Friday, January 31, 2014

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

SIMBA YAIKARIBISHA OLJORO JKT DAR
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania inaingia raundi ya 16 wikiendi hii kwa mechi nne ambapo kesho (Februari 1 mwaka huu) Simba itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ni sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Refa atakuwa Nathan Lazaro kutoka mkoani Kilimanjaro wakati Kamishna ni Hakim Byemba wa Dodoma. Uwanja wa Azam uliopo Mbagala siku hiyo kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Ashanti United na Mgambo Shooting kutoka Handeni mkoani Tanga kwa viingilio vya sh. 3,000 kwa sh. 10,000. Jumapili (Februari 2 mwaka huu) ni Yanga vs Mbeya City (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, saa 10 kamili jioni), na Azam vs Kagera Sugar (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi saa 10 kamili jioni). Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 5 mwaka huu) kwa mechi kati ya Tanzania Prisons vs Coastal Union (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Mgambo Shooting vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers vs Oljoro JKT (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), na JKT Ruvu vs Ashanti United (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi).



SERENGETI BOYS YAPANGIWA AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) itacheza na Afrika Kusini katika mechi za mchujo kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger. Serengeti Boys ambayo pamoja na nchi nyingine 17 zimeingia moja kwa moja katika raundi ya pili itaanzia mechi hiyo nyumbani kati ya Julai 18-20 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika nchini Afrika Kusini kati ya Agosti 1-3 mwaka huu. Ikifanikiwa kuitoa Afrika Kusini, Serengeti Boys itacheza mechi ya raundi ya tatu na ya mwisho na mshindi wa mechi kati ya Misri/Sudan vs Congo Brazzaville. Nchi nyingine ambazo zimeingia moja kwa moja raundi ya pili ni Afrika Kusini, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Congo Brazzaville, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Mali, Morocco, Nigeria, Rwanda, Senegal, Tunisia na Zambia. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kutangaza benchi la ufundi litakaloiongoza Serengeti Boys hivi karibuni.


BODI YA LIGI YAZIPIGA JEKI KLABU ZA FDL
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa sh. milioni 1.5 kwa kila klabu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Uamuzi wa kuzisaidia timu hizo ulifanywa katika kikao cha TPLB kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo fedha hizo zitalipwa kupitia kwenye akaunti za klabu husika. Hivyo klabu ambazo hazijawasilisha akaunti zao TPLB zinatakiwa kuwasilisha haraka. Klabu za FDL ni African Lyon, Burkina Moro, Friends Rangers, Green Warriors, Kanembwa JKT, Kimondo, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mkamba Rangers, Mlale JKT na Mwadui. Nyingine ni Ndanda, Pamba, Polisi Dar es Salaam, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Morogoro, Polisi Tabora, Stand United, Tessema, Toto Africans, Trans Camp na Villa Squad.

BAADA YA KUMKOSA DRAXLER, WENGER SASA AHAMISHIA NGUVU ZAKE KWA MKONGWE WA SWEDEN KALLSTROM.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa hawezi tena kumsajili kiungo mahiri wa klabu ya Schalke, Julian Draxler baada ya klabu hizo kushindwa kufikia makubaliano. Huku muda wa usajili wa dirisha dogo ukikaribia mwishoni Wenger sasa amehamishia nguvu zake kwa kiungo mkongwe Kim Kallstrom kutoka klabu ya Spartak Moscow ya Urusi ili aweze kuimarisha safu yake ya kiungo ambayo imekumbwa na majeruhi wengi. Arsenal ilishindwa kufikia makubaliano na Schalke baada ya klabu hiyo kutaka kutoa kiasi cha paundi milioni 25 au 30 lakini Wajerumani hao wao walitaka paundi milioni 37.3. Wakati akimkosa Theo Walcott kwa msimu mzima, Aaron Ramsey kwa wiki sita huku Jack Wilshere akiwa katika hatihati ya kucheza katika mechi dhidi ya Cardiff City, Wenger amepania kuongeza nguvu katika kikosi chake ili aweze kuhakikisha wanaweka hai matumaini yao ya kunyakuwa taji la Ligi Kuu.

CHICHARITO KUBAKIA UNITED - WAKALA.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa klabu ya Manchester United, Javier Hernandez maarufu kama Chicharito amedai kuwa mteja wake huyo hawezi kuondoka Old Traford katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo lakini anaweza kuondoka majira ya kiangazi. Nyota huyo wa kimataifa wa Mexico amekuwa akipambana kurejea katika kiwango chake toka awe chini ya David Moyes msimu huu akiwa amefunga mabao mawili katika mechi 14 alizocheza lakini wakala huyo aitwaye Eduardo Hernandez amesema klabu hiyo imesisitiza kuwa bado inamuhitaji nyota huyo. Pamoja na kuwa mkataba wa Chicharito unamalizika majira ya kiangazi mwaka 2015, lakini Hernandez amesema kuna uwezekano mkubwa mteja wake huyo ajaondoka baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. Wakala huyo aliendelea kudai kumekuwa na vilabu nchini Ujerumani, Ufaransa, Hispania na Italia ambavyo vinahitaji huduma ya nyota huyo hivyo hawezi kujua hali itakavyokuwa baada ya Kombe la Dunia.

KUSHINDA KOMBE LA DUNIA ITAKUWA NGUMU - REUS.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ujerumani, Marco Reus anaamini kuwa nchi hiyo itakabiliwa na wakati mgumu kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka huu lakini akasisitiza kuwa mabingwa hao mara tatu wa michuano hiyo watakwenda Brazil wakiwa na matumaini ya kufika mbali. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kuna uwezekano mkubwa akawemo katika kikosi cha nchi hiyo kinachonolewa na Joachim Low lakini amekuwa na tahadhari kuhusu uhakika wan chi yake kunyakuwa taji la nne kwenye michuano hiyo. Reus amesema michuano ya Kombe la Dunia ndiyo bora kabisa katika soka hivyo timu zote zonazoshiriki zinakuwa zimejiandaa vyema hivyo lazima hali itakuwa ngumu kwasababu kila timu inataka kushinda taji hilo kama ilivo kwao. Nyota huyo aliendelea kusema kuwa hakuna anayejua kinachoweza kutokea katika mashindano hayo kama vile majeruhi lakini hana shaka kwamba timu yake inaweza kufikia hatua ya fainali.

MKALI WA MIPIRA YA ADHABU, JUNINHO ASTAAFU SOKA RASMI.

BINGWA wa kupiga mipira ya adhabu (free Kick) Mbrazil Juninho Pernambacano ameamua kutundika daruga baada ya kudumu katika ulimwengu wa soka kwa kipindi cha miaka 20. Rais wa klabu ya Vasco da Gama ya Brazil, Roberto Dinamite alikaririwa akidai kuwa amezungumza na nyota huyo na kumhakikishia kuwa ameamua kupumzika rasmi mchezo wa soka. Juninho ambaye amesheherekea siku yake ya kuzaliwa Alhamisi akitimiza miaka 39 ameichezea Vasco da Gama mechi 393 katika vipindi vitatu tofauti. Akiwa na timu hiyo Juninho ameshinda taji la ligi mwaka 1997 na 2000, taji la Klabu Bingwa ya Amerika Kusini mwaka 1998 na Copa Mercosul mwaka 2000 huku akiwa amefunga mabao 76 kwa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Rio de Janeiro. Juninho pia amecheza soka kwa mafanikio nchini Ufaransa katika klabu ya Olympique Lyon na kufanikiwa kushinda mataji saba mfululizo ya Ligi Kuu nchini humo kuanzia mwaka 2002 mpaka 2008.

GET WELL SOON FALCAO - RONALDO.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo amemtakia heri ya kupona haraka Radamel Falcao na kudai kuwa soka limhitaji mshambuliaji huyo kwenye Kombe la Dunia. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anayecheza katika klabu ya Monaco ya Ufaransa, atakuwa nje kwa msimu wote uliobakia baada ya kuchanika msuli wa ndani katika goti lake la kushoto mapema Januari hatua ambayo inaweza kupelekea akaikosa pia michuano ya Kome la Dunia itakayofanyika Juni nchini Brazil. Hata hivyo, madaktari waliomfanyia upasuaji Falcao wamedai kuwa anaweza kupona kwa wakati kwa ajili ya michuano hiyona Ronaldo anamuomba iwe hivyo kwa nyota huyo wa kimataifa wa Colombia. Ronaldo amesema Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Colombia wanamsubiri na ana matumaini kuwa atapona haraka na kurejea uwanjani kwa wakati.

CITY YAINGIA SOKONI KWA FUJO, YAWATAKA WAWILI KWA MPIGO.

WAKATI pilikapilika za usajili wa dirisha dogo barani zikielekea ukingoni, vinara wa Ligi Kuu nchini Uingereza klabu ya Manchester City imepanga kusajili nyota wawili Eliaquim Mangala na Fernando kutoka klabu ya FC Porto ya Ureno. Pamoja na ushindi mnono wa mabao 5-1 waliopata dhidi ya Tottenham Hotspurs, meneja wa City Manuel Pellegrini bado anaonyesha hajaridhishwa na safu ya ulinzi ya kikosi chake ndio maana anataka kuongeza nguvu mpya kabla ya muda wa mwisho wa usajili leo usiku. City wanatarajiwa kutoa kitita cha paundi milioni 35 kwa ajili ya Mangala mwenye umri wa miaka 22 huku Mbrazil Fernando mwenye umri wa miaka 26 naye akitarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya kiungo. Mbali na City, Mangala ambaye ni raia wa Ufaransa amekuwa akizivutia timu kama Manchester United na Paris Saint-Germain ya Ufaransa. Kama Mangala akifanikiwa kutua City, itafungua milango kwa beki mahiri wa kimataifa wa Uingereza Joleon Lescott kuondoka klabuni hapo kwa mkopo.

MADAKTARI WAANZA KUMPUNGUZIA SCHUMACHER DOZI YA USINGIZI ILI AAMKE.

MENEJA wa dereva nyota wa zamani wa mashindano ya langalanga, Michael Schumacher amesema madaktari wanamtibu wameanza kupunguza dozi nzito za usingizi walizompa ili aweze kuamka taratibu. Meneja huyo Sabine Kehm amesema hatua hiyo ni muhimu kwa afya ya Schumacher na inaweza kuchukua muda mrefu. Schumacher alianguka na kuumia kichwani wakati akiteleza katika barafu huko katika milima ya Ufaransa Desemba 29 mwaka jana. Toka kipindi hicho madaktari wamekuwa wamemuweka katika dozi kubwa za usingizi ili ubongo wake uweze kupona wenyewe taratibu kwasababu ya upasuaji mara mbili aliofanyiwa kutokana na ajali aliyopata.

Thursday, January 30, 2014

TAARABT KUTIMKIA AC MILAN.

KLABU ya AC Milan ya Italia imetangaza kuwa Adel Taarabt tayari amewasili klabuni hapo kwa ajili ya kumalizia taratibu za uhamisho wake. Kiungo huyo wa klabu ya Queens Park Rangers ambaye msimu alikuwa akicheza kwa mkopo Fulham anatarajia kuhamia kwa vigogo hao wa soka nchini Italia. Nyota huyo wa kimataifa wa Morocco mwenye umri wa miaka 24 alitua katika Uwanja wa Ndege jijini Milan kwa ndege binafsi na uhamisho wake unatarajiwa kukamilika kabla ya muda wa mwisho wa usajili wa dirisha leo saa sita za usiku. Taarabt atakuwa mchezaji wa pili kutoka Ligi Kuu nchini Uingereza kutua Milan Januari hii baada ya Michael Essien kukamilisha usajili wake akitokea Chelsea.

SAMMER AMTAKA MANDZUKIZ KUPANDISHA KIWANGO CHAKE ILI AWEZE KUPATA NAMBA.

MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Bayern Munich, Matthias Sammer amemtaka Mario Mandzukic kuwa katika kiwango chake cha juu kwa msimu mzima uliobakia. Nyota huyo wa kimataifa wa Croatia aliachwa katika kikkosi cha timu hiyo ambacho kilishinda mabao 2-0 dhidi ya Borussia Monchengladbach na kuzua tetesi juu ya mustakabali wake siku zijazo haswa ukizingatia ujio wa Robert Lewandowski kiangazi. Hata hivyo, Sammer bado anaamini kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 bado anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha Bayern lakini anatakiwa kucheza kwa kiwango chake cha juu. Sammer amesema Mandzukic bado ni mchezaji muhimu kwao lakini kama akifanya kila analoweza kuhakikisha anarudi katika kiwango chake. Nyota huyo amecheza mechi 17 za Bundesliga msimu huu na kufunga mabao 10.

CHAN 2014 FINAL: GHANA KUKWAANA NA LIBYA.

TIMU ya taifa ya Ghana, Black Stars imewashangaza mabingwa wa soka wa Afrika timu ya taifa ya Nigeria kwa kuwang’oa kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN jana usiku. Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Free State ulimalizika kwa sare ya bila ya kufungana mpaka katika muda wa nyongeza huku Ghana wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja na kupelekea kupigiana mikwaju ya penati ambapo Ghana iliibua kwa ushindi wa matuta 4-1. Ghana sasa itachuana na Libya kaika mchezo wa fainali utakaochezwa Jumamosi jijini Cape Town ambapo hiyo itakuwa fainali yao ya pili katika michuano hiyo baada ya kupoteza kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwaka 2009. Libya wao walitinga haua hiyo baada ya wao pia kuindosha Zimbabwe kwa changamoto ya mikwaju ya penati 5-4 katika mchezo uliofanyika huko Bloemfontein.

VETTEL ASONONESHWA NA HALI YA SCHUMACHER.

BINGWA wa mashindano ya langalanga, Sebastian Vettel ameonyesha wasiwasi wake juu ya hali ya dereva nyota wa zamani wa mashindano Mjerumani mwenzake Michael Schumacher kutokana na majeraha ya kichwa aliyopata. Schumacher ambaye ni bingwa mara saba wa mashindano hayo amewekwa katika dozi ya usingizi toka alipogonga kichwa chake katika jiwe wakati akiteleza katika barafu mwezi uliopita. Vettel ameelezea masikitiko yake kuhusiana na hali ya nyota huyo na kudai hawajui atakuwa na hali gani pindi atakapoamka kutoka katika dozi ya usingizi aliyopewa. Vettel amesema ni jambo gumu hususani kwa familia na marafiki zake wa karibu kutokujua kitakachotokea lakini wanamuombea kila siku aamke akiwa katika hali yake ya kawaida.

MOURINHO AILALAMIKIA WEST HAM KWA KUPAKI BASI.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho ameponda aina ya uchezaji wa timu ya West Ham United na kudai kuwa ni wa karne ya 19 kufuatia timu yake kutoa sare ya bila ya kufungana katika Uwanja wa Stamford Bridge. Chelsea walifanya kila wanaloweza kuhakikisha wanapenya ngome ya West Ham wanaonolewa na Sam Allardyce lakini walishindwa na kujikuta wakigaana alama hivy kushindwa kuwafikia Arsenal ambao wameshuka mpaka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Akihojiwa Mourinho amesema kuwa mchezo waliocheza West Ham wa kizamani na haufanani na timu iliyokuwa katika Ligi Kuu. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa ni ngumu kucheza mechi wakati timu moja pekee ndio inayotaka kucheza huku nyingine ikifanya kazi ya kuzuia pekee.

Monday, January 27, 2014

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

TIKETI ZA ELEKTRONIKI ZIPO SOKONI
Mauzo ya tiketi za elektroniki kwa mechi tatu kati ya nne za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) tayari yameanza, hivyo wanatakiwa kununua mapema. Mechi hizo ni kati ya Coastal Union na Yanga itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na ile ya Azam dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Azam Complex. Kwa washabiki wa Dar es Salaam watakaokwenda Tanga kushuhudia mechi kati ya Coastal Union na Yanga wanashauriwa kuanza safari wakiwa na tiketi zao mikononi, hasa kwa wale watakaonunua kupitia maduka ya Fahari Huduma. Tiketi pia zinaweza kununuliwa kupitia mtandao wa M-Pesa kwa kupiga namba *150*03*02#. Kwa wanaotumia CRDB simbanking wanaingia kawaida kwa *150*03. Vilevile tunawakumbusha washabiki kuwa kwa viwanja ambavyo tayari vina mfumo wa tiketi za elektroniki hakuna tiketi zitakazouzwa uwanjani, hivyo wanaokwenda kwenye mechi wanatakiwa kuwa na tiketi zao mikononi.



YANGA YAINGIZA MIL 86/-, SIMBA MIL 53/-
Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zilizohusisha timu za Simba na Yanga na kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wikiendi zimeingiza jumla ya sh. 139,850,000. Yanga iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ashanti United pambano lake liliingiza sh. 86,035,000 kutokana na watazamaji 14,261. Mechi ya Simba ambayo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers kutoka Tabora iliingiza sh. 53,815,00 kwa watazamaji 9,629. Mgawanyo kwa mechi ya Yanga ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 13,123,983.05, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,910,300 wakati kila klabu ilipata sh. 20,650,211.50. Uwanja sh. 10,500,107.54, gharama za mechi sh. 6,300,064.53, Bodi ya Ligi sh. 6,300,064.53, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,150,032.26 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,450,025.09. Mechi ya Simba mgawo ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 8,209,067.80, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,910,300 wakati kila klabu ilipata sh. 12,595,211.50. Uwanja sh. 6,404,344.83, gharama za mechi sh. 3,842,606.90, Bodi ya Ligi sh. 3,842,606.90, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,921,303.45 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,494,347.13. Vilevile tiketi zinapatikana kupitia maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo katika maeneo mbalimbali nchini. Watakaonunua kupitia maduka hayo watapata tiketi na kwenda moja kwa moja uwanjani.

MARADONA AMPONDA PELE.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona ameanza vita vya maneno na Pele kwa kudai kuwa Mbrazil huyo kwa upande wake atabakia mchezaji bora namba mbili. Wawili wamekuwa wakitupiana maneno mara kadhaa kuhusu misimamo yao na Maradona anaonekana hakufurahishwa na Pele kupewa tuzo ya heshima ya Ballon d’Or katika sherehe zilizofanyika jijini Zurich, Switzerland mapema mwezi huu. Maradona ambaye alipewa zawadi kama hiyo katika miaka ya 90 bado anaamini kuwa yeye ndio namba moja na Pele siku zote anamfuata nyuma yake. Maradona aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Argentina aliiongoza nchi hiyo kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka 1986 na pia kushinda mataji ya ligi katika vilabu vya Barcelona ya Hispania, Napoli ya Italia na Boca Juniors ya nyumbani kwao Argentina. Kwa Pele yeye ameweka historia ambayo haijavunjwa na mchezaji yeyote kwa kunyakuwa mataji matatu ya Kombe la Dunia huku akiwa amefunga mabao 1,283 katika mechi 1,363 alizowahi kucheza.

ULIKUWA NI UAMUZI MGUMU KUMUUZA MATA - MOURINHO.

MENEJA wa Chelsea, Jose Mourihno amesema ulikuwa ni uamuzi mgumu kumuachia kiungo wa kimataifa wa Hispania Juan Mata kujiunga na mahasimu wao wa Ligi Kuu Manchester United. Mata mwenye umri wa miaka 25 aliondoka Chelsea na kuhamia United kwa ada iliyovunja rekodi ya klabu hiyo. Mourinho amesema meneja kazi ni kutoa maamuzi kama hayo lakini kwa upande wake ulikuwa ni uamuzi mgumu kwasababu bado alikuwa akipenda kubakiwa na nyota huyo katika kikosi chake. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anapenda kumfurahisha kila lakini ilishindikana kumfurahisha Mata kwasababu alikuwa hampi namba ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

BAINES APEWA MKATABA MPYA EVERTON.

KLABU ya Everton imempa mkataba mpya wa miaka minne beki wake mahiri Leighton Baines ambaye alikuwa akinyemelewa na klabu ya Manchester United. Beki huyo wa kimataifa wa Uingereza alikuwa amebakiza miezi 17 kabla ya mkataba wake kumalizika na kulikuwa na tetesi kuwa kocha United David Moyes alikuwa amemuweka katika rada zake. Kocha wa Everton Roberto Martinez alithibitisha kumuongeza mkataba beki huyo na kudai kuwa ni jambo zuri katika kuimarisha kikosi chao. Baines alijiunga na Everton mwaka 2007 na toka kipindi hicho amekuwa sehemu muhimu katika ukuta wa timu hiyo akiwa amecheza mechi 260 mpaka sasa.

Sunday, January 26, 2014

MESSI HAONDOKI BARCELONA - BABA.

BABA na wakala wa mchezaji nyota wa Barcelona, Lionel Messi kwapamoja wamesisitiza kuwa mshambuliaji huyo hawezi kujiunga na Paris Saint Germain, PSG au klabu nyingine yoyote katika kipindi hiki. Kumekuwa na tetesi kuwa matajiri hao kutoka jiji la Paris walikuwa wamepanga kutenda dau euro milioni 250 litakalovunja rekodi ya dunia kwa ajili ya kumsajili nyota huyo katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi. Hata hivyo baba wa mchezaji huyo Jorge Messi amekana tetesi hizo kwamba PSG wanaweza kumuondoa mwanae Camp Noun a kusisitiza hawezi kwenda popote kwasasa. Jorge amesema amesikia tetesi hizo na hajui zilipotokea na kuwahakikishia mashabiki wa Barcelona kuwa Messi bado ni mchezaji wao kwa miaka kadhaa mpaka hapo mkataba wake utakapomalizika mwaka 2018.




WAWRINKA BINGWA MPYA WA MICHUANO YA WAZI YA AUSTRALIA.

MCHEZAJI nyota wa tenisi Stanislas Wawrinka wa Switzerland amefanikiwa kumsimamisha kinara wa mchezo huo kutoka Hispania Rafael Nadal na kunyakuwa taji lake la kwanza la michuano ya wazi ya Australia katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Rod Laver Arena jijini Melbourne. Katika mchezo huo Wawrinka alitumia vyema udhaifu wa mpinzani Nadal ambaye alionekana kupata maumivu ya mgongo mapema katika mchezo huo na kumfunga kwa seti 3-1 zenye alama za 6-3 6-2 3-6 6-3. Wawrinka mwenye umri wa miaka 28 anakuwa mchezaji wa pili kutoka Switzerland kushinda taji la Grand Slam baada ya Roger Federer kufanya hivyo kwa kushinda mataji 17. Ushindi huo pia utampaisha Wawrinka ambaye kwasasa anashika nafasi ya nane katika orodha za ubora duniani, mpaka nafasi ya tatu katika orodha mpya zitakazotoka kesho akimshusha Andy Murray wa Uingereza aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.

FIFA YAIPA EFA SIKU 10 ZA KUJIELEZA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani, FIFA limekihoji Chama cha Soka nchini Misri, EFA kuhusu tuhuma kutoka katika vilabu vingi nchini humo wakilalamikia serikali kuingilia masuala ya michezo hususani soka. Vilabu vingi kama Al Ahly, Zamalek na El Tram vyote vimelalamika hadharani kuhusu serikali kuingilia mambo ya soka. Hatua hiyo imekuja kufuatia waziri wa michezo wan chi hiyo Taher Abu Zaied kufunja bodi ya ya Zamalek miezi michache iliyopita na kutaka kufanya hivyo tena katika bodi ya Al Ahly wiki iliyopita. FIFA imeitaka EFA kushughulikia tatizo hilo mapema kabla ya Februari 5 mwaka huu jambo ambao maofisa wa shirikisho hilo wameahidi kuzungumza na vilabu ili kutatua tatizo hilo.

MWAMUZI AMEKUWA MKALI SANA DHIDI YA BUFFON - CONTE.

MENEJA wa klabu ya Juventus, Antonio Conte amedai kuwa uamuzi wa kumtoa nje golikipa wa timu hiyo Gianluigi Buffon katika mchezo ulioisha kwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Lazio ulikuwa mkali sana. Buffon ambaye ni nahodha wa Juventus alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha Miroslav Klose wakati akielekea kufunga na kupelekea mwamuzi Davide Massa pia kuwazaiwadia Lazio penati ambayo ilitiwa kimiani na Antonio Candreva. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Conte mwenye umri wa miaka 44, amesema ni jambo la kusononesha kuwepo kwa sheria kama hiyo kwasababu anadhani penati pekee inatosha bila kuongeza na kadi nyekundu. Pamoja na kuhuzunishwa huko, Conte aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma na kuhakikisha wanaondoka na walau alama moja baada ya kusawazisha bao huku wakiwa wanacheza pungufu.

KUNA UWEZEKANO FALCAO KUWEPO KOMBE LA DUNIA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Colombia, Radamel Falcao hivi sasa anakimbizana na muda kwa kuwa fiti kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Juni mwaka huu nchini Brazil baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti jana. Madaktari waliomfanyia upasuaji mchezaji huyo wamempa zaidi ya asilimia 50 kwa 50 kwamba anaweza kupona kwa wakati na kushiriki michuano hiyo. Rais wa Colombia Juan Manuel Santos alimtembelea nyota huyo katika hospitali ya Trindade iliyopo jijini Porto Ureno wakati akitoka katika mkutano wa masuala ya kiuchumi uliokuwa ukifanyika huko Davos, Switzerland. Mara baada ya kumuona Santos amesema amemkuta nyota huyo katika hali nzuri na kuna mategemeo mazuri ya kupona kwa wakati kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia. Rais huyo aliongeza kuwa Colombia ina wachezaji wengi wazuri na kikosi imara lakini Falcao amekuwa alama ya timu ya taifa ya nchi hiyo. Nyota huyo anatarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitalini Jumatatu na kuendelea na matibabu yake jijini Monaco, Ufaransa.

RAMSEY NDIO MCHEZAJI KATIKA LIGI KUU UINGEREZA - VIEIRA.

NGULI wa zamani wa soka wa Ufaransa, Patrick Vieira anaamini kuwa kiungo wa Arsenal Aaron Ramsey ndio mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 amefunga mabao 13 katika mechi 27 alizocheza na kukisaidia kikosi cha Arsenal kinachonolewa na Arsene Wenger kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo. Ramsey haakuwemo katika kikosi cha Arsenal toka kipindi cha Boxing Day mwaka jana kutokana na maumivu ya msuli lakini Vieira amesema nyota huyo wa kimataifa wa Wales amekuwa sehemu muhimu ya timu hiyo katika kampeni zao msimu huu. Akihojiwa Vieira amesema toka kuanza kwa msimu Ramsey amekuwa katika kiwango kizuri kwasababu ya mabao aliyofunga akitokea katikati lakini pia mabao kadhaa aliyotengenezea wenzake. Vieira ambaye kwasasa na mwalimu wa timu za vijana za Manchester City, pia alimpongeza Wenger kwa kuwapa nafasi chipukizi na kuamini kuwa wanaweza.

Saturday, January 25, 2014

UNITED YAIWEKEA SOUTHAMPTON PAUNDI MILIONI 20 MEZANI KWA AJILI YA KINDA WAO SHAW.

KLABU ya Manchester United inatarajiwa kutaka kutumia kitita cha paundi milioni 23 kumsajili beki wa kushoto kutoka Southampton, Luke Shaw baada ya kukamilisha usajili wa Juan Mata kutoka Chelsea uliogharimu paundi milioni 37. United inatarajia kupeleka fedha hizo wikiendi hii ili kujaribu kuipiga bao Chelsea ambao nao wako mbioni kuwania saini ya kinda huyo wa miaka 18. Usajili wa Mata unatarajiwa kuvunja rekodi ya mchezaji ghali kusajiliwa na United, ukipiku usajili wa paundi milioni 30.75 zilizotolewa kumsajili Dimitar Berbatov mwaka 2008. Lakini Moyes ameonyesha bado ana kiu ya kusajili wachezaji zaidi kabla dirisha dogo la usajili halijafungwa Januari 31 ili kuimarisha kikosi chake ambacho kimeonekana kusuasua toka kuanza kwa msimu.

NIMESHAIVA VYA KUTOSHA KWA NAFASI YA KOCHA MKUU.

NGULI wa soka wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane amesema yuko tayari kuwa kocha mkuu baada ya kufanya kazi kama kocha msaidizi wa Carlo Ancelotti katika klabu ya Real Madrid. Zidane ambaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa michezo wa Madrid mwaka 2011, amechagua kuwa msaidizi wa Ancelotti baada ya Muitaliano huyo kutua klabu hapo kuziba pengo la Jose Mourinho aliyetimuliwa katika kipindi cha kiangazi. Kufuatia kupita miezi sita ya kwanza akiwa chiini ya Ancelotti, Zidane amesisitiza kuwa sasa anadhani yuko tayari kujaribu nafasi yake kama kocha mkuu na kuahidi kukitengeneza kikosi chake kuwa chenye kufanya mashambulizi. Zidane amesema ana hamu kubwa ya kupewa nafasi kamili ya ukocha kwasababu anajiona ana mambo mengi yanayoweza kunufaisha timu yoyote itakayomuhitaji. Zidane ambaye ameshinda mataji manane akiwa mchezaji wa Madrid, pia aliwashukuru Ancelotti na rais wa klabu hiyo Florentino Perez kwa kumsaidia katika kipindi chote ambacho amekuwa hapo.

LI NA BINGWA MPYA WA AUSTRALIA OPEN KWA WANAWAKE.

HATIMAYE mwanadada nyota wa tenisi kutoka China, Li Na ametawadhwa kuwa bingwa mpya wa michuano ya wazi ya Australia kwa wanawake baada ya kumfunga Dominika Cibulkova wa Slovakia katika mchezo wa fainali uliofanyika Katika uwanja wa Rod Laver Arena jijini Melbourne. Li Na ambaye amelikosa taji hilo mara mbili baada ya kufungwa na Kim Cylister katika fainali za mwaka 2011 na Victoria Azarenka mwaka jana, alifanikiwa kunyakuwa taji hilo kwa kumfunga Cibulkova kwa seti mbili bila majibu zenye alama za 7-6 6-0. Akiwa na Umri wa miaka 31, Li Na anakuwa mwanamke mwenye umri mkubwa kushinda taji hilo akivunja rekodi ya Margaret Court ambaye alishinda taji hilo mwaka 1973 akiwa na umri wa miaka 30. Kesho kutakuwa na mchezo mwingine wa fainali ya michuano kwa upande wa wanaume ambapo kinara Rafael Nadal wa Hispania atachuana na Stanislas Wawrinka wa Switzerland.


Friday, January 24, 2014

FERGUSON AULA UEFA.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA Michel Platini amesema shirikisho hilo limeteua kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson kuwa balozi wa makocha. Ferguson mwenye umri wa miaka 72 ameweka rekodi ya kudumu Old Traford kwa miaka 26 kabla ya kuamua kustaafu msimu uliopita baada ya kushinda mataji 13 ya Ligi Kuu akiwa na klabu hiyo. Akizungumza mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji jijini Nyon, Switzerland, Platini amesema Ferguson atakuwa mwenyekiti wa kongamano la makocha linafanyika kila mwaka na pia atakuwa mjumbe wa kamati ya ufundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani humo pamoja na Europa League. Akihojiwa kuhusiana na uteuzi huo Ferguson amesema ni heshima kubwa kwake na anakubaliana na uteuzi huo wa kuwa balozi wa UEFA.

CAPELLO KUBAKIA URUSI MPAKA 2018.

KOCHA wa timu ya taifa ya Urusi, Fabio Capello amefikia makubaliano ya kuongeza mkataba na nchi hiyo mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2018. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 alichukua nafasi ya Dick Advocaat Julai mwaka 2012 na kuisaidia nchi hiyo kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil akiwa amepoteza mechi mbili pekee katika kundi F la timu za Ulaya walilokuwepo. Mkataba wa sasa Capello ulikuwa umalizike baada ya michuano hiyo ya mwaka huu lakini ameongezewa mkataba mwingine mpya ambao utafikia tamati baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2018 ambayo Urusi itakuwa mwenyeji. Akihojiwa Capello amesema anamshukuru rais wa Umoja wa Soka wan chi hiyo, RFU pamoja na waziri husika wa michezo, Vitaly Mutko kwa kumuamini na kudai kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha anawapa furaha mashabiki wa Urusi. Urusi imepangwa katika kundi H sambamba na timu za Ubelgiji, Algeria na Korea Kusini.

AUSTRALIA OPEN 2014 FAINAL: MEN: NADAL VS WAWRINKA, WOMEN: LI NA VS CIBULKOVA

MCHEZAJI nyota wa tenisi anayeshika namba moja katika orodha za ubora kwa upande wa wanaume, Rafael Nadal amefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya wazi ya Australia baada ya kumgaragaza Roger Federer wa Switzerland. Nadal ambaye ni raia wa Hispania alifanikiwa kumchakaza mkongwe huyo kwa seti tatu bila majibu zenye alama za 7-6 6-3 6-3 na kutinga hatua hiyo ambapo sasa atakwaana na Stanislav Wawrinka. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa hilo katika fainali itakayochezwa Jumapili hii na kama akifanikiwa atakuwa mchezaji wa tatu kushinda kila taji Grand Slam mara mbili. Mbali na wanaume kwa upande wa wanawake pia kutakuwa na mchezo wa fainali utakaochezwa kesho ambapo mwanadada nyota kutoka China Li Na atachuana vikali na Dominika Cibulkova wa Slovakia. Li Na atakuwa na mategemeo makubwa ya kunyakuwa taji hilo safari hii baada ya kulikosa katika fainali mbili mfululizo zilizopita katika michuano hiyo.

SAKATA LA OKWI: NANI MKWELI TFF AU YANGA?

WINGU zito bado limeendelea kutanda kuhusiana na sakata la mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uganda Emmanuel Okwi baada ya Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini, TFF kumsimamisha.

Kamati hiyo iliyokutaka hivi karibuni ilimsimamisha mchezaji huyo ambaye ana kesi tatu katika Shirikisho la Soka Duniani, FIFA ili kupata uthibitisho wa uhalali wake baada ya kugundulika kuwa alikuwa amepewa kibali cha muda kuichezea klabu ya Villa kulinda kiwango chake wakati kesi yake ikiendelea.

Hatua hiyo ilizusha taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini hususani wapenzi wa Yanga wakiuliza kulikoni huku kukiwa na maswali mengi kuliko majibu katika sakata hilo.

Kutokana na hatua hiyo Yanga nao wameamua kufunguka na kueleza kinagaubaga jinsi walivyomsajili nyota huyo huku wakitoa vielelezo kadhaa kuonyesha uhalali wake wa kuwepo pande za Jangwani.

Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto kwa niaba ya uongozi wa timu hiyo aliweka bayani hatua zote walizopitia mpaka kuhakikisha wanampata nyota huyo ambaye kabla ya kutua Jangwani alikuwa kwa watani woa wa jadi Simba.

Kizuguto amesema “Young Africans ilikamlisha usajili wa mshambuliaji huyo tangu Disemba 15 mwaka 2013, na kupata hati ya uhamisho wake wa kimataifa (ITC) ambayo iliwasilishwa TFF pamoja na fomu mama za usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo TFF ilipitisha jina lake kwa kutupatia leseni no: 921225001 ambayo inamruhusu mchezaji kuichezea Young Africans na kisha kulituma CAF Disemba 31, 2013 kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika ambapo CAF nao walimuidhinisha kuwa mchezaji halali wa Young Africans kwa mashindano hayo.

Cha kustaajabisha siku mbili kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Kamati ya Maadili na hadhi za wachezaji wakamzuia mchezaji huyo kuichezea Young Africans ilihali akiwa ameshaidhinishwa na TFF na CAF kuwa mchezaji halali wa Young Africans.

Swali?? walikuwa wapi Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji kujiridhisha juu ya usajili ambao ulishakamilika tangu Disemba 15 2013?

Wanakuja kutoa maamuzi hayo mwezi mmoja na nusu baada ya dirisha la usajili kufungwa, ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom??”

Kutokana na hoja za pande zote mbili utakubaliana name kuwa kumekuwa na maswali mengi kuliko majibu kuhusiana na suala hilo, NANI MKWELI KATIKA HILI TFF AU YANGA?


MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU KUANZA KUTIMUA VUMBI.

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom-VPL kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza rasmi kesho kwa mechi nne zitakazochezwa katika miji ya Bukoba, Dar es Salaam na Tanga. Mabingwa watetezi Yanga watakuwa wageni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Azam FC na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro. Coastal Union itaikaribisha Oljoro JKT ya Arusha kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Kagera Sugar ikiikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Raundi ya 14 ya ligi hiyo itaendelea Jumapili Januari 26 kwa mechi mbili ambapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa shuhuda wa mechi kati ya Simba na Rhino Rangers kutoka Tabora wakati maafande wa JKT Ruvu na Mgambo Shooting watapambana Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam. Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini, TFF amesema viwanja vyote ambavyo tayari vimefungwa mfumo wa elektroniki vitatumia tiketi za elektroniki isipokuwa ywanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao wenyewe utachelewa kidogo ili kuangalia mfumo huo unavyofanya kazi katika viwanja vingine.


SUPER EAGLES KUWEKA KAMBI HOUSTON, TEXAS KWA AJILI YA KOMBE LA DUNIA.

MABINGWA wa Afrika, timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles wanatarajiwa kuweka kambi yao jijini Houston, Texas, Marekani kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya Kombe la Dunia litakalifanyika baadae mwaka huu nchini Brazil. Kocha wa Nigeria Stephen Keshi alikuwa amependekeza kikosi chake kuweka kambi yao ya mazoezi kati ya Miami au Houston lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Soka nchini humo, Chris Green amesema wameamua kuchagua mji huo. Green amesema wamechagua mji huo kwasababu wanataka kufanya vyema katika michuano hiyo ambayo wanashiriki kwa mara ya tano hivyo wanapaswa kujiandaa vyema. Nigeria ambao wanatarajia kuanza kambi yao rasmi Mei 25 mwaka huu, wamefanikiwa kutinga hatua ya timu 16 bora katika michuano hiyo mara mbili mwaka 1994 na 1998. Green pia amesema timu hiyo imepanga kucheza mechi nne za kirafiki kabla ya mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Iran utakaochezwa Juni 16.

HATMA YA KESI YA UZINZI YA KINA RIBERY NA BENZEMA KUJULIKANA ALHAMISI IJAYO.

WASHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Franck Ribery na Karim Benzema watarajia kujua hatma yao kama wameshinda kesi yao ya kumnunua mwanamke anayejiuza aliyekuwa chini umri Alhamisi ijayo baada ya mahakama ya jiji la Paris kuahirisha kesi hiyo kwa maamuzi zaidi. Mwendesha mashitaka Jean-ulien Xavier-Rolai aliomba wanasoka hao kuachiwa kutokana na kesi hiyo inayowakabili. Xavier-Rolai amesema ni suala lisilowezekana kupatikana kwa ushahidi kwamba Ribery alikuwa akijua mwanamke huyo aitwaye Zahia Dehar ambaye hivi sasa amekuwa mwanamitindo kuwa alikuwa chini ya umri wa miaka 18 kabla ya kuongeza kuwa Benzema pia anapaswa kuachiwa. Wachezaji hao ambao hawakuwepo mahakani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo uliochukua siku nne wanatuhumiwa kwa kulipia huduma ya kingono kwa nyakati tofauti kwa Dehar wakati alipokuwa na miaka 16 na 17. Ribery alikiri kilipia huduma hiyo lakini alidai kuwa hakuwa akijua umri halisi wa Dehar wakati Benzema yeye alikana shitaka hilo na kudai hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamitindo huyo. Kulipia huduma ya kingono sio kosa nchini Ufaransa lakini kama anayejiuza akiwa chini ya umri ni kosa.

NIMEJIUZULU KWASABABU YA USALAMA WA FAMILIA YANGU - ROSELL.

RAIS wa klabu ya Barcelona, Sandro Rosell ametangaza kujiuzulu rasmi wadhifa wake akidai kutishiwa maisha yeye pamoja na familia yake. Hatua hiyo ya Rosell imekuja wakati yeye na Barcelona wakiwa katika uchunguzi wa Mahakama Kuu ya Hispania kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za uhamisho wa Neymar kutoka Santos katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi mwaka jana. Rosell amesema kwa kipindi kirefu sasa familia yake pamoja naye wamekuwa wakiandamwa na vitisho vya kushambuliwa hatua ambayo ilimfanya kufikiria kama anaiweka familia yake katika hatari kwa kuendelea kuwa rais wa Barcelona. Tajiri huyo aliendelea kudai kuwa anadhani familia yake itafurahia uamuzi wake huo kwani umekuwa mjadala wa kipindi kirefu na baada ya kufikiria kwa makini. Nafasi ya Rosell sasa itashikiliwa na makamu wake Josep Maria Bartomeu mpaka hapo utakapoitishwa uchaguzi mwingine.

HAKUNA KINACHISHINDAKANA MBELE ZA MUNGU - FALCAO.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Monaco ya Ufaransa, Radamel Falcao bado hajakata tamaa kuwepo katika michuano ya Kombe la Dunia baadae mwaka huu pamoja na kuumia vibaya goti lake. Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia alibebwa na machela kutolewa uwanjani katika mchezo wa Kombe la Ligi nchini Ufaransa ambapo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Monts d’Or Azergues Jumatano. Klabu hiyo ilithibitisha kuwa nyota huyo aliyevunja rekodiya usajili atafanyiwa upasuaji baada ya vipimo kuonyesha ameumua kwa ndani kwenye goti lake la kushoto. Matumaini ya nyota huyo kucheza michuano ya Kombe la Dunia itakayoanza Juni 12 mwaka huu yanaonekana kutoweka lakini mwenyewe bado hajakata tamaa akidai kuwa anaweza kupona kwa wakati na kushiriki. Falcao amesema akiwajibu mashabiki wake waliokuwa wakimtumia ujumbe wa pole katika mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa mungu anaweza kufanya visivyowezekana vikawezekana nay eye anamuamini.

Thursday, January 23, 2014

MADRID YAENDELEZA REKODI YAO YA KUWA KLABU INAYOINGIZA MAPATO MENGI ZAIDI.

KLABU ya Real Madrid imetajwa kuwa klabu iliyoingiza mapato mengi zaidi katika msimu wa 2012-2013 na kuongeza rekodi yao ya kushikilia nafasi hiyo kwa misimu tisa mfululizo. Kwa mujibu wa takwimu hizo zinazotolewa na Deloitte Football Money League klabu hiyo ya Hispania imeingiza kiasi cha euro milioni 518.9 na kuwazidi mahasimu wao Barcelona kwa euro milioni 36.3. Klabu ya Manchester United ambayo imewahi kuongoza katika orodha hiyo msimu wa 1996-1997 na 2003-2004 imedondoka katika nafasi tatu za juu kwa mara ya kwanza na nafasi yao kuchukuliwa na mabingwa wa ulaya Bayern Munich ambao wamewazidi United kwa euro milioni 7.4. Klabu ya Paris Saint-Germain,PSG ya Ufaransa imekwea mpaka nafasi ya tano katika orodha hizo kutoka nafasi ya 10 waliyokuwepo baada ya kufanikiwa kuongeza mapato yao kwa asilimia 81. Orodha kamili ya vilabu 10 vinavyoingiza mapato zaidi nia kama ifuatayo, Madrid euro milioni 518.9, Barcelona euro milioni 482.6, Bayern Munich euro milioni 431.2, Manchester United euro milioni 423.8, PSG euro milioni 398.8, Manchester City euro milioni 316.2. Nyingine ni Chelsea euro milioni 303.4, Arsenal euro milioni 284.3, Juventus euro milioni 272.4 na AC Milan ndio wanafunga orodha ya kumi bora wakiingiza mapato yanayofikia euro milioni 263.5.

TULISTAHILI KUCHAPWA NA SUNDERLAND - MOYES.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes amedai kuwa kikosi chake kilistahili kuenguliwa katika michuano ya Kombe la Ligi na Sunderland jana. Baada ya kushinda mchezo wa nusu fainali ya mkondo wa pili katika Uwanja wa Old Traford timu zililazimika kucheza muda wa nyongeza na baadaye changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kutoka sare kwa mabao 3-3 katika michezo ya mikondo miwili waliyokutana. Katika changamoto ya mikwaju ya penati United walikosa mikwaju minne na kupelekea kutolewa katika michuano hiyo ambapo sasa majirani zao Manchester City watakwaana Sungerland katika mchezo wa fainali utakaochezwa katika Uwanja wa Wembley Machi 12 mwaka huu. Akihojiwa Moyes amesema kikosi chake hakucheza vizuri kustahili kusonga mbele na kuwapongeza Sunderland kuwa walistahili kusonga mbele kutokana na juhudi walizoonyesha.

MAN UNITED YAMNASA MATA.

KLABU ya Chelsea imekubali ofa ya paundi milioni 37 kwa ajili kumuuza kiungo wao nyota wa kimataifa wa Hispania, Juan Mata kwa klabu ya Manchester United. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 amefanyiwa vipimo vya afya leo kabla ya kukamilisha uhamisho wake. Mata anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne na nusu kuitumikia United. Nyota huyo aliaga wachezaji wenzake na viongozi wa Chelsea katika mazoezi ya timu hiyo huko Cobham jana.

AUSTRALIA OPEN 2014: LI NA, CIBULKOVA KUKWAANA FAINALI.

MWANADADA nyota katika tenisi kutoka China, Li Na amefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya wazi ya Australia baada ya kufanikiwa kumchapa chipukizi Euginie Bouchard katika mchezo wa nusu fainali. Li ambaye amepoteza michezo yake yote mitatu ya fainali katika michuano hiyo alifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumgaragaza Bourchard wa Canada kwa 6-2 6-4. Mwanadada huyo sasa atakwaana na Dominika Cibulkova wa Canada baada ya nyota huyo kumuondosha Agnieszka Radwanska kwa 6-1 6-2 katika nusu fainali nyingine iliyofabyika katika uwanja wa Rod Laver Arena. Wakati nyota watatu wanashika nafasi za juu katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake, Serena Williams, aliyekuwa bingwa mtetezi Victoria Azarenka na maria Sharapova wakiwa wametolewa hiyo itakuwa ni nafasi pekee kwa Li Na kunyakuwa taji hilo katika mchezo wa fainali Ijumaa baada ya kulisotea kwa miaka mitatu mfululizo.


KAMWAGA AUKWAA UKATIBU SIMBA, ASHA MUHAJI OFISA HABARI MPYA.


KLABU ya Soka ya Simba imefanya mabadiliko ya sekretarieti yake pamoja na kutangaza tarehe ya kufanya Mkutano Mkuu maalumu. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Aden Rage amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kufanyika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji. Rage amesema nafasi ya Katibu Mkuu wa klabu sasa itashikiliwa na aliyekuwa ofisa habari wake Ezekiel Kamwaga akisaidiwa na Stanley Philipo, nafasi ya muhasibu ikibakia kwa Eric Sekiete akisaidiwa na Amina Kimwambi. Nafasi ya ofisa habari sasa itashikiliwa na Asha Muhaji huku meneja wa timu akiwa Hussein Mbozi na Issa Mathayo atakuwa msimamizi. Rage pia amesema katika kikao hicho wamepanga Machi 23 mwaka huu kuwa tarehe ya Mkutano Mkuu Maalumu ambao utakuwa na ajenda moja ya kuhusu mabadiliko ya katiba. Wakati huohuo Rage amesema wamepokea barua kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Kamati ya Hadhi za Wachezaji wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA ambayo inawataka klabu ya Etoul du Sahel hadi Januari 27 mwaka huu wawe wametoa maelezo kuhusiana na hela ya mshambuliaji Emmanuel Okwi.

Wednesday, January 22, 2014

USAJILI WA OKWI YANGA WAZUIWA.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesimamisha usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika timu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana leo (Januari 22 mwaka huu) kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA. Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa. Katika FIFA kuna kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000. Hivyo, TFF imeiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.



AUSTRALIA OPEN 2014: BINGWA MTETEZI AZARENKA OUT.

BINGWA mtetezi wa michuano ya wazi ya Australia, mwanadada Victoria Azarenka ameng’olewa katika michuano hiyo baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Agnieszka Radwanska katika mchezo wa robo fainali. Katika mchezo huo Azarenka anayeshika nafasi ya pili katika orodha za ubora wa mchezo huo kwa upande wa wanawake alishindwa kutamba mbele ya Radwanska anayeshika nafasi ya tano kwa kufungwa seti 2-1 zenye alama za 6-1 5-7 6-0. Kipigo hicho kinamaliza ubabe wa Azarenka kushinda mechi 18 katika viwanja vya jiji la Melbourne kuanzia mwaka 2012 na kumaanisha kuondolewa kwa nyota wote wanaoshika nafasi ya tatu za juu baada ya Serena Williams na Maria Sharapova kuondolewa mapema. Radwanska sasa atakwaana na Dominika Cibulkova katika mchezo wa nusu fainali baada ya mwanadada huyo kumuondosha Simona Halep katika mchezo war obo fainali.

BINGWA CHAN KUNYAKUWA KITITA CHA DOLA 746,463.

PAMOJA na kuenguliwa katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani,CHAN katika hatua ya makundi, timu ya taifa ya Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana haikutoka mikono mitupu baada ya kukabidhiwa kitita cha dola 175,000 kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lao. Kamati ya Maandalizi ya michuano hiyo imedai kuwa jumla ya fedha zote za zawadi inafikia kiasi cha dola milioni tatu. Bingwa wa michuano hiyo atanyakuwa kitita cha dola 746,463 na mshindi wa pili atachukua kiasi cha 396,270 huku wa tatu na wanne wote wakichukua dola 248,821 kila mmoja. Timu ambazo zitakwamia katika hatua ya robo fainali zitachukua 175,096 huku zile ambazo zimeshika mkia katika kwenye makundi yao zikiambulia dola 92,156 kila moja. Michuano hiyo inayoendelea nchini Afrika Kusini inatarajiwa kufikia tamati yake Februari mosi mwaka huu.

MIDO ATEULIWA KUINOA ZAMALEK.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa AS Roma ya Italia na Ajax Amsterdam ya Uholanzi, Mido ameteuliwa kuwa kocha mpya wa klabu yake ya nyumbani ya Zamalek. Mido anachukua mikoba ya kocha Helmi Toulan ambaye alitimuliwa kufuatia sare ya bao 1-1 iliyopata Zamalek dhidi ya Haras El-Hodood katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Misri. Hiyo inakuwa mechi ya nne kwa Zamalek msimu huu ambapo klabu hiyo inashika nafasi ya nne baada ya kushinda mechi mbili kutoa sare moja na kufungwa moja. Mido ambaye anafikisha umri wa miaka 31 Februari mwaka huu anakuwa kocha mdogo zaidi katika historia ya soka nchini hiyo na hana uzoefu wa kutosha wa kufundisha. Nyota huyo ambaye alianza kusakata kabumbu Zamalek mwaka 1999 kabla ya kwenda kucheza Ulaya ameifungia timu ya taifa ya nchi hiyo mabao 19 katika mechi 51 alizocheza.

MAN UNITED MBIONI KUMSAJILI JUAN MATA.

KLABU ya Manchester United ina uhakika wa kumnyakua kiungo Juan Mata kutoka Chelsea kwa ada ya paundi milioni 37 mwishoni mwa wiki hii. Mazungumzo kuhusiana na uhamisho wa kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 25 yamefikia pazuri hivyo kuna uwezekano akafanyiwa vipimo vya afya kabla ya mwishoni mwa wiki. Mata amekuwa akitaka kuondoka Chelsea baada ya kushindwa kumshawishi kocha Jose Mourinho msimu huu. United ambao kwasasa wako katika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu wako katika changamoto kubwa ya kifedha kama wakishindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

NEGREDO KUFANYIWA VIPIMO VYA BEGA LAKE.

KLABU ya Manchester City, inatarajiwa kumfanyia vipimo Alvaro Negredo baada ya mshambuliaji huyo kuumia bega lake katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya West Ham United. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alianguka vibaya mwishoni baada ya kufunga mabao mawili na kuisadia City kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo wa mkondo wa pili. Kocha wa City Manuel Pellegrini alikiri kuwa nyota huyo kuwa katika maumivu makali lakini inabidi wasubiri ili kujua ameumia kiasi gani baada ya kufanyiwa vipimo. Pellegrini pia aliwasifu wachezaji wake kwa kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa kishindo baada ya kuingamiza West Ham kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi za mikondo miwili walizokutana.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

MZUNGUKO WA VPL KUANZA JUMAMOSI
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza Jumamosi (Januari 26 mwaka huu) kwa mechi tano katika miji ya Bukoba, Dar es Salaam, Tanga wakati mechi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting inahamishiwa uwanja mwingine. Ashanti United itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Coastal Union itacheza na Oljoro JKT katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar. Jumapili (Januari 26 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu na Mgambo Shooting itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex wakati Simba na Rhino Rangers zitaumana kwenye Uwanja wa Taifa. Mechi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine inahamishiwa uwanja mwingine kwa vile huo bado nyazi zake ambazo zimepangwa hivi karibuni hazijawa tayari kuhimili mechi hiyo. Hivyo Tanzania Prisons inatakiwa kutafuta uwanja mwingine unaokidhi viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya mechi hiyo, na nyingine dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Januari 29 mwaka huu. Pia matumizi ya tiketi za elektroniki yanaanza katika mzunguko huu kwa vile viwanja nane ambavyo tayari vimefungwa vifaa vya tiketi hizo. Vilevile tunakumbusha washabiki wa mpira wa miguu kuwa tiketi za elektroniki haziuzwi viwanjani.



TWIGA STARS KUIVAA ZAMBIA FEB 15 LUSAKA
Tanzania (Twiga Stars) itaivaa Zambia katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano ya mchujo ya Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayofanyika Februari 15 mwaka huu jijini Lusaka. Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Nkoloma kuanzia saa 9 kamili kwa saa za Zambia na itachezeshwa na mwamuzi Salma Mukansanga kutoka Rwanda. Mukansanga atasaidiwa na Wanyarwanda wenzake; Francine Ingabire, Sandrine Murangwa na Angelique Tuyishime. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Jackey Gertse kutoka Namibia.



KISHONGOLE, KESSY KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shrikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua Watanzania Alfred Rwiza Kishongole na Lina Kessy kuwa makamishna wa mechi za shirikisho hilo zitakazochezwa wikiendi ya Februari 14 mwaka huu. Kishongole ameteuliwa kusimamia mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Cote d’Or ya Shelisheli na Kabuscorp de Palanca ya Angola. Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mchujo itafanyika Shelisheli na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Abdoul Ohabee Kanoso. Waamuzi wengine ni Basile Alain Rambeloson, Augustin Gabriel Herinirina na Andofetra Avombitana Rakotojaona. Naye Kessy atakuwa kamishna wa mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Rwanda na Kenya itakayochezwa jijini Kigali. Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Cameroon. Mwamuzi wa kati ni Sylvie Abou wakati wasaidizi wake ni Winnie li Koudangbe, Lum Rochelle na Jeanne Ekoumou.

Tuesday, January 21, 2014

MALINZI AELEZEA MIKAKATI YAKE KWA LOWASSA.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kushoto) akizungumza na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambapo alimwelezea mikakati ya shirikisho lake katika kuinua kiwango cha mpira wa miguu Tanzania. Mkutano huo umefanyika ofisini kwa Lowassa jijini Dar es Salaam.
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema shirikisho lake limepanga malengo ya muda mfupi na mrefu ikiwa na sehemu ya mkakati wa kuendeleza na kuinua kiwango cha mchezo huo nchini. Malinzi ameeleza mikakati hiyo ya uongozi wake leo (Januari 20 mwaka huu) wakati alipomtembelea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Amesema uongozi wake umepanga malengo hayo ikiwemo kuandaa mashindano maalumu ya kutafuta vipaji mikoani ili kuondokana na mtindo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kuundwa na wachezaji kutoka katika klabu chache tu. Kwa upande wake Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli ameelezea matumaini yake kwa uongozi mpya wa TFF katika kuunga mkono juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kuimarisha na kuinyayua Tanzania katika ramani ya mpira wa miguu duniani.

CHAN 2014: UGANDA YAFUNGISHWA VIRAGO NA MOROCCO.

WAWAKILISHI pekee wa Afrika Mashariki katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani,CHAN timu ya taifa ya Uganda wameaga michuano hiyo baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Morocco katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Cape Town. Uganda walienguliwa kwa kufungwa mabao 3-1 na Morocco katika mchezo mkali wa kundi B ambao kama wangefanikiwa kushinda wangeweza kutinga robo fainali ya michuano hiyo. Katika mchezo mwingine w kundi hilo Burkina Faso nao walifungashwa virago kwa kutandikwa na Zimbabwe kwa bao 1-0. Michuano hiyo inaendelea tena leo ambapo Ethiopia ambao wameshatolewa katika michuano watakamilisha ratiba kwa kuchuana na Ghana katika Uwanja wa Free State, Mangaung huku Congo wakichuana na Libya katika Uwanja wa Peter Mokaba huko Polokwane.

BARCELONA KUUKARABATI UWANJA WA CAMP NOU KWA EURO MILIONI 600.

KLABU ya Barcelona imewasilisha mpango wa matengenezo ya Uwanja wa Camp Nou ambao utagharimu kiasi cha euro milioni 600 na kuwa na uwezo wa kuongeza mashabiki kufika 105,000. Mara ya kwanza Barcelona walikuwa wamefikiria kujenga uwanja mpya katika na eneo la Avenida Diagonal ambalo ni kituo kikubwa cha biashara katika jiji hilo lakini mpango huo ulikwama kutokana na gharama kubwa inayokadiriwa kufikia euro bilioni 1.2. Badala yake mabingwa hao watetezi wa La Liga wameamua kutumia nusu ya fedha hizo kuuukarabati uwanjani wa sasa ambapo utahusisha pia ujenzi wa paa kufunika uwanja huo. Rais wa Barcelona, Sandro Rosell amesema umekuwa uamuzi mgumu kutokana na mipango yote miwili kuvutia lakini wameamua kubakia hapo kwasababu ni sehemu ya historia ya klabu hiyo.