TIMU ya Mbeya City imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano mipya ya Nile Basin iliyoandaliwa na Baraza la Michezo kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati huko jijini Khartoum, Sudan. Mbeya City ambayo inashiriki michuano yake ya kwanza ya kimataifa ilitinga hatua hiyo baada ya kutoa sare ya bila ya kufungana na timu ya Etincelles ya Rwanda. Katika robo fainali Mbeya City watakwaana na Victoria University ya Uganda huku mechi zingine kwa timu zilizongia hatua hiyo ziliwakutanisha AFC Leopard ya Kenya itachuana na Defence ya Ethiopia. Mechi nyingine itashuhudia Al Merreikh ya Sudan wakichuana na Tchite Academy ya Burundi huku Al-Ahli Shandi wao wakiwa na kibarua kizito cha kupambana na Malakia ya Sudan Kusini.
Thursday, May 29, 2014
SAMATA, ULIMWENGU KUIONGEZEA NGUVU STARS.
KLABU ya TP Mazembe imewaruhusu wachezaji wake Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kujiunga na timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo tayari imewasili Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika. Taifa Stars itacheza na Zimbabwe (Mighty Warriors) katika mechi ya marudiano raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Mechi hiyo itachezwa Jumapili (Juni 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare. Samata na Ulimwengu watawasili Harare kesho (Mei 30 mwaka huu) saa 3.40 usiku kwa ndege ya Kenya Airways. Watajiunga na TP Mazembe mara baada ya mchezo huo ambapo Juni 2 mwaka huu watakwenda moja kwa moja Ndola, Zambia ambapo timu yao imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
MINALA AJISAFISHA BAADA YA KUGUNDULIKA KUWA HAKUDANGANYA UMRI WAKE.
CHAMA cha Soka nchini Italia kimethibitisha kuwa kiungo wa klabu ya Lazio, Joseph Minala hakudanganya kuhusiana na umri wake. Mtandao mmoja wa soka barani Afrika ulitoa madai Februari mwaka huu kuwa Minala ambaye ni mzaliwa wa Cameroon ana umri wa miaka 42 na sio miaka 17 anayotaja yeye. Suala hilo lilipelekea maofisa kufanyia uchunguzi taarifa hizo ambapo ilipelekea Manala mwenye kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo. Katika taarifa yake mara baada ya uchunguzi FIGC ilidai kuwa hawakupata ushahidi wowote ambao ungepelekea hatua za nidhamu kuchukuliwa. Minala alijiunga na Lazio yenye maskani yake jijini Rome majira ya kiangazi mwaka jana na aliiwakilisha timu hiyo katika michuano ya vijana ya Kombe la Viareggio Februari mwaka huu.
ARSENAL WAMPANDIA NDEGE MORATA.
MAOFISA wa klabu ya Arsenal, wamesafiri kwenda Hispania kwa matumaini ya kumamilisha dili kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid Alvaro Morata. Mshambuliaji huyo amekuwa akiwindwa na Arsene Wenger kwa muda mrefu na klabu imeamua kuanza harakati za kumsajili nyota huyo mwenye miaka 21 mapema, kwani Juventus nao pia wanamuwinda. Madrid wako tayari kumuuza lakini wanatarajiwa kusisitiza kutaka dau lao walilomnunulia kitu ambacho kinaonekana kitakuwa kigingi kikubwa kwa timu zinazomuhitaji. Arsenal walijaribu kumsajili kinda huyo wa kimataifa wa Hispania majra ya kiangazi mwaka jana na safari hii wanaamini uhakika wa kupata namba katika kikosi cha kwanza atakaoupata utawasaidia kumvutia kwao. Morata amefunga mabao tisa katika mechi 28 alizocheza akiwa na Madrid msimu huu na alitokea benchi katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Jumamosi na kuisadia timu yake kuisambaratisha Atletico Madrid. Arsenal pia wanamtaka mshambuliaji mwingine wa Madrid Karim Benzema lakini Carlo Ancelotti anamtaka nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kusaini mkataba mpya na timu hiyo.
MAJERUHI YAMKOSESHA WOODS MICHUANO YA US OPEN.
MCHEZAJI nyota wa gofu, Tiger Woods amejitoa katika michuano ijayo ya wazi ya Marekani ili aweze kupona sawasawa kufuatia upasuaji wa mgongo aliofanyiwa. Woods mwenye umri wa miaka 38 raia wa Marekani ambaye ni bingwa wa mataji makubwa 14 ya gofu, hajaonekana katika viwnaja vya gofu toka alipocheza michuano ya WGC-Cadillac Machi mwaka huu. Nyota huyo ambaye kwasasa ameporomoka katika orodha za ubora duniani mpaka nafasi ya tatu alikaririwa katika mtandao wake akidai kuwa bado hayuko fiti kwa ajili ya mashindano. Taarifa yake iliendelea kudai kuwa pamoja na kukosa mashindano mawili makubwa ya mwanzo na michuano mingine muhimu bado anaamini atarejea tena uwanjani mwaka huu. Woods alikosa michuano ya Masters iliyofanyika April mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza toka aanze kucheza mchezo huo baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.
HATUNA MATATIZO YA KIFEDHA YATAKAYOTULAZIMU KUUZA NYOTA WETU - MARIN.
OFISA mkuu wa klabu ya Atletico Madrid Angel Gil Marin amezionya timu zote barani Ulaya kuwa hawahitaji kuuza mchezaji yoyote kwa ajili ya matatizo ya kifedha. Baadhi ya wachezaji muhimu wa timu hiyo wamekuwa wakihusishwa na tetesi za kuondoka Vicente Calderon baada ya msimu mzuri ambao uliwasaidia kushinda taji la La Liga na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Pamoja na kuwa na nguvu ndogo za kiuchumi kulinganisha na wapinzani wao Real Madrid na Barcelona, Marin amesema hawana haja ya kuuza wachezaji wao ili waweze kuinuka kiuchumi. Marin pia alidokeza kuwa kunaweza kuwa na mikataba mipya na iliyoboreshwa kwa baadhi ya wachezaji wao huku nyota waliong’ara msimu huu kama Diego Costa, Miranda na Raul Garcia wakiripotiwa kuwindwa na vilabu vikubwa barani humo. Katika taarifa yake iliyotumwa katika mtandao wa timu hiyo Marin amesema hawana haja ya kuuza mchezaji yoyote katika kikosi chao cha kwanza ili waweze kuweka mahesabu yao sawa kwani wako tayari kuwaboreshea mikataba yao na kuwapa minono zaidi.
FABIANSKI AKUBALI KWENDA SWANSEA.
GOLIKIPA wa Arsenal, Lukasz Fabianski amekubali kujiunga na Swansea City wakati mkataba wake na klabu hiyo utakapomalizika mwezi ujao. Golikipa huyo wa kimataifa wa Poland alikataa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo ili kumzuia asiondoke na sasa ameamua kuhamia katika Uwanja wa Liberty unatumiwa na Swansea. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao, Arsenal walithibitisha kuondoka kwake na kumshukuru golikipa huyo kwa mchango wake aliotoa katika kipindi chote alichokuwepo na kumtakia kila la kheri huko anapokwenda. Golikipa huyo mwenye umri wa miaka 29 alijiunga na Arsenal akitokea Legia Warsaw mwaka 2007 na kucheza mechi 78 katika kikosi cha kwanza katika mashidano toka alipojiunga nao.
BARCELONA BADO VIWANGO - XAVI.
KIUNGO mahiri wa Barcelona, Xavi amesisitiza kuwa klabu hiyo bado itabakia kama moja ya timu kubwa duniani na anafikiri timu bora pekee ndio zinaweza kuifunga. Barcelona walipoteza taji la La Liga kwa Atletico Madrid huku waking’olewa na vijana haohao wa Diego Simeone katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku Real Madrid wakiwatambia kwa kuwafunga katika fainali ya Kombe la Mfalme. Pamoja na hayo Xavi haamini kama msimu uliopita unatoa ishara kwamba zama zao za kutamba zimekwisha. Xavi amesema wamekosa taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufungwa na timu hiyohiyo Atletico ambao walishinda taji la ligi na kuwa washindi wa pili Ulaya ndio maana anasema timu bora pekee ndio itakayoweza kuifunga Barcelona. Mara ya mwisho Barcelona kumaliza msimu mikono mitupu yaani bila taji lolote ilikuwa msimu wa mwaka 2007-2008.
WENGER ALIIPA TIMU YA TAIFA KIPAUMBELE KULIKO KLABU - WILSHERE.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger alikataa kumuharakisha kumchezesha Jack Wilshere baada ya kuumia kwasababu alikuwa akitaka kuhakikisha kiungo huyo anakuwa fiti kwa ajili ya Kombe la Dunia. Wilshere amesema Wenger ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa soka la kimataifa katika siku za nyuma alijiandaa kujitoa muhanga kwa balaa la majeruhi la muda lililoikumba Arsenal mwishoni mwa msimu ili aweze kuisadia timu ya taifa. Wilshere ambaye aliumia mguu akiwa katika majukumu ya kimataifa katika mechi kati ya Uingereza na Denmark Machi mwaka huu amesema alikuwa akidhani yuko tayari lakini Wenger alimkatalia kwa kumtaka afanye mazoezi zaidi ili awe fiti kwa ajili ya Kombe la Dunia. Nyota huyo mwenye miaka 22 amesema alijisikia furaha kupata ushauri huo mzuri kutoka kwa meneja wake ambaye ana uzoefu wa muda mrefu.
OSCAR AKANUSHA TETESI ZA KUTEMWA BRAZIL.
KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Brazil, Oscar amesema ameruhusiwa kuondoka katika kambi ya maandalizi ya nchi yake kwa ajili ya Kombe la Dunia ili aweze kuwepo hospitali wakati mtoto wake atapozaliwa katika siku chache zijazo. Kiungo huyo wa Chelsea aliandika katika mtandao wa kijamii kuwa bado yupo na mtoto wake bado hajazaliwa hivyo kuondoa uvumi uliozagaa kuwa anaweza kuwa ameachwa katika kikosi cha timu ya taifa kutokana na majeruhi. Oscar aliendelea kueleza kuwa bado anasubiri na hajaondoka katika kikosi cha nchi hiyo na kwa uwezo wa mungu mtoto wake atazaliwa salama. Kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilianza mazoezi yake jana ikiwa ni siku mbili toka wakutane katika kambi yao ya Granja Comary iliyopo nje kidogo ya jiji la Rio de Janeiro.
MMILIKI WA MAN UNITED AFARIKI DUNIA BAADA YA KUUGUA KWA MUDA MREFU.
KLABU ya Manchester United imekumbwa na simanzi kubwa kufuatia mmiliki wake Malcom Glazer raia wa Marekani kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 85. Familia ya Glazer iliinunua klabu hiyo kwa euro milioni 790 Mei mwaka 2005 licha ya kupata pingamizi kali kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo. Chini wa umiliki wake United wanajulikana kwa jina la utani Mashetani Wekundu walifanikiwa kushinda mataji matano ya Ligi Kuu na taji la Klabu Bingwa ya Ulaya mwaka 2008. Watoto wa bilionea huyo Joel na Avram ndiyo waliochukua nafasi ya kuingoza klabu hiyo katika shughuli za kila siku baada ya baba yao kupatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2006. Kifo cha Glazer hakitarajiwi kuadhiri umiliki wa United, kwani familia hiyo bado inamiliki asilimia 90 za hisa za klabu hiyo ambazo zimegawanywa sawa kwa watoto wake sita alionao. Huku asilimia 10 inayosalia inamilikiwa na wenye hisa katika soko la hisa la New York.
Tuesday, May 27, 2014
YAYA TOURE AZIDI KUWACHANGANYA CITY, ADOKEZA KUITAMANI PSG.
KIUNGO mahiri wa Manchester City, Yaya Toure amesema itakuwa heshima kwake kuichezea Paris Saint-Germain-PSG na kukuza uvumi juu ya mustakabali wake na klabu hiyo. Wakala wa mchezaji huyo wiki iliyopita alisisitiza mteja wake hakufurahishwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Uingereza baada ya kueleza kusononeshwa kwake na jinsi klabu hiyo ilivyoshindwa kumpa pongezi katika siku yake ya kuzaliwa. Toure aliunga mkono madai hayo na kubainisha atatoa taarifa rasmi kuhusiana na mustakabali wake baada ya Kombe la dunia na sasa amedokeza kuwa na nia ya kujiunga na PSG ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa. Nyota huyo amesema kwa jinsi PSg walivyojijenga na kuwa na nguvu barani Ulaya itakuwa heshima kwake kuwa sehemu ya timu hiyo siku moja kama wataona anafaa. Toure amekuwa mchezaji muhimu kwa City msimu huu akiwa amefunga mabao 20 katika ligi na kusaidia mengine tisa na kuifanya timu hiyo kunyakuwa taji la Ligi Kuu.
ROAD TO BRAZIL: DEL BOSQUE ATAMBA KUWA NYOTA WA KUTOSHA KUZIBA NAFASI YA COSTA KAMA AKISHINDWA KWENDA BRAZIL.
KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque anategemea Diego Costa atapona kwa wakati kutokana na majeraha ya msuli yanayomsumbua lakini anaamini mabingwa hao wa Ulaya na Dunia wanao wachezaji wengi wanaoweza kuziba nafasi yake kama akishindwa. Mshambuliaji huyo wa Atletico Madriod amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya msuli kwa takribani wiki mbili na kulazimika kutolewa nje katika dakika ya tisa ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid iliyochezwa Jumamosi iliyopita. Del Bosque amesema nyota huyo ana majeruhi ya msuli ambayo watakuwa wakiyatizama maendeleo yake ili waweze kufanya uamuzi katika dakika za mwisho. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa bado wana nafasi mpaka Juni 2 ili waweze kutaja kikosi chao cha mwisho cha wachezaji 23 hivyo haoni haja ya kuwa na haraka, kwani ikishindikana bado wanao wachezaji wengine wazuri wanaoweza kuziba nafasi yake. Kama nyota huyo mzaliwa wa Brazil akishindwa kupona kwa wakati kwa ajili ya michuano hiyo, Del Bosque bado ana wachezaji kama Fernando Torres, Alvaro Negredo na Fernando Llorente ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo vyema. Hispania itacheza mechi yake ya kujipima nguvu dhidi ya Bolivia jijini Seville, Ijumaa hii baada ya wachezaji wa Atletico na Real Madrid waliocheza katika fainali kujiunga na kikosi cha nchi hiyo.
MKONGWE PIZARRO AONGEZEWA ULAJI BAYERN.
KLABU ya Bayern Munich imedai kumuongeza mkataba mshambuliaji wake, Claudio Pizarro kwa msimu mmoja zaidi utakaomalizika mwakani. Nyota huyo wa kimataifa wa Peru mwenye umri wa miaka 35 alijiunga na Bayern mwaka 2012 kwa mara ya pili baada ya kuichezea Werder Bremen kwa miaka mitatu na kufunga mabao 10 katika mechi 17 alizocheza msimu uliopita ambapo mara nyingi alikuwa akianzia benchi. Pizarro ambaye anaongoza wachezaji wa kigeni kwa kufunga mabao mengi katika Bundesliga akiwa amefunga mabao 176 katika mechi 370 alionekana chaguo sahihi kwa Pep Guardiola baada ya mshambuliaji nyota wa kutegemewa Mario Mandzukic aliposhindwa kuelewana na kocha huyo mwishoni mwa msimu. Katika taarifa yake Ofisa Mkuu wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge amesema Pizarro ameonyesha msimu huu jinsi gani alivyokuwa hatari anapokuwa karibu lango la wapinzani na jinsi gani alivyo muhimu katika timu. Rummenigge amesema anafurahi kwamba wataendelea kupata huduma ya mchezaji huyo kwa msimu mwingine. Pizarro alicheza bayermn kuanzia mwaka 2001 hadi 2007 kabla ya kurejea Bremen mwaka 2009 ambako aliwahi kucheza kuanzia mwaka 1999-2001, baada ya misimu miwili yenye mafanikio katika klabu ya Chelsea.
ROAD TO BRAZIL: WAANDAMANAJI WAZONGA BASI LA WCHEZAJI WA BRAZIL WAKIENDA MAZOEZINI.
TIMU ya taifa ya Brazil, imeanza maandalizi yake ya Kombe la Dunia huku kukiwa na maandamano jijini Rio de Janeiro. Basi lililokuwa limebeba wachezaji kuwapeleka katika kambi iliyopo huko Hilltop lilizungukwa na walimu waliokuwa wakiandamana ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kupinga michuano hiyo. Baadae tena wakati timu hiyo ilipofika katika kambi yao ya mazoezi huo Granja Comary wachezaji walisalimiwa na mashabiki na waandamanaji zaidi. Maelfu ya wananchi wa Brazil wamekuwa wakiandamana kupinga gharama kubwa zilizotumika kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajiwa mwezi ujao. Brazil inakabiliwa na mechi za kirafiki dhidi ya Panama Juni 3 na Serbia Juni 6 kabla ya kucheza mechi yao ya ufunguzi ya michuano hiyo Juni 12 dhidi ya Croatia Juni 12 jijini Sao Paulo.
ROAD TO BRAZIL: DIEGO COSTA HATARINI KUZIKOSA FAINALI ZA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania mzaliwa wa Brazil, Diego Costa yuko hatarini kuzikosa fainali za Kombe la dunia baada ya madaktari kuonya jana kuwa majeruhi ya msuli yanaweza kumlazimisha kupumzika kwa wiki mbili. Costa mwenye umri wa miaka 25 alitolewa uwanjani baada ya kupita dakika tisa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kati ya timu yake ya Atletico Madrid na Real Madrid Jumamosi iliyopita baada ya kufanya matibabu ya dharura ya kuchanika msuli. Daktari Pedro Guillen ambaye ni mkuu wa kliniki ya Cemtro ambapo wachezaji wa Hispania hufanyiwa vipimo vyao, amesema Costa alikuwa bado hajapona majeraha yake hata kabla ya mchezo huo uliopita. Guillen aliendelea kudai kuwa nyota huyo anahitaji mapumziko ya wiki mbili, na anaweza kwenda Brazil lakini itategemea na jinsi atakavyoendelea. Kocha wa Hispania Vicente del Bosque amemua kusogeza mbele muda wa kutaja kikosi chake cha mwisho ili kufuatilia hali ya Costa na wachezaji wengine wa Atletico na Real Madrid baada ya fainali hiyo iliyopita. Hispania ambao ni mwabingwa wa Ulaya na mabingwa watetezi wa Kombe la dunia litakalofanyika nchini Brazil mwezi ujao wanatarajia kuanza kampeni yao dhidi ya Uholanzi Juni 13 mwaka huu.
ROAD TO BRAZIL: MAJERUHI YAZIDI KUIANDAMA CAMEROON.
NAHODHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o alipumzishwa wakati hofu ya majeruhi kuelekea katika Kombe la Dunia ikizidi kupanda wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Macedonia uliochezwa huko Austria. Mshambuliaji huyo wa Chelsea aliwekwa benchi kwasababu ya matatizo ya goti aliyonayo lakini Cameroon ilikumbwa na balaa lingine baada ya mshambuliaji wake mkongwe kulazimika kutolewa nje katika mchezo huo uliochezwa jana. Pierre Webo mwenye umri wa miaka 32 aliumia bega wakati akifunga bao la kuongoza kwa timu hiyo hatua ambayo ilimfanya kutolewa nje na nafasi kuchukuliwa na Eric Maxim Choupo-Moting aliyeongeza bao la pili dakika za mwisho. Webo na Eto’o wanaingia katika orodha ndefu ya wachezaji majeruhi ambao waliachwa katika mechi hiyo ili waweze kupona sawasawa akiwemo golikipa Charles Itandje, bekli Jean-Armel Kana-Biyik na viungo Edgar Salli, Jean Makoun na Stephen Mbia. Mechi hiyo ilichezwa pamoja na kutofikiwa makubaliano kati ya wachezaji na maofisa wa Shirikisho la Soka la Cameroon juu ya kiasi gani cha fedha watapewa kutoka kwa mdhamini mazungumzo ambayo yanatarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii. Cameroon wataanza kampeni yao kwa kuivaa Mexico Juni 13 huko Natal lakini bado wana mechi za kujipima nguvu dhidi ya Paraguay, ujerumani na Moldova kabla ya kwenda huko Brazil.
SITISHIKI NA TETESI ZOZOTE ZA USAJILI JUU YANGU - LALLANA.
KIUNGO wa klabu ya Southampton Adam Lallana amesema hawezi kusumbuliwa na tetesi juu ya mustakabali wake wakati akiwa katika majukumu ya kimataifa na timu ya taifa ya Uingereza. Nyota mwenye umri wa miaka 26 ametajwa kutengewa dau na Liverpool wakati akiwa katika maandalizi ya michuano ya Kombe la dunia ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 12 mwaka huu. Lallan amesema kama mustakabali utaamuliwa kabla au baada ya Kombe la Dunia hautakuwa na tofauti yoyote kwake kwani hivi sasa anatilia mkazo michuano hiyo iliyo mbele yake na kuhakikisha anacheza vyema kadri anavyoweza. Lallan ambaye alijiunga na Southampton mwaka 200, amefunga mabao 10 katika mechi 42 alizocheza msimu huu na kuisadia timu yake kumaliza katika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu nafasi ambayo ni ya juu zaidi kufikiwa toka wapande daraja. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa miaka minne iliyopita alikuwa akicheza Ligi Daraja Kwanza na alikuwa alikuwa akitizama Kombe la Dunia akiwa na wachezaji wenzake na kama mtu angemuambia kuwa atashiriki michuano itakayofuata asingeweza kumuamini kwa kipindi kile.
ROAD TO BRAZIL: HOTELI ZITAKAZOFIKIWA NA UINGEREZA NA ITALIA ZAKUTWA NA DOSARI YA VYAKULA VILIVYOPITILIZA MUDA.
RODGERS AONGEZEWA MKATABA LIVERPOOL.
MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na timu hiyo. Rodgers ambaye aliteuliwa kuchukua nafasi ya Kenny Dalglish mwaka 2012 aliiongoza timu hiyo kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kufuatia kukosekana kwa miaka mine. Mara baada ya kusaini mkataba huo Rodgers mwenye umri wa miaka 41 amesema ni heshima kubwa kwake kupata nafasi hiyo katika klabu hiyo kubwa. Liverpool walimaliza katika nafasi ya pili wakitofautiana kwa alama mbili na mabingwa wa Ligi Kuu Manchester City.
SUAREZ BADO MGUU NJE MGUU NDANI KOMBE LA DUNIA.
DAKTARI Alberto Pan aliyemfanyia upasuaji wa goti mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uruguay Luis Suarez amekataa kutoa muda rasmi wa mchezaji huyo kurejea uwanjani. Uwepo wa Suarez katika kikosi cha Uruguay kitakachoshiriki Kombe la Dunia umekuwa mashakani baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti wiki iliyopita. Pan amesema nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anaendelea vyema na bado anaweza kusafiri kwenda Brazil lakini hana uhakika juu ya wakati ambao atakuwa fiti kwa ajili ya kucheza. Daktari huyo aliendelea kudai kuwa ni jambo la hatari kutoa muda wa mchezaji huyo kuweza kucheza kwani itategemea na jinsi anatakavyopona, kitu cha msingi anachoweza kusema ni kwamba matumaini ya kwenda Brazil bado yapo.
Saturday, May 24, 2014
ROAD TO BRAZIL: KLINSMANN AJITETEA KUMUACHA DONOVAN KATIKA KIKOSI CHAKE INGAWA AMEKIRI ULIKUWA UAUZI MGUMU.
KOCHA wa timu ya taifa ya Marekani, Jurgen Klinsmann ametetea uamuzi wake wa kumuacha Landon Donovan katika kikosi cha wachezaji 23 watakaocheza Kombe la Dunia lakini amekiri ulikuwa ni mmoja ya uamuzi mgumu kuwahi kufanya akiwa kama kocha. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 alitangaza Alhamisi kuwa Donovan hatakuwa katika mipango yake kwa ajili ya michuano hiyo pamoja na kucheza mechi 156 na kufunga mabao 57 kwa nchi yake. Kuachwa kwa Donovan kulizua mshituko mkubwa haswa ikizingatiwa kila mtu alitegemea kiungo huyo mkongwe kuwemo katika kikosi hicho ambapo zingekuwa fainali zake za nne kushiriki. Klinsmann amesema ulikuwa uamuzi mgumu kwani alikuwa na mshambuliaji mwingine ambaye anamzidi Donovan kwa maeneo kadhaa. Kocha huyo Mjerumani aliendelea kudai kuwa ilikuwa vigumu kutoa habari hivyo lakini anashukuru kwani Donovan mwenyewe amechukulia vyema uamuzi wake.
MANCINI AMPIGIA DEBE DROGBA KWENDA JUVENTUS.
MENEJA wa klabu ya Galatasaray, Roberto Mancini ameishauri Juventus kumsajili Didier Drogba ambaye anaondoka kwa wakongwe hao wa jiji la Instabul kiangazi hiki. Mkongwe huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia jijini Turin baada ya kuisaidia Galatasaray kushinda taji la Ligi Kuu pamoja na Kombe la Ligi katika miezi minane ambayo amekuwa nchini Uturuki. Mancini anaamini kuwa Juventus watafanya vyema kumsajili Drogba wakati wakijipanga kutetea taji lao la Serie A sambamba kampeni zao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Akihojiwa Mancini amesema kama Juventus wakimchukua Drogba watakuwa wamefanya usajili mzuri kwani nyota huyo bado anaweza kuwasaidia na kupata matokeo wanayotaka katika mashindano yote.
ROBBEN AITOLEA NJE MANCHESTER UNITED.
WINGA mahiri wa klabu ya Bayern Munich Arjen Robben ameitolea nje Manchester United na kusisitiza kuwa hana sababu yoyote yakumfanya aondoke Alleanz Arena kiangazi hiki. Nyota huyo wa kimataifa wa Uholanzi amekuwa akihusishwa na kuhamia Old Trafford ambapo angeungana na kocha wake wa zamani Louis van Gaal. Robben mwenye umri wa miaka 30 amesema angekuwa tayari kurejea nchini Uingereza kama angekuwa hana furaha mahali alipo lakini anafurahia maisha yake jijini Munich. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa United sio chaguo lake kwasasa kwani bado anapenda kubakia Bayern na hadhani kama timu hiyo itamuuza kwasababu ndio kwanza ameongeza mkataba mpya. Mbali na kukataa kujiunga na United Robben alisifu uteuzi wa Van Gaal na kudai kuwa utaisadia timu hiyo kurejesha hadhi yake.
YAYA TOURE HATIHATI KOMBE LA DUNIA.
SHIRIKISHO la Soka la Ivory Coast limethibitisha kuwa Yaya Toure anapatiwa matibabu nchini Qatar kwa majeraha ambayo hayajawekwa wazi kabla ya kujiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya kambi yao ya mazoezi ya Kombe la Dunia iliyopo Marekani. Toure ni mchezaji pekee kati ya 28 walioteuliwa katika kikosi cha awali cha kocha Sabri Lamouchi kukosa mwanzo wa maandalizi ya Kombe la Dunia katika kambi yao iliyopo jijini Dallas. Katika taarifa ya shirikisho hilo imedai kuwa Toure atasafiri kuelekea Marekani Alhamisi ijayo. Hospitali ya moja inayojihusisha na matibabu ya michezo iliyopo jijini Doha ilithibitisha kumpokea mchezaji huyo kwa kile walichokiita katika taarifa yao majeraha madogo. Ivory Coast inatarajia kucheza mechi zake za kujipima nguvu nchini humo dhidi ya Bosnia mchezo utakaofanyika Mei 30 huko St Louis na El Salvador utakaofanyika huko Dallas Juni 4 kabla ya kuelekea Brazil Juni 6 mwaka huu. Ivory Coast wamepangwa kundi C sambamba na timu za Colombia, Ugiriki na Japan katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 12.
ROAD TO BRAZIL: RONALDINHO AAMUA KUPIGA HELA KIVINGINE KWA KULIPANGISHA JUMBA LAKE LA KIFAHARI.
BAADA ya kutemwa katika kikosi cha timu ya ya Brazil na kocha Luiz Felipe Scolari kwa ajili ya Kombe la Dunia, Ronaldinho amekuja na mbinu nyingine ya kumfanya kujipatia kipato katika michuano hiyo ya mwaka huu. Nyota huyo wa zamani wa Barcelona ameamua kukodisha jumba lake la kifahari lililopo jijini Rio de Janeiro kwa paundi 9,120 kwa usiku mmoja ili kuwapa mashabiki nafasi ya kuishi katika jumba lake. Ronaldo alithibitisha taarifa hizo kupitia mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa jumba lake hilo lenye vyumba vitano linakodishwa kupitia kampuni ya Airbnb.com wakati michuano hiyo itakayofanyika kiangazi hiki.
Jumba hilo ambalo linajumisha mabafu sita liko eneo maalamu lenye ulinzi mkali la Barra da Tijuca. Ronaldinho amelipamba jumba lake hilo kw apicha zake wakati akicheza katika timu za Paris Saint-Germain, AC Milan na timu yake ya taifa ya Brazil. Mtu anayetaka kupanga anatakiwa kutoa malipo ya awali ya paundi 600, lakini hairuhusiwi kuvuta sigara ndani, labda nje ya nyumba na kutakuwa na timu maalum ya watu wa kuhudumia wageni.
TAIFA STARS, MALAWI KUPAMBANA JUMANNE.
TAIFA Stars na Malawi (Flames) zinapambana Jumanne (Mei 27 mwaka huu) katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni. Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo wa marudiano wa michuano ya Afrika na Zimbabwe (Mighty Warriors) utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi na ile ya Zimbabwe. Malawi imewasili leo mchana (Mei 24 mwaka huu) kwa ndege ya Malawian Airlines kwa ajili ya mchezo huo ikiwa na msafara wa watu 27, na imefikia kwenye hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi jijini Dar es Salaam. Flames inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Baada ya mechi hiyo, Malawi itakwenda moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika itakayochezwa Mei 30 mwaka huu jijini Ndjamena.
Friday, May 23, 2014
PSG YAENDELEZA KUFURU ZA KUTUMIA FEDHA KWA KUMSAJILI LUIZ KWA DAU LA KUVUNJA REKODI.
KLABU ya Chelsea imefikia makubaliano na timu ya Paris Saint-Germain-PSG ya mauzo ya kiasi cha paundi milioni 40 kwa ajili ya beki wake David Luiz. Luiz mwenye umri wa miaka 27 alijiunga na Chelsea kwa ada ya paundi milioni 21.3 akitokea klabu ya Benfica ya Ureno Januari mwaka 2011. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa Chelsea imedai kuwa uhamisho huo umekubaliwa pia na mchezaji mwenyewe kuhusiana na mahitaji yake binafsi na tayari amefaulu vipimo vya afya. Beki huyo wa kimataifa wa Brazil alikuwa amebakisha mkataba wa miaka mitatu kati ya mitano aliyosaini Stamford Bridge Septemba mwaka 2012.
MADRID WATUA LISBON TAYARI KUIKABILI ATLETICO KATIKA FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA.
MSHAMBULIAJI nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amevuta hisia kubwa wakati aliporejea tena jijini Lisbon jana jioni wakati timu hiyo ilipotua nchini Ureno kuelekea katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Atletico Madrid. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alionekana kuwa mtulivu huku akizungumza na mchezaji mwenzake Pepe baada ya kushuka kutoka katika ndege binafsi ya timu hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Lisbon, ikiwa yamebaki masaa machache kabla ya mchezo huo utakaofanyika huko Estadio da Luz.
Ronaldo amerejea tena katika mji huo mkuu ambako alikaa miaka sita akiichezea timu ya Sporting Lisbon kabla ya kwenda Manchester United mwaka 2003 huku akiwa na uhakika wa kuwepo katika kikosi cha kwanza cha Carlo Ancelotti katika mchezo huo dhidi ya Atletico. Nyota huyo Mreno hajakuwepo katika kikosi cha Madrid toka walipotoa sare ya bao 1-1 na Villadolid Mei 7 mwaka huu ambapo alitolewa dakika nane ya mchezo kwasababu ya kuumia. Pamoja na hofu juu ya afya ya mchezaji huo, Ancelotti aliwaondoa hofu hiyo mashabiki wa Madrid kwa kuthibitisha kuwa Ronaldo ayakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kesho.
Ronaldo amerejea tena katika mji huo mkuu ambako alikaa miaka sita akiichezea timu ya Sporting Lisbon kabla ya kwenda Manchester United mwaka 2003 huku akiwa na uhakika wa kuwepo katika kikosi cha kwanza cha Carlo Ancelotti katika mchezo huo dhidi ya Atletico. Nyota huyo Mreno hajakuwepo katika kikosi cha Madrid toka walipotoa sare ya bao 1-1 na Villadolid Mei 7 mwaka huu ambapo alitolewa dakika nane ya mchezo kwasababu ya kuumia. Pamoja na hofu juu ya afya ya mchezaji huo, Ancelotti aliwaondoa hofu hiyo mashabiki wa Madrid kwa kuthibitisha kuwa Ronaldo ayakuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kesho.
ROAD TO LISBON: COSTA FITI KUIKABILI REAL MADRID, LAKINI PEPE NA BENZEMA MAJANGA.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Costa amefanikiwa kurejea kutoka katika majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa ajili ya mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid lakini Pepe alikosa mazoezi ya jana kutokana na kutojisikia vyema. Costa alipata majeruhi katika mchezo wa mwisho wa Atletico ambao uliwafanya kuwa mabingwa wapya wa La Liga baada ya kutoka ya bao 1-1 dhidi ya Barcelona na ilionekana kama angekosa mchezo huo wa fainali utakaofanyika jijini Lisbon. Lakini nyota huyo mzaliwa wa Brazil alisafiri kwenda nchini Serbia kupata matibabu maalumu ambayo hupewa farasi na huduma hiyo inaonekana kufanya maajabu kwani mshambuliaji huyo alionekana akifanya mazoezi ya kukimbia na wachezaji wenzake katika huko Estadio da Luz. Meneja wa timu ya Atletico Diego Simeone amesema Costa atafanyiwa uchunguzi zaidi uangalia majeraha mmengine yanayomsumbua ili kuona kama anaweza kuanza katika mchezo huo wa leo. Kwa upande wa kikosi cha Madrid imeonekana hakuna mashaka sana kuhusiana na nyota wake Cristiano Ronaldo na Gareth Bale lakini kumezuka wasiwasi mwingine wa kuwakosa Pepe na Karim Benzema kutokana na wawili hao kushindwa kufanya mazoezi kwa wiki yote.
BEKI WA NEWCASTLE ATISHIWA KUUAWA NA MASHABIKI WA URUGUAY.
BEKI wa klabu ya Newcastle United, Paul Dummett amepokea vitisho vya kuuawa katika mtandao kutoka kwa mashabiki wa Uruguay ambao wanamlaumu kwa majeraha ya goti aliyopata Luis Suarez. Nyota huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 27 alifanyiwa upasuaji wa goti jana lakini anategemea kupona kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwezi ujao. Mashabiki wa Uruguay walimshambulia Dummett mwenye umri wa miaka 22 kupitia mtandao wa kijamii wa twitter kwa faulo hiyo aliyomchezea Suarez katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hizo lakini haijajulikana moja kwa moja kama tukio hilo ndilo lilisababisha majeraha hao. Dimmett alitolewa nje kwa kadi nyekundu lakini baadae kadi hiyo iliondolewa. Kumekuwa hakuna ripoti yoyote ya majeraha ya Suarez katika mchezo dhidi ya Liverpool ambao walishinda mabao 2-0 lakini nyota huyo alianza kulalamika maumivu wakati akianza mazoezi na timu yake ya taifa mapema wiki hii.
PSG YAMTENGEA DAU NONO LUIZ.
BEKI mahiri wa kimataifa wa Brazil, David Luiz anakaribia kujiunga na klabu ya Paris Saint-Germain-PSG ndani ya saa 24 zijazo kwa dili kubwa ambalo litawagharimu matajiri hao wa Ufaransa paundi milioni 50. Makubaliano ya muda gani atakipiga huko bado hayajawekwa wazi na timu hiyo lakini uhamisho nyota huyo wa Chelsea mwenye wa miaka 27 utakuwa ni ghali zaidi kwa mchezaji wa nafasi yake ambao utawazidi Marquinos na Thiago Silva ambao wote walisajiliwa na PSG. Mara ada hiyo itakapokubaliwa na Chelsea, PSG wataomba ruhusa kutoka kwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil Luiz Felipe Scolari kusafiri kwenda katika michuano ya Kombe la Dunia kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya afya. Nchini Uingereza beki aliyewahi kununuliwa kwa kitita kikubwa alikuwa ni Rio Ferdinand wakati akiondoka Leeds kwenda Manchester United kwa ada ya paundi milioni 30.
COSTA ADAI HAOGOPI KUFUNDISHA WANAUME.
MWANAMAMA Helena Costa amedai haogopi kibarua kilichopo mbele yake baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa kocha katika timu ya soka ya wanaume. Costa mwenye umri wa miaka 36 ambaye alikuwa mng’amua vipaji wa timu Celtic amechukua mikoba ya kuinoa timu ya daraja la pili ya Clermont Foot ya Ufaransa. Akihojiwa katika mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari, Costa amesema haofii chochote kwani kama asingefikiria anaiweza kazi hiyo asingekuwa hapo. Kabla ya utauzi wa Costa, mwanamke aliyewahi kocha katika timu za wanaume barani Ulaya alikuwa Carolina Morace ambaye aliifundisha timu ya Viterbese inayoshiriki Serie C kwa mechi mbili mwaka 1999. Costa ambaye amewahi kuifundisha timu ya vijana ya wanaume ya Benfica na timu ya taifa ya wanawake ya Qatar aliteuliwa kushika wadhifa huo na rais wa Clermont Foot, Claude Michy Mei 7 mwaka huu.
ROSBERG KUPEWA MKATABA MPYA MARCEDES.
Wednesday, May 21, 2014
NYOTA WA GOFU MCLLROY AMPIGA CHINI MPENZI WAKE AMBAYE NI NYOTA WA TENISI WOZNIACKI WAKATI KADI ZA HARUSI ZIKIWA TAYARI ZIMESAMBAZWA.
MCHEZAJI nyota wa mchezo wa gofu kutoka Ireland ya Kaskazini, Rory MclIroy amevunja mahusiano yake ya uchumba na nyota wa tenisi mwanadada Caroline Wozniacki. MalIroy mwenye umri wa miaka 25 ambaye amewahi kushinda mataji mawili makubwa ya gofu na nyota huyo wa tenisi mwenye umri wa miaka 23 raia wa Denmark walitangaza kuvishana pete rasmi katika sherehe za mwaka mpya. Nyota huyo wa gofu amesema tatizo ni la kwake kwasababu baada ya kuanza kusambazwa kadi za harusi mwishoni mwa wiki iliyopita akagundua kuwa hayuko tayari kwa ajili ndoa. Wawili wamekuwa wapenzi kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
KILELE CHA MICHUANO YA BEACH SOCCER JUMAPILI.
MICHUANO ya mpira wa miguu ya ufukweni-beach soccer inatarajiwa kufikia kileleni Mei 25 mwaka huu kwa mchezo wa fainali utakaozikutanisha timu za Taasisi ya Teknologia Dar es Salaam-DIT na Chuo cha Elimu ya Biashara-CBE kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini hapa. Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini-TFF Boniface Wambura mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayoanza asubuhi anatarajiwa kuwa rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi. Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni. Tanzania inatarajiwa kushiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.
ETO'O AENDELEZA VITA VYAKE NA MOURINHO, AMUITA KIBARAKA.
MSHAMBULIAJI nyota wa Chelsea, Samuel Eto’o ameendeleza vita vya maneno na Jose Mourinho kwa kumfananisha kocha huyo na kibaraka huku akisisitiza bado ana uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu. Mourinho alinaswa katika picha ya video akitoa kauli za kuponda viwango vya washambuliaji wake katika sherehe zilizoandaliwa na wadhamini huko Switzerland Februari mwaka huu na kuwadai kuwa Eto’o anaweza kuwa mkubwa kuliko anavyodai. Nyota huyo wa kimataifa wa Cameroon ambaye amefunga mabao 14 kwa msimu wake mmoja akiwa Stamford Bridge alivunja ukimya wiki iliyopita kuhusiana na suala hilo na kumumfananisha Mourinho na mpuuzi. Akiulizwa tena mahusiano yake na kocha huyo Mreno katika mahojiano na mtandao wa Cafonline Eto’o amesema ukiachana na maneno ya vibaraka kuhusiana na umri wake yeye bado yuko fiti kimwili na katika umri wa miaka 33 anajisikia vyema na ameonyesha anaweza kufanya vyema kuliko wachezaji wenye umri mdogo. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa hatakwenda Marekani au Mashariki ya Kati kwasababu bado ataendelea kucheza katika ligi zenye hadhi ya juu kwasababu mapenzi yake na michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya bado hayajaisha.
FABIANSKI AKATAA OFA MPYA YA ARSENAL.
GOLIKIPA Lukasz Fabianski amekataa ofa ya mwisho ya Arsenal ili kumzuia kutoondoka katika kipindi cha majira ya kiangazi. Meneja Arsenal Wenger anamtaka golikipa huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwezi ujao kubakia na kumpa changamoto golikipa mwenzake Wojciech Szczesny katika kugombea namba katika kikosi cha kwanza msimu ujao. Lakini imebainika kuwa Fabianski mwenye umri wa miaka 29 anataka kubadilisha mazingira pamoja na ofa mpya aliyopewa ili kuboresha mkataba wake wa miaka saba. Klabu za Schalke, Borussia Dortmund sasa zinaongoza kutaka kumnasa kipa huyo wakati pia vilabu kadhaa vya Ligi Kuu nchini Uingereza navyo vimeonyesha nia ya kuhitaji huduma ya Fabianski.
PIQUE KUSAINI MKATABA MPYA WA MIAKA MINNE.
BEKI wa klabu ya Barcelona Gerard Pique amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka minne na timu hiyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anatarajiwa kusaini mkataba huo ambao utamuweka Camp Nou mpaka 2019 katika siku chache zijazo. Pique ambaye aliwahi kuichezea Manchester United kati ya mwaka 2004 na 2008, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika Juni 2015. Toka aliporejea Barcelona ambapo alianza katika timu ya watoto, Pique amecheza mechi 266, kushinda mataji manne ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Habari hizo za kukaribia kusaini mkataba mpya zimekuja ikiwa imepita siku moja baada ya klabu hiyo kutangaza Lionel Messi kusaini mkataba mpya na mchezaji wa zamani Luis Enrique kuwa kocha mpya wa timu hiyo.
CESAR KUREJEA QPR.
GOLIKIPA Julio Cesar anayecheza kwa mkopo katika timu ya Toronto ya nchini Marekani amedai kuwa klabu yake ya Queens Park Rangers-QPR inamuhitaji kurudi baada ya michuano ya Kombe la Dunia. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil alikutanishwa na beki wa zamani wa QPR na sasa kocha wa Toronto, Ryan Nelsen Februari ili kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa muda wakati timu hiyo iliposhuka daraja. Mkataba wa Cesar bado unamuhitaji kubakia Marekani mpaka Desemba mwaka huu lakini inaonekana atarejea tena Uingereza kwa ajili ya msimu mpya huku QPR wakibakisha kushinda mchezo mmoja wa mtoano dhidi ya Derby County kwa ajili ya kurejea katika Ligi Kuu msimu ujao. Cesar alifafanua kuwa itategemea itakavyokuwa baada ya Kombe la Dunia lakini QPR wamesema wanamhitaji Agosti kwa ajili ya msimu mpya ligi.
FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA MSIMU HUU INADHIHIRISHA UBORA WA LA LIGA - DI MARIA.
WINGA wa klabu ya Real Madrid, Angel Di Maria anaamini kuwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya Jumamosi dhidi ya Atletico Madrid unaelezea jinsi gani soka la Hispania lilivyokuwa na nguvu. Baadhi ya wachambuzi walidai kuwa fainali za michuano hiyo mwaka jana zilizohusisha timu za Ujerumani Bayern Munich na Borussia Dortmund zilikuwa dalili kuwa nchi hiyo ndiyo yenye nguvu kisoka. Hata hivyo, Di Maria anaamini ukweli kuwa La Liga ndio ligi bora umeonyeshwa msimu huu katika michuano ya Ulaya. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina amesema fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka huu inaonyesha dhahiri kwa kiasi gani soka la Hispania lilivyokuwa. Di Maria amekiri itakuwa fainali nzuri na ngumu dhidi ya mahasimu wao hao wa jiji la Madrid lakini watajitahidi kufanya kila wanaloweza ili kuendeleza rekodi yao barani humo.
TOURE AZIDI KUWACHANGANYA MANCHESTER CITY.
KIUNGO mahiri Yaya Toure ameongeza tetesi za kuondoka Manchester City kwa kudai kuwa hajui timu gani ataichezea msimu ujao. Wakala wa mchezaji huyo, Dimitri Seluk alifafanua mapema kwamba nyota huyo anaweza kuondoka kwaababu anafikiri hatendewi haki na haeshimiwi na wamiliki wa timu hiyo. Sasa Toure mwenye umri wa miaka 31 amesema kila kitu kiko wazi kuhusu mustakabali wake katika siku zijazo. Akiulizwa kama anaweza kucheza katika klabu nyingine nyota huyo alikubali na kudai hawezi kujua kwasababu kila kitu kinawezekana katika soka. Toure aliendelea kudai kuwa kutokana na kuwa na msimu mzuri kila mtu anamzungumzia na wakala wake muda wote amekuwa katika simu na anajua nachotakiwa kufanya kwasababu anamwamini. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast amesema kwasasa hawezi kujua yatakayotokea mbele lakini anataka kuhamishia mawazo yake katika michuano ya Kombe la Dunia na baada ya japo atajua cha kufanya huko. Toure amesaini mkataba mpya wa miaka minne na City Aprili mwaka jana.
FALCAO KUJIUNGA NA WACHEZAJI WENZAKE WA COLOMBIA KATIKA KAMBI YAO NCHINI ARGENTINA.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Colombia Radamel Falcao anatarajiwa kusafiri na timu ya taifa ya nchi hiyo katika kambi yao waliyoweka nchini Argentina pamoja na taarifa kuwa nyota huyo anaweza kutitoa mwenyewe katika michuano ya Kombe la Dunia. Nyota huyo anayecheza klabu ya Monaco alipata majeruhi ya mabaya ya goti wakati wa mchezo wa Kombe la Ufaransa Januari mwaka huu na kumekuwa na madai kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amekiri kushindwa kuwa fiti ili aweze kuiwakilisha nchi yake katika michuano hiyo nchini Brazil kiangazi hiki. Hata hivyo, kumetolewa taarifa na Shirikisho la Soka la Colombia wakibainihsa kuwa Falcao ambaye alifanya mazoezi na timu yake mwishoni mwa msimu bado anapambana ili kumuonesha kocha Jose Pekerman kwamba yuko fiti. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa Falcao atajiunga na wachezaji wenzake pindi watakaposafiri kwenda Buenos Aires na kwamba hivi sasa bado anafanya mazoezi ya viungo katika timu yake ya Monaco.
Tuesday, May 20, 2014
ADHABU HAITATUZUIA KUFANYA USAJILI TUNAOTAKA - AL MUBARAK
WASHABIKI KWENDA HARARE KUSHANGILIA STARS.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaandaa utaratibu utakaowawezesha washabiki kwenda jijini Harare, Zimbabwe kushuhudia mechi ya Taifa Stars. Mechi hiyo ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa ajili ya fainali zitakazochezwa Morocco mwakani itafanyika Jumapili (Juni 1 mwaka huu) jijini Harare. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0. Usafiri huo utakuwa wa basi ambapo washabiki wanatarajiwa kuondoka siku ya Ijumaa na kuwasili Jumapili mchana jijini Harare ambapo watashuhudia mechi na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo. Washabiki wanatakiwa kuwa na hati za kusafiria (pasipoti), nauli ya kwenda na kurudi itakuwa sh. 300,000.
USAJILI WA WACHEZAJI KUANZA JUNI 15.
USAJILI wa wachezaji kwa hatua ya kwanza msimu huu (2014/2015) unaanza Juni 15 hadi Agosti 3 mwaka huu wakati kipindi cha kutangaza wachezaji walioachwa au kusitishiwa mikataba ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu. Kipindi cha kwanza cha uhamisho wa wachezaji ni kuanzia Juni 15 mwaka huu hadi Julai 30 mwaka huu. Kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 4 na 11 mwaka huu. Kuthibitisha usajili hatua ya awali ni Agosti 12 hadi 14 mwaka huu. Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 14 na 29 mwaka huu. Kupitia na kutangaza majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4 mwaka huu. Uthibitisho wa usajili hatua ya pili ni Septemba 5 na 6 mwaka huu. Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu, na ratiba inatarajiwa kutoka mwezi mmoja kabla (Julai 24 mwaka huu).
MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 63/-.
MECHI ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe iliyochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 63,345,000. Mapato hayo katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 yametokana na washabiki 11,079 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000. Mgawo wa mapato hayo ni asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 9,662,796.61, gharama za kuchapa tiketi sh. 6,000,000, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 7,152,330.51, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 9,536,440.68 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa pamoja wamepata sh. 30,993,432.20.
TIMU YA U15 YAWASILI GABORONE.
TIMU ya Tanzania ya umri chini ya miaka 15 imewasili salama jijini Gaborone, Botswana kwa ajili ya michezo ya Afrika ambapo itacheza mechi yake ya kwanza Mei 22 mwaka huu dhidi ya Mali. Kikosi hicho cha wachezaji 16 chini ya Kocha Abel Mtweve kimetua jijini Gaborone jana (Mei 19 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South African Airways. Michezo hiyo itamalizika Mei 30 mwaka huu. Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Tanzania ni Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid, David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin, Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka. Nchi nyingine zinazoshiriki michezo hiyo kwa upande wa mpira wa miguu ni Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Mali na Swaziland. Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambazo nazo zilikuwa zishiriki kwenye michezo hiyo katika dakika za mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)