MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amefurahishwa kuwa nao tena Daniel Sturridge na Jordan Henderson haswa katika kipindi hiki ambacho ratiba ya mechi za ligi huwa ngumu. Wawili hao walirejea jana katika benchi la wachezaji wa akiba katika mchezo mgumu ambao Liverpool walishinda bao 1-0 dhidi ya Swansea City jana. Henderson aliyekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mguu na Sturridge goti, yaliwafanya kukaa nje kwa kipindi kirefu lakini sasa wamerejea katika wakati muhimu ambao Liverpool itakabiliwa na mechi nne ndani ya siku 12. Klopp amesema kurejea kwa wawili hao ni taarifa njema kwao kwani ni wachezaji muhimu na wamerejea wakati muafaka.
Monday, November 30, 2015
WENGER AJIPA MATUMAINI NA UBINGWA WA LIGI KUU.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger ana uhakika kikosi chake bado kipo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kukiri kupitia wakati mgumu. Arsenal walilazimishwa sare na Tottenham Hotspurs kabla ya kufungwa na ambao 2-1 na West Bromwich Albion wiki iliyopita na jana tena kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Norwich City. Wenger amekubali kuwa walipaswa kupata matokeo mazuri zaidi ya hayo lakini kutokana na Arsenal kuwa nyuma kwa alama mbili dhidi ya vinara Manchester City na Leicester City, kocha huyo Mfanrasa anaamini haina haja ya kuhamaki. Wenger amesema kwasasa wanapitia kipindi kigumu kwani wameshindwa kupata matokeo mazuri katika mechi zao tatu zilizopita za ligi lakini hana hofu kwakuwa hawajaachwa mbali sana.
VILABU URUSI VYAFUNGIWA KUSAJILI WACHEZAJI KUTOKA UTURUKI.
KLABU za Urusi zinatarajiwa kufungiwa kusajili wachezaji kutoka Uturuki katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari mwakani. Mahusiano kati ya nchi hizo yamekuwa yakizorota toka ndege ya kivita ya Urusi itunguliwe na majeshi ya Uturuki katika mpaka wa Syria na kuua pailoti mmoja. Waziri wa Michezo wa Urusi Vitaly Mutko amesema tayari ujumbe umeshapelekwa kwa vilabu kuwa haitawezekana kwao kusajili wachezaji kutoka Uturuki katika kipindi cha usajili kinachokuja. Mutko aliendelea kudai kuwa vikwazo hivyo havitaweza kuathiri wachezaji wa Uturuki ambao tayari wanacheza soka nchini humo akiwemo kiungo wa Rubin Kazan Gokdeniz Karadeniz ambaye alijiunga nao mwaka 2008. Mutko amesema yeyote ambaye ana ana mkataba unaoendelea ataendelea kufanya kazi kama kawaida.
ETOILE DU SAHEL MABINGWA KOMBE LA SHIRIKISHO.
KLABU ya Etoile Du Sahel ya Tunisia imefanikiwa kuichapa Arlando Pirates ya Afrika Kusini kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho uliochezwa jana katika Uwanja wa Olimpiki huko Sousse. Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na nahodha Ammar Jemal na kuifanya Etoile kuibuka ushindi wa jumla wa mabao 2-1 kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wao wa kwanza uliochezwa Soweto Jumamosi iliyopita. Mchezo huo ulichezwa chini ya ulinzi mkali kufuatia shambulio la bomu lililotokea jijini Tunis huku mashabiki wakipunguzwa na muda mchezo kuwekwa mapema zaidi kuliko ulivyopangwa awali. Ushindi huo umeifanya Etoile kukunja kitita cha dola 660,000 pamoja na nafasi ya kucheza mchezo wa Super Cup dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC.
KOBE BRYANT KUSTAAFU KIKAPU MWAKANI.
MCHEZAJI nyota wa Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani-NBA, Kobe Bryant ambaye anahesabiwa kama mmoja ya wachezaji bora kabisa katika historia, anatarajiwa kustaafu mchezo huo mwishoni mwa msimu. Bryant amefunga vikapu 32,683 katika kipindi cha miaka 20 alichoichezea timu ya Los Angeles Lakers na kumfanya kushika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa wakati wote wa NBA. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 37 ambaye ana medali za dhahabu za mashindano ya Olimpiki, amekuwa akisumbuliwa na majeruhi katika misimu ya karibuni na kumfanya kuwa chini ya kiwango msimu huu akiwa na Lakers. Bryant alitajwa kama Mchezaji Mwenye Thamani Zaidi wa NBA mwaka 2008 na amewahi kuchaguliwa katika kikosi cha NBA All-Star kwa nyakati 17 tofauti. Mchezo wa mwisho wa Bryant unatarajiwa kuwa dhidi ya Utah Jazz utakaochezwa Aprili 13 mwakani.
WAKAZI WA JIJI LA HAMBURG WAGOMA MJI HUO KUANDAA OLIMPIKI.
WAKAZI wa mji wa Hamburg, Ujerumani wamepiga kura ya kukataa mji huo kuwa mwenyeji wa michuano ya Olimpki na Paralimpiki mwaka 2024. Hamburg ulikuwa mmoja kati ya miji mitano iliyobakia katika kinyang’anyiro hicho, wakiwa sambamba na Rome, Paris, Budapest na Los Angeles. Lakini asilimia 51.7 ya wakazi wa mji huo na ule wa jirani wa Kiel ambako ndipo kungefanika mashindano ya maboti, walikataa katika kura za maoni zilizofanyika jana. Maofisa wa Kamati ya Olimpiki ya Ujerumani waliuchagua mji wa Hamburg katika kinyang’anyiro hicho badala ya Berlin. Ujerumani haijaandaa mashindano ya olimpiki toka ile iliyoandaliwa jijini Munich mwaka 1972.
KOCHA WA VALENCIA ABWAGA MANYANGA.
MENEJA wa Valencia, Nuno Espirito Santo amejiuzulu wadhifa wake huo jana baada ya kikosi chake kuchapwa bao 1-0 na Sevilla katika mchezo wa La Liga. Taarifa hizo zilivuja mitandaoni wakati mchezo bado ukiendelea na kocha huyo raia wa Ureno alithibitisha uamuzi wake katika mkutano na wana habari baada ya mchezo kumalizika. Santo alifafanua kuwa alikuwa tayari ameshaamua kuondoka klabu hap hata kabla ya mchezo huo wa jana na kuongeza kuwa wachezaji wake walikuwa hawajui kama itakuwa mechi yake ya mwisho. Kocha huyo amesema kabla ya mchezo alizungumza na rais wa klabu hiyo ambaye pia ndio mmiliki, Peter Lim na wote kukubaliana kuwa hali sio nzuri ndio maana akaamua kuondoka. Santo aliendelea kudai kuwa kikubwa anachokihitaji yeye ni klabu hiyo kufanya vyema ndio maana ameamua kuchukua uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa wengine.
FURY ANZA JEURI AKATAA KUZICHAPA NA HAYE.
BINGWA wa masumbwi wa uzito wa juu duniani, Tyson Fury amesema kamwe hatarajii kutetea mikanda yake ya ubingwa dhidi ya Mwingereza mwenzake David Haye. Fury aliushangaza ulimwengu wa masumbwi kwa kumtandika Wladimir Klitschko juzi na kutwaa mikanda ya WBA, IBF na WBO iliyokuwa ikishikiliwa na bondia huyo raia wa Ukraine. Lakini Fury bado hajamsamehe Haye kwa kujitoa mara mbili katika ratiba ya mapambano yao mwaka 2013 hatua ambayo anadai ilimsababishia matatizo ya kisaikologia. Akihojiwa Fury amesema kamwe hataweza kupigana na bondia huyo kwakuwa bado hajasahau alichomfanyia na kama ikitokea akilazimishwa kufanya hivyo yuko tayari kuachia mikanda yake.
Friday, November 27, 2015
CABALLERO ATAMBA KUZIBA PENGO LA HART.
GOLIKIPA wa akiba wa Manchester City Willy Caballero ana uhakika anaweza kuziba nafasi ya Joe Hart kama ya majeruhi ya kipa huyo namba moja wa Uingereza aliyopata katika mchezo dhidi ya Juventus Jumatano yatamuweka nje katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Southampton. Hart alipata majeruhi ya msuli wa paja katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutolewa nje kumpisha Caballero katika dakika ya 81 na kuna uwezekano pia wa kuukosa mchezo wa kesho. Akihojiwa Caballero amesema hajapenda Hart aumie lakini anapaswa kujiandaa kwasababu hayo ndio maisha ya kipa wa akiba. Caballero aliendelea kudai kuwa ni vizuri kucheza michezo kadhaa mfululizo lakini hilo litategemea na jinsi hali ya Hart itakavyokuwa.
ANELKA 'MZEE WA KUHAMAHAMA' ANATAFUTA KLABU NYINGINE.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Anelka yuko mbioni kutafuta klabu nyingine baada ya kushindwa kuiongoza Mumbai City kutinga hatua ya mtoano ya Ligi Kuu ya India. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 36 amekuwa kocha-mchezaji wa Mumbai ambao waling’olewa katika msimu wa pili wa ligi hiyo yenye timu nane baada ya sare ya bao 1-1 waliyopata nyumbani dhidi ya Kerala Blasters jana. Akihojiwa baada ya sare hiyo Anelka ambaye kuzichezea Arsenal, Real Madrid na Chelsea amesema hadhani kama ataendelea tena na kibarua chake. Anelka aliongeza kuwa lengo lao ilikuwa ni kufika hatua ya nusu fainali na lengo hilo halijafikiwa hivyo hajui kitu gani kitatokea dhidi yake.
RODRIGUEZ KUKAA NJE MIEZI MIWLI.
MENEJA wa klabu ya Southampton, Ronald Koeman amethibitisha kuwa mshambuliaji Jay Rodriguez anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alirejea katika kikosi hicho mwanzoni mwa msimu baada ya kukaa nje kwa zaidi ya mwaka mmoja akiuguzu majeruhi ya goti. Rodriguez amecheza mechi 12 msimu huu lakini hajacheza toka walipopata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Leicester City Octoba 17 mwaka huu. Wakati huohuo Koeman amekanusha tetesi zilizozagaa kuwa watamuuza mshambuliaji wao Sadio Mane akihusishwa kuhamia Chelsea au Manchester United. Koeman amesema hawana mpango wa kuuza mchezaji yeyote katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwakani.
RAIS WA CBF AJIUZULU WADHIFA WAKE FIFA.
RAIS wa Shirikisho la Soka la Brazil-CBF, Marco Polo Del Nero amejiuzulu wadhifa wake kama mjumbe wa kamati wa utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA anayewakilisha Shirikisho la Soka la Nchi za Amerika Kusini-Conmebol. Katika taarifa yake Conmebol ilithibitisha taarifa hizo ikidai kuwa sababu haswa ni shinikizo alilokuwa nalo kwa miezi kadhaa na nafasi yake itachukuliwa na Fernando Sarney. Sarney ni mtoto wa rais wa zamani wa Brazil na mmoja kati ya makamu wanne wa rais wa CBF. Del Nero alichukua mikoba ya Jose Maria Marin kuiongoza CBF Aprili mwaka huu na ataendelea na wadhifa wake huo.
STURRIDGE AUMIA TENA.
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Daniel Sturridge amepata majeruhi mapya baada ya kuumia mguu akiwa mazoezini na kumfanya kuukosa mchezo wa Europa League dhidi ya Bordeaux jana. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa akitarajia kurejea tena uwanjani jana baada ya kupona majeruhi ya goti ambayo yalimuweka nje toka Octoba 4 mwaka huu. Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uingereza alipelekwa kufanyiwa vipimo baada ya kulalamika maumivu ya mguu. Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema hajui sana kuhusu hali yake lakini hadhani kama ni tatizo litakalomuweka nje kwa muda mrefu. Sturridge amecheza mechi tatu pekee msimu huu huku msimu uliopita akicheza mechi 18 kutokana na majeruhi ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakimuandama.
VALBUENA AFUNGUKA KUHUSU BENZEMA NA SAKATA LA MKANDA WA NGONO.
MCHEZAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Mathieu Valbuena amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu Mfaransa mwenzake Karim Benzema na tuhuma za ulaghai za mkanda video ya ngono. Valbuena amesema Benzema alipendekeza ingawa moja kwa moja, kuwa awalipe watu waliokuwa wakimpa vitisho ili aweze kuupata mkanda huo. Benzema yuko chini ya uchunguzi akidaiwa kujuhusisha na sakata hilo ingawa mawakili wake wamesisitiza kuwa mteja wao hana hatia. Mkanda unadaiwa kuwa unawahusisha Valbuena na mpenzi wake.
EUROPA LEAGUE ROUNDUP.
MICHUANO ya Europa League imeendelea tena jana kwa michezo mbalimbali ya hatua ya makundi kuchezwa. Miongoni mwa mechi zilizochezwa ni Liverpool waliokuwa wakicheza na Bordeaux ya Ufaransa ambapo Waingereza hao walichomoza na ushindi wa mabao wa 2-1 ambayo yamefungwa na James Milner pamoja na Christian Benteke. Ushindi huo umeifanya Liverpool kufuzu hatua ya timu 32 za michuano hiyo huku wakiwa wamebaki na mchezo mmoja mkononi. Katika michezo mingine Tottenham Hotspurs waliibugiza Qarabag ya Azerbaijan bao 1-0, Schalke 04 ya Ujerumani ikiifunga Apoel Nicocia ya Cyprus bao 1-0 huku Monaco ya Ufaransa ikiichapa Anderlecht ya Ubelgiji mabao 2-0. FC Augsburg ya Ujerumani wametandikwa mabao 3-2 dhidi ya Athletic Bilbao ya Hispania, Ajax Amsterdam ya Uholanzi imeifunga Celtic ya Scotland mabao 2-1 na FK Krasnodar ya Urusi imeiadhibu Borussia Dortmund ya Ujerumani bao 1-0. Michuano hiyo itaendelea tena December 10 kwa michezo kadhaa ambapo Fenerbache ya Uturuki itaikabili Celtic, Spurs watakuwa wenyeji wa Monaco huku FC Sion ya Uswisi wakiwakaribisha Liverpool.
COE AJITOA KUWA BALOZI WA NIKE.
RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha-IAAF, Lord Coe amesitisha ushirikiano uliodumu kwa miaka 38 na kampuni kongwe ya vifaa vya michezo ya Marekani, Nike. Coe amekuwa balozi wa Nike kwa kipindi chote hicho na hatua ya kusitisha ushirikiano huo unatokana na madai ya mgongano wa kimaslahi kuhusu Eugene, Oregon kupewa uenyeji wa mashindano ta Riadha ya Dunia. Eugene, Oregon ndio yalipo makao makuu ya kampuni kubwa. Coe amesema amefikia hatua hiyo kutokana na minong’ono inayoendelea kwani haina faida kwa Nike wala IAAF. Coe pia ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kama mwneyekiti wa Chama cha Olimpiki cha Uingereza baada ya michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini Rio de Janeiro mwakani.
RUMMENIGGE AMPIGA KIJEMBE GUARDIOLA.
MWENYEKITI wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge jana amesisitiza kuwa hakuna mtu anayekosa mbadala kuelekea katika uamuzi wa mustakabali wa Pep Guardiola. Rummenigge amesema duniani hakuna anayekosa mbadala kwani wachezaji huja na kuondoka na hivyo pia kwa makocha. Guardiola mwenye umri wa miaka 44, yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na amesema atatangaza mipango yake ya baadae na klabu hiyo kabla ya kipindi cha Christmas huku Bundesliga ikitarajiwa kusimama kupisha majira ya baridi Desemba 20 mwaka huu. Rummenigge naye alithibitisha hilo jana na kuongeza kuwa kama uamuzi wa kocha huyo utakuwa vinginevyo ana uhakika watapata kocha mwingine mzuri wa kuendeleza pale atakapoishia yeye. Guardiola ambaye ameshinda mataji 19 akiwa kama kocha kwa klabu za Barcelona na Bayern, amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Ligi Kuu.
Thursday, November 26, 2015
VANA GAAL ATAMBA KUICHAPA WOLFSBURG.
MENEJA wa Manchester United, Louis van Gaal amekiri kikosi chake kinakabiliwa safari ya kwenda Wolfsburg katika mchezo wao wa mwisho wa makundi ya michuano Ligi ya Mabingwa Ulaya Desemba 8 mwaka huu lakini amejitapa kuwa watashinda na kutinga hatua ya timu 16 bora. United iko alama moja nyuma ya Wajerumani hao katika kundi lao kufuatia sare ya bila kufungana waliyopata dhidi ya PSV Eindhoven ya Uholanzi. United sasa watahitajika kushinda ili kusonga mbele kwasababu wana alama moja nyuma ya PSV wanaowafuatia ambao wana rekodi nzuri walipokutana nao. Akihojiwa Van Gaal amesema kila kitu kinawezekana na wana uwezo wa kushinda mahali popote kwani wameonyesha hilo katika Ligi Kuu na sasa wanapaswa kufanya katika michuano hiyo.
CHAMPIONS LEAGUE ROUNDUP.
MECHI za makundi za michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zilichezwa tena jana ambapo timu 16 kutoka makundi makundi manne zilijitupa uwanjani kupigania nafasi za kufuzu hatua ya mtoano. Katika michezo hiyo timu za Real Madrid, Paris Saint-Germain, Atletico Madrid, Benfica, Juventus na Manchester City zilifanikiwa kufuzu hatua ya timu 16 bora baada ya kushinda mechi zao. Madrid wao walisonga mbele kwa kushinda mabao 4-3 dhidi ya dhidi ya Shakhtar Donesk ya Ukraine katika mchezo wa kundi A huku Paris Saint Germain nao wakisonga mbele kwa kuichapa Malmo ya Sweden kwa mabao 5-0. Hali haikuwa nzuri sana kwa timu za Uingereza jana ambapo Manchester United waling’ang’aniwa sare ya bila kufungana na PSV Eindhoven ya Uholanzi huku City wao wakipigwa bao 1-0 na Juventus. United wanaoshika nafasi ya pili katika kundi B watalazimika kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya vinara wa kundi hilo Wolfsburg ya Ujerumani ili waweze kufanikiwa kufuzu huku wenzao City ambao tayari wamefuzu pamoja na kufungwa wao wakitafuta ushindi ili kumaliza vinara katika kundi D kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Borussia Moenchengladbach.
TOURE ADAI JUVENTUS WAMEWAOTEA.
KIUNGO Yaya Toure amesema Juventus walikuwa na bahati kuifunga Manchester City mara mbili katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya mabingwa hao wa Serie A kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo huo uliofanyika jana jijini Turin. Juventus walikuwa tayari wameshawachapa City mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Manchester na kipigo cha jana kimewafanya kuporomoka mpaka nafasi ya pili katika kundi D wakiwa nyuma ya Waitaliano hao. Akihojiwa Toure amesema kiukweli Juventus wamekuwa na bahati kwani katika mechi zote mbili walikuwa na nafasi ya kusawazisha au hata kushinda kabisa. Kiungo huyo aliendelea kudai kuwa ni jambo la kuhuzunisha kwani mchezo ulikuwa unaweza ukaenda upande wowote.
VALDES KUONDOKA MAN UNITED JANUARI.
KIPA wa Manchester United aliyetengwa Victor Valdes amesema anapambana kuwa huru kutoka katika kikosi cha timu hiyo kilicho chini ya meneja Louis va Gaal. Kipa huyo wa zamani wa Barcelona alijiunga na United akiwa mchezaji huru msimu uliopita lakini alisimamishwa na Van Gaal kwa kutokuelewana kufuatia kukataa kucheza katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21. Valdes bado anaendelea na mkataba wake Old Trafford na kutuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa ataendelea kujituma kwa bidii kimyakimya ili aweze kusajiliwa katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Valdes amesema hataki awakatishe tamaa wale ambao wanataka kumuona akicheza tena ndio maana anajituma kwa bidii huku akifurahia kazi yake hiyo.
DROGBA ATAKA KUINOA CHELSEA.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba amesema wana makubaliano ya kurejea katika klabu hiyo pindi atakapostaafu kucheza na anataka kuwa meneja. Drogba ambaye kwasasa anacheza soka lake nchini Canada, amewahi kufunga mabao 164 katika vipindi viwili tofauti alivyoichezea Chelsea. Akihojiwa Drogba mwenye umri wa miaka 37, amesema anataka kulipa fadhila kwa klabu hiyo ambayo ilimpa vitu vingi jambo ambalo amekubaliana na wakurugenzi. Mkongwe huyo aliendelea kudai kuwa anaweza kurejea klabu hapo kuchukua nafasi yeyote kama mkufunzi wa shule ya michezo ya timu hiyo, mshauri wa safu ya ushambuliaji, mkurugenzi wa michezo au hata meneja. Drogba alifunga penati ya ushindi iliyowapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 na kushinda taji la nne la Ligi Kuu katika kipindi chake cha pili alichorejea msimu uliopita kabla ya kujiunga na Montreal Impact inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani-MLS.
FLAMINI ATAMBA KUZIBA VYEMA NAFASI ZA COQUELIN NA ARTETA.
KIUNGO Mathieu Flamini ana uhakika anaweza kuisaidia Arsenal kuziba pengo la majeruhi Francis Coquelin na Mikel Arteta na adhabu muda mwingine wa kucheza utamsaidia kupandisha kiwango chake. Coquelin amesema wakicheza vyema katika safu ya kiungo wa ulinzi lakini anatarajiwa kukaa nje kwa miezi mitatu baada ya kupata majeruhi katika mchezo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya West Bromwich Albion huku Arteta naye akitarajiwa kukaa nje mwezi mmoja baada ya kupata majeruhi katika mchezo huohuo. Flamini ambaye yuko katika msimu wa mwisho katika mkataba wake amepania kuitumia vyema nafasi nafasi hiyo. Akihojiwa Flamini amesema muda mwingine sababu zinaweza kuwa nyingi hivyo inabidi ukubali kukaa benchi lakini ukipata nafasi unapaswa kuonyesha kuwa bado unaweza kucheza katika kikosi cha Arsenal. Arsenal itakabiliwa na kibarua kizito dhidi ya Norwich City katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumapili hii.
PELLEGRINI AMLILIA JOE HART.
MENEJA wa Manchester City, Manuel Pellegrini amesema ni ngumu kujua muda atakaokaa nje Joe Hart baada ya kupata majeruhi jana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao walifungwa na Juventus. Hart mwenye umri wa miaka 28 alibadilishana na golikipa wa kimataifa wa Argentina Wiily Caballero mwneye umri wa miaka 34 katika dakika za majeruhi kwenye mchezo huo waliofungwa bao 1-0. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Pellegrini amesema Hart alipata majeruhi ya msuli hivyo ni ngumu kujua ni muda gani haswa atakaa nje kwa wakati huu lakini kama watamkosa ana imani na Caballero kuziba nafasi yake. Bao pekee katika mchezo huo liliwekwa kimiani na nyota wa Juventus Mario Mandzukic ingwa hata hivyo wote wamefuzu hatua inayofuata katika kundi D.
BLATTER AIVIMBIA KAMATI YA MAADILI.
RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter aliyesimamishwa amedai kuwa anaamini Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo pekee ndio wenye uwezo wa kumuondoa madarakani na sio kamati ya maadili. Akijifananisha na rais wa nchi, Blatter amesema hakuna mtu wa kawaida anayeweza kumfukuza rais aliyechaguliwa zaidi ya bunge pekee. Rais huyo aliendelea kudai kuwa yeye sio ofisa wa wa FIFA bali ni rais aliyechaguliwa katika Mkutano Mkuu na kama kuna mtu habaliani na anavyofanya shughuli zake anapaswa kuwageukia wajumbe wa mkutano huo waliomchagua. Blatter amesema rais wa FIFA huwa anachaguliwa na wajumbe kutoka mashirikisho 209 na kila mmoja wao anapiga kura moja hivyo ni aibu kwake kwa kamati ya maadili kuja maamuzi ya kumsimamisha asiingie ofisini. Blatter alisimamishwa kwa siku 90 sambamba na makamu wake Michel Platini kwa tuhuma ya kufanya malipo yaliyoaminika ya paundi milioni 1.35 kwenda kwa rais huyo wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA mwaka 2011, ingawa wote wawili wamekanusha kufanya lolote baya.
ISCO AFUNGIWA MECHI MBILI.
KIUNGO wa Real Madrid, Isco amepewa adhabu ya kufungiwa michezo miwili jana kwa kosa la kumkwatua nyota wa Barcelona Neymar katika mchezo baina ya timu uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Katika mchezo huo wa La Liga maarufu kama Clasico uliofanyika katika Uwanja wa Santiago Barnabeu, Madrid alibugizwa mabao 4-0. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania, alikuwa ndio kwanza ameingia akitokea benchi katika kipindi cha pili kabla ya kufanya tukio hilo. Adhabu hiyo itamfanya Isco kukosa mechi ya ugenini ambapo Madrid wataifuata Eibar Jumapili hii pamoja na ule dhidi ya Getafe utakaofanyika Desemba 5 mwaka huu.
Wednesday, November 25, 2015
MULLER AWAPIGA BAO MESSI NA RONALDO.
MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Thomas Muller amekuwa mchezaji mdogo zaidi kupata ushindi wa mechi 50 za Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia timu hiyo kuichapa Olympiakos jana. Muller akiwa na umri wa miaka 26 amefikia rekodi hiyo akiwa mdogo kwa mwaka mmoja kuliko Lionel Messi na karibu mdogo kwa miaka miwili kuliko Cristiano Ronaldo. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani ambaye alicheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza Macho mwaka 2009, alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 4-0 waliopata dhidi ya Olympiakos. Akihojiwa Muller ambaye amefikia rekodi kwa kucheza mechi 75, amesema amefikia rekodi hiyo kwasababu anacheza katika klabu nzuri. Naye nahodha wa Bayern Philipp Lahm alimtania Muller kwa kumwambi kuwa anapaswa kuwanunulia vinywaji kwasababu wamekuwa sehemu kubwa ya mafanikio hayo.
ERIKSSON AMTAKA ROONEY KUFIKIRIA KWENDA CHINA.
KOCHA wa zamani wa Uingereza, Sven-Goran Eriksson amesema Wayne Rooney ataipaisha Ligi Kuu ya China na kumtaka mshambuliaji huyo wa Manchester United kufikiria kuhamia huko kama akija kuondoka Old Trafford. Eriksson ambaye kwasasa anainoa klabu ya Shanghai SIPG, amesema mchezo wa soka umekuwa ukiwa kwa kiwango cha kawaida nchini humo lakini ujio wa Rooney unaweza kusaidia kulikuza zaidi soka la huko. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa soka limekuwa kitu kikubwa nchini humo na uwepo wa nyota kama Robinho, Asamoah Gyan na Demba Ba umeleta vitu tofauti katika ligi. Eriksson amesema kutokana na uwezo wa juu alionao Rooney unaweza kulipeleka soka la huko katika viwango vingine.
GERRARD KUANZA MAZOEZI LIVERPOOL WIKI IJAYO.
NGULI wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard amethibitisha kurejea katika klabu hiyo wiki ijayo lakini kwa ajili ya kufanya mazoezi pekee. Kiungo huyo mkongwe wa klabu ya Los Angeles Galaxy mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea kufuatia msimu wa Ligi Kuu ya Marekani-MLS kusimama. Lakini nyota huyo wa zamani wa Uingereza alikanusha tetesi hizo na kudai kuwa atakwenda Anfield kwa ajili ya kufanya mazoezi chini ya meneja wa sasa Jurgen Klopp. Akihojiwa Gerrard amesema ana hamu kubwa ya kujifunza kutoka kwa Mjerumani huyo wakati atapokwenda kufanya nao mazoezi wiki ijayo. Gerrard ameitumikia Liverpool kwa miaka 17 kabla ya kuamua kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita.
DORTMUND KUMPIGANIA AUBAMEYANG.
KLABU ya Borussia Dortmund imedai itapambana kufa na kupona kuhakikisha wanabaki na mshambuliaji wao nyota Pierre Emerick Aubameyang. Vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya tayari vimeanza kummezea mate nyota huyo wa kimataifa wa Gabon kutokana na kiwango kikubwa katika ufungaji walichokionyesha msimu huu. Ofisa mkuu wa Dortmund Hans-Joachim Watzke amesema watapambana kadri wawezavyo kuhakikisha wanabaki na nyota huyo ambaye mpaka ameshafunga mabao 22. Watzke aliendelea kudai kuwa wachezaji wengine watakaopambana ili kuwabakisha ni pamoja na Matis Hummels, Ilkay Gundogan, Marko Reus na Henrikh Mkhitaryan.
KIPA WA ROMA AIFAGILIA BARCELONA.
GOLIKIPA wa AS Roma, Wojciech Szczesny amekiri kuwa kikosi chao kilikuwa kikicheza dhidi ya timu kutoka sayari nyingine baada ya Barcelona kuwararua kwa mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa jana. Szczesny alikosa nguvu ya kuwazuia Barcelona waliokuwa katika kiwango chao cha juu katika mchezo huo uliochezwa Camp Nou, huku nyota wake Lionel Messi na Luis Suarez wakifunga mabao mawili kila mmoja. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Szczesny amesema uliokuwa mzuri kuutizama kwasababu walikuwa wakicheza dhidi ya timu kutoka sayari nyingine. Kipa huyo aliendelea kudai kuwa alikuwa langoni akiichezea Roma lakini anafurahia alichokiona kwa timu pinzani kwani walikuwa wakicheza vyema na ilikuwa raha kuwatizama hata kama wamefungwa.
MOURINHO ALAUMU NYASI ZA UWANJA KUFUATIA TERRY KUUMIA.
MENEJA wa Chelsea, Jose Mourinho amelaumu nyasi za uwanja kusababisha majeruhi ya kifundo cha mguu ambayo yanaweza kumzuia nahodha John Terry kutocheza katika mchezo wa Ligi Kuu Jumapili hii dhidi ya Tottenham Hotspurs. Terry mwenye umri wa miaka 34 alitolewa nje katika machela katika dakika ya 72 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Maccabi Tel Aviv ambao walishinda mabao 4-0. Akihojiwa Mourinho amesema anafahamu kikubwa kilichosababisha Terry kuumia katika mchezo huo ni hali mbaya ya uwanja. Mapema kabla ya mchezo huo kocha huyo alilaumu uwanja huo wa Sammy Ofer kuwa na nyasi mbaya kufuatia kiungo wake Ramires kuumia wakati wa mazoezi Jumatatu.
CHAMPIONS LEAGUE ROUND UP.
MABINGWA watetezi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa, Barcelona jana wamefanikiwa kufuzu hatua ya timu 16 bora kufuatia ushindi mnono waliopata dhidi ya AS Roma ya Italia. Katika mchezo huo Barcelona wakiwa katika ubora wao waliwachakaza waitaliano hao kwa mabao 6-1 ambayo yalifungwa kwa ustadi mkubwa na Luis Suarez na Lionel Messi waliofunga mawili kila mmoja pamoja na Gerard Pique na Adriano. Barcelona waligundua mapema kuwa wamefuzu hatua ya mtoano kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliofanyika Camp Nou kufuatia BATE Borisov kutoka sare ya bao 1-1 na Bayer Liverkusen ya Ujerumani katika mchezo uliofanyika mapema huko Belarus. Wengine waliofanikiwa kufuzu jana ni mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich ambao bila ya huruma waliichakaza Olympiakos kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika Allianz Arena na kutoa mwanya kwa Arsenal walioshinda mchezo wao dhidi ya Dinamo Zagreb kwa mabao 3-0 kufufua upya matumaini yao ya kufuzu. Kama Bayern na Olympiakos wangetoka sare katika mchezo huo wote wawili wangefuzu hatua inayofuatia hivyo kuwaacha Arsenal wakiangukia katika michuano ya Europa League. Nao mabingwa Ligi Kuu Chelsea walikwea kileleni mwa kundi G kwa kuwachapa vibonde Maccabi Tel Aviv ya Israel kwa mabao 4-0 huku mchezo mwingine wa kundi hilo ukishuhudia Dynamo Kiev ya Ukraine wakiicharanga FC Porto ya Ureno kwa mabao 2-0.
WARRIORS WAWEKA REKODI YA KUTOFUNGWA NBA.
TIMU ya Golden State Warriors imeweka rekodi ya kutofungwa toka kuanza kwa msimu mpya wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani-NBA kwa ushindi mnono dhidi ya Los Angeles Lakers. Warriors walishinda mchezo huo uliofanyika jana kwa vikapu 111-77 na kuongeza rekodi yao nzuri ya ushindi katika mechi 16 walizocheza za NBA mpaka sasa. Ushindi huo unamaanisha Warriors wamevunja rekodi ya pamoja iliyowekwa na Houston Rockets msimu wa 1993-1994 pamoja na Washington Capitals msimu wa 1948-1949. Nyota wa Warriors anayeshikilia tuzo ya Mchezaji mwenye Thamani Zaidi-MVP, Stephen Curry alifunga alama 24 katika mchezo huo. Warriors sasa wanawinda kuivunja rekodi ya kushinda mechi 33 mfululizo iliyowekwa na Lakers katika msimu wa kawaida wa NBA mwaka 1972.
Tuesday, November 24, 2015
WENGER KUIPA UZITO EUROPA LEAGUE KAMA LIGI YA MABINGWA.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema ataipa uzito mkubwa michuano ya Europa League kama waking’olewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Arsenal wako wanasuasua katika kundi F wakiwa na alama tatu pekee katika michezo minne waliyocheza na wanatarajiwa kucheza na Dinamo Zagreb baadae leo wakijuwa kuwa wanaweza kutolewa kama wakifungwa. Nafasi ya tatu katika kundi hilo itawapeleka Arsenal katika Europa League na Wenger amesema hadhani kama kushiriki michuano hiyo kutaathiri dhamira yao ya kupigania taji la Ligi Kuu. Akihojiwa Wenger amesema kama kikosi chake kikienguliwa na kwenda kushiriki michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Ulaya basi hakuna kuwa ataipa uziti unaostahiki.
PIGO ARSENAL, COQUELIN NJE MIEZI MIWILI.
KLABU ya Arsenal imepata pigo kufuatia taarifa kuwa kiungo wake Francis Coquelin anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi miezi miwili kutokana na majeruhi ya goti. Meneja wa Arsenal Arsene Wenger alitangaza kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 24 alipata majeruhi hayo katika mchezo waliofungwa mabao 2-1 dhidi ya West Bromwich Albion Jumamosi iliyopita. Kiungo huyo sasa anatarajiwa kukosa mechi zote za mwezi ujao lakini Wenger ana matumaini makubwa kuwa ataweza kurejea uwanjani mapema kuliko inavyodhaniwa kutokana na vipimo alivyofanyiwa. Katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Wenger atakuwa na nafasi ya kusajili kiungo mwingine kuziba nafasi hiyo lakini mwenyewe amesisitiza kuwa tayari ana viungo wa kutosha katika kikosi chake kuziba nafasi hiyo.
GERRARD KUICHEZEA TENA LIVERPOOL.
KIUNGO mkongwe wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard anatarajiwa kuichezea tena klabu hiyo lakini katika kikosi cha manguli waliowahi kuichezea timu hiyo. Nahodha huyo wa zamani anatarajiwa kuwepo katika kikosi hicho cha manguli kitakachokwenda jijini Sydney sambamba na wakongwe wenzake kama Jamie Carragher na Ian Rush kwa ajili ya mchezo dhidi ya manguli wa Australia utakaochezwa Januari 7 mwakani. Kwasasa Gerrard yuko likizo kufuatia msimu wa Ligi Kuu ya marekani-MLS kumalizika ambapo anatarajiwa kurejea tena nchini humo Januari 15 wakati timu yake ya Los Angeles Galaxy itakapoanza mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya. Akihojiwa Gerrard amesema ni jambo kubwa kucheza katika kikosi rasmi cha wachezaji wakongwe hivyo ana hamu kubwa kukutana na wenzake ambao aliwahi kucheza nao. Mkongwe huyo aliendelea kudai kuwa mashabiki wa Liverpool ni bora na kucheza mbele yao tena litakuwa jambo la kipekee.
RONALDO HAENDI KOKOTE - MENDES.
WAKALA wa mshambuliaji Cristiano Ronaldo, Jorge Mendes amesema litakuwa suala lisilowezekana kwa nyota huyo wa kimataifa wa Ureno kuondoka Real Madrid na kuhamia Paris Saint-Germain –PSG wakati Monaco wakiamini kuwa hawana nafasi ya kumsajili. Ronaldo mwenye umri wa miaka 30, alizomewa na mashabiki wakati walipopokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka Barcelona katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, hivyo kuongeza tetesi za mustakabali wa nyota huyo. Miezi ya hivi karibuni, Ronaldo anayeongoza kwa mabao katika labu hiyo amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia kwa mabingwa hao wa Ufaransa lakini Mendes amekuwa akisisitiza kuwa Ronaldo atabakia nchini Hispania mpaka atakapotundika daruga zake. Akihojiwa kuhusiana na tetesi hizo Mendes amesema ni suala lisilowezekana kwa Ronaldo kuondoka Madrid kwania anatarajia kumalizia soka akiwa hapo.
PSG KUVAA JEZI MAALUMU KUKUMBUKA WALIOPOTEZA MAISHA KATIKA MASHAMBULIO YA PARIS.
WACHEZAJI wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG wanatarajiwa kuvaa fulana maalumu katika mechi zao mbili zitakazokuja kwa ajili ya kutoa heshima zao kwa wale waliofariki katika mashambulio ya kigaidi jijini Paris. Fulana hizo zitakuwa na ujumbe maalumu wenye maandishi ya kifaransa yanayosomeka kama Je suis Paris wakimaanisha mimi ni Paris. Mabingwa hao wa Ufaransa wamedai kufanya hivyo ili kuonyesha umoja wao pamoja na jamii ya kimataifa ya soka. PSG watakwaana na Malmo ya sweden katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho kabla ya kuikaribisha Troyes katika mchezo wa Ligue 1 Jumamosi hii.
BLATTER, PLATINI WAKABILIWA NA ADHABU YA KUFUNGIWA MIAKA SABA.
RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter na makamu wake Michel Platini ambao wote wamesimamishwa, wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kufungiwa miaka saba kama wakikutwa na hatia ya tuhuma za rushwa zinazowakabili. Wachunguzi wa kamati ya maadili ya FIFA kuna uwezekano mkubwa wakapendekeza adhabu juu ya malipo yasiyo ya uaminifu ambayo yalishuhudia Platini akilipwa paundi milioni 1.35 na Blatter. Kulikuwa hakuna mkataba wowote wa maandishi kufafanua malipo hayo ambayo Platini alipokea miaka tisa baadae. Kamati ya uamuzi inatarajiwa kutangaza matokeo ya uchunguzi huo majira ya Christmas. Wawili hao ambao wamesimamishwa kwa siku 90 wamekanusha kufanya jambo lolote baya wakifafanua kuwa malipo hayo yalifanyika kwa kwa kuaminiana kutokana na kazi iliyofanyika.
RAIS WA MADRID AMKINGIA KIFUA BENITEZ.
MENEJA wa Real Madrid Rafa Benitez ataendelea na kibarua cha kuinoa timu hiyo kama kawaida baada ya kuungwa mkono na rais wa klabu Florentino Perez. Shinikizo kubwa lilikuwa likimkabili kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 kufuatia kikosi chake kukubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa mahasimu wao Barcelona uliofanyika katika Uwanja wa Santiago Bernabeu. Mara baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa mashabiki wa Madrid walianza kuwazomea wachezaji huku wakipunga juu vitambaa vyeupe. Akihojiwa Perez amesema walifanya kikao cha bodi na kufanya tathmini ya hali inavyoendelea katika klabu hiyo na wameamua kumuunga mkono kocha huyo na kumpa msaada wowote ataohitaji. Perez aliendelea kudai kuwa Benitez ndio kwanza ameanza kibarua hivyo wana uhakika na uwezo wake kuwa ataweza kufikia malengo waliojiwekea.
Friday, November 20, 2015
EL CLASICO HAPATOSHI KESHO.
WINGA wa Real Madrid, Gareth Bale amesema yuko tayari kwa mapambano wakati kikosi chao kikijiandaa kwa ajili ya mchezo wa Clasico dhidi ya mahasimu wao Barcelona kesho. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales, mwenye umri wa miaka 26, alikuwa amepata majeruhi ya nyonga Octoba mwaka huu na kukosa michezo minne kabla ya katika mchezo waliofungwa na Sevilla Novemba 8. Akihojiwa Bale amesema amekuwa majeruhi kwa wiki sita hivyo hajapata muda wa kutosha kucheza msimu huu lakini anajisikia imara na fiti kwa ajili ya mchezo wa kesho. Madrid watakwenda katika mchezo huo wakiwa alama tatu nyuma ya Barcelona ambao wanaweza kuwa na mshambuliaji wao nyota Lionel Messi baada ya kupona majeruhi ya goti waliyopata Septemba mwaka huu. Messi ambaye ndio mfungaji kinara wa Clasico akiw na mabao 21, amerejea mazoezini na anaweza kurejea katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona sambamba na nyota wenzake Luis Suarez na Neymar. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ulinzi wa hali ya juu kufuatia tukio ya mashabulio ya kigaidi ya Paris, ambapo karibu walinzi wa kujitegemea 1,500 wanatarajiwa kufanya kazi wakati wa mchezo huo wakishirikiana na polisi wapatao 1,000.
CORINTHIANS MABINGWA WAPYA BRAZIL.
KLABU ya Corinthians wametawadhwa mabingwa wapya wa Brazil jana baada ya sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Vasco da Gama na kusaidiwa na kipigo cha mabao 4-2 walichpata Atletico Mineiro dhidi ya Sao Paulo ambacho kimewafanya kuongoza kwa alama 12 huku zikiw zimesalia mechi tatu. Corinthians ndio vinara wa mabao katika ligi na safu imara ya ulinzi huku pia wakiwa wameshinda mechi nyingi zaidi na kufungwa chache kuliko timu nyingine yeyote. Klabu hiyo hiyo imenyakuwa taji hilo ambalo ni la sita kwao wakiwa wanaongoza kwa alama 77 wakati Atletico waliokuwa wakifuatia wakiwa na alama 65. Akihojiwa golikipa wa Corinthians aliwapongeza wachezaji wenzake kwa jinsi walivyojituma na kuongeza kuwa walistahili taji hilo.
KOSCIENY HATIHATI KUIVAA WEST BROM KESHO.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa beki wa kati Laurent Koscielny ameathirika kwa kiasi kikubwa na tukio la mashambulio lililotokea jijini Paris na anaweza kumpumzisha katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya West Bromwich Albion kesho. Koscielny alikuwepo katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kilichokuwa kikicheza na Ujerumani huko Stade de France wakati tukio la mashambulio hayo lilipotokea na wakati wakicheza na Uingereza Jumanne, Wenger alibaini kuwa akili ya mchezaji huyo ilikuwa mahali pengine. Akihojiwa Wenger amesema Koscielny alicheza vyema katika mchezo dhidi ya Ujerumani lakini kwa jinsi alivyomuona katika mchezo wa Jumanne usiku hakuwa mwenyewe. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anadhani ameathirika kwa kiasi kikubwa hivyo hatafanya haraka kumtumia mpaka atakaporidhika kwamba yuko tayari.
WENGER ATAKA VIPIMO ZAIDI KUNG'AMUA WADANGANYIFU KATIKA SOKA.
MENEJA w Arsenal, Arsene Wenger anataka vipimo bora kwa ajili ya kugundua wachezaji wadanganyifu katika soka na kutaka vipimo vya damu view vikifanyika mara kwa mara. Chama cha Soka Uingereza-FA kilimtaka Wenger mwenye umri wa miaka 66, kufafanua kauli yake aliyotoa kuhusu dawa za kusisimua misuli katika mahojiano na gazeti moja la Ufaransa. Kocha huyo raia wa Ufaransa amesema yuko tayari kuzungumza na FA kwasababu anataka vipimo vifanyike kwa undani zaidi na juu juu kama hivi sasa ili kuweza kulikabili vyema tatizo hilo. Kiungo wa Dinamo Zagreb, Arijan Ademi alishindwa vipimo kufuatia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya walioshinda dhidi ya Arsenal Septemba mwaka huu. Na Wenger akihojiwa kuelekea mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya West Bromwich Albion, amesema ni ujinga kudhani soka halina masuala ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kama michezo mingine.
SINA MPANGO WA KUREJEA LIVERPOOL AU KLABU YEYOTE ULAYA - GERRARD.
NAHODHA wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard amesema kuwa hatarajii kusaini mkataba Anfield au klabu yeyote nyingine barani Ulaya Januari mwakani. Gerrard mwenye umri wa miaka 35, alijiunga na Los Angeles Galaxy baada ya mkataba wake kumalizika Liverpool majira ya kiangazi na msimu wake wa kwanza Ligi Kuu ya Marekani-MLS umemalizka hivi karibuni baada ya timu yake kumaliza katika nafasi ya tano katika Ukanda wa Magharibi. Nahodha huyo wa zamani wa Uingereza amekuwa akihusishwa na tetesi za kufanya usajili wa muda Liverpool wakati huu ambao msimu MLS umemalizika lakini Gerrard alirudia kauli kama aliyotoa meneja wa klabu hiyo Jurgen Klopp kuwa hatarejea kuitumikia timu hiyo. Gerrard amesema ameshastaafu kuitumikia timu ya taifa hivyo hana chochote cha kuonyesha barani Ulaya. Mkongwe huyo aliendelea kudai kuwa anachotaka hivi sasa ni kupumzika kwasababu anakabiliwa na msimu mrefu mwakani hivyo ni muhimu kwake kurejea akiwa imara.A
NITASHINDA VITA YA SARATANI - CRUYFF.
NGULI wa zamani wa soka wa Uholanzi, Johan Cruyff amesema ana imani kubwa atashinda mapambano yake dhidi ya maradhi ya saratani ya mapafu yanayomsumbua. Nguli huyo mwenye umri wa miaka 68 na mshindi wa tuzo tatu za Ballon d’Or aligundulika maradhi hayo mwezi uliopita. Akihojiwa Cruyff ambaye amewahi kucheza na kuwa kocha katika klabu za Ajax Amsterdam na Barcelona, amesema ana uhakika kila kitu kitakwenda sawa kwani anajisikia vyema. Cruyff aliendelea kudai kuwa matibabu ya mionzi aliyoanza ameyafanya kuwa rafiki yake kwasababu yanakwenda kuua maradhi hayo. Nguli huyo aliisaidia nchi yake Uholanzi kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1974 ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi.
WIMBO WA TAIFA WA UFARANSA KUPIGWA KATIKA MECHI ZA LIGI KUU.
WIMBO wa taifa wa Ufaransa wa La Marseillaise, unatarajiwa kupigwa kabla ya mechi zote za Ligi Kuu ya Uingereza mwishoni mwa wiki hii. Wimbo huo utaimbwa baada ya sarafu kurushwa kuamua nani ataanzisha mchezo, huku wachezaji wa timu zote mbili wakikusanyika kwenye duara katikati ya uwanja pamoja na waamuzi. Afisa mkuu wa Ligi ya Kuu Richard Scudamore amesema hatua hiyo ni ya kuunga mkono Ufaransa na kutoa heshima kwa wahanga wa tukio ya mashambulio ya kigaidi yaliyotokea huko Paris na kuuwa watu zaidi ya 129 Ijumaa iliyopita. Wimbo wa La Marseillaise pia ulichezwa wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati Uingereza na Ufaransa Jumanne katika Uwanja wa Wembley ambapo wenyeji Uingereza walishinda mabao 2-0. Kuna wachezaji 72 wanaocheza katika Ligi Kuu ambao wanatoka Ufaransa.
BOLT ATAKA MAJARIBIO MAN UNITED.
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi wa Jamaica, Usain Bolt anaamini yeye ndio jibu la matatizo ya Manchester United, akidai kuwa atapewa mkataba wa miaka mitano kama akifanyiwa majaribio Old Trafford. Mara kadhaa nyota huyo ameonyesha nia ya kutaka kuichezea klabu hiyo wakati Sir Alex Ferguson akiwa kocha Old Trafford. Hata hivyo, bingwa huyo wa medali sita za dhahabu za olimpiki anaamini kuwa sasa yuko katika nafasi nzuri na kumtaka meneja wa sasa Louis van Gaal kumpa nafasi kuonyesha thamani yake. Akihojiwa Bolt amesema katika mawazo yake anadhani anapaswa kufanya majaribio na kuona kama watakubali au watakaa kwa kuona hafai. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa anadhani yuko vizuri kwasababu yuko fiti, ana kasi, anaweza kumiliki mpira na kuelewa sheria zote za mchezo.
Thursday, November 19, 2015
NASRI NJE MPAKA FEBRUARI.
KIUNGO wa Manchester City, Samir Nasri ametangaza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa hategemei kucheza mechi yeyote ya kimashindano katika miezi mitatu ijayo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alipata majeruhi ya msuli katika mchezo wa Ligi Kuu walioshinda mabao 5-1 dhidi ya Bournemouth mwezi uliopita. Meneja wa City, Manuel Pellegrini alikuwa na matumaini kuwa Mfaransa huyo angeweza kurejea uwanjani katika mchezo wao dhidi ya Liverpool mwishoni mwa wiki hii. Lakini sasa matumaini hayo yanaonekana kufifia baada ya kiungo huyo kuweka wazi hataweza kurejea uwanjani mpaka Februari mwakani.
Subscribe to:
Posts (Atom)