DANNY Jordaan amechaguliwa kuwa rais mpya wa Chama cha Soka nchini Afrika Kusini-SAFA baada ya kushinda kinyang’anyiro cha uchaguzi uliohusisha wagombe wawili. Jordaan ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa kamati ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia 2010 alipata kura 162 dhidi ya 88 za mpinzani wake katika uchaguzi huo Mandla Mazibuko. Rais aliyemaliza muda wake Kirsten Nematandani alikosa nafasi ya kushiriki uchaguzi huo baada ya mikoa wanachama 52 ya SAFA kutomchagua. Katika kipindi chake cha miaka minne, Jordaan mwenye umri wa miaka 62 anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo masuala ya utawala, fedha na matokeo mabaya ya timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Bafana Bafana.
Monday, September 30, 2013
HAKUNA MPANGO WA KUMUUZA BENDER - LEVERKUSEN.
KLABU ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani imeweka wazi kuwa hawana mpango wa kumuuza kiungo wao Lars Bender baada ya ripoti kuwa nyota huyo alikuwa akiwaniwa na Arsenal. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani amekuwa akipanda kiwango na kuwa mmoja wa wachezaji wa kutegemewa wa Leverkusen toka lipojiunga nao akitokea klabu ya 1860 Munich mwaka 2009. Mkurugenzi mkuu wa klabu hiyo Michael Reschke aliuambia mtandao wa Kicker kuwa hawana mpango wa kumuuza nyota wao huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2017. Wakati huohuo mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Rudi Voller naye alisisitiza kuwa Leverkusen haijapata ofa kutoka klabu yoyote kwa ajili ya Bender.
REUS AMPA TANO LEWANDOWSKI.
KIUNGO mahiri wa klabu ya Borussia Dortmund, Marco Reus amempongeza nyota mwenzake wa timu hiyo Robert Lewandowski kwa kiwango kikubwa ambacho ameonyesha katika siku za karibuni. Lewandowski alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 iliyopata Dortmund dhidi ya Freiburg Jumamosi iliyopita na kufikisha mabao sita katika mechi saba za Bundesliga alizocheza msimu huu. Akihojiwa na mtandao wa klabu hiyo Reus alimsifu nyota huyo ni kudai kwamba ni mmoja kati ya washambuliaji bora kabisa duniani. Reus aliendela kusema kuwa Lewandowski ni aina ya mchezaji ambaye ni vigumu kumkaba wakati ukibakiwa nae peke yake na pia anajua kujiweka katika nafasi nzuri za kufunga.
WENGER ATOA TAHADHARI DHIDI YA NAPOLI.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amewaonya nyota wa kikosi chake kuwa Napoli sio timu ya kubeza na watakuja kutafuta ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya timu hizo utakaochezwa baadae leo. Arsenal kwasasa wanaongoza Ligi Kuu nchini Uingereza kwa tofauti ya alama mbili baada ya kushinda mechi yao dhidi ya Swansea City Jumamosi iliyopita. Huo unakuwa ushindi wa tano mfululizo kwa Arsenal kati ya mechi sita za ligi walizocheza huku wakipoteza moja dhidi ya Aston Villa. Lakini pamoja na timu yake kuonyesha kiwango kizuri Wenger ameonya kwamba Napoli watakuja kutafuta ushindi na sio matokeo mengine zaidi ya hayo hivyo inabidi wajipange ili kuhakikisha wanakabiliana nao.
GALATASARAY YAMNYATIA MANCINI.
KLABU ya Galatasaray ya Uturuki imebainisha kuanza mazungumzo ya awali na Roberto Mancini kuhusiana na nafasi ya umeneja iliyopo wazi. Klabu hiyo yenye maskani yake jijini Istanbul ilithibitisha katika ukurasa wake mtandao wa kijamii wa twitter kwamba Mancini alikutana na bodi ya wakurugenzi kwa ajili ya mazungumzo ya kumpa nafasi hiyo. Mancini ambaye ni raia wa Italia atachukua nafasi ya Fatih Terim ambaye alitimuliwa wiki iliyopita baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya. Manchester City walimtimua Mancini Mei mwaka huu ikiwa ni mwaka mmoja toka aiongoze klabu hiyo kushinda taji la kwanza la Ligi Kuu nchini Uingereza.
Saturday, September 28, 2013
FIFA YAILIMA ADHABU UKRAINE KWA UBAGUZI.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza kuufungia Uwanja wa Taifa wa Ukraine na pia nchi hiyo kucheza bila mashabiki katika mechi yao ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia watakayocheza nyumbani. Hatua hiyo imekuja kufuatia tukio la mashabiki wa soka wan chi hiyo kupiga kelele za kibaguzi katika mchezo baina ya timu ya taifa ya nchi hiyo na San Marino uliofanyika jijini Lviv. Katika taarifa yake, FIFA imedai kufikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha na ushahidi wa picha za video pamoja na ule uliowasilishwa na waamuzi. Mbali na kufungiwa mashabiki kwenye mchezo unaofuata, Ukraine haitaruhusiwa kutumia uwanja wake wa taifa uliopo Lviv katika mechi zozote za kufuzu kuanzia sasa mpaka katika michuano ya Kombe la Dunia 2018. Kamati ya nidhamu ya FIFA pia imeitoza nchi hiyo euro milioni 36,000.
ETO'O AITWA CAMEROON PAMOJA NA KUZUSHIWA KUSTAAFU.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o ameitwa katika kikosi cha wachezaji 25 cha timu ya taifa ya nchi hiyo ambacho kitakwaana na Tunisia kwenye mchezo wa hatua ya mtoano pamoja na vyombo vya habari kuripoti kuwa nyota huyo amestaafu soka la kimataifa. Vyombo vya habari vya nchi viliripoti kuwa Eto’o ambaye pia ndio nahodha wa Cameroon alitangaza kustaafu soka la kimataifa kwa sababu za kifamilia katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kushinda mechi yao dhidi ya Libya mapema mwezi huu. Hata hivyo Eto’o hakusema chochote kuhusiana na tetesi hizo na kocha wa Cameroon Volke Finke alipuuza tetesi hizo na kudai kuwa mshambuliaji huyo wa Chelsea mwenye umri wa miaka 32 ni mchezaji sahihi wa kukiongoza kikosi chake katika kutafuta nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia. Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza itapigwa katika Uwanja wa Rades jijini Tunis Octoba 13 huku ile ya marudiano ikichezwa jijini Yaounde Nevemba mwaka huu na mshindi wa jumla atafuzu michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani.
ARSENAL HAWANA UBAVU WA KUMALIZA TOP FOUR MSIMU HUU - OWEN.
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Liverpool na Manchester United, Michael Owen anaamini kuwa Arsenal hawana kikosi chenye uwezo wa kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza msimu huu. Kikosi cha Arsenal kinachonolewa na Arsene Wenger kwasasa kinaongoza ligi kwa tofauti ya mabao baada ya kushinda mechi zake nne kati ya tano walizocheza msimu huu. Pamoja na hivyo Owen anaamini Arsenal hawana nafasi ya kumaliza msimu wa ligi wakiwa katika nafasi nne kutokana na aina ya wachezaji waliopo katika kikosi cha Wenger. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa kama akipewa nafasi ya kuchagua wachezaji nyota wa ligi kutoka katika vilabu sita kwa Arsenal atamchukua mmoja pekee ambaye ni Mesut Ozil wengine waliobakia ni wachezaji wa kawaida. Owen amesema ukilinganisha na usajili waliofanya Chelsea, Tottenham Hotspurs na timu zingine anaona Arsenal nafasi yao itakuwa ndogo msimu huu.
MESSI AMEONYESHA USHAHIDI WA WAZI - WAKILI.
WAKILI wa mshambuliaji nyota wa Barcelona, Lionel Messi amesisitiza kuwa mteja wake huyo ameonyesha ushahidi wa wazi kuhusiana na kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili. Kesi ya nyota huyo wa kimataifa wa Argentina ilianza kusikilizwa jana ambapo alianza kujibu tuhuma hizo za kutolipa kodi stahiki kutokana na haki ya matumizi ya picha zake. Messi anatuhumiwa kuzitumia nchi za nje ya Hispania kama Belize na Uruguay kuuza haki ya matumizi ya picha kitu ambacho ni kinyume na sheria za kodi za nchi hiyo. Baba yake Messi, Jorge ambaye alilipa kiasi cha euro milioni tano katika mamlaka ya kodi nchini humo Agosti mwaka huu, pia naye anahusishwa na kesi hiyo na wote walitoa utetezi wao kwa nyakati tofauti jana.
Friday, September 27, 2013
SERENA WILLIAMS KUMALIZA MWAKA AKIWA KINARA.
MWANADADA nyota katika tenisi, Serena Williams wa Marekani anatarajiwa kumaliza mwaka akiwa kinara katika orodha za ubora wa mchezo huo kwa upande wa wanawake baada ya kufanikiwa kushinda mataji mawili ya Grand Slam mwaka huu. Williams mwenye umri wa miaka 32 alipoteza mechi nne pekee kwa mwaka huu na kushinda mataji tisa ikiwemo michuano ya wazi ya Ufaransa na Marekani. Hii ni mara ya tatu kwa mwanadada huyo kukaa kileleni kwenye orodha hiyo kwenye kalenda ya mwaka. Williams amekuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kushikilia nafasi hiyo wakati alipomng’oa Victoria Azarenka wa Belarus Februari mwaka huu.
WENGER KUENDELEA KUINOA ARSENAL.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesisitiza kuwa atakuwa tayari kusaini mkataba mpya na timu hiyo baada ya mmiliki wake Stan Kroenke kuonyesha nia ya kuendelea kumhitaji mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 63. Mkataba wa sasa wa Wenger unamalizika mwishoni mwa msimu huu lakini mwenyewe amesema hana haraka ya kuanza mazunguzo ya mkataba mpya. Lakini Wenger akihojiwa mara baada ya Kroenke kuzungumza nia ya klabu kumuongeza mkataba alidai anaipenda klabu hiyo na kutania kwamba atafurahi kama atakaa hapo milele. Wenger pia alimshukuru bosi wake huyo kwa kumpa heshima hiyo na kuonyesha kumuamini lakini akarudia kauli yake kwamba angependa kufanya kuisadia klabu hiyo kufanya vizuri msimu huu na hayo mengine yatafuata baadae. Arsenal inatarajia kusafiri kwenda Wales mwishoni mwa wiki hii kwenda kukwaana na Swansea City katika mechi ya Ligi Kuu nchini Uingereza.
FIFA YAIONYA TUNISIA.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limeionya serikali ya Tunisia kuingilia masuala ya soka baada ya waziri wa michezo wa nchi hiyo Tarek Dhiab kuliomba shirikisho hilo kuvunja uongozi wa soka wan chi hiyo. FIFA imeiataka serikali ya nchi hiyo kutoingilia masuala ya shirikisho la soka la nchi hiyo kwani watalazimika kuifungia nchi hiyo kama sheria zinavyosema. Hatua hiyo imepelekea Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ali Laarayedh kuitisha mkutano wa dharura ambao pia utahudhuriwa na wajumbe wa shirikisho hilo pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya michezo ili kujaribu kutatua tatizo lililopo. Mapema jana msemaji wa shirikisho la soka la nchi hiyo amesema kauli ya Dhiab inaweza kuwafanya wakafungiwa na FIFA hivyo kuzifanya timu zinashiriki michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika na Kombe la Shirikisho kukosa nafasi ya kuendelea.
MESSI AFIKA MAHAKAMANI KUHUDHURIA KESI YAKE YA UKWEPAJI KODI.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi na baba yake wanatarajiwa kufikishwa mahakamani nchini Hispania kujibu mashitaka ya ukwepaji kodi yanayowakabili. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 26 ambaye ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia mara nne mfululizo na baba yake Jorge Messi wanatuhumiwa na mamlaka kwa kukwepa kodi inayokadiriwa kufikia euro milioni nne. Wote wawili wanahisiwa kutumia kampuni za nje kuuza haki za kutumia picha ya Messi kinyume cha utaratibu. Messi na baba yake walikana tuhuma tuhuma hizo ambazo zilifanyika katika kipindi cha mwaka 2007 na 2009.
BALOTELLI AOMBA RADHI.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya AC Milan, Mario Balotelli ameomba radhi kuhusiana na tukio lililopelekea kufungiwa mechi tatu kwa kuzozana na mwamuzi. Nyota huyo wa kimataifa wa Italia alifungiwa kwa kumtukana na kumtishia mwamuzi mwishoni mwa mechi ambayo Milan ilifungwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Napoli. Balotelli alipewa kadi ya njano katika kipindi cha pili na kuongezwa kadi nyingine ambayo ilipelekea kupewa kadi nyekundu baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa kwa kosa la kumtishia mwamuzi. Akihojiwa Balotelli aliomba radhi wachezaji wenzake na mwamuzi wa mchezo huo kwa tabia aliyoonyesha baada ya mchezo huo na kuahidi kwamba atajitahidi kudhibiti hasira zake huko mbele.
Thursday, September 26, 2013
TATIZO LA UINGEREZA SIO WAGENI NI MBINU - VIEIRA.
NGULI wa soka wa zamani wa Ufaransa, Patric Vieira amedai kuwa kushindwa kwa timu ya taifa ya Uingereza kufanya vyema katika michuano mikubwa ni suala la ufundishaji na sio wachezaji wa kigeni wanaocheza katika Ligi Kuu. Mwenyekiti wa Chama cha Soka nchini Uingereza-FA, Greg Dyke hivi karibuni alidai kuwa timu ya taifa ya nchi hiyo inahitaji wachezaji zaidi wa kiingereza ambao wanacheza mara kwa mara katika vilabu vikubwa. Lakini Vieira anapingana na kauli hiyo ya Dyke na anadhani tatizo liko ndani zaidi hapo kuliko kudai uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni. Vieira amesema nchi hiyo inabidi kubadili mfumo wa ufundishaji ili uweze kwenda na wakati wa soka la kisasa. Nyota huyo ambaye kwasasa ni mwalimu wa kuinua vipaji katika klabu ya Manchester City amesema anadhani mchezo wa soka umebadilika kwa kiasi kikubwa hivyo hakuna jinsi inabidi na mbinu za ufundishaji pia nazo zibadilike. Uingereza haijawahi kwenda zaidi ya hatua ya robo fainali katika michuano ya Kombe la Dunia toka watinge nusu fainali mwaka 1990 na kushinda kombe hilo mara moja mwaka 1966.
QATAR YALALAMIKIWA KUWANYANYASA WAFANYAKAZI WA KIGENI.
WARATIBU wa michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar wamedai kushangazwa na matokeo ya uchunguzi ya jinsi wafanyakazi wa kigeni wanavyotendwa nchini humo. Kamati hiyo pia imesema serikali ya Qatar itafanyia kazi tuhuma zilizotolewa na gazeti la The Guardian kuhusiana na sakata hilo. Gazeti hilo lilidai wafanyakazi raia wa Nepal nchini Qatar wananyonywa na kunyanyaswa kwa kufanywa kama watumwa. Katika taarifa yake ofisa mkuu wa kamati hiyo ya maandalizi, Hassan Al Thawadi ameshangazwa na tuhuma hizo zilizotolewa na gazeti hilo na kudai kuwa watalifanyia uchunguzi ili kujua undani wake.
JUVENTUS "YAPOZI" KUFANYA MAZUNGUZO NA PIRLO KUHUSU MKATABA MPYA.
MKURUGENZI mkuu wa klabu ya Juventus ya Italia, Giuseppe Marotta amebainisha kusimamisha mazungumzo ya kumuongeza Andrea Pirlo mpaka mapema mwakani. Kiungo huyo wa kimataifa wa Italia mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa msimu wa 2013-2014 lakini Juventus wameonyesha kutokuwa na haraka na suala hilo. Pirlo alijiunga na Juventus kwa uhamisho huru akitokea AC Milan mwaka 2011 na ameisaidia timu hiyo kurejesha makali yake na kushinda taji la Serie A msimu uliopita huku akicheza karibu kilamechi toka kuanza kwa msimu mpya wa ligi. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34 hivi karibuni amesisitiza kuwa angependa kuongeza mkataba na Juventus lakini aliongeza kuwa atafanya hivyo kama akiona timu hiyo bado inamhitaji.
ARSENAL KUKWAANA NA CHELSEA KOMBE LA LIGI.
KLABU ya Arsenal imepangwa kuchezwa na Chelsea katika mchezo wa Kombe la Ligi mzunguko wa nne kwenye ratiba ya michuano hiyo iliyopangwa jana. Arsenal ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga West Bromwich Albion kwa changamoto ya mikwaju ya penati wakati Chelsea wao walisonga mbele kwa ushindi dhidi ya timu ya daraja la pili ya Swindon Town. Kwa upande mwingine Manchester United ambao wamewang’oa mahasimu wao Liverpool jana wamepangiwa kucheza na Norwich City katika Uwanja wa Old Traford. Timu zingine ni Tottenham Hotspurs watakwaana na Hull City, Newcastle United watacheza na Manchester City huku Sunderland wakiikaribisha Southampton. Mechi za mzunguko wa nne zinatarajiwa kuchezwa wiki inayoanzia Octoba 28 mwaka huu.
WAZIRI TUNISIA AOMBA FIFA KUVUNJA SHIRIKISHO LA NCHI HIYO.
WAZIRI wa michezo wa Tunisia, Tarak Dhiab ametuma barua rasmi kwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kutengua uongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo na kuzua msuguano mkubwa kati ya shirikisho hilo na wizara. Taarifa hizo zilipokelewa kwa mshangao mkubwa na wadau wa soka wa nchi hiyo ambapo hakuna sababu yoyote iliyotolewa na waziri kwa madai yake aliyoomba FIFA. Shirikisho hilo linatarajiwa kukutana katika mkutano wa dharura utakaohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya utendaji na wawakilishi kutoka wizara hiyo ili kujadili kinachoweza kutokea kutokana na maombi ya Dhiad. FIFA haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na hilo, hata hivyo msemaji wa shirikisho hilo Nabil Dabboussi amesema hatua hiyo ya waziri inaweza kupelekea vilabu vya Tunisia vikafungiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho.
Wednesday, September 25, 2013
MESSI AKASIRISHWA NA TAARIFA ZA UONGO DHIDI YAKE.
MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona, Lionel Messi amejibu kwa hasira taarifa kwamba alionyesha ishara baada ya kutolewa katika mchezo dhidi ya Real Sociedad ambao ulichezwa jana na Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 4-1. Katika mchezo huo Messi mwenye umri wa miaka 26 alifunga bao lake la saba msimu huu lakini kocha Gerard Martino alimtoa nje zikiwa zimebakia dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika. Vyombo vya habari vya Hispania viliripoti kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina hakufurahishwa na hatua ya Martino kumtoa nje. Akijibu tuhuma hizo Messi amekanusha kuonyesha ishara yoyote wakati akitoka na kudai kuwa hawezi kuvumilia uongo unaotolewa na vyombo vya habari.
LEWANDOWSKI KUJIUNGA NA BAYERN JANUARI.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Borussia Dortmund, Robert Lewandowski amebainisha kuwa atajiunga na Bayern Munich katika kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari mwakani na kumaliza utata juu ya mustakabali wake. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa akihusishwa na tetesi za kuhama Dortmund katika usajili wa majira ya kiangazi lakini klabu hiyo ilimkatalia kuondoka na kumlazimisha kucheza kwa msimu mwingine. Akihojiwa Lewandowski alithibitisha nia yake ya kwenda Munich na kwamba anatarajia kusaini mkataba Januari utakamuwezesha kujiunga na wababe hao wa soka nchini Ujerumani. Nyota huyo wa kimataifa wa Poland amefunga mabao 80 katika mechi 149 alizoichezea Dortmund toka ajiunge nao akitokea Lech Poznan mwaka 2010.
BOLT ATAKA KUMPIGA MSASA BALE KWENYE MBIO.
MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt wa Jamaica anaamini kuwa mshambuliaji nyota wa klabu ya Real Madrid ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi duniani lakini bingwa huyo anayeshikilia rekodi ya dunia kwenye mbio za mita 100 amesema anaweza kumfanya Bale kuwa na kasi zaidi. Bale alikimbia kwa kasi mpaka kufikia kilometa 40 kwa saa wakati wa mchezo baina ya Madrid na Villarreal akiwa nyuma kidogo ya kasi aliyotumia Bolt wakati anaweka rekodi ya dunia. Bolt ambaye anashikilia ubingwa wa olimpiki na dunia katika mbio za mita 100 na 200 amesema anaweza kumfundisha Bale kukimbia kwa kasi zaidi kama mchezaji huyo na Madrid watamuhitaji. Bolt aliongeza kuwa amewahi kufanya mazoezi na Cristiano Ronaldo na yuko tayari kufanya hivyo na nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs.
Tuesday, September 24, 2013
VAN PERSIE KUIKOSA LIVERPOOL.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester United anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwenye mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Liverpool baadae leo. Nyota huyo alipata majeraha ya msuli kabla ya mchezo dhidi ya mahasimu wao Manchester City uliofanyika katika Uwanja wa Etihad Jumapili iliyopita. Akihojiwa kuhusiana na hali ya Van Persie, meneja wa United David Moyes alithibitisha kumkosa nyota huyo katika mchezo dhidi ya Liverpool lakini anategemea atakuwa fiti kwa ajili ya mechi dhidi ya West Brom JUmamosi ijayo. Moyes pia amesema huu ni wakati wa kusahau kipigo cha mabao 4-1 walichopata kutoka kwa mahasimu wao City na anaamini bado anaendelea kuwaelewa wachezaji wake vyema.
BALE KUIVAA ATLETICO - ANCELOTTI.
MENEJA wa klabu ya Real Madrid amethibitisha kuwa mshambuliaji wake nyota Gareth Bale atakuwa fiti kabla ya mchezo dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid utakaopigwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Jumamosi. Bale alitakiwa kuwepo katika kikosi cha Madrid kilichoisambaratisha Getafe kwa kushinda mabao 4-1 Jumapili iliyopita lakini ilishindikana baada ya kuumia dakika za mwisho kabla ya kuanza kwa mechi hiyo. Ancelotti amesema nyota tayari ameanza kuafanya mazoezi mepesi mwenyewe na anadhani mpaka Jumamosi atakuwa tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Atletico. Kocha pia alikanusha tuhuma kwamba amewahi kumtumia mchezaji huyo mapema baada ya kujiunga na Madrid akitokea klabu ya Tottenham Hotspurs kwa uhamisho uliovunja rekodi.
BOLT AONGEZA MKATABA MNONO NA PUMA.
BINGWA mara tatu wa michuano ya olimpiki, Usain Bolt ameongeza mkataba mpya mnono zaidi wa udhamini na kampuni ya vifaa vya michezo ya Ujerumani Puma mpaka baada ya michuano ya olimpiki 2016 jijini Rio de Janeiro. Mwanariadha huyo nyota wa mbio fupi kutoka Jamaica mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akidhaminiwa na Puma toka mwaka 2003 na mara ya mwisho kuongeza mkataba wake na kampuni hiyo ilikuwa mwaka 2010. Mapema Bolt alidai kuwa anaweza kustaafu baada ya michuano ya 2016 lakini amebadili kauli yake siku za hivi karibuni na kudai anaweza kuendelea mwaka mmoja zaidi baada ya michuano hiyo. Bolt ameshinda medali sita za dhahabu katika michuano ya olimpiki na nane zingine katika mashindano ya riadha ya dunia mpaka sasa huku akishikilia rekodi ya kukimbia kwa kasi zaidi duniani kwenye mbio za mita 100.
ISTANBUL YAITISHIA WEMBLEY KATIKA KINYANG'ANYIRO CHA KUANDAA MICHUANO YA EURO 2020.
CHAMA cha Soka nchini Uingereza-FA kinaamini kuwa jiji la Istanbul liko mstari wa mbele katika mbio za kuwania nafasi ya kuandaa mechi za nusu fainali na fainali ya michuano ya Ulaya 2020. Katibu mkuu wa FA, Alex Horne amesema jijini hilo ndio watakuwa wapinzani wakubwa wa Wembley katika kuandaa mechi hizo baada ya Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kutangaza nchi 32 ambazo zimeonyesha nia ya kuandaa mechi hizo. Horne amesema baada ya Istanbul kupoteza nafasi ya kuandaa michuano ya olimpiki 2020 kwa Tokyo anadhani watapewa kipaumbele katika michuano ya hiyo. Mapema mwaka huu UEFA ilifikia maamuzi ya kuandaa michhuano hiyo katika miji 13 tofauti barani Ulaya badala ya nchi moja kama ilivyozoeleka hapo awali.
MTUKUTU BALOTELLI AFUNGIWA MECHI TATU.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya AC Milan, Mario Balotelli amefungiwa mechi tatu na kamati ya Ligi Kuu nchini Italia baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kwa kuzozana na mwamuzi katika mchezo dhidi ya Napoli Jumapili iliyopita. Balotelli ambaye alikosa penati na kufunga bao la kufutia machozi kwa timu yake katika dakika za majeruhi alipewa kadi ya pili ya njano na mwamuzi baada ya mpira kumalizika. Kwa kawaida mchezaji anayepewa kadi mbili za njano katika mchezo hukosa mechi moja lakini Balotelli amengezwa mechi mbili zaidi kwa tukio hilo la kumzonga mwamuzi hadharani. Mbali na adhabu hiyo ya Balotelli, Milan nao pia wamepewa adhabu ya kucheza bila mashabiki katika uwanja wao wa San Siro kwenye mechi nyingine ya ligi watakayocheza nyumbani kwasbabu ya mashabiki wao kufanya vitendo visivyo vya kiungwana kwa wenzao wa Napoli.
Monday, September 23, 2013
BALOTELLI ANATAKIWA AJIFUNZE KUFUNGA DOMO LAKE - ALLEGRI.
MENEJA wa klabu ya AC Milan, Massimiliano Allegri amemuonya Mario Balotelli kujifunza kufunga mdomo wake baada ya nyota huyo kupewa kadi nyekundu baada ya filimbi ya mwisho ambapo Milan walichapwa mabao 2-1. Katika mchezo huo Balotelli alikosa penati yake ya kwanza katika maisha yake ya soka la kulipwa na baadae kujikuta akipokea kadi ya pili ya njano kwa kuzozana na mwamuzi baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa. Alegri amesema akama mchezo umekwisha ni vizuri ukanyamaza kwani kuzozana na mwamuzi hakuwezi kubadilisha mchezo inabidi ajifunze hilo. Milan mpaka sasa imeambulia alama nne katika mechi nne za Serie A walizocheza lakini Allegri bado ana imani na kikosi chake kwamba kinaweza kubadilika na kufanya vyema katika siku zijazo.
MADRID KUMKOSA BALE JUMATANO.
KLABU ya Real Madrid imethibitisha kuwa winga wake mahiri Gareth Bale amepata maumivu ya paja hivyo kuwa na hatihati ya kukosekana katika mchezo wa Jumatano dhidi timu ya Elche. Bale alitarajiwa kuwemo katika kikosi cha Madrid kwenye mchezo dhidi ya Getafe Jana lakini aliondolewa baada ya kupata majeraha hayo wakati wakipasha misuli moto kabla ya mechi. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo imedai kuwa vipimo alivyofanyiwa Jumatatu asubuhi vimegundua tatizo hilo ambalo linaweza kumuweka nje ya uwanja kwa siku kadhaa. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Ancelotti amesema Bale anatarajiwa kuwa fiti katika mechi ya Jumamosi ijayo dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid, ingawa hata hivyo hakuwa na uhakika wa nafasi yake kwenye mechi ya katikati ya wiki.
SARE YAMSONONESHA BLANC.
MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Laurent Blanc ameeleza kusikitishwa kwake na matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Monaco jana na kudai kuwa kikosi chake kilihitaji matokeo mazuri zaidi ya hayo. Bao la mapema lilifungwa na Zlatan Ibrahimovic liliipa uongozi wa mapema PSG kwenye mchezo huo lakini mshambuliaji nyota wa Monaco Radamel Falcao alisawazisha bao hilo dakika 20 baadae na kupelekea timu hizo kugawana alama. Blanc amesema pamoja na kwamba Monaco walicheza vyema lakini kama na wao wangetumia vyema nafasi nyingi za wazi walizopata hakuna shaka kwamba wangeibuka kidedea kwenye mchezo huo. Kocha amesema inabidi wachezaji wachezaji wake wafanyie kazi suala hilo kwani kama wanatengeneza nafasi nyingi halafu wanakuwa hawazitumii sio rahisi kupata matokeo wanayohitaji. PSG inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1 wakiwa nyuma Monaco kwa alama mbili.
NAPOLI BADO HAIJAFIKIA KILELE CHAKE - BENITEZ.
MENEJA wa klabu ya Napoli, Rafael Benitez amesisitiza kuwa kikosi chake hakijafikia kiwango chake cha ubora kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AC Milan katika mchezo wa Ligi ya Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A uliofanyika jana. Mabao yaliyofungwa na Miguel Angel Britos na Gonzalo Higuain yaliisaidia Napoli kupata ushindi mwembamba katika Uwanja wa San Siro na kukwea mpaka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Serie A wakipishana kwa tofati ya mabao na vinara AS Roma. Pamoja na matokeo hayo Benitez anaamini kuwa Napoli bado ina nafasi kucheza vizuri zaidi ya ilivyo sasa na kuahidi kufanyia kazi mapungufu yaliyopo ili waweze kufanya vizuri zaidi huko mbele. Benitez pia aliwasifu wapinzani wao kwa kucheza vyema na kuwapa wakati mgumu mpaka dakika za mwisho huku akimsifu nyota wa Milan Mario Balotelli kwa kuwasumbua mabeki wake muda wote wa mchezo huo.
GABON YAMTIMUA KOCHA WAKE.
SHIRIKISHO la Soka la Gabon limetangaza kumtimua kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Paulo Duarte kufuatia kuenguliwa katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Katika taarifa yake shirikisho hilo lilidai kufikia hatua baada ya kuona mwenendo mbovu wa timu hiyo ambayo mbali na kushindwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia lakini ilishindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika mapema mwaka huu. Taarifa hiyo iliongeza kuwa kocha huyo Mreno hataondoka moja kwa moja kwani ataendelea kufanya kazi kama mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho hilo. Duarte mwenye umri wa miaka 44 pia amewahi kuinoa timu ya taifa ya Burkina Faso 2008 mpaka 2012 kabla hajatimuliwa kwa kushindwa kufanya vyema katika michuano ya mataifa ya Afrika iliyofanyika Gabon na Equatorial Guinea mwaka 2012.
MOYES ASINGIZIA RATIBA NGUMU.
MENEJA wa klabu ya Manchester United, David Moyes amelalamikia ratiba ngumu ya waliyopangiwa timu yake msimu huu kufuatia kipigo cha mabao 4-1 walichopata kutoka kwa mahasimu wao Manchester City. Kufuatia kipigo hicho cha jana ambacho kimeiacha United ikigaagaa katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, Moyes amerudia tena kauli yake kwamba wamepangiwa ratiba ngumu mwanzoni mwa msimu. Moyes amesema ana wasiwasi na ratiba ilivyopangwa kwani anaona kama ilipendelea na kuipa timu yake wakati mgumu mwanzoni. Mwanzoni mwa kampeni yao ya kutetea taji lao la ligi United walipoteza mchezo dhidi ya Liverpool kwa kufungwa bao 1-0 na baadae kutoa sare ya bila kufungana na Chelsea katika Uwanja wa Old Trafford. Lakini pamoja na malalamiko hayo Moyes amepania kusahau matokeo hayo na kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo kwani msimu wa ligi bado mrefu na wana nafasi ya kurejesha morali yao ya ushindi.
DI CANIO ATIMULIWA SUNDERLAND.
KLABU ya Sunderland imemtimua kocha wake Paolo Di Canio kufuatia kichapo cha mabao 3-0 ilichopata timu hiyo kutoka West Bromwich Albion katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza uliochezwa Jumamosi iliyopita. Di Canio ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Italia, anaiacha Sunderland ikiwa mkiani mwa msimo wa ligi kwa kuambulia alama moja katika mechi tano walizocheza mpaka sasa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 aliwajia juu wachezaji wake baada ya kipigo cha Jumamosi kwa kushindwa kujituma na kuonyesha ushirikiano pindi wawapo uwanjani hatua ambayo inapelekea kupata matokeo mabovu. Di Canio ambaye alianza kucheza soka katika Ligi Kuu nchini Italia kabla ya kuhamia ligi kuu na kucheza kwa misimu saba katika vilabu vya Sheffield Wednesday, West Hama United na Charlton Athletic alianza kazi ya umeneja katika klabu ya Swindon Town. Aliteuliwa kuwa meneja wa Sunderland Machi mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili baada ya Martin O’Neill kutimuliwa kipindi hicho.
TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.
PAMBANO LA AZAM, YANGA LAINGIZA MIL 138/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 walikuwa 24,020. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 21,079,525.42. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh. 10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,923,014.64. Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000.
MECHI YA TOTO, POLISI DOM KUPIGWA J2Mechi namba 12 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Toto Africans na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imesogezwa mbele kwa siku moja. Timu hizo za kundi C sasa zitapambana Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo ili kupisha mechi namba 10 kati ya Pamba na Stand United FC ya Shinyanga itakayochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu). Mechi nyingine za kundi hilo zitakazochezwa Jumamosi ni Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) wakati Kanembwa JKT na Polisi Mara zitacheza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 walikuwa 24,020. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 21,079,525.42. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh. 10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,923,014.64. Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000.
MECHI YA TOTO, POLISI DOM KUPIGWA J2Mechi namba 12 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Toto Africans na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imesogezwa mbele kwa siku moja. Timu hizo za kundi C sasa zitapambana Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo ili kupisha mechi namba 10 kati ya Pamba na Stand United FC ya Shinyanga itakayochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu). Mechi nyingine za kundi hilo zitakazochezwa Jumamosi ni Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) wakati Kanembwa JKT na Polisi Mara zitacheza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Sunday, September 22, 2013
SIMBA, MBEYA CITY ZAINGIZA MIL 123/-.
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mbeya City iliyochezwa jana (Septemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 123,971,000. Watazamaji 21,936 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 32 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 30,064,741.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 18,910,830.51. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 15,287,156.92, tiketi sh. 3,145,790, gharama za mechi sh. 9,172,294.15, Kamati ya Ligi sh. 9,172,294.15, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,586,147.08 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,567,003.28.
CHISORA ANYAKUWA TAJI LA HEAVYWEIGHT BARANI ULAYA.
BONDIA Dereck Chisora wa Uingereza amefanikiwa kumtandika Edmund Gerber katika raundi ya tano na kufanikiwa kushinda taji la uzito wa juu la Ulaya katika pambano lililofanyika jijini London. Chisora ambaye ni mzaliwa wa Zimbabwe alioenekana kumzidi Gerber kuanzia raundi raundi ya tatu mpaka Mjerumani huyo aliposhindwa kabisa kuendelea kwenye raundi ya tano. Bondia huyo ambaye sasa ameshinda mapambano 18 kati ya 22 aliyocheza, amesema anataka kupigana kugombea taji la dunia kwa mara nyingine baada ya kupigwa kwa pointi na Vitali Klitschko. Kwa upande mwingine pambano la mabondia David Haye na Tyson Fury wote wa Uingereza lililokuwa lifanyike Septemba 28 limesogezwa mbele baada ya Haye kuumia kwa kujikata wakati akiwa mazoezini. Haye mwenye umri wa miaka 32 alijikata juu ya jicho lake wakati akiwa mazoezini hatua ambayo ilipelekea kushonwa nyuzi sita ambazo zitaondolewa baada ya siku sita mpaka saba.
NILIOGOPA KWENDA KUKAA BENCHI CITY - ERIKSEN.
NYOTA mpya wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Christian Eriksen amekiri kuwa aliitosa klabu ya Manchester City kwasababu alikuwa anataka kuepuka kukaa benchi. Eriksen ameanza vyema maisha mapya White Hart Lane na kuwashangaza mashabiki katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Norwich na kufunga bao lake la kwanza akiwa na klabu hiyo katika mchezo wa Europa League dhidi ya Tromso. Nyota huyo amekiri kuwa vilabu vingi vikubwa vya Ligi Kuu nchini Uingereza vilikuwa vikimmendea kabla ya kwenda Spurs na kubainisha kuwa City ndio klabu iliyokaribia kumsajili. Eriksen aliendelea kudai kuwa ilimchukua muda kwenda Uingereza kwasababu alikataa mara kadhaa na mwaka jana City walitaka kumsajili lakini alisita kwasababu hakuwa na uhakika wa kucheza akienda huko.
BAYERN, DORTMUND WAKABANA KOO BUNDESLIGA.
KLABU ya Bayern Munich imefanikiwa kuifikia Borussia Dortmund kileleni kwa kuwa na alama sawa kwenye msimamo wa Ligi nchini Ujerumani maarufu kama Bundesliga baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Schalke jana. Mabao yaliyofungwa na Bastian Schweinsteiger na Mario Mandzukic katika kipindi cha kwanza na mengine ya Franck Ribery na Claudio Pizarro katika kipindi cha pili yaliyosha kuwapa Bayern ushindi huo huku hicho kikiwa kipigo chake cha kwanza kikubwa kwa Schalke nyumbani toka mwaka 1981. Mapema jana Dortmund walipoteza rekodi yao ya asilimia mia moja kwa kutoa sare ya bao 1-1 na Nuremberg katika mechi nyingine ya Bundesliga. Bayern na Dortmund zote zina alama 16 katika mechi sita walizocheza na pia wakiwa sawa kwa tofauti ya mabao lakini Dortmund wako kileleni kwasababu wamefunga mabao mengi zaidi ya Bayern.
ESPERANCE YAMALIZA MAKUNDI KWA USHINDI ASILIMIA MIA MOJA.
KLABU ya Esperance ya Tunisia imefanikiwa kupata ushindi wa ugenini baada ya kuifunga Coton Sport ya Cameroon kwa mabao 2-1 katika mechi za mwisho za makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mabingwa mara mbili wa Afrika wanafukuzia taji lao la tatu la michuano hiyo ikiwa ni miaka miwili pekee imepita toka wanyakuwe taji lingine. Esperace ambao wako katika kundi B tayari walikuwa wameshajihakikishia nafasi ya kusonga mbele kabla ya mchezo huo wakiwa na alama saba zaidi Coton Sport ambao nao pamoja nakipigo hicho lakini walisonga mbele baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo. Coton sasa watakwaana na mshindi wa kundi A ambaye ni Al Ahly katika hatua ya nusu fainali huku Esperance wao wakionyeshana kazi na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambao wameshika nafasi ya pili katika kundi A.
Saturday, September 21, 2013
UINGEREZA, SCOTLAND, WALES NA JAMHURI YA IRELAND KUTAFUTA UENYEJI EURO 2020.
SHIRIKISHO LA Soka barani Ulaya-UEFA limedai kuwa nchi za Uingereza, Scotland, Wales na Jamhuri ya Ireland ni mojawapo ya nchi zilizotuma maombi ya kuandaa mechi za michuano ya Ulaya 2020. UEFA imesema jumla ya nchi 32 ambao ni wanachama wake zimeonyesha nia ya kuandaa michuano hiyo baada ya maamuzi ya kufanya mashindano kuchezwa katika miji 13 kuzunguka bara la Ulaya. Uingereza inataka kuandaa mechi zake jijini London, Scotland imechagua Glasgow, Wales wamechagua mji wa Cardiff wakati Jamhuri ya Ireland wao watatumia mji wa Dublin. Mbali na hao lakini pia nchi vigogo wa soka barani humo wakiwemo Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uholanzi na Hispania pia na zenyewe zimeonyesha nia ya kutaka kuandaa mechi za michuano hiyo. UEFA itatoa uamuzi Septemba 25 mwakani nchi 13 ambazo zitakuwa wenyeji wa michuano hiyo.
TOTTI AONGEZA MIAKA MIWILI ROMA.
KLABU ya AS Roma ya Italia imethibitisha kuwa nyota wake Francesco Totti amesaini mkataba wa miaka miwili ambao utanfanya kubakia Stadio Olimpico mpaka 2016. Mkataba wa sasa wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu lakini baada ya kufanya mazungumzo ya kina na viongozi wa klabu hiyo nguli huyo alibainisha kuwa ameamua kubakia. Akizungumza na waandishi wa habari Totti amesema amefurahi kupata miaka mingine miwili na ana uhakika itakuwa yenye mafanikio huku pia akimshukuru rais wa klabu hiyo James Pallota na watu wote waliofanikisha. Totti alitangaza kustaafu majukumu ya kimataifa baada ya Italia kushinda Kombe la Dunia 2006 lakini kiwango kikubwa alichoonyesha msimu uliopita ambapo alifunga mabao 12 katika mechi 36 za Serie A, kimezua tetesi kuwa anaweza kurejea katika kikosi cha timu ya taifa.
MAN UNITED, CITY KUONYESHANA KAZI.
KLABU mahasimu kutoka mji mmoja za Manchester United na Manchester City zitajitupa uwanjani kukwaana kwa mara ya 166 huku kila mmoja akijua kipigo kitamuweka katika hatari ya kukaa mbali katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu nchi Uingereza. Katika msimu huu ni mechi pekee zimeshachezwa na kila timu mpaka sasa lakini timu zote hizo tayari zimeshapoteza alama ambapo United ilitoa sare na Chelsea na baadae kupoteza mchezo dhidi ya Liverpool huku City wao wakitoa sare na Stoke City na kupata kipigo kutoka kwa Cardiff City. Timu zote mbili ziko nyuma ya vinara wa ligi hiyo Liverpool kwa alama tatu na kama timu yoyote ikifungwa kwenye mchezo huo itajikuta ikiwa nyuma kwa alama sita hatua ambayo itawawia vigumu kupanda tena. Makocha wa timu zote mbili David Moyes wa United na Manuel Pellegrini wa City hiyo itakuwa mechi yao ya kwanza kukutana lakini Moyes ndio anayepewa nafasi kubwa kwasababu alikuwa na rekodi nzuri ya kuifunga City wakati akiinoa Everton. Katika misimu sita aliyokuwa meneja wa Everton, Moyes ameshinda mechi tisa kati ya 12 ambazo alikutana na City.
FIFA YASHTUSHWA NA UVUNJIFU WA SHERIA KATIKA MECHI ZA KUFUZU KOMBE LA DUNIA AFRIKA.
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limestushwa na jinsi timu za Afrika zilivyovunja sheria kwa kuchezesha wachezaji wasioruhusiwa katika mechi zake za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Mechi nane katika kinyang’anyiro hicho zilikumbwa na matatizo hayo kwasababu timu mojawapo ilichezesha mchezaji ambaye uraia wake una utata au yuko katik adhabu. Katika kesi zote hizo baadhi ya timu zilijikuta zikipewa ushindi wa mabao 3-0 baada ya wapinzani wao kukutwa na hatia hivyo kuathiri msimamo wa makundi kwa kiasi kikubwa. Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF, Mustapha Fahmy amesema kuna haja ya kulifanyia kazi suala hilo ili kujua kiini cha matatizo hayo na kujaribu kuzia yasije tokea tena siku za usoni. Mojawapo ya kesi za hivi karibuni ni Cape Verde kukosa nafasi ya kucheza hatua ya mtoano ili kupata timu tano za Afrika zitakazokwenda Brazil mwakani kwa kumchezesha mchezaji aliyekuwa kwenye adhabu katika ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Tunisia.
ANCELOTTI ALINIBAKISHA MADRID.
WINGA mahiri wa klabu ya Real Madrid, Angel Di Maria amebainisha kuwa aliamua kubakia klabuni hapo baada ya kujadiliana mustakabali wake na muargentina mwenzake anayecheza klabu ya Paris Saint-Germain Ezequiel Lavezzi na kocha wake carlo Ancelotti. Kulikuwa na tetesi kuwa winga huyo alikuwa akitaka kuondoka Santiago Bernabeu mapema katika kipindi cha usajili wa majira wa kiangazi lakini alichagua kubakia pamoja na ugumu wa kupata namba katika kikosi cha Madrid kilichosheheni nyota kibao. Di Maria amesema aliamua kubakia pamoja na kujua aina ya wachezaji ambao wangekuja klabuni hapo kwasababu anajiamini kwa kipaji alichokuwa nacho. Nyota huyo anasema mbali na kuzungumza na Lavezzi lakini pia alizungumza na Ancelotti na alimuhakikishia kuwa mchezaji atakayekuwa bora ndio atakayempanga katika kikosi chake cha kwanza.
Thursday, September 19, 2013
WORLD CUP 2022: WAJUMBE WA UEFA WAUNGA MKONO MICHUANO HIYO KUCHEZWA MAJIRA YA BARIDI.
WAJUMBE kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa Shirikisho la Soka barani Ulaya wameunga mkono mpango wa kuhamisha michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kuchezwa katika majira ya baridi baada ya kukubaliana kwamba haitawezekana michuano hiyo kuchezwa katika majira ya kiangazi kama ilivyo kawaida. Makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Duiani-FIFA Jim Boyce alithibitisha kuwa jambo walilokubaliana katika mkutano huo ni kwamba Kombe la Dunia nchini Qatar haliwezi kuchezwa katika majira ya kiangazi. Hata hivyo Boyce aliongeza kuwa kila mtu amekubaliana na hilo lakini ni tarehe halisi ya kuhamisha michuano hiyo ndio hawajafikia maamuzi yake. Suala la michuano hiyo kuandaliwa majira ya kiangazi nchini Qatar limekuwa likizua mjadala mkubwa kutokana na joto kali katika kipindi hicho linaloweza kufikia nyuzi joto 50. Kamati ya Utendaji ya FIFA inatarajiwa kukutana Octoba 3 mwaka huu huko jijini Zurich, Switzerland ili kujadili mapendekezo ya kuhamisha michuano hiyo katika majira ya baridi.
SUAREZ YUPO FITI - RODGERS.
MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amesema mshambuliaji nyota wa timu hiyo Luis Suarez yuko tayari kurejea katika kikosi cha kwanza baada ya wiki kadhaa za kufanya mazoezi na maandalizi mazuri. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay atamaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi 10 kwa kumuuma beki wa Chelsea Branislav Ivanovic April mwaka huu, katika mchezo dhidi ya Southampton Jumamosi. Hiyo itakuwa habari njema kwa Rogders kumtumia nyota huyo katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Manchester United Jumatano ijayo. Lakini meneja huyo alipuuza habari hizo na kudai kuwa hana uhakika kama atamtumia Suarez katika kikosi chake cha kwanza kwenye mchezo huo pamoja na kwamba anajua amefanya mazoezi ya kutosha wakati akiitumikia adhabu yake.
CESAR AVUNJIKA KIDOLE MAZOEZINI.
KLABU ya Queens Park Rangers-QPR imetangaza kuwa golikipa wake Julio Cesar atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita mpaka nane kutokana na majeraha. Cesar alifanyiwa upasuaji baada ya kuvunjika kidole chake cha mkono wa kushito wakati wa mazoezi Jumanne. Golikipa huyo alitegemewa kuondoka QPR mara baada ya klabu hiyo kushuka daraja masimu uliopita lakini ilishindikana kutokana na kukosa ofa aliyohitaji kutoka timu zingine. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ndio golikipa chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ambacho kinanolewa na Luis Felipe Scolari na kuna uwezekano mkubwa wa kukosa mechi za kimataifa za kirafiki dhidi ya Korea Kusini na Zambia mwezi ujao.
WACHEZAJI WAMEKOSA UKOMAVU - MOURINHO.
MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekiri kikosi chake kinakosa ukomavu baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa FC Basel katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya uliofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge. Katika mchezo huo wenyeji Chelsea ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Oscar muda mchache kabla ya mapumziko lakini Basel walinikiwa kubadilisha matokeo katika kipindi cha pili kwa mabao yaliyofungwa na Mohamed Salah na Marco Streller. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Mourinho amesema anafikiri kikosi chake kimekosa ukomavu wa kutosha ili kupambana na shinikizo lolote linalotokea katika mechi. Mourinho amesema watakwenda nyumbani wakiwa na huzuni kutokana na kipigo hicho lakini wataamka na kuufanyia kazi udhaifu wao ili kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao nyingine.
MBABE WA MOHAMMAD ALI AFARIKI DUNIA.
BINGWA wa zamani wa ngumi za uzito wa juu, Ken Norton wa Marekani ambaye alimtandika Mohammad Ali amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Norton ambaye afya yake ilianza kuyumba baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi na kupooza sehemu kubwa ya mwili wake, amefariki dunia akiwa katika kliniki moja iliyopo jijini Las Vegas, Nevada. Bondia huyo alimvunja Ali taya katika pambano lao walilocheza kwa mara ya kwanza jijini San Diego, California mwaka 1973 ambapo alishinda pambano hilo. Katika pambano lao la mwisho lililofanyika Septemba mwaka 1976 katika Uwanja wa Yankee uliopo jijini New York, Ali alishinda kwa ushindi mwembamba na kurejesha taji lake la uzito wa juu. Norton alianza kucheza ngumi wakati akiwa mwajiriwa wa jeshi la wanamaji nchini Marekani na muda mfupi baadae aliacha shughuli za jeshi na kuingia katika ulimwengu wa ngumi za kulipwa mwaka 1967. Bondia huyo alishinda taji lake la kwanza la uzito wa juu mwaka 1977, na baada ya kustaafu alijishughulisha na mambo ya utangazaji na pia kushirikishwa katika sinema kadhaa.
TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.
MIL 58/- ZAPATIKANA MECHI YA SIMBA, MGAMBO
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mgambo Shooting Stars iliyochezwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 58,365,000. Watazamaji 10,241 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 23 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 6-0. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 13,839,327.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,903,135.59. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,036,946.16, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 4,222,167.70, Kamati ya Ligi sh. 4,222,167.70, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,111,083.85 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,641,954.10.
MIKATABA YA MAKOCHA VPL, FDL YATAKIWA TFFShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa siku 14 kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na za Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) kuwasilisha mikataba ya makocha wao. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Septemba 12 mwaka huu imebaini klabu nyingi hazijawasilisha mikataba ya mabenchi yao ya ufundi, kitu ambacho ni matakwa ya kikanuni. Siku hizo 14 zimetolewa kuanzia Septemba 17 mwaka huu. Kwa klabu ambazo zitashindwa kuwasilisha mikataba hiyo na vielelezo vingine ndani ya mudau huo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mgambo Shooting Stars iliyochezwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 58,365,000. Watazamaji 10,241 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 23 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 6-0. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 13,839,327.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,903,135.59. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,036,946.16, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 4,222,167.70, Kamati ya Ligi sh. 4,222,167.70, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,111,083.85 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,641,954.10.
MIKATABA YA MAKOCHA VPL, FDL YATAKIWA TFFShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa siku 14 kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na za Ligi ya Daraja la Kwanza (FDL) kuwasilisha mikataba ya makocha wao. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Septemba 12 mwaka huu imebaini klabu nyingi hazijawasilisha mikataba ya mabenchi yao ya ufundi, kitu ambacho ni matakwa ya kikanuni. Siku hizo 14 zimetolewa kuanzia Septemba 17 mwaka huu. Kwa klabu ambazo zitashindwa kuwasilisha mikataba hiyo na vielelezo vingine ndani ya mudau huo zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.
Subscribe to:
Posts (Atom)