MATAJIRI wa Ufaransa klabu ya Paris Saint-Germain wako tayari kuwarudishia Manchester United fedha yao kwa ajili ya kumsajili Angel Di Maria. Di Maria mwenye umri wa miaka 27 amekuwa chini ya kiwango toka asajiliwe kwa kitita kilichovunja rekodi cha paundi milioni 59.7 kutoka Real Madrid kiangazi mwaka jana. PSG ambao pia walikuwa wakimtaka mwaka jana, wako tayari tena kutoa kitita kikubwa kwa ajili ya kumng’oa nyota huyo Old Trafford. Kitu kikubwa kinachowapa nafasi PSG kumchukua nyota huyo kiangazi ni uhakika wa ushiriki wao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ukilinganisha na United ambao bado wanapigana kupata nafasi hiyo. Tayari meneja wa United Louis van Gaal ameshamfungulia milango Di Maria kwa kukiri kuwa hatakuwa na mpango wa kumzuia kama akiamua kuondoka.
Tuesday, March 31, 2015
XAVI AKANUSHA KUSAINI MKATABA AL SADD.
KIUNGO wa Barcelona Xavi Hermandez amekanusha taarifa kuwa anajipanga kusaini mkataba na klabu ya Al Sadd inayoshiriki Ligi Kuu nchini Qatar. Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alitumia siku nne za mapumziko kupisha michezo ya kimataifa nchini Qatar huku rais wa Al Sadd Mohammad Al Ali akidai kuwa na uhakika wa kumsajili mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 35. Hata hivyo, baada ya kurejea Hispania, Xavi amesisitiza kuwa alienda Qatar kwa ajili ya mapumziko na familia yake na sio vinginevyo. Xavi anategemewa kwa kiasi kikubwa kuondoka Barcelona mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia kwa miaka 24 toka alipoibuka kutoka katika academy maarufu ya timu hiyo ya La Masia. Mbali na Al Sadd, Xavi pia amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda katika timu ya New York City FC ya Marekani ambako ataweza kukutana na mchezaji mwenzake wa zamani David Villa.
UEFA YAZISHITAKI MONTENEGRO NA URUSI.
SHIRIKISHO la Soka Ulaya-UEFA limevishitaki vyama vya soka vya Montenegro na Urusi kufuatia mchezo baina ya timu zao za taifa wa kufuzu michuano ya Ulaya mwakani kushindwa kufanyika huko Podgorica. Mchezo huo ulisitishwa katika kipindi cha pili baada ya vurugu zilizowahusisha wachezaji na viongozi huku golikipa wa Urusi Igor Akinfeev akitolewa mapema kwa kupigwa fataki kutokea jukwaani. Montenegro wao wanashitakiwa kwa kuandaa mchezo ambao haukuchezwa ukamalizika wakati nchi zote mbili zikishitakiwa kwa mashabiki wake kurusha mafataki na vitu vingine uwanjani. Urusi wao wametuma malalamiko yao rasmi UEFA wakitaka kupewa ushindi wa mchezo huo ambao mpaka unasimamishwa na mwamuzi Diniz Aytekin hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
QATAR SASA MWENDO MDUNDO.
OFISA wa kamati ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar amesema hadhani kama kutahitajika vipoza hewa katika viwanja kama ilivyoahidiwa wakati wakitafuta nafasi hiyo. Mapema mwezi huu Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilitegua kitendawili cha muda mrefu wa muda gani haswa michuano hiyo itachezwa na kuamua kuwa ichezwe wakati wa majira ya baridi ya Novemba na Desemba mwaa huo. Changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili katika kuandaa michuano hiyo wakati wa kiangazi ilikuwa ni jinsi na kutengeneza vipoza hewa kwa ajili ya joto kali linafikia nyuzi joto 40 wakati huo. Hata hivyo sasa ofisa huyo Dario Cadavid amesema kuwatakuwa hakuna umuhimu tena wa kutumia vipoza hewa kwasababu michuano hiyo itafanyika wakati wa majira ya baridi kama ilivyoamuliwa. Pamoja na hayo Cadavid aliendelea kudai kuwa bado wataufanyia kazi mfumo huo wa vipoza hewa kwa ajili ya mechi zao chache za ligi ambazo huchezwa wakati wa joto kali.
FALCAO AFIKIA REKODI YA MABAO COLOMBIA.
MSHAMBULIAJI nyota anayekipiga kwa mkopo Manchester United, Radamel Falcao amefanikiwa kufikia rekodi ya mabao katika timu yake ya taifa ya Colombia baada ya kufikisha mabao 24 jana. Falcao alichukuliwa kwa mkopo kutokea AS Monaco, amefikia rekodi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Arnoldo Iguaran baada ya kufunga bao kwa njia ya penati wakati Colombia ikiigaragaza Kuwait kwa mabao 3-1. Hilo linakuwa bado la tatu kufungwa na Falcao katika michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa aliyoichezea Colombia baada ya kufunga mengine mawili wakati waliposhinda mabao 6-0 dhidi ya Bahrain. Falcao mwenye umri wa miaka 29 amekuwa na msimu mbaya toka atue United kwani amefanikiwa kufunga mabao manne pekee katika michezo 22 aliyocheza msimu huu.
Monday, March 30, 2015
TENGA AISHUKURU TFF KWA KUMUUNGA MKONO.
MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati-CECAFA, Leodegar Chilla Tenga amelishukuru Shirikisho la Soka Tanzania-TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika-CAF katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 7, mwaka huu mjini Cairo, Misri. Tenga amesema hayo katika mkutano wa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuzungumzia uchaguzi wa CAF na FIFA. Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Wakati huohuo Tenga amezungumzia pia msimamo wa bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA anayetetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Uswisi. Vilevile Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Joseph Sepp Blatter katika uchaguzi wa FIFA. Katika mkutano huo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa tamko rasmi kuwa kwa niaba ya TFF atampigia kura Joseph Sepp Blatter.
BAYERN YATAMBA KUONYESHA JEURI YA FEDHA USAJILI WA KIANGAZI.
AL SADD WAZIDI KUMKOMALIA XAVI.
YAYA TOURE KUAMUA HATMA YAKE IVORY COAST WIKI HII.
KIUNGO mahiri wa klabu ya Manchester City, Yaya Toure amesema anatarajia kuamua kuhusu mustakabali wake wa kuitumikia timu yake ya taifa ya Ivory Coast wiki hii. Akiwa nahodha Toure ameiongoza Ivory Coast kunyakuwa taji lao la kwanza la michuano ya Mataifa ya Afrika nchini Guinea Ikweta mapema mwaka huu toka wafanye hivyo tena mwaka 1992. Toure mwenye umri wa miaka 31 amesema anafikiria kufuata nyayo za kaka yake Kolo ambaye tayari amestaafu soka la kimataifa baada ya michuano hiyo. Akihojiwa Toure amesema anadhani malengo yake yametimia hivyo anataka kusubiri kwa siku chache kabla ya kuamua mustakabali wake. Nyota huyo anadhani wakati wake wa kuachia vijana chipukizi ili aweze kutilia mkazo klabu yake umefika.
NEWCASTLE YATANGAZA KUINGIZA FAIDA.
KLABU ya Newcastle United imetangaza kuweka rekodi kwa mapato ya mwaka baada ya kuingiza kiasi cha paundi milioni 18.7, ukiwa ni mwaka wan ne mfululizo kutengeneza faida. Hata hivyo deni la klabu hiyo limeendelea kubakia vilevile paundi milioni 129, ukiwa ni mkopo kutoka kwa mmiliki wake Mike Ashley. Mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo Lee Charnley amesema faida inayopata klabu hiyo inatokana na kuungwa mkono na Ashley kwani kunawapa uimara ambao unawasaidia kukua ndani na nje ya uwanja. Charnley amesema matokeo hayo yanamaanisha kuwa wanasonga mbele kwani wana uwezo wa kutumia kiasi kwa ajili ya kuimarisha kikosi na kiasi kingine kwenda katika maeneo mengine ya biashara.
WENGER AMVALIA MABOMU RAHEEM STERLING.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anajipanga kuingia katika kinyang’anyiro cha kutaka kumsajili winga wa Liverpool Raheem Sterling katika majira ya kiangazi. Wenger amekuwa akimhusudu sana nyota huyo na yuko tayari kujaribu bahati yake kutokana na sakata juu ya mkataba linaloendelea katika klabu yake. Sterling mwenye umri wa miaka 20 amesimamisha mazungumzo kuhusu mustakabali wake mpaka majira ya kiangazi ili kuhamishia nguvu zake katika soka lakini Liverpool wanahofu kuwa hatasaini mkataba mpya. Kuchelewa huko kumezigutusha klabu kubwa ambazo pia zinamtamani wakiwemo Real Madrid, Bayern Munich na Manchester City. Arsenal nao wanajipanga kuingia katika kinyang’anyiro hicho kujaribu tena kumsajili baada ya kushindwa kumsajili wakati akiwa na miaka 10 mwaka 2010.
CHELSEA WAMTENGEA BALE KITITA CHA PAUNDI MILIONI 75.
KLABU ya Chelsea inaripotiwa kuwa inajipanga kutenga kitita cha paundi milioni 75 kwa ajili ya kumng’oa winga wa Real Madrid Gareth Bale katika majira ya kiangazi. Chelsea wamekuwa wakihusishwa na taarifa za kumtaka Bale katika wiki chache zilizopita kufuatia tetesi kuwa nyota huyo anataka kuondoka Madrid. Na sasa taarifa zinadai kuwa Chelsea wako tayari kutoa kitita cha paundi milioni 75 kwa ajili ya kupata saini ya winga huyo wa kimataifa wa Wales. Bale bado anadai anafurahia kuendelea kuwepo Madrid lakini Chelsea wanajipanga kumpa ofa ya mshahara wa paundi 300,000 kwa wiki ili kukamilisha usajili wake. Kama akiamua kuondoka Madrid Bale ndio atakuwa mchezaji anayelipwa zaidi Chelsea.
SCHALKE WADAI KUMKOMALIA KHEDIRA HATA WASIPOFUZU LIGI YA MABINGWA.
MKURUGENZI wa michezo wa klabu ya Schalke, Horst Heldt amesisitiza kuwa kushindwa kwao kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuwezi kuathiri dhamira yao ya kutaka kumsajili kiungo wa Real Madrid Sami Khedira. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani alithibitisha mapema mwezi huu kuwa anatarajia kuondoka Santiago Bernabeu wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huku Schalke ikiwa ni mojawapo ya vilabu vinavyowania kumsajili. Ingawa Schalke wapo katika hatari ya kuikosa michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao kutokana na kuwa nafasi ya tano katika msimamo wa Bundesliga hivi sasa, bado wana uhakika jambo hilo haliwezi kupoteza nafasi yao ya kumrejesha Khedira Ujerumani. Heldt amesema uamuzi wa mchezaji mwenyewe mara nyingi huwa hautegemei kama watafuzu michuano hiyo au la. Kiongozi huyo aliendelea kudai kuwa pamoja na kwamba wanajua hawako peke yao katika kinyang’anyiro hicho lakini ana uhakika bado wanaweza kupata saini yake mwishoni mwa msimu.
MICHUANO YA KUFUZU ULAYA YAZIDI KUNOGA.
HEKAHEKA ya kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ya Ulaya inayotarajiwa kufanyika mwakani iliendelea tena jana kwa michezo kadhaa kupigwa katika viwnaja tofauti. Katika mchezo hiyo Ureno waliokuwa wenyeji walifanikiwa kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuichapa Serbia kwa mabao 2-1. Kwa upande mwingine Hungary wao walishindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Ugiriki katika mchezo wa kundi F huku Ireland ya Kaskazini ikiichapa Finland kwa mabao 2-1 katika mchezo mwingine wa kundi hilo. Kwa upande wa kundi D mabingwa wa dunia Ujerumani waliionyesha kazi Georgia kwa kuichapa mabao 2-0, Jamhuri ya Ireland ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Poland huku Scotland wakiwafundisha soka Gibraltar kwa kuwachapa mabao 6-1.
Saturday, March 28, 2015
WELBECK AACHWA UINGEREZA KUTOKANA NA MAJERUHI.
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Arsenal, Danny Welbeck ameondolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza baada ya kupata majeruhi ya goti katika mchezo dhidi wa kufuzu michuano ya Ulaya dhidi ya Lithuania jana ambapo walishinda kwa mabao 4-0. Majeruhi hayo ya Welbeck yalikuja kipindi cha pili cha mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Wembley na kupelekea kutolewa nje katika dakika ya 77. Chama cha Soka cha Uingereza kilithibitisha majeruhi ya mchezaji na kudai kuwa tayri wameshamrudisha katika klabu yake kwa ajili ya vipimo zaidi. Welbeck sasa atakosa mchezo wa kirafiki wa kimataifa Jumanne ijayo dhidi ya Italia utakaochezwa jijini Turin.
KOCHA WA UJERUMANI ADAI USHINDI KWAKE NI MUHIMU KULIKO MABAO.
KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew amesema hatajali idadi ya mabao katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Georgia kwani jambo muhimu analotaka yeye na kushinda. Mabingwa hao wa dunia wamekuwa akisuasua toka washinde taji la Kombe la Dunia nchini Brazil baada ya kupoteza mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwakani dhidi ya Poland, sare ya nyumbani dhidi ya Ireland huku akiifunga Scotland kwa tabu. Jumatano iliyopita Ujerumani ilipata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Australia na sasa wanakabiliwa na kibarua kingine huko Tbilisi wakati Loew atakapokuwa akijaribu kusahau matokeo mabaya na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi dhidi ya Georgia. Ili kujiimarisha katika kundi lao la D. Loew amesema kwao hivi ushindi ndio jambo la muhimu na sio idadi mabao watakayofunga kwani wanahitaji alama tatu muhimu ili kujiimarisha katika kundi lao baada ya matokeo yasiyoridhisha katika michezo yao iliyopita.
VAN DER VAART KUIKACHA HAMBURG KIANGAZI.
OFISA mkuu wa klabu ya Hamburg ya Ujerumani, Dietmar Beiersdorfer amebainisha kuwa nahodha wa timu hiyo Rafael van der Vaart anatarajiwa kuondoka pindi mkataba wake wa sasa utakapomalizika Juni mwaka huu. Kiungo huyo ambaye amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia katika Ligi Kuu nchini Marekani ataondoka kama mchezaji huru Juni na Beiersdorfer amethibitisha kuwa Van der Vaart hana mpango wa kuongeza mkataba mwingine. Beiersdorfer amesema mbali na Van der Vaart lakini pia tayari wameshazungumza na Marcell jansen, Heiko Westermann na Slobodan Rajkovic kuhusu mipango yao na wanasubiri uamuzi wao wa aidha kubakia au kuondoka. Mapema mwezi huu klabu ya Sporting Kansas City ya Marekani ilithibitisha kuwa na nia ya kumsajili Van der Vaart wakati pia akihusishwa na tetesi za kurejea katika klabu yake ya utotoni ya Ajax Amsterdam.
ZAMBIA YAKWEPA ADHABU KIJANJA.
SERIKALI ya Zambia imemlipa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Dario Bonetti ili kuepusha adhabu ya kufungiwa na Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA. Bonetti raia wa Ufaransa ambaye amewahi kuinoa Chipolopolo kuanzia Julai mwaka 2010 hado Octoba mwaka 2011 amekuwa akiidai nchi hiyo kiasi ha dola 432,000. Kocha huyo alitimuliwa huku kukiwa kumebaki miezi tisa katika mkataba wake na pamoja na kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2012. Bonetti alipelekea malalamiko yake FIFA kulishitaki Shirikisho la Soka la Zambia na kesi ilikuwa ikitarajiwa kutolewa maamuzi Agosti mwaka huu. Hata hivyo kufuatia Zimbabwe kuenguliwa katika michezo ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 kwa kushindwa kumlipa kocha wao wa zamani Jose Claudinei Georgini kulikwua na hofu kuwa Zambia wangeweza kupata adhabu kama hiyo hivyo kuamua kumlipa kabla.
URUSI KUISHITAKI MONTENEGRO BAADA YA VURUGU.
SHIRIKISHO la Soka la Urusi-RFU linakusudia kuwasilisha malalamiko yao rasmi Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA baada ya mchezo wao wa kufuzu michuano ya Ulaya mwakani dhidi ya Mintenegro kusitishwa. Mchezo uliochezwa jana huko Podgorica ulianza kwa utata wakati golikipa wa Urusi Igor Akinfeev kupigwa na kitu mfano wa fataki kutokea jukwaani baada ya mchezo kuanza hatua ilipelekea mchezo huo kusimamishwa kwa muda. Mchezo huo uliendelea tena baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya nusu saa huku Akinfeev akikimbizwa hospitalia kutokana na tukio hilo. Baada ya Roman Shirokov kuokoa penati kwa Urusi katika dakika ya 66, mchezaji Dmitri Kombarov alionekana kupigwa na kitu kingine kama hicho kutokea jukwaani hatua ambao ilizusha vurugu kali ndani na nje ya uwanja na kupelekea mchezo kusitishwa kabisa. Rais wa RFU Nikolai Tolstoy amekaririwa akidai kuwa hawezi kuwalaumu mashabiki kwa tabia walioonyesha kwani tayari walikuwa wamewaonya maofisa wa UEFA wakati wa tukio la kwanza lakini waliamua mchezo uendelee. Tolstoy amesema kwa maono yake mchezo huo ulitakiwa kusitishwa toka mara ya kwanza na Montenegro kunyang’anywa alama.
WENGER APISHANA NA WALCOTT.
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesisitiza kuwa majadiliano ya mkataba na Theo Walcott yameanza pamoja na mshambuliaji huyo kudai kuwa bado. Walcott aliandika katika ukurasa wake wa twitter jana kuwa mazungumzo kuhusu mkataba mpya na Arsenal yalikuwa bado kufanyika jambo ambalo linaonekana kuwa na mkanganyiko baada ya Wenger kudai kuwa tayari wameshaanza kuzungumza naye. Akihojiwa Wenger amesema tayari wameshaanza kuzungumza na Walcott kuhusu uwezekano wa kuongeza mkataba mpya nay eye binafsi anataka nyota huyo aendelee kuitumikia timu hiyo. Walcott amekuwa akipambana kurejea katika kikosi cha kwanza cha Gunners toka atoke katika majeruhi yaliyomchukua karibu mwaka mzima kupona.
JORDI ALBA KUIKOSA UHOLANZI.
KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque amethibitisha kuwa Jordi Alba amerejeshwa Barcelona baada ya kupata majeruhi ya msuli wa paja katika mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya dhidi ya Ukraine jana. Nyota huyo wa zamani wa Valencia alitolewa nje zikiwa zimebaki dakika 11 mchezo huo walioshinda bao 1-0 na nafasi yake kuchukuliwa na Juan Bernat wa Sevilla. Del Bosque tayari amethibtisha kuwa atakosa huduma ya mchezaji huyo katika mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uholanzi Jumanne ijayo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa tayari madaktari wa Hispania wameshairifu timu yake na wanatarajia kumruhusu kwa ajili ya kwenda kufanyiwa vipimo zaidi.
HARRY KANE AFURAHIA KUFUNGA BAO KATIKA MCHEZO WAKE WA KWANZA KUICHEZEA UINGEREZA.
MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uingereza, Harry Kane amebainisha kuwa na wakati mzuri baada ya kufanikiwa kufunga bao katika sekunde 80 toka aanze kuitumikia timu yake ya taifa kwa mara ya kwanza wakati walipopata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Lithuania jana. Akiwa ameshaifungia klabu yake ya Tottenham Hotspurs mabao 29, Kane alianzia benchi katika mchezo huo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwakani lakini aliingia katika dakika ya 71 akichukua nafasi ya Raheem Sterling na kufunga bao ndani ya dakika mbili. Akihojiwa Kane mwenye umri wa miaka 21 amesema sio mbaya kwa kuanzia kwani amekuwa akiiota siku hiyo kwa kipindi kirefu na anashukuru amefanikiwa kutimiza nia yake hiyo. Kane aliendelea kudai kuwa kuiwakilisha timu yake kimataifa na kuisaidia kushinda ni jambo linalomfanya kuwa na fahari kubwa.
Thursday, March 26, 2015
DUDEK AMSHAURI SZCZESNY KUONDOKA ARSENAL.
GOLIKIPA wa zamani wa Liverpool, Jerzy Dudek amemtaka Wojciech Szczesny kuondoka Arsenal baada ya kupoteza nafasi yake kama golikipa namba moja kwa David Ospina. Golikipa huyo alipoteza nafasi hiyo Januari mwaka huu baada ya kukutwa akivuta sigara bafuni baada ya klabu hiyo kufungwa na Southampton katika Uwanja wa St Mary. Toka wakati huo Ospina amekuwa akipata nafasi ya kuanza katika kikosi cha Arsenal na Dudek anadhani wakati umefika kwa Szczesny kuondoka Emirates na kwenda kutafuta timu anayoweza kupata nafasi ya kuanza katika majira ya kiangazi. Dudek amesema suala hilo ni muhimu na Szczesny anapswa kulifikiria kwa makini kwani inavyoonekana tayari ameshapoteza nafasi yake Arsenal.
KHEDIRA ATHIBITISHA KUONDOKA MADRID.
KIUNGO wa klabu ya Real Madrid, Sami Khedira amethibitisha kuondoka katika timu hiyo wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani amecheza mechi zaidi ya 100 za ligi katika kipindi cha miaka mitano alichokuwa Santiago Bernabeu lakini ameshindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba wa sasa. Khedira mwenye umri wa miaka 27 amesema anataka kutafuta changamoto mpya baada ya kupoteza nafasi yake kwa nyota wengine wa Madrid kama Toni Kroos na Luka Modric lakini amesisitiza bado hajaamua aelekee wapi msimu ujao. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa hajafikia makubaliano na klabu yeyote mpaka sasa, kitu pekee anachofahamu ni kuwa hatakuwa na Madrid msimu ujao kwasababu ya kutafuta changamoto mpya.
PELE ATAMBA KUWA HATA NEYMAR HAWEZI KUMFIKIA.
NGULI wa soka wa Brazil, Pele amesisitiza kuwa hata Neymar hawezi kufikia ubora wake wakati alipokuwa akisakata kabumbu. Nguli huyo ambaye amewahi kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia akiwa na Brazil na kufunga mabao zaidi ya 1,000 enzi zake, ameshwaona wachezaji kadhaa ambao walikuwa wkaipigania kufikia rekodi yake toka astaafu. Mojawapo ya wachezaji hao ni Ronaldo ambaye amefunga mabao 62 katika mechi za kimataifa na Romario ambaye alikaririwa mapema mwezi huu kuwa Neymar anaweza kuipita idadi ya mabao 77 aliyofunga Pele kwa Brazil. Akiulizwa kama anadhani Neymar anaweza kuchukua nafasi yake kama mchezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika soka la Brazil, Pele amesema hadhani kama hilo linawezekana. Pele alifafanua kuwa haoni kama litawezekana kuwa na mfalme mpya au Pele mpya kwasababu mama yake na baba yake tayari walishafunga kizazi zamani.
ANDERSON KUENDELEA KUBAKIA LAZIO - WAKALA.
WAKALA wa mshambuliaji Felipe Anderson amesisitiza kuwa mteja wake amefurahi kukataa kwenda kwenye klabu zinazoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubakia Lazio msimu huu baada ya kusaini mkataba mpya. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye amefunga mabao 10 na kutoa pasi za mwisho nane katika mechi 25 alizoichezea Lazio msimu huu amekuwa akihusishwa kuwindwa na vilabu mbalimbali vikiwemo Manchester United na Chelsea. Lakini wakala wa mchezaji huyo Stefano Castagna amesema Lazio haitapata tabu kumbakisha nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwaka 2020, kwani anafurahia maisha ya Rome. Castagna amesema mteja wake hana mpango wowote wa kuondoka majira ya kiangazi kwani anafurahi kuitumikia klabu hiyo na anapenda kujiimarisha zaidi akiwa hapo.
FA KUMUONGEZA MKATABA HODGSON MWAKANI.
MWENYEKITI wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA Greg Dyke anapanga kuzungumza na kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Roy Hodgson kuhusu mkataba mpya mapema mwaka ujao. Hodgson mwenye umri wa miaka 67 alichukua mikoba ya Fabio Capello Mei mwaka 2012 lakini kikosi chake kilijikuta kiking’olewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia mwaka jana. Hata hivyo, Uingereza ndio wanaoongoza kundi lao katika mechi za kufuzu michuano ya Ulaya mwakani baada ya kushinda mechi zao nne za kwanza. Mkataba wa sasa wa Hodgson unamalizika baada ya michuano ya Ulaya itakayofanyika nchini Ufaransa na Dyke amesema mapema mwakani watajadiliana kuhusiana na mustakabali wa kocha huyo. Hodgson ambaye amewahi kuinoa Switzerland kuanzia mwaka 1992 mpaka 1995, aliiwezesha Uingereza kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ulaya mwaka 2012 ambapo walitolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penati na Italia.
BENDTNER ATAMBA BAADA YA KUPIGA HAT-TRIC WAKATI DENMARK IKIISAMBARATISHA MAREKANI.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Denmark, Nicklas Bendtner amefurahia kiwango alichokionyesha wakati nchi yake ilipoitandika Marekani kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa jana lakini anaamini angeweza kufunga mabao zaidi. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye ameanza kwa kusuasua katika klabu yake mpya ya Wolfsburg jana aliibuka nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika za mwishoni na kuipa ushindi huo muhimu Denmark. Akihojiwa Bendtner amesema anadhani alicheza vyema na kama ingekuwa siku nyingine angeweza kufunga mabao zaidi kutokana na nafasi alizopata. Nyota huyo pia alimpongeza kocha wao Morten Olsen mwenye umri wa miaka 65 ambaye naye alikubaliana na mshambuliaji huyo kuwa Denmark ilistahili kushinda kwa mabao mengi zaidi.
KOMBE LA MFALME KUFANYIKA KATIKA UWANJA WA CAMP NOU.
MCHEZO wa fainali ya Kombe la Mfalme kati ya Athletic Bilbao na Barcelona unaotarajiwa kuchezwa Mei 30 mwaka huu, utafanyika katika Uwanja wa Camp Nou. Kwa kawaida fainali ya michuano hiyo hufanyika katika uwanja huru lakini kutokana na klabu ya Real Madrid kukataa kutumika kwa uwanja wake wa Santiago Bernabeu kuliamuliwa kupigwa kura katika mkutano na Shirikisho la Soka la Hispania. Hakuna timu yeyote iliyotumia katika uwanja wake katika mchezo wa fainali toka mwaka 2002 wakati Deportivo La Coruna walipoifunga Real Madrid katika uwanja wao. Katika mkutano huo viwanja vya Vicente Calderon wa Sevilla na Mestalla wa Valencia vyote vilikuwa vikitafuta nafasi ya kuandaa fainali hiyo lakini waliondolewa katika duru la kwanza la kura na kubaki na Camp Nou pamoja na Uwanja wa San Mames wa Bilbao. Ushindi katika mchezo huo utaifanya Barcelona kufikisha mataji 27 ya michuano hiyo, wakati Bilbao wao wako katika nafasi ya pili katika orodha kwa kufikisha mataji 23 kama wakishinda.
SARE YAMPA WASIWASI LOEW.
KOCHA wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew amedai kuwa kikosi chake kilishindwa kutumia mfumo wao wakati walipotoa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Australia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika jana. Katika mchezo huo mabingwa hao wa dunia ndio waliotangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Marco Reus kabla ya Australia kusawazisha na kuongeza bao kupitia kwa Mile Jedinak na James Troisi. Mshambuliaji Lukas Podolski aliyeingia akitokea benchi aliisawazishia Ujerumani bao katika dakika ya 81 ya mchezo na kupelekea timu hizo kutoshana nguvu katika mchezo huo. Akihojiwa kuhusiana na mchezo huo, Loew anadhani kikosi chake kilishindwa kuendeleza mipango na aina ya uchezaji walioanza nao katika kipindi cha kwanza. Kocha huyo amesema mwanzoni walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kabisa kucheza mchezo wao katika kipindi cha pili hivyo kupelekea mchezo kuwaelemea.
Wednesday, March 25, 2015
RATIBA CHAN KUPANGWA APRILI 5.
RATIBA ya mechi za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN inatarajiwa kupangwa Aprili 5 mwaka huu jijini Cairo, Misri. Timu zipatazo 42 zinatarajiwa kuwemo katika ratiba hiyo iliyogawanyishwa kwa kanda kutoka mataifa wanachama wa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF. Kanda ya Kaskazini ambayo itajumuisha timu za Libya, Morocco na Tunisia watacheza wenyewe katika hatua ya mzunguko huku timu mbili za juu zikitarajiwa kufuzu kwa ajili ya fainali hizo. Kanda zingine zitakuwa zimegawanywa kama ifuatavyo, kanda ya magharibi A itakuwa na timu za Gambia, Guinea, Guinea Bissau, Liberia, Mali, Mauritania, Senegal, Sierra Leone ambapo washindi wawili ndio watasonga mbele. Magharibi B kutakuwa na Burkina Faso, Côte d’Ivoire, Ghana, Niger, Nigeria, Togo ambapo pia timu mbili ndio zitasonga mbele huku kanda ya kati ikijumuisha timu za Cameroon, Afrika ya Kati, Congo, Chad, DR Congo, Gabon na timu tatu ndio zitasonga mbele. Kanda ya kati-mashariki itakuwa na timu za Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Sudan, Tanzania, Uganda ambapo timu tatu pia ndio zitasonga mbele huku kanda ya Kusini ikijumuisha timu za Angola, Botswana, Comoros, Mauritius, Lesotho, Mozambique, Namibia, Seychelles, South Africa, Swaziland, Zambia and Zimbabwe. Mechi za kufuzu zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Juni 19 mpaka 21 na Agosti 28 mpaka 30 ambapo timu 15 zitakazofuzu zitaungana na wenyeji Rwanda katika fainali ya michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Januari 16 mpaka Februari 7 mwakani.
PIQUE AWAPONDA WANAOMKOSOA CASILLAS.
BEKI wa klabu ya Barcelona, Gerard Pique anaamini golikipa Iker Casillas ndio angekuwa shujaa wake kama angekuwa mshabiki wa Real Madrid. Beki huyo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akicheza pamoja na Casillas katika timu ya taifa ya Hispania toka mwaka 2009 wakati alipoitwa kwa mara ya kwanza baada ya kurejea Barcelona akitokea Manchester United. Baada ya kuwa chini ya kiwango mwaka jana, Pique amerejea tena katika ubora wake mwaka huu na kuisaidia Barcelona kuwafunga mahasimu wao Madrid Jumapili iliyopita. Pique amewaponda wale wanaobeza uwezo Casillas kwani bado anaamini anaweza kurejea katika kiwango chake cha juu kabisa. Nyota huyo amesema kama angekuwa mshabiki wa Madrid, Casillas ndio angekuwa shujaa wake kwani ni mfano kwa wachezaji wote wa timu hiyo.
JUVENTUS HAINA UBAVU WA KUMZUIA POGBA KUONDOKA - MAROTTA.
OFISA mkuu wa Juventus, Giuseppe Marotta hadhani kama klabu hiyo itaweza kumzuia kiungo Paul Pogba kama ataamua anataka kwenda kucheza mahali pengine katika majira ya kiangazi. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa kihusishwa na vilabu kadhaa tajiri katika miezi ya karibuni vikiwemo Real Madrid, Paris Saint Germain na Chelsea ana kumekuwa na tetesi kuwa anaweza kufikia thamani ya euro milioni 100. Ingawa Marotta amesisitiza kuwa mpaka sasa Pogba hajaonyesha nia yeyote ya kuondoka, anafikiri itakuwa jambo lisilowezekana kumbakisha Turin kama akiamua kutafuta changamoto nyingine. Marotta amesema Pogba mwenyewe ndio atakaeamua mustakabali wake wa aidha kubakia Italia au kwenda sehemu nyingine kwani hawataweza kushindana na vilabu tajiri wakiamua kumpa kitita kikubwa zaidi yao. Juventus inayonolewa na Massimiliano Allegri hivi sasa ipo kileleni mwa Serie A kwa tofauti ya alama 14.
FALCAO A-BEEP KUONDOKA UNITED.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United Radamel Falcao amedokeza jana kuwa anaweza kuondoka katika timu hiyo mwishoni mwa msimu kutafuta timu anayoweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia alikosa michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana kutokana na majeruhi, baadae alihamia United kwa mkopo akitokea Monaco ya Ufaransa ambako ameshindwa kutamba. Akihojiwa Falcao amesema anafikiri kila mchezaji anahitaji kucheza na anafurahia kucheza ndio maana anataka kuisaidia United katika michezo nane ya Ligi Kuu iliyobakia na baada ya hapo chochote kinaweza kutokea. Falcao aliendelea kudai kuwa wakati msimu utakapokwisa atakaa chini na kufanya tathmini na kuamua kitu gani kitakuwa bora kwake. Nyota huyo amesema anahitaji kutafuta mahali ambapo anaweza kupata nafasi kucheza mara kwa mara.
USHANGILIAJI KUMPONZA RONALDO.
RAIS wa Ligi ya Soka ya Hispania-LFP, Javier Tebas amedai kuwa mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo anaweza kufungiwa kwa kosa la ushangiliaji wakati aliposawazisha bao katika mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Barcelona. Ronaldo sio mara yake ya kwanza wakati akifunga bao katika Uwanja wa Camp Nou kuonekana akiwataka mashabiki wa Barcelona kutulia kwani alifanya hivyo tena katika mchezo uliopita. Tebas amesema wanatakiwa kuwa waangalifu na ushangiliaji wa aina yeyote wenye ujumbe wa uchochezi wa mchezaji wakati akifunga bao au kwenye tukio lolote kwani kunaweza kuzuka vurugu zinazowea kusababisha maafa. Rais huyo aliendelea kudai kuwa suala hilo litaangaliwa kwa makini na kuna uwezekano Ronaldo akatozwa faini au hata kufungiwa.
MABINGWA WA DUNIA UJERUMANI KUVAA VITAMBAA VYEUSI KUOMBOLEZA WALIOFARIKI KATIKA AJALI YA NDEGE.
MABINGWA wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani wanatarajiwa kuvaa vitambaa vyeusi na kusimama dakika moja kabla ya mchezo wao wa kirafiki utakaochezwa baadae dhidi ya Australia ili kutoa heshima zao kwa watu waliofariki katika ajali ya ndege kwenye Milima ya Ufaransa. Rais wa Chama cha Soka cha Ujerumani-DFB, Wolfgang Niersbach alithibitisha kuwepo kwa dakika moja ya maombolezo kabla ya mchezo huo wa kimataifa utakaofanyika Kaiserslautern. Zaidi ya nusu ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo wanaaminika kuwa raia wa Ujerumani. Niersbach amesema wanafanya hivyo ili watu waliopotelewa na ndugu zao katika ajali hiyo iliyotokea jana wajue kuwa familia ya soka iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Wanafunzi 16 wa Ujerumani waliokuwa katika safari ya kishule wanahofiwa kuwa miongoni mwa abiria 144 na wafanyakazi sita waliouawa wakati ndege ya shirika la ndege la Germanwings ilipopata ajali wakati ikisafiri kwenda Duesseldorf kutokea Barcelona.
MAJERUHI WAMPAGAWISHA HODGSON.
KOCHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson anategemea wachezaji zaidi kujitoa katika kikosi chhake baada ya mchezo wao wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya Lithuania. Nyota wa Liverpool Daniel Sturridge na Adam Lallana wote waliondolewa katika kikosi cha timu hiyo juzi kutokana na majeruhi huku Luke Shaw na Fraser Forster nao wakitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita. Kutokana na hali jinsi ilivyo, Hodgson anaamini anaweza kuwapoteza wachezaji zaidi kwa majeruhi mara baada ya mchezo wao dhidi ya Lithuania. Wachezaji wengine wa timu hiyo kama Wayne Rooney, Raheem Sterling na Harry Kane wanaonekana kama hawako fiti kwa asilimia mia moja kwa mujibu wa kocha huyo.
SKRTEL AKANUSHA KUMKANYAGA DE GEA KWA MAKUSUDI LAKINI ASHINDWA RUFANI.
BEKI wa Liverpool, Martin Skrtel amekanusha mashitaka anayotuhumiwa kwa kumkanyaga golikipa wa Manchester United David De Gea. Tukio hilo lilitokea katika dakika za majeruhi ya mchezo kati ya timu hizo ambapo United iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa Anfield Jumapili iliyopita. Beki huyo wa kimataifa wa Slovakia mwenye umri wa miaka 30, alishitakiwa jana na anakabiliwana adhabu ya kufungiwa mechi tatu lakini mwenyewe amedai tukio hilo lilikuwa bahati mbaya. Mwamuzi wa mchezo huo Martin Atkinson hakuliona tukio hilo lakini waamuzi watatu wa zamani wamekubaliana kuwa alitakiwa kutolewa nje baada ya kuona marudio ya picha za video. Kama Skrtel akifungiwa mechi hizo inamaanisha kuwa ataukosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal utakaochezwa Aprili 4 mwaka huu na mwingine dhidi ya Newcastle United utakaochezwa Aprili 13 pamoja na ule wa maruadiano ya robo fainali wa Kombe la FA dhidi ya Blackburn Rover Aprili 8. Nahodha wa timu hiyo Steven Gerrard tayari atakosa michezo hiyo baada ya kunyukwa kadi nyekundu katika mchezo huo baada ya kupita sekunde 38 toka aingie akitokea benchi katika kipindi cha pili.
UINGEREZA KUTAFUTA UENYEJI WA KOMBE LA DUNIA 2026.
MWENYEKITI wa Chama cha Soka cha Uingereza-FA, Greg Dyke amesema nchi hiyo inaweza kufikiria kuingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta uenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026. Uingereza iliingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta uenyeji wa fainali za mwaka 2018 lakini walishindwa vibaya na Urusi waliopewa jukumu hilo. Hata hivyo Dyke amesema jaribio lao litategemea kama rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA Sepp Blatter ataendelea kubakia madarakani. Dyke aliendelea kudai kuwa pia kuteuliwa kwa David Gill raia wa Uingereza katika kamati kuu ya uongozi wa FIFA inaweza kuongeza ushawishi wa kugombea nafasi hiyo. Mwenyekiti huyo wa FA amesema Uingereza itachukua hatua hiyo iwapo tu sera zitakuwa za wazi lakini haitaomba nafasi hiyo wakati Blatter akiwa bado yuko madarakani.
Tuesday, March 24, 2015
STARS YAWASILI MWANZA TAYARI KUWAKABILI MALAWI.
TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imewasili salama leo asubuhi jijini Mwanza, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa siku ya jumapili Machi 29, 2015 dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames), mechi itakayochezwa kwenye dimba la Uwanja wa CCM Kirumba. Kikosi cha Stars kimeondoka kikiwa na wachezaji 18 ambao wameripoti kambini jana, huku kiugo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini Qatar akitarajiwa kuungana na wenzake leo mchana jijini Mwanza. Wachezaji waliopo kambini jijini Mwanza ni, magolikipa Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC), walinzi ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Aggrey Morris (Azam FC) , Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Haji Mwinyi (KMKM), Hassan Isihaka na Abdi Banda (Simba SC). Wengine ni Amri Kiemba, Frank Domayo, Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Haroun Chanongo (Stand United), John Bocco (Azam FC), Juma Luizio (Zesco United), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe). Mchezaji Mcha Khamis wa Azam FC amejiondoa kikosini kutokana na kuwa majeruhi, huku wachezaji wa Young Africans wakitarajiwa kujiunga na kikosi hicho cha timu ya Taifa mara tu baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya JKT Ruvu siku ya jumatano.
HUWA SIPENDI KUWAKARIPIA WACHEZAJI WANGU - WENGER.
MENEJA wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri mara kadhaa kutaka kuwagombeza au kuwapigia kelele wachezaji wake lakini amekuwa mara nyingi amekuwa akijizuia. Arsenal bado imeendelea kujiimarisha katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu hivyo kuweka hai matumaini yao ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiulizwa mbinu anazotumia kuwasiliana na wachezaji wake, Wenger amesem mara nyingi huwa hapendi kuwa mkali au kuwapigia kelele wachezaji wake kwani hilo linaweza kuleta madhara zaidi. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa siku zote wakati timu inapofungwa hata wachezaji wenyewe hukasirika hivyo kama ukiendelea kuwakaripia badala ya kuongea nao taratibu unaweza kuwafanya wakapoteza hali yao ya kujiamini.
MALAWI KUWASILI ALHAMISI TAYARI KUIVAA STARS.
UEFA YAZIONYA TIMU KUHUSU WACHEZAJI WAO KUWABUGUDHI WAAMUZI.
KATIBU mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Gianni Infantino amezionya timu zote zilizotinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwaonya wachezaji wao kutowabugudhi waamuzi. Infatino pia ameongeza shirikisho hilo halitaunga mkono kutumia picha video ili kugundua makosa ya waamuzi wakati mchezo ukiendelea. Ofisa wa waamuzi wa UEFA Pierluigi Collina alizionya timu za Atletico Madrid, Barcelona, Bayern Munich, Juventus, Monaco, Paris Saint Germain, Porto na Real Madrid katika kikao walichokutana Ijumaa iliyopita. Kikao hicho kilichofanyika jijini Nyon, Uswisi kimekuja ikiwa imepita siku moja baada ya shirikisho hilo kumfungia mechi tatu beki wa PSG Serge Aurier kwa kutoa maneno ya kashfa kwa mwamuzi katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Chelsea. Aurier hakucheza mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 lakini alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook kumponda mwamuzi Bjorn Kuipers kwa kumtoa nje kwa kadi nyekundu Zlatan Ibrahimovic.
KLOSE KUGEUKIA UKOCHA AKITUNDIKA DARUGA ZAKE.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Miroslav Klose ana mipango ya kuja kuwa kocha pindi atakapotundika daruga zake rasmi huku akipendelea zaidi kufanya kazi nchini kwao katika Bundesliga. Akihojiwa Klose ambaye alistaafu soka la kimataifa baada ya michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil, amesema malengo yake ni kuja kuwa kocha wa Bundesliga. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa pindi atakapokuwa akitafuta leseni ya ukocha atafanya bidii zote kama anavyofanya katika mambo yake mengi. Klose mwenye umri wa miaka 36 ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya Lazio ya Italia, aliweka rekodi katika Kombe la Dunia kwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika michuano hiyo akiwa mabao 16. Nyota huyo alifikisha bao la 16 baada ya kufunga bao katika mchezo ambao Ujerumani uliwashindilia bila huruma wenyewe wa michuano hiyo Brazil kwa mabao 7-1.
SHABIKI WA LIVERPOOL AJINADI KUMZUIA BALOTELLI KUTOPATA KADI YA PILI YA NJANO.
SHABIKI mmoja wa Liverpool amedai kuwa yeye ndio aliyesaidia kuepusha kadi ya pili nyekundu katika mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Manchester United baada ya kumzuia Mario Balotelli kutokwenda kumvaa Chris Smalling. Wakiwa tayari wamempoteza nahodha wao Steven Gerrard aliyetolewa baada ya kucheza kwa sekunde 38 toka alipoingia kipindi cha pili, Liverpool tayari walikuwa na upungufu wakati Balotelli aliyekuwa na kadi ya njano alipotaka kukwaruzana na Smalling baada ya kukwatuliwa. Hatua hiyo ilimfanya Balotelli kupepesuka mpaka pembeni mwa uwanja sehemu za matangazo na shabiki huyo Shaun Leatherbarrow aliyekuwa karibu amesema ilikuwa ni jukumu lake kumtuliza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Italia. Shabiki huyo amesema alifanya hivyo baada ya kuona jinsi Balotelli alivyochukizwa na kitendo hicho na pengine angeweza hata kumvaa Smalling kama asingemtuliza na kupata kadi nyingine ya njano.
MADRID YAANZA KUWACHUKULIA HATUA MASHABIKI WALIOSHAMBULIA MAGARI YA WACHEZAJI.
KLABU ya Real Madrid imemsimamisha mjumbe mmoja wa timu hiyo na kuwabaini mashabiki wengine wawili waliohusika kubugudhi na kupiga magari ya baadhi ya wachezaji baada ya mchezo dhidi ya Barcelona. Mshabiki mmoja walinaswa katika picha za video akishambulia kioo cha gari la Jese na wengine wawili wakijaribu kulipiga mateke gari la Gareth Bale. Beki Sergio Ramos pia alikuwepo eneo hilo wakati tukio likitokea ambapo alisimamisha gari lake na kujaribu kuwaambia mashabiki hao kuwa wanachofanya sio sahihi. Bale alijiunga na Madrid akitokea Tottenham Hotspurs katika majira ya kiangazi mwaka 2013 na amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu hiyo kilichoshinda Kombe la Mfalme na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita. Hata hivyo msimu huu umekuwa sio mzuri kwa Bale kwani amekuwa akiandamwa na majeruhi na kupelekea kutokuwa fiti kwa asilimia mia moja hivyo kuwafanya mashabiki kumzomea katika baadhi ya michezo.
FA YAJIPANGA KUBORESHA TIMU YA TAIFA KWA KUPUNGUZA WACHEZAJI WA NJE.
SHIRIKISHO la Soka la Uingereza-FA linakusudia kuandaa sheria itakayopunguza idadi ya wachezaji kutoka nje ya nchi za umoja wa Ulaya kusajiliwa katika ligi ya nchi hiyo. Mwenyekiti wa FA Greg Dyke amesema Ligi Kuu iko kwenye hatari ya kutowasaidia wachezaji wazawa kama hatua za makusudi na haraka hazitachukuliwa kusaidia suala hilo. Katika mpango huo FA pia itaweka sheria ngumu kwa wachezaji wenye vipaji waliokulia nchini humo. Mikakati hiyo yote ina dhumuni la kuimarisha timu ya taifa ya Uingereza ambayo imekuwa haifanyi vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
STURRIDGE PANCHA TENA.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uingereza Daniel Sturridge anatarajiwa kuikosa michezo ya nchi yake dhidi ya Lithuania na Italia baada ya kupata majeruhi tena. Nyota huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 25 alipata majeraha ya nyonga katika mchezo dhidi ya Manchester United uliofanyika Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Anfield. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa Chama cha Soka cha nchi hiyo-FA, kilithibitisha taarifa hiyo na kudai kuwa nyota huyo amerejea katika klabu yake jana jioni. Hatua hiyo inafuatia baada ya kufanyiwa vipimo na madaktari kung’amua kuwa hataweza kulitumikia taifa lake katika michezo hiyo. Kukosekana kwa Sturridge kunaweza kuwa nafasi kwa Harry Kane kupata nafasi yake ya kwanza kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa ya nchi hiyo. Mbali na Sturridge lakini pia mchezaji mwenzake wa Liverpool Adam Lallana naye alirudishwa baada ya kuwa majeruhi na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo wa Tottenham Hotspurs Ryan Mason.
Sunday, March 22, 2015
MAN UNITED YAICHAPA LIVERPOOL NYUMBANI KWAO HUKU GERRARD AKIPEWA KADI NYEKUNDU.
KLABU ya Manchester United leo imefanikiwa kujiimarisha katika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuifunga Liverpool mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Anfield. Katika mchezo huo United ndio walitangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Juan Mata katika dakika ya 11 kabla ya kiungo huohuyo kuongeza bao lingine katika dakika ya 59. Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo kwa kumchezea faulo Andre Herrera ikiwa zimepita sekunde 48 toka aingie uwanjani akitokea benchi akichukua nafasi ya Adam Lallana. Bao la kufutia machozi la Liverpool katika mchezo huo lilifungwa na Daniel Sturridge huku Wayne Rooney akikosa penati katika dakika za mejeruhi ambayo iliokolewa na Mignolet.
Subscribe to:
Posts (Atom)