapopata nafasi atafanya hivyo kwasababu yeye ni mfanyabiashara. Arsenal inaweza kujiimarisha zaidi kiuchumi kama wakifanikiwa kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao na sare waliyopata katika mchezo huo haijawaharibia sana kwani imewaacha katika nafasi ya nne mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. 

SHAKHTAR DONETSKI WATAWADHWA MABINGWA UKRAINE KWA MARA YA NNE MFULULIZO.

KLABU ya Shakhtar Donetski imefanikiwa kunyakuwa taji la nne mfululizo la Ligi Kuu nchini Ukraine baada ya kufanikiwa kupambana wakitoka nyuma na kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Metalist Kharkiv. Mchezaji wa Brazil Ilsinho ndio aliyekuwa shujaa wa mchezo huo baada ya kufanikiwa kuisawazishia timu yake bao katika dakika ya 84 baada ya mshambuliaji wa zamani wa Shakhtar Marco Devic kuifungia timu yake bao la kuongoza katika dakika ya 34. Mpaka sasa Shakhtar imefanikiwa kushinda jumla ya mataji nane ya ligi kwa kuziacha Metalist na Dynamo Kiev pengo la alama 15 nyuma huku kukiwa kumebakia mechi nne kabla ya msimu kumalizika. Shakhtar pia imeweka rekodi ya kushinda taji hilo kwa haraka zaidi katika historia ya Ligi Kuu nchini Ukraine.

WACHEZAJI NA HUGHES NDIO CHANZO CHA QPR KUSHUKA DARAJA.

MCHEZAJI mtukutu wa Queens Park Rangers-QPR ambaye anacheza kwa mkopo katika klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa Joey Barton amewaponda wachezaji pamoja na kocha aliyetimuliwa Mark Hughes kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kushuka daraja msimu huu. Barton aliondoka QPR na kujiunga na Marseille mwanzoni mwa msimu lakini kiungo huyo wa zamani wa Manchester City haraka amewalaumu wachezaji wenzake na Hughes ambaye ndiye aliamua kumpeleka kwa mkopo ufaransa. Kiungo huo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter mara baada ya QPR kuthibitika kushuka darajakwa kutoka sare ya bila ya kufungana na Reading, kuwa uamuzi wa Hughes kununua wachezaji wanaolipwa fedha nyingi kabla ya kuanza kwa msimu ndio chanzo cha timu hiyo kushuka daraja. Wachezaji wa fedha nyingi waliosajiliwa hawakuwa wakicheza kwa kujituma akimtolea mfano Jose Bosingwa ambaye alikuwa akitoka uwanjani huku akicheka wakati timu yao imeshuka daraja. Barton amesema ni aibu kuona mchezaji ambaye amekuwa akilipwa fedha nyingi anatoka uwanjani huku anacheka wakati timu imefanya vibaya hiyo inaonyesha wazi kwamba walikuwa hawajitumi ili kuhakikisha timu yao inapata matokeo mazuri.

BECKENBAUER AIONYA BAYERN.

MCHEZAJI nyota wa zamani wa Ujerumani Magharibi, Franz Beckenbauer ameionya klabu ya Bayern Munich kuwa Barcelona haitasita kutumia mbinu chafu katika mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano. Barcelona walibamizwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Allianz Arena wiki iliyopita na Beckenbauer ana wasiwasi kuwa Barcelona watatumia mbinu zote kuhakikisha wanageuza ametokeo hayo. Amesema katika mchezo huo Barcelona itatumia mbinu zote katika kitabu kujaribu kuitoa Bayern mchezoni na kama wakishindwa hawatasita kutumia mbinu chafu mradi wafanikiwe lengo lao. Lakini pamoja na yote hayo Beckenbauer hadhani kama Bayern wataifanya kazi ya Barcelona kugeuza matokeo kuwa rahisi sana kutokana na kikosi bora walichonacho hivi sasa.

GARETH BALE MCHEZAJI BORA WA MWAKA WA PFA.

KIUNGO wa klabu ya Tottenham Hotspurs Gareth Bale amekuwa mchezaji wa tatu kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa upande wa wakubwa na wachezaji wanaochipukia kwa msimu mmoja, tuzo ambazo hutolewa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa nchini Uingereza. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Wales mwenye umri wa miaka 23 ambaye pia alishinda tuzo ya wakubwa mwaka 2011, amefunga mabao 19 katika ligi msimu huu na kuwa nyuma ya kinara wa mabao Robin van Persie mwenye mabao 25 na Luis Suarez mwenye mabao 23. Akikabidhiwa tuzo hiyo Bale amesema ni heshima kubwa kwake kunyakuwa tuzo hizo mbili muhimu na kushukuru wapiga kura kwa kutambua mchango wake haswa ikizingatiwa kumekuwa na majina makubwa mengine katika orodha iliyokuwepo. Bale anaungana na wachezaji wengine walioshinda tuzo ya wakubwa mara mbili ambao ni Cristiano Ronaldo, Thierry Henry, Alan Shearer and Mark Hughes wakati walioshinda tuzo zote mbili kwa mwaka mmoja ni Ronaldo mwaka 2007 na Andy Gray mwaka 1977.

Sunday, April 28, 2013

UNITED INGEWEZA KUNYAKUWA TAJI BILA YA VAN PERSIE - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa Manchester United ingeweza kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uingereza hata bila ya kuwepo mfungaji wake mahiri Robin van Persie. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliondoka Arsenal na kujiunga na United katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi na amefunga mabao 24 katika mechi 31 za ligi msimu huu. Pamoja na kiwango bora alichokionyesha nyota huyo msimu huu lakini Wenger amekataa kumpa umuhimu wote yeye na kudai kuwa pengo la alama 13 kati ya United na Manchester City waliokuwa wanawafukuza kwa karibu ni kushuka kwa kiwango cha City. Amesema pamoja na kwamba Van Persie ametoa mchango wake lakini United walikuwa wana uwezo wa kufanya hivyo haswa ikizingatiwa mwaka jana walilikosa taji hilo kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga na kuwaachia ubingwa huo City. Wenger ameongeza kuwa katika kipindi cha muda mfupi ujao watarejea katika ushindani kama ilivyokuwa zamani lakini la muhimu kwasasa ni kumaliza katika nne za juu hilo ndio wanaolipa kipaumbele ili waweze kushiriki Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao. 

GIGGS ALINIPA TABU SANA KIPINDI NACHEZA - LAUREN.

BEKI wa zamani wa kimataifa wa Cameroon na klabu ya Arsenal Lauren Mayer amebainisha kuwa mshambuliaji wa Manchester United Ryan Giggs alikuwa akimpa wakati mgumu kumkaba wakati akicheza soka. Lauren ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal ambacho kilimaliza msimu wa mwaka 2004 bila kufungwa katika Ligi Kuu nchini Uingereza yuko jijini Kampala kwa mwaliko wa mpango wa kuinua vipaji wa Airtel rising stars. Beki huyo nyota wa zamani pia alimtaja mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry kama mmoja wa washambuliaji wagumu kuwakaba pindi walipokuwa mazoezini kwasababu ya kasi na ufundi wa hali ya juu aliokuwa nao. Lauren amesema wakati akicheza alipata wakati mgumu kumkaba Giggs kwasababu alikuwa mjanja sana na ilikuwa sio rahisi kugundua anachotaka kufanya awapo na mpira kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa nafasi yake. Nyota huyo pia amesema kama ilivyo kwa mashabiki wengine wa Arsenal nay eye anachukizwa na kitendo cha timu hiyo kutoshinda taji lolote kwa kipindi kirefu lakini ana imani na kocha Arsene Wenger kwa mba atarekebisha hilo na mambo yatakuwa mazuri kipindi kifupi kijacho.

ROONEY MCHEZAJI TAJIRI ZAIDI EPL.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester United, Wayne Rooney ndio mchezaji mwenye fedha nyingi zaidi katika Ligi Kuu nchini humo akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia paundi milioni 51. Wachezaji 24 wa ligi kuu nchini humo ni miongoni mwa orodha ya wanamichezo 100 matajiri nchini Uingereza na Ireland. Utajiri wa Rooney umeongezeka kwa paundi milioni sita kwa mwaka jana na ukijumlisha na utajiri wa mkewe Coleen unafikia kiasi cha paundi milioni 64. Mchezaji mwenzake wa United Rio Ferdinand yeye yuko katika nafasi ya pili akiwa na utajiri unaofikia paundi milioni 42 wakati mshambuliaji wa Stoke City Michael Owen yuko katika nafasi ya tatu akiwa na kiasi cha paundi milioni 38. Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, David Beckham ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya Paris Saint Germain ya Ufaransa yeye anashika nafasi ya 11 katika wanamichezo matajiri duniani akiwa na utajiri unaofikia paundi milioni 165 ambapo nafasi ya kwanza katika orodha hiyo inashikiliwa na mcheza gofu Tiger Woods mwenye utajiri unaofikia paundi milioni 570.

BILBAO YAITIBULIA BARCELONA MIPANGO YA UBINGWA.

KLABU ya Barcelona inabidi isubiri wiki nyingine ili iweze kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania baada ya Athletico Bilbao kulazimisha sare ya mabao 2-2 Jana huku mahasimu wao Real Madrid nao wakijichimbia katika nafasi ya pili baada ya kuwafunga ndugu zao Atletico Madrid mabao 2-1. Ushindi wa Barcelona dhidi ya Bilbao na kama mahasimu wao Madrid wangefungwa katika mchezo wao ungeiongezea pengo la alama 16 Barcelona huku wakiwa wamebakiwa na mechi hivy moja kwa moja kutangazwa mabingwa wapya wa La Liga. Lakini kwa matokeo yalivyokuwa jana Barcelona bado wana mchezo mmoja zaidi ili waweze kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu. Barcelona ina kibarua kigumu Jumatano ijayo mbele ya Bayern Munich ambapo inatatakiwa kupata ushindi wa zaidi ya mabao manne ili iweze kukata tiketi ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza.

LIVERPOOL WALIKUWA SAHIHI - FERGUSON.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini kuwa Liverpool walikuwa sahihi kutochukua hatua dhidi ya mshambuliaji wao Luis Suarez kabla ya kufungiwa mechi 10 na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa kumng’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic. Ferguson amesema tukio hilo linamkumbusha jinsi walivyotendwa na FA baada ya mshambuliaji wake Eric Cantona kumpiga teke la kung-fu mshabiki wa Crystal Palace mwaka 1995. Ferguson amedai kuwa FA iliwahakikishia kuwa hatachukua hatua zaidi kama United watamuadhibu mchezaji huyo lakini pamoja na United kumfungia Cantona miezi minne, chama hicho kiliongeza adhabu na kufikia miezi nane. Kwa matokeo hayo yaliyowakuta United kipindi hicho Ferguson amesema ameelewa kwanini Liverpool hawakumuadhibu nyota huyo mapema.

Saturday, April 27, 2013

NYOTA WA BIRMINGHAM MBARONI KWA KUSABABISHA AJALI.

POLISI nchini Uingereza wamebainisha kumkamata mshambuliaji mtukutu wa klabu ya Birmingham City Marlon King kwa tuhuma za uendeshaji hatarishi. King alishikiliwa na polisi kufuatia ajali iliyohusisha magari matatu katika kitongoji cha Nottinghamshire jana ajali ambayo ilipekekea mtu mmoja kujeruhiwa vibaya huku mchezaji huyo akiachiwa baadae kwa dhamana wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea. Msemaji wa klabu hiyo iliyopo ligi daraja pili amethibitisha kuwa na taarifa ya ajali ambayo imemhusisha mchezaji wao na kudai kuwa suala hilo bado linachunguzwa na polisi hivyo hawezi kuzungumzia zaidi. King alifanyiwa upasuaji wa mguu mwezi uliopita ambao utamfanya kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima.

NEYMAR KUONDOKA SANTOS.

MAKAMU wa rais wa klabu ya Santos ya Brazil, Odilio Rodriguez amebainisha kuwa Neymar ameiambia klabu hiyo kuwa yuko tayari kuondoka kwenda timu nyingine na hatarajii kusaini mkataba mwingine. Mkataba wa mshambuliaji huyo nyota unatarajiwa kuisha katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2014 na Santos walikuwa na nia ya kumbakisha kinda huyo mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Hatahivyo, Neymar mwenye umri wa miaka 21 ameweka wazi kuwa muda wake wa kuwepo Santos unakaribia kufikia mwishoni ambapo anataka kwenda kuonyesha ujuzi wake mahali pengine. Rodriquez alithibitisha hilo na tayari vilabu mbalimbali vikubwa barani Ulaya vimekuwa vikipigana vikumbo kutaka sahihi ya nyota huyo.

VILANOVA KUENDELEA KUINOA BARCELONA MSIMU UJAO.

KOCHA wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova ana nia ya kuendelea kuinoa klabu hiyo msimu ujao pamoja na athari za matibabu yake ya kansa ya koo na pia anaamini kuwa kikosi chake inaweza kuitoa Bayern Munich na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa katika mkutano wake wa kwanza na waandishi toka alipotoka katika matibabu ya mionzi jijini New York mwezi mmoja uliopita, Vilanova amesema bado ana shauku kubwa na kuendelea na kazi yake na hakuna mara moja alipofikiria kuacha. Vilanova amesema madaktari kuwa kitu kizuri cha kufanya kwasasa ili kumsaidia kupona ni kufanya kazi na anafurahia jambo hilo. Kocha huyo pia mbali na timu yake kugaragazwa na Bayern kwa mabao 4-0 Jumanne iliyopita lakini ameonyesha kujiamini kwamba wachezaji wake wanauwezo wa kugeuza matokeo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa katika Uwanja wa Camp Nou Jumatano ijayo. Vilanova amesema anaamini wachezaji wake wanaweza kufanya maajabu katika mchezo huo haswa ikizingatiwa watakuwa wakicheza mbele ya mashabiki wao ingawa amekiri itakuwa kazi ngumu kwani wapinzania wao nao hawataifanya kazi yao iwe rahisi.

BENCHI LAMKIMBIZA KOLO TOURE MAN CITY.

BEKI wa kimataifa wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City, Kolo Toure amethibitisha kuwa anatarajia kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu lakini hakuweka wazi timu atakayokwenda akitoka hapo. Toure mwenye umri wa miaka 32 alisajiliwa akitokea Arsenal kwa ada ya paundi milioni 16 lakini amekuwa hapati namba katika kikosi cha City baada ya kucheza mechi 12 pekee katika msimu wa mwaka 2012-2013 huku kukiwa hakuna uhakika wa kuongezewa mkataba mwingine. Toure amesema ni miaka minne toka atue City ikiwemo misimu miwili mizuri ambayo alikuwa akicheza mara kwa mara lakini anaona muda wake wa kuwepo umekwisha baada ya kusubiria kupewa mkataba mwingine kwa kipindi cha miezi miwili bila mafanikio. Amesema ni muda wa kuwaza hali yake ya mbele ingawa familia yake wakiwemo watoto wanaupenda mji huo na kudai pia hana mpango wa kutoka nje ya Uingereza kwasababu ndio nchi pekee ya Ulaya anayojua tamaduni zake toka atoke kwao Ivory Coast mwaka 2002. Klabu ya Monaco ya Ufaransa imeonyesha nia ya kutaka sahihi ya nyota huyo lakini wamedai kuwa hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanza na wakala wa mchezaji huyo.

DEL BOSQUE AALIKWA KONGAMANO LA CAF.

KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vincente del Bosque atarajiwa kuwa mgeni wakati wa kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF mwezi ujao jijini Cairo, Misri. CAF imeandaa kongamano hilo kwa kuwashirikisha wataalamu kwa lengo la kutathmini michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Gabon na Equatorial Guinea mwaka 2012 na ile ya Afrika Kusini iliyofanyika mwaka huu. Shirikisho hilo limedai kuwa lengo kubwa la kongamano hilo litakafanyika kuanzia Mei 11 mpaka 13 ni kuchambua mbinu za kiufundi katika michuano hiyo miwili iliyopita na kuangalia mapungufu yake ili waweze rekebisha au kuboresha zaidi katika michuano ijayo. Kwa mujibu wa maofisa wa CAF Del Bosque ambaye ameshinda Kombe la Dunia 2010 na Kombe la Ulaya mwaka 2012 akiwa na Hispania anategemewa kubadilishana uzoefu wake mkubwa alionao katika mkutano huo.

ERIKSSON ATUMA CV ZAKE KUOMBA KIBARUA CAMEROON.

SHIRIKISHO la Soka nchini Cameroon-Fecafoot limebainisha kuwa majina makubwa akiwemo kocha wa zamani wa Uingereza Sven-Goran Erikkson wanafikiriwa kupewa kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo. Msemaji wa Fecafoot, Junior Binyam amesema kuwa wamepokea maombi zaidi ya 100 ya makocha mbalimbali wakitaka kibarua cha kuinoa timu hiyo inayaojulikana kwa jina la utani kama Indomitable Lions. Binyam amesema kuna baadhi ya makocha wa nyumbani lakini wengi walioomba ni makocha wa kigeni wakiwemo mchezaji wa zamani na kocha wa klabu ya Paris Saint-Germain Luis Fernandez, Eriksson, kocha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC Claude Le Roy na kocha wa zamani wa Ufaransa Roger Lemerre. Katika majina hayo yote yatateuliwa majina matatu ambayo yatapelekwa kwa waziri wa michezo wan chi hiyo kwa ajili ya uteuzi rasmi wa atakayechukua nafasi hiyo ambayo iliachwa wazi na Jean Paul Akono aliyetimuliwa kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo.

Friday, April 26, 2013

WAPUUZI WACHACHE HAWAWEZI KUNIFANYA NIONDOKE ITALIA - BOATENG.

KIUNGO wa klabu ya AC Milan, Kevin-Prince Boateng amesisitiza kuwa ana furaha kuwepo klabuni hapo na kuongeza kuwa matukio ya kibaguzi ambayo yamekuwa yakimuandama katika siku za karibuni hayawezi kumfanya aondoke Italia. Boateng mwenye umri wa miaka 26 kwa mara nyingine tena amekuwa mhanga wa mambo kibaguzi wakati timu yake ilipopoteza mchezo wa Serie A dhidi ya Juventus mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo kiungo huyo wa kimataifa wa Ghana ameweka wazi kuwa hawezi kuruhusu kikundi kidogo cha watu kimfanye aondoke Italia. Boateng amesema anajisikia vyema kuwapo Milan na anachukulia kama nyumbani kwake hivyo atakaa hapo kwa kipindi kirefu kijacho. Amesema kuna kipindi alikuwa akifikiria kuondoka lakini amemua kubaki na hatarajii kwenda kokote kwasababu ya kikundi kidogo cha wapuuzi.

WATU WANAPASWA WATUHESHIMU BADALA YA KUTUPONDA - INIESTA.

KIUNGO wa klabu ya Barcelona, Andres Iniesta amesisitiza kuwa watu hawaitendei haki timu hiyo baada ya kufungwa na Bayern Munich mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Watu ambali mbalimbali wamekuwa wakiponda kiwango cha timu hiyo baada ya kupigo hicho cha kushtusha walichikipata katika Uwanja wa Allianz Arena Jumanne huku wengi wengi wao wakidai enzi za timu hiyo kung’ara zimekwisha. Hata hivyo Iniesta amesisitiza kuwa ni mapema mno kudai kuwa kiwango cha timu hiyo kimekwisha na kuwataka watu wawape heshima zaidi kwasababu wanastahili. Iniesta amesema katika kipindi cha misimu mitano wameshinda taji la Ligi ya Mabingwa mara tatu na kufika zaidi ya mara tatu nusu fainali na kwasasa wanakaribia kunyakuwa taji la nne la ligi na kwao hayo ni mafanikio makubwa. Nyota huyo aliendelea kusema kuwa badala ya watu kuwaponda wanatakiwa wawaheshimu kwasababu wamekuwa wakijitolea kwa kila kitu pindi wanapokuwa uwanjani na wamefanikiwa mambo mengi. Barcelona inatarajiwa kukwaana na Athletico Bilbao baadae leo katika mchezo wa La Liga .

SUAREZ KAONYESHA MFANO MBAYA - CAMEROON.

WAZIRI mkuu wa Uingereza, David Cameroon amesema mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez amenyesha mfano mbaya kwa kumng’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic. Suarez tayari amepewa adhabu ya kufungiwa mechi 10 na Chama cha Soka cha Uingereza kwa tukio hilo. Akihojiwa katika kipindi kikoja cha radio nchini Uingereza, Cameroon amesema akiwa kama baba na binadamu hadhani kama wanapaswa kutoa adhabu kali wakati mchezaji akifanya vitendo kama hivyo. Waziri mkuu huyo aliendelea kusema kuwa ni jambo linaloeleweka kama jopo la FA likikutana kutoa adhabu hiyo litamchukulia mchezaji huyo kama kioo cha jamii hivyo kutoa adhabu hiyo ili iwe mfano na kwa nyota wengine ambao vijana wadogo huwaiga kutokana na mafanikio waliyopata. Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers amedai kuwa kauli hiyo ya Cameroon ndio imepelekea Suarez kupewa adhabu kubwa ingawa waziri mkuu huyo alipinga vikali akidai kuwa amesema hivyo kama baba anayetizama soka.

BAYERN YAMKANA LEWANDOWSKI.

KLABU ya Bayern Munich ya Ujerumani imetoa taarifa kupinga kwamba wamefikia makubaliano ya uhamisho na mshambuliaji wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski. Wakala wa mshambuliaji wa kimataifa wa Poland, Maik Barthel jana alidai kuwa mteja wake huyo anataka kuondoka Dortmund katika kipindi cha majira kiangazi na kuongeza kuwa wameshafikia makubaliano binafsi na klabu nyingine na kuzua uvumi kwamba atahamia Bayern. Hata hivyo Bayern wamebainisha kuwa hakuna ukweli wowote kuhusiana na taarifa kwamba tayari wamemsajili Lewandowski. Lewandowski mwenye umri wa miaka 24 ana mkataba na Dortmund unaomalizika mwaka 2014 lakini ameshatoa msimamo wake kuwa hana mpango wa kuongeza mkataba mwingine na klabu hiyo.

SUAREZ AMEJITAKIA - WENGER.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amedai kuwa adhabu ya kufungiwa mechi 10 aliyopewa mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez ni matokeo ya tabia zake kipindi cha nyuma. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay amekubali adhabu ya kufungiwa mechi tatu kwa tukio alilofanya na amepewa siku moja kukata rufani dhidi ya adhabu ya mechi saba zaidi zilizoongezwa. Wenger amesema anaamini tabia za nyota huyo kipindi cha nyuma ndio zimepelekea kupewa adhabu za mara kwa mara hivyo hana wa kumlaumu zaidi ya yeye mwenyewe. Suarez amekuwa akiingia matatani mara kwa mara kutokana na tabia zake za kushindwa kudhibiti hasira zake ambapo aliwahi kufungiwa mechi saba wakati akiwa katika klabu ya Ajax Amsterdam kwa kumng’ata kiungo wa PSV Eindhoven Otman Bakkal kwenye bega Novemba mwaka 2010. Mbali na tukio hilo nyota huyo ambaye alinunuliwa na Liverpool kwa paundi milioni 23 alifungiwa mechi nane na kutozwa faini ya paundi 40,000 na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa kumfanyia vitendo vya kibaguzi beki wa Manchester United Patrice Evra.

Thursday, April 25, 2013

RUVU SHOOTING, SIMBA SASA KUCHEZA MEI 5.

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Ruvu Shooting na Simba iliyokuwa ichezwe leo (Aprili 25 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa itafanyika Mei 5 mwaka huu kwenye uwanja huo huo. Mabadiliko hayo yametokana na Serikali kuutumia uwanja kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za Muungano ambazo kitaifa zitafanyika kesho (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawaomba radhi washabiki kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na mabadiliko hayo na ghafla. Ratiba ya mechi nyingine za VPL zinabaki kama zilivyo. Ligi hiyo inaendelea kesho (Aprili 26 mwaka huu) kwa mechi kati ya Coastal Union na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Jumapili (Aprili 28 mwaka huu) itakuwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni Simba dhidi ya Polisi Morogoro.

GIROUD ASHANGAZWA NA UAMUZI WA FA.

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Oliver Giroud amekishambulia Chama cha Soka nchini Uingereza-FA baada ya uamuzi wake wa kutupilia rufani yake ya kupinga kadi nyekundu aliyopewa. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alitolewa nje na mwamuzi Andre Marriner kwa kumchezea vibaya Stanislav Manolev wakati wa mchezo baina ya Arsenal na Fulham Jumamosi iliyopita hivyo kupelekea kufungiwa mechi tatu kwasababu ya kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja. Giroud mwenye umri wa miaka 26 amekuwa akijitetea kwamba aliteleza bahati mbaya kwenye tukio hilo na baada ya rufani yake kutupiliwa mbali amewakosoa FA kwa hatua waliyochukua. Giroud amesema ameshangazwa na hatua iliyochukuliwa na FA dhidi yake, sio kwamba imemuumiza ila anadhabu sheria za Uingereza zimekuwa kali sana ukilingasha na makosa yanayofanywa.

MBONA AIWINDA NAFASI YA KUINOA INDOMITABLE LIONS.

MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Patrick Mboma ameonyesha nia yake ya kuifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo na anakusudia kutuma maombi yake Shirikisho la Soka la Cameroon-Fecafoot siku moja baada ya Waziri wa Michezo Adoum Garoua kulitaka shirikisho hilo kufanya mchakato wa kupata kocha mpya. Mshambuliaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 42 alikuwemo katika kikosi cha nchi hiyo ambacho kilinyakuwa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2000 na 2002 na pia kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika. Hata hivyo Mboma hajawahi kufundisha timu yoyote na wadau wa soka nchini humo wamedai kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Paris Saint Germain na Parma hana uzoefu wa kutosha wa kumuwezesha kupewa nafasi ya kuinoa timu hiyo. Lakini pamoja na wadau kuponda uwezo wake Mboma amesema haimkatishi tamaa na atatuma maombi yake kuiwinda nafasi hiyo.

BRAZIL YAZOMEWA NA MASHABIKI WAKE.

TIMU ya taifa ya Brazil imejikuta ikizomewa na mashabiki wake wenyewe baada ya kujikuta wakitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Chile katika mechi ya kwanza ya kirafiki katika uwanja utakaotumika kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2014. Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja mpya uliofanyiwa ukarabati wa Mineirao uliopo jijini Horizonte ni ya mwisho kwa kocha Luis Felipe Scolari kabla ya kutaja kikosi cha mwisho Mei 14 kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Juni mwaka huu. Pamoja na mashabiki wengi wapatao 53,000 kujitokeza katika mchezo huo, walionyesha kutofurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa baada ya Chile kuonekana wakimiliki mpira zaidi ya wenyeji wao. Mshambuliaji nyota wa Brazil, Neymar akihojiwa mara baada ya mchzo huo amesema hali ya kuzomewa na mashabiki wao wameshaizoea na wanaichukulia hali hiyo kama changamoto.

MWAMUZI AANGUKA UWANJANI NA KUFA BURKINABE.

MWAMUZI wa Burkina Faso ameanguka na kufariki dunia jana jijini Ouagadougou wakati akifanyiwa vipimo vya afya. Mwamuzi huyo Ouangraoua Moumouni ambaye pia alikuwa katibu mkuu wa Chama cha Waamuzi wa nchi hiyo-UNAF , alikuwa akifanyiwa majaribio yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka la Burkina Faso-FBF alianguka uwanjani wakati zoezi hilo likiendelea. Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 38 alitangazwa amekufa muda mchache baadae wakati akipatiwa huduma ya kwanza uwanjani hapo lakini familia yake ilikataa uchunguzi wa mwili wake na kuamua kumzika siku hiyohiyo. Moumouni kwa kawaida amekuwa akisimamia mechi za Ligi Kuu nchini Burkina Faso pamoja na zile za mashindano ya Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF.

MBABE WA MADRID AWA LULU ULAYA.


MUDA mchache baada ya kuiangamiza Real Madrid kwa kufunga mabao manne, mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Robert Lewandowski amekuwa ‘almasi’ baada vilabu mbalimbali kujaribu kuiwinda sahihi yake. Vilabu hivyo ni pamoja na Bayern Munich na Manchester United ambao wameanza kuhaha kila kona ili kuhakikisha wanamnasa nyota huyo mapema. Mabao manne aliyofunga dhidi ya Real Madrid, yamemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuifunga timu hiyo ya Hispania mabao manne katika mechi ya ligi ya mabingwa. United wangekuwa wa kwanza kumpata nyota huyo lakini meneja wake Alex Ferguson akataka kuwe na subira lakini Bayern ambao wamenyakuwa ubingwa wa Ujerumani wanaonekana ndio wenye nafasi kubwa ya kumpata kwasasa.

Wednesday, April 24, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF LEO.

TAIFA STARS KUCHEZA MICHUANO YA COSAFA
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayofanyika Julai mwaka huu nchini Zambia. Taifa Stars inashiriki michuano hiyo ya timu za Taifa za nchi wanachama wa COSAFA ikiwa timu mwalikwa. Nchi wanachama wa COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoro, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. Michuano hiyo itafanyika kuanzia Julai 6 hadi 21 mwaka huu katika miji ya Lusaka, Ndola na Kabwe. Ratiba ya makundi ya michuano hiyo itapangwa Mei 3 mwaka huu jijini Lusaka. Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika miaka mitatu iliyopita. Hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo baada ya kucheza ya kwanza iliyofanyika mwaka 1996 nchini Zimbabwe. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi ujao kujiandaa kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech. Juni 16 mwaka huu Taifa Stars itacheza na Ivory Coast jijini Dar es Salaam katika mechi nyingine ya mchujo ya Kombe la Dunia wakati Juni mwishoni na Julai mwanzoni itacheza mechi ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Uganda. Wakati huo huo, waandishi wa habari wanaotaka kuripoti michuano hiyo wanatakiwa kuwasilisha majina yao TFF kabla ya Aprili 27 mwaka huu ili maombi yao yatumwe COSAFA kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho (Accreditation).

BABU YAKE VAN PERSIE AMPONGEZA MJUKUU WAKE.

BABU yake mshambuliaji nyota wa Manchester United, Robin Van Persie amempongeza mjukuu wake kwa kunyakuwa taji la Ligi Kuu nchini Uingereza na kudai kuwa amemuandalia zawadi kubwa ya busu wakati atakapokutana na nyota huyo mwezi ujao. Mzee huyo aitwaye Wim Camp alikuwa akitizama katika luninga akiwa nyumbani kwake Prinksenbeek, Breda nchini Uholanzi wakati mwanae alipofunga mabao yote matatu katika ushindi uliowahakikishia ubingwa wa ligi hiyo huku wakiwa wamebakiwa na michezo sita mokononi. Camp mwenye umri wa miaka 92 bado hajazungumza na mjukuu wake toka wafanikiwe kunyakuwa taji hilo lakini amedai anasubiri kwa hamu ili aweze kumpa pongezi zake kipindi watakapokutana. Mzee huyo amedai anatarajia kumtembelea mjukuu wake Mei 4 wakati ambapo Manchester United watakwaana na Chelsea ingawa amedai kuwa mechi hiyo haitakuwa muhimu sana lakini lazima amkumbatie na kumpiga busu kwa kazi nzuri aliyofanya. 

MAREKANI KUMDAI ARMSTRONG FIDIA.

SERIKALI ya Marekani inataka fidia ya zaidi paundi milioni 78 baada ya kufungua mashtaka dhidi ya mwendesha baiskeli Lance Armstrong. Mwendesha baiskeli huyo mwenye umri wa miaka 41 ambaye amefungiwa anatuhumiwa kukiuka masharti ya mkataba na timu yake ya zamani na anatajwa kupata utajiri kwa njia ya udanganyifu wakati alipodanganya na kushinda mashindano ya Tour de France. Katika taarifa iliyowasilishwa mahakamani imedai kuwa watoa Huduma za Posta nchini Marekani wamekuwa wakilipa kiasi cha paundi milioni 26 kwa ajili ya udhamini wa timu ya baiskeli ya nchi hiyo kuanzia mwaka 1998 mpaka 2004. Armstrong amekiri kuwa alikuwa akitumia dawa za kuongeza nguvu katika mataji yake yote saba ya Tour de France aliyowahi kushinda.

LEOZ AJIUZULU UJUMBE FIFA.

MJUMBE wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Nicolas Leoz kutoka Paraguay amejiuzulu wadhifa wake huo kutokana na kile alichodai kuwa na matatizo ya kiafya ikiwa ni siku chache kabla ya shirikisho hilo halijatangaza uchunguzi wa bakshishi katika michuano ya Kombe la Dunia. FIFA ilithibitisha kupokea barua ya Leoz mwenye umri wa miaka 84 ambaye pia ataachia ngazi wadhifa wake wa urais wa Shirikisho la Soka la Amerika Kusini-CONMEBOL. Leoz ambaye amefanyiwa upasuaji wa moyo mara kadhaa amekuwa mjumbe katika bodi ya FIFA kuanzia mwaka 1998 na amekuwa rais wa CONMEBOL kuanzia mwaka 1986. Katika barua yake Leoz amesisitiza kuwa uamuzi aliochukua ni binafsi kutokana na matatizo ya kiafya aliyonayo kwani hawezi kusafiri mara tano kwa mwaka kama ilivyokuwa zamani.

CAVANI ATENGEWA MKATABA MNONO NA PSG.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG ya Ufaransa imemtengea mkataba mnono wa euro milioni 8.5 kwa msimu mshambuliaji nyota wa Napoli ya Italia Edinson Cavani. Imeripotiwa na vyombo vua habari nchini humo kuwa mkurugenzi wa michezo wa klabu ya PSG, Leonardo ameshafanya vikao kadhaa na wakala wa nyota huyo kuzungumzia uhamisho wake kutoka Napoli ambao unakaribia kufikia kiasi cha euro milioni 63. Mbali na PSG vilabu vingine vikubwa barani Ulaya ambavyo vimeonyesha nia ya kuhitaji sahihi ya nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay ni pamoja na Real Madrid, Manchester City na Chelsea. Cavani mwenye umri wa miaka 26 ana mkataba na Napoli mpaka 2015 ambao unamuwezesha kulipwa kiasi cha euro milioni 1.4 kwa msimu.

RONALDINHO APEWA UNAHODHA MECHI DHIDI YA CHILE.

RONALDINHO anatarajiwa kupewa unahodha wa timu ya taifa ya Brazil katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Chile hatua ambayo itamuweka katika nafasi nzuri ya kujumuishwa katika kikosi kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho. Kocha wa Brazil Luis Felipe Scolari ameonyesha matumaini yake kwa Ronaldinho ambaye amaewahi kunyakuwa tuzo ya mchzaji bora wa dunia mara mbili kwa kumpa unahodha kwenye mechi ya mwisho kabla hajatangaza kikosi cha michuano ya Kombe la Shirikisho. Scolari tayari amebainisha kuwa kuna uwezekano akamchukua kati ya Ronaldinho au Kaka kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika June mwaka huu. Kaka atakosa mchezo dhidi ya Chile kwasababu ni wachezaji wanaocheza katika vilabu vya Brazil peke ndio waliochaguliwa kwa ajili ya mchezo huo kirafiki kitendo ambacho kinampa nafasi kubwa kama akionyesha kiwango kizuri.

Bayern Munich VS Barcelona 4-0 (23-4-2013) Highlights

MABINGWA wa Ujerumani, Bayern Munich wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya baada ya kuitandika Barcelona 4-0 katika mchezo wa kwanzawa nusu fainali nchini Ujerumani. Mabao mawili ya Thomas Müller, na yale ya Mario Gomez na Arjen Robben yaliizamisha Barcelona ambayo ilikuwa na nyota wake wote wakutegemewa, akiwemo Messi ambaye alikosa michezo kadhaa kabla ya kuanzishwa usiku huu. Hii imekuwa mara ya kwanza kwa Barcelona kufungwa mabao 4-0 tangu mwaka 1997 walipofungwa na Dynamo Kiev ya Urusi mwaka 1997 kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani ulaya. Bayern Munich wametoka kutawazwa kuwa mabingwa wa Ujerumani wiki chache zilizopita na iwapo watafanikiwa kuiondosha Barcelona na kutinga hatua ya fainali ya michuano ya klabu bingwa, itakuwa fainali yao ya tatu kushiriki ndani ya miaka minne. Michuano hiyo itaendelea tena leo usiku ambapo mahasimu wa Barcelona, Real Madrid watakuwa na kibarua kizito pale itakapokaribishwa katika Uwanja wa Signal-Iduna-Park kukwaana na wenyeji Borussia Dortmund kwenye mchezo unaotaajiwa kuwa mgumu na wa kusisimua.

Tuesday, April 23, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KOCHA KIM ATANGAZA YOUNG TAIFA STARS
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametangaza timu ya pili ya Taifa (Young Taifa Stars) atakayoitumia kuangalia wachezaji ambao baadaye anaweza kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa. Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo (Aprili 23 mwaka huu) kabla ya kutaja kikosi hicho, Kim amesema timu hiyo ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliozinduliwa Aprili 4 mwaka huu ukilenga kuendeleza wachezaji. Amesema timu hiyo inajumuisha wachezaji ambao wamepita umri wa kuchezea timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na wakubwa ambao hawajapata fursa ya kuingia Taifa Stars, lakini atatumia Young Taifa Stars kuangalia uwezo wao. “Timu hii ni kiungo kati ya vijana na wakubwa. Wengi wa wachezaji watakuwa vijana, lakini wakubwa wachache watapata fursa ya kuwemo ili kuangalia uwezo wao hata kama uko nyuma waliwahi kuchezea Taifa Stars. Lakini timu hii vilevile ni changamoto wa wachezaji wa Taifa Stars kuwa wapo wanaosubiri wazembee ili wachukue nafasi zao,” amesema. Young Taifa Stars yenye wachezaji 30 itakuwa na kambi ya siku tano jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 2 hadi 6 mwaka huu. Wachezaji walioitwa ni Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ali Mustapha (Yanga) ambao ni makipa. Mabeki ni Kessy Hassan (Mtibwa Sugar), Kennan Ngoma (Barnsley FC, Uingereza), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), David Mwantika (Azam), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Waziri Salum (Azam), Samih Nuhu (Azam) na Emily Mgeta (Simba). Viungo ni Haruna Chanongo (Simba), Edward Christopher (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), William Lucian (Simba), Jonas Mkude (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jimmy Shoji (JKT Ruvu), Abdallah Seseme (Simba), Ramadhan Singano (Simba), Farid Mussa (Azam) na Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar). Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Zahoro Pazi (JKT Ruvu), Twaha Hussein (Coastal Union), Abdallah Karihe (Azam) na Juma Luizio (Mtibwa Sugar).

AFRICAN LYON, JKT RUVU KUUMANA CHAMAZI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 24 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya wenyeji African Lyon na JKT Ruvu. Mechi hiyo namba 165 itachezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Kamishna Hamisi Kisiwa wa Dar es Salaam. Waamuzi wa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni ni Hashim Abdallah, Omari Kambangwa, Abdallah Selega na Said Ndege wote wa Dar es Salaam.

KANSELA MERKEL ASONONESHWA NA KASHFA YA UKWEPAJI KODI YA HOENESS.

KANSELA wa Ujerumani Angela Merkel amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi inayomkabili rais wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness, huku Hoennes mwenyewe akisema hatajiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi unaoendelea dhidi yake. Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema kwamba watu wengi nchini Ujerumani wamefadhaishwa na Hoennes, na hivyo ndivyo alivyo pia Kansela Merkel. Kwa mujibu wa Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa zaidi kutokana na ukweli kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio tu kwamba anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga mkono jithada kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni kwenye jamii ya Ujerumani. Mwishoni mwa wiki, Hoeness alinukuliwa na gazeti la kila wiki la Focus akisema kwamba aliripoti mwenyewe kwa mamlaka juu ya akaunti yake ya fedha kwenye benki moja nchini Switzerland hapo mwezi Januari. Waendesha mashitaka wamekiri kwamba wameanzisha uchunguzi huo kufuatia ripoti iliyopelekwa kwao na Hoeness mwenyewe kupitia mshauri wake wa masuala ya fedha. Hata hivyo, Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana mpango wowote wa kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi. 

BAYERN VS BARCELONA HAPATOSHI LEO ALLIANZ ARENA.

Vita kusaka tiketi ya kusafiri kwenda jijini London kwenye mchezo wa fainali wa klabu bingwa barani Ulaya inaanza usiku huu kati ya Mabingwa wa soka nchini Ujerumani Bayern Munich dhidi ya inayotajwa kuwa timu bora kwa vilabu vya soka duniani kwa wakati huu Barcelona. Kocha wa Bayern, Jupp Heynckes amesema haogopeshwi na urejeo wa nyota wa Barcelona, Lionel Messi kuelekea mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya. Messi hajacheza mchezo wowote wa Barcelona toka alipoingia kama mchezaji wa akiba na kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainali katika mchezo robo fainali dhidi ya Paris St-Germain ya Ufaransa. Lakini kuna kila dalili Muanjetina huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye ndiye mchezaji bora wa dunia kwa sasa,akajumuishwa kwenye kikosi cha Barcelona kwenye mchezo wa usiku wa leo. Mwezi uliopita Messi aliweka rekodi kwenye ligi ya Hispania kwa kuwa mchezaji aliyezifunga timu zote zinazoshiriki ligi kuu nchini humo maarufu kama La Liga kwa misimu miwili mfululizo. Barcelona inapambana kutaka kutwaa taji la tatu la klabu bingwa barani Ulaya ndani ya miaka mitano, Huku Bayern ambao msimu ujao watakuwa chini ya aliyekuwa kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, wao wanapambana kutafuta nafasi ya kucheza fainali yao ya tatu ndani ya miaka minne. Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Allianz Arena mjini Munich nchini Ujerumani,majira ya saa nne kasorobo usiku kwa saa Afrika Mashariki.

ADHABU KALI YAMSUBIRIA SUAREZ.

Chama cha soka nchini Uingereza, FA kimenuia kumpa adhabu kali mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez kwa kitendo chake cha kumng'ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic katika mchezo wa Jumapili iliyopita baina ya Liverpool na Chelsea,mchezo uliomalizika kwa sare ya 2-2. FA imesema mwamuzi wa mchezo huo hakukiona kitendo hicho uwanjani lakini marejeo ya picha za mchezo huo zilionyesha Suarez alimng'ata Ivanovic,kitendo ambacho kinachukuliwa kama vurugu mchezoni na adhabu yake ni kufungiwa mechi tatu lakini adhabu hiyo haitoshi kwa tukio alilolifanya Suarez. Suarez amepewa muda wa mpaka saa 12 jioni jumanne ya April 23, awe amekubali au kukataa kosa hilo kabla ya tume ya kudhibiti maadili haijakutana hapo siku ya jumatano kutoa hukumu stahili kwa kosa hilo. Mwenyewe Suarez aliishakiri kufanya kosa hilo na kumuomba Ivanovic msamaha kwa njia ya simu na kuwaomba mashabiki wa soka wamsamehe kwa kosa hilo. Klabu yake ya Liverpool imempa adhabu ya kumpiga faini mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay.

Monday, April 22, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

RAIS TENGA ATOA MIPIRA YA DOLA 30,000
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai vya kuendeleza vijana (academies). Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL). Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali popote. “Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga. Amesema amesema mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.
Rais Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira. Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.
“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama watoto hawachezi. “Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,” amesema Rais Tenga. Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25 (minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne). Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala. Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani.



COASTAL, AZAM KUCHEZA SIKU YA MUUNGANO
Timu za Coastal Union ya Tanga na Azam zitapambana Aprili 26 mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27 mwaka huu, lakini imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa fursa Azam kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco. Mechi hiyo itachezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa (Pwani), Vicent Mlabu (Morogoro) wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Mohamed Mkono wa Tanga. Charles Komba wa Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya 24. Baada ya mechi ya Tanga, Azam itarejea Dar es Salaam siku inayofuata tayari kwa safari ya kwenda Rabat itakayofanyika Aprili 28 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa wikiendi ya Mei 3, 4 au 5 mwaka huu. Keshokutwa (Aprili 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Iwapo Azam itafanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho kutakuwa na marekebisho ya ratiba ya VPL. Hiyo ni kutokana na raundi inayofuata ya Kombe la Shrikisho kuchezwa wikiendi ya Mei 17, 18 na 19 mwaka huu ambapo bado haijajulikana Azam itaanzia wapi (nyumbani au ugenini) iwapo itavuka. Mechi nyingine za VPL mwezi ni Aprili 25 (Ruvu Shooting vs Simba- Uwanja wa Taifa), na Aprili 28 (Simba vs Polisi Morogoro- Uwanja wa Taifa).



WAMOROCCO WA AZAM WAINGIZA MIL 50/-
Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS FAR Rabat ya Morocco iliyochezwa juzi (Aprili 20 mwaka huu) imeingiza sh. 50,850,000. Fedha hizo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka suluhu zimetokana na watazamaji 8,268 waliokata tiketi. Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 7,354. Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za tiketi sh. 5,575,500, asilimia 15 ya uwanja sh. 6,791,175, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 4,527,450 na asilimia 75 iliyokwenda kwa klabu ya Azam ni sh. 33,955,875. Mechi iliyopita ya Azam katika michuano hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ya Liberia iliingiza sh. 44,229,000 kutokana na watazamaji 17,128 waliokata tiketi. Viingilio vilikuwa sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A.



MECHI YA JKT RUVU, YANGA YAINGIZA MIL 66/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga iliyochezwa jana (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 66,568,000 kutokana na watazamaji 11,864. Viingilio katika mechi hiyo namba 106 iliyomalizika kwa Yanga kutoa dozi ya 3-0 kwa wenyeji wao vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,702,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,154,440.68. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,984,450.40, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,790,670.24, Kamati ya Ligi sh. 4,790,670.24, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,395,335.12, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 931,519.21 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 931,519.21.

BAHRAIN GRAND PRIX KUPEWA MIAKA MINGINE MITANO.

MMILIKI wa mashindano ya magari yanayokwenda kasi ya langalanga Bernie Ecclestone amesema atakuwa mtu mwenye furaha kama watawaongeza mkataba mwingine wa miaka mitano Bahrain Grand Prix pamoja na utata uliopo juu ya suala la usalama. Ecclestone ambaye mara nyingi amekuwa akiikosoa serikali ya Bahrain kwa kupewa dhamana na kuandaa mashindano hayo kwasababu ya kutoa nafasi kwa waandamanaji wa kisiasa. Lakini mara baada ya mashindano yaliyomalika Jana na taji kuchukuliwa na Sebastian Vettel wa Red Bull, bosi amesema watakuwa na furaha kuwapa Bahrain mkataba mpya wa miaka mitano kwani anadhani wamefanya kazi nzuri na hajaona tatizo lolote. Miaka miwili iliyopita mashindano hayo yalisogezwa mbele na baadae kusimamishwa kabisa baada ya maandamano ya kidemokrasia yasiyokoma yaliyopelekea watu 35 kufariki kutokana na vurugu hizo. Mwaka jana Bhrain iliruhusiwa kuandaa michuano hiyo baada ya Ecclestone na Chama cha Mashindano ya Langalanga-FIA kudai kuwa wamehakikishiwa kuwepo kwa usalama wa kutosha katika eneo hilo.

CISSE AONJA JOTO LA UBAGUZI BAADA YA KUAMUA KUTOKA NA MZUNGU.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Newcastle United, Papiss Cisse na rafiki yake wa kike wamekuwa wakitumiwa ujumbe na watu mbalimbali ambao ni wabaguzi wakipinga mahisiano yao. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 27 ana mahusiano na Rachelle Graham mwenye umri wa miaka 22 ambaye ni mnyange wa mji wa Newcastle. Mnyange huyo ambaye ni mzungu alilikuwa akichangisha fedha kwa kuruka umbali wa futi 13,000 kutoka angani ili ziweze kusaidia kununulia gari la wagonjwa kwenda Senegal na wawili hao walitumiwa ujumbe wa kibaguzi katika mtandao kwa sababu ya tukio hilo. Polisi wa Newcastle wanafuatialia tukio hilo kama uhalifu wa chuki baada ya mama yake Rachelle kutoa taarifa za mtandao huo.

PFA KUMPA USHAURI NASAHA SUAREZ.

CHAMA cha Wanasoka wa Kulipwa-PFA kimesema kuwa mshambuliaji nyota wa Liverpool, Luis Suarez atapatiwa ushauri wa namna ya kuzikabili hasira zake kufuatia tukio lake la kumg’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay tayari ameshamuomba radhi Ivanovic kwa tukio hilo alilofanya katika mchezo wa ligi baina ya timu hizo ambao uliisha kwa sare ya mabao 2-2 lakini klabu yake imeshamtoza faini na kunauwezekano mkubwa FA nao wakatoa adhabu baadae. Suarez mwenye umri wa miaka 26 alifungiwa kucheza mechi saba baada ya kufanya tukio kama hilo wakati akiwa katika klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi kipindi cha nyuma ambapo alimng’ata Otman Bakkal wa PSV. Nyota huyo asiyetabirika pia alishawahi kufungiwa mechi nane katika Ligi Kuu nchini Uingereza baada ya kumfanyia vitendo vya kibaguzi Patrice Evra wa Manchester United. Ofisa Mkuu wa PFA Gordon Taylor amesema hakuna shaka juu ya kiwango bora alichonacho nyota huyo lakini inasikitisha kwa vitendo vya ambavyo amekuwa akivifanya ndio maana wameamua kumsaidia ili aweze kuzikabili hasira zake.