Thursday, January 31, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF.

KIM ATEUA 21 STARS WA KUIVAA CAMEROON
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili (Februari 3 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable Lions). Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi mwaka huu. “Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonyesha wako tayari. “Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la Dunia. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia. Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar). Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

SAMBA AFAULU VIPIMO VYA AFYA QPR.

KLABU ya Queens Park Rangers inakaribia kukamilisha uhamisho wa beki Christopher Samba kutoka klabu ya Anzhi Makhachkala baada ya kufikia makubaliano na mchezaji huyo kufaulu vipimo. Beki huyo wa zamani wa Blackburn mwenye umri wa miaka 28 amesajili kwa ada ya paundi milioni 12.5 ambapo atakuwa akipokea kitita cha paundi 100,000 kwa wiki ikiwemo posho na mambo mengine. Nyota huyo alithibitisha kufanyiwa vipimo vya afya jijini London katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter jana. Mbali na Samba lakini pia meneja wa QPR Harry Redknapp yuko mbioni kumfukuzia mshambuliaji wa klabu ya Stoke City Peter Crouch.

KAGAWA AITWA TENA JAPAN.

KIUNGO nyota wa klabu ya Manchester United, Shinji Kagawa ameitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya Japan kitakachocheza mchezo wa kirafiki na Latvia Jumatano ijayo baada ya kupona na kurejea katika kiwango. Kagawa alikosa baadhi ya michezo ya nchi yake ukiwemo mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ambao walipata ushindi mwembamba wa mabao 2-1 dhidi ya Oman Novemba mwaka jana kwasababu majeraha ya mguu aliyopata wakati anaichezea United. Kagawa alirejea katika kikosi cha United Desemba baada ya kupona na ameonyesha kurejea katika kiwango chake wakati timu yake hiyo ikiongoza Ligi Kuu nchini Uingereza kwa alama saba zaidi ya mahasimu wao Manchester City wanaoshika nafasi ya pili. Kocha wa Japan Alberto Zaccheroni amesema amekuwa akimfuatilia nyota huyo katika mechi alizocheza karibuni na ameshawishika kumuita tena kuimarisha kikosi chake baada ya kurejea katika kiwango chake.

ADEBAYOR AIPONDA CAF KUHUSU UWANJA WA MBOMBELA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amewabwatukia Shirikisho la Soka la Barani Afrika na Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon kwa hali mbaya ya Uwanja wa Mbombela uliopo jijini Nelspruit. Adebayor ambaye anacheza katika klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza aliulalamikia uwanja huo kuwa na mchanga na mabonde baada ya Togo kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo watacheza na Burkina Faso Jumapili. Mbali na Adebayor, nahodha wa timu ya taifa ya Zambia Christopher Katongo naye alilalakia uwanja huo mapema wiki hii akidai kuwa inafanya timu yake ishinde kucheza mchezo wake wa kupasiana kama walivyozoea. Adebayor alidai michuano ya Afcon ni mikubwa barani Afrika na dunia nzima wanaangalia hivyo kuwa na viwanja vya aina hiyo ni jambo la kusikitisha. Nyota huyo amesema CAF lazima litafutie ufumbuzi suala hilo haraka ili wasiitie doa michuano hiyo ambayo mpaka sasa inaendelea vyema.

NFF YAWAJAZA MAPESA WACHEZAJI SUPER EAGLES.

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles wamepokea posho ya dola 30,000 kila mmoja kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini humo-NFF baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon. Nigeria iliigaragaza Ethiopia kwa mabao 2-0 na kufanikiwa kusonga mbele pamoja na Burkina Faso katika Kundi na kuziacha Ethiopia pamoja na mabingwa watetezi wa michuano hiyo kuyaaga mashindano hayo. Nigeria imeshiriki Afcon mara 17 na kufanikiwa kuvuka hatua ya makundi mara 15 na sasa nchi hiyo itakwaana na Ivory Coast timu ambayo inapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji la michuano hiyo. Pamoja na Ivory Coast kupewa nafasi kubwa lakini kocha Nigeria Steven Keshi amesema ameandaa mbinu madhubuti ya kupambana na wapinzani wao ili kuhakikisha wanasonga mbele kwenye michuano hiyo.

BWALYA ASIKITISHWA NA KUTOLEWA KWA ZAMBIA.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Zambia, Kalusha Bwalya amesema amesikitishwa na matokeo ya timu ya taifa ya nchi hiyo yaliyopelekea kuvuliwa ubingwa wao katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea. Zambia walilazimishwa sare ya bila ya kufungana na Burkina Faso katika mchezo wao wa mwisho wa kundi C uliochezwa katika Uwanja wa Mbombela na matokeo hayo yalishindwa kuwavusha kwenda robo fainali baada ya Nigeria kuifunga Ethiopia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo uliochezwa katika Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg. Kalusha aliuambia mtandao wa shirikisho hilo kuwa wachezaji wa timu hiyo inabidi wajilaumu wenyewe kwa kutolewa mapema kwasababu hakuna timu yoyote kwenye mashindano hayo iliyopata maandalizi mazuri kama wao. Kalusha ambaye aliwahi kuwa mchezaji nyota wan chi hiyo amesema waliiandaa timu kwa muda wa kutosha na mategemeo yao ilikuwa ni kufika mbali zaidi ikiwezekana kutetea taji hilo lakini imeshindikana. Kwasasa Kalusha amesema inabidi wasahau michuano hiyo na kuhakikisha wanajiandaa vyema zaidi ili waweze kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil 2014.

Reading vs Chelsea 2-2 Goals And Highlights 30.01.2013

Real Madrid vs Barcelona 1-1 All Goals and Highlights 30/01/2013

Arsenal vs Liverpool 2-2 30/01/2013 All Goals & Full Highlights

Togo vs Tunisia 1:1 Goals and Highlights 30.01.2013 CAN2013

Algeria VS Ivory Coast 2-2 All Goals & Full Highlights 30-1-2013 HD

Wednesday, January 30, 2013

OBI MIKEL ATAMBA NIGERIA KUCHUKUA AFCON.

KIUNGO nyota wa kimataifa wa Nigeria, John Obi Mikel amedai kuwa timu yake ya taifa itaibuka kidedea katika michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini baada ya kutinga hatua ya robo fainali. Nigeria ilifanikiwa kutinga hatua hiyo jana baada ya kuibugiza Ethiopia kwa mabao 2-0 na sasa wanakabiliwa na mchezo dhidi ya Ivory Coast ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la michuano hiyo kutokana nyota wake waliosheheni kwenye kikosi chake. Obi Mikel amesema kutokana na kiwango cha hali walichocheza katika mchezo dhidi ya Ethiopia ana imani kuwa wanaweza kuvuka kikwazo kilichopo mbele yao kama wakiendeleza juhudi zilezile. Nigeria imemaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi C ambalo linaongozwa na Burkina Faso.

SHENHUA KUMSHITAKI DROGBA FIFA.

KLABU ya Shanghai Shenhua ya China imedai kuwa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Ivory Coast Didier Drogba hana haki ya kusaini mkataba katika klabu ya Galatasaray ya Uturuki kwakuwa bado hajamaliza mkataba wake. Galatasaray walithibitisha Jumatau kuwa Drogba mwenye umri wa miaka 34 ameshakubali kusaini mkataba wa miezi 18 na klabu hiyo unaokadiriwa kufikia kiasi cha euro milioni sita huku kiasi euro milioni nne akikabidhiwa nyota huyo. Hatahivyo Shenhua ambao walimsajili Drogba baada ya kuondoka Chelsea katika kipindi cha majira ya kiangazi msimu uliopita walionyesha kushangazwa na taarifa hizo na wameamua kulipeleka Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA ili lipate ufumbuzi. Kwasasa Drogba yuko ya timu yake ya taifa katika michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini huku timu yake ikiwa tayari imesonga mbele katika hatua ya robo fainali baada ya kushinda michezo yake miwili ya kwanza.

Tuesday, January 29, 2013

MESSI KUSAINI MKATABA BARCELONA.

RAIS wa klabu ya Barcelona, Sandro Rosell amesema kuwa mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Lionel Messi anatarajiwa kuongeza mkataba wiki ijayo. Mkataba huo mpya ambao Messi anatarajiwa kusaini utamuweka katika klabu hiyo mpaka 2018 lakini Rosell alibainisha kuwa hakuna klabu yoyote iliyokuja kutaka kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Argentina. Rosell amesema klabu haijapokea maombi yoyote ya mchezaji huyo kutoka vilabu vingine na ana uhakika kama wapo waliomfuata lazima atakuwa amewakatalia. Messi mwenye umri wa miaka 25 anakuwa mchezaji wa tatu ndani ya wiki moja kukubali kusaini mkataba mpya kufuatia habari kuwa Carles Puyol na Xavi Hernandez nao kukubali kuongeza mikataba yao na Rosell ana uhakika golikipa Voctor Valdes naye atafuata nyayo hizo.

USALAMA NI JAMBO LINALOPEWA KIPAUMBELE - VALCKE.

MAOFISA wa ngazi za juu wa michezo wamesisitiza kuwa usalama litakuwa jambo linalopewa kipaumbele nchini Brazil katika michuano ya Kombe ya Dunia na Olimpiki ikiwa ni tahadhari kufuatia moto uliozuka katika klabu moja ya usiku na kuua watu wapatao 231. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa ajali iliyotokea huko Santa Maria mji uliopo kusini mwa nchi hiyo ni mojawapo ya ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea. Hatahivyo Valcke amesema ajali hiyo ya moto haihusiani na usalama ndani ya viwanj ambavyo vitatumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi June 15 hadi 30 mwaka huu pamoja na ile ya Kombe la Dunia mwakani. Amesema katika michuano hiyo wameandaa watu na kuwapa mafunzo ya kutosha na kuwa na uwezo kuwaondoa watu waliojaa uwanjani katika muda wa dakika nane pindi tukio la hatari linapotokea. Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa kamati ya maandalizi ya michuano ya Olimpiki 2016, Carlos Vilanova amesema tukio la moto lililotokea linaweza kutokea mahala popote duniani na wala halihusiani na uwezo wa Brazil kuandaa mashindano makubwa. Vilanova amesema nchi hiyo imekuwa ikiandaa matamasha makubwa kwa miaka mingi kama Rio Carnaval na mafataki yanayorushwa katika kipindi cha mwaka mpya kwenye ufukwe wa Copacabana ambao hukusanya watu zaidi ya milioni mbili lakini hakujawahi kutokea tukio lolote baya.

STARS KUCHUANA NA CAMEROON.

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na Cameroon mchezo ambao utapigwa Jumatano ijayo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi inatarajiwa kuwa na nyota wote wan chi hiyo akiwemo mshindi mara nne wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika Samuel Eto’o na kiungo wa Barcelona Alex Song ambao wote wamejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 21 walioitwa. Mabingwa hao wa zamani wa Afrika wanatarajiwa kukutana jijini Amsterdam kabla ya kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao na Taifa Stars. Shirikisho a Soka nchini-TFF lipo katika mchakato wa maandalizi ya mchezo huo ambao katika siku chache zijazo kila kitu kitakuwa tayari. Cameroon ilishindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya kutolewa na Cape Verde ambao wametinga robo fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Afrika Kusini.

USHINDI LAZIMA NA UWEZO TUNAO - RENARD.

KOCHA wa mabingwa watetezi wa michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon Zambia, Herve Renard amesema kuwa ni lazima wapate ushindi katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Burkina Faso utakaochezwa katika Uwanja wa Mbombela baadae leo. Renard amesema wapinzani wao Burkina faso wanahitaji sare yoyote ili wasonge mbele huku wao wakihitaji ushindi wa aina yoyote lakini hilo haliwakatishi tamaa kwani walishakutana na hali kama hiyo katika michuano hiyo mwaka jana. Kocha huyo alitamba kuwa kikosi chake kinaweza kushinda mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa baadae leo na kuweka matumaini ya kutetea taji lao kwa kusonga mbele katika hatua ya robo fainali. Katika mchezo mwingine wa Kundi C Nigeria nao watakuwa na kibarua kigumu wakati watakapocheza na Ethiopia jijini Rustenburg ambapo yoyote atakayepata ushindi kwenye mchezo huo atasonga mbele kwenye hatua ya robo fainali.

Monday, January 28, 2013

ABIDAL ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI BAADA YA UCHUNGUZI.

BEKI wa kushoto wa klabu ya Barcelona, Eric Abidal ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kufanyiwa vipimo kufuatia upasuaji wa kupandikiza moyo aliofanyiwa April mwaka jana. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa aligundulika kuwa na uvimbe wa kansa katika ini lake Machi 2011 ambao ulimhitaji kufanyiwa upasuaji mkubwa lakini upasuaji huo haukutatua tatizo hilo moja kwa moja. Mwaka mmoja baadae klabu yake ilitangaza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 atatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini jingine na mwezi mmoja baada alifanyiwa upasuaji huo uliokuwa na mafanikio. Abidal anategemewa kujiunga na wenzake mazoezini wiki ijayo baada ya kufanyiwa vipimo kuangalia maendeleo ya ukuaji wa ini lake jipya ambalo alipewa na mpwa wake. Beki huyo hatacheza mchezo wowote wa mashindano toka Februari mwaka jana wakati wa mchezo baina ya Barcelona na Atletico Madrid ambao walishinda kwa mabao 2-1. 

GALATASARAY YAKIRI KUMNYATIA DROGBA.

KLABU ya Galatasaray ya Uturuki imethibitisha kuwa wako katika mazungumzo ya kuangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji mkongwe wa kimataifa wa Ivory Coast Didier Drogba. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo ulidai tayari wamwshaanza mazungumzo rasmi juu ya uhamisho wa nyota huyo kutoka klabu ya Shanghai Shenhua ya China. Kuna tetesi zimeripotiwa katika magazeti ya huko yakidai kuwa wamefikia makubaliano na nyota huyo na atapatiwa mkataba wa miezi 18 huku akipewa posho ya euro 30,000 katika kila mchezo ataocheza. Drogba mwenye umri wa miaka 34 aliondoka Chelsea kwenda China mwaka jana baada ya kuisadia Chelsea kunyakuwa taji lake la kwanza la michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya.

RANI KHEDIRA AONGEZWA MKATABA STUTTGART.

KLABU ya VfB Stuttgart ya nchini Ujerumani imetangaza kumuongeza mkataba utakaofikia tamati 2015 kinda wake Rani Khedira ambaye ni mdogo wa nyota wa kimataifa wa Ujerumani na klabu ya Real Madrid Sami Khedira. Rani ambaye ametimiza miaka 19 Jumapili iliyopita tayari amepandishwa katika kikosi cha kwanza cha Stuttgart ingawa kiungo huyo bado hajacheza mchezo wowote katika Ligi Kuu nchini Ujerumani maarufu kama Bundesliga. Kiungo huyo ambaye yuko katika kikosi cha vijana chini ya miaka 19 cha nchi hiyo amesifiwa na Mkurugenzi wa Michezo wa Stuttgart Fredi Bobic kama mchezaji mwenye kipaji na atakaekuwa na uwezo mkubwa kusakata kabumbu katika siku za usoni. Sami Khedira ambaye ameshacheza michezo 36 ya kimataifa na Ujerumani alicheza katika klabu ya Stuttgart kwa kipindi cha miaka 15 kabla ya nyota huyo mwenye miaka 25 kutimkia Madrid baada ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010.

GRELLA ATUNDIKA DARUGA.

KIUNGO wa kimataifa wa Australia, Vince Grella ambaye pia amewahi kucheza katika vilabu vya Blackburn Rovers na Parma katika miaka 17 alioyocheza soka ameamua kustaafu mchezo huo baada ya kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Grella mwenye umri wa miaka 33 alitangaza uamuzi huo mapema leo ikiwa ni siku mbili baada ya kuumia katika mchezo wake wa kwanza na klabu yake mpya ya Melbourne Heart inayoshiriki Ligi Kuu nchini Australia maarufu kama A-League. Akitangaza uamuzi huo Grella amesema anaona miaka 17 aliyocheza soka inatosha kwakuwa mwili wake hivi sasa hauwezi kukabiliana na mikiki ya uwanjani. Grella alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Australia ambacho kilishirikisho michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani na 2010 nchini Afrika Kusini na kucheza michezo 46 ya kimataifa. Kwa upande wa vilabu nyota huyo aliwahi kucheza katika vilabu vya Parma, Empoli na Torino zote za Italia kabla ya kutimkia Uingereza katika klabu ya Blackburn ambayo aliondoka mwaka jana.

AFCON 2013: MWAMUZI AFUNGASHIWA VIRAGO.

MWAMUZI kutoka Misri ambaye alichezesha mchezo wa kundi C kati ya Nigeria na Zambia Ijumaa iliyopita katika Uwanja wa Mbombela jijini Nelspruit, Gehad Grisha ameondolewa kuchezesha mechi zingine za michuano hiyo inayoendelea nchini Afrika Kusini. Grisha aliwapatia penati yenye utata Zambia katika dakika za majeruhi za mchezo baina ya timu hizo kitendo ambacho kilipelekea kuamsha hasira za wachezaji na viongozi waliokuwepo katika benchi la ufundi. Shirikisho la Soka la Nigeria-NFF liliwasilisha malalamiko yao mbele ya Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kuhusu suala la mwamuzi huyo. CAF ilithibitisha kumuondoa Grisha kwenye orodha ya waamuzi wake baada ya kufanyia uchunguzi suala hilo na kugundua makosa aliyofanya kwenye mchezo huo. Nigeria inahitaji ushindi katika mchezo wake wa kesho utakaofanyika jijini Rustenburg dhidi ya Ethiopia ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

AFCON 2013 YAFIKIA PATAMU.

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika-Afcon inatarajiwa kuendelea tena baadae leo ambapo timu nne kundi B zitakuwa zikitafuta nafasi ya kusonga mbele katika michezo yao ya mwisho. Katika michezo ya leo Ghana ambao wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kama vinara wa kundi hilo watachuana na Niger ambayo nayo inaweza kupata nafasi kama wakifanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC timu ambayo imekuwa ikionyesha kandanda la kuvutia katika michuano hiyo inatarajiwa kusaka ushindi wa kwanza dhidi ya timu ngumu ya Mali baada ya kutoka sare katika michezo yake miwili iliyopita. Katika michezo ya kundi A iliyochezwa jana, timu ngeni katika michuano hiyo Cape Verde iliandika historia nyingine kwa kuilaza Angola kwa mabao 2-1 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Cape Verde nchi ambayo ni kisiwa kinachokadiriwa kuwa na watu wapatao 500,000 inajiunga na wenyeji Afrika Kusini ambao nao walisonga mbele wakiwa vinara wa kundi lao pamoja na Ivory Coast ambao walitinga hatua hiyo mapema.

Sunday, January 27, 2013

WACHEZAJI WAWILI WAPOTEZA MAISHA VURUGU ZA PORT SAID.

WADAU wa soka nchini Misri wako katika maombolezo baada ya mchezaji wa Marek Mahmoud Abd Al Halem na golikipa wa zamani wa Al Masry Tamer Fahalawas kuuwawa katika vurugu zinazoendelea huko Port Said. Watu zaidi ya 30 wameuliwa Port Said kuanzia Jumamosi katika mapigano waandamanaji na vikosi vya usalama vya eneo hilo vurugu ambazo zilizuka baada ya Mahakama nchini humo kuwahukumu kifo watu 21 ambao walihusika katika vurugu ziliouwa watu 74 katika mchezo wa soka kati ya Al Masry na Al Ahly. Mashabiki wa timu zote mbili ambao wanajulikana kama Ultras wanadai kuwa polisi nao walihusika kwa kiasi kuchangia vifi vilivyotokea Port Said na kumlaumu rais wa Misri Mohammed Morsi kwa kushindwa kulisuka upya jeshi hilo. Mwenyekiti wa Merekh Morsy Sarhan alithibitisha kifo cha Abd Al Halem ambaye alijunga na timu hiyo miezi michache iliyopita ambapo tukio hilo lilimkuta wakati akielekea mazoezini. Sarhan aliongeza kuwa wataomboleza kifi cha mchezaji huyo kwa siku tatu ambaye alipigwa risasi pamoja na kutokuwa na hatia na kuwataka watu kuheshimu maamuzi ya mahakama ili maisha ya mchezo wa soka nchini humo yarejee kama kawaida.

CITY YAPATA PIGO.

BEKI wa Manchester City, Vincent Kompany anatarajiwa kuukosa mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Queens Park Rangers-QPR baada ya kuumia katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Stoke City ambao walishinda kwa bao 1-0. Kocha msaidizi wa City David Platt amesema ni mapema mno kujua mchezaji huyo atakaa nje muda gani lakini mchezo wa Jumanne dhidi ya QPR lazima ataukosa. Kompany alilazimika kutolewa nje kwa kuumia baada ya nusu saa katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Britannia ambapo taarifa zaidi juu ya hilo zitatolewa baadae baada ya kufanyiwa vipimo vya afya kuchunguza ukubwa wa tatizo. Kuumia kwa Kompany ambaye ni beki wa kati kutakuwa pigo kubwa kwa klabu hiyo ambayo tayari imemkosa nyota wake anayeweza kucheza katika nafasi hiyo YayaToure ambaye yuko na timu yake ya taifa Ivory Coast katika michuano ya Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini.

ILIKUWA NI KAMA KAMARI - WENGER.

MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa kuwapumzisha baadhi ya nyota wake katika mchezo wa mzunguko wa nne wa Kombe la FA dhidi ya Brighton ilikuwa ni kama kucheza kamari ambayo angeweza kushindwa. Kikosi cha Wenger ambacho kilikuwa kikicheza ugenini katika Uwanja wa Amex iliwapumzisha nyota wake Theo Walcott, Jack Wilshere na Santi Cazorla kuanza katika kikosi cha kwanza. Lakini kocha huyo ilibidi aongeze nguvu katika kipindi cha pili kwa kumuingiza Walcott ambaye alifunga bao na kuipeleka timu hiyo katika mzunguko wa tano wa michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 3-2. Wenger alidai kuwa kiendo cha kubadilisha wachezaji na kuwapumzisha wengine kilikuwa ni kama kamari ambapo kama angeshindwa angelaumiwa kwa maamuzi mabovu aliyochukua lakini bahati nzuri haikutokea hivyo. Arsenal iko katika harakati za kusaka taji lao la kwanza baada ya kupita miaka nane bila kuambulia chochote.

JUVENTUS YAMSAJILI ANELKA.

RAIS wa klabu ya Juventus ya Italia, Beppe Moratta amesema wamemsainisha mkataba wa miezi mitano mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Nicolas Anelka kutoka klabu ya Shanghai Shenhua ya China. Anelka mwenye umri wa miaka 33 anakuwa mchezaji wa pili mwenye jina kubwa kusajiliwa na mabingwa hao wa Serie A ndani ya wiki moja baada ya klabu hiyo pia kumnyakuwa nyota wa kimataifa wa Hispania Fernando Llorente ambaye atajiunga na klabu hiyo Julai 1 mwaka huu. Moratta amesema Juventus walikuwa wakihitaji kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ambayo imepwaya ndio maana wakaamua kumsajili Anelka na kama akifanya vizuri mwishoni mwa msimu wanaweza kufikiria kumuongeza muda mwingine. Anelka ambaye alianza kucheza soka katika klabu ya Paris Saint-Germain-PSG ya Ufaransa na abaadae kucheza katika vilabu vya Arsenal, Real Madrid na Chelsea kabla ya kuondoka kwenda Shanghai ambapo kuna tetesi kuwa amechoshwa na maisha ya klabu hiyo.

AFCON 2013: ALGERIA YAFUNGISHWA VIRAGO MAPEMA, IVORY COAST SAFI.

ALGERIA imekuwa timu ya kwanza kuyaaga mashindano ya Mataifa ya Afrika-Afcon baada ya kukubali kipigo cha pili mfululizo kutoka kwa Togo katika mchezo wa kundi D uliochezwa katika Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini. Algeria ambayo inashika nafasi ya 22 katika orodha za ubora duniani ilikubali kipigo cha mabao 2-0 na kuwa timu ya kwanza kigogo kuyaaga mashindano hayo katika hatua ya makundi baada ya kufungwa pia katika mchezo wa kwanza dhidi Tunisia. Katika michezo mingine iliyochezwa jana ya kundi hilo Ivory Coast walifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuifunga Tunisia kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Gervinho, Yaya Toure na Didier Ya Konan. Ivory Coast ambayo inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo inakuwa timu ya kwanza kusonga mbele katika kundi hilo baada ya kujikusanyia alama zote sita katika michezo miwili waliyocheza. Mzunguko wa mwisho katika kundi hilo utazikutanisha timu za Ivory Coast na Algeria ambao tayari wameshayaaga mashindano hayo huku mchezo mgumu ukitarajiwa kuwa kati ya Tunisia na Togo ambao wote watakuwa wakitafuta nafasi ya kusonga mbele.

Saturday, January 26, 2013

EURO 2020 KUCHEZWA KATIKA MIJI 13 TOFAUTI.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limetangaza kuwa michuano ya Ulaya 2020 itaandaliwa katika nchi 13 huku nusu fainali na fainali za michuano hiyo zitachezwa katika uwanja mmoja. Katibu Mkuu wa UEFA Gianni Infantino amesema hakuna uwanja zaidi ya mmoja utakaotumika katika nchi ambayo itapewa nafasi kuandaa mechi, katika timu 24 zinazoshiriki michuano hiyo na viwnaja hivyo vitachaguliwa Septemba mwaka 2014. UEFA walipiga kura Desemba mwaka jana kuandaa michuano hiyo katika miji tofauti kuzunguka bara hilo kuliko ilivyokuwa kawaida ambapo michuano hiyo imekuwa ikiandaliwa na nchi moja au mbili. Shirikisho limedai kuwa kufanya hivyo kutasaidia nchi ndogo ambazo hazitaweza kuzihudumia nchi 24 zinazoshiriki michuano hiyo kupata uhondo kwa kuandaa mojawapo ya mechi. Rais wa UEFA Michel Platini amesema uwanja utakaotumika kwa ajili ya mechi za nusu fainali na fainali unatakiwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 70,000 na mashabiki 60,000 kwa viwanja vya robo fainali huku hatua ya makundi ambayo itakuwa na mechi 16 viwanja vyake vinatakiwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 50,000.

BEBETO KUKABIDHIWA TIMU YA VIJANA.

SHIRIKISHO la Soka nchini Brazil linajipanga kumteua mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa nchi hiyo, Bebeto kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 20 itakayoshiriki katika michuano ya Amerika Kusini. Akihojiwa kuhusu suala hilo Bebeto amesema kuwa matokeo mabovu katika siku za karibuni yamechangia mabadiliko hayo katika timu za vijana kwakuwa ndio msingi wa kupata timu nzuri ambayo itapambana kuhakikisha wanabakisha nyumbani Kombe la Dunia 2014. Shirikisho hilo limedai kuwa nyota huyo ambaye anakumbukwa kwa aina ya ushangiliaji wake akiwa kama amempakata mtoto katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 iliyofanyika Marekani atateuliwa rasmi kushika nafasi hiyo wiki ijayo. Hatahivyo wadau wa soka nchini humo wamedai kuwa Bebeto ana uwezo mdogo katika kufundisha akiwa amewahi kufundisha klabu moja ya Amerika iliyopo jijini Rio de Janeiro mwaka 2010.

FERGUSON AWAJIA JUU WANAOMPONDA KIPA WAKE.

MENEJA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amemkingia kifua golikia wake David de Gea baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Hispania kulaumiwa kuruhusu bao la kusawazisha katika mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs mwishoni mwa wiki iliyopita. Wachambuzi wa soka wa luninga Alan Hansen na Gary Neville walimlaumu De Gea kwa makosa aliyofanya na kuruhusu Clint Dempsey kuisawazishia timu yake bao lakini Ferguson amesema hatilii maanani habari hizo. Ferguson amesema bado anamwamini De Gea kuwa golikipa wake namba moja na maneno ya watangazaji hao hayawezi kumbadilisha anavyofikiria. Katika mchezo huo United ambao ndio vinara wa Ligi Kuu nchini Uingereza ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Tottenham bao ambalo lilisawazishwa katika dakika za lala salama.

NIGERIA ITASONGA MBELE - OBI MIKEL.

KIUNGO wa kimataifa wa Nigeria, John Obi Mikel anaamini kuwa kikosi cha nchi hiyo kinachojulikana kama Super Eagles kitasonga katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini. Mpaka sasa Super Eagles haijapata ushindi wowote katika michezo miwili kwenye michuano hiyo lakini wanaweza kusonga mbele kama wakishinda mchezo wao wa mwisho katika kundi C dhidi ya Ethiopia utakaochezwa Januari 29. Nigeria ilikuwa na nafasi ya kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mchezo wao dhidi ya mabingwa watetezi Zambia lakini walishindwa kufanya hivyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na kufikisha alama mbili. Lakini Obi Mikel anaamini kuwa nchi hiyo itasonga mbele kwa kuhakikisha wanapata alama zote tatu katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ethiopia. Nyota huyo anayecheza katika klabu ya Chelsea ya Uingereza aliwataka wachezaji wenzake kutokata tamaa baada ya kupata sare ya pili dhidi ya Zambia badala yake wanatakiwa wajipange ili kuhakikisha wanashinda mchezo wao ujao.

WENGER AMTABIRIA UNAHODHA WILSHERE.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa kiungo wake nyota Jack Wilshere siku moja atakuwa nahodha wa timu hiyo pamoja na timu yake ya taifa ya Uingereza. Nyota huyo anatarajiwa kukabidhiwa unahodha katika kikosi cha timu hiyo baadae leo ambacho kitacheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Brighton baada ya Wenger kuamua kuwapumzisha Mikel Arteta na Thomas Vermaelen. Wenger amesema Wilshere ni mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye uchu wa kupata ushindi kitu ambacho anatakiwa awe nacho kiongozi wa timu ili kuwahamasisha wenzake. Kocha aliendelea kusema kuwa kwa maoni yake nyota huyo anaweza kuwa nahodha mzuri wa Uingereza katika siku za baadae lakini alikataa kuingia ndani zaidi kwa kudai kuwa swali hilo anayeweza kulijibu vizuri ni kocha wa nchi hiyo Roy Hodgson.

Friday, January 25, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

VUMBI LA LALA SALAMA VPL LABISHA HODI
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa katika viwanja sita tofauti. Mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka Oman kwenye ziara ya mafunzo. Pia Kocha wake mpya, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses Basena na Jamhuri Kihwelo. Mwamuzi wa kimataifa Israel Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo African Lyon inatarajiwa kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya kusitisha kibarua cha Pablo Velez kutoka Argentina kutokana na kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza. Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza. Coastal Union ambayo kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo Mzimbabwe Tinashe Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga. Timu zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani ambapo sheria 17 zinazotawala mpira wa miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa refa Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi. Ni mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba. Maafande wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.

WAZEE WA UTURUKI WAISUBIRI PRISONS DAR
Yanga iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Vinara hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.
Wakati ameingiza wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha wa Tanzania Prisons, Jumanne Chale amempoteza David Mwantika katika dirisa hilo. Beki huyo ametua katika timu ya Azam.

LYON YAONGOZA USAJILI DIRISHA DOGO
African Lyon ndiyo klabu iliyoongoza kwa kusajili wachezaji wengi kwenye dirisha dogo kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaotoa bingwa wa Tanzania Bara, lakini pia timu tatu ambazo msimu ujao zitarudi kucheza Ligi Daraja la Kwanza. Kati ya wachezaji 65 waliotua katika klabu mbalimbali katika dirisha hilo, Lyon ndiyo iliyoongoza kwa kuwanasa 12. Miongoni mwao hao, wawili (Ibrahim Job na Shamte Ally) imewachukua kwa mkopo kutoka Yanga. Pia watano imewapandisha kutoka katika kikosi chake cha U 20. Wachezaji hao ni Nurdin Musa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na jarufu Kizombi. Wengine walioingia katika timu hiyo katika dirisha dogo ni Juma Seif (Huru), Buya Jamwaka (Burkina Faso), Takang Valentine (Huru) na Yusuf Mgwao (Huru). Nayo Polisi Morogoro katika kuhakikisha inaondoka mkiani mwa ligi imesajili wachezaji wanane katika dirisha dogo kama ilivyofanya Oljoro JKT ya Arusha. Wachezaji wa kigeni walioingia katika dirisha dogo ni Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo (Azam), Donald Obimma na Ulugbe Chika (Toto Africans), Zuberi Hamis na Tinashe Machemedze (Coastal Union), Musa Mudde na Abel Dhaila (Simba).

NI DJOKOVIC NA MURRAY FAINALI AUSTRALIA OPEN.

MCHEZAJI tenisi nyota kutoka Uingereza, Andy Murray amefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya wazi ya Australia baada ya kumfunga Roger Federer wa Switzerland katika mchezo nusu fainali uliofanyika katika Uwanja wa Rod Laver Arena jijini Melbourne. Murray anayeshika namba tatu katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanaume alifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumfunga Federer anayeshika namba mbili kwa ubora kwa 6-4 6-7 6-3 6-7 6-2. Sasa Murray atakwaana na Novak Djokovic anayeshika namba moja katika orodha hizo katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuchezwa Jumapili. Kwa upande wanawake wanadada nyota kutoka Italia Sara Errani na Roberta Vinci wa Italia wamefanikiwa kushinda taji la michuano hiyo la wawili wawili baada ya kuwafunga Ashleigh Barty na Casey Dellacqua kwa 6-2 3-6 6-2. Errani na Vinci walizima ndoto za Barty na Dellacqua ambao ni raia wa Australia kunyakuwa taji hilo kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya nyumbani kwao. 

PIQUE AMZAWADIA BAO MWANAE MILAN.

BEKI wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Barcelona Gerard Pique amemzawadia bao aliloshinda katika mchezo wa jana dhidi ya Malaga mtoto wake wa kiume aliyezaliwa Januari 22. Katika mchezo huo wa jana wa Kombe la Mfalme ambao Barcelona ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 Pique alifunga bao la pili mwanzoni mwa kipindi cha na kushangiliwa huku ameweka kidole chake mdomoni. Mtoto huyo aitwaye Milan Pique Mebarak akichukua jina la babu yake kwa upande wa baba yake na pia kwa upande wa mama yake mwanamuzi nyota wa muziki wa pop Shakira Mebarak. Katika taarifa nyingine beki wa Barcelona Eric Abidal amerejea tena hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini April mwaka jana. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo imedai kuwa Abidal atakaa hospitalini kwa kipindi cha siku tatu mpaka nne ili kuangalia kwa makini maendeleo ya uapndikizaji wa ini aliofanyiwa.

FENERBAHCE KUCHEZA EUROPA LEAGUE UWANJA MTUPU.

KLABU ya Fenerbahce ya Uturuki italazimika kucheza mchezo wao wa nyumbani wa michuano ya Europa League huku milango ikiwa imefungwa baada ya mashabiki wake kurusha mafataki na vitu ningine uwanjani wakati wa mchezo dhidi ya Borussia Moenchengladbach Desemba mwaka jana. Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA pia limeitoza faini Fenerbahce ya euro 40,000 kwa vurugu hizo zilizotokea katika Uwanja wa Sukru Saracoglu nchini Ujerumani Desemba 6 ambapo Borussia ilishinda kwa mabao 3-0. Katika taarifa yake UEFA imesema kuwa imeamua kutoa adhabu kwa klabu hiyo baada ya kufanya tukio kama hilo tena katika mchezo wa mtoano wa michuano ya Klabu Bingwa arani Ulaya dhidi ya Spartak Moscow Agosti mwaka jana. Fenerbahce itaitumikia adhabu hiyo katika mzunguko wa timu 32 kwenye mchezo wa pili dhidi ya klabu ya BATE Borisov ya Belarus Februari mwaka huu.

UEFA YATAKA UKOMO WA URAIS FIFA UWE MIAKA 12.

Maofisa wa soka barani Ulaya wametaka kikomo cha urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwa miaka 12 ikiwa ni miaka minne zaidi ya mshauri wa mambo ya rushwa wa shirikisho hilo alivyoshauri. Katika taarifa yake UEFA wamesema kuwa wajumbe wake kutoka mataifa 53 wamependekeza kuwa FIFA wafuate utaratibu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kwa rais wake kukaa madarakani kwa kipindi cha miaka 12. Rais wa sasa wa FIFA Sepp Blatter atamalizia miaka yake 17 akiwa katika nafasi hiyo wakati kipindi chake kitakapomalizika mwaka 2015. Rais wa UEFA Michel Platini ambaye amesema hata gombea tena nafasi hiyo kipindi chake kitakapomalizika ndio anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Blatter baada ya kuondoka. Lakini bado mapendekezo ya UEFA bado yanatofautiana na mshauri wa FIFA Mark Pieth ambaye alipendekeza kikomo cha urais wa shirikisho hilo kuwa miaka nane ili kusadia kupunguza mambo ya rushwa na ufisadi.

BARCELONA KUWAKARIBISHA WACHOVU OSASUNA.

VINARA wa Ligi Kuu nchini Hispania, maarufu kama La Liga Barcelona inatarajia kuikaribisha Osasuna Jumapili ili kujaribi kurejesha makali yao baada ya kupata kipigo cha kwanza 3-2 dhidi ya Real Sociedad katika ligi hiyo Jumamosi iliyopita. Barcelona ambao waliweka rekodi katika nusu ya kwanza ya msimu kwa kupoteza alama mbili pekee wanaongoza La Liga wakiwa juu ya Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili kwa alama nane huku mahasimu wao Real Madrid wakiwa katika nafasi ya tatu kwa tofauti ya alama 15. Hata hivyo mwishoni mwa iliyopita Barcelona alijikuta wakipoteza mchezo baada ya kuongoza kwa mabao mawili mapema katika kipindi cha kwanza na hiyo imekuwa kama tahadhari kwao wakati kukiwa kumebakiwa mechi 18 kabla ya ligi hiyo kumalizika. Pamoja na kipigo hicho, Barcelona imeonyesha katikati ya wiki hii kwamba tayari wameshasahau wakati walipoigaragaza Malaga mabao 4-2 katika robo fainali ya pili ya Kombe la Mfalme na kutinga hatua ya nusu fainali ambapo sasa watakutana na Madrid. Katika mchezo wa Jumapili Barcelona itamkosa beki wake tegemeo Gerard Pique ambaye alipewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Sociedad.

Thursday, January 24, 2013

TASWA KUANDAA MDAHALO WA WAGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI TFF.

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimepanga kufanyika mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Uamuzi wa kuendesha mdahalo huo ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana (Januari 23, 2012), ambapo pia kilijadili masuala mbalimbali yahusiyo chama hicho. Tayari kikao kimeiagiza Sekreterieti ya TASWA ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa kuzungumza na vituo vya televisheni ili uweze kuoneshwa moja kwa moja kwenye vituo hivyo ili wananchi waweze kuwasikia wagombea hao. Pia mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kuweza kufanikisha tukio hilo la kuendesha mdahalo wa 'live' kwenye televisheni. Nafasi ambazo wahusika watafanyiwa mdahalo ni Rais na Makamu wa Rais. TASWA imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa, hivyo itafanya mawasiliano na TFF ili iweze kupata msaada wa karibu kufanikisha jambo hilo. Tunaamini ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo, ambapo mdahalo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo, wahariri wa baadhi ya michezo na wadau wachache wa soka. Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya michezo.TASWA inaamini Majura ambaye ni mwanachama wa TASWA akiwa pia amepata kuwa Katibu wa TASWA FC na Mhazini wa TASWA ni mtu makini, asiyeyumba na mwenye kutenda haki. Pia Kamati ya Utendaji imesisitiza katika kikao chake kwamba uchaguzi wa TFF haimuungi mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo TASWA inaonya kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo wa TASWA kwamba chama kinawaunga mkono ili wapate mteremko kufikia malengo yao hazitatimia. Kama kuna kiongozi au mwanachama wa TASWA ambaye anamuunga mkono mgombea yeyote wa TFF, huo utakuwa msimamo wake binafsi si wa chama na kama atahusisha chama kwa namna yoyote atakuwa anakosea na hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba ya chama. Tunawaomba waandishi wa habari za michezo nchini kuzidisha umakini kipindi hiki cha uchaguzi wa TFF na kujiepusha na makundi ya aina yoyote ambayo yatatia doa taaluma ya habari kwa namna yoyote ile.

REAL MADRID YAONGOZA KWA KUINGIZA FEDHA NYINGI.

KLABU ya Real Madrid imeendelea kuongoza katika orodha za vilabu vinavyoingiza fedha nyingi zaidi duniani baada ya kuwa klabu ya kwanza ya michezo kuingiza kiasi cha euro milioni 500 kwa msimu mmoja. Mapato hayo ambayo wameyapata katika msimu wa mwaka 2011-2012 yanawafanya kuongoza katika orodha hiyo kwa misimu nane mfululizo wakifuatiwa na mahasimu wao Barcelona ambao wanashika nafasi ya pili kwa kuingiza kiasi cha euro milioni 483 msimu uliopita. Nafasi ya tatu katika orodha hiyo inakwenda kwa Manchester United ambao msimu uliopita waliingiza kiasi cha euro milioni 395.9 wakifuatiwa na Bayern Munich katika nafasi ya nne euro milioni 368.4 huku ya tano ikishikiliwa na Chelsea wanaoingiza euro milioni 322.6. Arsenal wameporomoka mpaka nafasi ya sita kutoa nafasi ya nne waliokuwepo msimu wa mwaka juzi kwa kuingiza kiasi cha euro milioni 290.3, Manchester City wamekwea mpaka nafasi ya saba kwa kuingiza euro milioni 285.6 wakifuatiwa na AC Milan katika nafasi ya nane euro milioni 256.9. Timu nyingine ni Liverpool inayoshika nafasi ya tisa kwa kuingiza kitita cha euro 233.2 na kumi bora inafungwa na bibi kizee wa Turin klabu ya Juventus walioingiza kiasi cha euro 195.4. 

TOP 20: (All figures in millions of euros)
1. Real Madrid (Spain) 512.6 
2. Barcelona (Spain) 483
3. Manchester United (England) 395.9
4. Bayern Munich (Germany) 368.4
5. Chelsea (England) 322.6
6. Arsenal (England) 290.3
7. Manchester City (England) 285.6
8. AC Milan (Italy) 256.9
9. Liverpool (England) 233.2
10. Juventus (Italy) 195.4
11. Borussia Dortmund (Germany) 189.1
12. Inter Milan (Italy) 185.9
13. Tottenham Hotspur (England) 178.2
14. Schalke 04 (Germany) 174.5
15. Napoli (Italy) 148.4
16. Olympique Marseille (France) 135.7
17. Olympique Lyon (France) 131.9
18. Hamburg SV (Germany) 121.1
19. AS Roma (Italy) 115.9
20. Newcastle United (England) 115.3

AUSTRALIA OPEN: DJOKOVIC ATINGA FAINALI.

BINGWA mtetezi wa michuano ya wazi ya Australia, Novak Djokovic amefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo kwa kumgaragaza David Ferrer na kufanikiwa kujiweka katika nafasi nzuri ya kunyakuwa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo. Katika mchezo huo Djokovic raia wa Serbia alimfunga Ferrer anayetoka Hispania kwa 6-2 6-2 6-1 akitumia muda wa saa moja na dakika 29 ambapo sasa anasubiri mshindi katika mchezo mwingine wa nusu fainali kati ya Roger Federer na Andy Murray. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Djokovic amesema ulikuwa mchezo rahisi kuliko alivyotegemea kwani alianza vizuri kwa kujiamini toka mwanzo na kucheza katika kiwango bora kabisa. Kama akifanikiwa kuchukua taji hilo katika fainali itakayochezwa Jumapili atakuwa mchezaji wa kwanza kwa upande wa wanaume toka kuanzishwa kwa mashindan hayo ya wazi mwaka 1968.

AUSTRALIA OPEN: AZARENKA, LI NA KUKWAANA FAINALI.

BINGWA mtetezi wa michuano ya wazi ya Australia, Victoria Azarenka amefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo baada ya kumfunga mbabe wa Serena Williams, Sloane Stephens katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jijini Melbourne. Katika mchezo huo Azarenka aliondoka uwanjani kwa karibu dakika 10 ili kupata matibabu lakini baadae alirejea tena na kufanikiwa kumfunga Stephanes kwa 6-1 6-4. Mwanadada huyo raia wa Belarus mwenye umri wa miaka 25 anayeshika namba moja katika orodha za ubora duniani sasa atakutana na Li Na katika hatua ya fainali baada ya mwanadada huyo kutoka China kumuondosha Maria Sharapova wa Urusi. Li Na mwenye umri wa miaka 30 aliyekuwa katika kiwango bora alifanikiwa kumfunga Sharapova anayeshika namba mbili katika orodha za ubora kwa 6-2 6-2 akitumia muda wa dakika 93.

Hazard RED CARD Kicks BALLBOY in the RIBS | Swansea 0-0 Chelsea


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ubelgiji na klabu ya Chelsea, Eden Hazard ameomba radhi kwa kumpiga muokota mipira ambaye alikuwa akimzuia kuchukua mpira katika nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Swansea City jana. Hazard ambaye alitolewa nje, alikutana na kijana huyo aitwaye Charlie Morgan ambaye ni mtoto wa mkurugenzi wa Swansea Martin Morgan katika chumba cha kubadilishia nguo na kumuomba radhi kwa kitendo alichomfanyia. Swansea ambao walishinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Stamford Bridge walifanikiwa kuwazuia Chelsea na kupata sare ya bila ya kufungana katika Uwanja wa Liberty na kujikatia tiketi ya kucheza fainali na Bradford City. Katika maelezo yake Hazard amesema hakudhamiria kumpiga mateke kijana huyo kama inavyoonekana kwani alichodhamiria yeye ni kupiga mpira lakini kwakuwa kijana huyo alikuwa ameulalia ndio maana akaonekana kama anampiga. Nyota huyo aliendelea kusema alizungumza na tayari ameshamuomba msamaha kijana huyo alipokuja katika chumba cha kubalishia nguo mara baada ya kumalizika mchezo huo hivyo suala hilo limekwisha.

BAGGIO AJIUZULU UKURUGENZI WA KICHEZO ITALIA.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Italia, Roberto Baggio amejiuzulu wadhifa wake kama mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo akidai kuzuiwa kufanya kazi yake aliyotaka. Nyota huyo wa zamani ambaye alikuwepo katika kikosi cha Italia kilchomaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1990 na 1994 aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya kikosi cha timu ya taifa wakiwa kama mabingwa watetezi kushindwa kupenya katika hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2010. Baggio amesema kuwa aliwasilisha mawazo yake yaliyokuwa na kurasa 900 kwa shirikisho hilo mojawapo likiwa kujaribu kuinua vipaji vya vijana lakini hakujibiwa chochote ndio maana akaamua kujiuzulu. Italia ilimaliza katika nafasi ya pili katika michuano ya Ulaya mwaka jana baada ya kufungwa na Hispania chini ya kocha Cesare Prandelli.

Wednesday, January 23, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF LEO.

KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF YAAHIDI HAKI  
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeahidi wadau wa mchezo huo kuwa itafanya kazi zake kwa misingi ya haki. Akizungumza baada ya uzinduzi wa Kamati hiyo uliofanywa Dar es Salaam leo mchana (Januari 23 mwaka huu) na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo yenye wajumbe watano Idd Mtiginjola amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki. Mtiginjola amesema Kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu ikiwemo Katiba husika. “Niwakikishie kuwa hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,” amesema Mtiginjola ambaye kitaaluma ni Mwanasheria akiwa ni Wakili wa Kujitegemea. Baada ya uzinduzi, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments) mbalimbali zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, Katiba ya TFF na Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mbali ya Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria. Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.

AFCON 2013: MAHUDHURIO BADO SIO YAKURIDHISHA.

PAMOJA na mahudhurio mabovu, hali ya hewa imekuwa nzuri karibu kila mechi katika michezo nane ya ufunguzi wa michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon inayoendelea nchini Afrika Kusini. Mahudhurio madogo sio kitu cha kushangaza katika mechi za ufunguzi za mashindano ya Afrika lakini kujua haswa idadi ya mashabiki waliohudhuria huwa ni kitu kigumu kwakuwa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF na kamati ya maandalizi huwa mara chache ndio huzungumzia idadi kamili ya waliohudhuria. Siti tupu viwanjani zimekuwa hazileti muonekano mzuri wa mashindano hayo katika picha za luninga zinazoonyeshwa duniani kote, ingawa hata hivyo mashabiki hao wachache, na hali nzuri ya hewa ni vitu ambavyo vimekuwa vikileta msisimko katika michuano hiyo. Kelele za vuvuzela, filimbi za plastiki zilizojizolea umaarufu mkubwa katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 mpaka watu wengine hususani wa mataifa ya Ulaya kuzipiga marufuku katika viwanja vyao ndio zimekuwa zikiweka uhai uwanjani katika michuano ya mwaka huu.

AUSTRALIA OPEN: FEDERER KUKWAANA NA MURRAY NUSU FAINALI.

MCHEZA anayeshika namba mbili katika orodha za ubora, Roger Federer wa Switzerland amefanikiwa kumfunga Jo-Wilfried Tsonga katika robo fainali ya michuano ya wazi ya Australia inayoendelea jijini Melbourne. Federer alifanikiwa kumfunga kwa tabu Tsonga kwa 7-6 4-6 7-6 3-6 6-3 na sasa atakutana na Andy Murray wa Uingereza katika hatua ya nusu fainali baada ya muingereza huyo kumuondosha Jeremy Chardy wa Ufaransa. Kwa upande wanawake bingwa mtetezi wa michuano hiyo Victoria Azarenka alimfunga Svetlana Kuznetsova na kujihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo. Mwanadada huyo anayeshika namba katika orodha za ubora duniani sasa atakutana na chipukizi mwenye miaka 19 Sloane Stephens wa Marekani ambaye alimuondosha Serena Williams katika robo fainali.

BUFFON KUSTAAFU AKIWA JUVENTUS.

VYOMBO vya habari nchini Italia vimeripoti kuwa golikipa wa kimataifa wa Italia Gianluigi Buffon anatarajia kusaini mkataba mpya na mabingwa wa Serie A klabu ya Juventus utakaodumu mpaka 2015. Buffon ambaye amefikisha miaka 35 Jumatatu anategemea kusaini mkataba utakaokuwa na thamani ya euro milioni nne kwa kila msimu ikiwa ni punguzo la moja ya tatu ya mkataba wake unaoishia. Meneja wa Juventus Antonio Conte alikaririwa akisema kuwa Buffon ni mojawapo ya makipa bora kabisa duniani na amefurahi kwamba atabaki nao. Buffon ambaye alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Italia kilichonyakuwa Kombe la Dunia mwaka 2006 alitua Juventus mwaka 2001 na kufanikiwa kushinda mataji matatu ya Serie A na matatu ya Kombe la Italia.

CAF YAITOZA FAINI ETHIOPIA KUFUATIA VURUGU ZA MASHABIKI WAKE.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limelitoza faini ya dola 10,000 Shirikisho la Soka la Ethiopia baada ya mashabiki wake kutupa mavuvuzela pamoja na chupa za maji uwanjani wakati wa mchezo wao dhidi ya Zambia ambao walitoka sare ya bao 1-1 Jumatatu. CAF ilitangaza kuwa nusu ya adhabu hiyo ya dola 10,000 itasamehewa kama tu mashabiki wa Ethiopia hawatarudia tukio hilo katika kipindi chote cha mashindano. Ethiopia inayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 31 ina mashabiki wengi waliokuja kuiunga mkono timu yao lakini mchezo wao wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Mbombela uliingia dosari baada ya mwamuzi Eric Otogo-Castane alipompa kadi nyekundu golikipa Jemal Tassew muda mchache kabla ya mapumziko. Mara baada ya mwamuzi huyo kutoa kadi vuvuzela na chupa za maji zilimiminika uwanjani zikitokea jukwaani huku makocha na wachezaji wa akiba wakijificha wasiumizwe na vitu hivyo wakati mtangazaji uwanjani hapo alikiwaomba mashabiki hao kutulia. Mashabiki hao wa Ethiopia pia wanaweza kufungiwa kuingia uwanjani katika mchezo wa Ijumaa dhidi ya Burkina Faso labda CAF ipate uhakika kutoka EFF kuwa watawadhibiti mashabiki wao.

Tuesday, January 22, 2013

AFCON 2013: KESHI ATEGEMEA KUMTUMIA MOSES IJUMAA.

NIGERIA inamatarajio kuwa winga wake anayecheza katika klabu ya Chelsea ya Uingereza, Victor Moses atakuwa amepona goti kwa wakati kabla ya mchezo wao wa Ijumaa dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon Zambia. Moses hakuwemo katika kikosi cha nchi hiyo ambacho kilitoa sare ya bao 1-1 na Burkina Faso kwasababu ya kujiuguza goti lake na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa Dynamo Kiev ya Ukraine Brown Ideye. Kocha wa Nigeria Stephen Keshi amesema alimwacha kumtumia Moses kuhofia kujitonesha tena lakini ana matumaini winga huyo atakuwa fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Zambia. Beki Efe Ambrose anayecheza klabu ya Celtic Glasgow ataukosa mchezo wa Ijumaa baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Burkina Faso na nafasi yake inategemewa kuchuliwa na Kenneth Omeruo. 

NITASTAAFU NIKIWA BARCELONA - INIESTA.

KIUNGO nyota wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Barcelona, Andres Iniesta amebainisha kuwa hana mpango ya kuondoka katika klabu hiyo na kudai kuwa anataka kutundika daruga akiwa hapo. Iniesta mwenye umri wa miaka 28 ameshacheza mechi zaidi ya 400 katika kikosi cha kwanza cha Barcelona toka alipotoka katika shule ya klabu hiyo na anategemea kuendelea kuwepo zaidi hapo. Akihojiwa Iniesta amesema nia yake ni kucheza mpaka atapostaafu akiwa katika klabu hiyo na kitu pekee kinachoweza kubadilisha ni kiwango chake kwani kama kitashuka na klabu kuamua kumuacha ndio anayoweza kuondoka. Nyota pia alikiri kuwa timu hiyo inakabiliwa na wakati mgumu hivi sasa na wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanarejea katika kiwango chao haraka kabla ya mchezo wa Kombe la Mfalme dhidi ya Malaga.

PLATINI AMPONGEZA PRINCE BOATENG.

RAIS wa Shirikisho la Soka arani Ulaya, Michel Platini ametofautiana na rais wa Shirikisho la Soka la Dunia Sepp Blatter kuhusu suala la Kevin-Prince Boateng kuwaongoza wachezaji wenzake wa AC Milan kutoka uwanjani baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi mapema mwezi huu. Blatter amesema wachezaji hawapaswi kujichukuliwa sheria mkononi ingawa alidai kuwa mashabiki wanaokutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo wanapaswa kuchuliwa hatua aidha kwa klabu kukatwa alama au kufungiwa kabisa. Hatahivyo, Platini aliiambia radio moja nchini Ufaransa kuwa anakiunga mkono kitendo kilichofanywa na nyota huyo wa kimataifa kutoka Ghana kwani tatizo hilo linaonekana kuota mizizi katika siku za karibuni. Platini mwenye umri wa miaka 57 amesema ulikuwa ni uamuzi wa kishujaa uliofanywa na wachezaji wa Milan na baada ya tukio hilo aliwapigia simu na kuwapongeza.

AUSTRALIA OPEN: FERRER, SHARAPOVA WATINGA NUSU FAINALI.

MCHEZAJI nyota wa tenisi anayeshika namba nne katika orodha za ubora duniani David Ferrer amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya wazi ya Australia baada ya kumfunga Mhispania mwenzake Nicolas Almagro katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Rod Laver Arena jijini Melbourne. Katika mchezo huo Ferrer ilibidi apambane kiume baada ya kuwa nyuma kwa seti mbili na kufanikiwa kumfunga Almagro kwa 4-6 4-6 7-5 7-6 6-2 ambapo sasa anatarajia kukutana na aidha Novak Djokovic au Tomas Berdych katika hatua ya nusu fainali. Kwa upande wa wanawake mwanadada Maria Sharapova aayeshika namba mbili katika orodha za ubora naye alifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kumuondosha Mrusi mwenzake Ekaterina Makarova. Sharapova sasa atachuana na Li Na wa China ambaye naye alitinga hatua hiyo baada ya kumsambaratisha Agnieszka Radwanska.

Monday, January 21, 2013

AUSTRALIA OPEN: FEDERER, MURRAY WATINGA ROBO FAINALI.

WACHEZAJI nyota wa mchezo wa tenisi, Roger Federer anayeshika namba mbili katika orodha za ubora duniani na Andy Murray anayeshika namba tatu wameonyesha ubora wao kwa kutinga robo fainali ya michuano ya wazi Australia. Federer raia Switzerland alifanikiwa kutinga hatu hiyo baada ya kumfunga Milos Raonic wa Canada kwa 6-4 7-6 6-2 akitumia muda wa saa moja na dakika 53 wakati Murray alimsambaratisha Gilles Simon wa Ufaransa kwa 6-3 6-1 6-3 akitumia muda wa saa moja na dakika 35. Murray sasa takutana na Jeremy Chardy katika hatua ya robo fainali wakati Federer atapambana na Jo-Wilfried Tsonga katika hatua ya robo fainali. Kwa upande wa wanawake bingwa mtetezi wa michuano hiyo Victoria Azarenka ametinga hatua ya robo fainali baada ya kumfunga kirahisi Elena Vesnina na kujiweeka katika nafasi nzuri ya kukwaana na Serena Williams katika hatua ya nusu fainali. Azarenka alimfunga Vesnina kirahisi kwa 6-1 6-1 na kukata tiketi ya robo fainali ambayo atacheza na Svetlana Kuznetsova wakati Williams ambaye anaonekana yuko katika kiwango bora alimsambaratisha Maria Kirilenko kwa 6-2 6-0 na kutinga hatua hiyo.