Friday, April 29, 2016

KLOPP AIONYA VILLARREAL.



MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp ameionya Villarreal kuwa watakuwa tayari kwa ajili yao wakati watakapokutana tena katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Europa League katika Uwanja wa Anfield wiki ijayo. Liverpool walitandikwa bao 1-0 na Villarreal katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika jana baada ya Adrian kupata bao hilo pekee dakika ya 90 katika Uwanja wa El Madrigal. Akihojiwa Klopp amesema hiyo ilikuwa hatua ya kwanza na bahati mbaya wameteleza lakini hana shaka kuwa watakuwa tayari kukabiliana na wapinzani wao hao wiki ijayo. Klopp aliendelea kudai kuwa kwasasa wanakwenda kufanyia kazi baadhi ya vitu ili watakapokutana katika mchezo ujao wawe wameimarika zaidi.

Thursday, April 28, 2016

MAN UNITED KUPIGA UZI MWEUPE FAINALI YA FA.


KLABU ya Manchester United imepangwa kuwa timu ya ugenini katika mchezo wa fainali wa Kombe la FA dhidi ya Crystal Palace hivyo kumaanisha kuwa watavaa fula zao nyeupe, kaptura nyeusi na soksi nyeupe Katika Uwanja wa Wembley Mei 21 mwaka huu. Palace wao watakuwa kama wenyeji wa fainali hiyo baada ya kurushwa shilingi hivyo watavaa jezi zao zilizoeleka za nyekundu na bluu. Fulana za fainali ya mwaka huu zitarudisha kumbukumbu ya klabu hizo mbili mara ya mwisho zilizpokutana katika fainali ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Wembley mwaka 1990 wakati United walivyovaa nyeupe dhidi ya rangi zilizoeleka za Palace. Fainali ya mwaka 1990 timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 baada ya muda wa nyongeza kabla ya kurudiana tena katika uwanja huohuo na United kushinda kwa bao 1-0.

OZIL AAMUA KUIHENYESHA ARSENAL.

KIUNGO wa Arsenal, Mesut Ozil amesema hana haraka ya kusaini mkataba mpya na anaweza kusubiri mpaka mwishoni mwa msimu kwa ajili ya mzungumzo na klabu. Ozil na Alexis Sanchez wote wamebakisha mikataba ya miaka miwili huku Arsenal wakiwa tayari kuwapa mikataba mirefu zaidi kipindi cha kiangazi. Lakini Ozil, ambaye tayari amevunja rekodi ya Ligi Kuu kwa kutoa pasi nyingi za kusaidia kwa msimu mmoja, alikaririwa katika mahojiano na redio moja nchini Ujerumani akidai kuwa hana haraka yeyote kusaini mkataba mpya. Ozil amesema bado ana mkataba wa miaka miwili hivyo ataona itavyokuwa pindi msimu utakapomalizika.

DEL PIERO ATIA BARAKA ZAKE LEICESTER WACHUKUE UBINGWA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Italia, Alessandro Del Piero ana matumaini Leicester City watatwaa taji la Ligi Kuu ili kuonyesha hakuna kinachoshindikana katika ulimwengu wa michezo. Leicester ambao wanadaiwa alama tatu pekee ili watwae taji hilo kwa mara ya kwanza, wanaongoza ligi kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Tottenham Hotspurs wanaoshika nafasi ya pili. Msimu huu umekuwa wa kipekee kwao haswa kutokana na jinsi walivyohaha miezi 12 iliyopita wasishuke daraja. Ushujaa huo ulioonyeshwa na Leicester umewapelekea kujizolea mashabiki kutoka pmbe zote za dunia akiwa nguli wa Juventus Del Piero ambaye amewahi kucheza chini ya Claudio Ranieri wakati akiwa Turin. Del Piero amesema anependa Leicester watwae taji hilo kwasababu litakuwa jambo ambalo unaweza kuwaambia wajukuu kuwa hakuna kinachoshindikana katika michezo.

PSG YAMTIA KITANZI CHIPUKIZI WA UFARANSA.

CHIPUKIZI wa kimataifa wa Ufaransa, Odsonne Edouardo amesaini mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa na mabingwa wa Ligue 1 Paris Saint-Germain jana. Edouard alionyesha kiwnago kizuri katika michuano Ligi ya Vijana ya UEFA, akifunga mabao matatu na kusaidia mengine matatu katika mechi nane alizocheza na kufanya Laurent Blanc kumjumuisha katika kikosi chake kitakachopiga kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao. Chipukizi huyo pia alionyesha kiwango bora katika michuano ya Ulaya kwa vijana chini ya umri wa maiak 17 mwaka jana ambapo alifunga mabao nane yakiwemo matatu aliyofunga katika mchezo wa fainali dhidi ya Ujerumani. Edouard mwenye umri wa miaka 18 alijiunga na akademi ya PSG mwaka 2011.

JUVENTUS WAMNG'ANG'ANIA POGBA.

KLABU ya Juventus inadaiwa kutokuwa na mpango wowote wa kumuuza kiungo wake Paul Pogba majira ya kiangazi. Klabu hiyo tayari imefanikiwa kutwaa taji lake la tano mfululizo la Serie A na sasa wako katika mipango ya usajili lakini kuuza wachezaji wake nyota haitakuwa sehemu ya malengo yao. Mkataba wa sasa wa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa unatarajiwa kuisha mwaka 2019 na ofisa mkuu wa Juventus Beppe Marotta tayari ameshasisitiza Pogba ambaye ameshacheza mechi 175 toka atue Turin akitokea Manchester United, hatakwenda popote. Akihojiwa na radio moja nchini Italia mapema mwezi huu, Marotta amesema walishafanya maamuzi juu ya Pogba mwaka jana kuwa ataendelea kuwatumikia na mwenyewe anafurahia kuwepo hapo.

SIMEONE ATAMBA BAADA YA KUIZABUA BAYERN.



MENEJA wa Atletico Madrid, Diego Simeone anadhani kikosi chake kilikaribia kufikia ubora wake kufuatia ushindi wa bao 1-0 waliopata dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa nusu fainali ya mkono wa kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana. Huku wakishabikiwa kwa nguvu na mashabiki wao katika Uwanja wa Vicente Calderon, Atletico walifanikiwa kupata bao hilo pekee katika dakika ya 11 kupitia kwa nyota wake Saul Niguez. Katika kipindi chote cha mchezo vijana wa Simeone walionyesha umahiri wao mkubwa katika kuzuia mashabulizi makali ya wapinzani wao ambao muda wote walikuwa langoni mwao. Akihojiwa kuhusiana na mchezo huo, Simeone aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango kikubwa walichoonyesha akidai walicheza sawa kama katika robo fainali walipokutana na Barcelona. Simeone aliongeza kuwa Bayern walikuwa na uwezo wa kubadili na hata kupata ushindi lakini bahati haikuwa upande wao kutokana na umahiri wa wachezaji wake.

Tuesday, April 26, 2016

DAVID SILVA KUIKOSA MADRID KATIKA MARUDIANO.

KIUNGO wa Manchester City, David Silva anatarajiwa kukosa mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alipata majeruhi ya msuli wa paja katika kipindi cha kwanza cha mchezo wa jana ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana. Na Pellegrini amebainisha kuwa hadhani kama kiungo hiyo anaweza kupona kwa wakati kabla ya mchezo wao wa wiki ijayo. Akihojiwa Pellegrini amesema Silva amepata majeruhi na hadhani kama atakuwa fiti ndani ya wiki moja.

DELE ALLI AINGIA MATATANI.

KIUNGO wa Tottenham Hotspurs, Dele Alli anaweza kukosa mechi zilizobakia msimu huu baada ya kushitakiwa kwa utovu wa nidhamu na Chama cha Soka cha Uingereza-FA. Hatua hiyo inakuja kufuatia picha cha video kuonyesha Alli akimpiga ngumi Claudio Yacob katika mchezo wao dhidi ya West Bromwich Albion juzi. Tukio hilo halikujumuisha katika taarifa ya mwamuzi wa mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Matukio kama hayo ya utovu wa nidhamu adhabu yake ni kufungiwa mechi tatu, hivyo kama chipukizi hiyo atakutwa na hatia anaweza kukosa mechi zote tatu za Spurs zilizobakia msimu huu. Alli ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na Chama cha Wachezaji Kulipwa-PFA Jumapili iliyopita, amepewa mpaka baadae leo awe amejibu tuhuma hizo.

ARSENAL YAMUWANIA MSHAMBULIAJI WA CHELSEA.

KLABU ya Arsenal, inadaiwa kuwa na mipango ya kumuwania mshambuliaji wa Chelsea Dominic Solanke. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 yuko katika mzungumzo ya mkataba na Chelsea lakini anataka mkataba atakaolipwa paundi 50,000 kwa wiki. Lakini wakati Arsenal wakiwa hawataweza kufikia mshahara anaohitaji mshambuliaji huyo, wako tayari kumuhakikishia nafasi ya katika kikosi cha kwanza cha timu yao. Solanke ambaye mkataba wake unamalizika majira ya kiangazi, kwasasa yuko kwa mkopo katika klabu ya Vitesse ambako amefunga mabao saba katika mechi 24 alizocheza.

PELLEGRINI AANZA VISINGIZIO.

MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amedai Ligi Kuu imepuuza juhudi zao za kutaka mchezo wao wa Jumapili hii dhidi ya Southampton kusogezwa mbele ili wapate muda wa zaidi wa kujiandaa na mchezo wao wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. City na Madrid jana walitoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa michuano hiyo uliofanyika katika Uwanja wa Etihad na sasa wanakabiliwa na kibarua kizito pale watakapowafuata mabingwa hao wa kihistoria kule Santiago Bernabeu. Akihojiwa Pellegrini amesema wenzao Madrid watakuwa na muda zaidi wa kujiandaa kwani watakuwa na mchezo wa La Liga dhidi ya Real Sociedad Jumamosi wakati wao watachea jumapili. Meneja huyo aliendelea kudai wamejitahidi kufanya kila wawezalo ili wabadilishiwe mchezo huo lakini imeshindana kutokana haki za matangazo ya moja kwa moja.

KOMPANY AWACHIMBA MKWALA MADRID.

NAHODHA wa Manchester City, Vincent Kompany amedai asingejisikia vyema kama angekuwa nafasi waliyopo Real Madrid kufuatia sare ya bila kufungana waliyopata jana katika mchezo wa nusu fainali ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Madrid wanaonolewa na Zinedine Zidane, walikuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa bila uwepo wa nyota wao Cristiano Ronaldo, haswa baada ya kufungwa ugenini na Wolfsburg katika hatua ya robo fainali. Timu zote mbili zilipata tabu kutengeneza nafasi katika mchezo huo na zinatarajiwa kukutana tena katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumatano ijayo kupigania nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo. Akihojiwa Kompany amesema anategemea wao kupata mabao katika mchezo huo na kama hilo likiwezekana utakuwa mzuri. Kompany aliendelea kudai kuwa wanajivunia rekodi nzuri waliyonayo kwa mechi zao ugenini hivyo hadhani kama wapinzani wao wanapaswa kufurahia.

Monday, April 25, 2016

RONALDO NA KIKOSI KIZIMA CHA MADRID WATUA MANCHESTER TAYARI KUIKABILI CITY.






JUVENTUS WATWAA TAJI LA TANO MFULULIZO LA SERIE A.

KLABU ya Juventus, imetwaa taji la Serie A kwa msimu wa tano mfululizo baada ya Napoli kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya AS Roma jioni hii. Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fiorentina jana uliwafanya kulikaribia taji hilo, na kushindwa kupata ushindi wa Napoli kunamaanisha kuwa hakuna timu yeyote itakayoweza kuifikia Juventus kwasasa. Msimu huu haukuwa rahisi kwa Juventus kwani Octoba 28 mwaka jana walikuwa wako katika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya alama 11 kufikia kileleni. Hata hivyo mambo yalianza kuwaendelea vyema na kujikuta wakishinda mechi 24 kati ya 25 walizocheza toka wakati huo.

MESSI ATIMIZA AHADI YAKE KWA STEPHEN CURRY.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi ametoa ahadi yake kwa kumtumia Stephen Curry jezi yake yenye namba 10 mgongoni baada ya nyota huyo wa kikapu wa timu ya Golden State Warriors kufikisha mashabiki milioni 10 wanaomfuatilia katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram. Desemba mwaka jana, Messi alipokea fulana ya Warriors kutoka kwa Curry wakati alipofikisha mashabiki milioni 30 wanaomfuatilia katika mtandao huo wa kijamii. Messi aliapa kulipa fadhila wakati Curry atakapofikisha mashabiki milioni 10 na amefanya hivyo kama alivyoahidi. Messi alituma video katika ukurasa wake wa Instagram akionyesha jezi yake aliyosaini ambayo alipanga kumtumia Curry huku akimpongeza kwa mafanikio aliyopata.

FAINALI YA KOMBE LA FA YAMPA KIBURI VAN GAAL.

MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amesisitiza amefanya kazi nzuri kukijenga kikosi na kuongeza kuwa amekuwa akifanya kazi na wachezaji ambao hawana ubora anaotaka. United wako nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa wamebaki na mechi nne, huku wakiwa wamefuzu hatua ya fainali ya Kombe la FA baada ya kuichapa Everton mabao 2-1 katika Uwanja wa Wembley. Van Gaal amekuwa akilaumiwa mara kadhaa kutokana na kikosi chake kucheza chini ya kiwango hatua ambayo sasa meneja huyo Mholanzi anailaumu klabu kwa kukosa wachezaji wepesi na wabunifu. Akihojiwa Van Gaal amesema aliwahi kusema kila kitu huko nyuma kwamba siku zote amekuwa akifundisha wachezaji ambao ubora wao sio aliohitaji. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kipindi chote cha msimu amekuwa akihangaika na majeruhi wengi katika kikosi chake cha kwanza jambo ambalo limewarudisha nyuma kwa kiasi fulani.

CHIELLINI KUENDELEA KUSOTA BENCHI.

BEKI wa Juventus, Giorgio Chiellini anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu zaidi baada ya kupata majeruhi mengine akiwa mazoezini. Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo nyota huyo wa kimataifa wa Italia ambaye alikosa mchezo wa jana walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Fiorentina anatarajiwa kuwa nje kwa siku 15 hadi 20 baada ya kuumia goti lake la kulia. Chiellini mwenye umri wa miaka 31, amekuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili msimu huu baada ya kuumia goti pamoja na paja. Juventus wanaweza kutawadhwa mabingwa wa Serie A kwa mara ya tano mfululizo leo kama Napoli wanaoshika nafasi ya pili wakishindwa kuichapa AS Roma.

ZABALETA ATAMBA KUIFUNGA MADRID.

KIUNGO wa Manchester City, Pablo Zabaleta anaamini kikosi chao kina nafasi ya kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Real Madrid kuliko kama wangekuwa wanacheza na Bayern Munich au Atletico Madrid. Madrid ambao wamefunga mabao 26 msimu huu katika michuano hiyo wanatarajia kukwaana na City baadaye leo katika Uwanja wa Etihad kwenye nusu fainali ya mkondo wa kwanza. Pamoja na kufunga mabao mengi katika kampeni zao, hata hivyo Madrid nao wamekuwa na tatizo katika safu yao ya ulinzi kwa wameruhusu mabao mengi pia na Zabaleta anaamini kwa aina yao ya mchezo wanaweza kuwatoa mabingwa hao wa kihistoria. Akihojiwa Zabaleta amesema timu zote tatu ni ngumu lakini anadhani wao kupangwa na Madrid ni afadhali kidogo kwani kuna baadhi ya vitu wanashabihiana.

HAZARD KUBAKIA STAMFORD BRIDGE.

MENEJA wa Chelsea, Guus Hiddink amedokeza kuwa Eden Hazard anatarajia kuendelea kubakia Stamford Bridge msimu ujao. Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amekuwa nje ya uwanja kwa karibu miezi miwili kabla ya kurejea na kufunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu msimu huu katika ushindi wa mabao 4-1 waliopata dhidi ya Bournemouth katika Uwanja wa Vitality. Hazard alikuwa mmoja wa wachezaji walioachwa katika kikosi cha kwanza na Jose Mourinho kabla hajatimuliwa Chelsea Desemba mwaka jana na Real Madrid na Paris Saint-Germain zimekuwa zikiripotiwa kumfuatilia kwa karibu nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji. Akihojiwa Hiddink amesema anaamini klabu na mchezaji wote wana furaha na anategemea nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 kuendelea kubakia Stamford Bridge msimu ujao.

GIGGS AFUATA NYAYO ZA FERGUSON.

MENEJA msaidizi wa Manchester United, Ryan Giggs ametunukiwa tuzo ya heshima ya Merit inayotolewa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa-PFA. Winga huyo wa zamani wa United, aliibuka rasmi Old Trafford miaka 25 iliyopita na kufanikiwa kushinda tuzo zote za PFA za mchezaji bora wa mwaka pamoja na chipukizi bora wa mwaka katika kipindi chake akicheza soka. Giggs anafuata nyayo za nguli wa United Sir Alex Ferguson, Sir Matty Busby na Sir Bobby Charlton ambao wote wamewahi kushinda tuzo hiyo. Akipokea tuzo hiyo Giggs aliwashukuru wale wote ambao wamekuwa karibu naye katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.

MAHREZ, ALLI WATWAA TUZO ZA PFA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Leicester City, Riyad Mahrez amefanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ambayo inatolewa na Chama cha wachezaji wa Kulipwa-PFA. Mahrez amefunga mabao 17 na kutengeneza mengine 11 katika mechi 34 za ligi alizocheza na kuisaidia Leicester kukaribia kutwaa taji la Ligi Kuu. Nyota huyo wa kimataifa wa Algeria alipigiwa kura ya kutwaa tuzo hiyo na wachezaji wenzake wa kulipwa. Kiungo wa Tottenham Hotspurs, Dele Alli mwenye umri wa miaka 20 yeye aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka chipukizi wakati mwanadada Izzy Christiansen anayekipiga Manchester City yeye ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa wanawake. Mwanadada Beth Mead mwenye umri wa miaka 20 anayekipiga Sunderland amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka chipukizi kwa wanawake.

Friday, April 22, 2016

RONALDO HATIHATI KUIKOSA MAN CITY WIKI IJAYO.

KLABU ya Real Madrid imethibitisha kuwa Cristiano Ronaldo amepata majeruhi ya msuli wa paja, hivyo kuibua wasiwasi wa kutokuwepo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City wiki ijayo. Nyota huyo wa kimataifa wa ureno alitoka mwenyewe nje mwishoni mw amchezo dhidi ya Villarreal juzi huku akishikilia mguu wake wa kulia. Meneja wa Madrid Zinedine Zidane alidai kuwa hadhani kama majeruhi hayo yatakuwa mabaya wakati Ronaldo mwenyewe akiandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa instagram kuwa kila kitu kilikuwa kinaenda sawa baada ya tukio hilo. Hata hivyo, baada ya kufanyiwa vipimo imegundulika kuwa nyota huyo alipata majeruhi ya msuli na haijulikani ni kw amuda gani atakaa nje ya uwanja.

HODGSON AMUHAKIKISHIA ROONEY SAFARI YA EURO.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amemuhakikishia Wayne Rooney nafasi katika kikosi chake cha wachezaji 23 atakaowaita kwa ajili ya michuano ya Euro 2016 lakini alikataa kuhakikisha kama mshambuliaji huyo wa Manchester United atapata namba katika kikosi cha kwanza. Kutokana na kuwa na washambuliaji wengi wazuri wakiwemo wanaoongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu, Harry Kane mwenye mabao 24 na Jamie vardy mabao 22, Hodgson amesema Rooney anaweza kuachwa katika kikosi cha kwanza. Akihojiwa Hodgson amesema kwasasa ushindani ni mkubwa hivyo hawezi kumuhakikishia nahodha wake nafasi ingawa atamjumuisha katika kikosi chake. Uingereza itakabiliana na Urusi, Slovakia na Wales katika kundi B kwenye michuano hiyo ya timu 24 ambayo inatarajiwa kuanza Juni 10 nchini Ufaransa.

MARTINEZ ADAI HANA HOFU YA KUTIMULIWA EVERTON.

MENEJA wa Everton, Roberto Martinez amesema haofii mustakabali wake na kuwa kikosi chake kinapaswa kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo. Everton ambao hawajapata ushindi katika mechi zao saba zilizopita, walitandikwa mabao 4-0 na Liverpool juzi, matokeo ambayo Martinez ameyaelezea kama mabaya. Klabu hiyo inakabiliw ana mchezo mwingine mgumu Jumamosi hii wakati watakapochuana na Manchester United katika Uwanja wa Wembley katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA. Akihojiwa Martinez amesema hana mpango wa kufuatilia watu wanasemaje kuhusu uwezo wake wa kuendelea kuinoa klabu hiyo kwani wana mambo muhimu ya kufanya. Meneja huyo aliongeza kuwa kwasasa wanafanyia kazi makosa ambayo yamekuwa aykijitokeza katika kikosi chao ili waweze kufanya vyema mechi zao zijazo.

BAYERN KUWEKA HISTORIA BUNDESLIGA.

KLABU ya Bayern Munich inaweza kuweka historia Jumamosi hii kwa kutwaa taji la nne mfululizo la Bundesliga wakati watakaposafiri kwenda jijini Berlin kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Hertha Berlin. Ushindi katika mchezo huo utakaofanyika katika Uwanja wa Olimpiki utaifanya Bayern kujiimarisha kileleni kwa tofauti ya alama saba huku kukiwa kumebaki michezo saba huku wakiomba Borussia Dortmund wapoteza mchezo wao dhidi ya Stuttgart. Kama Dortmund akipoteza mchezo huo na Bayern kushinda hakuna shaka kuwa watatangazwa mabingwa kwani hakuna timu itakayoweza kufikia alama walizonazo. Kutwaa taji la Bundesliga mapema kutawapa ahueni katika mchezo wao utakaofuata wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano ijayo ambapo watasafiri kuifuata Atletico Madrid.

HODGSON KUMUACHA MPEMBA WA MAN UNITED.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema atalazimika kumtoa sadaka mchezaji ambaye ana sababu nyingi zaidi za kuitwa ili aweze kumuongeza chipukizi Marcus Rashford katika kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Euro 2016. Mshambuliaji huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 18, amefunga mabao saba katika mechi 13 alizoichezea United toka alipopandishwa kikosi cha wakubwa Februari mwaka huu. Hodgson amekuwa akifurahishwa a chipukizi huyo lakini amesema kuna uwezekano mdogo wa kumchukua kwenda naye Ufaransa katika michuano hiyo. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa utakuwa uamuzi wa kijasiri kumjumuisha katika kikosi chake.

BERLUSCONI BADO AING'ANG'ANIA AC MILAN.

RAIS wa AC Milan, Silvio Berlusconi ameelezea uvumi uliozagaa kuhusu timu hiyo kununuliwa na kampuni kutoka China, akisisitiza ataiuza klabu hiyo pale tu atakapoona kuwa itakuwa katika mikono salama. Milan imekuwa katika mazungumzo na mfanyabiashara wa Thailand Bee Taechaubol ambaye amekubaliano yao ya awali ni kununua hisa asilimia 48 za klabu hiyo. Toka wakati huo kuna taarifa zimezagaa kuwa kampuni kutoka China inataka kuinunua klabu hiyo huku vyombo vya habari nchini Italia vikidai kuwa yuko tayari kutoa kitita cha euro milioni 700. Akihojiwa Berlusconi amekiri kuwa wataka kuu lakini kama mnunuzi sahihi atapatikana ili ajihakikishie kuwa anaiacha Milan katika mikono salama.

Thursday, April 21, 2016

RATIBA YA KOMBE LA SHIRIKISHO; YANGA KWENDA ANGOLA.

KLABU ya soka ya Yanga imepangwa kucheza na klabu ya GD Esperanca ya Angola katika hatua ya mtoano ya timu 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Yanga iliangukia katika michuano hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa Afrika baada ya kufungwa na Al Ahly ya Misri kwa mabao 2-1 jana hivyo kuondolewa kwa jumla ya mabao 3-2 katika mechi mbili walizokutana. Katika hatua hiyo Yanga wanatarajiwa kuanzia nyumbani kabla ya kwenda ugenini ambapo mechi za mkondo wa kwanza zikitarajiwa kuchezwa Mei 6 na 8 huku zile za marudiano zikitarajiwa kuchezwa Mei 17 na 18. Baadhi ya mechi zingine zilizopangwa katika ratiba hiyo wababe wa Azam FC, Esperance ya Tunisia wao watavaana na MO Bejaia ya Algeria huku TP Mazembe waliovuliwa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika wao wakipangwa kucheza na Stade Gabesien ya Tunisia.

Wednesday, April 20, 2016

NEUER AONGEZA MKATABA NA BAYERN.

KIPA wa Bayern Munich, Manuel Neuer amesaini mkataba mpya ambao utamuweka Allianz Arena mpaka mwaka 2021. Kipa huyo wa kimataifa wa Ujerumani alitua Bayern akitokea Schalke msimu wa 2011-2012 na toka wakati huo amekuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Taarifa za hivi karibuni zilikuwa zikidai kuwa Neuer anaweza kushawishika kuungana na Pep Guardiola katika klabu ya Manchester City msim ujao lakini sasa amezima tetesi hizo kwa kusaini mkataba mpya na mabingwa hao wa Ujerumani. Neuer sasa anakuwa amefuata nyayo za kina Jerome Boateng, Thomas Muller, David Alaba na Javi Martinez ambao nao wameongeza mikataba yao katika miezi ya karibuni.

INFANTINO ATAKA PICHA ZA VIDEO ZISAIDIE WAAMUZI KOMBE LA DUNIA 2018.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino ana matumaini michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 itakayofanyika nchini Urusi, itakuwa ya kwanza kutumia msaada ya picha za video kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi kufanya uamuzi sahihi. Machi mwaka huu, Bodi ya Kimataifa ya mchezo huo-IFAB ilidai kuwa itafanyia majaribio teknologia hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ili kusaidia mabao yanayofungwa, kadi nyekundu, makosa ya kufananisha na penati. IFAB ilikuwa imepanga kuanza kufanya majaribio hayo msimu wa 2017-2018 lakini Infantino amesema majaribio yataanza sasa na kuchukua muda wa miaka miwili. Infantino raia wa Uswisi ambaye alichukua nafasi ya Sepp Blatter Februari mwaka huu aliongeza kuwa mpaka kufikiza Machi 2018 watakuwa wamehafahamu kama mfumo huo utafaa au haufai. Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA limeichagua kampuni ya Uingereza ya Hawk-Eye kutumika katika mechi zote za michuano ya Euro 2016. Mfumo wa Hawk-Eye ambao ndio unaotumika katika mechi za Ligi Kuu ulichaguliwa badala ya ule wa kampuni ya Ujerumani wa Goal Control ambao ulitumika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Tuesday, April 19, 2016

TETESI ZA USAJILI ZILIZOJIRI HUKO MAJUU.

Maskauti wa Barcelona walikwenda nchini Ujerumani kumtizama Pierre-Emerick Aubameyang lakini walirejea wakiwa na malengo tofauti ya kumsajili beki wa kati Mats Hummels ambaye mkataba wake na Borussia Dortmund unatarajiwa kumalizika mwaka 2017.
Chanzo: Bild

KLABU ya Ajax Amsterdam inatarajiwa kumuwania Klaas-Jan Hunterlaar ambaye atamaliza mkataba wake na Schalke mwaka 2017. Mshambuliaji huyo ambaye anaweza kwenda kuziba nafasi ya Arek Milik anafahamu kuwa anawindwa na klabu hiyo.
Chanzo: Algemeen Dagblad

KLABU ya Real Madrid huenda ikamruhusu Lucas Silva kurejea nchini kwao Brazil katika klabu ya Cruzeira pindi mkopo wake katika klabu ya Marseille utakapomalizika.
Chanzo: L’Equipe

BEKI wa Corinthians, Fagner anatizamwa kwa karibu na klabu ya Barcelona ingawa hakuna mazungumzo yeyote yaliyofanyika na mchezaji huyo ambaye anatajwa kuwa atakuja kuziba nafasi ya dani Alves.
Chanzo: SporTV

KLABU ya Manchester City inadaiwa kumfukuzia chipukizi wa Celtic, Kieran Tierney baada ya beki huyo kuonyesha kiwnago bora katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Scotland dhidi ya Rangers. Liverpool na Southampton nazo pia zinatajwa kumuwania.
Chanzo: Daily Mail

PSG YAANZA MAZUNGUMZO NA MOURINHO.

KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG inadaiwa kuwa katika mazungumzo na meneja wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho. PSG tayari wameshanyakuwa taji la La Liga msimu huu na wako katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la Kombe la Ligi na Kombe la Ufaransa, hata hivyo lengo lao kubwa lilikuwa ni kuvuka hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kufuatia kuenguliwa katika michuano hiyo ya Ulaya na Manchester City, meneja wa klabu hiyo Laurent Blanc amekuwa katika hatari ya kutimuliwa kufuatia taarifa hizo. Mourinho amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Manchester United kwa kipindi kirefu lakini uwezekano wa timu hiyo kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao unaweza kumfanya Louis van Gaal kuendelea na kibarua chake. PSG walipotafutwa kutoa kauli yao kuhusiana na taarifa hizo walikataa kusema chochote.

ARDA TURAN AUGUA GHAFLA BARCELONA IKIIFUATA DEPORTIVO.

KLABU ya Barcelona inafuatilia kwa karibu afya ya Arda Turan kuelekea mchezo wao a kesho dhidi ya Deportivo La Coruna baada ya kiungo huyo kuugua ghafla. Arda alikosa mazoezi ya kikosi cha Barcelona leo kutokana na kuugua na atafanyiwa vipimo kesho asubuhi kabla ya mchezo huo.  Barcelona ilithibitisha taarifa hizo na kudai kuwa wataweza kumtumia hapo kama akipewa ruhusa na madaktari baada ya kuridhishwa na maendeleo ya afya yake. Barcelona wanaonolewa na Luis Enrique watakuwa wakijaribu kubadili matokeo katika mchezo huo baada ya kupoteza mechi zao nne zilizopita hali ambalo inatishia mbio zao za kutetea taji la La Liga.

VARDY HUENDA AKAADHIBIWA ZAIDI NA FA.

MSHAMBULIAJI wa Leicester City, Jamie Vardy huenda akakabiliwa na adhabu zaidi baada ya kushitakiwa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa makosa ya kinidhamu. Vardy mwenye umri wa miaka 29, alizozana na mwamuzi Jon Moss baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Jumapili iliyopita mabao walitoa sare ya mabao 2-2 na West Ham United. FA pia imeishitaki Leicester kwa kushindwa kuwatuliza wachezaji wake baada ya West Ham kupata penati katika dakika ya 83 ya mchezo. Vardy na Leicester wamepewa mpaka Alhamisi hii wawe wamejibu tuhuma zinazowakabili kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi.

VIDAL AMTAKA SANCHEZ BAYERN.

KIUNGO wa Bayern Munich, Arturo Vidal amedai ataunga mkono hatua zozote zitakazochuliwa na klabu hiyo kwa ajili ya kumuwnaia nyota wa Arsenal Alexis Sanchez. Wachezaji hao wanajuana vyema kutokana na majukumu ya kimataifa wakiwa katika kikosi cha Chile, na Sanchez amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Ujerumani mara kadhaa huku kocha ajaye Carlo Ancelotti akidaiwa kuwa shabiki wake mkubwa toka akiwa Barcelona. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Vidal amesema amekuwa akicheza na Sanchez toka wakiwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 hivyo itakuwa vyema akija kucheza naye tena katika ngazi ya klabu. Bayern inakaribia kunyakuwa taji la Bundesliga na Vidal mwenye umri wa miaka 28 anataka washinde mataji yote msimu huu kwa kuwa bado yako ndani ya uwezo wao.

USHINDI WAIPA JEURI SPURS.



MSHAMBULIAJI wa Tottenham Hotspurs, Harry Kane amewaonya Leicester City kuwa bado wako nyuma yao baada ya kupunguza pengo la alama na kubaki tano dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu. Spurs waliongeza shinikizo kwa Leicester baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Stoke City katika Uwanja wa Britania jana usiku. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Kane mwenye umri wa miaka 22, amesema bado wataendelea kuwafukizia Leicester mpaka mwisho. Nyota huyo ambaye alifunga mabao mawili jana na kufikisha jumla ya mabao 24 msimu huu, aliendelea kudai kuwa kama wakiendelea kucheza kama walivyocheza jana hadhani kama kuna itaweza kuwafunga.

Monday, April 18, 2016

YANGA, AZAM KUWEKA HISTORIA MPYA AFRIKA.

VILABU vinavyoshiri michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF, zinatarajiwa kuweka historia mpya kwa kucheza kwa mara ya kwanza mechi zao katikati ya wiki. Mechi za michuano hiyo mara nyingi zilizoeleka kuchezwa mwishoni mwa wiki lakini CAF sasa wameamua kubadilisha na kuchezwa katika siku ya Jumanne na Jumatano kutokana na maombi mengi yaliyotolewa kwao. Katika taarifa yake CAF imedai kuwa wamekuwa wakipata maombi mengi za mechi za michuano hiyo kuchezwa katikati ya wiki ili kutovuruga ratiba za mechi zao za ligi mwishoni mwa wiki. Timu za Tanzania, Yanga iliyopo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam iliyopo Kombe la Shirikisho zinatarajiwa kuwepo uwanjani katikati wiki hii kucheza mechi zao za mkondo wa pili. Yanga wao wataifuata Al Ahly jijini Cairo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa huku Azam wao wakielekea Tunisia kuifuata Esperance baada ya kuibuka kidedea kwa kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Chamazi.

Friday, April 15, 2016

RATIBA CHAMPIONS LEAGUE NA EUROPA LEAGUE.

KLABU ya Manchester City imepangwa kucheza na mabingwa wa kihistoria Real Madrid katika ratiba ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopangwa leo. Hatua hiyo inamaanisha City wanaweza kukutana na meneja wao ajaye Pep Guardiola katika hatua ya fainali baada ya Bayern Munich kupangwa kucheza na dhidi ya Atletico Madrid katika nusu fainali nyingine. Guardiola anatarajiwa kuchukua nafasi ya meneja wa sasa City Manuel Pellegrini majira ya kiangazi. Mechi za nusu fainali zinatarajiwa kuchezwa Aprili 26 na Mei 4 kwa mechi za marudiano huku ile ya fainali ikipangw akuchezwa katika Uwanja wa San Siro Mei 28. 
Kwa upande wa ratiba ya nusu fainali ya michuano ya Europa League, Villarreal watakwaana na Liverpool huku Shakhtar Donetsk wao wakipangw akucheza na Sevilla. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa Aprili 28 kwa mechi za mkondo wa kwanza na zile za marudiano zitachezwa Mei 5 huku fainali ikitarajiwa kufanyika Mei 18 Basel, Uswisi.

PELE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA RAFIKI YAKE CRUYFF.

NGULI wa soka wa Brazil na mshindi mara tatu wa Kombe la Dunia, Pele ametuma salamu zake za rambirambi kwa marehemu Johan Cruyff, akimuelezea nguli huyo wa Uholanzi kama mtu aliyebadilisha mchezo wa soka. Cruyff alifariki Machi 24 mwaka huu baada ya kuugua kwa kipindi kifupi na kuacha kumbukumbu ya kipekee katika soka mabyo kamwe haitaweza kusahaulika kirahisi. Nguli huyo aliiongoza Ajax Amsterdam kunyakuwa mataji matatu ya Ulaya akiwa mchezaji na pia kuisaidia Barcelona kunyakuwa taji hilo mwaka 1992 wakati akiwa kocha. Cruyff pia aliibuka mchezaji bora katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974, akiwa na kikosi cha Uholanzi ambacho kilifungwa na Ujerumani Magharibi katika hatua ya fainali. Akihojiwa Pele amesema hana shaka kuwa Cruyff ni mmoja kati ya wachezaji waliobadilisha kabisa soka la Ulaya na alifanya hivyo akiwa na mchezaji na baadae kama kocha.

WENGER BADO AOTA UBINGWA WA LIGI KUU.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger haamini kama mbio za Ligi Kuu zimekwisha na kusisitiza kuwa wanapaswa kushinda kila mechi wakati shinikizo likiongezeka kwa wapinzani wao. Arsenal wako nyuma ya vinara Leicester City wakitofautiana kwa alama 13, lkini wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Akihojiwa Wenger amekiri kuna shinikizo kubwa lakini zaidi kwa wpainzani wao hivyo wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo wao na kuona hali itakavyokuwa huko mwisho. Arsenal wanatarajiwa kuvaana na Crystal Palace Jumapili hii huku Leicester wakipambana na West Ham United na Tottenham Hotspurs waoashika nafasi ya pili wakichuana na Stoke City Jumatatu ijayo.

XAVI AIKUMBUKA BARCELONA.

NAHODHA wa zamani wa Barcelona, Xavi amesema amekumbuka maisha yake katika klabu hiyo baada ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita. Xavi aliyetokea katika akademi maarufu ya klabu hiyo ya La Masia, aliondoka Camp Nou kiangazi mwaka jana baada ya kupita miaka 25 na kwenda klabu ya Al Sadd ya Qatar. Hata hivyo, baada ya kukaribia mwaka toka aondoke Hispania, Xavi amebainisha kuwa ameikumbuka Barcelona. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 36, amesema anakumbuka zaidi hali inavyokuwa katika vyumba vya kubadilishia nguo na utani wanaofanyiana pamoja na kila kitu kuhusu klabu hiyo. Xavi pia amekiri anaweza kugeukia ukocha pindi atakapotundika daruga zake siku zijazo.

KLOPP AKISIFIA KIKOSI CHAKE.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amesifu ari waliyokuwa nayo wachezaji wake na kudai kuwa walipambana kufa na kupona na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Europa League. Liverpool walitoka nyuma wakiwa wameshafungw amabao 3-1 na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 jana dhidi ya Borussia Dortmund na kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-4. Akihojiwa Klopp amesema ni vigumu kuelezea ilivyokuwa kwani mchezo ulikuwa wa ajabu na ulikuwa usiku mzuri katika Uwanja wa Anfield. Mabao ya Liverpool katika mchezo huo yalifungwa na Divock Origi, Philippe Coutinho, Mamadou Sakho na Dejan Lovren huku yale ya Dortmund yakifungwa na Henri Mkhitaryan na Pierre-Emerick Aubameyang aliyefunga mawili. Klopp aliendelea kudai kuwa walistahili ushindi huo kwakuwa walitengeneza nafasi nyingi na kupambana na kama mashetani.

Monday, April 11, 2016

CHINA YABAINISHA MIPANGO YAKE YA KUJA KUWA SUPER POWER KWENYE SOKA.

TAIFA la China limezindua mikakati yake ya kuja kuwa taifa lenye nguvu kisoka ifikapo mwaka 2050, kwa mipango ya kupata vijana wadogo na wakubwa zaidi ya milioni 50 wachezaji soka ifikapo mwaka 2020. Malengo mengine yanajumuisha kuwa na walau vituo vya soka 20,000 kwa ajili ya mazoezi na viwanja 70,000 ifikapo mwaka 2020. Wakati China ikifanya vyema katika michuano ya Olimpiki na Paralimpiki, taifa hilo limefanikiwa kufuzu mara moja pekee katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2002. Rais wa China Xi Jinping ameonyesha kuwa na shauku kubwa katika soka ambapo mara kadhaa amekuwa akikaririwa akidai kuwa anataka taifa hilo kutwaa Kombe la Dunia katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

KOMPANY MAJANGA TENA.

NAHODHA wa Manchester City, Vincent Kompany hatarajiwi kuwepo katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho dhidi ya Paris Saint-Germain, kutokana na majeruhi. Meneja wa City Manuel Pellegrini amesema Kompany hayuko fiti asilimia 100 hivyo haitawezekana kumtumia. Beki huyo mwenye umri wa miaka 30, hajacheza mechi yeyote toka alipoumia katika sare ya bila kufungana waliyopata dhidi ya Dynamo Kiev. City na mabingwa Ufaransa PSG walitoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa jijini Paris wiki iliyopita.

RAFINHA KUWAKOSA ATLETICO.

KLABU ya Barcelona inatarajia kukosa huduma ya Rafinha katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid, kutokana na majeruhi yanayomsumbua. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil alirejea hivi karibuni baada ya kukaa nje kwa miezi saba kufuatia kuumia goti, alicheza dakika 26 katika mchezo Barcelona walioshinda mabao 2-1 dhidi ya Atletico wiki iliyopita kabla ya kuanza katika mchezo wa Jumamosi iliyopita waliofungwa bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad. Rafinha alimpisha Andres Iniesta wakati wa mapumziko na sasa Barcelona wametangaza kuwa nyota huyo alipata matatizo ya msuli ambayo yatamuweka nje kwa muda. Katika taarifa ya klabu hiyo iliyotumwa katika mtandao wake imedai kuwa kurejea kwake uwanjani kutategemea jinsi gani atavyopona haraka.

KIPA WA ARSENAL AIPA NAFASI LEICESTER KUTWAA TAJI.

GOLIKIPA wa AS Roma, Wojciech Szczesny amesema ana matumaini Leicester City watwae ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu pamoja na kuwepo kwake katika virabu vya Arsenal. Golikipa huyo aliondoka Arsenal kwenda Roma kwa mkopo kiangazi mwaka jana baada ya ujio wa Petr Cech na amekuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza toka aanze kuichezea klabu hiyo ambayo inashika nafasi ya tatu katika Serie A. Matumaini ya Arsenal kutwaa ubingwa yaliingia dosari nyingine Jumamosi iliyopita wakati walipolazimishwa sare ya mabao 3-3 na West Ham United na kuwaacha nyuma Leicester City kwa alama 13. Akihojiwa Szczesny amekiri kuwa angependa kuona Leicester wakishinda taji hilo badala ya klabu yake ya Arsenal. Golikipa huyo amesema hakuna yeyote katika soka anaweza kuelezea maajabu yanayofanywa na Leicester, hivyo pamoja na kuinga mkono Arsenal lakini angependa zaidi kuona vijana hao wa Claudio Ranieri wakishinda taji la Ligi Kuu.