Wednesday, December 31, 2014

KAPUNOVIC ATUA TAYARI KUINOA SIMBA.

HATIMAYE kocha mpya wa klabu ya Simba, Goran Kopunovic raia wa Serbia amewasili jijini Dar es Salaam leo asubuhi huku akitamba kuwa anaifahamu yanga vizuri. Akihojiwa na blog ya Bin Zubeiry, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Dar es Salaam, kocha huyo kijana amesema mafurahi kuja kuinoa Simba kwani ni klabu kubwa na amepania kuiletea mafanikio. Kapunovic amesema anatarajia kukutana na uongozi wa Simba kwa mazungumzo na kusaini mkataba na baada ya hapo ataanza kazi rasmi. Akizungumzia kuhusu wapinzani wa jadi, Yanga SC, Kopunovic amesema kwamba anawajua vizuri na anafahamu kuhusu soka ya Tanzania kwa ujumla. Kapunovic anakuja baada ya kutimuliwa kwa kocha Patric Phiri kutoka Zambia kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo kikiwemo kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar.

CISSE AKUBALI YAISHE.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Newcastle United, Papiss Cisse amekubali kosa lake alilofanya katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu yake dhidi ya Everton. Cisse ambaye amefunga mabao tisa msimu huu, alimpiga kiwiko beki Seamus Coleman katika mchezo huo wa Jumapili iliyopita na anatarajiwa kutumikia adhabu ya mechi tatu. Nyota huyo sasa atakosa mechi za ligi dhidi ya Burnley na vinara Chelsea na mchezo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la FA dhidi ya Leicester City. Katika mchezo huo Newcastle walishinda kwa mabao 3-2 dhidi ya Everton.

NASRI AITISHA CHELSEA KUWA WAO WANAFUKUZA MWIZI KIMYA KIMYA.

KIUNGO wa klabu ya Manchester City Samiri Nasri amewaonya mahasimu wao Chelsea kuwa timu ina uzoefu wa kuwafukuzia katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu. Kikosi cha City kilicho chini Manuel Pellegrini kinashika nafasi ya pili mbele ya vinara Chelsea kwa tofauti ya alama tatu wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya Sunderland kesho. City walifanikiwa kushinda taji la ligi msimu uliopita pamoja na kuwa nyuma ya Arsenal na Liverpool kwa kipindi kirefu wakati wa kampeni hizo na Nasri anaamini kuwa uzoefu huo unawapa nafasi katiika mbio za ubingwa msimu huu. Akihojiwa Nasri amesema kila mmoja anakuwa imara na kadri umri wao unavyozidi kusonga mbele ndio uzoefu nao unaongezeka. Nasri aliendelea kudai kuwa wanajifunza mambo mengi katika timu hiyo kwani wameshapitia mambo mengi tofauti hivyo wanajua jinsi gani ya kukabiliana na changamoto.

RONALDO NI BORA LAKINI MESSI ANAKIPAJI CHA KIPEKEE - RAKITIC.

MCHEZAJI nyota wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic anadhani kuwa wakati Cristiano Ronaldo akiwa mchezaji bora, Lionel Messi ni mchezaji wa mwenye kipaji cha kipekee ambacho kinamfanya kuwa juu ya kila mchezaji katika sayari hii. Ronaldo na Messi wote wapo katika orodha ya kugombea tuzo ya Ballo, d’Or sambamba na golokipa wa kimataifa wa Ujerumani Manuel Neuer. Ronaldo amevunja rekodi ya ufungaji wakati akiisaidia Real Madrid kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia na Kombe la Mfalme katika miezi 12 iliyopita. Kwa upande wa Neuer yeye ameisaidia Bayern Munich kushinda mataji mawili kabla ya kuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Ujerumani kilichonyakuwa Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil. Rakitic anafahamu vyema uwezo wa wawili hao ingawa hata hivyo anadai hajawahi kukutana na yeyote anayefikia kiwango cha Messi na anadhani anastahili kuchukua tuzo hiyo. Rakitic amesema kuna mmoja pekee ambaye yuko juu ya wote naye ni Messi halafu wengine ndio wanafuatia.

ODIMWINGIE KUPEWA MKATABA NA STOKE.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Nigeria, Peter Odemwingie anatarajiwa kupewa mkataba mpya na klabu ya Stoke City pamoja na kuwa nje ya uwanja kutokana na majeruhi. Odemwingie amekuwa nje toka Agosti akisumbuliwa na majeruhi ya goti lakini nyota huyo wa zamani wa West Bromwich Albion na Cardiff City anatarajia kumaliza mkataba wake na Stoke mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo kumekuwa na taarifa njema kwake kwani Stoke wanapanga kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi pamoja na kufikisha umri wa miaka 34 msimu ujao. Meneja wa Stoke Mark Hughes amebainisha kuwa kila kitu sawa kwa Odemwingie pamoja na kuwa nje kwa kipindi kirefu msimu huu. Nyota huyo tayari ameanza mazoezi ya kukimbia nje na anakaribia kurejea katika afya yake ya kawaida.

BLANC KUTOA UAMUZI WA MWISHO KUHUSIANA NA SUALA LA CAVANI NA LAVEZZI.

MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG Laurent Blanc amesema anasubiri ufafanuzi kabla ya kutoa uamuzi kuhusiana na mustakabali wa Edinson Cavani na Ezequiel Lavezzi. Hakuna mshambuliaji yeyote kati ya hao aliyesafiri na kikosi cha PSG karika ziara yao ya Morocco hivyo kuzidisha tetesi kuwa klabu hiyo inaweza kusikiliza ofa zitakazotolewa katika kipindi cha usajili mwezi ujao. Cavani amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Arsenal, wakati Liverpool na Inter Milan wao wameripotiwa kumtaka Lavezzi. Hata hivyo, Blanc amesisitiza hakuna kilichoamuliwa mpaka wachezaji hao watakaporejea kwa ajili ya mazoezi Januari 2. Blanc amesema wanasubiri baadhi ya ufafanuzi kutoka kwao wakati watakapowasili ndipo watoe uamuzi wao kuhusiana na mustakabali wao.

BAADA YA KUHARIBU SHEREHE YA REAL MADRID HUKO DUBAI, EL SHAARAWY ADAI HANA MPANGO WA KUONDOKA MILAN.

MSHAMBULIAJI nyota wa AC Milan, Stephan El Shaarawy amesisitiza hana mpango wowote wa kuondoka katika timu hiyo na badala yake amepania kuipa mafanikio katika mwaka unaokuja. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 amekuwa akisumbuliwa na majeruhi katika miezi 12 iliyopita lakini sasa anaonekana kurejea katika kiwango chake tena baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-2 waliopata dhidi ya Real Madrid jana. Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa kesho, El Shaarawy alikuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka San Siro lakini mwenyewe sasa amepania amepania kufurahia mwaka ujao akiwa na timu hiyo. Nyota huyo aliwaambia wanahabari huko Dubai ulipofanyika mchezo wao dhidi ya Madrid kuwa hana mpango na hajafikiria kuondoka Milan kwasasa.

RAIS WA ATLETICO ADAI SIMEONE NDIO ALIOMBA TORRES ASAJILIWE.

RAIS wa klabu ya Atletico Madrid, Enrique Cerezo amedai kuwa wamemsajili tena Fernando Torres kwa maombi kutoka kwa meneja wa timu hiyo Diego Simeone. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amekubalia kupelekwa kwa mkopo kwa mabingwa hao wa Hispania baada ya kusajili na AC Milan kwa mkataba wa moja kwa moja kutoka Chelsea. Cerezo anadai kuwa mazungumzo na mshambuliaji huyo yalianza baada ya Simeone kuomba asajiliwe jambo ambalo ni nadra sana kwake. Rais huyo amesema Simeone huwa hana tabia ya kuomba kuomba lakini kwa suala la Torres aliufuata uongozi na kueleza nia yake jambo ambalo wamemtimizia.

BALE HAUZWI NG'O - PEREZ.

RAIS wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez amedai kuwa Gareth Bale hawezi kuondoka katika klabu hiyo. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales mwenye umri wa miaka 25 ambaye alijiunga na Madrid akitokea tottenham Hotspurs kwa kitita cha paundi milioni 85 mwaka 2013, amekuwa akihusishwa na taarifa za kurejea nchini Uingereza katika klabu ya Manchester United. Akihojiwa Perez amesema hawajapata ofa yeyote kutoka kwa United au klabu yeyote kwa ajili ya Bale. Rais huyo aliendelea kudai kuwa kama anavyofikiria Madrid bila Cristiano Ronaldo ndio anavyofikiria na kwa Bale pia hivyo hadhani kama anaweza kuondoka.

Monday, December 29, 2014

RONALDO AMALIZA MWAKA 2014 KWA KISHINDO, AKWAA TUZO YA GLOBE SOCCER AWARDS.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo amemaliza mwaka kwa staili ya aina yake kwa kubeba tuzo ya mchezaji bora wa mwaka au Globe Soccer Awards huko Dubai. Ronaldo amekuwa na mwaka mzuri huku akivunja rekodi kwa kuwa na mabao mengi katika msimu mmoja wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati alipoiongoza Real Madrid kunyakuw ataji lake la 10 la michuano hiyo. Nyota huyo pia anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or inayotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa mara ya pili mfululizo Januari 12 mwakani lakini anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Lionel Messi na Manuel Neuer. Ronaldo ambaye alikuwepo mwenyewe kupokea tuzo hiyo katika sherehe zilizofanyika katika Hotel ya Atlantis Palm aliwashukuru mashabiki, wachezaji wenzake na viongozi wa Real Madrid kwa ushirikiano wanaompa na kufanya kupata mafanikio hayo. Kwa upande mwingine kocha wa Madrid Carlo Ancelotti naye alitunukiwa tuzo hiyo kama kocha wa bora wa mwaka kutokana na mafanikio aliyoipa timu hiyo kwa mwaka huu.

AFCON 2015: MALI YATAJA SILAHA ZAKE.

MODIBO Maiga ametajwa katika kikosi cha wachezaji 23 cha timu ya taifa ya Mali kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon huko Guinea ya Ikweta pamoja na kukosa mechi zote za kufuzu. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye anacheza kwa mkopo katika klabu ya Metz ya Ufaransa akitokea West Ham United hajaitumikia nchi yake kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja. Mfungaji kinara wa timu ya Wolverhampton Wanderers Bakary Sako ambaye amefunga mabao saba msimu huu naye amejumuishwa katika kikosi hicho. Sako sasa watakosa mechi tano za Wolves ambao wanapambana kupanda katika Ligi Kuu msimu ujao. Kiungo wa klabu ya Bordeaux Abdou Traore ni mchezaji mwingine aliyeitwa katika kikosi hicho baada ya kukosekana kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mali ambao walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye michuano iliyopita wamepangwa katika kundi gumu la D sambamba na timu za Ivory Coast, Cameroon na Guinea.

AFCON 2015: LEMINA AICHOMOLEA GABON.

MCHEZAJI nyota Mario Lemina ambaye alikuwemo katika kikosi cha vijana chini ya miaka 20 cha Ufaransa kilichonyakuwa Kombe la Dunia mwaka jana amekataa mwaliko wa kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Gabon kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon. Kocha wa Gabon Jorge Costa itabidi aende katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 17 mpaka Februari 8 bila kiungo huyo wa Marseille. Lamina ambaye ni mzaliwa wa Gabon aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa yote yanayosemwa ni tetesi lakini tayari alifanya mawasiliano na nchi hiyo kuwa hatakwenda katika michuano hiyo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 ana matumaini ya kuitwa katika kikosi cha timu ya wakubwa ya Ufaransa. Mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubemeyang ni mojawapo ya jina kubwa lililomo katika kikosi cha Gabon ambacho pia kinawajumuisha beki wa Cardiff City Bruno Ecuele Manga na mshambuliaji wa Charlton Frederick Bulot. Gabon wamepangwa katika kundi A sambamba na wenyeji Guinea ya Ikweta, Burkina faso na Congo Brazzaville.

PARDEW AKWEPA KITIMOTO CHA WANA HABARI.

MENEJA wa klabu ya Newcastle United, Alan Pardew amekwepa kutoa kauli kuhusiana na taarifa kuwa anaweza kuwa meneja mpya wa klabu ya Crystal Palace. Pardew mwenye umri wa miaka 53, alishindwa kutimiza majukumu ya wanahabari baada ya ushindi wa mabao 3-2 waliopata dhidi ya Everton jana. Kocha msaidizi wa Newcastle John Carver ambaye ndiye aliyekwenda katika mkutano wa wanahabari amesema Pardew hakutoa sababu yeyote kwanini hakwenda kuzungumza na wanahabari hao. Palace walimtimua kocha wa Neil Warnock Jumamosi iliyopita ikiwa imepita miezi mine pekee huku timu hiyo ikiendelea kuning’inia katika mstari wa kushuka daraja.

ITACHUKUA MUDA MREFU SCHUMACHER KURUDI KATIKA HALI YAKE.

MENEJA wa dereva nyota wa zamani na bingwa wa dunia wa mashindano ya langalanga Michael Schumacher amedai kuwa bado ana safari ndefu ya kupona kutokana na majeruhi ya kichwa aliyopata katika ajali wakati akiteleza katika barafu. Meneja huyo Sabine Kehm alikaririwa akidai kuwa itachukua muda mrefu kwa Schumacher kurudi katika hali yake ya kawaida. Kauli ya Sabine imekuja baada ya taarifa kuwa Schumacher ameanza kuwasiliana na watu wake wa karibu kwa macho. Ukiwa umepita mwaka mmoja toka Schumacher apate ajali hiyo, Sebine alikanusha madai hayo kwa kudai sio taarifa za kweli.

POCHETTINO KUIONGEZEA NGUVU SPURS JANUARI.

MENEJA wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino amepanga kujadili uwezekano wa kufanya usajili wakati dirisha dogo la usajili Januari litakapofunguliwa Alhamisi hii. Spurs walimaliza mwaka 2014 kwa sare ya bila kufungana dhidi ya United katikamchezo wa Ligi Kuu uliofanyika katika Uwanja wa White Hart Lane Jana wakati wakiendelea kupambana kumaliza katika nafasi nne za juu. Timu hiyo pia imefanikiwa kutinga hatua ya timu 32 bora katika michuano ya Europa League na nusu fainali katika Kombe la Ligi katika msimu wa kwanza wa kocha huyo raia Argentina. Ili kuongeza nguvu katika kikosi chake kutokana na mashindano mengi wanayoshiriki, Pochettino amedokeza kuwa anajipanga kuleta sura mpya mwezi ujao. Pochettino amesema anafurahia kikosi alichonacho lakini kipindi cha usajili kikifika watakaa na klabu kujadili maeneo ya kuimarisha. Spurs wana kibarua kizito katika mchezo wao unaofuata dhidi ya Chelsea ambao utachezwa pia katika Uwanja wa White Hart Lane katika simu ya mwaka moja.

TAJIRI WA BIRMINGHAM ADAI KUTAKA KUMSAJILI RONALDO AKIWA KINDA.

MMILIKI wa klabu ya Birmingham David Sullivan amedai timu hiyo ingeweza kumsajili Cristiano Ronaldo kwa paundi milioni sita kabla ya kujiunga na Manchester United mwaka 2003. Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alisajiliwa na United iliyokuwa chini ya Sir Alex Ferguson akiwa na umri wa miaka 18 akitokea klabu ya Sporting Lisbon kwa kitita cha euro milioni 15.5. Ronaldo aliitumikia United kwa miaka sita akishinda taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na matatu ya Ligi Kuu kabla ya kusajiliwa na Real Madrid mwaka 2009. Hata hivyo, Sullivan amedai kuwa Birmingham ingeweza kumnasa kinda huyo ambaye aliletwa kwao kabla ya kuchagua kujiunga na United. Sullivan amesema kabla ya Ronaldo kwenda United walimpa ofa ya paundi milioni sita lakini baadae alichagua kwenda Old Trafford badala yao.

SANCHEZ AKANUSHA KUWA NYOTA ARSENAL.

MSHAMBULIAJI mahiri wa klabu ya Arsenal, Alexis Sanchez amekanusha taarifa kuwa yeye ndio nyota wa timu hiyo kwa msimu huu, akisisitiza yeye ni kama wachezaji wengine. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile alihamia Emirates kwa kitita cha euro milioni 40 wakati wa majira kiangazi na sasa anaongoza akiwa amefunga mabao 15 msimu huu. Lakini pamoja na hayo, Sanchez anaamini kuwa meneja Arsene Wenger ana vipaji vingi katika kikosi chake. Sanchez amesema hakubaliani na suala la kuwa nyota kwani kikosi chao kina wachezaji wengi wakubwa wenye hadhi ya dunia. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa katika kikosi cha Arsenal yeye ni kama wachezaji wengine, ila amepata bahati ya kuanza vyema.

TOURE KUIKOSA SUNDERLAND MWAKA MPYA.

KLABU ya Manchester City inatarajiwa kukosa huduma ya kiungo wake Yaya Toure katika mchezo dhidi ya Sunderland Alhamisi hii kutokana na kusumbiliwa na matatizo ya nyonga. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alikosa mchezo dhidi ya Burnley jana akisumbuliwa na majeruhi ya msuli aliyopata katika mchezo dhidi ya West Bromwich Albion uliochezwa Desemba 26. Huku wakiwa tayari wamewakosa Sergio Aguero, Edin Dzeko na Vincent Kompany, City watakuwa wakikabiliwa na mtihani mwingine wa kukosa Toure. Meneja wa City manuel pellegrini amebainisha kuwa ingekuwa hatari kumchezesha Toure katika mchezo dhidi ya Burnley na kuthibitisha kuwa watafuatilia afya yake inavyoendelea leo.

VAN GAAL ASINGIZIA UCHOVU WA SIKUKUU KUFUATIA SARE DHIDI YA SPURS.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Louis van Gaal amedai kuwa kikosi chake kilikuwa kikipambana kutafuta uhai katika kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs uliomalizika kwa sare ya bila ya kufungana. Ushindi katika mchezo huo ungewawezesha United kupunguza pengo la alama dhidi ya timu za Chelsea na Manchester City ambao wote nao walipoteza alama. Van Gaal amelaumu ratiba ngumu ya kipindi cha sikukuu kuwa chanzo kikubwa kwa kikosi chake kushindwa kufanya vyema katika mchezo wa jana. Kocha huyo amesema kisayansi imethibitishwa kuwa mwili hauwezi kurejea katika hali yake ya kawaida katika muda wa saa 48.

NAFURAHI KUREJEA NYUMBANI - TORRES.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Hispania, Fernando Torres ameeleza furaha yake ya kukubali kujiunga na Atletico Madrid kwa mkopo kutoka AC Milan mpaka mwishoni mwa msimu ujao. Nyota huyo ameshindwa kung’ara akiwa na Milan baada ya kujiunga nao kwa mkopo Agosti, ambapo amefunga bao moja katika mechi 10 za Serie A alizocheza. Hata hivyo, baada kukubali kujiunga kwa mkataba wa moja kwa moja na Milan, Torres mwenye umri wa miaka 30 sasa amekubali kujiunga na Atletico kwa mkopo klabu ambayo ndio iliyomuibua akiwa kinda. Torres amesema kuna wakati kila atalazimika kurudi nyumbani ivyo anajisikia furaha kurejea tena mahali alipoibukia. Nyota huyo amesema kwa kipindi kirefu amekuwa amekuwa akisema hawezi kuficha alipotokea hivyo ni heshima kubwa kwake kurejea tena Atletico.

West Ham vs Arsenal 1-2 2014 All Goals Highlights

Sunday, December 28, 2014

MOURINHO ALIA NA MWMAUZI KUFUATIA KUAMBULIA SARE.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anaamini kuwa kuna kampeni zinendelea kuwashawishi waamuzi kutoa uamuzi tofauti dhidi ya timu yake. Mourinho amekasirishwa na mwamuzi Anthony Taylor kwa kushindwa kutoa penati katika sare ya bao 1-1 waliyopata dhidi ya Southampton. Kiungo Cesc Fabregas alipewa kadi kwa kujirusha baada ya kuanguka katika eneo la hatari baada ya kukwatuliwa na Matt Target. Baada ya mchezo huo Mourinho aliiambia BBC kuwa vyombo vya habari, watangazaji mameneja wa timu zingine wote wanatoa shinikizo kwa waamuzi hivyo anadhani kuna kampeni inaoendelea dhidi ya timu yake. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kila anajua kuwa ni penati lakini mwamuzi alifanya makosa tena makosa makubwa pamoja na kwamba ni binadamu.

Saturday, December 27, 2014

DI MARIA PANCHA TENA.

KIUNGO mahiri wa klabu ya Manchester United, Angel Di Maria aliachwa katika mchezo ambao timu hiyo ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Newcastle United kutokana na majeruhi. Meneja wa United Louis van Gaal amebainisha Di Maria alipata majeruhi wakati wa muda wa mazoezi katika kipindi cha krismas. Kocha huyo ambaye kikosi chake kitakwaana na Tottenham Hotspurs kesho bado hajajua ni wakati gani nyota wake huyo atarejea uwanjani. Van Gaal amesema kwasasa itabidi wasubiri kuona vipimo vitakavyokuwa ili wajue ni muda gani atakaa nje. Di Maria mwenye umri wa miaka 26 ndio kwanza alikuwa amerejea katika kikosi cha United katika mchezo dhidi ya Aston Villa Desemba 20 baada ya kukosekana kwa wiki tatu kutokana na matatizo ya msuli wa paja.

HAKUNA ANAYEWEZA KUMFIKIA MESSI KWA UBORA - PEDRO.


MSHAMBULIAJI wa klabu ya Barcelona, Pedro amedai kuwa mchezaji mwenzake Lionel Messi ndio mchezaji bora kuliko yeyote duniani na anastahili kushinda tuzo ya Ballon d’Or mbele ya Cristiano Ronaldo. Messi amewahi kushinda tuzo hiyo kwa mara nne mfululizo kabla ya Ronaldo kuingilia kati na kunyakuwa tuzo hiyo mwaka jana ikiwa ni mara ya pili kwa upande wake. Baada ya kuisaidia Real Madrid kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Mfalme mwaka huu, Ronaldo ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kunyakuwa tuzo hiyo katika sherehe zitakazofanyika Januari 12 mwakani. Mafanikio makubwa aliyopata Messi kwa mwaka huu ni kuiongoza timu yake ya taifa ya Argentina kucheza fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil wakati golikipa wa Bayern Munich Manuel Neuer yeye ni mchezaji mwingine wa tatu aliyeyopo katika orodha hiyo. Pamoja na kutopewa nafasi mwaka huu, Pedro anaamini kuwa hakuna mchezaji yeyote katika sayari hii anayeweza kumfikia Messi katika ubora wake uwanjani.

Wednesday, December 24, 2014

REDKNAPP AMKOMALIA AUSTIN.

MENEJA wa klabu ya Queens Park Rangers-QPR, Harry Rednapp amesema mshambuliaji wake kinara wa mabao Charlie Austin hatauzwa katika usajili wa dirisha dogo Januari mwakani lakini mustakabali wake utategemea kubaki kwa timu hiyo katika Ligi Kuu. Austin mwenye umri wa miaka 25 ambaye amefunga mabao 11 msimu huu na kumfanya kuwa mchezaji anayeongoza kwa mabao katika ligi Uingereza amebakisha miezi 18 katika mkataba wake wa sasa. Akihojiwa na wana habari kuelekea safari yao ya kuifuata Arsenal kesho, Redknapp amesema hana mpango wa kumuuza mshambuliaji huyo katika dirisha dogo. Lakini pamoja na hayo Redknapp amekiri kuwa hataweza kumzuia katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi kama wakishindwa kubaki katika Ligi Kuu kwasababu mwenyewe anataka kuendelea kucheza hapo mpaka atakapostaafu. QPR haijapata alama yeyote ugenini msimu huu lakini alama 17 walizofanikiwa kuzichukua katika mechi zao za nyumbani zimewasaidia kuwaondoa katika hatari ya kushuka daraja mpaka nafasi ya ya 16.

BARCELONA KWENDA QATAR FEBRUAR KUTIMIZA MSHARTI YA MDHAMINI.

KLABU ya Barcelona, inatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Qatar kwa ajili ya mchezo wa kirafiki Februari 4 mwakani. Barcelona ambao kwasasa wako katika nafasi ya pili ya msimamo wa La Liga wanatarajia kucheza mechi hiyo kwa ajili ya kutimiza masharti ya mdhamini wao Kampuni ya Uwekezaji ya Michezo ya Qatar wanaodhamini fulana zao. Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumatano, siku tatu baada ya mchezo wa nyumbani dhidi ya Villarreal huku wakikabiliwa na mchezo mwingine dhidi ya Athletic Bilbao Februari 8. Mechi hiyo ilitangazwa wakati wa kikao cha bodi ya klabu hiyo lakini haikutajwa timu atakayocheza nayo.

ALEX SONG APIGWA CHINI CAMEROON.

KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Volke Finke ametaja kikosi cha awali cha wachezaji 27 kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta. Kocha huyo raia wa Ujerumani ameteua wachezaji wengi waliokuwemo katika mechi za kufuzu, lakini amemuacha kiungo Alex Song. Song hajaichezea Cameroon toka alipotolewa nje kwa kadi nyekundu katika kipindi cha mabao 4-0 walichopata kutoka kwa Croatia katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil. Kiwango kizuri alichokionyesha msimu huu akiwa kwa mkopo katika klabu ya West Ham United akitokea Barcelona, kilizua tetesi kuwa angeweza kuitwa katika timu ya taifa. Cameroon wanatarajiwa kuanza maandalizi nyumbani na watacheza mechi ya kirafiki na Congo Brazzaville Januari 7 kabla ya kusafiri kwenda Gabon kwa ajili ya kambi yao nyingine na kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini Januari 11.

TETESI ZA USAJILI: UNITED YAMTENGEA BALE PAUNDI MILIONI 120, ARSENAL WAJIPANGA KUCHUKUA CAVANI.

UONGOZI wa klabu ya Manchester United, umedai kuwa tayari kutoa kitita cha paundi milioni 120 kwa ajili ya kumsajili winga Gareth Bale mwenye umri wa miaka 25 kutoka klabu ya Real Madrid katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Bale ambaye ni mmoja kati ya wachezaji ghali zaidi ulimwenguni alisajiliwa na Madrid kwa kitita kilichoweka rekodi cha paundi milioni 85.3 mwaka 2013. Wakati huo huo kocha Laurent Blanc wa klabu ya Paris Saint-Germain anafikiria kumuachia mshambuliaji wake Edinson Cavani mwenye umri wa miaka 27 kwa gharama ya paundi milioni 50 kama Arsenal watamhitaji katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo. Kwingineko Manchester City nao imetenga kitita cha paundi milioni 25 kwa ajili ya kumuwinda mshambuliaji wa Atletico Madrid Mario Mandzukic mwenye umri wa miaka 28.

IVORY COAST WAGOMEA BAJETI KIDUCHU WALIYOPEWA NA SERIKALI KWA AJILI YA AFCON.

SHIRIKISHO la Soka la Ivory Coast-FIF limegomea bajeti kiduchu waliyopewa na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ushiriki wa timu ya taifa, katika michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon mwakani. Serikali ya nchi hiyo imekubali kutoa dola 575,805 kwa ajili ya timu hiyo itakayokwenda kushiriki fainali hizo zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Januari 17 hadi Februari 8 huko Guinea ya Ikweta. Pamoja na hayo, makamu wa rais w FIF, Sory Diabate amewaambia wana habari kuwa hawataweza kwenda kushiriki michuano hiyo kwa kiasi hicho cha fedha kwani walishawsilisha bajeti yao kwa ufafanuzi mzuri. Ivory Coast walikuwa wakitarajiwa kuanza mazoezi yao chini ya kocha Herve Renard huko Abu Dhabi, Januari 5 mwakani. Timu hiyo imepangwa katika kundi D sambamba na timu za Mali, Cameroon na Guinea.

ALGERIA BADO WAKOMAA EBOSSE ALIFARIKI KWA KUPIGWA NA KITU CHENYE NCHA KALI.

WAZIRI wa habari nchini Algeria Mohammed Tahmi amesisitiza kwamba kifo cha mchezaji wa kimataifa wa Cameroon Albert Ebosse kilisababishwa na mashabiki waliokuwa wakirusha vitu. Tahmi ambaye alikuwa akizungumza na radio ya Algeria alikuwa akijibu ripoti ya wiki jana ya daktari wa kuchunguza mauaji kwamba majereha ya Ebosse yalisababishwa na mashambulizi. Ebosse mwenye umri wa miaka 25 aliaga dunia Agosti 23 mwaka huu baada ya klabu yake JS Kabylie kupoteza mchezo nyumbani. Tahmi amesema walifanya uchunguzi wao ambao ulionyesha kuwa mchezaji huo aliuawa kutokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali kutoka kwa mashabiki waliogadhabishwa na timu yao kufungwa. Waziri huyo aliendelea kudai kuwa vitu vilirushwa kutoka pande zote mbili na wachezaji wote walilengwa wakati wakielekea katika vyumba vya kubadilishia nguo lakini kwa bahati mbaya tukio likamtokea Ebosse. Suala hilo kwa sasa liko mahakamani ambapo uamuzi utatolewa.

CHELSEA HAINA UWEZO WA KUMSAJILI MESSI - MOURINHO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekiri kuwa hana uwezo wa kumsajili Lionel Messi kwasababu ya sheria kali za matumizi ya fedha za Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA. Mwezi uliopita Chelsea ilitangaza kuingiza faida iliyovunja rekodi ya paundi milioni 18.4 kwa mwaka uliomalizika June mwaka huu, ambayo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa mapato na uuzwaji kwa wachezaji. Lakini kutokana na sheria za UEFA Mourinho amesisitiza kuwa hataweza kuwa na nafasi ya kumsajili Messi ambaye dau lake la kumng’oa Barcelona linakadiriwa kuwa paundi milioni 205. Akihojiwa na kituo kimoja cha redio kocha huyo Mreno amesema hawezi kuwa na nafasi hiyo kutokana na sheria za sasa za UEFA zinazoweka kikomo matumizi ya vilabu ili kujaribu kuweka usawa kwa vilabu vingine visivyokuwa na pesa.

KOCHA WA LEICESTER AKUBALI KUTUMIKIA ADHABU ALIYOPEWA.

MENEJA wa klabu ya Leicester City, Nigel Pearson amethibitisha jana kuwa hatakata rufani kufuatia adhabu ya kufungiwa mechi moja kufuatia kuwatukana mashabiki wa timu hiyo. Pearson alifungiwa mechi moja na kutozwa faini ya paundi 10,000 baada ya kukutwa na hatia ya kujibishana na mashabiki wakati wa mchezo dhidi ya Liverpool ambao walifungwa mabao 3-1 mapema mwezi huu. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 sasa atakosa kuwemo katika benchi la ufundi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspurs Desemba 26 mwaka huu. Akihojiwa Pearson amesema haoni sababu ya kukata rufani kwani anataka suala hilo limalizike ili aweze kuendelea na masuala mengine.

KHEDIRA ATAMANI KUONGEZA MKATABA MADRID.

KIUNGO wa kimataifa wa Ujerumani, Sami Khedira ameeleza kuwa atafurahi kuongeza mkataba wake na klabu ya Real Madrid kama wakifikia makubaliano. Khedira ambaye ambaye msimu huu amekuwa akiandamwa na majeruhi, amekuwa sio chaguo la kwanza la kocha Carlo Ancelotti kwani amekuwa akiwachagua Toni Kroos na Luka Modric badala yake. Vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa kuwa Khedira anaweza kuhamia Bayern Munich pamoja na vilabu kadhaa Uingereza ikiwemo Arsenal ambayo imeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake. Khedira mabaye alijiunga na Madrid akitokea klabu ya VfB Stuttgart mwaka 2010 amedai kuwa kwasasa yuko fiti na anatumaini atapata muda zaidi wa kucheza. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kama wakifikia makubaliano anayohitaji atafurahi kuendelea kuitumikia Madrid kwa kipindi kingine zaidi ya June 2015 ambapo ndipo mkataba wake wa sasa unapomalizika.

BOLTON YAMSAJILI MKONGWE HESKEY.

KLABU ya Bolton Wanderers imetangaza kumsajili mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Uingereza Emile Heskey kwa mkataba wa muda mfupi. Heskey mwenye umri wa miaka 36 amekuwa akifanya mazoezi na klabu hiyo huku akikitumikia kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 katika mchezo dhidi ya Reading Jumatatu iliyopita. Mkongwe huyo ambaye ameitumikia Uingereza mechi 62 alikuwa akicheza katika klabu ya Newcastle Jets ya Australia ambayo ilimuachia April mwaka huu. Bolton kwasasa inasubiri ITC ya mshambuliaji ili kukamilisha usajili wake.

RONALDINHO ATISHIWA KUFUKUZWA MEXICO KWA UTORO.

RAIS wa klabu ya Queretaro ya Mexico ametishia kumfukuza Ronaldinho kama hatarejea kwa wakati katika timu hiyo. Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 34 ambaye amewahi kushinda Kombe la Dunia mwaka 2002 sambamba na tuzo za Ballon d’Or mwaka 2004 na 2005 hajarejea toka apewe likizo huku msimu mpya ukitarajiwa kuanza. Msimu mpya nchini humo unatarajiwa kuanza Januari 11 mwakani lakini Queretaro tayari wameshaanza maandalizi toka Desemba 8 huku wakiwa tayari wamecheza mechi kadhaa za kirafiki bila nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain, Barcelona na AC Milan. Rais wa klabu hiyo Arturo Villanueva ametishia kuwa kama Ronaldinho hataripoti mpaka kufikia wiki ijayo atakuwa hana jinsi bali kumtimua na nafasi yake kumpa mchezaji mwingine.

EFA KUAJIRI KOCHA WA KIGENI.

CHAMA cha Soka cha Misri-EFA kimetangaza kuwa kocha wake ajaye kwa ajili ya timu ya taifa ya nchi hiyo atakuwa raia wa kigeni. EFA ilimtimua kocha wa zamani, Shawky Gharib baada ya kushindwa kuipeleka nchi hiyo katika michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwezi ujao huko Guinea ya Ikweta. Makamu wa rais wa EFA, Hassan Farid amesema baada ya kikao na wajumbe wa bodi wa chama hicho wameazimia kuwa kocha ajaye awe raia wa kigeni. Farid amesema mpaka sasa wana CV za makocha sita wa kigeni ambapo kamati husika itachagua kocha mmoja kati ya hao.

Tuesday, December 23, 2014

RAMSEY FITI KUIVAA SOUTHAMPTON, ARTETA BADOBADO.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amebainisha kuwa nahodha wake Mikael Arteta atachelewa kidogo kupona majeruhi yanayomsumbua lakini kiungo Aaron Ramsey anaweza kuwa fiti kwa ajili ya mchezo dhidi ya Southampton wakati wa mwaka mpya. Arteta alipata majeruhi mwezi uliopita katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund. Wenger amesema nahodha wake huyo anaendelea vyema lakini atachelewa kidogo kuliko ilivyotegemewa lakini Ramsey anaweza kurejea katika mchezo dhidi ya Southampton. Ramsey alikuwa akirejea katika kiwango chake cha msimu uliopita akiwa amefunga mabao matatu katika mechi mbili kabla ya kutolewa wakati wa mapumziko katika mchezo dhidi ya Galatasaray mapema mwezi huu. Wenger pia amebainisha kuwa Laurent Koscielny naye anakaribia kurejea katika kikosi cha kwanza na anaweza kuwepo katika kikosi chake kitakachopambana na West Ham United huko Upton Park.

CAGLIARI YAMTIMUA KOCHA WAKE.

KLABU ya Cagliari inayoshiriki Ligi Kuu nchini Italia imemtimua kocha wake Zdenek Zeman kutokana na matokeo yasiyo ya kuridhisha kwa timu hiyo. Klabu hiyo imeshinda mechi mbili pekee chini ya kocha huyo raia wa Jamhuri ya Czech na kuwaacha katika nafasi ya 18 katika msimamo wa Serie A. Kipigo cha mabao 3-1 walichopata ugenini dhidi ya vinara wa Serie A Juventus Alhamisi iliyopita ndio ulikuwa mchezo wa mwisho kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 67. Katika taarifa yake klabu hiyo ilimshukuru kocha huyo kwa kipindi chote ambacho wamekuwa naye kwa miezi kadhaa na kumtakia kila la heri popote atakapokwenda. Kocha wa zamani wa klabu ya Al Jazira, Walter Zenga ambaye kwasasa hana kibarua ndio anapewa nafasi ya kubwa ya kuchukua mikoba ya Zeman.

MOYES AMUWINDA PIENAAR.

TAARIFA kutoka nchini Uingereza zimemhusisha Steven Pienaar na tetesi za kuhamia La Liga kuungana na meneja wake wa zamani David Moyes katika klabu ya Real Sociedad. Pienaar anajulikana kwa kupendwa na Moyes kutokana na bidii zake na Everton wanaoenekana kuwa tayari kupokea ofa kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 32. Everton wanaangalia uwezekano wa kumsajili Joel Campbell kutoka Arsenal na kama dili hilo lilikubali Pienaar anaweza kuruhusiwa kuondoka. Huu ni msimu wa nne kwa Pienaar toka ajiunge na Everton mwaka 2007 lakini majeruhi yamekuwa yakimkwamisha nyota huyo mara kwa mara.

NILIFANYA UAMUZI SAHIHI KUJA MADRID - KROOS.

KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Kombe la Dunia, Toni Kroos anaamini ushindi wa Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia unaonyesha jinsi kati alivyokuwa sahihi kuondoka Bayern Munich na kwenda Real Madrid. Kiungo huyo alijiunga na Madrid katika kipindi cha majira ya kiangazi kwa kitita cha euro milioni 30 na kuisaidia timu hiyo kushinda taji hilo Jumamosi iliyopita. Madrid waliwatandika mabingwa wa soka Amerika Kusini San Lorenzo kwa mabao 2-0 katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo uliofanyika jijini Marakech, Morocco. Kroos ambaye pia alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia wakati akiwa Bayern amesema amefurahishwa kumaliza mwaka kwa kunyakuwa taji.  Nyota huyo amesema amefurahi kushinda taji hilo kwa mara ya pili huku akidai litakuwa na maana kubwa kwa kampeni zao za msimu huu.

CARRICK MCHEZAJI BORA KWA UINGEREZA KWASASA - FERGUSON.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema Michael Carrick ndiiye mchezaji bora kwa Uingereza kwasasa. Kikosi cha United kilicho chini ya Louis van Gaal kimeshinda mechi sita mfululizo toka carrick mwenye umri wa miaka 33 arejee kutoka katika majeruhi ya kifundo cha mguu Novemba mwaka huu. Akihojiwa Ferguson amesema anadhani Carrick ndio kiungo bora wa kati katika soka la Uingereza na mchezaji bora raia wa Uingereza. Kurejea kwake kumeongeza nguvu katika kikosi cha Van Gaal huku kocha huyo akimpa unahodha msaidizi Ijumaa iliyopita.

NAPOLI YAMALIZA UTAWALA WA JUVENTUS KWA KUNYAKUWA SUPER CUP.

KLABU ya Napoli jana ilimaliza utawala wa Juventus katika Super Cup ya Italia baada ya kufanikiwa kuifunga kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo uliofanyika huko Doha, Qatar. Golikipa wa Napoli, Rafael ndio alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuokoa penati ya Simeone Padoin. Katika muda wa kawaida Carlos Tevez aliipa Juventus bao la kuongoza kabla ya kusawazishwa na Gonzalo Higuain na kufanya timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza. Ushindi unakuwa kama kisasi kwa Napoli ambao walitandikwa mabao 4-2 katika muda wa nyongeza wakati walipokutana katika mchuano huo mwaka 2012.

ALI ANAENDELEA VYEMA HOSPITALI.

MSEMAJI wa nguli wa zamani wa masumbwi Muhammad Ali amedai kuwa hali ya bondia huyo inaendelea vyema toka alazwe hospitalini hapo kwa maradhi ya maambukizi katika mapafu. Msemaji Bob Gunnell amesema madaktari wanaomtibu Ali wana matumaini ya kumruhusu katika kipindi cha karibuni. Gunnell aliendelea kudai kuwa familia ya nguli huyo bado inaomba suala hilo kuachwa kuwa la binafsi na kushukuru maombi yote ya kumtakia heri. Ali mwenye umri wa miaka 72 bingwa wa wa zamani mara tatu wa uzito wa juu duniani ambaye anaugua ugonjwa wa kutetemeka au Parkinson alikimbizwa hospitali Jumamosi iliyopita. Ali aligundulika kuwa na Parkinson mwaka 1984, miaka mitatu baada ya kutangaza kustaafu masumbwi.

Monday, December 22, 2014

ALAMA TATU ALIZOCHUKUA KWA STOKE ZAMPA JEURI MOURINHO.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anaamini ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Stoke City na kuwahakikishia nafasi ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu katika kipindi cha Krismasi, ulikuwa na thamani zaidi ya alama tatu walizopata.Mabao ya John Terry na Cesc Fabregas walitosha kuihakikishia ushindi Chelsea na kuwafanya kuongeza pengo la alama tatu dhidi  ya wapinzani wao Manchester City. Baada ya kupata kichapo katika Uwanja wa Britannia msimu uliopita, Mourinho amefurahi msimu huu kupata ushindi katika uwanja huo. Akihojiwa Mourinho amesema kupata ushindi katika uwanja wa Stoke unatakiwa kuwa na timu nzuri yenye uwezo wa kuiga aina ya mchezo wa timu hiyo. Kocha huyo aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha krismasi mpaka mwaka mpya wana ratiba ngumu hivyo ushindi huo ulikuwa muhimu kwao ili kuongeza morali katika timu hususani baada ya kufungwa na Newcastle United katika mchezo wao uliopita. Chelsea inakabiliwa na mchezo dhidi ya West Ham United utakaochezwa siku moja baada ya krismasi, baadae watasafiri kuifuata Southampton Desemba 28 kabla ya kuikaribisha Tottenham Hotspurs Januari mosi.

2014 KAMWE HAITASAHAULIKA KWA MADRID - ANCELOTTI.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema kitendo cha timu yake kushinda taji la Klabu Bingwa ya Dunia kinawafanya kumaliza mwaka 2014 kwa mafanikio. Mabingwa hao wa Ulaya walifanikiwa kuwafunga mabingwa wa Amerika Kusini San Lorenzo kwa mabao 2-0 na kutwaa taji hilo huko Marakech, Morocco hivyo kufikisha mataji manne kwa mwaka huu. Makombe mengine ambao yamechukuliwa na Madrid kwa mwaka huu ni pamoja na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Mfalme na Super Cup ya Ulaya. Akihojiwa Ancelotti amesema wamefanya vizuri na kamwe hawatausahau mwaka huu kwani umoja ndani ya timu umekuwa kama familia. Madrid imefanikiwa kufunga jumla ya magoli 178 kwenye mashindano yote na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mwaka mmoja.


WAAMUZI 18 KUTOKA TANZANIA WATAMBULIKA FIFA.

SHIRIKISHO la soka Duniani-FIFA limetoa orodha mpya ya waamuzi linaowatambua ambapo katika orodha hiyo kuna jumla ya waamuzi 18 kutoka Tanzania, miongoni mwao wakiwemo 11 wapya na saba wa zamani. Waamuzi wapya wa kati kutoka Tanzania ni Mfaume Ali Nassor kutoka Zanzibar pamoja na Martin Saanya kutoka Morogoro, pia wamo waamuzi watatu wa kike ambao ni Florentina Zabron, Jonesia Rukyaa pamoja na Sofia Ismail. Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wanaume ni Frank John Komba na Soud Idd Lila, kwa upande wa wanawake ni Kudura Omary Maurice, Hellen Joseph Mduma, Dalila Jafari Mtwana na Grace Mawala. Waamuzi wa zamani wa Tanzania kwenye orodha ya FIFA, kwa upande wa wanaume ni Israel Mujuni Nkongo na Waziri Sheha Waziri, kwa upande wa waamuzi wasaidizi ni Josephat Bulali, Fernand Chacha, John Longino Kanyenye, Ali Kinduli na Samuel Hudson Mpenzu.

GUITERREZ KUREJEA TENA UWANJANI BAADA YA UPASUAJI WA SARATANI.

KIUNGO wa klabu ya Newcastle, Jonas Gutierrez anatarajiwa kurejea tena uwanjani akianzia mchezo wa vijana chini ya umri wa miaka 21 dhidi ya West Ham United utakaochezwa leo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alirejea katika klabu yake hiyo mwezi uliopita na amekuwa akifanya mazoezi baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe wa saratani korodani. Gutierrez alifanyiwa upasuaji nchini kwao Argentina kuondoa uvimbe huo Septemba mwaka huu na baadae kupatiwa matibabu ya mionzi. Mechi yake ya mwisho kucheza ilikuwa April mwaka huu wakati Norwich City alipopelekwa kwa mkopo.

MKONGWE CAHILL BADO ATAMANI KUCHEZA KWA MIAKA MINNE ZAIDI.

MSHAMBULIAJI mkongwe wa kimataifa wa Australia, Tim Cahill anadhani kwasasa yuko fiti na anafikiri anaweza kuendelea kucheza kwa msimu minne zaidi mpaka kufikia miaka 40. Cahill amesema anatarajia kutafuta mkataba wa miaka miwili au mitatu wakati mkataba wake na klabu ya New York Red Bulls ya Marekani utakapomalizika mwakani. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 35 ambaye yuko katika kikosi cha Australia kinachojiandaa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Asia mwezi ujao, amesema anafikiria kurejea Ligi Kuu Uingereza ambako amecheza kwa miaka tisa akiwa na Everton. Cahill amesema kwasasa bado ana mkataba na Red Bulls lakini pindi utakapomalizika anafikiria kutafuta klabu itakayompa mkataba mrefu ili aweze kuendelea kusakata kabumbu.

MASHABIKI WA SOKA KUANZA KURUHUSIWA TENA KUTIZAMA MECHI ZA LIGI MISRI.

MASHABIKI wa soka wa Misri wanatarajiwa kuruhusiwa kuhudhuria mechi za Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitatu. Mashabiki nchini humo walikuwa wamefungiwa kuhudhuria mechi za ligi ya nyumbani toka tukio la Port Said Februari mwaka 2012 wakati zilipozuka vurugu ambazo zilipelekea vifo vya zaidi ya watu 70. Chama cha Soka nchini humo-EFA kimedai kuwa wizara ya mambo ya nchi na wizara ya michezo na vijana wamekubaliana kuruhusu mashabiki kuhudhuria mechi za Ligi Kuu wakati itakapoanza mzunguko wake wa pili. EFA imefafanua kuwa mashabiki wapatao 10,000 wataruhusiwa katika mechi zitakazochezwa katika viwanja vilivyopo Cairo na Alexandria huku wengine 5,000 wakiruhusiwa katika viwanja vidogo nchini humo. Hata hivyo adhabu itaendelea kwa michezo itakayohusisha vilabu vyovyote kati ya sita vikubwa nchini humo. Klabu za Al Ahly, Zamalek, Al Ittihad, Ismaily, Al Masry na Damanhur zote zitaendelea kucheza katika uwanja mtupu pindi mojawapo itakapokutana na mwenzake.

RONALDO ATENGENEZEWA SANAMU MAALUMU.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ametengenezewa sanamu maalumu. Sanamu hilo limewekwa katika mji wa kisiwa cha Madeira nchini Ureno mahli ambapo ndipo aliposaliwa mwanasoka huyo. Ronaldo aliungana na familia yake, wakiwemo mama, kaka na dada zake kwenda kuzindua sanamu hilo. Baadhi ya wadau wa soka nchini humo wamekuwa wakiikosoa sanamu hiyo na kudai kuwa haijafanana na nyota huyo. Pamoja na sanamu, Ronaldo ana makumbusho maalum kwa ajili yake katika kisiwa cha Madeira.