Thursday, November 29, 2012

FERRARI CONSIDER SEBASTIAN VETTEL PROTEST.

TIMU ya Ferrari inajaribu kuangalia kama kuna ushahidi wa kutosha ili waweze kupinga matokeo ya ubingwa wa dunia wa mashindano ya Langalanga na wakifanikiwa kuna uwezekano mkubwa matokeo hayo yakabadilishwa. Timu hiyo inafuatilia picha za video ambazo zinamuonyesha dereva wa Red Bull Sebastian Vettel akilipita gari lingine kimamkosa katika mashindano ya Grand Prix iliyofanyika nchini Brazil Jumapili iliyopita. Fernando Alonso kutoka Hispania alipoteza taji hilo kwa alama toka kwa Vettel lakini mjerumani huyo anaweza kupoteza alama nne kama akikutwa na hatia ya kuvunja sheria katika mashindano hayo. Chombo cha Kusimamia mashindano hayo-FIA kimekataa kuthibisha kama kinafanyia uchunguzi tukio hilo. Picha za video zinamuonyesha Vettel akimpita dereva wa timu ya Toro Rosso, Jean Eric mahali ambapo haparuhusiwi katika mzunguko wa nne wa michuano hiyo.

MANCINI AMPONDA BALOTELLI.

MENEJA wa klabu ya Manchester City, Roberto Mancini amesema bado hajafurahishwa na kiwango cha mshambuliaji wa timu hiyo Mario Balotelli pamoja na nyota huyo kufunga bao lake la kwanza la Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Wigan Athletic jana usiku. Balotelli ambaye ameanza katika kikosi cha kwanza mara sita kati ya 14 msimu huu alifunga bao la kuongoza dakika ya 69 wakati Cit ambao hawajapoteza mchezo wa ligi msimu huu wakishinda mabao 2-0 na kubakia nafasi ya pili katika msimamo nyuma ya Manchester United kwa tofauti ya alama moja. Mancini alimsifisia mshambuliaji huyo kwa kufunga bao muhimu katika mchezo huo lakini kocha anafikiri kuwa Balotelli anaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo kwasababu ni mchezaji wa kiwango cha juu. Kocha aliendelea kusema kuwa kama mchezaji huyo akiongeza bidii katika mazoezi anaweza kufikia kiwango cha Cristiano Ronaldo au Lionel Messi.

SCOLARI ATAJWA KUCHUKUA MIKOBA YA MENEZES.

Kuna habari zimesambaa nchini Brazil kuwa Luiz Felipe Scolari ndio anatarajiwa kuwa mpya wa timuya taifa ya nchi hiyo. Brazil imekuwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya kumtimua Mano Menezes Ijumaa iliyopita kufuatia kushindwa kufikia malengo waliyoweka katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini London mwaka huu. Scolari ambaye alikiongoza kikosi cha Brazil kunyakuwa Kombe la Dunia mwaka 2002 amekuwa hana kibarua kwasasa baada ya kuondoka katika klabu ya Palmeiras Septemba mwaka huu. Taarifa hizo zilisema kuwa Scolari ambaye amewahi kukinoa kikosi cha Chelsea alifanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka nchini Brazil-CBF ambapo anatarajiwa kutangazwa rasmi baadae. Rais wa CBF Jose Maria Marin alithibitisha kufanya mazungumzo na makocha kadhaa ingawa hakutaja jina la Scolari ili kuangalia ni kocha gani wanaweza kumpa mikoba ya kuingoza Brazil katika michuano ya Kombela Dunia 2014 ambayo wao watakuwa wenyeji.

Wednesday, November 28, 2012

CASILLAS AWAPONDA MASHABIKI WANAOMZOMEA MOURINHO.

NAHODHA wa klabu ya Real Madrid, Iker Casillas amemkingia kifua Jose Mourinho baada ya kocha huyo raia wa Ureno kupigiwa filimbi na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakati wa mchezo wa Kombe la Mfalmeuliofanyika katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumanne. Kumekuwa na shinikizo la mgawanyiko kuhusu Mourinho baada ya kikosi chake kuwa nyuma kwa alama 11 mbele ya mahasimu wao Barcelona ambao wanaongoza La Liga ndio sababu kubwa iliyochangia mashabiki hao kupiga filimbi huku wengine wakitaja jina lake katika mchezo huo ambao Madrid ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Alcoyano. Casillas amesema kuwa anadhani miezi michache iliyopita watu ambao walikuwa wakipiga filimbi katika mchezo wa Jumanne ndio watu ambapo walikuwa wakipiga makofi na kushangilia wakati waliposhinda taji la La Liga. Kipa huyo aliongeza kuwa kumbukumbu huwa ni ndogo katika soka na labda watu wamesahau ni nani aliyekiongoza kikosi cha timu hiyo kushinda taji la La Liga kwa kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi na kupata alama nyingi zaidi. Aliendelea kusema kuwa mashabiki wanatakiwa kukumbuka na nyakati za furaha ambazo walipata na kuendelea kuishangilia timu yao ili iweze kufanya vizuri zaidi.

MSAIDIZI WA MANCINI AFUNGIWA MECHI MBILI NA UEFA.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limemfungia mechi mbili za Ulaya kocha msaidizi wa Manchester City, David Platt baada ya kutolewa na kupelekwa jukwaani wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid wiki iliyopita. Platt hataruhusiwa kuwepo katika benchi la wachezaji wa akiba wakati wa mchezo wa mwisho wa City dhidi ya Borussia Dortmund wiki ijayo. Katika taaifa ya UEFA`ambayo ilitumwa katika wavuti wake imesema kuwa Kamati ya Nidhamu ilimkuta na kosa Platt kwakuonyesha tabia isiyofaa katika mchezo huo hivyo kupelekea mwamuzi kumwamuru kwenda kukaa jukwaani. UEFA pia imeitoza faini ya paundi 12,000 klabu ya Manchester City baada ya wachezaji wake watano kupewa kadi za katika mchezo huo ambapo wamepewa siku tatu kama wanataka kukata rufani kuhusiana na adhabu hizo.

UEFA YAFIKIRIA KUONGEZA TIMU 32 ZAIDI LIGI YA MABINGWA ULAYA.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA linafikiria kuikacha michuano ya Europa League ili kuboresha michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuongeza timu zaidi kutoka 32 mpaka tinu 64. Rais wa UEFA, Michel Platini amesema kuwa bado wako katika mazungumzo na wanatarajia kutoa maamuzi 2014 kwasasa hakuna lolote lililoamuliwa kuhusiana na suala hilo. Kama mabadiliko hyo yakipitishwa inamaanisha Uingereza itakuwa na saba katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, nne ambazo huyo zinafuzu ligi ya mabingwa na tatu zingine zinazoshiriki Europa League. UEFA inapanga kubadilisha mfumo wa mashindano ya Ulaya kuanzia mwaka 2015.

TFF KUTETA NA SERIKALI.

TENGA, WIZARA WATETA KUZUIWA AKAUNTI YA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lina imani kuwa mazungumzo kati yake, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yatamaliza tatizo la kushikiliwa akaunti ya TFF kutokana na malipo ya kodi ya mishahara ya makocha wa kigeni. Rais wa TFF, Leodegar Tenga alizungumza na waandishi wa habari jana juu ya uamuzi wa TRA kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB kukata sh. 157,407,968 ikiwa ni malipo ya Kodi ya Mapato ya Mshahara wa Mfanyakazi (P.A.Y.E) ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake. Katika mzozo huo wa muda mrefu, TFF imejitetea kuwa haiwezi kulipa kodi hiyo kwa kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo mlipaji wa mishahara ya makocha hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ya kulipia makocha wa michezo tofauti, ukiwemo mpira wa miguu. “Hili ni suala nyeti ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya pande zote. Ninataka kuwahakikishia kuwa suala hili linazungumzwa na tayari nimeshafanya mazungumzo na maofisa wa Wizara na tumekubaliana kukutana na pande zote wakati wowote; iwe leo jioni au kesho. “Ni matumaini yangu kuwa suala hili litakwisha na jana nimetoka Kampala (Uganda kwenye Kombe la Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na viongozi wa Wizara na wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza suala hili. “Nimezungumza na wenzetu wa Serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Fedha zilizokamatwa si zetu; ni fedha za klabu na zimetolewa na mdhamini ambaye tumekubaliana namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa ajili ya kulipia kodi. Lakini TRA wanazishikilia kwa sababu Premier League iko chini ya TFF,” amesema Rais Tenga. Tenga amesema TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi na hivyo wana haki ya kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, mwajiri ndiye anayetakiwa kukata kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi. “Hivyo hatuwezi kuilaumu TRA kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini pia hatuna uwezo huo wa kulipa fedha hizo kwa sababu, kwanza hatuna na pili sio sisi tunaolipa mishahara ya hawa makocha,” amesisitiza Rais Tenga. Akizungumzia historia ya suala hilo, Tenga aliishukuru Serikali kwa msaada ambao imekuwa ikiutoa katika mpira na kwamba ahadi ya Rais Kikwete ya kusaidia kulipa makocha wa timu za taifa imeusogeza mpira wa miguu karibu na Serikali na karibu na Rais. “Rais Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani (mwaka 2005) anajua kuwa kuna tatizo kwenye mpira na akatoa ahadi ya kulipa walimu wa mpira. Ahadi hiyo imefanya ukaribu uliopo sasa kati ya mpira na Serikali; kati ya mpira na Rais sasa kuwa mkubwa. Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kwenye mpira, yaani kulipa walimu. “Sasa sisi ni administrators wa hawa walimu. Tunachofanya ni kuandaa mikataba ambayo ni standard duniani kote kwa mujibu wa taratibu za FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu). Kwa kawaida makocha wa kigeni huwa wanatayarishiwa mikataba ambayo ni tax free (isiyo na kodi). Baada ya kuingia nao mikataba, huwa tunaipeleka wizarani ambao ndio wanawalipa makocha moja kwa moja kwenye akaunti zao,” amesema Rais Tenga. Katika mkutano huo na waandishi, Rais Tenga pia aliipongeza timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa kuanza vizuri mashindano ya Kombe la Chalenji, akisema ushindi huo ni ishara nzuri hasa kutokana na ukweli kuwa kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi na akataka Watanzania waendelee kuiunga mkono. Tenga pia alisema kumekuwepo na malalamiko kuhusu makato ya mechi na kwamba suala hilo ni la muda mrefu na kwamba TFF imepiga hatua kubwa tangu ilipoanza kulishughulikia.

TAARIFA KUTOKA TFF LEO.

STARS KUINGIA KAMBINI BAADA YA CHALENJI
Timu ya Taifa (Taifa Stars) inatarajia kuingia kambini baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Namboole jijini Kampala, Uganda. Michuano hiyo iliyoanza Novemba 24 mwaka huu itamalizika Desemba 8 mwaka huu. Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen, Stars itaingia kambini kujiandaa kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) itakayochezwa Desemba 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Baada ya pambano dhidi ya Chipolopolo, wachezaji watapata mapumziko ya wiki mbili kabla ya kuingia tena kambini Januari 6 hadi 20 mwakani kwa ajili ya mechi nyingine za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco. Kim anatarajia kuongeza kipa mmoja kwenye kikosi chake ili kuwasaidia nahodha Juma Kaseja na Deogratias Munishi pamoja na chipukizi kadhaa kutoka timu za Taifa za vijana za Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys. Vilevile Kim anafuatilia wachezaji wengine kwenye timu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ambayo pia inashiriki michuano ya Kombe la Chalenji ikiwa katika kundi C pamoja na timu za Eritrea, Malawi na Rwanda.

ZICO AJIUZULU KUINOA IRAQ.

ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya Iraq, Zico ameamua kujiuzulu wadhfa wake huo baada ya kudai kuwa Shirikisho la Soka la nchi hiyo limeshindwa kufikia makubaliano waliyokubaliana katika mkataba wake. Kujiuzulu kwa Zico ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil kumekuja ikiwa bado Iraq inapigania nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2014 itakayofanyika nchini Brazil. Iraq inashika nafasi ya tatu katika kundi B kwa timu za uapnde wa bara la Asia wakiwa na alama 5 katika michezo mitano waliyocheza wakipishana alama moja na Australia ambao wako katika nafasi ya pili huku Japan akiongoza kundi hilo kwa alama 13. Timu mbili ndio zitafuzu moja kwa moja kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2014 wakati timu itakayoshika nafasi ya tatu itakwenda katika hatua ya mtoano. 

CAF YATOA ORODHA YA MAKUNDI YALIYOBAKIA KATIKA TUZO ZA MWAKA HUU.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limetoa orodha ya makundi yaliyobakia katika tuzo zinazotolewa na shirikisho hilo kwa mwaka huu ambayo ni timu bora ya soka ya wanaume na wanawake pamoja na tuzo ya mchezaji mwenye kipaji zaidi. Mabingwa wa Afrika Zambia, Ivory Coast ambao wanaongoza kwa ubora barani Afrika, Cape Verde ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 na Jamhuri ya Afrika ya Kati ndio timu zilizoteuliwa kugombea tuzo ya timu bora ya taifa. Mabingwa wapya wa soka wa Afrika kwa upande wa wanawake Equatorial Guinea, timu ya taifa ya wanawake ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Ghana ambao walinyakuwa medali ya fedha katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu, timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Falcon ndio timu zitakazogombea tuzo hizo kwa upande wa wanawake. Katika tuzo ya mchezaji mwenye kipaji zaidi lugha nyingine unaweza kuita Most Promising Talent wachezaji watakaochuana kugombea tuzo hiyo ni pamoja na Mohamed Salah wa Misri, Pape Moussa Konate wa Senegal, na Victor Wanyama wa Kenya. Washindi wa tuzo katika makundi hayo watajulikana Desemba 20 mwaka huu katika sherehe zitakazofanyika jijini Accra, Ghana.

ADRIANO AFUNGIWA MCHEZO MMOJA KWA KUSHINDWA KUCHEZA FAIR PLAY.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limemfungia mchezo mmoja mshambuliaji wa Shakhtar Donetsk, Luiz Adriano kwa tabia isiyokuwa ya kimichezo wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Nordsjaelland wiki iliyopita. Adriano ambaye ni raia wa Brazil alifunga bao wakati timu yake ikijaribu kurejesha mpira kwa golikipa wa Nordsjaelland kufuatia mchezaji wa timu hiyo kuumia. Katika taarifa ya UEFA iliyotumwa katika wavuti wake imesema kuwa kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo imeamua kumfungia mchezaji huyo mechi moja kwa tukio lake hilo. Klabu ya Shakhtar katika taarifa yake imeunga mkono adhabu hiyo iliyotolewa na UEFA na kuonyesha kusikitishwa na tukio hilo lililotokea Novemba 20 mwaka huu. Mara baada ya mchezo kusimama na mchezaji wa Nordsjaelland kupatiwa matibabu mwamuzi aliruhusu mchezo kuendelea ambao beki wa Shakhtar William alipiga mpira kuurejesha kwa wapinzani wao kama Fair Play lakini Adriano aliunasa na kumpiga golikipa chenga na kufunga bao kitendo ambacho kilizua taharuki kwa wachezaji wakilalamikia kitendo cha Adriano.

HIDDINK KUSTAAFU MWISHONI MWA MSIMU.

MENEJA wa klabu ya Anzhi Makhachkala, Guus Hiddink amesema kuwa anatarajia kustaafu kufundisha soka mwishoni mwa msimu huu. Hiddink amewahi kuziongoza timu za taifa za Uholanzi na Korea Kusini katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia na pia kuifikisha Urusi nusu fainali ya michuano ya Kombe la Ulaya pamoja na kushinda Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi. Kocha huyo ambaye mkataba wake na klabu ya Anzhi unaishia katikati ya mwaka 2013 amesema kuwa bado anajiona ana nguvu za kuendelea kufundisha lakini inabidi awe mwangalifu asifundishe kwa muda mrefu. Hiddink mwenye umri wa miaka 66 ambaye amewahi kuzifundisha pia klabu za Real Madrid na Chelsea amekiri kuwa kama akifanikiwa kuiwezesha Anzhi kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa mwakani anaweza kubakia hapo kwa mwaka mmoja zaidi.

Tuesday, November 27, 2012

LUIZ ADRIANO - NO FAIR PLAY || Nordsjaelland vs Shakhtar Donetsk 2-5 || ...

SIMBA WAMLILIA SHARO MILIONEA.

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku mkoani Tanga. Kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kutokana na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania. Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki. Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi alizokuwa akifanya. Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia. "Ifahamike kwamba Sharo Milionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo," alisema Rage. Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya haki. Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu kwao. Kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa. Mola na ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani Mkeity (Sharo Milionea).

WAZO LA KUONGEZA NCHI WENYEJI KATIKA MICHUANO YA EURO 2020 KUJADILIWA BRUSSELS.

KWA mujibu wa Chama cha soka cha Ujerumani-DFB mpango wa kuandaa michuano ya Ulaya mwaka 2020 katika nchi zote za bara hilo tofauti na nchi moja au mbili kama ilivyo hivi sasa linaonekana kuungwa mkono na mashirikisho mengi mengi ya soka barani humo. Kuelekea mkutano wa siku mbili wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA ambao utafanyika jijini Brussels, Katibu Mkuu wa DFB Helmut Sandrock amesema kuwa mara ya kwanza walishangazwa na wazo hilo lililotolewa na rais wa UEFA Michel Platini. Pendekezo hilo ambalo bado halijapitishwa na Kamati ya Utendaji ya UEFA litashuhudia nchi 12 mwenyeji wa michuano hiyo ambayo itajumuisha nchi 24 zitakazoshiriki tofauti na 16 kama ilivyo hivi sasa. Sandrock aliendelea kusema kuwa mara ya kwanza walishangazwa na wazo hilo lakini baadae walikaa chini kama DFB kuangalia upya pendekezo hilo na kuona kama kweli linafaa wazo linaonekana linawezekana. Platini alitoa wazo hilo la kuongeza nchi wenyeji kwenye michuano hiyo ili kupunguza muda mrefu wa maandalizi pamoja na gharama ambazo nchi hupata wakati wa maandalizi ya michuano hiyo.

SIMEONE AFURAHISHWA NA KIWANGO CHA ATLETICO.

MENEJA wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone ameonyesha kufuruhishwa na kiwango cha timu yake katika msimu huu wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga. Atletico wamefanikiwa kushinda michezo yao 13 kati ya 15 waliyocheza katika ligi hiyo na wapo nyuma kwa vinara wanaaongoza ligi hiyo Barcelona kwa alama tatu. Simeone aliwasifia wachezaji wake kwa kiwango walichokionyesha katika mchezo dhidi ya Sevilla Jumapili iliyopita na kufanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0. Hatahivyo kocha huyo alikataa kuzungumzia mchezo wa la Liga dhidi ya Real Madrid ambao utachezwa Jumamosi kwasababu ya mchezo wa Copa del Rey dhidi ya Real Jean ambao wanatarajia kucheza katikati ya wiki hii. Simeone ambaye ana umri wa miaka 42 amesema kuwa haitakuwa jambo la busara kuwazungumzia Real Madrid na kuwadharau Real Jean ambao wanatarajiwa kucheza nao kabla ya Real.

BRAZIL WACHOMOA KUMUHITAJI GUARDIOLA.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Brazil, Jose Maria Marin amekanusha taarifa kuwa watamteua kocha wa zamani wa Barcelona Pep Guardiola kukiongoza kikosi cha nchi hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Marin amesema kuwa kuna nafasi ndogo sana wa kuchukua kocha mgeni kwani wameshinda mara tano michuano ya Kombe la Dunia wakiwa na kocha mzawa hivyo hawaoni umuhimu wa kuwa na kocha wa kigeni katika kampeni za michuano ya 2014. Chanzo kimoja cha habari kilichokaribu na Guardiola kilidai Jumamosi kuwa Brazil ndio timu pekee ambayo kocha huyo yuko tayari kufundisha baada ya Mano Menezes kutimuliwa baada ya kuinoa timu hiyo kwa miaka miwili na nusu. Wakati akiinoa Brazil, Menezes amekiongoza kikosi cha nchi hiyo kushinda michezo 21 kati ya 40 ukiwemo mchezo wa fainali ya olimpiki ambao walipoteza kwa Mexico na kukosa medali ya dhahabu.

GERRARD, LAMPARD MIONGONI KATIKA ORODHA YA VIUNGO 15 WA FIFPRO 2012.

VIUNGO nyota wa kimataifa wa Uingereza, Steven Gerrard na Frank Lampard wametajwa kuwa miongoni wa viungo 15 waliopo katika orodha itakayounda kikosi cha dunia 2012 maarufu kama FIFPro. Eden Hazard, David Silva na Yaya Toure ni miongoni mwa wachezaji wengine ambao wanacheza katika Ligi Kuu nchini uingereza ambao nao wametajwa katika orodha hiyo. Viungo watatu kati ya hao ndio watachaguliwa kuunda kikosi cha dunia majina ambayo yatatangazwa wakati wa sherehe za utoaji tuzo ya mchezaji bora wa dunia maarufu kama Ballon d’Or Januari 7 mwakani. Klabu ya Barcelona imetoa wachezaji viungo wanne kwenye orodha hiyo ambao ni Sergio Busquets, Csec Fabregas, Andres Iniesta na Xavi Hernandez ambao waliisaidia timu ya taifa ya Hispania kutetea taji lao la Ulaya. Mbali na hao wachezaji wengine waliokuwepo katika orodha ya viungo 15 pamoja na nchi na vilabu wanavyotoka ni pamoja na Xabi Alonso-Hispania na Real Madrid, Luka Modric-Croatia na Real Madrid, Mesut Ozil-Ujerumani na Real Madrid. Wengine ni Andrea Pirlo-Italia na Juventus, Franck Ribery-Ufaransa na Bayern Munich. David Silva-Hispania na Manchester City, Bastian Schweinsteiger-Ujerumani na Bayern Munich.

Monday, November 26, 2012

TEVEZ AFUNGIWA KUENDESHA GARI.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Manchester City, Carlos Tevez amenyang’anywa leseni ya kuendeshea gari baada ya kushindwa kutoa vielelezo vilivyohitajika baada ya gari lake kukamatwa likiwa katika mwendo wa kasi. Gari la Tevez lilivuka kiwango cha mwendo kasi kilichowekwa katika mji wa Morecambe, kaskazini mwa jiji la London Machi 28 mwaka huu wakati wachezaji wa akiba wa City walipokwenda kucheza dhidi ya wachezaji wa akiba wa timu ya Morecambe. Wakili wa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina, Gwyn Lewis aliwaambia mahakimu wa Lancaster kuwa mteja wake alikubali kuwa hakuwakilisha vielelezo vyovyote kuhusiana na tukio na kwa kosa hilo ndio mahakama ikapelekea kumpa adhabu hiyo. Tevez ambaye alipokea taarifa hizo asubuhi jana hakuwepo wakati wa usikilizaji wa shauri lake hilo na muda kamili ambao atafungiwa leseni yake utajulikana Desemba mwaka huu.

CECAFA TUSKER CUP: KILIMANJARO STARS VS BURUNDI.

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara-Kilimanjaro Stars inasubiri kutupa karata yake nyingine kesho wakati itakapopambana na Burundi katika mchezo wa michuano ya Kombe la Tusker ambalo linaandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA. Katika mchezo wa kwanza Kilimanjaro Stars ilifanikiwa kuisambaratisha Sudan kwa kuifunga mabao 2-0 hivyo kama wakishinda mchezo dhidi ya Burundi watakuwa wamejihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Kocha wa Kilimanjaro stars Kim Poulsen amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Burundi ambao waliifunga Somalia mabao 5-1 yamekamilika na ana uhakika kuwa ataibuka na ushindi kwenye mchezo huo. Poulsen alitamba kuwa kikosi chake ambacho kimesheheni wachezaji vijana kitafanya vizuri katika michuano hiyo na pia aliwasifu washambuliaji wake Mrisho Ngassa na John Bocco kwa kucheza kwa kuelewana na kuipa ushindi timu hiyo katika mchezo kwanza. 


VETTEL AFANIKIWA KUTETEA TAJI LA DUNIA.

DEREVA nyota wa mbio za Langalanga wa timu ya Red Bull, Sebastian Vettel amefanikiwa kushinda taji la dunia la tatu mfululizo kwa tofauti ya alama tatu katika michuano ya Brazil Grand Prix. Katika tukio ambalo mbio hizo ziliathiriwa na mvua, Vettel alipambana na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya sita baada ya kuporomoka mpaka nafasi ya mwisho katika mzunguko wa kwanza kufuatia kupata ajali. Mpinzani wake katika mbio hizo Fernando Alonso wa Ferrari alimaliza katika nafasi ya pili ambapo alikuwa akihitaji Vettel kumaliza chini ya nafasi ya saba ili aweze kunyakuwa taji la dunia. Dereva wa timu ya Force India, Nico Hulkenberg alikatwa alama baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kumgonga Lewis Hamilton wakati akijaribu kumpita dereva huyo wa timu ya McLaren. Vettel anakuwa dereva mdogo zaidi katika historia kushinda mataji matatu ya dunia akizidiwa miaka sita na Ayrton Senna ambaye ndiye dereva watatu kushinda mataji matatu mfululizo.

MBIO ZA UBINGWA BADO HAZIJAISHA - VILANOVA.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova amesisitiza kuwa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga bado hazijaisha pamoja na kikosi chake kuongeza pengo la alama 11 na mabingwa watetezi wa ligi hiyo Real Madrid. Barcelona ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Levante jana usiku na kutumia nafasi baada ya Real Madrid kupoteza mchezo wao wa Jumamosi kwa kufungwa na Real Betis kwa bao 1-0. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Vilanova aliwapongeza wachezaji kwa kuonyesha juhudi na kuihakiikishia ushindi timu lakini akasisitiza kuwa mbio za ubingwa bado kwakuwa wapo Atletico Madrid ambao wanafuatia katika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama tatu pekee. Kocha huyo aliendelea kusema kuwa Atletico wameanza msimu vizuri kitu ambacho sio cha kushangaza kwasababu walimaliza msimu uliopita wakiwa katika kiwango cha juu hivyo inabidi kuhakikisha wanelekeza nguvu zao kushinda kila mchezo ili kuendelea kukalia usukani wa La Liga.

"FULECO" MWANASESERE WA KOMBE LA DUNIA 2014.

SHIRIKISHO LA Soka Duniani-FIFA limetoa jina la Fuleco kwa mwanasesere utakaotumika katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, neno ambalo waandaji wamesema kuwa linahusu ufahamu wa mazingira. Karibu nusu ya watu zaidi ya milioni 1.7 ambao walipiga kura katika mitandao walichagua jina Fuleco tofauti na mengine yaliyokuwepo katika kinyang’anyiro hicho ya Zuzeco na Amijubi. Utamaduni wa kuwa na mwanasesere katika Kombe la Dunia ulianza mwaka 1966 wakati wa michuano iliyofanyika Uingereza ambayo waliipa jina la World Cup Wille. Toka kipindi hicho wanasesere wamekuwa wakionekana katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974 iliyofanyika Ujerumani ambao iliitwa Tip Tap ikimaanisha wavulana wawili wa nchi hiyo, Pique ikimaanisha pilipili katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Mexico mwaka 1986 na Zakumi ikimaanisha Chui jina ambalo lilitumika katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini. Fuleco anatarajiwa kuonekana rasmi jijini Sao Paulo baadae wiki hii katika sherehe za upangaji wa ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo itafanyika Juni mwakani.

Sunday, November 25, 2012

HATTON ASTAAFU NGUMI KWA MARA YA PILI BAADA YA KIPIGO.

BONDIA Ricky Hatton kutoka Uingereza mbaye amewahi kuwa bingwa wa dunia wa uzito wa Light Weight ametangaza kustaafu tena mchezo huo baada ya kupewa kipigo na Vyacheslay Senchenko katika pambano lililofanyika jijini Manchester. Hatton mwenye umri wa miaka 34 hajapigana toka mwaka 2009 lakini kurejea kwake ulingoni baada ya muda huyo kuliishia katika raundi ya tisa katika pambano hilo lililofanyika Jumamosi. Bondia anadai kuwa alikuwa akihitaji pambano moja ili kuona kama anaweza kurejesha makali yake kama zamani lakini hilo limeshindikana hivyo hana budi kuachana na mchezo huo ili kufanya mambo mengine. Hatton alitangza kurejea ulingoni Septemba mwaka huu ikiwa ni miezi 14 toka alipotangaza kustaafu mchezo huo kwa mara kwanza. Pambano la mwisho kucheza kabla ya kuamua kuachana na mchezo huo lilikuwa dhidi ya Manny Pacquiao lililofanyika jijini Las Vegas, Marekani mwaka 2009 ambalo alipoteza. 

SNEIJDER HATIHATI INTER.

MENEJA wa michezo wa klabu ya Inter Milan, Marco Branca amependekeza kuwa kiungo Wesley Sneijder hatachezeshwa mpaka atakapokubali kuongeza mkataba wake. Kiungo huyo wa kimataifa kutoka Uholanzi mwenye umri wa miaka 28 amekuwa nje ya uwanja toka Septemba mwaka huu baada ya kuumia amekuwa akihusishwa na taarifa za kuondoka katika klabu hiyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu. Sneijder alihusishwa na taarifa za kuhamia Uingereza katika klabu ya Manchester United mwaka 2011 lakini alikanusha tetesi hizo na kudai hajafanya mazungumzo rasmi juu ya kuhamia huko. Branca amesema kuwa kwasasa watakuwa wavumilivu wakati wakiangalia uwezekano wa kumshawishi nyota huyo ili aongeze mkataba utakaomuwezesha kubakia klabuni hapa kwa muda zaidi. Sneijder alijiunga na Inter Milan mwaka 2009 akiwa amecheza katika vilabu vya Ajax Amsterdam ya Uholanzi na Real Madrid ya Hispania.

GUARDIOLA AIMEZEA MATE BRAZIL.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Barcelona, Pep Guardiola atafurahi kama akipewa kibarua cha kuinoa Brazil ambayo wiki iliyopita ilimtimua kocha wake Mano Menezes. Tetesi hizo Guardiola kutaka kuinoa Brazil ziliandikwa na gazeti la michezo la Lance ambalo lilidai kutoa taarifa hizo kwa mtu wa karibu wa kocha huyo. Guardiola ambaye aliifundisha Barcelona kwa mafanikio baada ya kuchukua mikoba ya kuinoa kutoka kwa Frank Rijkaard mwaka 2008, aliamua kuacha kuifundisha timu hiyo katika kipindi cha majira ya kiangazi na kuamua kupumzika. Katika kipindi cha miaka minne ambayo amekuwa akiinoa Barcelona, Guardiola amefanikiwa kunyakuwa mataji 14 yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

BOLT, FELIX WANYAKUWA TUZO YA WANARIADHA BORA WA MWAKA.

WANARIADHA nyota wanaoshikilia medali za dhahabu katika michuano ya Olimpiki, Usain Bolt na Allyson Felix wamenyakuwa tuzo ya wanariadha bora wa mwaka kwa wanaume na wanawake. Wanaridha hao walitunukiwa tuzo hizo na Shirikisho la Riadha la Kimataifa-IAAF katika sherehe zilizofanyika jijini Barcelna, Hispania jana. Bolt ambaye ni raia wa Jamaica alifanikiwa kutetea medali zake katika mbio za mita 100 na 200 jijini London anakuwa mwanaridha wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara nne mfululizo. Katika michuano ya olimpiki Felix alinyakuwa medali tatu za dhahabu na kufanikiwa kunyakuwa tuzo hiyo mbele ya Jessica Ennis wa Uingereza ambaye naye alikuwepo katika orodha ya mwisho ya wawanariadha wanaogomea tuzo hiyo. 
Felix ambaye anatoka Marekani alifanikiwa kunyakuwa medali za dhahabu katika mbio za mita 200 na pia alikuwa sehemu ya wanariadha walioshinda mbio za kupokezana vijiti za mita 100 na 400 hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushinda medali tatu za dhahabu katika michuano hiyo toka mwaka 1988.

MOURINHO ALIA NA MWAMUZI.

BAO lililofugwa na Benat Etxebarria jana usiku liliipa ushindi wa kushangaza wa bao 1-0 dhidi ya Real Madrid katika mchezo uliochezwa jijini Seville na kuwaacha mabingwa hao watetezi nyuma kwa alama nane kwa Barcelona ambao wanaongoza La Liga huku wakiwa bado na mchezo mmoja mkononi. Matokeo hayo yanaifanya Madrid kubakia katika nafasi ya tatu wakiwa wamejikusanyia alama 26, huku wakiwa wamepitwa alama tano na Atletico Madrid ambao wanashika nafasi ya pili. Mahasimu wa Madrid, Barcelona wanaweza kuongeza pengo na kufikisha alama 11 kama wakiwafanikiwa kushinda mchezo wao wa baadae leo dhidi ya Levante ambao wanashika nafasi ya sita. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo meneja wa Madrid Jose Mourinho amelaumu waamuzi kwa kushindwa kumudu mchezo huo na kuonyesha upendeleo kwa wapinzani wao kitu ambacho kilichangia kwa kiasi wao kupoteza mchezo huo muhimu.

Saturday, November 24, 2012

ABOU-TRIKA AMONG THREE NOMINEES OF AFRICAN BASED PLAYER OFO THE YEAR AWARD.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limetangaza orodha ya majina matatu ya wachezaji wanaocheza soka barani Afrika watakaogombania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2012. Majina hayo yaliyotajwa na CAF ni pamoja na wachezaji wa kimataifa wa Zambia ambao wanacheza katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Reinford Kalaba na Stopila Sunzu pamoja na nyota wa kimataifa wa Misri na klabu ya Al Ahly Mohamed Abou-Trika. Wachezaji nyota wa timu ya Esperance ya Tunisia Youssef Msakni na Tannick N’Djeng waliachwa katika orodha hiyo pamoja na kukiongoza kikosi cha timu hiyo katika mchezo wa fainali wa Ligi ya Mabingwa ya Afrika ambao walipoteza kwa Al Ahly kwa mabao 3-2. Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa katika sherehe zitakazofanyika jijini Accra, Ghana Desemba 20 mwaka huu.

REDKNAPP KUINOA QPR.

HARRY Redknapp ametajwa kuwa meneja mpya wa klabu ya Queens Park Rangers kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Mark Hughes. Redknapp ambaye alitimuliwa katika klabu ya Tottenham Hotspurs June mwaka huu amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ambayo haijashinda mchezo hata mmoja katika Ligi Kuu nchini Uingereza msimu huu. Katika taarifa iliyotumwa katika wavuti wa klabu hiyo wasaidizi wa Hughes, Mark Bowen na eddie Niedzwiecki ndio watakaokuwa makocha wa muda wakati wa mchezo dhidi ya Manchester United na Redknapp atakuwa akitazama mchezo huo jukwaani. Akihojiwa mara baada ya uteuzi huo Redknapp mwenye umri wa miaka 65 amesema kuwa amefurahishwa kuinoa klabu hiyo pamoja na changamoto zilizopo mbele yake za kuhakikisha klabu hiyo inarejesha makali yake ili kuepuka balaa la kushuka daraja.

ARSENAL YALAMBA MKATABA MNONO.

KLABU ya soka ya Arsenal, imekubali kuongeza mkataba wenye thamani ya paundi milioni 150 kwa ajili ya udhamini wa fulana wa kampuni ya ndege ya Emirates. Mkataba huo mpya ambao utamalizika mwishoni mwa msimu wa 2018-2019 utakuwa na thamani ya paundi milioni 30 mwaka kwa timu hiyo inayotoka kaskazini mwa jiji la London. Ofisa Mkuu wa klabu hiyo Ivan Gazidis alithibisha katika wavuti wao juu makubaliano yaliyofikiwa katika mkataba huo mpya ambao utaifanya kuwa mojawapo ya vilabu zenye mikataba minono ya fulana zake. Gazidis ameapa kuwa meneja wa klabu hiyo Arsenal Wenger atapewa sehemu ya pesa hizo ili kuimarisha kikosi chake kiweze kukata kiu ya mashabiki wake kwa kunyakuwa kombe mwishoni mwa msimu. Chini ya mkataba huo kampuni ya Emirates itaendelea kutumia jina lake katika uwanja wa Arsenal mpaka 2028.

MENEZES ATIMULIWA KUINOA BRAZIL.

Shirikisho la Soka nchini Brazil limetangaza kusitisha mkataba na kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Mano Menezes. Menezes amekuwa akiandamwa na wadau wengi wa soka nchini Brazil kwa kushindwa kuifanya timu kurejesha makali yake ya miaka ya nyuma kitu mara nyingi shirikisho la nchi hiyo limekuwa likifumbia macho lawama hizo. Kocha huyo ambaye amechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka 2010 amekuwa akiandamwa kwa kushindwa kuiongoza Brazil kunyakuwa medali yake ya kwanza ya dhahabu katika michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini London mwaka huu pamoja na kutolewa kwa timu hiyo kushiriki michuano ya Copa America mwaka 2011. Shirikisho hilo limesema kuwa kocha mpya ambaye atachukua nafasi ya Menezes atatangazwa mapema Januari mwakani.

ESSIEN HATI HATI KUCHEZA MWAKA HUU.

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Michael Essien bado hajajua rasmi lini atarejea tena uwanjani na kuna uwezekano wa kutocheza tena mwaka huu kutokana majeruhi yanayomsumbua. Majeruhi yanayomsumbua Essien ambayo bado madaktari wa timu hiyo hawajayachunguza kwa undani yamekuwa yakimzuia mchezaji kushindwa kufanya mazoezi na timu hiyo. Essien amekuwa akikumbwa na tatizo la kuwa majeruhi kwa muda mrefu kabla ya hajanunuliwa kwa mkopo kutoka Chelsea kitu ambacho kimemfanya kushindwa hata kuitumikia timu yake ya taifa ya Ghana. Tatizo la Essien lilianza wakati wa mchezo dhidi ya timu ya Real Mallorca, baada ya kucheza dakika 90 katika michezo mitatu mfululizo dhidi ya Celta Vigo, Borussia Dortmund na Mallorca. 

Friday, November 23, 2012

NI BAHATI KWA BANITEZ KUPEWA CHELSEA WAKATI WA CLUB WORLD CUP - FERGUSON.

MENEJA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema kuwa ni bahati kwa Rafael Banitez kuteuliwa kukinoa kikosi cha Chelsea wakati ambapo wanakaribia kwenda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia. Banitez ambaye amewahi kuifundisha Liverpool alichukua nafasi ya Roberto Di Matteo ambaye alitimuliwa Jumatano baada ya kuifundisha kwa kipindi cha miezi nane. Benitez alifanikiwa kunyakuwa taji la michuano hiyo muda mfupi baada ya kupewa mikoba ya kuinoa Inter Milan ya Italia na anaweza kufanya hivyo tena akiwa na Chelsea mwezi ujao. Ferguson amesema kuwa katika CV za Banitez anaweza kuwa na vikombe viwili vya Klabu Bingwa ya Dunia bila kufanya kazi kubwa ya kujenga timu akitolea mfano kocha huyo aliposhinda taji la michuano hiyo wakati alipochukua timu kutoka kwa Mourinho. Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia ni michuano ambayo hushirikisha mabingwa wa vilabu kutoka mabara sita duniani.

SINA URAFIKI NA RONALDO NJE YA UWANJA - ALONSO.

KIUNGO nyota wa Real Madrid, Xabi Alonso amekiri kuwa hana urafiki wa karibu na mshambuliaji nyota wa hiyo Cristiano Ronaldo lakini wamekuwa wakiheshimiana kwakuwa wanafanya kazi pamoja. Toka mwanzoni mwa msimu kumekuwa na tetesi katika kambi ya Madrid baada ya mchezaji huyo kuonyesha hana furaha kuwepo klabuni hapo hadharani. Alonso ambaye ni kiungo wa zamani wa Liverpool amekuwa wa kwanza kuweka wazi mahusiano aliyonayo na nyota huyo wa zamani wa Manchester United na kukiri kuwa urafiki wao ni pindi wawapo uwanjani lakini baada ya hapo kila anashika hamsini zake. Pamoja na kukiri kutokuwa na urafiki wa karibu na Ronaldo lakini alimsifia nyota kuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu na amekuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho kinachonolewa na kocha Jose Mourinho. Alonso pia alimsifia Mourinho kwamba ni kocha bora na amejifunza mengi kutoka kwake tofauti na watu wengi wasiomfahamu wanavyomchukulia.

MAZUNGUMZO YA WAAMUZI LIGI KUU UINGEREZA KUREKODIWA.

WAAMUZI wa Ligi Kuu nchini Uingereza watakuwa wakirekodiwa mazungumzo yao wakati wa mechi za ligi hiyo kufuatia tukio la mwamuzi Mark Clattenburg. Hatua hiyo imechukuliwa ili kuepusha tukio lililomtokea Clattenburg ambaye alituhumiwa kumtolea lugha ya kibaguzi kiungo wa Chelsea John Mikael Obi ingawa baadae Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA. Katika taarifa iliyotolea meneja mkuu wa Chama cha Waamuzi wa Kulipwa nchini humo, Mike Riley imesema kuwa watatambulisha mfumo mpya wa PGMOL ambao utakuwa na uwezo wa kurekodi mazungumzo yote wakati wa mechi husika. Clattenburg alikuwa mwamuzi katika mchezo wa ligi kuu kati ya Chelsea na Manchester United uliochezwa Octoba 28 wakati Ramires ambaye anacheza timu moja na Mikel Obi alipodai kwamba alimsikia mwamuzi huyo akimtolea maneno ya kibaguzi kiungo huyo.

Thursday, November 22, 2012

WATANO KUGOMBEA TUZO YA BBC AFRICAN PLAYER OF THE YEAR.

MAJINA matano ya wachezaji watakaogombea tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika mwaka huu ambayo inatolewa na Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC yametangazwa rasmi. Majina ya wachezaji hao ni pamoja na Yaya Toure ambaye anaingia katika orodha hiyo kwa mara ya pili mfululizo akiungana na nyota mwenzake kutoka Ivory Coast, Didier Drogba, Demba Ba kutoka Senegal, Younes Belhanda kutoka Morocco na nahodha wa Zambia Christopher Katongo. Mshindi wa tuzo hiyo ataamuliwa na mashabiki wa soka barani Afrika Afrika ambao wanatapa nafasi ya kupiga kura mpaka Alhamisi Desemba 13 mwaka huu ya kuchagua mchezaji wanayedhani amefanya vizuri. Wachezaji hao wamechaguliwa kugombea tuzo hiyo kutokana na kufanya vizuri kwa mwaka huu katika vilabu na timu zao za taifa ambapo mshindi anatarajiwa kutangazwa Jumatatu Desemba 17 mwaka huu.

DI MATTEO AELEZA MAPENZI ALIYONAYO KWA CHELSEA PAMOJA NA KUTIMULIWA.

ROBERTO Di Matteo amezungumzia mapenzi yake ya dhati aliyonayo kwa klabu ya Chelsea pamoja na kutimuliwa kuinoa timu hiyo baada ya kukabidhiwa miezi nane iliyopita. Kocha huyo alifanikiwa kushinda kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA baada ya kushika nafasi kwa muda baada ya aliyekuwa kocha wa timu Adres Villas Boas kutimuliwa ingawa baadae alipewa mkataba wa miaka miwili. Akihojiwa mara baada ya taarifa za kutimuliwa kutolewa Di Matteo amesema kuwa anajivunia mafanikio aliyopata katika kipindi kifupi alichokuwa meneja wa klabu hiyo ambayo amekuwa na mapenzi nayo kwa kipindi kirefu. Di Matteo alijiunga na Chelsea kama mchezaji mwaka 1996 na kufunga mabao 26 katika michezo 175 aliyocheza kabla ya kuamua kutundika daruga kwasababu ya kuwa majeruhi akiwa na umri wa miaka 31. Aliyewahi kuwa meneja wa Liverpool, Rafael Banitez ndio ameteuliwa kuchukua nafasi ya Di Matteo mpaka msimu huu utakapomalizika.

CHELSEA YAPANGA KUMREJESHA DROGBA STAMFORD BRIDGE.

KLABU ya Chelsea iko katika mazungumzo ambayo kuna uwezekano wa kuona mshambuliaji wake wa zamani Didier Drogba akirejea Stamford Bridge akitokea klabu ya Shanghai Shenhua ya China kwa mkopo. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 34 anataka kujiweka fiti kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 katika kipindi hiki ambacho msimu wa ligi nchini china umemalizika. Drogba ameliomba Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kumpa ruhusa ya kuhama kabla ya kipindi cha usajili cha dirisha dogo Januari mwakani ombi ambalo shirikisho hilo limedai inalishughulikia. Chelsea katika kipindi cha karibuni imekuwa ikikabiliwa na tatizo la mshambuliaji kutokana na Fernando Torres kushuka kiwango huku Daniel Sturridge kuwa majeruhi. Drogba ambaye pia amehusishwa na tetesi za kwenda Liverpool, alikaa katika klabu Chelsea kipindi cha miaka nane baada ya kusajiliwa akitokea Olympique Marseille ya Ufaransa mwaka 2004.

WENGER SASA ATAKA KUONGOZA KUNDI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amepanga kutumia kikosi chake cha kwanza katika mchezo wa mwisho wa kundi B wa Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na timu yake kufuzu hatua ya timu 16 bora. Arsenal ilifanikiwa kutinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga Montpellier ya Ufaransa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika jana lakini wanatarajia kusafiri kuifuata Olympiakos Desemba 4 katika mchezo wa mwisho huku wakiwa katika nafasi ya pili mbele ya Schalke 04 ambao wanaongoza kundi hilo. Wenger amesema kuwa amepanga kutumia kikosi chake kamili katika mchezo huyo ili kujaribu kushinda na kumaliza wakiwa vinara wa kundi hilo kitu ambacho kitakuwa muhimu. Kama wakimaliza vinara katika kundi lao watapangiwa timu ambazo zimeshika nafasi ya pili katika makundi mengine na kama wakishindwa kufanya hivyo na kumaliza katika nafasi ya pili watapangiwa kucheza na washindi wa makundi mengine katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Wednesday, November 21, 2012

Full HD Manchester City Vs Real Madrid 1- 1 2012 All Goals & Highlights ...

Schalke Vs Olympiakos 1-0 All Goals & Highlights 21/11/2012

Arsenal vs Montpellier 2-0 ALL GOALS & HIGHLIGHTS 21-11-2012

FC Porto Vs Dinamo Zagreb 3-0 All Goals & HighLights 21.11.2012 HD

PSG vs Dynamo Kyiv 2-0 All Goals And Highlights HD 21/11/2012

TAARIFA MBALIMBALI TFF LEO.

TIKETI ZA FAINALI ZA AFCON 2013 KUPATIKANA KWA MTANDAO
Washabiki wanaotaka kushuhudia Fainali za 29 za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusiniwatapata tiketi kwa njia ya mtandao. Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tiketi kwa ajili ya washabiki (public tickets) wanaotaka kuhudhuria fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu, zitauzwa kupitia mtandao wa www.afcon2013booking@eqtickets.com. Piatiketi zitapatikana kupitia simu namba +27 879803000. Fainali hizo zinazoshirikisha timu 16 zitachezwa Johannesburg, Nelson Mandela Bay, Mbombela, Durban na Rustenburg. Mechi ya fainali itachezwa Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Soccer City jijini Johanesburg kuanzia saa 2 usiku kwa saa za Afrika Kusini. Mechi ya ufunguzi wa fainali hizo itachezwa Januari 19 mwaka huu ambapo wenyeji Afrika Kusini (Bafana Bafana) wataumana na Cape Verdekuanzia saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Soccer City. Angola na Morocco zitacheza mechi ya pili kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 3 usiku. Timu zote hizo ni za kundi A. Mabingwa wateteziZambia wako kundi C na wataanza mechi yao ya kwanza Januari 21 mwaka huu dhidi ya Ethiopia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Mbombela. Timu nyingine katika kundi hilo ni Nigeria na Burkina Faso.

DI MATTEO ATIMULIWA CHELSEA.

Mabingwa wa Ulaya klabu ya Chelsea imeamua rasmi kuvunja mkataba na kocha wake Roberto Di Matteo kufuatia matokeo mabaya ambayo yamekuwa yakiikabili timu hiyo katika michezo yake ya hivi karibuni. Hatua ya klabu hiyo kumtimua Di Matteo imekuja kufuatia kufungwa na Juventus kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kipigo ambacho kimewaweka katika hati hati ya kushindwa kusonga mbele katika michuano hiyo. Katika taarifa iliyotumwa katika wavuti wa klabu hiyo imesema kuwa klabu hiyo imeamua kufanya mabadiliko ya haraka baada ya kuona timu hiyo kisuasua katika michiano mbali mbali inayoshiriki ikiwemo ligi ya mabingwa na ligi kuu nchini Uingereza. Taarifa iliendelea kusema kuwa klabu itatangaza muda mfupi baadae meneja ambaye atachukua mikoba ya Di Matteo. 




EUROPA LEAGUE ACTION.

Michuano ya Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League inatarajiwa kutimua vumbi tena leo huku kila timu ikijaribu kuhakikisha inatinga katika hatua ya timu 32 bora za michuano hiyo. Timu za Anzhi mkhachkala ya Urusi, Udinese ya Italia, Liverpool ya Uingereza na Young Boys ya Switzerland zote zitajitupa uwanjani kusaka ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo. Katika michezo mingine ya leo mabingwa watetezi wa michuano hiyo Atletico Madrid ya Hispania itaikaribisha Hapoel Tel Aviv ya Israel, Rubin Kazan ya Urusi nao watakuwa wenyeji wa Inter Milan ya Italia wakati Basel ya Swtzerland itaikaribisha Sporting Lisbon ya Ureno. Katika viwanja vingine Tottenham Hotspurs watakuwa na kibarua kigumu cha kusaka ushindi ugenini mbele ya Lazio ya Italia wakati waingereza wenzao Newcastle United wenyewe watakuwa nyumbani kuikabili Maritimor ya Ureno.

REKODI BINAFSI HAINA UMUHIMU KWANGU - MESSI.

Mshambuliaji wa Barcelona, LIONEL MESSI amesisitiza kuwa mawazo yake yapo katika kuisaidia timu yake kuliko kufikia rekodi ya kufunga mabao 85 katika kipindi cha mwaka mmoja aliyoweka GERD MULLER wa Ujerumani. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina aliifungia Barcelona mabao mawili na kuisadia timu yake hiyo kuifunga Spartak Moscow mabao 3-0 na kumfanya kufikisha mabao 80 kwa mwaka huu lakini Messi amesema mataji kwa timu yake ndio muhimu zaidi kuliko rekodi binafsi. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo kuhusiana na suala ya yeye kuikaribia rekodi ya MULLER, MESSI amesema kuwa kitu muhimu kwake ni timu yake kupata matokeo mazuri ndio maana amekuwa akifanya juhudi pamoja na wachezaji wenzake kuhakikisha hilo linawezekana. Naye kocha wa Barcelona TITO VILANOVA aliungana na MESSI akidai kuwa nyota huyo hachezi ili aweze kuvunja rekodi bali kuisaidia timu ili iweze kufanya vizuri.

BOLT KUHAMIA KATIKA KRIKETI AU SOKA BAADA YA 2016.

Mwanariadha nyota wa mbio fupi USAIN BOLT anatarajiwa kutoshiriki mashindano ya riadha ambayo ni ya mwisho kwa mwaka huu ya Twenty20 League lakini ataweza kuhamia katika mchezo wa kriketi au soka baada ya michuano ya Olimpiki 2016. Wakala wa mwanariadha huyo RICKY SIMMS amesema kuwa kwasasa nyota huyo ni mwanariadha alielekeza nguvu zake katika maandalizi ya mashindano ya Dunia ya riadha yatakayofanyika jijini Moscow 2013. SIMMS alikiri kuwa nyota huyo ana ndoto za kucheza kriketi au soka wakati ambapo atastaafu mchezo wa riadha lakini itakuwa baada ya olimpiki ya 2016 itakayofanyika jijini Reo de Janeiro, Brazil. BOLT ni mwanariadha anayepewa heshima kubwa kwasasa baada ya kufanikiwa kutetea mataji yake yam bio za mita 100, 200 na mita 400 za kupokezana vijiti katika michuano ya olimpiki iliyofanyika iliyopita.

Tuesday, November 20, 2012

MESSI AENDELEA KUVUNJA REKODI MBALIMBALI.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi ameendeleza rekodi yake ya kufunga mabao baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao timu yake ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Spartak Moscow. Mabao hayo ya nyota huyo aliyofunga jana yamemwezesha kufikisha mabao 56 katika michuano hiyo ya Ulaya na kumuweka sawa katika nafasi ya pili ya wafungaji bora wa bara hilo akiwa sambamba na Ruud van Nisterlrooy wakizidiwa na Raul ambaye yeye amefunga mabao 71. Messi pia amefikia rekodi ya Raul ya kufunga bao katika nchi 19 tofauti katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na kumpita nyota huyo huyo wa zamani kwa kufunga mabao zaidi ya mawili katika mechi 14 za michuano hiyo. Nyota huyo amebakisha mabao matano pekee kufikia rekodi ya Gerd Muelller aliyefunga mabao 85 ndani ya mwaka mmoja katika mashindano yote rekodi ambayo aliiweka mwaka 1972. Messi amekuwa akiongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi cha miaka minne iliyopita huku msimu uliopita akifikisha mabao 14 ambayo ndio mengi zaidi kwa msimu.

HENRY KUREJEA TENA ARSENAL JANUARI.

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry anaweza kurejea tena katika klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa jiji la London kwa mkopo kutokea katika klabu ya New York Red Bull ya Marekani Januari mwaka huu. Meneja wa Arsenal, Arsenal Wenger alibainisha hayo katika wavuti wa klabu hiyo kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumsajili nyota huyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili kwasababu amekuwa akifanya nao mazoezi nab ado anaonekana ana uwezo ya kukabiliana na mikiki ya ligi. Henry ambaye ana rekodi ya kufunga mabao 228 alirejea katika klabu hiyo Januari mwaka jana na kufunga bao katika mchezo dhidi ya Leeds United katika Kombe la FA na kufunga bao la ushindi katika dakika za mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Sunderland. Wenger ameonyesha nia ya kumrejesha tena shujaa wake huyo na anaamini kuwa anaweza kuwa msaada mkubwa haswa ikizingatiwa kuwa anaweza kuwapoteza washambuliaji wake wawili Gervinho kutoka Ivory Coast na Marouane Chamakh ambao kuna uwezekano mkubwa wa kuitwa kuzitumikia timu zao za taifa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Januari mwakani. 

Galatasaray vs Manchester United 1-0 Full Goals and Highlights 20/11/2012

Valencia vs Bayern Munich 1-1 ALL GOALS & HIGHLIGHTS

Luiz Adriano Goal vs FC Nordsjaelland vs Shakhtar Donetsk 2-5 Controvers...

Juventus Vs Chelsea 3-0 All Goals and Highlights 20/11/2012

Spartak Moscow Vs Barcelona 0-3 All Goals & Highlights 20.11.2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

NYAMLANI ATEULIWA KAMATI YA AFCON 2013  
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani ameteuliwa kuwemo kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini. Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo wa CAF kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu una jumla ya watu 148. Nyamlani ni mmoja wa wajumbe watatu watakaoshughulia masuala ya rufani. Wajumbe wengine ni Prosper Abega kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon. Nyamlani ni mjumbe wa Bodi ya Rufani ya CAF yenye watu 12.

MECHI YA SERENGETI BOYS YAINGIZA MIL 23/-  
Mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville iliyochezwa juzi (Novemba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,021,000. Mapato hayo yametokana na washabiki 18,022 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 10,000, sh. 5,000, sh. 2,000 na sh. 1,000. Washabiki 15,850 walikata tiketi za sh. 1,000. Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 3,511,677.97 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 5,956,635), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh. 400,000), Wachina- Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na ulinzi wa mechi (sh. 3,500,000). Kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 1,000,537, asilimia 10 ya uwanja sh. 500,269, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 250,134, asilimia 45 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,251,209, asilimia 20 ya TFF (sh. 1,000,537) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 50,027.

UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA KATAVI (KAREFA) Mchakato wa uchaguzi wa KAREFA umefutwa kutokana na wagombea watano kati ya nane vyeti vyao vya elimu ya sekondari kuwa na utata. Mchakato wa uchaguzi huo utaanza upya Novemba 21 mwaka huu.

UCHAGUZI WA TASMA  
Mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utaanza upya Novemba 26 mwaka huu baada ya mchakto wa sasa kupata wagombea kwenye nafasi mbili tu za Kamati ya Utendaji ya chama hicho.

UCHAGUZI WA CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA RUKWA (RUREFA)  
Mchakato wa uchaguzi wa RUREFA utaanza Novemba 26 mwaka huu na Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA itapewa maelekezo ya usimamiaji wa uchaguzi huo baada ya mchakato wa awali kuwa umefutwa kutokana na kufanyika bila kuzingatia kanuni za uchaguzi.

JUVENTUS YAMUWINDA DROGBA.

KLABU ya Juventus ya Italia inapanga kumsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Ivory Coast Didier Drogba anayecheza kwenye klabu ya Shanghai Shenhua ya China katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Mabingwa hao wa Serie A wamekuwa sokoni kwa kipindi kirefu wakitafuta mshambuliaji ambapo katika kipindi cha karibuni wamekuwa wakihusishwa na Fernando Llorente na Pablo Asvaldo na hivi sasa wamehamishia nguvu zao kumsajili Drogba mwenye umri wa miaka 34. Drogba alijunga na kabu hiyo inayoshiriki Ligi kuu nchini China kutoka Chelsea katika kipindi cha usajili cha majira ya kiangazi lakini anaonekana hana furaha na ana nia ya kurejea Ulaya tena. Sababu ya Drogba ambaye analipwa euro milioni 12 kwa mwaka ni kutofurahishwa na mazingira ya klabu hiyo kumcheleweshea mshahara wake zaidi ya mara moja toka alipohamia huko. Hatahivyo Juventus wanakabiliwa na wakati mgumu wa kumsajili mchezaji huyo kwa kuwa wamepanga kupunguza mshahara wake kama akikubalia kujiunga nao na kumlipa euro milioni 4.5 kwa mwaka pamoja na posho nyingine.

HUGHES KUBAKIA QPR.

MENEJA wa Queens Park Rangers, Mark Hughes atabakia kuinoa klabu hiyo ambayo inasuasua katika mstari wa kushuka daraja kufuatia mkutano aliofanya na Ofisa Mkuu wa klabu hiyo Philip Beard. Kuna taarifa zilizosambaa kuwa Hughes ambaye amewahi kuwa kocha wa Wales alifukuzwa baada ya wawili kukutana katika uwanja wa mazoezi jana lakini mwakilishi wa kocha huyo Kia Joobchian alikanusha tetesi hizo na kudai sio za kweli. Hughes amekuwa na matokeo mabaya toka mwanzoni mwa msimu huu akiwa ameambulia alama nne pekee katika michezo 12 ambayo timu hiyo imecheza msimu huu hivyo kushika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Blackburn Rovers, Manchester City na Fulham amesisitiza kuwa hawezi kujiuzulu kibarua hicho kufuatia kufungwa nyumbani mabao 3-1 na Southampton ambao wote wanapigania kutoshuka daraja.

KAGAWA KUKAA NJE WIKI NNE ZAIDI.

KIUNGO nyota wa klabu ya Manchester United, Shinji Kagawa ameongezewa wiki zingine nne kukaa nje ya uwanja kutokana na majeruhi yanayomsumbua. Kiungo huyo wa kimataifa wa Japan mwenye umri wa miaka 23 aliumia mguu wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao timu yake ilishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Braga Oktoba 23 mwaka huu. Meneja wa United Sir Alex Ferguson alimtegemea mchezaji huyo kupona katika kipindi cha wiki nne mpaka tano lakini nyota huyo ameonekana kupona taratibu hivyo kuna uwezekano wa kukaa nje ya uwanja kwa nyingine nne nyingine. Pamoja na habari mbaya kuhusu Kagawa lakini Ferguson amefarijika baada ya beki wake nyota Phil Jones kurejea katika kikosi chake baada ya kuumia mgongo wakati maandalizi ya msimu mpya wa ligi hiyo. Beki huyo mwenye umri wa miaka 20 anatarajiwa kuwepo katika mchezo wa kundi H leo ambapo United watakuwa wageni wa Galatasaray ya Uturuki.