Friday, July 29, 2016

SHABIKI AKAMATWA CHUMBA CHA KUFULIA HOTELINI AKITAKA KUONANA NA NEYMAR.

SHABIKI wa nyota wa Barcelona, Neymar amekamatwa baada ya kukutwa katika chumba cha kufulia katika hoteli waliyofikia timu ya taifa ya Brazil kuelekea katika michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini Rio de Janeiro. Neymar na wachezaji wenzake kwasasa wanajiandaa na michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao ambapo wataanza kwa kucheza na Afrika Kusini Agosti 4 na pia kucheza na Iraq na Denmark katika mechi zao zingine za kundi A. Maandalizi yao yaliathiriwa kwa muda na kijana mwenye umri wa miaka 21 aliyefanikiwa kupenya na kuingia katika hoteli hiyo iliyopo katika mji wa Goiania. Ofisa wa polisi Vladimir Passos aliwaambia wanahabari kuwa wafanyakazi wa hoteli waligundua kitu tofauti na kuwaita kuja kumkamata kijana huyo ambaye alijitetea kuwa alikuwa akitaka kuonana na Neymar. Hata hivyo, inadaiwa kuwa baadae kijana huyo alihojiwa baada ya kuhojiwa na kugundulika alitumia kitambulisho feki cha Shirikisho la Soka la Brazil-CBF kilichomuwezesha kuingia hotelini humo.

KLOPP AMPONDA MOURINHO "KIAINA"

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp amekiri kuwa hatishiki na klabu mahasimu ambao wanasajili wachezaji kwa fedha nyingi na kudai kuwa yeye anataka kufanya mambo tofauti Merseyside. Kutokana na Manchester United chini ya Jose Mourinho kukaribia kufanya usajili wa kiungo wa Juventus Paul Pogba kwa zaidi ya paundi milioni 100, meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund anafurahia mipango yao ya usajili. Liverpool imesajili wachezaji wawili kwa fedha nyingi kiaangazi hiki ambao ni Saido Mane waliyemsajili kutoka Southampton kwa kiasi cha paundi milioni 34 na kiungo wa Newcastle United Georgio Wijnaldum aliyesajili kwa paundi milioni 23. Akihojiwa Klopp amesema kama unasajili mchezaji mmoja kwa paundi milioni 100 halafu anakuja kuumia mambo yote lazima yaende vibaya ndio maana hataki kutumia fedha nyingi kwa ajili ya mchezaji mmoja.

SCHWEINSTEIGER ATUNDIKA DARUGA SOKA LA KIMATAIFA.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Bastian Schweinsteiger ametangaza kustaafu rasmi soka la kimataifa. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 anayekipiga katika klabu ya Manchester United, alikuwa sehemu ya kikosi cha Ujerumani kilichotwaa Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014. Schweinsteiger anastaafu akiwa mchezaji wan ne kuitumikia nchi yake mechi nyingi zaidi, akiwa amecheza mechi 120 nyuma ya Lothar Matthaus aliyecheza mechi 150, Miroslav Klose mechi 137 na Lukas Podolski mechi 129. Nyota huyo aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Ujerumani mwaka 2004 na anashikilia rekodi ya kuichezea nchi hiyo mechi nyingi zaidi za michuano ya Ulaya, akiwa amecheza mechi 15.

DEAL ALMOST DONE: POGBA TO MAN UNITED.

KIUNGO wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba anatarajiwa kuwa mchezaji wa Manchester United kwa mara nyingine baada ya klabu hiyo kukubali kumsajili kwa kitita cha zaidi ya paundi 100 kutoka Juventus jana usiku. Hatua hiyo inamaanisha kuwa mchezaji huyo aliyeondoka Manchester United mwaka 2012, sasa atarejea kwa usajili utakaovunja rekodi ya dunia. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, anatarajiwa kukamilisha usajili wake huo baadae leo, baada ya wakala wake Mino Raiola kufanya mazungumzo zaidi na maofisa wa Juventus na mawakili jijini Turi jana mchana. Pogba anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya jijini Los Angeles baada ya kumaliza likizo yake huko Florida kabla ya kusaini mkataba wa miaka mitano ambao utamuwezesha kulipwa kiasi cha paundi 290,000 kwa wiki.

MSHINDI WA PUSKAS AWARD ATUNDIKA DARUGA.

MSHAMBULIAJI wa Brazil, Wendell Lira ameacha kucheza mpira miezi sita baada ya kushinda tuzo ya bao bora la mwaka inayojulikana kama Puskas Award, ili aweze kuanza kazi yake mpya ya kuwa mchezaji wa mipira ya kwenye video. Bao alilofunga nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa timu yake ya Goianesia dhidi ya Atletico Goianiense ndio lililompatia tuzo hiyo na kuwapiku nyota wengine kama Lionel Messi na Alessandro Florenzi katika tuzo za Ballon d’Or Januari mwaka huu. Lakini nyota huyo sasa ametangaza kutundika daruga zake na kuamua kujikita zaidi katika shughuli za michezo ya video. Moja ya sababu kubwa zilizomfanya kuachana na soka amesema ni uongo uliokithiri huku akishindwa kufafanua zaidi kwa undani suala hilo.

GUARDIOLA AELEZA UCHU WAKE KWA STONES.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amethibitisha kuwa na nia ya kumsajili beki wa Everton John Stones. Inadaiwa kuwa Everton wanataka kiasi cha paundi milioni 50 kwa ajili ya beki huyo mwenye umri wa miaka 22 ambaye kiangazi mwaka jana alikaribia kiduchu kujiunga na Chelsea. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo mara baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Borussia Dortmund ambao walishinda kwa changamoto ya mikwaju penati 6-5, Guardiola amesema kila mtu anafahamu kuwa watajaribu kumsajili. Stones alikuwa sehemu ya kikosi cha Uingereza kilichokwenda kushiriki michuano ya Ulaya mwaka huu lakini hakucheza mechi yeyote wakati nchi hiyo ilipotolewa katika hatua ya timu 16 bora.

KAZI ZA UN ZILINIPA UZOEFU WA KUFANYA KAZI FIFA - SAMOURA.

KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Fatma Samoura amesema miaka aliyotumia kufanya kazi katika kingo za vita wakati akiwa Umoja wa Mataifa ndio uliomuandaa kuja kufanya kazi yake hiyi mpya. Mwanamama huyo raia wa Senegal mwenye umri wa miaka 54, alianza rasmi kibarua chake katika shirikisho hilo mwezi uliopita. Akihojiwa Samoura amesema amefanya kazi karibu maeneo yote ya hatari duniani ikiwemo Afghanistan, Liberia, Sierra Leone, Timor ya Mashariki, Kosovo na Nigeria. Samoura aliendelea kudai kuwa anadhani miaka yake 20 iliyopita katika shughuli ilimuandaa vyema tayari kwa kibarua hicho. Samoura anakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa Katibu Mkuu wa FIFA toka kuanzishwa kwake.

Wednesday, July 27, 2016

KLABU KUFANYA MABADILIKO WACHEZAJI WANNE KATIKA FA MSIMU HUU.

KLABU zitaruhusiwa kutumia mchezaji wanne wa akiba wakati wa muda wa nyongeza katika hatua za mwishoni za michuano ya Kombe la FA msimu huu. Mfumo huo ambao unatarajiwa kupitishwa na Bodi ya Kimataifa ya Soka ulifanyiwa majaribio katika michuano ya Copa America kiangazi hiki. Sheria hiyo inatarajiwa kuanza kutumika katika Kombe la FA kuanzia hatua ya robo fainali. Ofisa mkuu wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA, Martin Glenn amesema hatua hiyo ni muhimu na ajili ya manufaa ya wachezaji. Michuano ya mwaka huu ya FA inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Ijumaa ya Agosti 5 wakati mechi 184 za hatua ya awali zitafanyika.

MASCHERANO AKUBALI KUBAKI BARCELONA.

KLABU ya Barcelona imetangaza kufikia makubaliano na Javier Mascherano juu ya mkataba mpya na ulioboreshwa wa miaka mitatu. Nyota huyo wa kimataifa wa Juventus amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Juventus ambao tayari wameshamsajili Dani Alves mapema kiangazi hiki. Hata hivyo, mkurugenzi wa taasisi ya mahusiano Albert Soler amethibitisha kuwa Mascherano amekubalia kubakia katika klabu hiyo aliyojiunga nayo mwaka 2010 akitokea Liverpool. Soler amesema kwasasa hawawezi kuzungumzia tena kuhusu Mascherano kwani tayari ameshakubali kuongeza miaka mingine mitatu. Taarifa hizo zimetoka wakati Barcelona wakimtambulisha kiungo wao mpya Andre Gomes ambaye wamemsajili kutoka Valencia kwa mkataba wa miaka mitano.

HIGUAIN APEWA NAMBA 9 JUVENTUS.

MSHAMBULIAJI mpya wa Juventus, Gonzalo Higuain amepewa jezi namba 9 kwa ajili ya kampeni za msimu 2016-2017. Higuain ambaye amejiunga na mabingwa hao wa Serie A kwa kitita cha euro milioni 90 na kuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa kwa fedha nyingi katika historia ya soka, alitambulishwa mbele ya mashabiki baada ya kukamilisha vipimo vya afya. Mashabiki wa Juventus walimpokea kwa shangwe shujaa wao huyo mpya ambaye ametua Turin akitokea kwa mahasimu wao Napoli. Jezi namba tisa imekuwa ikivaliwa na nyota kadhaa waliowahi kupita katika klabu hiyo akiwemo Alvaro Morata, Zlatan Ibrahimovic na Marcelo Salas.

GUARDIOLA APIGA CHINI VIBONGE CITY.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amewaengua mazoezini baadhi ya wachezaji wake katika kikosi cha kwanza mpaka hapo watakapofikia uzito unaohitajika. Beki wa timu hiyo, Gael Clichy amesema meneja huyo raia wa Uholanzi amewataka wachezaji kuepuka kula pizza, juice na vyakula vingine vizito ili kuepuka kuongezeka uzito. Akihojiwa kuhusiana na hilo, Guardiola amesema sio kwamba wachezaji hao wamezidi uzito lakini anataka wachezaji wake wawe fiti. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa suala la uzito ni muhimu kwani mchezaji anapokuwa hayupo fiti kuna athari kadhaa ikiwemo kushindwa kuwa kasi ya kutosha au kushindwa kuruka juu kwa haraka. City wanatarajiwa kukwaana na Borussia Dortmund kesho katika mchezo wa kirafiki wa michuano ya Kimataifa utakaofanyika huko Shenzhen, China.

ARSENAL MAJANGA.

BEKI wa Arsenal, Per Mertesacker anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa kufuatia kusumbuliwa na majeruhi ya goti yaliyomzuia kujiunga na wachezaji wenzake katika ziara ya Amerika Kaskazini. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alinainisha hayo katika mkutano wake na wanahabari kuelekea mchezo wao wa kirafiki dhidi ya nyota wa Ligi Kuu ya Marekani-MLS utakaofanyika huko San Jose. Wenger amesema Mertesacker alipata majeruhi hayo katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Lens Ijumaa iliyopita na sasa inabidi watafute mbadala ili wapate mchezaji mwenye uzoefu katika nafasi hiyo. Meneja huyo pia alithibitisha kuwa mchezaji mpya aliyesajiliwa msimu huu Granit Xhaka naye atapata nafasi ya kucheza katika mchezo huo.

IBRAHIMOVIC ABAINISHA KUMCHOMOLEA BECKHAM KWA AJILI YA UNITED.

MSHAMBULIAJI mpya wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic amebainisha kuwa alimkatalia David Beckham na Ligi Kuu ya Marekani-MLS kwa ajili ya kuja kufanya kazi na rafiki yake Jose Mourinho Old Trafford. Nyota huyo wa kimataifa wa Sweden aliondoka Paris saint-Germain-PSG mwishoni mwa msimu uliopita na kupata ofa kadhaa kabla ya kuamua kujiuanga na United na kucheza kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu. Beckham akiwa tayari ameshanunua ardhi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya jijini Miami, nahodha huyo wa zamani wa Uingereza alijaribu kumshawishi mchezaji mwenzake huyo wa zamani wa PSG kujiunga naye wakati klabu yake ikiw ana lengo la kuingia MLS mwaka 2018. Akihojiwa Ibrahimovic amesema Beckham ni rafiki yake mkubwa na alimuambia aende kucheza katika timu yake ya Miami lakini alimkatalia kwasababu anaamini wakati huu haukuwa muafaka. Nyota huyo amesema kwasasa anataka kufanya vitu vikubwa akiwa na United, labda pengine huko mbele ndio anaweza kufikiria kwenda MLS.

JUVENTUS WAKOMAA NA EURO MILIONI 120 KWA POGBA.

KLABU ya Juventus inadaiwa kunga’ang’ania kiasi cha euro milioni 120 kwa ajili ya kiungo Paul Pogba hivyo kuweka uhamisho wake kwenda Manchester United mashakani. Mabingwa hao wa Italia pia wanasisitiza United walipe ada ya wakala Mino Raiola kwa ajili ya dili hilo ambayo ni euro milioni 25 hivyo kumaanisha jumla iwe euro milioni 145 pamoja na mshahara wa euro 300,000 kwa wiki. Taarifa zilizozagaa zinadai kuwa ili usajili huo ukamilike Juventus ndio wanahitaji vitu hivyo jambo ambalo limewafanya United kutulia na kujipanga upya. Mara baada ya kukamilisha usajili wa Gonzalo Higuain jana, ofisa mkuu wa Juventus Beppe Marotta alidokeza kuhusu suala la Pogba akidai kuwa kwasasa kila kitu kimesimama kwanza.

Monday, July 25, 2016

BAADA YA KUACHWA, ARTETA AIFANYIA "UNDAVA" ARSENAL.

KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Mikel Arteta amehatarisha kuwaudhi mashabiki wa klabu hiyo kufuatia kufuta vitu vyote katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ambayo vinahusiana na wakati akiwa Emirates. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, aliondoka Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na kuchukua kibarua cha ukocha chini ya Pep Guardiola kwa mahasimu wao wa Ligi Kuu Manchester City. 
Kutokana na kutaka kuanza upya, Arteta alifuta vitu vyote vinavyohusiana na wakati akiwa Arsenal na sasa anafuatilia ukurasa rasmi wa klabu yake hiyo mpya sambamba na wachezaji wengi katika kikosi cha Guardiola. Hata hivyo, Arteta amewaacha baadhi ya marafiki zake wa Arsenal ambao ni Santi Carzola, Hector Bellerin na Petr Cech.

CHELSEA, EVERTON ZAPIGANA VIKUMBO KUMUWANIA KOULIBALY.

KLABU za Chelsea na Everton zimetajwa kumtaka Kalidou Koulibaly, huku beki huyo akitaka kuondoka Napoli kwa mujibu wa wakala wake. Wiki iliyopita taarifa zilizagaa kuwa beki huyo mwenye umri wa miaka 25 alitolewa ofa ya kwenda Arsenal, ingawa Arsene Wenger alikataa kiasi cha euro milioni 45 kilichohitajika. Everton na Chelsea zimekuwa zikimuwinda Koulibaly kipindi hiki cha usajili na wakala wa nyota huyo wa kimataifa wa Senegal, Bruno Satin amethibitisha mteja wake anaweza kwenda Ligi Kuu. Bruno amesema Jumamosi iliyopita walikutana na kujaribu juu ya kuongezewa mkataba mpya, hata hivyo hawakufikia muafaka kwani madhumuni makubwa ya mchezaji huyo ni kuondoka na sio kuongeza mkataba. Wakala huyo aliendelea kudai kuwa Napoli imekuwa ikisema Koulibaly ni mchezaji mkubwa lakini wamekuwa hawalioni hilo katika ofa yao ya mkataba mpya.

INTER YATHIBITISHA NAPOLI KUMUWINDA ICARDI.

MKURUGENZI wa michezo wa Inter Milan, Piero Ausilio amethibitisha kuwa wamekuwa mawasiliano na Napoli juu ya Mauro Icardi, wakati akisisitiza mshambuliaji huyo hatakwenda popote. Napoli wameamua kumfukuzia mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina kama mbadala wa Gonzalo Higuain ikiwa atakwenda Juventus. Hata hivyo, Ausilio amesema Napoli wanapoteza muda wao bure kwani hawana mpango wowote wa hata kuingia katika mazungumzo ya kumuuza nahodha wao huyo. Akiulizwa kuhusiana na suala hilo, Ausilio alikiri kuwepo kwa mawasiliano lakini hawana mpango wowote wa kuwauzia Napoli mshambuliaji huyo.

POCHETTINO ACHOMOA KUINOA ARGENTINA.

MENEJA Mauricio Pochettino amejitoa kufuatia tetesi kuwa anaweza kuchukua nafasi ya Gerardo Martino kama kocha wa mpya wa Argentina, na kudai kuwa huu sio wakati muafaka wa kuondoka Tottenham Hotspurs. Pochettino mwenye umri wa miaka 44, ni moja kati ya majina yaliyotajwa kuhusishwa na kibarua hicho kufuatia kujiuzulu kwa Martino baada ya Argentina kufungwa tena na Chile katika fainali ya michuano ya Copa America. Lakini Pochettino ambaye amesaini mkataba mpya wa miaka mitano na Spurs Mei mwaka huu, amesisitiza anafurahia kuendelea kuwepo White Hart Lane. Meneja huyo amesema anadhani tetesi ni suala la kawaida kwasababu yeye ni kocha raia wa Argentina ambaye anafundisha moja ya klabu kubwa nchini Uingereza. Lakini pamoja na tetesi hizo, Pochettinho aliendelea kudai kuwa kwasasa anafurahia kazi yake na kwasababu hiyo hadhani kama ni wakati muafaka kuikacha Spurs.

ALLEGRI AGOMA KUZUNGUMZIA KUONDOKA KWA POGBA NA UJIO WA HIGUAIN.

MENEJA wa Juventus, Massimiliano Allegri amesema klabu inafanya vizuri na shughuli za usajili kiangazi hiki lakini amekataa kuzungumzia mustakabali wa Paul Pogba anayewindwa na Manchester United au suala la ujio wa mshambuliaji wa Napoli Gonzalo Higuain. Leo, vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti kuwa United wameongeza ofa yao ya paundi milioni 92 kwa kuongeza paundi milioni 10 ili waweze kumnasa kiungo huyo kwa usajili utakaovunja rekodi ya dunia. Hata hivyo, Allegri alikataa kutoa kauli yeyote kuhusiana na suala hilo pamoja na zile taarifa za Juventus kukaribia kukamilisha usajili wa Higuain utakaowagharimu kiasi cha euro milioni 97.4. Akizungumza na wanahabari jijini Melbourne kuelekea mchezo wao wa kirafiki wa michuano ya kimataifa dhidi ya Tottenham Hotspurs kesho, Allegri amesema hatazungumza masuala ya usajili kwani wapo hapo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Spurs.

AUBAMEYANG AIRAHISISHIA KAZI MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang amedai kuwa kuichezea Real Madrid ni moja ya malengo yake makubwa na mabingwa hao wa Ulaya ndio klabu pekee inaweza kumshawishi kuondoka Ujerumani. Mapema mwaka huu katika mahojiano nyota huyo wa kimataifa wa Gabon alidai kumuahidi babu yake kuwa siku moja atakuja kuichezea Madrid. Taarifa zimekuwa zikizagaa kuwa mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 39 akiwa na Dortmund msimu uliopita, amekuwa akiwaniwa kwa fedha nyingi na klabu za Manchester City na Atletico Madrid kiangazi hiki. Lakini mwenyewe sasa ameweka wazi kuwa ni Zinedine Zidane pekee anayeweza kumng’oa kutoka Signal Iduna Park. Akihojiwa Aubameyang amesema kwa mwaka huu uhamisho hautawezekana lakini klabu pekee anayoweza kwenda badala ya Dortmund ni Madrid na kama hawatakuja kumuwania basi hana mpango wa kwenda popote.

ALLARDYCE AKATAA KUMUHAKIKISHIA ROONEY UNAHODHA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Sam Allardyce amesema kibarua chake kipya kitakuwa na changamoto kubwa katika maisha yake ya soka. Akizungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza toka ateuliwe kushikilia wadhifa huo, Alladyce amesema hazina yake kubwa ni suala la utawala. Allardyce ambaye aliisaidia Sunderland isishuke daraja msimu uliopita, amechukua nafasi ya Roy Hodgson aliyeondoka baada ya kutofanya vyema katika michuano ya Ulaya iliyofanyika nchini Ufaransa mwaka huu. Sammy Lee aliyekuwa msaidizi wa Allardyce wakati akiinoa Bolton Wanderers, naye ataungana katika benchi ya ufundi la Uingereza. Allardyce amesema anafahamu kuwa kibarua hicho kitakuwa na changamoto kubwa katika maisha yake ya soka lakini ana matumaini atapata mafanikio kama ilivyo huko nyuma. Kocha huyo pia amesema hatafanya uamuzi wowote kuhusu unahodha wa Wayne Rooney mpaka atakapokutana na wachezaji na viongozi wengine.

HALI MBAYA YA HEWA YAPELEKEA MCHEZO WA UNITED NA CITY KUFUTWA HUKO CHINA.

MECHI ya kirafiki kati ya miamba wa Uingereza, Manchester City na Manchester United, imefutwa kutokana na hali mbaya ya hewa. Mchezo huo uliokuwa umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Bird Nest uliopo jijini Beijing, China ungekuwa wa kwanza kuzikutanisha timu hizo wakiwa na mameneja wao wapya Pep Guardiola na Jose Mourinho. Jana, Mourinho alikuwa amedokeza kwamba hali katika uwanja huo ilikuwa mbaya. Hata kabla ya mechi kuahirishwa rasmi, Guardiola alikuwa amesema matumaini yake ni kwamba wachezaji wake wasiumie. Klabu zote mbili zimeafiki kwa pamoja kuahirisha mchezo huo huku United wakitarajiwa kurejea Uingereza leo na City wao watasafiri kwenda Shenzhen kesho kwa ajili ya kwenda kucheza na Borussia Dortmund ya Ujerumani Alhamisi. Mvua kubwa ilinyesha Jumapili na watabiri wa hali ya hewa walisema mvua zaidi ingenyesha Jumatatu.

Friday, July 22, 2016

RASMI: ARSENAL YAKAMILISHA USAJILI WA BEKI WA BOLTON.

KLABU ya Arsenal imetangaza kukamilisha usajili wa beki Rob Holding kwa mkataba wa muda mrefu kutoka Bolton Wanderers inayoshiriki ligi daraja la tatu hivi sasa. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20, amecheza mechi 30 msimu uliopita wakati Bolton ikishushwa kutoka katika ligi ya ubingwa msimu uliopita. Akihojiwa na mtandao wa klabu hiyo, Holding amesema kuichezea Arsenal ni ndoto aliyokuwa nayo toka mtoto hivyo anafurahi kupata nafasi hiyo. Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Arsenal imelipa kiasi cha paundi milioni mbili kwa ajili ya kupata saini ya Holding ambaye anaweza kucheza beki wa kati au namba nne. Huo unakuwa usajili wa tatu kufanywa na meneja wa Arsenal Arsene Wenger kiangazi hiki baada ya kiungo Granit Xhaka na mshambuliaji Takuma Asano.

BAADA YA GOTZE, DORTMUND SASA YAMNASA SCHURRLE.

KLABU ya Borussia Dortmund imetangaza kumsajili rasmi Andre Schurrle kutoka Wolfsburg ya Ujerumani. Nyota huyo wa zamani wa Chelsea amesaini mkataba wa miaka mitano na Dortmund akijiunga nao siku moja baada ya kumsajili Mario Gotze. Akihojiwa na mtandao wa klabu hiyo, Schurrle amesema Dortmund ni moja kati ya klabu kubwa Ulaya huku wakiwa na kikosi imara na kinachovutia. Schurrle aliendelea kudai kuwa ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri akiwa na Dortmund na kuwaomba mashabiki wamuunge mkono ili aweze kusaidia kuleta mataji.

WAKALA WA POGBA ADAI ANAJALI ZAIDI MASLAHI YA MTEJA WAKE KULIKO REKODI.

WAKALA wa Paul Pogba, Mino Raiola amesema hajali sana kama Manchester United watatoa ada itakayovunja rekodi kwa ajili ya kumnasa mteja wake kutoka Juventus na kusisitiza anachojali yeye ni mkataba mnono atakaoupata. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliondoka Old Trafford kwenda kujiunga na Juventus akiwa mchezaji huru mwaka 2012 na toka wakati huo ameimarika na kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani akishinda mataji manne mfululizo ya Serie A. Taarifa zinadai kuwa Pogba mwenye umri wa miaka 23 anakaribia kujiunga na United kwa kitita cha euro milioni 110, wakati taarifa zingine zikidai Raiola anaweza kukunja kiasi cha euro milioni 21 katika dili yeyote itakayofanikiwa. Kama akisajili wa kiasi hicho, atakuwa ameipita rekodi ya dunia ya usajili ya euro milioni 100 ambazo Real Madrid walilipa kwa ajili ya kumsajili Gareth Bale kutoka Tottenham hotspurs. Hata hivyo, Raiola amesema ada ya uhamisho wa Pogba sio vitu vinavyomtia shaka kwasasa kwani yeye anachijali zaidi ni mteja wake kupata mkataba mnono.

DAKTARI BINGWA WA MIFUPA AMUONDOA HOFU BA.

Daktari wa upasuaji wa Demba Ba, Olivier Bringer amewasili jijini Shanghai na kubainisha kuwa ana uhakika mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea ataweza kurejea tena uwanjani na kucheza soka la ushindani. Daktari huo mtaalamu wa masuala ya mifupa kutoka Ufaransa, alitua jijini humo jana na moja kwa moja alikwenda katika hospitali ya Putuo ambako nyota huyo wa kimataifa wa Senegal amelazwa toka alipovunjika vibaya mguu wake wa kushoto wakati akiichezea timu yake ya Shenghua Jumapili iliyopita. Bringer amesema ana uhakika Ba ataweza kupona na kurejea kucheza soka tena baada ya miezi michache. Ba anatarajiwa kufanyiwa vipimo vingine kesho wakati timu ya madaktari waliokuja na Bringer itakapopewa maendeleo ya nyota huyo na madaktari wa hospitali hiyo aliyolazwa.

BARCELONA YAKUBALI KUMSAJILI GOMES.

KLABU ya Barcelona imetangaza kufikia makubaliano na Valencia ya kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ureno Andre Gomes. Gomes ameitumikia Valencia kwa misimu miwili baada ya kuhamia hapo akitokea Benfica Julai mwaka 2014. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kilichotwaa taji la michuano ya Ulaya mwaka huu. Taarifa zinadai kuwa Barcelona imelipa kiasi cha euro milioni 40 kwa ajili ya kupata saini ya Gomes ambaye amecheza mechi 30 na kufunga mabao matatu msimu uliopita. Usajili wake ukikamilika atakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Barcelona baada ya Samuel Umtiti, Lucas Digne na Denis Suarez.

LONG AJITIA KITANZI SOUTHAMPTON.

MSHAMBULIAJI wa Southampton, Shane Long amejitia kitanzi kwa kusaini mkataba mpya wa miaka minne na klabu hiyo. Long ambaye alihamia Southampton akitokea Hull City miaka miwili iliyopita, anatarajiwa kuendelea kuitumikia klabu hiyo mpaka mwaka 2020. Nyota huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Ireland, amefunga mabao 21 katika misimu miwili ambayo amecheza Southampton. Akihojiwa Long amesema kikubwa kilichomsukuma kusaini mkataba huo ni mashabiki wa klabu ambao siku zote wamemfanya ajisikie yuko nyumbani. Long anatarajiwa kufanya kazi chini ya meneja mpya wa Southampton baada ya kocha wa zamani wa Lyon na Nice Claude Puel kuchukua nafasi ya Ronaldo Koeman ambaye amekwenda kuinoa Everton.

Thursday, July 21, 2016

HISPANIA YAPATA KOCHA MPYA BAADA YA DEL BOSQUE KUONDOKA.

SHIRIKISHO la Soka la Hispania, limemteua Julian Lopetegui kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo akichukua nafasi ya Vicente del Bosque. Del Bosque alijiuzulu wadhifa wake huo kufuatia kutofanya vyema katika michuano ya Ulaya mwaka huu na sasa Lopetegui, meneja wa zamani wa FC Porto ndiye atakayeiongoza nchi hiyo kuelekea katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018. Lopetegui amewahi kuviongoza vikosi cha timu ya taifa ya Hispania kwa vijana chini ya umri wa 19, 20 na 21, huku akishinda taji la michuano ya Ulaya akiwa na vikosi vya vijana chini ya umri wa miaka 19 na 21. Kocha huyo pia amewahi kuiongoza Porto kwa misimu miwili huku akimaliza katika nafasi ya pili msimu wa 2014-2015 na tatu msimu uliofuata kabla ya kutimuliwa Januari mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na Rui Barros. Lopetegui mwenye umri wa miaka 49, ambaye aliwahi kucheza katika klabu za Real Madrid na Barcelona akiwa kipa, kibarua chake cha kwanza kitakuwa mwezi ujao wakati watakapochuana na Ubelgiji katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

RASMI: GOTZE AREJEA DORTMUND.

KLABU ya Borussia Dortmund imetangaza kumsajili tena kiungo Mario Gotze kutoka kwa mahasimu wao wa Bundesliga Bayern Munich. Katika taarifa yake waliyoitoa katika mtandao wao, Dortmund wamekubali kumsajili tena kiungo kwa mkataba utakaomalizika mwaka 2020 na anatarajiwa kukamilisha uhsmaisho huo baada ya kufaulu vipimo vya afya. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 24, ambaye mkataba wake unamalizika msimu ujao, alishindw akung’aa toka atue Allianz Arena mwaka 2013 kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Bayern nao walithibitisha suala hilo katika mtandao wao na kumshukuru Gotze kwa mchango wake katika kipindi chote cha miaka mitatu waliyokuwa naye.

ATLETICO YAGONGA UKUTA KWA HIGUAIN.

RAIS wa Napoli, Aurelio De Laurentiis amebainisha kuwa walikataa ofa ya euro milioni 60 na wachezaji wawili au watatu kutoka Atletico Madrid kwa ajili ya mshambuliaji Gonzalo Higuain. Higuain mwenye umri wa miaka 28, amekuwa akitajwa kuwindwa na klabu za Juventus na Arsenal huku akiwa amewekewa kitenzi cha euro milioni 94 katika mkataba wake. Hata hivyo, Atletico ambao wanatafuta mshambuliaji mpya kiangazi hiki ndio wamekuwa wa kwanza kutuma ofa yao kwa Napoli. De Laurentiis amesema ni Atletico pekee waliotuma ofa yao kwani rais wake alimpigia simu na kumtaarifu ofa ya euro milioni 60 na wachezaji wawili au watatu lakini alimwambia haitawezekana. Juventus pia wameripotiwa kuanza mazungumzo wiki hii lakini De Laurentiis amepuuza tetesi hizo akidai kuwa hadhani kama wanaweza kuwauzia wapinznai wao silaha.

MAN UNITED YAKUBALI KUMWAGA EURO MILIONI 110 KWA POGBA.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kukubali kuvunja rekodi ya uhamisho kwa kumsajili Paul Pogba kwa kitita cha euro milioni 110. Maofisa wa klabu hiyo ya Ligi Kuu walikutana na maofisa wa Juventus mapema jana kujadili uhamisho wa kumpeleka Pogba Old Trafford. Sasa imefahamika kuwa United wamekubali kutoa kitita cha euro milioni 110 kwa Pogba ambacho kitapita kile kiwango kilichovunja rekodi wakati Real Madrid walipolipa euro milioni 100 kwa ajili ya gareth Bale mwaka 2013. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano Old Trafford. Kiungo anadaiwa kuwa tayari kukubali mshahara wa euro milioni 13 kwa mwaka akiwa Old Trafford, kiwango ambacho kitakuwa ni karibu mara tatu ya mshahara anaochukua hivi sasa Juventus.

BIG SAM KUKABIDHIWA MIKOBA YA HODGSON.

MENEJA wa klabu ya Sunderland, Sam Allardyce anatarajiwa kuteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza huku uthibitisho wake ukitegemewa kutolewa wakati wowote leo. Meneja huyo anatarajiwa kuondoka Sunderland baada ya miezi tisa ya kuinoa klabu hiyo ya Ligi Kuu. Allardyce atachukua nafasi ya Roy Hodgson ambaye alijiuzulu Juni mwaka huu baada ya Uingereza kutandikwa na vibonde Iceland katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Ulaya iliyofanyika mwaka huu. Meneja huyo mwenye umri wa miaka 61, ambaye amewahi kuzinoa timu za West Ham United, Newcastle United, Bolton Wanderers na Nottingham Forest, alizungumza na Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA wiki iliyopita na sasa amechaguliwa badala ya meneja wa Hull City Steve Bruce. Kitu pekee kilichobakia hivi sasa ni mazungumzo ya kuilipa fidia Sunderland kwani Allardyce alikuwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja katika klabu hiyo.

Wednesday, July 20, 2016

SHERIA KALI MPYA ZAWEKWA KUDHIBITI TABIA MBAYA KATIKA LIGI KUU.

MPANGO wa kupunguza tabia zisizovumilika kwa wachezaji na mameneja katika soka la Uingereza umetangwazwa rasmi leo. Katika taarifa iliyotolewa na Ligi Kuu, Ligi ya Soka ya Uingereza na Chama cha Soka cha nchi hiyo imedai kuwa maadili mabovu yamefikia hatua ya kutokubalika. Kuanzia msimu huu mpya wa ligi, kadi nyekundu zitaonyeshwa kw mchezaji atakayemfuata mwamuzi wa mchezo na kutumia lugha isiyokuwa sahihi au kumuonyesha ishara yeyote mbaya. Tabia katika maeneo ya benchi la ufundi pia nazo zitachukuliwa hatua kali. Mwenyekiti wa Ligi Kuu, Richard Scudamore amesema kumekuwa na wasiwasi kwa kipindi kirefu kuwa wachezaji wamekuwa wakivuka mipaka kwa tabia zao wanazoonyesha.

Makosa ambayo mchezaji anaweza kupewa kadi ya njano.
*Kuonyesha wazi kutomuheshimu mwamuzi wa mchezo,
*Kuonyesha shari kwa maamuzi yaliyotolewa
*Kumvaa mwamuzi uso kwa uso
*Kumkimbilia mwamuzi ili kupinga uamuzi uliotolewa
*Shambulizi, lugha ya matusi au ya kunyapaa na ishara ishara yeyote kumuelekea mwamuzi
*Kugusana na mwamuzi yeyote katika tukio ambalo sio la kumfanyia fujo
*kadi ya njano walau kwa mchezaji mmoja wakati wachezaji wawili au wa zaidi wa timu watakwenda kumzonga mwamuzi.

Makosa mapya ambayo mchezaji anaweza kupata kadi nyekundu ni*Kama mchezaji atamvamia mwamuzi na kumshambulia, kutumia lugha ya matusi au kunyapaa au kumnyooshea ishara ishara kwenda kwake
*Kugusana na mwamuzi wa mchezo kwa nia ya kumfanyia fujo au kupingana na uamuzi wake

ARSENAL YAMGEUKIA KOULIBALY.

BEKI wa Napoli, Kalidou Koulibaly anadaiwa kutolewa ofa na klabu kadhaa kubwa za Ulaya ikiwemo Arsenal. Nyota huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 25, ambaye anawindwa pia na klabu za Ligi Kuu za Chelsea na Everton anadaiwa kuthaminishwa kwa kitita cha euro milioni 45 ambacho hakuna yeyote aliyefikia. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger yuko sokoni kiangazi hiki akitafuta beki wa kiwango cha juu na wakati Koulibaly akibakia kwenye orodha ya wachezaji wanaowahitaji hakuna ofa yeyote iliyotolewa mpaka sasa. Wenger anakaribia kukamilisha usajili wake wa tatu kiangazi hiki kufuatia Rob Holding kufaulu vipimo vya afya huku mambo binafsi yakitarajiwa kujadiliwa katika siku chahe hizi.

LEICESTER CITY YAMTIA KITANZI NAHODHA WAKE.

NAHODHA wa Leicester City Wes Morgan amesaini mkataba mpya ambao utamuweka katika klabu hiyo mpaka Juni mwaka 2019. Beki huyo mwenye umri wa miaka 32 amecheza kila dakika katika mechi za ligi msimu uliopita wakati Leicester ilipokwenda kutwaa taji la Ligi Kuu. Morgan alijiunga na Leicester akitokea Nottingham Forest Januari mwaka 2012 na mpaka ameishaichezea klabu hiyo mechi 182 za ligi. Akihojiwa na mtandao wa klabu hiyo, Morgan amesema amefurahishwa sana na hatua hiyo kwani kila mtu anafahamu jinsi anavyoipenda klabu hiyo.

URENO YAMUONGEZA KOCHA WAKE MKATABA.

CHAMA cha Soka cha Ureno-FPF kimetangaza kumuongeza mkataba kocha Fernando Santos mpaka 2020 baada ya kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kutwaa taji la michuano ya Ulaya mwaka huu. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 61, ambaye amekuwa akikinoa kikosi hicho toka Septemba mwaka 2014, aliiongoza Ureno kutwaa taji lake la kwanza kubwa la kimataifa pamoja na kucheza bila nyota wake Cristiano Ronaldo katika fainali dhidi ya wenyeji Ufaransa mapema mwezi huu. Mkataba wake mpya alioongezwa utamfanya kukiongoza kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na ile ya ijayo ya Ulaya. Santos amewahi kufundisha klabu kubwa nchini Ureno zikiwemo Benfica, Sporting Lisbon na Porto huku pia akiwahi kuinoa timu ya taifa ya Ugiriki.

POGBA ADAIWA KUOMBA KUONDOKA KWENDA UNITED.

VYOMBO vya habari nchini Italia vimeripoti kuwa Paul Pogba ameihabalisha Juventus kuwa anataka kuondoka katika klabu hiyo na kwenda kujiunga na Manchester United. Tetesi hizo zimekuja kufuatia madai kuwa makamu mwenyekiti wa United Ed Woodward ameikosa safari ya ziara ya China kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo ya kumnasa kiungo huyo. Magazeti mbalimbali ya nchini Italia yamepamba kurasa zao na taarifa mbalimbali za kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa huku mengine yakienda na mbali na kudai kuwa tayari wameshaafikiana makubaliano na United. Gazeti lingine lilidai kuwa Pogba anatarajiwa kusaini mkataba mnono wa miaka mitano ambao utamfanya kupata mara mbili ya mshahara anaopata hivi sasa.

CONTE AMKOMALIA COSTA.

MENEJA mpya wa Chelsea, Antonio Conte amesema mshambuliaji wake Diego Costa ataendelea kubaki katika klabu hiyo msimu ujao na ni mchezaji muhimu katika mipango yake. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania, amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea katika klabu yake ya zamani ya Atletico Madrid. Costa mwenye umri wa miaka 27 amefunga mabao 36 katika mechi 77 alizocheza toka amejiunga na Chelsea mwaka 2014. Akihojiwa kuhusiana na suala hilo, Conte amesema Costa atabakia nao kwani amekuwa akijituma na anafurahia kufanya kazi na wachezaji wenzake pamoja naye.

BA KUENDELEA KUCHEZA SOKA AKIPONA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Shanghai Shenghua Demba Ba amesisitiza hatastaafu soka pamoja na kupata majeruhi mabaya ya kuvunjika mguu katika mchezo wa Ligi Kuu ya China. Katika tukio hilo la kutisha lililotokea Jumapili iliyopita wakati wa mchezo wa derby ya Shanghai, Ba alipinga mguu vibaya mguu wake wa kushoto baada ya kukwatuliwa na beki w SIPG Sun Xiang wakati akijaribu kuwania mpira. Mara baada ya kuvunjika hofu ilizuka kuwa soka la Ba mwenye umri wa miaka 31 linaweza kukomea hapo, lakini mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea, West ham United na Newcastle United amesema hana mpango wowote wa kutundika daruga zake. Akihojiwa Ba amesema anafahamu kuwa hayo ni majeruhi mabaya lakini anafahamu anaweza kuvuka mtihani huo hivyo hawezi kukata tamaa. Ba amesema msimu wa ligi ya huko unamalizika Novemba na mpya unaanza Machi hivyo atajitahidi kufanya kila awezalo ili aweze kupona kwa wakati tayari kwa msimu ujao.

Tuesday, July 19, 2016

MAN UNITED SASA WATENGA OFA YA KUFURU KWA POGBA.

KLABU ya Manchester United inadaiwa kutuma ofa ya mwisho ya euro milioni 125 kwa ajili ya kiungo wa kimataifa wa Ufaransa Paul Pogba. United chini ya meneja wake mpya Jose Mourinho wamekuwa wakihaha kumuwania nyota huyo na wako tayari kuvunja rekodi ya dunia ya usajili kwa ajili ya kiungo huyo wa Juventus. Dili la jumla linadaiwa kuwa litawagharimu United kiasi cha euro milioni 185, huku klabu hiyo ikiwa tayari kumpa ofa ya mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya euro milioni 12 kwa kila msimu. Taarifa zinadai pia kuwa Pogba anatarajia kukunja asilimia 20 ya ada hiyo ya mauzo yake ambayo itakuwa kiasi cha euro milioni 25.

MADRID YAKARIBIA KUMNASA GOMES.

KLABU ya Real Madrid inadaiwa kukaribia kumsajili kiungo wa Valencia Andre Gomes kwa kitita cha euro milioni 50. Valencia wanadaiwa kutaka kwanza euro milioni 65 kwa ajili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 lakini Madrid wao wanataka kulipa euro milioni 50 na zingine waje kumalizika baadae. Taarifa zinadai kuwa Zinedine Zidane anamuona nyota huyo wa kimataifa Ureno kama chaguo sahihi atakaeweza kubadilishana na Luka Modric. Manchester United, Chelsea na Barcelona nazo pia zinamuwania mchezaji huyo.

ARSENAL YANYATIA BEKI LA BOLTON.

KLABU ya Arsenal, inadaiwa kutenga ofa ya paundi milioni mbili kwa ajili ya beki wa Bolton Wanderers Rob Holding. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 ni zao kutoka katika shule ya soka ya Bolton na alikuwepo katika kikosi cha Uingereza cha vijana chini ya umri wa miaka 21 ambacho kilishinda taji la Toulon kiangazi hiki. Holding alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Bolton msimu uliopita baada ya kuibuka katika kikosi cha timu hiyo mwanzoni mwa msimu. Kwa upande mwungine, Wanderers wanafikiria kutoa ofa kwa beki wa zamani w Brighton Gordon Greer.


MARIO GOTZE ANUKIA DORTMUND.

OFISA mkuu wa Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amesema angefurahi kuona Mario Gotze akiichezea tena timu hiyo lakini amesisitiza hakuna dili lolote lililofanyika mpaka sasa na Bayern Munich. Mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge alibainisha mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa klabu hizo mbili zipo katika mzungumzo ya kujadili uhamisho wa Gotze. Gotze mwenye umri wa miaka 24, alisababisha mtikisiko wakati alipoondoka Dortmund kwenda kujiunga na mahasimu woa wa Bundesliga Bayern mwaka 2013, lakini toka wakati huo ameshindwa kung’aa akiwa na mabingwa hao wa Ujerumani. Lakini pamoja na mazungumzo kuwa bado yanaendelea, Watzke amesisitiza kuwa bado safari ni ndefu kwa pande hizo mbili kufikia makubaliano. Watzke amesema pamoja na kuwa anatamani Gotze arejee tena Dortmund lakini mazungumzo bado yanaendelea na hakuna uamuzi wowote ulioafikiwa.

NITARUDI NIKIWA IMARA ZAIDI - RONALDO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameapa kurejea tena akiwa imara zaidi tayari kwa ajili ya msimu wa 2016-2017 baada ya kupata majeruhi ya goti katika michuano ya Ulaya mapema mwezi huu. Ronaldo huku akibubujikwa na machozi alitolewa nje kwa machela baada ya kupata majeruhi ya goti katika mchezo wa fainali ya michuano ya Ulaya ambao Ureno walishinda dhidi ya wenyeji Ufaransa jijini Paris. Nyota huyo aliumia katika kipindi cha kwanza kufuatia kukwatuliwa na kiungo wa Ufaransa Dimitri Payet huku taarifa zikidai kuwa anaweza kukosa mwanzo wa msimu wa La Liga na Madrid. Hata hivyo, Ronaldo alituma picha za video katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram akiwaondoa hofu mashabiki wake na kudai kuwa atarejea akiwa imara zaidi.

NEYMAR NJE TUZO ZA MCHEZAJI BORA WA ULAYA.

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya-UEFA limetangaza majina ya wachezaji 10 watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya kwa msimu wa 2015-2016. Nafasi kubwa miongoni mwa majina hayo yaliyoteuliwa anapewa nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu Real Madrid Cristiano Ronaldo ambaye mbali na kutwaa mataji mawili makubwa ya Ulaya kwa klabu na nchi yake lakini pia ndiye mfungaji bora wa bara hil msimu uliopita. Majina 10 yaliyoteuliwa yametolewa katika orodha ya wachezaji 37 walioteuliwa awali na shirikisho hilo kabla ya kupigiwa kura ya mchujo. Mbali na Ronaldo katika orodha hiyo lakini pia wapo Lionel Messi na Luis Suarez kutoka Barcelona, Gareth Bale, Toni Kroos na Pepe wote kutoka Madrid, Thomas Muller na Manuel Neuer kutoka Bayern Munich, Antonio Griezmann kutoka Atletico Madrid na Gianluigi Buffon kutoka Juventus.

Friday, July 15, 2016

EL CLASICO DESEMBA.

KLABU za Barcelona na Real Madrid zinatarajiwa kukutana Desemba katika ratiba mpya ya msimu wa 2016-2017 wa La Liga iliyotolewa leo. Madrid waliomaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga nyuma ya Barcelona msimu uliopita, watasafiri kwenda Camp Nou katika wikiendi ya Desemba 3 au 4 ukiwa ni mchezo wao wa mwisho kwa la Liga kabla ya kusafiri kwenda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia nchini Japan wakiwa kama mabingwa wa Ulaya. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 8 na kumalizika Desemba 18 mwaka huu. Mechi ya marudiano kati ya mahasimu hao wa La Liga inatarajiwa kufanyika Santiago Berbabeu kati ya Aprili 22 au 23 mwakani.

RONALDO AMEUNGA MKONO UJIO WANGU LA LIGA - NANI.

WINGA mpya wa Valencia, Nani amesema mchezaji mwenzake wa Ureno Cristiano Ronaldo ameunga mkono hatua yake hiyo ya kwenda La Liga kufuatia mafanikio waliyopata katika michuano ya Ulaya. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, amesaini mkataba wa miaka mitatu na Valencia akitokea Fenerbahce ya Uturuki kwa kitita cha euro milioni 8.5 ambapo alidumu kwa msimu mmoja baada ya kuondoka Manchester United. Nani alianza katika mechi zote saba na kufunga mabao matatu wakati Ureno ilipotwaa taji la Ulaya, huku rafiki yake na mchezaji mwenzake Ronaldo akimuunga mkono kupata mafanikio wakati atakapocheza soka kwa mara ya kwanza nchini Hispania. Winga huyo alitambulishwa mbele ya mashabiki 12,000 wa Valencia waliojitokeza Mestalla jana na anatarajiwa kushindana na Ronaldo pindi msimu wa la Liga utakapoanza. Akihojiwa Nani amesema Ronaldo alimpongeza na kumwambia kuwa Valencia ni klabu kubwa nchini humo na ataweza kuzoea haraka mazingira ya La Liga.

ROMA YAMTENGEA NACHO EURO MILIONI 15.

KLABU ya AS Roma inadaiwa kufikiria kutuma ofa ya euro milioni 15 kwa ajili ya kumuwania beki wa Real Madrid, Nacho. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, amecheza mechi 22 msimu uliopita na kwasasa amekuwa chaguo la nne kwa Zinedine Zidane baada ya Sergio Ramos, Pepe na Raphael Varane. Kabla ya kurejea kwa maandalizi ya msimu mpya, Nacho alielezwa na Madrid kuwa bado wanamuhitaji, wakati mchezaji mwenyewe naye akipania kupigania nafasi yake. Lakini Zidane sasa anatarajiwa kukutana na beki huyo kuzungumzia mustakabali wake na uhamisho wake kwenda Roma utategemea na matokeo ya kikao hicho.